Saturday, March 31

Mrema na kisa cha kufukuzwa uwaziri, kujiondoa CCM na alivyotimkia NCCR

Kwa vijana wa leo taarifa hizi kwao ni ngeni. Kwa waliokuwapo wakiwa na ufahamu na kumbukumbu sahihi ni zilipendwa.
Ilikuwa mwaka 1995 Tanzania ilishuhudia mtikisiko katika nyanja ya siasa, na hatimaye kuendesha Uchaguzi Mkuu wa kwanza ulioshirikisha vyama vingi vya siasa ambao ulikuwa na hamasa za kila aina.
Kabla ya uchaguzi huo, nchi na hasa Chama Cha Mapinduzi kilitikiswa na tukio hili maarufu. Ilikuwa Februari 24 pale ilipotangazwa kuwa Rais Ali Hassan Mwinyi amemtimua Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, Augustino Mrema kwa kushindwa uwajibikaji wa pamoja.
Nini kilimkuta
Hatua hii ilitokana na mvutano katika Serikali ya Mwinyi, kutokana na mjadala ndani ya Bunge kuhusu ripoti ya Kamati, iliyoibua suala la mfanyabiashara wa kigeni, V. G. Chavda aliyekuwa anamiliki mashamba kadhaa ya katani nchini.
Kabla ya hapo, suala hilo lilikuwa likiandikwa sana na vyombo vya habari kwa miezi kadhaa. Kamati ya Bunge ilishauri Chavda akamatwe na kushtakiwa kwa kashfa ya kuvuja mamilioni ya shilingi.
Kamati ilimtuhumu kwa kutafuna Sh916 milioni za Mfuko wa Kubadilisha Madeni, alizokopeshwa na Serikali kwa ajili ya kuendeleza mashamba yake ya katani lakini hakufanya hivyo.
Baadhi ya mawaziri, isipokuwa Mrema, walikuwa wanamwona kama hana hatia. Februari 11, 1995 Serikali ilimtimua nchini. Siku tatu baadaye, Mahakama Kuu iliizuia Serikali kumtimua.
Baada ya hatua hiyo, ndipo Mrema akiwa bungeni, aliacha kukaa kwenye sehemu ya mawaziri, akakaa sehemu ya wabunge wa kawaida, alitumia fursa hiyo kuishutumu Serikali ya Mwinyi kwa kumkumbatia Chavda.
Alisema dhamiri yake ingemsuta kama angekubaliana na jinsi Serikali ilivyokuwa inaendesha suala la Chavda. Baada ya msimamo huo, Rais Mwinyi alitangaza kumtimua uwaziri kwa kushindwa uwajibikaji wa pamoja. Licha ya kwamba awali Mrema alisema asingehama CCM, baadaye alisema alikuwa ananyanyaswa na chama hicho tawala na hivyo akaamua kujivua uanachama. Siku mbili baadaye alijiunga na NCCR-Mageuzi, ambako aliyekuwa mwenyekiti, Mabere Marando alimpisha kwenye nafasi hiyo.
Katika kumbukumbu ya matukio hayo, Mrema anasema kutokana na uadilifu aliokuwa nao isingekuwa rahisi kwake kunyamazia suala la tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mkonge kwa wajanja wachache akiwamo mfanyabiashara mwenye asili ya India, V. G Chavda.
“Nchi ilikuwa inaibiwa, nilisikia uchungu sana. Nilikuwa napambana mwenyewe, haukuwa msukumo wa Serikali, ni Mrema pekee.”
Mrema anasema hata hivyo hilo halikumnyima usingizi, badala yake aliamua kupambana na kuhakikisha mfanyabiashara huyo anafikishwa katika vyombo vya dola.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mrema ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa TLP, anasema licha ya kufanya kazi vizuri akiwa CCM, siku moja aliona ni busara kukihama chama hicho na kutimkia upinzani ili aweze kutimiza kile alichokiamini.
“Siwezi kusema nilinyanyasika CCM, Rais Ali Hassan Mwinyi alikuwa ananipenda sana kutokana na utendaji wangu lakini ukweli ni kwamba watu wanaishi kwa malengo, pale nilipokuwa nimefika nisingefanya zaidi, nikajiuliza mbona nina uwezo zaidi kwa nini nang’ang’ania huku?”
“Nina marafiki wakasema kama CCM hawawezi kukupa nafasi ya kufanya zaidi kwa nini usiondoke, nikaamua kufanya maamuzi,” anasisitiza Mrema.
Uchaguzi Mkuu
Akiwa tayari NCCR-Mageuzi, Mrema aliteuliwa kuwania urais katika Uchaguzi huo wa kwanza wa vyama vingi. Alionekana kuwa na nguvu na mvuto mkubwa kwa wakati huo kutokana na kufanya kazi ya kupambana na uhalifu, rushwa, ubadhirifu na unyanyasaji wanawake alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu.
Hata hivyo, uchaguzi huo ulimalizika kwa kada wa CCM Benjamin Mkapa kuwa Rais wa Awamu ya Tatu kushinda na Mrema kuibuka katika nafasi ya pili.
Katika matokeo hayo, Mkapa alipata kura 4,026, 422 (asilimia 61.82), Mrema kura 1,808, 616 (asilimia 27.77), Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF kura 418, 973, (asilimia 6.43) na John Cheyo wa UDP, kura 258,734 (asilimia 3.97).
Wazo la urais
Mrema ambaye alijipatia umaarufu mkubwa katika uchaguzi huo na kura zake kuendelea kupungua taratibu kila alipogombea, anasema wazo la kugombea urais alilipata kutoka kwa “wapambe na washauri wake wa siasa”.
“Vijana walisema nihamie upinzani ili tusaidie nchi maana mambo yalikuwa hayaendi na wakati huo chama kilichoonyesha kunipenda kilikuwa NCCR-Mageuzi.”
“Mimi sikuwa hata na Sh100, lakini kila kitu walifanya wao ili kuhakikisha ninashinda na kuwa Rais wa Tanzania,” anasisitiza Mrema.
Hata hivyo, Mrema anasema baadaye aligundua kuwa marafiki wake hao hawakuwa na nia njema kwake, bali walitaka kumtumia kujipatia vyeo.
Mrema anasema, pamoja na kushawishiwa na marafiki hao, yeye aliamini kwamba angeweza kufanya mambo vizuri zaidi kama angekuwa Rais, kwani aliona akiwa waziri wa mambo ya ndani na naibu waziri mkuu alishindwa kutekeleza mambo mengi kutokana na kuwa na wakubwa zaidi yake.
Mgogoro NCCR- Mageuzi
Baada ya uchaguzi huo, chama kilichomsimamisha kugombea urais, NCCR-Mageuzi, hakikupata tena utulivu. Anasema baada ya wenzake ndani ya NCCR-Mageuzi kuona ameshindwa kuwavusha katika uchaguzi na kuwapeleka ikulu, walianza maneno wakisema chama si wingi wa wafuasi huku wakitoa mifano ya vyama vingine duniani vyenye wafuasi wachache lakini vimeshinda uchaguzi.
