Friday, December 1

Polisi wamshikilia mwanamke aliyemvika mwenzake pete ya uchumba


Geita. Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mtumishi wa mgodi wa GGM, Milembe Suleiman anayetuhumiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsi moja.
Mfanyakazi huyo ambaye ni ofisa ugavi kitengo cha manunuzi anashikiliwa baada ya ‘video’ inayomwonyesha akimvisha pete ya uchumba mwanamke mwenzake kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
Video hiyo ambayo imezua mijadala hasa ikizingatia kwamba iko kinyume cha utamaduni wa Kitanzania na Serikali ambayo imekuwa ikikemea na kupiga marufuku vitendo vya mapenzi ya jinsi moja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo amesema wanamshikilia kwa uchunguzi kwa kuwa nchi hairuhusu mambo hayo.
Ofisa Habari wa GGM, Dili Tenga amesema hayo ni masuala binafsi ya mfanyakazi hivyo wao kama mgodi hawawezi kuyazungumzia lakini wanaviachia vyombo vya dola viendelee na uchunguzi wake.

Aliyepandikizwa figo Muhimbili aenda nyumbani


Dar es Salaam. Mgonjwa wa kwanza kupandikizwa figo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prisca Mwingira  ameruhusiwa kurudi nyumbani leo Ijumaa baada ya kuwa chini ya uangalizi wa jopo la madaktari bingwa wa figo kwa siku 10.
Prisca (30) ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mikese mjini Morogoro, amechangiwa figo na mdogo wake Batholomeo Mwingira (27).
Akizungumza na vyombo vya habari leo Ijumaa mara baada ya kutoka chumba cha uangalizi maalum (ICU), Prisca ameishukuru Serikali kugharamia matibabu yake na kuiomba kuwekeza zaidi katika matibabu ya kibingwa ili kusaidia Watanzania wengi wasio na uwezo wa kufuata gharama nje ya nchi.
“Kwa kipekee napenda kumshukuru sana ndugu yangu, kaka yangu Batholomeo kwa kupenda niendelee kuishi. Madaktari bingwa wa figo Muhimbili tangu wamenipokea wamekuwa wakinipa matibabu mbalimbali, nimesafishwa damu kwa muda wa mwaka mmoja wamenishauri na mpaka katika matibabu ya kupandikiza figo nyingine,"

Ajira 200,000 kutolewa


Arusha. Shirika lisilokua la Kiserikali  la Hand in Hand Eastern Afrika  linatarajia kutengeneza ajira 200,000 kwa miaka mitano katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2022 kwa kuwezesha vikundi vya uzalishaji kufungua biashara mpya pamoja na kuziendeleza zilizopo .
Mpango huo utafanyika kwa kushirikisha wadau mbalimbali ikiwemo serikali na taasisi binafsi kwa kuhakikisha kuwa vikundi vya uzalishaji vinawezeshwa na kupatiwa mikopo ili kupanua wigo  utakaosababisha ongezeko la ajira nchini.
Ofisa Mkuu wa Shirika hilo Afrika Mashariki, Albert Wambugu amesema leo Desemba mosi  kuwa wamekua wakitoa mafunzo katika vikundi vya uzalishaji juu ya kuanzisha biashara mpya ,kuboresha ambazo tayari zimeanzishwa pamoja na jinsi ya kujiwekea akiba na kuwekeza.
Ofisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Arusha, Blandina Nkini amesema kuwa serikali imekua ikitoa mikopo kwa wanawake na vijana ili kupunguza tatizo la ajira kwa kuhamasisha watu kujikita katika shughuli za uzalishaji mali na kujiajiri.
“Taasisi binafsi zinapaswa kushirikiana  na serikali kuangalia ni jinsi gani tunaweza kuondoa umasikini miongoni mwa vijana wengi kwa kuwapa stadi za kazi na kuwaongezea mitaji kwenye biashara ambazo zimeshaanzishwa sanjari na kuwawezesha kupata masoko” amesema Nkini
Amesema wakati nchi  inaelekea kwenye uchumi wa viwanda ,wanawake na vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuzalisha mali ghafi za viwanda pamoja na wao wenyewe kuanzisha viwanda.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kenyatta ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Shirika hilo, Catherine Ndungo amesema malengo ya kuanzishwa shirika  hilo ni kuwasaidia watu wenye kipato cha chini ya dola moja kwa siku ambayo ni sawa na Sh2,000 kupatiwa kuwapatia mbinu za kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Droo Kombe la Dunia: Nigeria wakabidhiwa Argentina tena

