Kiongozi wa kambi hiyo, Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari juzi mjini Dodoma alisema hawatawasilisha hotuba za bajeti za upinzani hadi watumishi wa sekretarieti yao ambao mikataba yao hutolewa na Bunge watakaporejeshwa.
Mbunge wa Mvomero (CCM), Sadiq Murad alisema uamuzi huo utaifanya hata Serikali kushindwa kujitafakari katika mipango yake.
Murad ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, alisema jana kuwa maoni ya upinzani ni muhimu hivyo watafakari upya uamuzi huo.
Lakini Mbunge wa Kavuu (CCM), Dk Pudenciana Kikwembe alisema hakuna shida kwa wapinzani kusoma au kutosoma bajeti mbadala kwa kuwa ni watu wa hapana tu.
Alisema demokrasia inawaruhusu kuchangia bajeti kwa hotuba au hata kunyamaza.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Dk Charles Kitima alisema tangu utawala wa awamu ya tatu, Tanzania ilizoea kupata mawazo mbadala yanayotolewa na upinzani.
“Ieleweke kuwa mawazo mbadala yanajenga Taifa imara lenye kuwajibika,” alisema Dk Kitima.
Dk Kitima aliungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda aliyesema, “Hii ni hasara kwa wananchi. Mambo yaliyokuwa yakiibuliwa na upinzani sasa hayatafanyika, Serikali haitajua wapi inakosea.”
Alisema Serikali inaweza kuandaa bajeti inayopendelea eneo moja lakini upinzani katika hotuba zao watasema haina uwiano sawa hivyo irekebishwe na Serikali ikalifanyia kazi.
“Wakati mwingine, mambo muhimu na makubwa yalikuwa yanaibuliwa katika hotuba hizo na mawaziri walikuwa makini kufuatilia kujua upinzani wanasema nini juu ya wizara zao, sasa hilo halitakuwapo na bajeti zitakuwa zinapita tu,” alisema.
Mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Atway Selemani alisema si sahihi kwa upinzani kuchukua uamuzi huo kwa kuwa bajeti za wizara vivuli hutoa sura na udhaifu wa bajeti za Serikali.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Harrison Sogo alisema uamuzi huo una athari za moja kwa moja kwa wananchi ambao wamekuwa wakitegemea hotuba hizo kupata taarifa juu ya hali ya kiuchumi.
Imeandikwa na Habel Chidawali (Dodoma), Ibrahim Yamola na Kelvin Matandiko (Dar).