Mrema anasema wenzake waliojenga hoja ya kuwa na chama chenye wafuasi wacache, walianza njama za kutaka kumng’oa uongozi na uanachama hali iliyosababisha NCCR-Mageuzi kuwa na migogoro ya mara kwa mara.
“Kilichotokea ni kuwa viongozi wa NCCR- Mageuzi waliamini mimi nitawavusha kwa kugawana vyeo pindi ningeshinda urais, lakini hilo halikutokea wakaanza kutengeneza visa dhidi yangu,” anasema.
Mrema anasema baada ya kuona hilo haliwezekani maadui zake wakapanga mkutano Tanga kumng’oa. Anasema kwa mujibu wa taarifa alizokuwa “amezinyaka”, maadui zake walipanga kumtoa katikati ya mkutano huo lakini ikabidi apambane ili kuhakikisha hilo halitokei.
“Niliponea chupuchupu, nilikuwa nife siku ile, hali ilikuwa mbaya ukiangalia picha huwezi amini, ilibidi nijifiche chini ya meza lakini hawakufanikisha walichotaka kwa sababu mimi ndiyo nilikuwa na nguvu,” anasema.
Mwaka 1999, Mrema alijiondoa katika chama hicho na kuutelekeza ubunge wa Temeke na kujiunga na TLP, akiwa na kundi kubwa la wanachama.
Hatua hiyo iliporomosha idadi ya wabunge wa NCCR-Mageuzi kutoka 19 iliopata 1995, hadi mmoja mwaka 2000; na kuongeza wabunge wa TLP kutoka sifuri mwaka 1995 hadi watano mwaka 2000.
Kazi anazojivunia
Mrema ambaye ndiye muasisi wa ujenzi wa vituo vidogo vya polisi na sungusungu nchini, anasema kutokana na kuongezeka wa matukio ya uhalifu aliona ni bora shughuli za usalama zikawa karibu na wananchi.
“Ilikuwa creativity (ubunifu) yangu tu, lengo ilikuwa ni kusogeza huduma kwa jamii na kweli ilisaidia sana,” anasisitiza.
Mrema anasema kinachomfurahisha mpaka sasa licha ya jeshi hilo kufanya maboresho kadhaa, bado hawajapoteza lengo la msingi la vituo hivyo na kwamba vinafanya kazi vizuri.
Hata hivyo, anasema kuwa inahitajika msukumo zaidi ili kuboresha huduma katika vituo hivyo lakini pia kuendeleza majina ya waasisi kwa lengo la kuwaenzi.
‘Mfano kuna vituo vilipewa jina langu lakini leo hii ukienda vimefutwa, waliangalie hili ingawa hawapishani sana na wazo langu bado naona wanatumia mbinu zilezile. Kuhusu ulinzi wa sungusungu, Mrema anasema aligundua kuwa hata wakiwa na polisi wengi sana kila kona bila kushirikisha wananchi ni kazi bure.“Wananchi ndiyo wanalinda nchi jeshi la polisi bila ushirikiano na wananchi huwezi fanikiwa hapa ilibidi niwe mbunifu zaidi ndiyo nikaamua kutoa motisha ya Sh50,000 kwa kila kikundi kitakachofanikisha kukamata silaha au mali.”
“Nililazimisha matajiri watoe fedha na kuwalipa polisi ama vikundi hivyo vilivyokuwa vikikamata magendo; nilifanya hivyo ili kuwaongezea ari, kwani mtu anatoa maisha yake kwa sababu ya nchi, ikasababisha polisi na wananchi kuwa na moyo wa kufanya kazi.”
Usuluhishi wa ndoa
Mwenyekiti huyo wa TLP anasema katika uamuzi wake wa kusuluhisha ndoa hakukurupuka ingawa kuna baadhi ya watu walihoji iweje afanye kazi hiyo wakati siyo kiongozi wa dini.
Anasema kwa wakati huo yeye alikuwa waziri wa mambo ya ndani, wizara ambayo inashughulika na masuala ya uhalifu na kwamba wahalifu wote walikuwa chini yake.
“Mwanaume anayempiga mkewe ni sawa na mhalifu mwingine, wanawake walikuwa wanavunjwa meno, wanatelekezwa, wakifanya jambo dogo tu wanapigwa mpaka wanazimia. Ilikuwa kawaida kabisa kumnyanyasa mwanamke na jamii ikaona sawa.”
“Nilitaka kukomesha vitendo hivyo watu wasione ni kawaida. Haiwezekani, huo ni uonevu na ni uhalifu kama mwingine; siku moja nilipata taarifa kuna mama ametelekezwa na watoto na ananyanyasika, nikatoa siku saba kwamba naenda Moshi na kabla sijafika, nataka huyo mwanamme awe ameripoti. Huwezi amini yule aliyemtelekeza alipanda basi akafika kabla mimi sijafika.”
Mrema anasema hakutaka wanawake waonewe maana yeye ana mama na dada zake anaowaheshimu hivyo alitaka kila mwanamke aheshimiwe.
Anasema kutokana na tukio hilo siku moja mwaka jana alikutana na yule mama, ambaye kwa sasa ameshakuwa mzee na kuja kumkumbatia huku machozi yakimdondoka.
“Nikashangaa kwa nini mama mzee analia vile, nilikuwa simjui kwa sababu sikuwahi kumuona kwani nilisikia taarifa yake kutoka kwa mmoja wa wakuu wa mikoa, lakini mama huyo alieleza jinsi uamuzi wake ulivyoirejeshea furaha maishani mwake.
“Mama yule alisema ni mimi ndiyo nilisababisha mumewe arudi nyumbani na kusomesha watoto wake na sasa watoto hao wanafanya shughuli na kupata kipato cha kumlea yeye na baba yao, lakini pia mumewe alirudi na kumuhudumia kama kawaida kwa kumuhofia Mrema.”
Kama kawaida yake, Mrema haachi kutamba, anasema ulifika wakati alikuwa akijulikana kuliko hata baadhi ya mawaziri kwa utendaji wake wa kazi jambo lililompa nguvu na ari ya kufanya kazi zaidi.
“Kuna kitu siwezi kukisahau maishani mwangu, nakumbuka siku moja Rais Mwinyi alikwenda kikazi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na aliporejea aliniita ofisini kwake kisha kunipa salamu zangu kutoka kwa wananchi wa huko.
“Nilishangaa sana, yaani Rais anatembelea eneo na kutatua mambo mengi, lakini inafika mahali anasimamishwa na wananchi kisha wanamwambia aje anisalimie. Hii iliniongezea ari ya kufanya kazi zaidi kwani ilionyesha wazi wananchi wana imani na mimi.”

