Monday, October 16

Watoto wa Rohingya wazama wakikimbia mauaji Myanmar

Mkimbizi wa Rohingya aliyevuka mpaka kuingia Bangladesh akiwa anatayarisha makazi ya muda katika kambi ya wakimbizi
Polisi nchini Bangladesh wanasema watu watano wamezama, wanne kati yao ni watoto, na wengine wengi hawajulikani walipo.
Ajali hiyo imetokea baada ya boti lililokuwa na Waisalmu wa Rohingya 50 kutoka jimbo la Myanmar la Rakhine, walipokuwa wakielekea Bangladesh kwa kutumia mto Naf.
Serikali ya Bangladesh inasema kwamba waokoaji wameopoa miili ya mwanamke mmoja na watoto wanne katika eneo la tukio mapema Jumatatu.
Maafisa wa Bangladesh wanasema watu 21 wamesalimika katika ajali hiyo.
Vyanzo vya habari nchini Bangladesh vimeripoti kuwa zaidi ya Wa-Rohingya nusu milioni wameshavuka mpaka kuingia nchi ya jirani Bangladesh katika wiki za hivi karibuni.
Watu hao wanakimbia ili kujinusuru kutokana na mashambulizi yanayofanywa na jeshi la Burma, baada ya wanamgambo wa Rohingya kufanya mashambulizi kwa vikosi vya serekali.

Wanajeshi wa Iraq waingia Kirkuk, Wakurdi watoroka

Kirkuk on Oktoba 16, 2017Haki miliki ya pichaAFP
Image captionWanajeshi wakitumia trekta kuharibu bango la rais wa Wakurdi Massud Barzani kusini mwa Kirkurk
Wanajeshi wa serikali ya Iraq wameingia katikati mwa mji wa Kirkuk baada ya kuteka maeneo muhimu ya mji huo unaozozaniwa kutoka kwa wapiganaji wa Kikurdi.
Maelfu ya watu waliukimbia mji huo kabla ya wanajeshi wa Iraq kufika.
Jeshi la Iraq limeingia Kirkuk wiki tatu baada ya Jimbo la Kurdistan kuandaa kura ya maoni ya uhuru.
Wanajeshi hao wanalenga kuchukua tena udhibiti wa maeneo ambayo yamekuwa yakidhibitiwa na Wakurdi tangu wapiganaji wa Islamic State walipofurushwa maeneo hayo.
Wakazi wa maeneo yanayodhibitiwa na Wakurdi, yakiwemo Kirkuk, waliunga mkono pakubwa kura ya maoni ya kujitenga na Iraq iliyoandaliwa 25 Septemba.
Ingawa mji wa Kirkuk unapatikana nje ya jimbo la Kurdistan nchini Iraq, wakazi wa mji huo waliruhusiwa kushiriki kura hiyo ya maoni.
Waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi alishutumu kura hiyo na kusema ilikuwa kinyume na katiba.
Kirkuk, Iraq (16 Oktoba 2017)Haki miliki ya pichaREUTERS
Image captionJeshi la Iraq lilitangaza kwamba limedhibiti viwanda na visima vya mafuta baada ya wapiganaji wa Kikurdi wa Peshmerga kuondoka
Serikali ya jimbo la Kurdistan ilisisitiza kwamba ilikuwa kura halali.
Maafisa wa Marekani wamesema wanashauriana na pande zote kuzuia kuongezeka kwa uhasama.
Map showing Iraqi Kurdistan and areas controlled by Kurdish forces

Ukweli kuhusu njaa unauma sana

Ukweli unaohusiana na kitisho cha njaa miongoni mwa familia nyingi barani Afrika ni jambo linalouma sana, hasa inapozingatiwa kwamba hili ni bara lenye ardhi kubwa yenye rutuba, sambamba na rasilimali kadhaa.

Somalia Mogadischu | unterernährtes Kleinkind (DW/S. Petersmann)
Ni moja  ya matukio au hali kama hizi ambapo mtu hugunduwa kile hasa kinachotokea. Daktari na muuguzi wanaanza kumpatia matibabu na kumrejeshea pumzi mtoto mdogo. Mzazi ameduwaa pembezoni mwa kitanda.
Baada ya dakika chache, daktari anamtaka muuguzi asitishe jaribio lake. Kimya kinatawala. Baada ya hapo inasikika sauti ya kilio. Muuguzi anachukua chombo kimoja na kukiweka pembeni mwa kitanda cha hospitali. Hapo tena hatuoni kinachoendelea.
Tukio hili  katika zahanati moja kaskazini mwa Kenya, ni mojawapo ya hali za kuhuzunisha sana kuhusu utafiti wetu juu ya janga la njaa barani Afrika.
Inaonesha kwamba watu milioni 26 wanaokabiliwa na njaa si watu wenye kutiliwa maanani na ni wazi kwamba kinachowakabili baadhi yao ni zaidi na kitisho.  
Somalia Mogadischu | unterernährtes Kleinkind (DW/S. Petersmann)
Watoto nchini Somalia walio na ugonjwa wa utapiamlo
Msichana huyo mdogo katika zahanati hiyo nchini Kenya hakufariki dunia kwa sababu ya ugonjwa usiotibika au kutokana na ajali, lakini alifariki kwa sababu hakula kitu kwa muda mrefu.
Njaa si suala linalogonga vichwa vya habari

