Sunday, September 3

DKT. HARRISON MWAKYEMBE AMPONGEZA BALOZI WA CHINA

Na. Benedict Liwenga-WHUSM.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa pongezi za dhati kwa Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youking kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka katika kudumisha ushirikiano baina ya Tanzania na China hususani katika nyanja za masuala ya habari, utamaduni, sanaa na michezo.

Pongezi hizo amezitoa hivi karibuni wakati wa hafla ya kumuaga balozi huyo iliyowakutanisha baadhi ya Viongozi wa Chama cha Ushirikiano wa Rafiki wa Tanzania na China wakiwemo Waandishi wa habari.

Moja ya mambo makubwa muhimu yaliyofanyika chini wakati wa kipindi cha Balozi Lu Youking ni tukio la utiaji saini mwezi Machi mwaka huu ambapo Serikali ya Tanzania na China zilitiliana saini Mkataba wa Ushirikiano wa Kiutamaduni wa Miaka mitatu ambao utawapa fursa vijana 200 kutoka Tanzania kila mmoja kwenda China kwa ajili ya kupata mafunzo katika nyanja mbalimbali za habari, sanaa na utamaduni.

“Balozi Lu Youking umetuachia zawadi kubwa sana sisi Wanahabari wa Tanzania, sasa hivi mimi na wenzangiu Wizarani tunakamilisha utaratibu wa utekelezaji wa Mkataba huu ili tuanze kuutekeleza mapema iwezekenavyo”, alisema Dkt. Mwakyembe.

Aliongeza kuwa, Balozi Lu Youking hivi karibuni ameshirikiana na Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Balozi Mbelwa Kairuki katika kuhakikisha kwamba Waandishi wa habari 10 kutoka Tanzania wanaondoka mwezi ujao kuelekea nchini China kwa ajili ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya habari.

Kwa upande wake Balozi Lu Youking alisema kwamba, urafiki kati ya Tanzania na China umekuwa wa afya na imara zaidi ya nusu karne akikumbushia kuwa, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake aliwahi kusema kwamba, Tanzania ina marafiki wengi, lakini China ni zaidi ndiyo maana Rais wa China, Mhe. Xi Jinping alichagua Tanzania kuwa kituo chake cha kwanza Afrika wakati wa ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuwa mkuu wa nchi.

Aliongeza kuwa, kila mwaka zaidi ya Wanafunzi 700 kutoka Tanzania huenda China kwa ajili ya masomo zaidi na kutokana na hilo, matokeo ya ushirikiano wa China na Tanzania umekuwa wa manufaa katika maeneo yote ya uchumi wa Tanzania na maendeleo ya jamii na kwa kila maisha ya Mtanzania.

“Uhusiano wa China na Tanzania umetoa mwongozo kwa Ushirikiano wa Kusini na Kusini yaani South-South Cooperation, hivyo kutokana na maendeleo ya ushirikiano huu katika uwezo wa uzalishaji kati ya China na Tanzania na mpango wa Ukanda mmoja njia moja, tunaamini ushirikiano huu utakuwa na matunda zaidi”, alisema Balozi Youking.

Urafiki baina ya Tanzania na China ulianzishwa na Waasisi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha China, Bw. Mao Tse-Tung (Mao Zedong) ambapo uhusiano baina wa nchi hizi mbili kwa sasa umekuwa kwa kasi na kuleta maendeleo baina ya pande zote mbili.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe(kulia) akimpongeza Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youking wakati alipowasili kwa ajili ya kushiriki hafla ya kumuaga balozi huyo iliyofanyika katika mgahawa wa Great Wall Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akiongea na wageni waalikwa pamoja na Viongozi mbalimbali waliohudhulia hafla ya kumuaga balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youking iliyofanyika katika mgahawa wa Great Wall Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youking akiongea na wageni waalikwa pamoja na Viongozi mbalimbali waliohudhulia hafla ya kuagwa kwake iliyofanyika katika mgahawa wa Great Wall Jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Chama cha Ushirikiano wa Urafiki baina ya Tanzania na China, Dkt. Salim Ahmed Salim (kushoto) akimpongeza Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youking mara baada ya kumalizika kwa hafla ya kumuaga balozi huyo iliyofanyika katika mgahawa wa Great Wall Jijini Dar es Salaam.(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)