Maaskofu wakana njama za kumpindua Museveni


Kampala, Uganda. Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Kampala, Dk Cyprian Kizito Lwanga Ijumaa alipuuza ripoti zinazodai kwamba anafanya njama za kumpindua Rais Yoweri Museveni.
Kauli ya Dk Lwanga imekuja baada ya kupigiwa simu na mtu asiyejulikana akidai kwamba serikali imepata habari zinazomhusisha askofu na njama za kuipindua serikali. Mpiga simu huyo alirudia kumwambia askofu kwamba serikali imepandikiza wafichua siri ndani ya mfumo wa kanisa, ambao walimpelekea habari rais kuhusu mpango huo.
Dk Lwanga alisema habari nyingi potofu zinapelekwa kwa rais na wanasiasa, watumishi wa serikali, wafanyabiashara, maofisa wa polisi na mashirika ya upelelezi kama Shirika la Usalama wa Ndani (ISO), Shirika la Ujasusi wa Nje (ESO) na Shirika la Upelelezi Jeshini (CMI).
Alikuwa akizungumza katika mkusanyiko wa waumini kwenye viwanja vya Old Kampala ambako maelfu ya watu walihudhuria Ibada Takatifu ya Ijumaa Kuu baada ya kushiriki kumbukizi ya njia ya msalaba, tukio la kila mwaka la kuigiza safari ya Yesu Kristo hadi anafika eneo aliposulubishwa.
Dk Lwanga alisema mpiga simu asiyejulikana alimtaka awe mwangalifu akisema yanaweza kumkuta ya Janan Luwum, askofu mkuu wa Kanisa la Uganda, ambaye aliuawa na vyombo vya usalama vya serikali, Februari 16, 1977.
Askofu Lwanga, ambaye alionyesha mshtuko kuhusu madai kwamba anataka kuipindua serikali aliwataka watoa siri waache kumlisha uongo Rais.
Lwanga alisema baadhi ya watoa habari walifukuzwa kanisani na sasa wanaonekana kuwa watakatifu mbele ya rais. Ametoa wito kwa Rais Museveni kukutana nao ili kupata ukweli.
Pia alimtaka Rais Museveni aonyeshe ukarimu kwa kuwaeleza viongozi wa Kanisa kwamba amepandikiza vijana wa ISO, ESO au CMI. Lwanga, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Pamoja la Makanisa Uganda (UJCC), aliwaambia watumishi kwamba hawawezi kutumia kanisani kufanya kazi za usalama.

Tusikubali kuwa wachuuzi wa bidhaa za wengine

Wimbo wa Tanzania ya viwanda unazidi kunoga kila kukicha.
Kwa viongozi wetu wakuu wa nchi, watendaji serikalini na wanasiasa kwa jumla, msemo wa viwanda hauwatoki midomoni kila wanapopata fursa katika majukwaa.
Kimsingi, msemo huo hauwezi kuwatoka kwa kuwa wao ndio wadau wa kwanza kama watoa dira kuelekea Tanzania ya viwanda.
Hata hivyo ili tufikie kwenye maono haya ya viongozi wetu kuhusu viwanda, tunahitaji kubadili fikra kutoka kuwa Taifa la walaji na wachuuzi hadi Taifa la waanzisha viwanda wa kutengeneza bidhaa.
Viwanda tunavyovipigia debe kuwa vijengwe kwa mamia na hata kwa maelfu kila kona ya nchi, havitatokana na wawekezaji kutoka nje pekee. Unahitajika mchango na ushiriki madhubuti wa Watanzania wenyewe katika kuanzisha viwanda vya aina mbalimbali. Na viwanda hivi havitaanzishwa kama mtazamo utaendelea kuwa uleule wa utokanao na fikra za kuwa walaji au wachuuzi pekee.
Kwa mfano, kwa nini Watanzania wengi waishie kuuza viatu na nguo? Kwa nini hatufikirii kuanzisha viwanda vya kutengeneza bidhaa hizo lhali tumejaaliwa malighafi tele?
Kwa nini Watanzania wengi waishie kuuza matunda magengeni na sokoni, lakini washindwe kuanzisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vya kusindika matunda hayo wakajihakikishia tija zaidi?
Tuna mfano mzuri wa namna hivi sasa Watanzania kwa makundi wanavyochangamkia fursa kwenye kilimo, lakini wengi utakuta ama wanalima au ni wauzaji wa bidhaa zitokanazo na kilimo.
Tunachokosa ni ule uthubutu wa kuongeza thamani bidhaa hizo na mwishowe kuzipeleka sokoni kama bidhaa tofauti na ilivyokuwa awali.
Tunaamini kama Watanzania tutaukumbatia uthubutu wa kuongeza thamani bidhaa mbalimbali za kilimo na ufugaji, tutapiga hatua kubwa katika mchakato wa uanzishwaji wa aina mbalimbali za viwanda nchini.
Lakini pia tunapopiga chapuo mabadiliko haya ya kimtazamo na kifikra kwa Watanzania, hatuna budi pia kuzipa neno mamlaka husika zinazosimamia sekta ya bidhaa kama Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na mamlaka nyingine za kiserikali.
Uzoefu unaonyesha baadhi ya vyombo hivi vinarudisha nyuma juhudi za Watanzania wanaojaribu kujiongeza. Hii ni kwa sababu ya kuwapo kwa taratibu na masharti yasiyo rafiki.
Kwa mfano, leo ni vigumu kwa mwananchi wa kawaida kuanzisha kiwando kidogo cha kusindika matunda. Anayejaribu atakumbana na mlolongo wa masharti ambayo mwishowe yatamkatisha tamaa.
Bado mamlaka zetu zina mtazamo wa kiwanda kwa kuangalia ukubwa wa ardhi anayomiliki mwekezaji, au jengo linalotumika kuzalisha bidhaa.
Ni muhali kwa mtu kuanzisha kiwanda kidogo ndani ya ua wake, kwa sababu tumejiaminisha kuwa kiwanda hakiwezi kuwa ndani ya nyumba ya mtu.
Lazima tukubali kuwa miaka 57 ya uhuru, Watanzania hatuna budi kuwa watu tunaoweza kujitafutia chakula, kukipika na kujiandalia mezani. Vinginevyo kuendelea kuwa walaji na wachuuzi wa bidhaa zinazotengenezwa na wengine, tukubali kuwa wategemezi wa kudumu wa maendeleo katika dunia hii ya ushindani.

