Thursday, January 10

Tucta yataka haki ya migomo,maandamano katika katiba

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limependekeza kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, migomo na maandamano viwe haki ya msingi ya raia.
Wakati Tucta likitoa pendekezo hilo, Chama cha UPDP kimeungana na CCM kutaka mgombea binafsi aruhusiwe, huku NCCR Mageuzi kikiungana na Chadema kutaka umri wa urais ushushwe na apunguziwe madaraka.
Tucta, mbali na kutaka maandamano na migomo viruhusiwe, limependekeza hayo yafanyike kisheria baada ya kufutwa sheria kandamizi zinazowabana wafanyakazi wanaodai haki na masilahi yao.
Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya alisema jana baada ya kuwasilisha maoni ya shirikisho hilo kuwa Katiba Mpya lazima iwe mkombozi wa wafanyakazi.
Alisema wanataka Katiba itamke kwamba kila mfanyakazi atakuwa na haki ya kugoma na kufanya maandamano wakati wanapoona haki zao hazizingatiwi.
“Sheria zilizopo zinazoruhusu maandamano na migomo ni kandamizi. Tunataka Katiba Mpya izifute na ziwepo sheria ambazo si kandamaizi ili kuwapa nafasi wafanyakazi kudai haki zao kwa maandamano bila vikwazo.”
Mgaya alisema Katiba Mpya iwe na kifungu kitakachoeleza uhusiano kazini ili kuhakikisha wafanyakazi wananufaika na kazi wanazofanya.
“Tunataka Katiba Mpya itamke kila mfanyakazi atakuwa na haki ya kushiriki na kushirikishwa kupitia vyombo mbalimbali vya mashauriano na vinavyohusika katika uamuzi wa kazi. Hiyo itakuwa njia sahihi ya kutoa nafasi kwa wafanyakazi kueleza mambo ambayo wanaona hawanufaiki nayo katika sehemu zao za kazi,” alisema.
Pia alisema: “Tunataka Katiba Mpya itamke kwamba ndani ya Bunge kutakuwa na uwakilishi wa wafanyakazi ili kutatua matatizo ya wafanyakazi.”
UPDP na mgombea binafsi
Mkurungezi wa Sheria na Katiba wa UPDP, Juma Nassoro alisema pamoja na mambo mengine, wamependekeza mgombea binafsi aruhusiwe katika nafasi zote za uongozi isipokuwa urais.
Alisema mfumo wa sasa unaolazimisha mgombea kutokana na chama cha siasa ni kuwanyima wananchi wasio na vyama kushiriki katika uongozi wa nchi kwa kutumia haki yao ya kuchagua na kuchaguliwa.
Alisema mantiki ya kutaka mgombea wa urais atokane na vyama vya siasa ni kutoa nafasi kwa wananchi kufanya tathmini za sera za vyama husika... “Yawezekana mtu akajitokeza kuwa mgombea urais na akawa na sera inayopingana na Katiba na maadili ya nchi. Ili kuepuka hilo Katiba Mpya isiruhusu mgombea binafsi kwa nafasi ya urais.”
Pia alisema wamependekeza muundo wa Serikali uwe wa Serikali tatu; Tanganyika, Zanzibar na Muungano... “Katika uongozi kwenye Serikali hizo kutakuwa na marais watatu kutoka kila Serikali huku Serikali za Tanganyika na Zanzibar zikiwa na mawaziri viongozi na ya Muungano ikiwa na waziri mkuu atakayeteuliwa na Rais wa Muungano na kuthibitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.”
NCCR na umri wa Rais
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia kwa upande wake alisema wametaka Rais asirundikiwe madaraka makubwa na asiruhusiwe kuteua viongozi wa mihimili mingine ya dola.
“Umri wa mtu kupiga kura uwe miaka 18, ila tunataka mtu mwenye miaka 21 ndiye awe na uwezo wa Kikatiba kugombea ubunge na udiwani pamoja na uwakilishi Zanzibar,” alisema Mbatia na kuongeza: “Katika urais tumependekeza kuwa umri wa kugombea nafasi hiyo uwe miaka 35 badala ya 41 ya sasa.”
Pia NCCR-Mageuzi kimependekeza muundo wa Serikali tatu; Tanganyika, Zanzibar na Serikali Kuu Shirikisho yenye mamlaka ya kidola, ambayo itakuwa chini ya mkataba unaoeleweka kimataifa.
Chama hicho pia kimependekeza Katiba kukitambua Kiswahili kuwa lugha ya taifa na itumike kufundishia katika ngazi zote za elimu.
Kuhusu mgombea binafsi alisema chama hicho kimependekeza Katiba iruhusu kwa kuwa kila mwananchi anayo haki ya kuchagua na kuchaguliwa hata kama si mfuasi wa chama chochote cha siasa.
“Haki ya kuchagua na kuchaguliwa ni ya kila mtu na inalenga mtu mmojammoja na si chama cha siasa, taasisi au kikundi cha watu,” alisema Mbatia.
Kuhusu muundo wa Serikali alisema wamependekeza kwamba Baraza la Mawaziri lisiwe kubwa kama ilivyo sasa na Katiba iweke idadi ya wizara na majina yake na zisizidi 15.
Jukwaa la Katiba na jinsia
Jukwaa la Katiba Tanzania limetaka Katiba Mpya iguse maeneo yote muhimu ikiwa ni pamoja na wanawake, wazee na watu wenye ulemavu ili kuhakikisha haki zao zinatambulika kikatiba.
Pia linataka itamke raia wa nchi hii ni nani na haki anazopaswa kupewa ili kumtofautisha na wageni wanaoingia.Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba alisema Katiba ya sasa haimtofautishi raia wa Tanzania na wa kigeni kwani haielezi ni nani na haionyeshi haki anazopaswa kupewa.
Kuhusu elimu, Kibamba alisema Katiba Mpya itamke kwamba elimu ya ngazi ya msingi iwe hadi kidato cha nne ili kuongeza uelewa wa wanafunzi na itamke pia kwamba elimu hiyo itakuwa ni haki ya msingi kwa kila raia.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Aidan Mhando na Daniel Mwingira