RAIS DKT. MAGUFULI PAMOJA NA MKEWE MAMA JANETH MAGUFULI WASALI KATIKA KANISA LA WAADVENTISTA WASABATO LA MAGOMENI JIJI DAR ES SALAAM


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amepiga magoti pamoja na  mkewe Mama Janeth Magufuli wakati wakiombewa sala  na Maaskofu wa Kanisa hilo la Waadventista Wasabato, Sala iliyokuwa ikiongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania Marc Walwa Malekana(wa kwanza kushoto)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mkewe Mama Janeth Magufuli wakati wakikabidhi mifuko 400 ya Saruji itakayotumika katika ujenzi wa Kanisa hilo la Wasabato la Magomeni Mwembechai jijini Dar es Salaam.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru Mama Navana Cable aliyeambatana na mtoto  wake Rebecca Cable ambao familia yao imeahidi kumalizia ujenzi wa Kanisa hilo la Waadventista la Wasabato mara baada ya Rais Dkt. Magufuli kuendesha Harambee ya Papo kwa papo Kanisani hapo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza Mhariri Mtendaji waMagazeti ya Serikali (TSN) Dkt. Jim Yonaz mara baada ya kuahidi kuchangia katika kanisa hilo.

Waziri Mstaafu katika awamu iliyopita Steven Wasira naye akichangia katika Harambee hiyo Kanisani hapo.


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru Ndugu Dkt. Edward Hosea mara baada ya kuchangia katika ujenzi wa kanisa hilo la Wasabato lililopo Magomeni.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimshika mkono mtoto ambaye alikua anamsalimia wakati akitoka ibadani katika kanisa hilo la Magomeni.
Waumini mbalimbali wa Kanisa hilo wakiwa ibadani kama wanavyoonekana pichani. PICHA NA IKULU

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amepiga magoti na mkewe Mama Janeth Magufuli pamoja na Waumini wengine wa Kanisa la Waadventista Wasabato Ushirika wa Magomeni Mwembechai katika Ibada ya Jumamosi kanisani hapo  jijini Dar es Salaam.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na   mkewe Mama Janeth Magufuli wakiimba nyimbo katika ibada hiyo ya Jumamosi katika Kanisa la Waadventista Wasabato Ushirika wa Magomeni Mwembechai jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na   mkewe Mama Janeth Magufuli wakisikiliza neno katika Ibada hiyo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisoma neno pamoja na mkewe Mama Janeth Magufuli kanisani hapo wakati wa Ibada ya jumamosi.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na waumini wa Kanisa la Waadventista la Wasabato Ushirika wa Magomeni Mwembechai  kabla ya kuendesha Harambee ya Ujenzi wa kanisa hilo ambapo zaidi ya Sh. 25milioni ziliahidiwa kukusanywa.