Hizi ndio sababu zinazowanyima wasanii mikataba huku Zari akizikomba


Kwa namna yeyote ile umaarufu ni lazima umfaidishe msanii. Zari alianza kwa kufanya All White Party ambayo ilivunja rekodi ya kujaza watu katika Ukumbi wa Mlimani City mwaka 2014.
Akiwa na Diamond ameshiriki katika mikataba ya matangazo ya Vodacom, Msasani Shopping Mall na Danube.
Hii ndio inapaswa kuwa faida ya umaarufu. Wanamuziki, wanamichezo, waigizaji na wanaopata umaarufu kutokana na namna mbalimbali kwa kiasi kikubwa wanategemea mikataba ya kutangaza bidhaa ili kujiongezea kipato.
Mikataba hii ina fedha nyingi kama msanii atajipanga. Diamond Platnumz ni mmoja kati ya wasanii ghali Afrika Mashariki na Kati. Kampuni ikitaka kufanya kazi naye lazima ijipange. Ameshawahi kuvuta mkwanja mrefu kutoka Coca Cola, Vodacom na Red Gold kwa kupewa ubalozi.
Lakini kupata mkataba wa ubalozi sio kitu rahisi. Kampuni zinajiuliza mara mbilimbili iwapo msanii husika ana thamani inayoendana nayo.
Chris Brown, Oscar Pistorius, Tiger Woods, Cate Moss na wengine waliziingiza katika mgogoro kampuni zilizowapa migogoro baada ya kufanya yanayoenda kinyume na sura ya kampuni.
Hakuna mfanyabiashara anayetaka kujihusisha kwa namna yoyote na mbakaji, ‘mla unga’, mzinzi, mchepukaji, mwizi au mwenye sifa mbaya yoyote.
Wakati mwingine huingia kichwa kichwa bila kufanya utafiti wa kina, lakini utandawazi umerahisisha kazi hiyo, katika viganja vyake anaweza kuzivuta taarifa za msanii.
Kuna msanii wenye sifa hizo?
Watu maarufu hawaishiwi skendo, ziwe za kutengeneza au za kweli. Yapo makosa wanayofanya bila kujua na wanayoyajua.
Kwa kifupi hakuna msanii ‘msafi’ lakini kila mmoja anaweza kujiepusha au kujisafisha.
Ingawa si mfano sahihi kuutumia, lakini kutokana na umaarufu wake inabidi kukumbushia sakata la mwanamasumbwi Manny Pacquiao na kampuni ya Nike ambayo ililazimika kumwamwaga baada ya kutoa kauli zinazokwenda kinyume na mtazamo wa kampuni hiyo.
Pacquiao aliomba radhi hata baada ya kampuni hiyo kusitisha mkataba naye. Miaka miwili baadaye alipewa mkataba mwingine na kampuni hiyo na hapa tunajifunza kwamba kumbe hata kujutia ni dawa.
Kwa mfano unakuta picha chafu za msanii zinavuja mtandaoni au anafanya tukio lolote la aibu, lakini haombi msamaha hata kwa kuonyesha tu kuwa amefedheheka.
Kwa nini Zari anapata mikataba?
Utauliza mbona Zari ana picha chafu mtandaoni. Ni kweli ana video chafu katika mtandao lakini je, alipiga mwenyewe? Je, sio kwamba aliyeipiga alikuwa na lengo la kujipatia fedha kupitia jina la mwanamke huyo? Anajutia? Ndio.
Inapotokea amepiga picha katika vazi la kuogelea au namna yoyote ile lakini ametumia mpiga picha maalumu (proffesional camera) au filter huwa ni kwa lengo la kibiashara.
Hata Beyonce na Jay Z hupiga picha za faragha lakini kwa kutumia wapiga picha maalumu. Hii ni kwa lengo la kuwaonyesha mashabiki maisha yao nje ya kile wanachokifanya. Ni sehemu ya burudani. Kinachoburudisha zaidi kwenye sanaa ni upande wa pili wa maisha ya mastaa.
Solange Knowles ambaye ni mdogo wa Beyonce aliwahi kunaswa akimshambulia kwa mateke shemeji yake Jay Z. Ni tukio lililowavutia wengi duniani. Lilizungumzwa sana hasa kwa kuwa watu waliamini amani imetawala katika familia hiyo.
Famili hiyo ilitoa maelezo kwa mashabiki wao wakikiri kuwa hata wao hupatwa na mikasa kama hiyo. Ni kawaida.
Kupiga picha kihasara hasara, kutojutia pale wasanii wanapofanya makosa ni miongoni mwa mambo yanayowafanya wakose dili hizi.
Kwa mfano mwigizaji Faiza Ally alihoji sababu za kampuni ya Kedz kumpa mkataba Zari. Je, hakustahili?
Alistahili kwa sababu amejua kulitumia vyema jina lake katika raha na shida. Walipokuwa kwenye penzi zito na Diamond walishirikiana kuingiza fedha, halkadhalika katika utengano wao pia.
Pia, alistahiki kwa sababu anaishi kistaa. Anaheshimu jina lake.
Ukitazama ujumbe alioandika Zari akitangaza kuachana na Diamond unamwona mwanamke anayejua thamani ya jina lake mbele ya jamii. Inawezekana ulikuwa uamuzi mgumu kuliko lakini ilibidi ifike mwisho.
Zari anaitwa bingwa wa ‘kujiedit’, basi hata Beyonce anapaswa kuingia katika kundi hili kwa sababu hakubali kupigwa picha ovyo na anazozitoa huwa zimepita katika tanuru la kusafishwa zionekane zinavyoonekana.
Kwa hiyo ni ruksa kujiedit, ni ruksa kuweka picha za faragha zilizopigwa kitaalamu na ni sawa kwa msanii kufanya makosa ili mradi tu ayajutie.
Anayofanya watu maarufu wengi hawafanyi. Wanakurupuka kutafuta kiki na kuharibu brand zao.
Wasanii wafanye nini?
Kwanza watambue kuna fedha nyingi katika ubalozi kama wataamua kuyatumia majina yao vyema.
Hapa na pale wasanii wamewahi kupata ubalozi wa makampuni mbalimbali lakini ndoa hizo huwa hazidumu au huisha vibaya.
Makampuni na mashirika yamejaribu kujiweka na wasanii lakini umekuwa urafiki wa mashaka.
Wasanii wa Nigeria wamejitengenezea maisha katika nyanja hiyo. Hakuna msanii mkubwa asiye na mkataba wa kampuni ambao ni wa mamilioni ya fedha. Wanaendesha magari mazuri, wanamiliki majumba ya kifahari siyo kwa kutegemea sanaa peke yake bali mikataba kama hii ambayo sasa wasanii wanaanza kulialia inachukuliwa na Zari.
Kuteleza sio kuanguka. Wapo wasanii waliowahi kukumbwa na kashfa mbalimbali nchini lakini ukiwaangalia na maisha yao yalivyobadilika unaona kabisa wanajutia yaliyotokea. Muhimu ni kuonyesha kujutia na kuchukua hatua.
Kikubwa kuliko vyote ni kulinda jina na kuchangamkia fursa. Msanii anaweza kuwa na jina kubwa lakini kama hawezi kulitumia au kuzichangamkia fursa atabaki akizisoma tu kwenye magazeti kama hivi.