World Cup draw stageHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Nigeria wamepangwa kwenye kundi moja na Argentina kwa mara nyingine, Misri nao wakapangwa na Urusi na Uruguay baada ya droo ya Kombe la Dunia 2018 kufanywa nchini Urusi.
Panama, ambao wanacheza Kombe la Dunia mara ya kwanza wamepangwa na Ubelgiji na England na Tunisia.
Iceland, walioshangaza wengi kwa kufuzu, wamepangwa kucheza na Nigeria, Croatia na Argentina katika Kundi D.
Mechi ya ufunguzi itakuwa kati ya Urusi na Saudi Arabia.

Droo kamili ya Kombe la Dunia:

  • Kundi A: Urusi, Saudi Arabia, Misri, Uruguay
  • Kundi B: Ureno, Uhispania, Morocco, Iran
  • Kundi C: Ufaransa, Australia, Peru, Denmark
  • Kundi D: Argentina, Croatia, Iceland, Nigeria
  • Kundi E: Brazil, Uswizi, Costa Rica, Serbia
  • Kundi F: Ujerumani , Mexico, Sweden, Korea Kusini
  • Kundi G: Ubelgiji , Panama, Tunisia, England
  • Kundi H: Poland, Senegal, Colombia, Japan.
Mpangilio wa mechi za makundi
A
B
C
D
E
E
G
H

Nani wanapigiwa upatu kushinda?

Mabingwa watetezu Ujerumani wanapigiwa upatu kushinda, wakifuatwa na Brazil, Uhispania, Argentina, Ufaransa, Ubelgiji na kisha England.
Ujerumani chini ya Joachim Low wanatafuta kuwa nchi ya kwanza kushinda Kombe la Dunia mtawalia tangu Brazil wakiwa na Pele 1958 na 1962.
Nani alivutia zaidi mechi za kufuzu?
GermanyHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionIreland Kaskazini walikuwa miongoni mwa timu tano ambazo zilishindwa mechi zote mbili na Ujerumani mechi za kufuzu
Ujerumani hawajashindwa mechi hata moja ya fainali za au za kufuzu kwa Kombe la Dunia tangu nusu fainali ya 2010 dhidi ya Uhispania.
Walimaliza michuano ya kufuzu 2018 wakiwa wameshinda mechi 10 kati ya kumi walizocheza, na kufunga mabao 43. Walifungwa mara nne pekee.
Ubelgiji, Uhispania na England wote walimaliza mechi za kufuzu Ulaya bila kushindwa.
Brazil walitamba mechi za kufuzu Kombe la Dunia - lakini baada ya kumuondoa meneja Dunga na kumuingiza Tite.
Barani Asia, Iran walipitia makundi mawili bila kushindwa - mechi 18 bila kushindwa, ambapo mechi 12 kati ya hizo hawakufungwa bao hata moja.
Morocco walifuzu bila kufungwa bao hata moja katika kundi lao la kufuzu Afrika, ambapo walimaliza juu ya Ivory Coast.
Nani wanacheza mara ya kwanza?
PanamaHaki miliki ya pichaTWITTER
Image captionRais wa Panama Juan Carlos Varela alitangaza sikukuu ya taifa baada yao kufuzu
Iceland ndiyo nchi ya kwanza pekee yenye raia ambao ni chini ya milioni moja kuwahi kufika Kombe la Dunia.
Hawakuwa wamefuzu kwa michuano mikubwa kabla ya kushiriki Euro 2016 ambapo waliwalaza England katika safari yao ya kufika robo fainali.
Panama, taifa la Amerika ya Kati, nao walifika Kombe la Dunia baada ya bao la ushindi la dakika ya 88 dhidi ya Costa Rica, bao ambalo pia liliwazuia Marekani kufuzu.
Nani miamba ambao wameachwa nje?
Christian PulisicHaki miliki ya pichaEPA
Image captionMarekani walilazwa na 2-1 Trinidad & Tobago na kushindwa kufuzu Kombe la Dunia
Walioshangaza zaidi walitoka Ulaya.
Mabingwa mara nne Italia walishindwa kufuzu kwa mara ya kwanza tangu 1958 baada ya kuondolewa na Sweden.
Uholanzi pia walishindwa kufuzu.
Jamhuri ya Czech, Wales, Scotland, Austria, Bosnia-Herzegovina na Uturuki ni miongoni mwa nchi nyingine za Ulaya zilizoshindwa kufuzu hatua ya makundi.
Jamhuri ya Ireland, Ireland Kaskazini na Ugiriki pia waliondolewa kwenye mechi za muondoano za kufuzu baada ya makundi.
Jimbo la Concacaf, Marekani walishindwa kufuzu kwa mara ya kwanza tangu 1986.
Barani Afrika, Ivory Coast, Cameroon na Ghana - wote ambao walishiriki Kombe la Dunia Brazil 2014 - pia hawakufuzu.
Chile, walioorodheshwa nafasi ya tisa duniani, pia walishindwa kufuzu.
Tiketi zinauzwaje?
Fifa wamepokea maombi 3.5 milioni ya tiketi, 300,000 yakiwa maombi ya tiketi za mechi ya fainali uwanjani Luzhniki.
Asilimia 57 ya maombi yametoka kwa wakazi wa je ya Urusi.
Tiketi ya bei nafuu zaidi ya fainali Kombe la Dunia ambayo raia asiye wa Urusi anaweza kununua ni ya £345.

