Nairobi, Kenya. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu atakuwa miongoni mwa wakuu wa nchi 20 wanaotarajiwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rais Uhuru Kenyatta Jumanne ijayo ambayo imetangazwa na Gazeti la Serikali kuwa ya mapumziko.
Kwa mujibu wa gazeti la The Times Of Israel, Netanyahu atawasili kwa sherehe hizo mapema Jumanne na ataondoka saa chache baadaye baada ya sherehe hizo.
Hata hivyo, msemaji wa serikali Eric Kiraithe jana alishindwa kutaja orodha ya wakuu wa nchi waliothibitisha kuhudhuria na akaishia kuahidi kutoa ufafanuzi zaidi Ijumaa.
Julai 2016, Netanyahu alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Israeli aliyeko madarakani kufanya ziara nchini Kenya. Katika ziara ile Kenyatta aliahidi kuisaidia Israel kupata hadhi ya kuwa mwangalizi katika Umoja wa Afrika (AU).