Serikali iingilie kati kero ya mabasi haya


Ndivyo wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaama tulivyoaminishwa awali kwamba Usafiri wa Mabasi ya Mwendo wa Haraka (Udart) baada ya kuanza ungeondoa adha ya foleni, hivyo kutuwezesha kuwahi kwenye shughuli za maendeleo na nyinginezo za kijamii. Lakini hali imekuwa ni tofauti kwani changamoto nyingi zimeibuka na zinatia doa hata nia ya Serikali ya kutaka kuona wakazi wa jiji hili wanapata usafiri wa uhakika ambao ungeondoa kero hasa ya kutumia muda mwingi kwenye foleni. Nasema hivyo kwa sababu tayari kuna tatizo la abiria kukaa vituoni kwa muda mrefu kutokana na mabasi hayo kuchelewa kufika.
Imekuwa si ajabu kwa msafiri kukaa zaidi ya saa moja kituoni asione basi hata moja likipita.
Kwa sababu kuchelewa kwa mabasi kufika kituoni husababisha msongamano wa watu hali inayohatarisha hata afya zao.
Awali, wasimamizi wa mradi huu waliuaminisha umma kuwa kutokana na kasi ya mabasi hayo, abiria sasa angesubiri kituoni kwa angalau dakika tano, kisha kuanza safari.
Ukiacha hilo tatizo la kuchelewa kwa mabasi, lakini pia kwa sasa hakuna mawasiliano kati ya abiria na wahusika kwenye vituo kama ilivyokuwa awali.
Kulikuwa na matangazo ya mara kwa mara yaliyokuwa yakitolewa pindi tatizo lolote likitokea hata kama ni la kuchelewa kwa mabasi kufika katika kituo husika kwa muda uliopangwa, lakini sasa hivi matangazo hayo hayapo tena.
Lakini naamini kwamba hadi sasa Rais atakuwa amesikia malalamiko au kujionea kupitia vyombo vya habari kuhusu kero wanazopata abiria, hali ambayo imewakatisha tamaa wengine ya kutumia usafiri huo, huku baadhi wakiendelea kuutumia kwa sababu hawana njia nyingine ya kusafiri hasa wakazi wengi wa Mbezi Mwisho.
Kwa hiyo inawezekana kabisa kama usafiri huu ungekuwa wa uhakika watu wengi hata wale wanaotumia usafiri wa magari yao binafsi wangevutiwa kuutumia, hii ingekuwa ni sehemu ya kuingiza faida kwa mradi huo.
Udart kama wakiondoa kero hizo, wanamudu kusafirisha abiria wengi zaidi na mapato yao yanaweza kuongezeka mara dufu ya sasa, lakini kwa sasa wanapata abiria kwa sababu daladala za safari za Muhimbili, Kariakoo na Posta zilizuiwa.
Naamini hata kama hatutangaziwi lakini ni wazi kuna hasara hadi sasa ambayo inaweza kuwa imesabababishwa na uongozi au miundombinu, kwani tumeshuhudia katika msimu wa mvua karakana ikiwa imezungukwa na maji na mabasi kushindwa kutoka.
Ingawa inawezekana pia kuna hasara ambayo pengine haihusiani na Udart, lakini ni hasara kwa Serikali pia kwa sababu watu wakikosa usafiri inamaanisha wanashindwa kuwahi kwenye shughuli zao za maendeleo.
Serikali iingilie kati kuhakikisha mradi huu unatoa huduma bora iliyokusudiwa badala ya kuwa kero na kuwakosesha abiria amani kutokana na usumbufu na kukosa uhakika wa safari hasa wakati wa msimu wa mvua.
Tatizo la kujaa kwa maji eneo la Jangwani, Serikali pia iangalie jinsi ya kulitafutia ufumbuzi haraka, ikiwamo kuwatumia wahandisi washauri ambao watasaidia kuhakikisha ufumbuzi wa tatizo la eneo hilo linapatikana.
Nasema hivyo kwa sababu haya ninayojiuliza mimi, ndiyo wanayojiuliza wananchi huko nje, ni kwanini karakana ya mabasi hayo ilijengwa kwenye eneo lile ambalo ni la mkondo mkubwa wa maji yaendayo baharini?
Je! Wahandisi walioshauri kujengwa kwa karakana ile walikuwa na lengo gani?
Pamoja na yote hayo naona siyo wakati tena wa kuendelea kujiuliza maswali hayo tunachotamani wengi hivi sasa ni kupata huduma nzuri, kwamba Serikali ione umuhimu wa kuboresha miundombinu hiyo

Miguna amlaumu Odinga kwa yanayomkuta Dubai


Nairobi, Kenya. Sinema juu ya hatima ya mwanasheria machachari Dk Miguna Miguna bado inaendelea na kwa mara ya kwanza amemtupia lawama kiongozi wa muungano wa upinzani wa Nasa Raila Odinga kwa kushindwa kumsaidia kurejea Kenya.
Katika taarifa yake aliyoituma kutoka Dubai, Falme za Kiarabu alikosafirishwa kwa nguvu na serikali, Miguna Jumamosi alimshutumu Odinga kwa kufanya karamu na watesi (wa mwanasheria huyo).
“Raila Odinga hawezi na hapaswi kukaa akifurahia Sikukuu ya Pasaka na wadhalimu huku mtu aliyesimamia kiapo chake cha kuwa rais wa watu “anauawa” na walewale waliomwibia ushindi katika uchaguzi uliopita na ambao wameua na kuwatia vilema wafuasi wake,” alisema.
Ingawa waziri mkuu huyo wa zamani hajatoa maoni yoyote hadharani kuhusu kuondolewa nchini kwa Miguna na kusafirishwa hadi Dubai, alijaribu kumwokoa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jumatatu jioni.
Ripoti zinaonyesha Odinga aliondoka kwenye uwanja wa ndege baada ya juhudi za kutafuta ufumbuzi, ikiwemo ya kumpigia simu Rais Uhuru Kenyatta, kugonga ukuta.
Serikali, vyanzo vinasema, ilisisitiza kwamba Miguna lazima asalimishe pasipoti yake ya Canada kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini.
Raila ambaye ni kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na ambaye amekubali kushirikiana kufanya kazi na serikali ya Kenyatta kwa ajili ya uponyaji wa nchi na umoja, alihudhuria kwa muda kusikiliza kesi juu ya uraia wa Miguna katika Mahakama Kuu.
Miguna amewahimiza wafuasi wake kumtaka Raila achukue hatua kwa sababu mateso yote anayopata ni matokeo ya kiapo alichomsimamia.
Pia amewataka wafuasi wake kuandamana na kuishinikiza serikali kuheshimu amri za mahakama na imruhusu kurejea nyumbani.
“Kusanyeni makundi makubwa ya watu waandamane, pigeni kelele na mdai kwamba haki zangu za kuzaliwa, kikatiba na kisheria ziheshimiwe na zizingatiwe,” alisema.
“Waheshimu amri za mahakama; nirejeshewe pasipoti yangu ya Kenya au nipewe mpya; ulinzi na usalama wangu uwepo.”
"Naomba kuokolewa kutoka Dubai, niruhusiwe kuondoka kwa usalama na kuingia kwenye nchi nilikozaliwa ya Kenya bila kukawia,” alisema.
"Mzaliwa wa Kenya hawezi kuzuiwa kuingia kwenye nchi aliyozaliwa. Sijawahi kuukana uraia wangu. Mahakama zimethibitisha na zimetambua uraia wangu."
Dk Miguna pia aliomba apatiwe huduma ya matibabu haraka akidai kemikali aliyodungwa wakati anasafirishwa inazidi kuathiri afya yake.
“Ni lazima nimwone dokta au tabibu na nifanyiwe vipimo vya kujua aina ya kemikali,” alisema.