Sita washikiliwa kwa kukutwa na mifupa ya albino, ulimi wa simba


Mbozi. Watu sita wanashikiliwa na polisi mkoani Songwe kwa tuhuma za kukutwa na vipande vitatu vya mifupa ya mtu wanayedai kuwa ni albino, pamoja na mafuta na ulimi unaodhaniwa kuwa wa simba.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Mathias Nyange alisema jana kuwa watu hao walikamatwa juzi saa 7:00 mchana katika mji wa Tunduma wilayani Momba na askari waliokuwa doria.
Alisema watuhumiwa hao walikutwa na mafuta ya simba, mifupa mitatu ya albino, mfupa mmoja wa mnyama ambaye hajajulikana, na vipande viwili vya ulimi, vitu vinavyosadikiwa kuwa ni vifaa vya tiba asili.
Kamanda Nyange alidai kuwa baada ya kuhojiwa, watuhumiwa walikiri kuwa mifupa waliyokutwa nayo ni ya albino waliyemkata mkono mkoani Morogoro.
Alisema kati ya watuhumiwa hao wawili ni wakazi wa Morogoro, wawili wakazi wa Mbozi, mmoja ni mkazi wa Wilaya ya Momba na mwingine ni kutoka Nakonde nchini Zambia.
Nyange alisema watuhumiwa hao wanatarajia kupelekwa mkoani Morogoro ambako ndiko wanakotuhumiwa kutenda kosa.
Wakati huohuo, Nyange amesema watu watatu wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 na 30 wamefariki dunia baada ya kupigwa risasi na askari waliokuwa doria saa 4:00 usiku wa Novemba 30 baada ya kukaidi amri ya kusimama ya polisi ambao waliwatilia shaka.
Baada ya kukataa kutii amri ya kusimama, polisi waliwafuatilia na baadaye watu hao walianza kuwafyatulia risasi, jambo ambalo kamanda huyo alisema liliwalazimisha askari kuanza kujibizana nao.
Alisema baada ya kuwapekua walikutwa na silaha moja aina ya bastola iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za short gun ikiwa na risasi moja na pia walikutwa na mapanga mawili pamoja na kipande kimoja cha nondo.

