TAMKO LA NCCR MAGEUZI KUHUSU UFISADI WA IPTL KUPITIA AKAUNTI YA TEGETA ESCROW
UTANGULIZI
Itakumbukwa na watanzania kuwa kwa takribani miezi miwili sasa watanzania wamekuwa wakishuhudia bunge la bajeti ambalo pamoja na mambo mengine, hoja ya ufisadi wa fedha za Umma zilizochotwa kifisadi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow ilichukua sehemu kubwa ya mjadala wan chi hii. Kama chama tunachukua nafasi hii kumpongeza Mbunge wetu Mhe David Kafulila kwa ujasiri wake wa kutimiza wajibu wake wa kibunge kwa kiwango cha juu kabisa katika kuhakikisha Bunge linakuwa na udhibiti wa fedha za serikali ambazo ni mali ya Umma.
Aidha, Chama kinachukua nafasi hii kuwapongeza wabunge wote wanaounda Kambi rasmi ya upinzani hususani wa CHADEMA na CUF pamoja na NCCR MAGEUZI kwa ushirikiano wao mkubwa katika kuhakikisha wanaisimamia serikali katika mambo yote ya msingi likiwemo hili la ufisadi wa fedha za akaunti ya Escrow. Wameonesha mfano mzuri ndani ya bunge na tunaomba wadau wote wa maendeleo tuungane katika vita hii kwani ni kwa maslahi ya Taifa letu masikini kabisa. Kwa nukta hii tunaomba viongozi wa dini, Asasi za kiraia(NGO), Wanazuoni watanzania kwa ujumla tuungane pamoja kutaka uwajibikaji ili kudhibiti mzimu huu wa ufisadi wa IPTL/ESCROW ulioanza tangu awamu ya pili ya uongozi wan chi hii na sasa huenda ukaendelea kulitafuna taifa hadi awamu wa tano.
KWANINI ESCROW AKAUNTI ILIFUNGULIWA
Pamekuwa na upotoshaji wa maksudi kabisa kuhusu sababu za kufunguliwa akaunti hii. Upotoshaji huu umefanywa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali bungeni na watuhumiwa wenzake kwa maana ya Maswi na Muhongo kwa maana ya watuhumiwa ambao tayari wamesikika wakizungumzia suala hili. Watuhumiwa hawa wamesikika wakidai kuwa escrow ilifunguliwa kufuatia mgogoro baina ya wabia wa IPTL kwa maana ya Mechmar mwenye 70% na VIP mwenye 30%. Haya wanayapotosha ili kuhalalisha hoja yao kuwa fedha hizo sio za serikali
NCCR MAGEUZI inapenda Umma wa Watanzania ufahamu kuwa akaunti hii ilifunguliwa na pande mbili; Tanesco na Serikali kwa upande mmoja na IPTL kwa upande wa pili. Na kwamba Akaunti hii ilifunguliwa kufuatia mgogoro wa malipo ya gharama za umeme ambapo Tanesco ililalamika kuwa inatozwa zaidi. Msingi wa Tanesco kulalamika kutozwa zaidi kulitokana na IPTL kudanganya kuhusu mtaji wa asilimia 30% (equity) ambapo ilidai iliwekeza dola 38millioni kumbe iliwekeza dola 50, sawa na Tsh 50,000/= wakati huo mwaka 1995-1998 ambapo exchange rate ya dola kwa Tsh ilikuwa 1; 1000.
Nikatika msingi huo, Mwaka Februari2014 Mahakama ya Usuluhishi wa migogoro ya kibiashara ICSID ilielekeza gharama ziangaliwe upya tangu TANESCO ilipoanza kununua umeme wa IPTL maka 2002 mpaka 2014 ili kuona ni kwa kiasi gani IPTL ilipata fedha isiyostahiki na kiasi gani ilikuwa stahiki ili kuweka msingi wa mgawo wa fedha za escrow.
Hivyo Akaunti ya Escrow ilifungulimwa mwaka 2006 ikiwa ni miaka miwili tangu 2004 ambapo TANESCO ilibaini kasoro hiyo ya udanganyifu uliofanywa na IPTL kwenye equity ya dola 38milioni wakaweka dola 50.
KWANINI FEDHA ZA ESCROW NI MALI YA UMMA
Fedha ya Escrow ni mali ya Umma kwa sababu zifuatazo;
1.Ziliwekwa kusubiri kumalizika mgogoro wa gharama ambazo IPTL ilikuwa anatoza TANESCO kifisadi. Mgogoro huo ambao msingi wake ulitokana na IPTL kudanganya kuhusu mtaji wa dola 38milioni kumbe ilikuwa dola50.Mpaka sasa hakuna mahala mgogoro huo umeamuliwa.
2.Ndio sababu Hukumu ya awali ya ICSID ilielekeza pande mbili zifanye hesababu upya ili kubaini ni kiasi gani IPTL ilizidisha na ni kiasi gani ilikuwa halali kwa kuangalia tangu mwaka 2002.