Papa asikitika vijana kurithi dunia iliyoharibika


Rome, Italia. Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amewaambia waumini siku ya Ibada ya Ijumaa Kuu kwamba “anaona aibu” kwamba kizazi kipya cha watu kitarithi dunia “iliyoharibiwa kwa migawanyiko na vita”.
Papa Francis alisema hayo mjini hapa baada ya kukamilisha njia ya msalaba chini ya ulinzi mkali mbele ya waumini wapatao 20,000 ambao walibeba mishumaa kuzunguka jengo la kihistoria la Colossium. Alisema dunia imemezwa na “ubinafsi wakati watoto, wagonjwa na wakongwe wakiwa wamesahaulika”.
Njia ya msalaba inakumbusha mateso aliyoyapitia Yesu Kristo kabla ya kusulubiwa. Usalama ulikuwa umeimarishwa vikali katika mji mkuu huo wa Italia, kufuatia wiki kadhaa za kamata kamata dhidi ya washukiwa wa ugaidi.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia, Marco Manniti alitoa tahadhari mapema wiki hii juu ya uwezekano mkubwa wa shambulio la kigaidi dhidi ya nchi yake.
Maafisa usalama wapatao 10,000 wanashika doria kuhakikisha usalama mjini Roma, hususan katika siku hizi za Pasaka.

Kuwapinga maaskofu wa Kanisa Katoliki, KKKT ni kutoipenda nchi

Mhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la
Mhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya,  Everisto Chengula akihubiri katika Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kitaifa katika Kanisa la Bikira Maria wa Fatma,  Mwanjelwa Mbeya. Picha na Godfrey Kahango 
Mtanzania mwenye kuipenda nchi yake, jambo la kwanza ataomba utaifa uheshimiwe. Utaifa una pande mbili; mosi ni amani, utulivu na mshikamano. Pili ni ustawi wa hali za kimaisha. Katika kushughulikia yote hayo lazima kuwe na usawa. Hivyo basi, ulinzi namba moja wa utaifa ni kuwapo kwa usawa miongoni mwa wananchi.
Usawa haupatikani kwa kadirio lenye kugawiwa na mtu mmoja au kikundi cha watu. Usawa huratibiwa kwa mujibu wa Katiba. Maana Katiba ndiyo mfumo na utaratibu wa kimaisha ambao wananchi wanakuwa wamekubaliana kuufuata. Hivyo basi, kuendesha nchi kwa ridhaa ya makundi yote ni lazima Katiba ifuatwe.
Kuvunja Katiba kuna tafsiri mbili; ya kwanza ni kuharibu utaratibu wa kimaisha ambao nchi iliazimia kuuishi. Pili ni kuwagawa watu. Kwa maana hiyo, jaribio lolote la kuvunja Katiba linabeba sura ya kuharibu utaifa. Kwani utaifa hauwezi kuonekana kwenye jamii iliyogawanywa, ama kikabila au kidini, hata kwa matabaka ya kiuchumi na itikadi za kisiasa.
Tanzania siyo nchi ya chama kimoja cha siasa. Kila chama kilichosajiliwa kisheria kina haki ya kuendesha shughuli zake za kisiasa ilimradi kisivunje Katiba na sheria za nchi. Kuzuia vyama kufanya shughuli zao halali za kisiasa ni kuvunja Katiba. Chama kimoja kupata upendeleo kuliko vingine ni kuwagawa wananchi. Usawa ndiyo ngao ya utaifa.
Kila Mtanzania anao uhuru wa kujiunga na chama chochote cha siasa au kuishi bila chama. Uhuru huo siyo zawadi bali ni haki yake ya kikatiba. Na kwa utashi wake huo, anayo haki ya kuhudumiwa na Serikali Kuu, vilevile Serikali za Mitaa bila kubaguliwa. Kwa kuzungumzia eneo hili, hatuwagusi wafanyakazi wa umma ambao masharti yao ya ajira yanawabana kujihusisha na vyama vya siasa.
Tanzania ni ya maskini na matajiri. Asiwepo kiongozi wa kujenga huruma na maskini au awe upande wa matajiri na kuwakandamiza maskini. Ubaguzi wa matabaka ya kiuchumi ni hatari mno. Wachina walipogawanywa kwa matabaka, ilitokea vita kati ya chama cha mabwanyenye, Kuomintang, dhidi ya Communist cha makabwela. Mpaka mwaka 1949, jumla ya watu milioni nane walikuwa wamepoteza maisha na wengine kupoteza viungo.
Tafakuri ya maaskofu
Februari mwaka huu, wakati wa kuelekea kuanza kwa kipindi cha siku 40 za toba ya Kwaresma, Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), lilitoa waraka kuhusu hali ya kisiasa na kijamii ilivyo nchini na kugusia, vilevile kuonya yale mambo ambayo viongozi hao wa Kanisa Katoliki waliona yanahitaji masahihisho au utatuzi.
Machi 15, mwaka huu, maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), walikutana na kuandika waraka kwa waumini wao na Watanzania kwa jumla. Waraka huo waliuita Ujumbe wa Pasaka wa Baraza la Maaskofu wa KKKT. Kilichomo humo ni maonyo juu ya mambo ambayo viongozi hao wa kiroho wameona hayapo sawa.
Ukipitia hoja zote, kile ambacho kimezungumzwa na maaskofu wa Kanisa Katoliki na KKKT kinalenga kujenga utaifa. Unaweza kuiona shabaha ya viongozi hao kwamba wanalilia usawa. Anayehubiri usawa ndiye mwenye kustawisha upendo. Hakuna jamii inayoweza kupendana ikiwa watu wake hawaoni usawa miongoni mwao. Jamii iliyogawanywa kamwe haitapendana.
Maaskofu wanataka Katiba iheshimiwe, maana hiyo ndiyo ilani kuu ya maisha ya watu kwenye nchi yao. Yeyote mwenye kutetea Katiba ndiye mlinzi wa utaifa. Anayetetea au kulinda utaifa huyo anataka usawa, kwa hiyo ndiye mwenye kuipiga jamii yenye upendo. Sasa basi, unawezaje kuwapinga maaskofu? Ni rahisi kumtafsiri kila anayewapinga maaskofu kuwa haipendi Tanzania. Mpingaji huyo akiwa Mtanzania, maana yake si Mtanzania mzuri.
Haivutii kuona watu wanapaza sauti kuwasema maaskofu, wengine wanawashambulia binafsi. Unaweza kujiuliza; kweli maaskofu wamefanya makosa kutoa waraka wenye kuagiza Katiba iheshimiwe? Maaskofu wanatenda kosa kusema kwamba usawa na haki katika ufanyaji wa shughuli za kisiasa vinapokosewa kutasababisha machafuko? Yaani maaskofu waone mambo hayapo sawa kisha wao wanyamaze tu!
Viongozi wa dini wanapaswa kuhubiri upendo, maana maandiko matakatifu yanasema jamii yenye watu wasiopendana haiwezi kuuona ufalme wa Mungu. Popote panapokosekana upendo basi na chuki huchipua. Maaskofu wanaona jinsi ambavyo chuki inainyemelea nchi. Watu wanataka maaskofu wakae kimya, wasiikemee chuki. Kuwapinga maaskofu kunahitaji moyo wa kikatili dhidi ya Tanzania.
Waraka wa TEC
Waraka wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC) ulisainiwa na maaskofu 36. Ulielezea mazingira ya utawala bora kuwa ni mabaya Tanzania. Uligusia jinsi ambavyo shughuli za kisiasa zinavyopigwa marufuku, wakati ni shughuli halali kikatiba na kwa sheria za nchi. Maaskofu hao walieleza kwamba makongamano, maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama haipaswi kuzuiwa.
Kabla ya kuelezea hali ya kisiasa nchini ambayo kwa tafsiri ya maaskofu ni mbaya, walitoa neno lenye kuuliza, je, kila mmoja ni mlinzi wa mwenzake? Neno ambalo asili yake ni Biblia, pale Cain ambaye ni mtoto wa Adam, alipoulizwa kwa sauti ya Mungu alipo mdogo wake Abel. Cain alijibu: “Mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
Hivyo, TEC katika waraka wao walisisitiza kuwa na dhamira njema kwa kila mtu kujiona ni mlinzi wa mwenzake. Jamii isome alama za nyakati ili kuwezesha maisha bora yenye maelewano. Yote ambayo yamesemwa na TEC, uponyaji wake upo kwenye dhamira njema. Katiba ya nchi iheshimiwe. Shughuli halali zisiharamishwe kwa sababu ya matakwa binafsi. Kama walivyosema maaskofu, haya mambo ya watu kuona wananyimwa haki zao, husababisha matokeo mabaya, hasa wahusika wanapoona ni lazima wazipate na kuanza kuzidai kwa njia zenye shari.
TEC walisema kuhusu kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari na baadhi ya vyombo kufungiwa, kwamba kunapunguza haki ya kimsingi ya Watanzania kupata habari katika wigo mpana. Walisema pia kwamba Mahakama na Bunge ambayo ni mihimili huru ya dola, inayopaswa kujisimamia kutekeleza majukumu yake ya kikatiba, haipo huru kwa sasa.
Kimsingi waraka wa TEC uligusa maeneo mengi, lakini yaliyohusu siasa ni hayo. Ukishayapitia jiulize; kuna ubaya gani wamefanya? Ni kweli kwamba shughuli za siasa zimepigwa marufuku. Kuna wabunge wananyimwa mpaka fursa ya kukutana na wapiga kura wao ili kujadili maendeleo na uwakilishi wao kwa jumla.
Hayo yapo wazi na inafahamika kuzuia hayo ni kinyume na Katiba, vilevile sheria za nchi. Je, maaskofu wakae kimya?
Waraka wa KKKT
Waraka wa maaskofu wa KKKT, ukiwa na kichwa Ujumbe wa Pasaka, katika tafakuri ya nchi, vilevile waraka huo umepewa utambulisho wa “Taifa Letu Amani Yetu” na umesainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo.
Yaliyoguswa ni masuala yenye kuhusu hali za kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa na masuala mengine muhimu, vilevile waligusia kuhusu kupatikana kwa Katiba Mpya.
Kwa uungwana kabisa, yapo maeneo maaskofu wa KKKT wameipongeza Serikali. Walisema zipo jitihada zinazofanywa na Serikali kuboresha maisha ya wananchi. Maaskofu hao wamekiri kwamba wameshuhudia nia njema kuhusu uvunaji na umiliki wa rasilimali za nchi kwa manufaa ya taifa zima. Vilevile waliipa heko Serikali kwa jitihada zake za kukusanya kodi ili kujijengea uwezo wa kuihudumia nchi.
Hata hivyo, maaskofu wa KKKT waliitaka Serikali kutambua kwamba sekta binafsi na mashirika ya dini ni wadau wa maendeleo na si washindani wa Serikali katika kuchangia maendeleo ya Taifa.
Kimsingi maaskofu wana hoja za msingi. Hata mashehe nao wanapaswa kusema wanayoona hayaendi sawa.
Shehe Mussa Kundecha alisema pia jinsi shughuli za kisiasa zinavyoonekana sasa kuwa kama kuna kutoridhika kuhusu uwepo wa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Kuutetea utaifa siyo kuchanganya dini na siasa, bali ni kupigania usawa. Anayewapinga wanaotetea utaifa huyo haitakii mema Tanzania.
Wakataka jitihada za makusudi na za mara kwa mara zifanyike kuondoa dhana ya ushindani kati ya Serikali na wadau hao ili kuimarisha uhusiano mwema kati ya Serikali na sekta binafsi.