Kwa wiki kadhaa, waandishi habari wa Deutsche Welle wamekua wakifuatilia mzozo wa njaa barani Afrika. Wamezungumza na wasaidizi, wataalamu, wanasiasa na zaidi ya yote wahusika, ili kupata zaidi juu ya sababu ya watu wengi kuwa katika hali ya njaa.
Wakati wa kufanyika mradi huu si jambo la nadra. Tayari kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu, mashirika ya msaada yamekuwa yakitoa tahadhari kubwa kwamba hali mbaya kabisa ya ukame kuwahi kuonekana katika miongo ya karibu inaweza kuzuka barani Afrika na Yemen.
Lakini muda si mrefu baada ya hapo,  mzozo huo haukutiliwa maanani katika vichwa vya habari, licha ya kwamba hali leo bado haijaboreka . Katika nchi mbili zilizoathirika zaidi, Sudan Kusini na Somalia, zaidi ya  watu milioni 14 bado wanategemea msaada wa chakula.
Sababu ni binaadamu 
Nini kimesababisha hali hii? Jibu la mwandishi ni wazi: Sio maumbile lakini binadamu.
Mabadiliko ya tabia nchi duniani, ukataji miti mkubwa na kutumiwa kwa ardhi na kundi fulani tu la watu kunawafanya wadau wadogo wadogo kuzidi kukabiliwa na ugumu wa maisha.
Hunger in Somalia (picture-alliance/Photoshot)
Njaa nchini Somalia, wananchi wakipatiwa chakula cha msaada
Lakini mbali na hayo, migogoro ya kisiasa inasababisha uharibifu mkubwa zaidi. Nchi zinazoathirika zaidi ni kuanzia Nigeria hadi Sudan Kusini mpaka Somalia - ama  kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe au makundi ya kigaidi ambayo yanalifanya eneo zima kuwa lisilokuwa na usalama. Huduma ya afya, elimu au usalama ni sawa na kuwa neno la kigeni kwa raia wengi. Badala  yake kikundi kidogo cha watu kinajitajirisha  na mara nyingi kwa utajiri mkubwa.
Matumaini ya shaka shaka
Pamoja na hayo, kikundi cha waandishi habari kimerejea na ripoti za matumaini. Kwa mfano, Somalia ina serikali mpya tangu mwanzoni mwa mwaka baada ya zaidi ya  miaka 20 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Watazamaji wengi angalau wana matumaini yenye shaka shaka - na kila mahala waandishi walikutana na watu walio katika mazingira ya kipekee, lakini hawakukata tamaa.
Binadamu sio tu ndiye sababu wa  janga la njaa, lakini pia ndiye suluhisho. Zaidi kuhusu njaa barani Afrika kuanzia tarehe 16 Oktoba, sikiliza matangazo yetu ya Deutsche Welle kila siku kwenye anwani: www.dw.com.
Mwandishi: Jan-Phillip Scholz
Tafsiri: Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Iddi Ssessanga

ACT- Wazalendo kumjadili Mwigamba


Dar es Salaam. Chama cha ACT- Wazalendo kitakutana Ijumaa Oktoba 20, 2017 kujadili masuala kadhaa, likiwemo la kujizulu kwa mwenyekiti wake wa Kamati ya Kampeni na Uchaguzi Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Samson Mwigamba.
Mwigamba leo Jumatatu, Oktoba 16 ameandika barua ya kujizulu uongozi na kueleza atabaki kuwa mwanachama wa kawaida ili aweze kupata fursa ya kuwahoji kwa matendo viongozi.
"Nimeamua kukaa kando kwa kuwa tumekuwa hatukubaliani na baadhi ya mambo ndani ya chama na hasa kiongozi wetu… wacha nikae pembeni niwe mwanachama ili niwe na nafasi ya kuwahoji vizuri viongozi wetu masuala mbalimbali na nitabaki kuwa mwanachama mwema,’’ amesema alipozungumza na Mwananchi.
Akizungumzia uamuzi huo, Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe amesema, “Nimepokea barua yake. Tutatafakari suala hilo na masuala mengine yanayohusiana na hayo kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi wa chama Ijumaa.”
“Ndugu Mwigamba ataalikwa kwenye kikao hicho. Ninamshukuru sana kwa utumishi wake uliotukuka kwenye chama na ninamtakia kila la kheri. Mchango wake na kujitoa kwake kwa hali na mali hakutasahaulika kwenye chama chetu,” amesema  Zitto.

