“Embu jiulize ni namna gani shujaa wa taifa angejisikia pale ambapo amekaa mbele ya watu wa rika tofauti jinsia tofauti wenye mirengo tofauti ya kisiasa wote wakimsifia na kumshukuru kwa werevu wake wakulipigania taifa?”
Maneno ya Mama Graca Machel mwanaharakati wa masuala ya wanawake na watoto wa Afrika akiongea mbele ya umati wa watu kutoka maeneo mbalimbali duniani waliofika kutoa salamu za mwisho wakati wa kuaga mwili wa Marehemu Winnie Mandela aliyefariki tarehe 2 Aprili 2018 nchini afrika kusini.
Winnie Madikizela-Mandela (81) alikuwa mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo hali iliyopelekea kufungwa mara kadhaa mbali na kuendelea kupokea vitisho lakini aliendea kuwa mwanaharakati mpaka mauti yaliyomfika.
Winnie Mandela ambaye kwa wengi anafahamika kama mama wa taifa la Afika Kusini pia alikuwa mke wa Nelson Mandela kwa miaka 38 toka mwaka 1958 mpaka walipoachana mwaka 1996 na kufanikiwa kupata watoto wawili.
Akiongea katika Msiba huo mama Graca Machel ambaye amekuwa akimuita Marehemu Winnie Mandela “dada mkubwa” amesema ni wakati sasa wa kuwaita mashujaa wa taifa na kuwashukuru wangali wakiwa hai kwakuwa hakuna ajuae kama wanasikia na kuona vile wanavyosifiwa wakati wa Misiba yao.
Pia amekemea tabia ya jamii kuwananga na kuwasema watoto wa wapigania uhuru kwakuwa wengi wao wamekosa miongozi na malezi bora ya wazazi kwakuwa wazazi wao walikuwa na ujasiri wa kuacha familia zao na kupigania taifa hivyo si sawa kuwasema na kuwanyooshea vidole badala yake waoneshe upendo zaidi kwao katika kile kilichofanywa na wazazi wao.
Kuhusu rambirambi na ahadi zinazotolewa misibani Mama Graca amewataka wananchi na wanasiasa kuacha maneno ya hadaa kwakuwa mengi yanayoahidiwa hayatekelezwi.
Akitolea mfano wa ahadi zilizotolewa wakati wa wa msiba wa Nelson Mandela miaka mitano iliyopita amesema “ kwasasa ukiangalia Afrika kusini mambo yamekuwa mabaya zaidi ya kipindi Mandela yuhai na hii inaonesha kiasi gani watu hawaishi ahadi zao walizoahidi na ndio jambo hata leo watu wengi wameahidi kuendeleza harakati za Winnie Mandela lakini nani anajua kama zitatekelezwa?”
Badala yake amewataka wanajamii kwa ujumla kuamka na kusaidia kuinua jamii kwakuwa zaidi ya asilimia 50 ya wananchi ni masikini na hakuna juhudi za mmoja mmoja zakulikomboa taifa katika tatizo hilo badala yake kila mtu anaitupia lawama serikali.
Katika hotuba hiyo Graca Machel kwa zaidi ya robo saa aliahidi kutomzungumzia Winnie Mandela kwakuwa kila mtu amekuwa akifanya hivyo na badala yake kuitaka jamii kubadilika.
Mama Graca Machel ambaye alikuwa mke wa Nelson Mandela tangu mwaka 1998 mpaka mauti yalipomkuta mwaka 2013 alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu Winnie Mandela na wamekuwa wakishirikiana katika masuala mbalimbali ya kutetea haki za raia nchini Afrika kusini na afrika kwa ujumla.