Simanzi yatawala kifo cha Mtanzania aliyeuawa Uingereza


Arusha. Simanzi imetawala nyumbani kwa Mtanzania, anayeishi Uingereza, Leila Mtumwa aliyeuawa usiku wa kuamkia leo.
Leila anadaiwa kuchomwa kisu na mumewe nchini Uingereza.
Akizungumza na MCL Digital, leo Machi 31, mama wa mtoto huyo, Hidaya Mtumwa amesema amepokea kwa mshtuko habari za kifo cha mtoto wake.
"Juzi usiku nilikuwa nilizungumza naye tulicheka, nilikuwa namwambia kuna mwandishi wa habari anataka kunihoji mambo ya Pepe Kalle aliyenitungia wimbo, sasa baadaye akaniambia anawahi taksi atanipigia," amesema.
Amesema hata hivyo baada ya kupata taarifa ya msiba sasa anaomba kusaidiwa mwili wa mtoto wake kurejeshwa nchini.
Akiwa nchini Tanzania miaka ya 1990, Pepe Kalle alitunga kibao cha Hidaya kilichopata umaarufu kwa wapenzi wa muziki kote Tanzania. 
Akiwa miongoni mwa wanamuziki kutoka DR Congo, Pepe Kalle amewahi kufanya ziara nchini mara kadhaa na kundi lake la Empire Bakuba lililokuwa na wanamuziki wengine mahiri kina Papy Tax, Bileku Mpasi na wengineo wakiwamo wacheza shoo wawili wafupi, Emoro na Jolie Bebe.  Pepe Kalle, alifarki dunia mwaka 1998. 

Kuvunjika penzi la Diamond na Zari kwamtokea puani Kifesi


Sakata la kuvunjika kwa penzi la mwanamuziki Diamond Platnumz na Zari The Bosslady halijapoa na sasa limemuondoa mpiga picha wake, Andrew Kisula maarufu Kifesi ambaye ametangaza kuacha kufanya kazi  naye baada ya kuwapo tetesi kuwa anaweza kufukuzwa.
Tetesi za uwezekano wa kufukuzwa kwa mpiga picha huyo zilianza kuzagaa jana asubuhi  zikihusishwa na kitendo cha kumuandikia waraka mzito bosi wake akimsihi asiachane na Zari kwa kuwa ni mwanamke mwenye akili.
Kupitia mtandao wa Instagram, Kifesi aliandika: Blaza angu Chibu, hivi kweli ndio umekubali huyu mwanamke wa baraka uliopewa na Mungu akakupa na kafamilia kazuri aende. Duh haya bana.. Akili ni nywele kila mtu ana zake.”
Ilielezwa kuwa kauli hiyo haikuufurahisha uongozi wa WCB ambao Diamond anauongoza na kupanga ‘kumshughulikia’ mapema wiki ijayo.