Mbowe kueleza maendeleo hali ya Lissu


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kesho Jumanne Oktoba 17, 2017 atazungumzia maendeleo ya afya ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Lissu aliyeshambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi akiwa katika makazi yake Area D mjini Dodoma Septemba 7, amelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya akiendelea na matibabu.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, baada ya kuulizwa kuhusu hali ya Lissu, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amesema:
“Kesho saa 5:00 asubuhi nitakuwa na mkutano na waandishi wa habari, nitazungumzia hali ya Lissuna mambo mengine yanayoendelea.”
Baadaye katika taarifa ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha chama hicho, Tumaini Makene amesema mkutano huo utafanyika makao makuu ya Chadema Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“Kupitia Mwenyekiti, Freeman Mbowe chama kitatoa taarifa kwa Taifa kuhusu maendeleo ya Tundu Lissu, mrejesho wa michango, gharama za matibabu,” amesema Makene.
MCL Digital itarusha mkutano huo moja kwa moja ku

ACT Wazalendo yaungana na Somalia kuomboleza


Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza kupokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya watu zaidi ya 250 vilivyotokea Mogadishu, nchini Somalia.
Vifo hivyo vimetokana na mlipuko wa mabomu yaliyokuwa yamewekwa ndani ya lori mjini Mogadishu.
Mbali ya vifo hivyo, watu zaidi ya 400 wamejeruhiwa katika tukio hilo.
Shambulio hilo linadaiwa kutekelezwa na kikundi cha kigaidi cha Al-Shabab usiku wa Jumamosi Oktoba 14, 2017.
Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatatu na Venance Msebo, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa ACT Wazalendo imesema inasikitisha kuona maisha ya mamia ya watu yakikatizwa kikatili, wakati viongozi, wananchi na taasisi mbalimbali duniani zikifanya juhudi kuhakikisha dunia inakuwa sehemu salama ya kuishi.
“Tunatoa pole kwa Serikali na wananchi wa Somalia, tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mamia ya ndugu zao,” imesema taarifa hiyo.
ACT Wazalendo imetoa wito kwa Serikali za Somalia na Tanzania, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Afrika na jumuiya za kimataifa kuendelea na juhudi za kuleta amani nchini Somalia.
“Juhudi za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kuepusha maafa na madhara zaidi yanayoweza kusababishwa na kutokuwepo usalama nchini Somalia,” amesema Msebo katika taarifa hiyo.
ACT Wazalendo imesema Somalia isipokuwa salama Afrika haiwezi kuwa salama

UPELELEZI WA KESI YA KUSAMBAZA TAARIFA ZA UONGO BADO HAUJAKAMILIKA


Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imeelezwa kuwa, upelelezi dhidi ya kesi ya kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii  wa Face book kuhusu mazungumzo kati ya Serikali na wawakilishi wa kampuni ya Acacia, inayomkabili Mkazi wa Chato Geita, Obadia Kiko bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali, Adolf Mkini amesema hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kesi hiyo ilipokuja kwa kutajwa.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 14 mwaka huu.

Katika kesi hiyo, inadaiwa Agosti 3, mwaka huu huko Chato Geita mshtakiwa obadia anadaiwa kusambaza maneno kuwa " Taarifa kutoka kikao cha mazungumzo kati ya Serikali na wawakilishi wa kampuni ya Acacia kuwa wanasheria wa upande wetu wanashindwa kutafsiri baadhi ya vifungu vya sheria hadi kufikia kuomba msaada kwa wanasheria wa Acacia sasa huoni hivi ni vituko mwizi anakusaidia sheria haahaa haha."

Inadaiwa aliendelea kusambaza maneno kuwa "Mazungumzo bado yanaendelea lakini wanasheria wetu wamebanwa sana ukizingatia wale jamaa wana vielelezo vyote vya mikataba kiukweli tumuombe mungu maana Serikali ikitaka kuvunja mkataba na Acacia gharama kubwa zitatuusu."

"Lakini pia kuendeleza uvyama utatugharimu saana,  baada ya mh. Rais Magufuli angewashirikisha Mawakili wasomi waliokwishaiva wakili Lissu, wakili Kibatara na Fatma Karume kwenye mambo ya umuhimu kama haya yeye kaleta uchama sasa itatugharimu .// Dicteta Magufuli mist go" . Maneno hayo yanadaiwa kusambazwa na mshtakiwa huyo kupitia mtandao huo wa kijamii wa Facebook.