3.Ndio sababu fedha hizo zilionekana kwenye vitabu vya shirika la Umma Tanesco
4.Ndio sababu Kamati ya PAC, Spika na Waziri Mkuu wote wamelekeza CAG achunguze akaunti hiyo kwani kisheria CAG hana mamlaka ya kuchunguza fedha za wafanyabiashara bali fedha za Umma. Na CAG anachunguza fedha za Umma kwenye makampuni ambayo umiliki wake sio chini ya asilimia 50
MASWI, MUHONGO, MRAMBA, WEREMA NA IPTL NDIO WALISHINIKIZA UFISADI HUU
May 30, 2014 Waziri wa Nishati na Madini Mhe Muhongo alidanganya Bunge kuwa uamuzi wa Serikali kumlipa IPTL/PAP ulikuwa uamuzi wa hukumu ya Mahakama ya Setemba 2013. Ukweli ni kwamba hukumu hiyo hakuna mahala ilielekeza PAP alipwe fedha hizo. Ukweli ni Kwamba uamuzi wa kifisadi wa kutoa fedha hizo ulifanywa na Wizara ya Nishati na Madini na Tanesco kwa upande mmoja na IPTL kwa upande wa pili na ukapewa Baraka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hivyo Tunaomba Umma uelewe hivyo.
NYARAKA ZA PAP KUMILIKI ASILIMIA 70 ZA IPTL NI ZA KUGUSHI
Nyaraka za TRA zinaonesha kwamba SingaSinga ambaye ndiye mliki wa PAP alinunua hisa asilimia za 70 za IPTL kutoka kwa PIPERLINK kwa 480millioni, na kwamba PIPERLINK ilinunua Asilimia hiyo 70 kutoka kwa Merchmar kwa Tsh6millioni wakati kampuni hiyohiyo ilinunua asilimia 30 kutoka kwa VIP alinunua kwa 120billioni. Pia inaonesha kwamba kodi ililipwa disemba 6, 2013 wakati alipewa hela za escrow tangu Novemba 2013. Kwa tafsiri nyingine alilipwa fedha za Escrow kabla ya kuwa mmiliki halali wa IPTL.
Na zaidi Umma unapaswa kuelewa kuwa Kwa mujibu wa sheria ya kodi(Finance Act 2012), hisa zinapouzwa kutoka kampuni moja kwenda nyingine uhamishaji huo unathibitishwa na waziri wa wizara husika baada ya kodi kulipwa. Sasa muulizeni waziri wa Nishati na Madini ni lini uhamishaji huo wa hisa aliupitisha kama waziri? Na zaidi taarifa za TRA zinaonesha kuwa kodi ya mauzo ya hisa hizo asilimia 70 kutoka Mechmar kwenda PIPERLINK na Kutoka PIPERLINK kwenda PAP ilipwa tarehe moja yaani Disemba6, 2013.
Huu ni uthibitisho kuwa documents hizi zote ni za kughushi, na watanzania hawawezi kuchezewa akili kiasi hiki.
MKATABA WA WIZARA YA NISHATI NA IPTL KWENDA BOT NI UFISADI
Mkataba huu ulikuwa kifisadi kwasababu hauna msingi wowote wa kisheria wala kimkataba. Mkataba wa kuzitoa fedha hizi ni wa kifisadi mgogoro uliosababisha fedha hiyo iwekwe hapo haukuwa na haujamalizika. Ndio msingi wa hukumu ya mahakama ya ICSID uliotaka mahesabu kufanywa upya. Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa mkataba wa IPTL, pande mbili zilikubaliana kuwa maamuzi kuhusu mgogoro baina yao utamuliwa na mahakama ya ISCID na sio vinginevyo.
MMILIKI WA PAP ANA REKODI YA UFISADI AFRIKA SIO MWEKEZAJI
Kwa mujibu wa report ya wikleaks, Singasinga anaetajwa kuwa mmiliki wa kampuni ya PAP ametajwa katika orodha ya mafisadi waliohusika katika skendo ya ufisadi wa Goldenberg nchini Kenya jina lake likiwa no8 akishirikiana na mtoto wa Rais mstaafu wa Kenya, Gideon Moi. Huu ndio ufisadi mkubwa kupata kufanyika nchini Kenya, uliohusisha Majaji, Viongozi wakubwa kisiasa, familia ya rais na watendaji wakubwa serikalini. Kama CCM haitachukua hatua kali kuhusu ufisadi huu wa escrow ijiandae kufuata nyayo za chama cha KANU kwani kuna kufanana sana kwa skendo hii na ile ya Goldenberg.
KIFO CHA MGIMWA KICHUNGUZWE
Mhe Mbunge David Kafulila, alisisitiza ndani ya Bunge kuwa kama tungekuwa na Bunge makini hata kifo cha aliyekuwa waziri wa Fedha, Mhe Mgimwa kilipaswa kuchunguzwa. Chama kinapenda kusisitiza kauli hiyo kwakuwa Mzee Mgimwa aliugua na kufariki katika kipindi ambacho kulikuwa na shinikizo kubwa la kutoa fedha za escrow bank kuu. Hivyo Kama Chama tunapenda Umma uelewe kuwa huo ndio msingi wetu wa kutaka uchunguzi wa kifo hicho. Na familia ya Mhe Mgimwa tunaipa pole kutonesha madonda lakini tunafanya haya kwasababu ndugu yao alikuwa public figure, alikuwa kiongozi ndani ya nchi hivyo umma una maslahi na chochote kinachomuhusu mtu huyu.