Kuthibitisha kuwa kuondoka kwa Kifesi kunahusiana na tukio la Zari, dada wa mwanamuziki Diamond, Esmah aliandika katika mtandao huo akifafanua kuwa kilichomwondoa ni kuingilia maisha ya bosi wake.
Esmah alikuwa miongoni mwa watu waliotoa maoni katika tamko la mpiga picha huyo la kutangaza kujiondoa katika kazi hiyo akisema aache kusema uongo.
“Acha uongo Kifesi sema umefukuzwa, kuacha kazi kufuatilia maisha ya bosi wako. Yametushinda sie utayaweza mtu baki,” alihoji Esmah ambaye ni mfanyabiashara wa vitenge.

Profesa Kitila amwandikia barua Mkuu wa KKKT


Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo amemwandikia barua Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Askofu Frederick Shoo akitoa maoni yake binafsi kwa kanisa hilo kuhusu maudhui ya waraka wa maaskofu wa kanisa hilo uliotolewa hivi karibuni.
Waraka wa maaskofu 27 wa KKKT ulitoka hivi karibuni na ulitarajiwa kusomwa katika makanisa yote ya kilutheri Machi 25, 2018.
Katika waraka huo maaskofu walizungumzia  Katiba mpya, uchumi, siasa na jamii.
“Katika kutoa maoni yangu kuhusu Waraka huo, ninalenga mambo makubwa mawili ambayo ni pongezi kwenu, na pili ni mtazamo wangu juu ya baadhi ya masuala yaliyomo katika Waraka huo,” amesema Kitila katika barua yake aliyoisaini Machi 29 mwaka huu.
Pamoja na kuwapongeza maaskofu hao, Kitila ameandika katika barua yake kuwa maudhui yaliyowekwa katika waraka wa maaskofu hao, hayaakisi hadhi na wajibu wa msingi wa kanisa.
“Kama ambavyo mmekuwa mkitufundisha siku zote, na vile tusomavyo katika Biblia Takatifu, ninafahamu kuwa kazi za msingi za kanisa ni zile ambazo Bwana wetu Yesu Kristo alizifanya alipokuwa duniani,”amesema.
Kitila ambaye ameandika barua hiyo kama muumini wa KKKT, amesema anakubaliana na mengi maaskofu waliyogusia katika Waraka huo akiamini yamefundisha na kuponya roho za waumini kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, alichambua hoja katika maeneo matano zilizoibuliwa na maaskofu hao na kusema ni sahihi lakini akatahadharisha kuwa ni muhimu kwa kanisa kujiepusha na kuonekana lipo upande fulani katika mijadala ya kitaifa inayogusia jamii.
“Kwa kufanya hivyo, mtaepusha migawanyiko isiyo ya lazima kwa waumini ndani ya kanisa na wananchi kwa ujumla.” Amesema.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa kanisa kupima kwa umakini mkubwa uzito wa kila neno kabla ya kutoa kauli katika umma.
“Ni hatari kwa Kanisa kutoa kauli inayosababisha maumivu na mifarakano badala ya kuponya.”

Twaweza: Raia Tanzania wanasema hawako huru kukosoa kauli za utawala

Wananchi wangependa kuwa huru kukosoa watawala iwapo hawataridhika na maamuzi ya SerikaliHaki miliki ya pichaTWAWEZA
Image captionWananchi wangependa kuwa huru kukosoa watawala iwapo hawataridhika na maamuzi ya Serikali
Idadi kubwa ya wananchi (60%), nchini Tanzania wanasema hawako huru kukosoa kauli zinazotolewa na Rais wakati asilimia 54 wanasema hivyo kuhusu kauli zinazotolewa na Makamu wa Rais na asilimia 51 Waziri Mkuu.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la utafiti lisilo la serikali, Twaweza.
Wananchi wanajisikia huru zaidi kuwakosoa wabunge wao kuliko wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.
Kwa mujibu wa shirika la Twaweza, hali hii inaweza kuwa ni kwa sababu wananchi wanawachagua wabunge kuwa wawakilishi wao na hivyo wanaona kuwa mbunge anajukumu la kusikiliza mahitaji na vipaumbele vyao na kuvifanyia kazi ipasavyo.
Wananchi wanaunga mkono kwa kiasi kikubwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari. Wananchi nane kati ya kumi (81%) wanaona ukosoaji wa viongozi wa taifa kama jambo muhimu kwani itawasaidia kujirekebisha na si kuwashushia hadhi.
Asilimia 62 ya wananchi wanasema ni bora zaidi kwa magazeti yanayochapisha taarifa zisizo sahihi kuomba radhi na kuchapisha marekebisho kuliko kufungiwa ama kutozwa faini na serikali. Na wananchi wengine (54%) wanasema serikali isiruhusiwe kuyaadhibu magazeti kabla ya kupata kibali kutoka mahakamani.
Utafiti wa TwawezaHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionUtafiti wa Twaweza

Uhuru wa kujieleza

Utafiti huu umebaini kuwa wananchi wanaunga mkono kwa kiasi kikubwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari. Wananchi nane kati ya kumi (81%) wanaona ukosoaji wa viongozi wa taifa kama jambo muhimu kwani itawasaidia kujirekebisha na si kuwashushia hadhi.

Wananchi wengi hawafahamu sheria mpya zinazosimamia masuala ya taarifa

Sheria mbalimbali zinazohusiana na masuala ya taarifa zimetungwa na Bunge katika miaka ya hivi karibuni, ikiwemo Sheria ya Takwimu, Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa na Sheria ya Huduma za habari. Hata hivyo, wananchi wachache wanazifahamu sheria hizo.

'Misingi kufuatwa'

Akiwa kwenye uzinduzi wa utafiti huo jijini Dar es salaam, msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas alisema kuwa 'kumkosoa Rais maana yake ametenda jambo ambalo hukubaliani nalo.Lakini kuna misingi ya kufuatwa . Uwe na utafiti, hoja zinzaofaa na lugha unayotumia.'
Hivi karibuni kumekuwa na ukosoaji dhidi ya kinachodaiwa kuwa kuminywa kwa uhuru wa kujieleza,
Tukio linalokumbukwa ni la Mkalimani aliyedaiwa kutafsiri maneno yasiyo sahihi kutoka kwa mmoja wa watalii aliyetembelea hifadhi ya Ngorongoro, ambaye baadae na
mkalimani huyo anayeitwa Simon Sirikwa aliwekwa chini ya ulinzi kutokana kile kilichokuwa kinatafsiriwa kudaiwa kuwa kilikuwa kinapotosha uhalisia wa maneno yaliyokuwa yakizungumzwa na mtalii aliyekuwa akisifia kile alichokiona baada ya kutembelea eneo hilo la utalii.