Ilidaiwa kuwa maneno hayo yalikuwa na lengo la kupotosha umma

Sheikh Ponda afafanua kauli yake kwa wanahabari


Dar es Salaam. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda amesema alichozungumza hakikuwa uchochezi bali alitoa tahadhari kwa matukio yanayojitokeza na jinsi ya kuyakabili kwa mustakabali wa amani ya nchi.
Sheikh Ponda ametoa kauli hiyo kwa mara ya kwanza tangu alipotiwa nguvuni na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam akituhumiwa kutoa lugha ya uchochezi katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumatano wiki iliyopita.
Katika mkutano huo, alizungumzia masuala mbalimbali yakiwemo ya utekaji, kuokotwa miili ya watu na mazungumzo aliyoyafanya kati yake na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya akiuguza majeraha baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu baada ya kutoka kuripoti Polisi, Sheikh Ponda amesema, “Nilizungumza kwa nia nzuri kwa masilahi ya Taifa na umma. Nilikuwa nakumbushia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwamba vina wajibu wa kusimamia amani na usalama.”
Amesema, “Kile nilichozungumza nimewaeleza nilikuwa sahihi na sikuwa na nia mbaya hata kidogo… leo saa tatu nimeripoti na nimeelezwa niondoke na watakaponihitaji muda wowote watanipigia simu.”
Kuhusu upekuzi uliofanyika nyumbani kwake Ubungo- Kibangu, Sheikh Ponda amesema, “Tulikwenda kukagua siku hiyo ya Ijumaa kama saa mbili usiku, walidai wanatafuta kama kuna nyaraka zozote za uchochezi lakini hawakuzikuta. Tuliporudi polisi dhamana ilishindikana kwa kuwa wakubwa hawakuwepo.”
Ponda alijisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi Ijumaa Oktoba 13 asubuhi kwa wito wa Jeshi la Polisi lililompa saa 72.
Baada ya kujisalimisha alishikiliwa kwa mahojiano na baadaye askari walikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake na aliachiwa Jumamosi Oktoba 14 akitakiwa  kuripoti leo.

Makamu wa Rais akemea tochi kugeuzwa chanzo cha rushwa


Moshi. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewaonya askari wa kikosi cha usalama barabarani kutogeuza tochi kuwa chanzo cha kudai rushwa.
Pia, amewataka kutowanyanyasa madereva ambao wanazingatia sheria za usalama barabarani.
Kwa upande wa madereva amewataka kuwaona askari kuwa ni walinzi wao.
Amesema hayo leo Jumatatu katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani uliofanyika kitaifa mkoani Kilimanjaro katika viwanja vya Mashujaa mjini Moshi.
Samia amesema takriban asilimia 76 ya ajali za barabarani husababishwa na makosa ya kibinadamu kutokana na utumiaji wa simu wakati wa kuendesha gari, uchovu wa madereva na ulevi.
Amesema sababu nyingine zinazochangia ajali za barabarani ni miundombinu mibovu ya barabara inayochangia kwa asilimia nane na ubovu wa magari unaochangia kwa asilimia 16.
Makamu wa Rais amesema idadi kubwa ya ajali hizo zinasababishwa na uzembe wa waendesha bodaboda ambao unaweza kuepukika.
Samia amesema Taifa limeendelea kupoteza nguvu kazi, watu kupata ulemavu wa maisha na wengine kubaki wajane.
“Mwaka huu kuanzia Januari hadi Septemba kumekuwa na ajali za pikipiki 42,721 zilizoua watu 1,613 na kusababisha majeruhi 1,597,” amesema.
Amesema Mkoa wa Kilimanjaro umeripotiwa kuwa na ajali 84 za bodaboda zilizosababisha vifo 61 na majeruhi 21.
Samia ameeleza kusikitishwa kwa Tanzania kutajwa katika ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa ni nchi inayoongoza kwa ajali ikiwa na asilimia 33.
Ameliagiza Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na wadau kuzingatia na kuelekeza nguvu kwenye kudhibiti makosa makubwa matano hatarishi.
Ameyataja makosa hayo kuwa ni mwendo kasi, ulevi, kutovaa kofia ngumu, kutovaa mikanda ya usalama katika gari na ukosefu wa vifaa vya usalama kuwalinda watoto wadogo wakiwa ndani ya gari.
Makamu wa Rais amewataka kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa watumiaji wote kupitia taasisi mbalimbali, kujipanga na kuhakikisha wanabadilishana uzoefu wa namna ya kukabiliana na tatizo la ajali.
Amewataka kutoa machapisho yenye kutoa elimu kwa makundi yote ya watumiaji wa barabara na kusimamia mafunzo ya umahiri wa uendeshaji wa vyombo vya moto.
Pia, amewataka askari wa usalama barabarani kufanya doria za mara kwa mara katika barabara kuu na za ndani ili kudhibiti makosa ya usalama barabarani na ajali zisizo za lazima.
Kwa upande wa abiria amewataka kuwa makini na kujenga tabia ya kutoa taarifa za uvunjifu wa sheria za usalama barabarani.

Ray C apiga marufuku nyimbo zake kuimbwa jukwaani


Dar es Salaam. Mwanamuziki Rehema Chalamila ‘Ray C’ amesema hatasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanamuziki wanaoimba nyimbo zake bila makubaliano
Nyota huyo ambaye kwa sasa yupo nje ya nchi ameimbia Mwananchi kuwa hawezi kuvumilia vitendo hivyo kwasababu vinalenga kumuharibia biashara yake ya muziki ambayo ndio maisha yake.
Amesema, “Muziki ni biashara huwezi ukalipwa pesa nyingi halafu ukapanda jukwaani ukaimba nyimbo za msanii mwingine bila makubaliano. Huu ni ufinyu wa ubunifu,”
Kauli hiyo ya Ray C imekuja siku moja baada ya kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa hakufurahishwa na kitendo cha Nandy kuimba wimbo wake bila ridhaa yake.
Aliandika, “Jamani hii tabia siyo nzuri. Kama mnaona umuhimu wa sauti yangu kwenye show zenu muwe mnaniita basi. Sina saratani ya koo ya kushindwa kuziimba hizo nyimbo! Nandy hii ni mara ya mwisho ukipanda tena fanya kazi zako.
Hii ni mara ya pili ujue! Mashabiki zangu hamuwatendei haki, maana hatatukigongana muda mwingine hata salamu hamnipi kwa hiyo sitaki mazoea,”
Haikupita muda mrefu Nandy naye akajibu, “Dada angu Ray C, mimi ni mmoja wa wasanii wanaokukubali ulikuwa miongoni mwa watu mliotufungulia njia ya muziki wetu ulipo. Sitaacha kukuheshimu na kukubali, siamini kukusifia na kukuenzi ni lazima uwe umekufa’’.
“Nafanya jambo hili zuri kwa moyo wangu mzuri kama ulivyomuenzi mama Mwanahela kwa nyimbo zake. Heshima yangu kimuziki kwako itabaki siku zote kama nilivyoimba nyimbo za wengine,”.
Hata hivyo Ray C amesema hana ukaribu wala mazoea na Nandy kiasi cha kuamua kuimba nyimbo zake bila makubaliano.
 “Sikutaarifiwa na wala sikushirikishwa, mimi nilishawahi kurekodi cover za Mwanahela lakini nilimfuata nikamlipa na akanipa baraka zake. Sheria za hatimiliki zinajulikana ndiyo maana tuna Cosota,”

Nabaki Afrika: Mauzo vifaa vya ujenzi yameshuka, ukandarasi yameongezeka


Kutokana na uchumi wa wananchi kubana, biashara ya vifaa vya ujenzi wa nyumba imepungua huku vile vya ukandarasi wa miradi mikubwa ukiongezeka zaidi ya mara dufu.
Hayo yamebainishwa na meneja mkuu wa Kampuni ya Nabaki Afrika, Mark McCluskey mwishoni mwa wiki alipozungumza na gazeti hili kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii (Site) ya siku tatu yaliyomalizika mwishoni mwa juma.
Tangu mwaka huu uanze, McCluskey alisema uuzaji wa vifaa vya ujenzi umepungua kwa asilimia 10 ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka jana.
“Tumeuza asilimia 50 tu ya vifaa hivyo mwaka huu. Hata hivyo vifaa kwa ajili ya ujenzi wa barabara mauzo yake yameongezeka kwa asilimia 1,000 (mara 10 zaidi),” alisema McCluskey.
McCluskey alisema ongezeko katika mauzo ya vifaa vya utengenezaji wa barabara ni matokeo ya mipango na usimamizi wa Rais John Magufuli ambaye anatekeleza miradi mingi ya aina hiyo sanjari na kusimamia ubora.
Kuhusu kusambaza na kupigia debe bidhaa zinazotengenezwa nchini McCluskey alisema kipaumbele chao kwenye bidhaa yoyote bila kujali ilikotengenezwa ni ubora.
“Kuna bidhaa kadhaa tunachukua nchini lakini nyingine tunaagiza kutoka nje ya nchi kupata ubora stahiki ambao unatufanya tuendeee kuwa imara sokoni. Katika utengenezaji wa baadhi ya bidhaa inahitajika teknolojia ya hali ya juu ambayo wakati mwingine inakuwa bado haijafika nchini,” alisema McMluskey.

MHASIBU WA UBALOZI AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA UTAKATISHAJI FEDHA

  Mhasibu wa Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Joyce Moshi, (56) akitoka katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo mara baada ya kusomewa mashtaka aliyonayo.