WAZIRI MKUU MAJALIWA ATEMBELEA MRADI WA KIWANDA CHA SUKARI, GEREZA MBIGIRI MKOANI MOROGORO


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa(Mb) akisalimiana na Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya kufufua Kiwanda cha Sukari na Kilimo cha miwa katika Gereza la Mbigiri Mkoani Morogoro Septemba 2, 2017. Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Mifuko ya Jamii ya PPF na NSSF limeingia ubia katika mradi huo wa uchumi wa viwanda chini ya Kampuni ya MKULAZI.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa(Mb) akiangalia mbegu za miwa kabla ya kuzipanda katika eneo la Shamba la miwa alipowasili Gereza Mbigiri katika ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya kufufua Kiwanda cha Sukari na Kilimo cha miwa katika Gereza la Mbigiri Mkoani Morogoro Septemba 2, 2017. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama.
Shamba la miwa katika mradi wa Kiwanda cha Sukari na Kilimo cha miwa - MKULAZI katika eneo la Gereza la Mbigiri Mkoani Morogoro likiwa limestawi kama inavyoonekana katika picha.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akitoa hotuba fupi kwa  Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza Mkoani Morogoro, Watendaji wa Kampuni ya MKULAZI pamoja na Wananchi wanaoishi jirani na Gereza Mbigiri katika ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya kufufua Kiwanda cha Sukari na Kilimo cha miwa katika Gereza la Mbigiri Mkoani Morogoro Septemba 2, 2017.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akitoa maelezo mafupi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim(hayupo pichani) namna Jeshi hilo lilivyojipanga katika kuhakikisha kuwa ufufuaji wa Kiwanda cha Sukari na Kilimo cha miwa katika Gereza la Mbigiri Mkoani Morogoro unakamilika kama ilivyopangwa ambapo matarijio ni kuwa Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha sukari tani 50,000 kwa mwaka.
Maafisa Waandamizi wa PPF na NSSF wakifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa (hayupo pichani).
Baadhi ya Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wa Mkoani Morogoro wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya kufufua Kiwanda cha Sukari na Kilimo cha miwa katika Gereza la Mbigiri Mkoani Morogoro Septemba 2, 2017.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof. Godius Kyaharara akitoa maelezo mafupi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya kufufua Kiwanda cha Sukari na Kilimo cha miwa katika Gereza la Mbigiri Mkoani Morogoro Septemba 2, 2017.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(kushoto) akiteta jambo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage(kulia) mara baada ya ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ambapo amekagua maandalizi ya kufufua Kiwanda cha Sukari na Kilimo cha miwa katika Gereza la Mbigiri Mkoani Morogoro Septemba 2, 2017.
Mkurugenzi Mkuu wa PPF William Erio akitoa neno la shukurani mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maandalizi ya kufufua Kiwanda cha Sukari na Kilimo cha miwa katika Gereza la Mbigiri Mkoani Morogoro Septemba 2, 2017.
Ujenzi wa maghala ya kuhifadhia sukari katika mradi wa Kiwanda cha Sukari cha MKULAZI kilichopo Gereza Mbigiri ukiendelea katika hatua mbalimbali kama inavyoonekana katika picha.
Wataalam wazalendo ambao wanajitolea katika ujenzi wa mradi wa Kiwanda cha Sukari – MKULAZI Mbigiri wakitambulishwa mbele ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa(hayupo pichani. (Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

FUATILIENI MAENDELEO YA VIWANDA KATIKA MAENEO YETU-MAJALIWA

                                       
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji katika mikoa yote nchini kuhakikisha wanafuatilia maendeleo ya viwanda mbalimbali katika maeneo yao.

Amesema mpango wa Serikali wa kujenga uchumi wa viwanda unalenga kuinua uchumi wa Taifa kutoka wa chini kwenda wa kati, hivyo ni muhimu kuvifuatilia.Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumamosi, Septemba 2, 2017) alipozungumza na watendaji na wananchi wa mkoa wa Morogoro alipofanya ziara katika kiwanda cha Moproco.

Alisema licha ya kukuza uchumi wa Taifa, viwanda vitasaidia katika kutatua tatizo la ukosefu wa ajira hususani kwa vijana kwani vinauwezo wa kuajiri watu wengi.“Viwanda hivi vinatupa uhakika wa ajira nchini kwa sababu vinauwezo wa kuajiri watu wengi na wa kada mbalimbali, hivyo ni muhimu tukafuatilia utendaji wake.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa mbali na kutoa ajira nyingi, pia viwanda vitawezesha wakulima kupata soko la uhakika la mazao yao na kukifanya kilimo kuwa na tija.Alisema kwa muda mrefu sekta ya viwanda nchini ilikuwa haifanyi vizuri jambo ambalo lilisababisha kuongezeka kwa tatizo la ajira na mazao yalikosa soko.

Hata hivyo Waziri Mkuu alitoa wito kwa wafanyakazi walioajiriwa katika viwanda mbalimbali kuwa waaminifu ili kuviwezesha viwanda hivyo kuendelea na uzalishaji.Pia aliwataka wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ili kuviwezesha viwanda kuwa na uhakika wa upatikanaji wa malighafi ndani ya chini.

Awali Meneja Mkuu wa kiwanda cha Moproco, Bw. Arif Abood aliiomba Serikali kuongeza kodi kwa mafuta yanayotoka nje ya nchi ili kulinda viwanda vya ndani.Alisema uingizwaji wa mafuta kutoka nje ya nchi kwa kiasi kukubwa ulichangia kufungwa kwa viwanda vya ndani vya mafuta kutokana na kukosa soko.

Katika ziara hiyo Waziri Mkuu aliambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mheshimiwa Charles Mwijage pamoja na maofisa wengine wa Serikali.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L.P 980,
40480-DODOMA 
JUMAPILI, SEPTEMBA 3, 2017.


Waziri Mkuu. Kassim Majaliwa akishiriki kupanda mbegu za miwa katika Shamba la Gereza Mbigiri kwa ajili ya maandalizi ya kufufua Kiwanda cha Sukari na Kilimo cha miwa katika Gereza la Mbigiri Mkoani Morogoro jana Septemba 2, 2017.Picha na ofisi ya Waziri Mkuu

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA TAMASHA LA WASANII WANAWAKE WA MKOA WA KUSINI UNGUJA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan jana alifungua Tamasha la Wasanii Wanawake wa mkoa wa Kusini Unguja.

Tamasha hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa Coco Blue ,Jambiani na kuhudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali pamoja na wananchi wa mkoa wa Kusini Unguja.

Makamu wa Rais aliwashukuru Waandaaji wa Tamasha hilo ambao wamesaidia kuwaleta wanawake wa mkoa wa Kusini pamoja.Makamu wa Rais amewapongeza wanawake wa mkoa wa Kusini kwa kuwa wa kwanza kutekeleza wazo lililowazwa na kuonyesha utamaduni wa Kusini.

Mhe. Samia alisema Utamaduni wa zamani hauna budi kuendelezwa ili vijana wa sasa wajue wapi tumetoka, wapi tulipo na wapi tunaelekea.Akivitaja baadhi ya vitu alivyoviona kwenye ufunguzi huo kama Manda, Mabobwe ,Vipopoo, ngoma ya Msanja ambavyo kwa pamoja vina lengo la kuleta yale mazuri ya zamani ambayo yametutoka.

Alisema Vijana wengi hawajui Kiwe-jiwe la kusagia chakula (Blender za Bibi zetu) wao wanajua Blender, hivyo ni vyema Tamasha hili likaja na vitu vingi mwakani waelewe hata maji tuliyatunza kwenye Mtungi ambao wao kwa sasa wanayajua Majokofu.

Hivyo aliwasihi Wanawake wa kusini kufufua tamaduni zetu na kuzidumisha, alisema sema yeye anatoka Kizimkazi ambapo ngoma maarufu ni Shomoo na Dandaro .Makamu wa Rais alisema kuwa Utamaduni utasaidia kuwafunza watoto wetu uzalendo,mazingira, nidhamu ya maisha kwani utamaduni unajumuisha kila kitu kuanzia chakula, mavazi, vifaa vilivyotumika,filamu, ngoma na burudani mbali mbali.

Mhe. Samia aliwapongeza sana wanawake wa mkoa wa Kusini kwa kutoka kwenye utamaduni wa kukaa tu na badala yake kufanya shughuli zinazowaingizia kipato. “Nimefurahishwa kuona wakina Mama sasa hivi wanatoka wana Vikundi vya Kulima tumeonyeshwa wanalima Tungulee, wanalima Karoti,wanalima michicha hii yote ni utamaduni kwamba tumetoka kwenye utamaduni wa kukaa tu na kusubiri bwana haji lakini sasa tunatoka tunajituma na sisi tunapata mapato yetu tunaendelea na maisha yetu”

Makamu wa Rais alisema ni wajibu wa kila mama kutunza na kufundisha watoto wetu Tamaduni zetu, “Tunautamaduni ambao hautakiwi kuonyeshwa mbele za watu na ule nao tufundishe watoto wetu, tusiuache , tunakuwa wa kisasa mno , tunajifanya wa kisasa mno kiasi ambacho mambo mengine tunayaacha lakini ambao kwa sie tuliofanyiwa huko nyuma unajua faida yake na watoto wetu wanaokosa kufanyiwa sasa hivi tunaona hasara yake”

Mwisho Makamu wa Rais alitoa rai kwa waandaaji wa Tamasha hilo kuhakikisha linafanyika kila mwaka na kujumuisha tamaduni mbali mbali zenye lengo la kujenga na kuimarisha mshikamano pamoja na kudumisha upendo na amani katika jamii, aliwashukuru wadhamini waliosaidia kufanikisha Tamasha hilo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. SAMIA SULUHU HASSAN akiangalia kofia iliofumwa kwa mikono wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Wasanii Wanawake wa mkoa wa Kusini Unguja uliofanyika jana kwenye ukumbi wa Coco Blue Jambiani.
  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Wasanii Wanawake wa Mkoa wa Kusini Unguja liliofanyika jana kwenye ukumbi wa Coco Blue, Jambiani.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Wasanii Wanawake wa Mkoa wa Kusini Unguja liliofanyika kwenye ukumbi wa Coco Blue, Jambiani.

WAKIMBIZI WA BURUNDI KUANZA KUREJEA KWAO SEPTEMBA 7 MWAKA HUU

Wakimbizi wa Burundi waliokimbia machafuko nchini kwao wataanza kurejea nchini kwao ifikapo Septemba 7 hadi Desemba 31, mwaka huu mara baada ya pande tatu ikiwemo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Burundi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), kutiliana saini Mpango wa Kuwarejesha wakimbizi baada ya mkutano uliochukua takribani siku tatu katika kuandaa mpango huo.

Wakitiliana saini makubaliano hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki,Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu ya Uzalendo kutoka nchini Burundi, Pascal Barandagiye na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania, Chansa Kapaya, mwishoni mwa wiki wote walikubaliana kutekeleza vipengele vilivyopo katika makubaliano hayo yakiwa na lengo la kuwarudisha wakimbizi walioomba kurejea nchini Burundi, baada ya hali ya Amani na utulivu kurejea.

Akizungumza baada ya kutiliana saini makubaliano hayo Waziri Mwigulu, alisema umefika wakati wa wakimbizi wa Burundi kurudi nchini kwao kuungana na familia zao na ndugu waliobaki ili kusaidia kujenga uchumi wa nchi yao baada ya kuwa katika machafuko yaliyosababisha kukimbia nchi yao kwa muda mrefu.

“Mimi kama mwanauchumi ninaona madai yao ya kurudi nchini Burundi kujishughulisha na shughuli za kilimo ni maamuzi mazuri huku pia wakisisitiza kurejea kwa Amani na Utulivu nchini kwao kuwa ni sababu ya msingi ya kufikia kuomba kurejea, sisi kama Serikali tutahakikisha zoezi hilo la urejeaji nchini kwao linaenda salama tukishirikiana na Serikali ya Burundi kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchini Burundi,” alisema Mwigulu.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu ya Uzalendo kutoka nchini Burundi, Pascal Barandagiye, amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania na Watanzania wanaoishi kwenye maeneo yaliyotumika kuwahifadhi wakimbizi kwa ukarimu wao walioonyesha muda wote kwa raia kutoka nchini Burundi huku akisisitiza kurejea kwa hali ya Amani na utulivu ambao hapo mwanzoni ilitoweka.

“Nawaomba wananchi wetu warejee nchini ili tuweze kuijenga Burundi yetu ambayo hivi sasa kuna Amani na utulivu, pia naishukuru Serikali ya Tanzania na Watanzania ambao wamekua wakiwaonyesha ukarimu wakimbizi kutoka Burundi na kuwapa hifadhi nchini hapa,”alisema Barandagiye.

Kwa upande wao Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) kupitia kwa Mwakilishi wao nchini,Chansa Kapaya, wameahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha wakimbizi wa Burundi 6,800 walioomba kurejea nchini kwao wanasahiliwa na kurejeshwa kwao katika hali ya utu na usalama huku shirika hilo likizishukuru Serikali za Tanzania na Burundi kwa msaada wao walioupata katika kushughulikia masuala ya wakimbizi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba,akibadilishana nyaraka na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania,Chansa Kapaya(kulia) zenye makubaliano juu ya Mpango wa Kuwarejesha Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa mkoani Kigoma.Makubaliano hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki, Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere,jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu ya Uzalendo kutoka nchini Burundi, Pascal Barandagiye, akibadilishana nyaraka na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania, Chansa Kapaya (kulia) zenye makubaliano juu ya Mpango wa Kuwarejesha Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa mkoani Kigoma.Katikati ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.Makubaliano hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki, Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Wajumbe kutoka Serikali ya Burundi wakiongozwa na Balozi wa Burundi nchini Tanzania,Gervais Abayeho wakiwa katika Mkutano wamakubaliano juu ya Mpango wa Kuwarejesha Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa mkoani Kigoma.Makubaliano hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki,Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Wajumbe kutoka Mashirika mbalimbali ya kimataifa wakiwa katika Mkutano wa makubaliano juu ya Mpango wa Kuwarejesha Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa mkoani Kigoma.Makubaliano hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki, Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