TAWALA ZA MAJIMBO NA SERIKALI ZA MITAA

1. Nchi ya Tanganyika itagawanywa katika maeneo kumi ya kikanda yatakayojulikana kama Majimbo kama ifuatavyo:

(a) Jimbo la Nyanza Magharibi ambalo litaundwa na mikoa ya sasa ya Kagera, Geita na Shinyanga;

(b) Jimbo la Nyanza Mashariki litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Mara, Mwanza na Simiyu;

(c) Jimbo la Ziwa Tanganyika litakalojumuisha mikoa ya sasa ya Kigoma, Katavi na Rukwa;

(d) Jimbo la Kati litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Tabora, Singida, Dodoma na Iringa;

(e) Jimbo la Kaskazini litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara;

(f) Jimbo la Pwani ya Kaskazini litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Tanga, Wilaya za Bagamoyo, Chalinze, Kibaha, Kisarawe na Mkuranga katika Mkoa wa sasa wa Pwani na Wilaya za Gairo, Kilosa, Mvomero, Morogoro na Kilombero katika Mkoa wa sasa wa Morogoro;

(g) Jimbo la Mji Mkuu wa Dar es Salaam;

(h) Jimbo la Pwani ya Kusini litakaloundwa na mikoa ya sasa Lindi, Mtwara na Wilaya za Rufiji na Mafia katika Mkoa wa sasa wa Pwani, na Wilaya ya Ulanga katika Mkoa wa sasa wa Morogoro;

(i) Jimbo la Nyanda za Juu Kusini litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma;

2. Majimbo yataongozwa na Gavana atakayechaguliwa moja kwa moja na wananchi katika Jimbo husika.

3. Miji, manispaa na jiji ndani ya majimbo itaongozwa na Meya atakayechaguliwa moja kwa moja na Wananchi katika Mji husika;