Trump na Urusi: Mshauri wa zamani Michael Flynn akiri kuwahadaa FBI

Michael Flynn arrives at Washington court for hearing on 1 Dec 2017Haki miliki ya pichaREUTERS
Image captionMichael Flynn akiwasili Washington
Aliyekuwa mshauri mkuu wa masuala ya usalama wa taifa wa Donald Trump, Michael Flynn, amekiri kwamba aliandikisha taarifa ya uongo kwa idara ya uchunguzi wa jinai ya Marekani, FBI, mwezi Januari.
Bw Flynn alishurutishwa kujiuzulu mwezi mmoja baada yake kupotosha ikulu ya White House kuhusu mkutano wake na balozi wa Urusi kabla ya Trump kuingia madarakani.
Mashtaka dhidi yake yaliwasilishwa na mwanasheria maalum Robert Mueller kama sehemu ya uchunguzi kuhusu tuhuma kwamba Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani wa 2016.
Bw Flynn alifika mahakamani Ijumaa.
Alikiri kosa moja ya kutoa makusudi "taarifa za uongo, za kubuni na za kupotosha".
Kwa mujibu wa mwanahabari wa AFP, Bw Flynn aliulizwa na Jaji Rudolph Contreras iwapo alitaka kukiri makosa hayo na akajibu kwa kusema "Ndio".
Jaji aliendelea: "Nakubali kukiri kwako makosa. Hivyo hakutakuwa na kusikizwa kwa kesi na labda huenda kusiwe na rufaa."
Alijisalimisha kwa FBI kabla ya kufanyika kwa kikao cha mahakama Ijumaa asubuhi mjini Washington DC.
Msaidizi huyo wa zamani wa Trump ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi katika utawala wa Trumpa ambaye amepatikana na hatia katika uchunguzi huo unaoendeshwa na Mueller.
Michael FlynnHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionMichael Flynn alijiuzulu Februari
Oktoba, meneja wa zamani wa kampeni za urais wa Trump, Paul Manafort, alituhumiwa kula njama ya kuilaghai Marekani katika shughuli za kibiashara na Ukraine.
Aidha, iliibuka kwamba msaidizi mwingine wa zamani, George Papadopoulos, amekiri makosa ya kutoa taarifa za uongo kwa maajenti wa FBI.

Ukimwi tishio Njombe



Dar es Salaam. Mkoa wa Njombe umetajwa kuongoza kuwa na asilimia 11.4 ya watu wanaishi na virusi vya Ukimwi huku Zanzibar wanaoishi na virusi hivyo ni chini ya asilimia 1.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa ametoa takwimu hizo leo Desemba 1 katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani ambayo Kitaifa imefanyika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Dk Chuwa amesema mkoa wa Lindi umekuwa wa mwisho kwa watu wenye virusi  vya ukimwi na  idadi ya asilimia  0.1 huku maambukizo kwa Jiji la Dar es Salaam yamepungua hadi kufikia asilimia 4.7 ikiwa na maana watu 133,971 wanaishi na ugonjwa huo.
Mkurugenzi huyo amesema kwa ujumla watu 1.4 milioni nchini Tanzania wanaishi na virusi vya Ukimwi na takwimu hizo ndiyo rasmi hivyo asitokee mtu au kikundi cha watu kupotosha.
"Nasema kwa sababu kuna watu wanakurupuka na kuja na takwimu zao. Naomba watambue takwimu ni fani kama fani nyingine na zina miiko yake," amesema Dk Chuwa
Hata hivyo, Dk Chuwa amesema Serikali haimzuii mtu au kikundi kufanya utafiti ila ni lazima awasiliane na ofisi ya takwimu wapitie dodoso zake kabla ya kuruhusiwa kufanya.
Amesema atakayekiuka na kupotosha takwimu adhabu yake iliyowekwa kisheria ni kifungo cha miaka mitatu au faini Sh10 milioni au vyote kwa pamoja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, Justin Mwinuka ameiomba Serikali kutengeneza Sheria zitakazoratibu upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya ukimwi (ARV).
Mwinuka amesema uwepo wa sheria hiyo utasaidia kuwabana watu wanaofanya biashara kupitia dawa hizo.Amesema wagonjwa wengi hawapati dawa kutokana na kushindwa kumudu gharama.
"Tuna changamoto ya uhaba wa dawa na zinazopatikana zinauzwa sasa wagonjwa wanashindwa kupata fedha za kununua,"
Mwinuka pia ameomba watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kuingizwa kwenye mpango wa kaya maskini Tasaf ili waweze kutatua changamoto ya uhakika wa lishe.