WANAFUNZI WA TUSIIME WASAIDIA WASIOJIWEZA

WANAFUNZI wa shule ya Msingi ya Tusiime ya Tabata jijini Dar es Salaam, wametoa msaada wa vyakula na vitu mbalimbali kwa watu wasiojiweza wanaolelewa katika kituo cha Mama Teresa cha Mburahati, Dar es Salaam.

 Msaada huo ambao umetokana na michango ya wanafunzi wa shule hiyo ni pamoja na unga, mchele, mafuta ya kupikia na vinywaji vya aina mbalimbali.Akizungumza punde tu baada ya kukabidhi msaada huo, mmoja wa wanafunzi wa Tusiime, Agnes Heke  amesema walianza kuchangishana wenyewe kwa wenyewe muda mrefu lengo ikiwa ni kusaidia watu wanaolelewa kwenye kituo hicho.

Alisema dhamira ya kusaidia wenzao wa kituo hicho inatokana na mafundisho ya upendo wanayofundishwa wakiwa shuleni Tusiime.“Tumekuwa tukifundishwa kuwajali wenye shida na kwa kweli tulianza kuchangishana muda na leo hii tumeona hiki tulichopata tuwape wenzetu, huu ni mwanzo maana kadri tutakavyokuwa tunapata tutarudi kuwasaidia,” alisema Agnes.

Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Mkuu wa Taaluma wa shule hiyo, Maxon Wilson amesema  msaada uliotolewa na wanafunzi hao ni sehemu tu na wameahidi kuendelea na moyo huo wa upendo kwa wenzao.Alisema msaada uliotolewa na wanafunzi hao unadhihirisha kuwa mafunzo ya maadili na kuwapenda wenzao wanayoyafundisha yamewaingia vema na wanayazingatia kwa dhati.

Mmoja wa wazee wanaolelewa na kituo hicho, Elizabeth Daudi, aliishukuru shule ya Tusiime kwa namna ambavyo imewafundisha wanafunzi wake kuwa na upendo kiasi cha kuamua kuchanga kwa ajili yao.“Msaada huu ni ishara kwanza mafunzo ya upendo mnayoyapata shuleni yamefanyakazi, hatukutarajia kupata msaada kama huu tunawashukuru na Mungu awazidishie,” alisema kwa niaba ya wenzake.

Alishukuru msaada huo wa wanafunzi wa Tusiime kwani umekuja wakati muafaka kwani huwa wanaishiwa na vyakula mara kwa mara.“hatuna maneno ya kutosha kuelezea furaha yetu , tunaomba watu wengine waige mfano wa Tusiime, waone watu  wanaolelewa hapa ni wajamii nzima,” alisema.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi  Tusiime, ya Tabata Dar es Salaam, Agnes Heke na Ibrahim Shaban wakikabidhi vyakula mbalimbali kwa Bi. Elizabethi Daudi asiyeona ambaye ni mmoja wa watu wasiojiweza wanaolelewa kwenye kituo cha Mama Teresa Mburahati jijini Dar es Salaam.Msaada huo umetokana na michango ya wanafunzi wenyewe.
 Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya  Tusiime ya Tabata wakiwa wamebeba vyakula mbalimbali na sabuni kwa ajili ya kutoa msaada kwenye kituo cha watu wasiojiweza wanaolelewa kwenye kituo cha Mama Teresa Mburahati jijini Dar es Salaam. Msaada huo umetokana na michango ya wanafunzi wenyewe.