Na Karama Kenyunko, Blogu ya Jamii.
MHASIBU wa Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Joyce Moshi, (56), leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka tisa matatu ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo  wizi akiwa mtumishi wa umma, kujipatia fedha kwa njia ya uongo na utakatishaji wa fedha USD 150,000.

Mwendesha mashtaka wakili wa serikali, Wankyo Simon amedai Octoba 25 mwaka jana, katika ofisi ya Ubalozi wa Tanzania katika jiji la Maputa nchini msumbiji mshtakiwa Joyce kwa lengo la kufanya udanganyifu alighushi barua ya tarehe 25 October 2016 kwa madhumuni ya kuonesha kuwa ubalozi wa Tanzania nchni Msumbiji umeelekeza benki ya Millenium Bim, Maputo kuamisha USD 10,000 kutoka akaunti namba 79667362 kwenda akaunti namba 182283177 inayomilikiwa na Joyce Moshi.

Imedaiwa kuwa, akaunti zote hizo zipo katika benki ya Millennium Bim-Julius Nyerere Maputo, huku akijua kuwa siyo kweli.
Aidha mshtakiwa Joyce anayeishi Temeke anadaiwa Februari 10 mwaka huu huko huko Ubalozini nchini msumbiji, alighushi USD 100,000 na pia Aprili 12 mwaka huu alighushi tena USD 40,000.
Katika shtaka linguine Wankyo alidai kuwa, Oktoba 25, mwaka jana katika benki ya Millenium Bim-tawi la Julius Nyerere lililopo Maputo nchini Msumbiji. 

Imedaiwa, mshtakiwa akifahamu na kwa njia ya udanganyifu aliwasilisha nyaraka ambayo ni barua ya tarehe Oktoba 25 mwaka jana kwa dhumuni la kuonyesha kuwa,  ubalozi wa Tanzania nchni Msumbiji umeelekeza benki ya Millenium Bim, Maputo kuamisha USD 10,000 kutoka akaunti namba 79667362 kwenda akaunti namba 182283177 inayomilikiwa na Joyce Moshi.
 
Pia aligushi barua ya Februari 10 mwaka huu ili kuhamisha USD 100,000 na barua ya Aprili 12 mwaka huuu ili kuhamisha USD 40,000.
Mshtakiwa Joyce anadaiwa pia kuwa, katika siku tofauti tofauti kati ya Oktoba 25 mwaka jana na Aprili mwaka huu, katika ofisi hizo za Ubalozi, akiwa muajiriwa wa utumishi wa umma wa kitengo cha fedha ubalozini hapo, aliiba USD 150,000 mali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania.

Pia Joyce anadaiwa kujipatia kiasi hicho cha pesa kwa njia ya udanganyifu kwa kujifanya kuwa ameelekezwa kutoa fedha hizo kutoka akaunti namba 79667362 kwenda akaunti namba 182283177 inaymilikiwa na Joyce Moshi huku akaunti zote hizo zimehifadhiwa kwenye benki hiyo ya Millenium.

katika shtaka la mwisho imedaiwa, katika tarehe tofauti kati ya Octoba 25 mwaka jana na Aprili 12 mwaka huu alijipatia USD 150,000 huku akijua kuwa fedha hizo ni matokeo ya kosa la kughushi.

Hata hivyo, mshtakiwa amekana shtaka hilo na amerudishwa rumande kwa kuwa kosa la utakaishaji halina dhamana na kesi hiyo imeairishwa hadi Octoba 30 mwaka huu.

VYAKULA UNAVYOTAKIWA KUEPUKA KULA KAMA UNATAKA KUPUNGUZA UZITO WA MWILI

Na Jumia Travel Tanzania

Leo siku ya Oktoba 16 dunia inaadhimisha Siku ya Chakula Duniani ambapo Shirika la Chakula Duniani (FAO) kila mwaka huadhimisha kwa shughuli na kauli mbiu mbalimbali. Kwa mwaka huu kauli mbiu ni ‘Badili Hali ya Uhamiaji ya Baadaye: Wekeza Katika Usalama wa Chakula na Maendeleo ya Vijijini.’ Kwa mujibu wa FAO, dunia inapitia mabadiliko kadha wa kadha kila kukicha. 

