Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali haitafuta mbio za Mwenge wa Uhuru kwa kuwa ni alama ya Uhuru na Utaifa wa nchi na kwamba unatoa mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo, kuwaunganisha Watanzania na kuimarisha Muungano.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 14 Oktoba, 2017 katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, kumbukumbu ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Wiki ya Vijana zilizofanyika kitaifa katika uwanja wa Amaan uliopo Mjini Magharibi, Zanzibar.
Pamoja na kauli hiyo Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitaendeleza mbio za mwenge wa uhuru na kuutetea Muungano kwa nguvu zote. “Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu inasema Shiriki Kukuza Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo ya Nchi yetu. Nimefarijika zaidi kusikia kuwa katika Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu jumla ya viwanda 148 vimezinduliwa, viwanda hivyo vimejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 468.46 na vinatarajiwa kuzalishaji ajira 13,370.
Hii ndio sababu tumekuwa tukihimiza ujenzi wa viwanda na hizi ni baadhi ya faida za Mwenge” amesema Mhe. Rais Magufuli. Kuhusu Kumbukumbu ya Mwl. Nyerere, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuwa wazalendo, kuthamini utu na usawa wa binadamu na muhimu zaidi kujitathimini ni kwa kiasi gani wanajiepusha na vitendo vinavyoathiri ustawi wa nchi na watu wake kama vile wizi, rushwa, ubinafsi na kukosa uzalendo.
Ametolea mfano wa Mwl. Nyerere ambaye mwanzoni mwa uongozi wake alipochaguliwa kuwa Rais wa Tanzania aliamua kupunguza mshahara wake na kukataa kuongeza mishahara ya wafanyakazi wengine Serikalini kwa maelezo kuwa hawezi kuongeza mishahara ya wachache wakati wananchi wengi ni masikini na hawapati huduma muhimu za afya, elimu na maji.
“Ninaposema hivyo simaanishi kuwa mishahara isiongezwe. La hasha. Ninachosema ni kwamba kabla ya kudai nyongeza ya mishahara ni lazima kwanza kufahamu uwezo wa Serikali, lakini pia tutambue kuwa kuna Watanzania wenzetu wengi tu wanaohitaji kuboreshewa huduma.
Hata hivyo baada ya kukamilisha zoezi la uhakiki wa watumishi hewa na vyeti feki, Serikali imewapandisha vyeo na kuwarekebishia mishahara watumishi 59,967 ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 159.33 zimetengwa kwenye bajeti ya mwaka huu na mishahara mipya itaanza kulipwa kuanzia mwaka huu. Na kwa upande wa Zanzibar kima cha chini cha mshahara kimeongezwa kutoka Shilingi 150,000/- hadi kufikia Shilingi 300,000/-” