Saturday, March 31

Papa asikitika vijana kurithi dunia iliyoharibika


Rome, Italia. Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amewaambia waumini siku ya Ibada ya Ijumaa Kuu kwamba “anaona aibu” kwamba kizazi kipya cha watu kitarithi dunia “iliyoharibiwa kwa migawanyiko na vita”.
Papa Francis alisema hayo mjini hapa baada ya kukamilisha njia ya msalaba chini ya ulinzi mkali mbele ya waumini wapatao 20,000 ambao walibeba mishumaa kuzunguka jengo la kihistoria la Colossium. Alisema dunia imemezwa na “ubinafsi wakati watoto, wagonjwa na wakongwe wakiwa wamesahaulika”.
Njia ya msalaba inakumbusha mateso aliyoyapitia Yesu Kristo kabla ya kusulubiwa. Usalama ulikuwa umeimarishwa vikali katika mji mkuu huo wa Italia, kufuatia wiki kadhaa za kamata kamata dhidi ya washukiwa wa ugaidi.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia, Marco Manniti alitoa tahadhari mapema wiki hii juu ya uwezekano mkubwa wa shambulio la kigaidi dhidi ya nchi yake.
Maafisa usalama wapatao 10,000 wanashika doria kuhakikisha usalama mjini Roma, hususan katika siku hizi za Pasaka.

No comments:

Post a Comment