Watu wengi wamelazimika kuhama makazi yao kutokana na sababu tofauti kama vile kuongezeka kwa migogoro na kutokuwepo usalama wa kisiasa. Lakini njaa, umasikini, na kuongezeka kwa matukio ya hali ya hewa yanayochangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa ni sababu zingine za muhimu zinazochangia katika kupelekea watu kuhama.
Miongoni mwa changamoto kubwa inayowakumba watu siku za hivi karibuni ni katika upatikanaji wa chakula, matumizi yake na namna ya kudhibiti ili kutoleta athari katika mwili. Kwa kuwa leo ni maadhimisho ya ‘Siku ya Chakula Duniani,’ Jumia Travel ingependa kukushirikisha aina za vyakula vya kupunguza au kuacha kula kabisa kama unataka kupunguza uzito wa mwili wako.
Chipsi. Kwa wakazi wengi wa sehemu za mijini kama vile jiji la Dar es Salaam, chipsi ni mojawapo ya chakula kinachotumiwa na idadi kubwa ya watu. Na hii ni kutokana na upatikanaji wake kwa urahisi karibu kwenye kila maeneo wanapoishi. Kwa mujibu wa tafiti, chakula hiki kinaongeza uzito  mwilini kutokana na kuwa na kalori nyingi ndani yake na ni rahisi kuzila nyingi zaidi kwa mpigo. Tafiti pia zinaendelea kwa kuelezea kuwa chipsi pengine ndiyo chakula kinachochangia kuongeza uzito kuliko chakula chochote. Hivyo basi, kwa afya yako unashauriwa kuvichemsha kwa maji na kula badala ya kukaanga.
Vinywaji vyenye sukari nyingi. Vinywaji vinavyotengenezwa na kuongezewa sukari ili kuwa vitamu vinatajwa kuwa ni mojawawapo vyakula hatari zaidi kiafya duniani. Vinahusishwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa uzito na vinaweza kuwa na madhara zaidi mwilini endapo vitatumiwa kwa kiasi kikubwa. Ingawa vyakula hivi huwa na kalori nyingi lakini ubongo wako hauvitambui kama ni vyakula vigumu. Kwa hiyo, kama una nia ya dhati kabisa ya kupungua uzito ni vema ukaachana na vinywaji vya aina hii.

Chokoleti. Inafahamika watu wengi hupendela chokoleti kutokana na utamu wake lakini ni hatari sana kiafya. Hutengenezwa kwa kuongezewa sukari nyingi zaidi, mafuta na unga uliosafishwa zaidi kiwandani kwa kiasi fulani. Chokoleti zina kalori nyingi huku virutubisho vikiwa ni vichache. Kipande cha kawaida cha chokoleti kina kadiriwa kuwa kalori takribani 200-300, huku vipande vikubwa zaidi vinaweza kuwa nazo nyingi zaidi. Lakini kwa bahati mbaya unaweza kukutana na chokoleti karibu kila mahala tena zikiwa zimewekwa kwa kutamanisha zaidi ili kukushawishi kununua. Inashauriwa kama unataka kula chakula kidogo cha kawaida badala yake kula kipande cha tunda au karanga angalau.
Juisi za viwandani. Juisi nyingi za matunda unazoziona madukani zinakuwa na virutubisho vidogo sana ukilinganisha na tunda halisi. Nyingi huwa zinatengenezwa viwandani na kuongezewa sukari. Kiukweli, huwa na sukari nyingi na kalori sawa na soda, tena inawezekana vikazidi. Kwa kuongezea juisi za viwandani hazina nyuzinyuzi ambazo unaweza kuzipata kwenye matunda halisi. Hivyo basi unashauriwa ni vema ukala tunda kamili badala ya juisi kwani faida zake haziwezi katu kulingana kama wengi tunavyoamini.

Mikate, biskuti na keki. Vyakula hivi huongezewa na virutubisho vingi ambavyo havina faida kwa mwili. Tena wakati mwingine huongezewa mafuta hatarishi ambayo yanahusishwa kuwa chanzo cha magonjwa tofauti. Kwa kawaida vyakula hivi havishibishi hivyo utatamani kuvitumia zaidi na hivyo kupelekea kula sumu zaidi.
Baadhi ya vileo (hususani bia). Kwa kiasi kikubwa pombe hutuongezea kalori nyingi kuliko wanga na protini mwilini mwetu. Hata hivyo, suala la kunywa pombe na kuongezeka uzito bado halijadhibitishwa moja kwa moja. Unywaji wa pombe wa kawaida unaweza kuwa hauna matatizo na wakati mwingine huhusishwa na kupunguza uzito. 
 
Lakini kwa upande mwingine, unywaji wa kupindukia hupelekea kuongezeka kwa uzito wa mwili. Aina ya kileo unachokunywa pia ni kitu cha kuzingatiwa. Kwa mfano, unywaji wa bia unawdza kupelekea kuongezeka uzito, huku unywaji wa divai (wine) unaweza kuwa na faida kwa afya ya mwili.