HATMA YA USALAMA WA MBUNGE KAFULILA
Mhe Spika amegoma kuchukua hatua kuhusu mwongozo uliombwa na mbunge Mhe David Kafulila kuhusu kutishiwa maisha ndani na nje ya Bunge. Kama Chama Tunapenda kurejea na kusisitiza kuwa tuna hofu na uhai wa Mbunge wetu hasa kutokana na mazingira yanayozunguka ajenda hii anayoisimamia ikiwa inagusa vigogo na mafisadi wakubwa. Tunao uzoefu wa mazingira kama haya pale kijana Amina Chifupa alipozungumzia madawa ya kulevya, tunao uzoefu na kilichotokea kwa Dr Mvungi alipokuwa mhimili imara wa serikali tatu ndani ya Tume ya warioba, wote tunafahamu kilichowakuta. Kama chama kwakuwa Bunge la vyombo vya dola havioni umuhimu huo, tunamwachia Mungu, lakini chochote kikitokea tunafahamu ushiriki wa serikali na vyombo vyake.
SPIKA MAKINDA ANADHALILISHA BUNGE
Kazi ya Bunge ni kusimamia Serikali. Ufisadi wa IPTL ulianza tangu awamu ya pili 1994. Ni aibu kwa Spika kukataa Bunge lisichukue jukumu lake la kuichunguza serikali. Wote mnafahamu CAG alivomsafisha Jailo au PCCB ilivosafisha Richmond. Ni katika Msingi huo, Kama chama tunashauri suala hili linalogusa vigogo wakubwa nchini, lichunguzwe na Bunge lenyewe kupitia Kamati teule au uchunguzwe ufanywe na Kampuni za Kimataifa za ukaguzi kama ilivofanyika kwenye fedha za EPA.
Mhe Mbunge alitoa ushahidi wa hukumu ya Septemba 2013 ikionesha dhahili kuwa hakuna mahala hukumu ile ilielekeza IPTL/PAP wapewe fedha hizo za Escrow. Na kuthibitisha kuwa waziri huyu alizungumza uongo bungeni kwa jambo nyeti kama hili, lakini Spika badala ya kutumia kanuni ya kusema uongo anaelekeza mbunge aende PCCB, Kambiwa na nani PCCB wanachunguza uvunjifu wa kanuni za bunge?
Aidha, Ni udhaifu wa Spika huyu ndio sababu haoni aibu kwa Bunge lake kuwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa bodi ya Tanesco. Hii Kamati inawezaje kukosoa uchafu wa TANESCO katika mazingira hayo? Au ndio sababu taarifa ya Kamati hiyo haikuzungumza chochote kuhusu ufisadi wa escrow unaohusu TANESCO na wizara yake?
JAJI WEREMA AJIPIME KAMA ANASTAHILI KUENDELEA KUWA JAJI NA MWANASHERIA MKUU
Uamuzi wa Jaji Werema kutaka kupigana bungeni hata kuzuiwa na Mhe Sitta na Wasira na baadae nje ya Bunge kumtishia uhai Mhe Mbunge ni kielelezo kuwa amepungukiwa sifa za msingi kuweza kuendelea kuwa mwanasheria mkuu wa serikali. Ni aibu serikali ya Kikwete kuwa na Mwanasheria mkuu ambaye kazi yake kubwa ni kuelekeza na kushauri utawala wa sheria nchini harafu anageuka na kuwa mfano wa raia mwenye mapenzi ya kujichukulia sheria mkononi ndani ya bunge na kuahidi kukata kichwa mbunge anaemkosoa. Hii haijapata kutokea katika historia ya Tanzania.
MWISHO
Tunapenda kuhitimisha kwamba tunaitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti kuhusu ufisadi huu, na kwamba haturidhishwi na hatua zinazochukuliwa, na kwamba tutafanya utaratibu wa kuwasiliana na vyama ndani ya UKAWA kuona namna bora zaidi ya kulisukuma suala hili ili watanzania waelewe namna nchi yao inavotafunwa. Tunaomba vyama vyote ndani na nje ya UKAWA vitambue ukweli huu kama ambavyo wameanza kutambua ili tusaidiane kuelimisha Umma kuhusu ufisadi huu na watanzania wafanye maamuzi ya nchi yao kwani wanayo haki ya kuhoji na kufaidi utajiri wa taifa lao kwani hawapo kwenye ardhi hii kama wakimbizi au tumbili kama inavyotambuliwa na Serikali ya CCM sasa. Wiki ijayo tutaanza ziara ziara Mkoani Kigoma wakati taratibu zingine zinaendelea kushughulikiwa. Wiki ijayo tutaanza ziara ziara Mkoani Kigoma wakati taratibu zingine zinaendelea kushughulikiwa.
Imesainiwa na;
…………………………….
NYAMBABE
KATIBU MKUU