Seneta afutiwa shahada ya sheria kwa kudanganya


Nairobi, Kenya. Chuo Kikuu cha Nairobi kimefuta cheti cha shahada ya sheria ya Seneta wa Meru, Mithika Linturi kwa tuhuma za kutumia stakabadhi bandia kusajiliwa katika chuo hicho.
Uamuzi huo uliafikiwa na Baraza Kuu la chuo hicho baada ya kufanya uchunguzi wa kina kwa ushirikiano na Tume ya Elimu ya Juu kuhusu uhalali wa stakabadhi alizotumia seneta huyo kusomea sheria katika chuo hicho.
Hata hivyo, seneta huyo amewaambia waandishi wa habari kuwa uamuzi wa chuo hicho umechochewa kisiasa na kwamba alitumia vilelezo sahihi kusajiliwa chuoni hapo.
Hii si mara ya kwanza kwa Linturi kupata pigo kuhusu elimu yake kwani wiki moja iliyopita Jaji wa Mahakama ya Juu mjini Meru, Ann Ong’injo aliagiza tume ya uchaguzi pamoja na ofisa aliyesimamia uchaguzi eneo hilo, Samuel Gichichi kuwasilisha nakala za vyeti halali vya elimu vya seneta huyo. Hatua hiyo ilikuja baada ya  Mugambi Imanyara kupinga kortini ushindi wa Linturi kama Seneta wa Meru.
Linturi alikuwa miongoni mwa wanasiasa 106 waliokuwa wanachunguzwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC)kwa madai ya kikiuka kipengele cha maadili katika katiba kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8.

TBA yaanza kusimamia Tanesco iondoe vifaa kwenye jengo lao

Dar es Salaam. Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambaye amepewa kazi ya kubomoa jengo la Tanesco Ubungo, leo Ijumaa ameanza kusimamia shirika hilo litoe madirisha, vitu pamoja na viyoyozi ili waanze kazi ya kubomoa kama ilivyoagizwa na Rais John Magufuli.
TBA imechelewa kuanza ubomoaji wa jengo hilo baada ya Tanesco kuomba waondoe wenyewe madirisha, milango na AC, kazi ambayo amepewa kuifanya mpaka leo Ijumaa jioni kabla ya ubomoaji kuanza.
Akizungumza na gazeti hili leo Ijumaa wakati uondoaji wa madirisha ukiendelea, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA, Mhandisi Elius Mwakalinga amesema kazi waliyonayo ni kubwa lakini wamejipanga kuikamilisha kwa wakati.
"Mpaka sasa hatujapata mchoro wa jengo hili baada ya kujengwa, tunachofanya ni kupima na kuchora ili kuepusha madhara. Unaweza ukakata bomba la gesi hapa ikawa shida tena," amesema Mwakalinga.