Aiskrimu. Chakula hiki ni kitamu sana lakini ni hatari kwa afya ya mwili wako. Kwani kina kalori nyingi na huongezewa sukari nyingi kwenye utengenezaji wake. Matumizi kwa kiasi kidogo hayana madhara lakini ni vigumu sana kujizuia kutokutumia kiasi kikubwa kwa wakati mmoja. Unaweza kutengeneza wewe mwenyewe nyumbani ili kuweka virutubisho vingi zaidi lakini pia kujizuia kutumia nyingi zaidi, tenga kiasi kidogo na kingine kifiche ili kujizuia zaidi.

Pizza. Chakula hiki ni maarufu sana maeneo ya mijini kutokana na upatikanaji wake wa haraka lakini sio vizuri kiafya kabisa. Huwa na kalori nyingi na kutengenezwa kwa kuongezewa virutubisho hatari kwa afya kama vile unga na nyama zinazochakatwa viwandani.
Kutokana na makala haya unaweza kuwa umegundua kwamba vyakula vingi huwa vinatengenezwa viwandani na kuwekewa kemikali nyingi ili kuongezewa ladha na kutumika kwa muda mrefu zaidi. Jumia Travel ingepependa kukushauri kula vyakula vya asili zaidi au kupika mwenyewe kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unajitengenezea fursa ya kuepuka magonjwa mengi zaidi sasa na siku za usoni.

Vigogo wa chuo cha Uhasibu (TIA) wapata dhamana.


Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.

Baada ya kukaa gerezani kwa siku tano, leo vigogo wawili wa zamani wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) wameachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana waliyopewa ma Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Washtakiwa hao ambao wametimiza masharti ya na kuachiwa kwa Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba ni, Kaimu Mtendaji wa (TIA), Shaha Hanzuruni na Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Onesphor Luhungu wa Hakimu Mkazi Mkuu, 

Katika masharti yao ya dhamana kila mshtakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini bondi ya milioni 250 na pia mdhamini mmoja kati ya wadhamini hao kuwasilisha fedha taslimu mahakamani Sh 250 milioni ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha na kwamba mali hiyo ni lazima iwepo Dar es Salaam.

Mbali na hayo kila mshtakiwa alitakiwa kusalimisha pasi yake ya kusafiria mahakamani na wasitoke nje ya jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha Mahakama.

Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 24,2017 ambapo washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali (PH).Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka na kusababisha hasara ya Sh 1, 097,681,107.

Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Takukuru, Leonard Swai akiwasomea hati ya mashtaka washtakiwa hao alidai kuwa, kati ya Januari Mosi, 2012 na Desemba 30,2014 katika Chuo cha Uhasibu Tanzania kwa nafasi zao, walitumia madaraka vibaya kwa kutofuata taratibu za ununuzi katika kununua ardhi ya kampasi ya Chuo cha TIA Mwanza.

Alidai kuwa kitendo hicho kilisababisha Vedastus Ngasa Lukago kupata manufaa ya Sh 1, 097, 681,107.

Swai alidai kuwa, katika kipindi hicho cha Januari Mosi,2012 na Desemba 30,2014 washtakiwa hao wakiwa waajiliwa wa Chuo hicho, kwa ridhaa na kwamatendo yao walisababisha hasara ya Sh 1, 097,681,107.

Fedha ambayo ni Mali ya Chuo cha Uhasibu Tanzania kutokana na kutokufuata taratibu za manunuzi wakati wa kusaini mkataba wa ununuzi wa ardhi ya Chuo Cha Uhasibu Tanzania kampasi ya Mwanza.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.Washtakiwa hao, wanatetewa na Wakili , Jamuhuri Johnson.

AJALI ZA BODABODA ZINACHANGIA ONGEZEKO LA WENYE MATATIZO YA UBONGO

Ajali za pikipiki maarufu bodaboda, zimechangia matatizo ya ubongo kiwango kikubwa kulinganisha na ajali nyingine.
Mbali na ajali za bodaboda, kuanguka kwenye mti nayo inadaiwa kuongeza idadi ya Watanzania wenye matatizo ya ubongo hasa kupasuka kwa mishipa ya fahamu na saratani ya ubongo.
Daktari Bingwa wa Upasuaji Ubongo na Mishipa ya Fahamu wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Samuel Swai amesema leo kutokana na hali hiyo serikali hulazimika kuwapatia rufaa ya matibabu wagonjwa kati ya saba hadi nane kwenda nchini India ambako yanatolewa katika utaalamu wa kiwango cha hali ya juu.
“Ingawa Moi ina uwezo wa kufanya upasuaji wa ubongo hata hivyo hulazimika kuwapatia rufaa wagonjwa ambao huhitaji huduma ya kibingwa zaidi kwenda India kwa sababu bado hatujitoshelezi Kwa upande wa vifaa na gharama za matibabu ni kubwa ambapo mgonjwa mmoja hugharimu kati ya Sh milioni 20 hadi 25 kufanikisha upasuaji ambazo serikali hugharamia,” amesema.