Amesema suala kubwa wanalolizingatia kwenye ubomoaji huo ni usalama na kwamba watatoa mafunzo maalumu kwa wafanyakazi kuhusu kujikinga wakati kazi hiyo ikiendelea.
Amebainisha kwamba watabomoa jengo la mbele pekee bila kuathiri lile la nyuma. Hata hivyo, amekiri kwamba jengo litakalobaki litakosa mwonekano mzuri kwa sababu sehemu ya mbele inayobeba sura ya jengo itakuwa imeondolewa.
"Tutatumia teknolojia mbili katika kubomoa jengo hili ambazo ni manual na mechanical. Tungeweza kutumia njia ya kulipua lakini tumeona itaathiri shughuli nyingine za kiuchumi," amesema.
Mwakalinga amesema athari zitakazojitokeza wakati wa ubomoaji ni kelele pamoja na vumbi. Amesema wamefanya tathmini ya jengo na kuangalia athari za mazingira na kujiridhisha kwamba ni chache.
Kuhusu gharama za ubomoaji, Mwakalinga amebainisha kwamba bado hawajakubaliana kuhusu hilo lakini watakaa na Tanesco kuzungumza kuhusu gharama hizo.
"Sheria ya manunuzi ya umma inasema ukishampa mtu kazi bila kutangaza tenda mnapata fursa ya kukaa na kujadili gharama wakati kazi inaendelea. Kwa hiyo, tutakaa na kuzungumzia hilo, hii ni taasisi ya umma na agizo limetoka kwa Rais," amesema Mwakalinga.

Wawili wapatikana wakisafirisha mende kwa ndege China

Uwanja wa ndegeHaki miliki ya pichaKANKAN NEWS
Maafisa wa forodha katika uwanja mmoja wa ndege nchini China wa walipigwa na butwaa walipofungua mkoba wa wanandoa wawili na kugundua kwamba ulikuwa umejaa mende.
Kwa mujibu wa gazeti la Beijing Youth Daily maafisa katika uwanja wa ndege wa Baiyun kusini mwa Guangdong waligundua kulikuwa na viumbe waliokuwa wanatembea walipoweka mikoba ya wawili hao kwenye mtambo wa x-ray wa kukagua mizigo.
"Kulikuwa na mfuko wa plastiki wa rangi nyeupe na ndani kulikuwa na vitu vya rangi nyeusi vilivyokuwa vinatambaa," afisa mmoja wa usalama kwa jina Xu Yuyu aliambia Kankan News.
"Mmoja wa wafanyakazi aliufungua mkoba huo na mende wengi wakatoka na kuanza kutambaa. Karibu alie," alisema Bi Xu.
Walipoulizwa ni kwa nini walikuwa wanawasafirisha mende hao, mwanamume huyo alisema ni wa kutumiwa kama dawa ya kuchua ngozi ya mke wake.
Hakufafanua ni tatizo gani la ngozi linamsumbua mke wake, lakini Bi Yu anasema maafisa walifahamishwa kwamba: "Ni sehemu ya tiba ya jabi. Unawachanganya mende na mafuta fulani na kujipaka kwenye ngozi.
Gazeti la Beijing Youth Daily linasema viumbe walio hai huwa hawaruhusiwi kubebwa kama mizigo ndani ya ndege na kwa hivyo wawili hao walitakiwa kuwaacha na maafisa wa usalama uwanja wa ndege.
Haijabainika mende hao walifanyiwa nini baadaye.
Hii si mara ya kwanza kwa maafisa wa usalama uwanja wa ndege kupata vitu vya kushangaza wakikagua mizigo.
Agosti, maafisa waligundua mwanamume mmoja aliyekuwa anasafirisha mikono miwili ya binadamu.

Museveni: Kujiepusha na pombe kumechangia maisha marefu

Kitabu hicho cha Museveni kilichapishwa mwaka 1997Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amefichua kwamba huwa hanywi pombe na kusema hilo limechangia maisha yake marefu.
Museveni, 73, ameandika kwenye Twitter kwamba uamuzi wake huo umemkinga dhidi ya maradhi na kusema kwamba hana "muda wowote wa magonjwa".
Wabunge nchini Uganda kwa sasa wanajadili mswada ambao unaondoa kikomo kwenye umri wa rais, ambacho kwa sasa ni miaka 75.
Sheria isipofanyiwa marekebisho na kikomo hicho kuondolewa, Bw Museveni hawezi kuruhusiwa kuwania kwa muhula wa sita uchaguzi wa mwaka 2021.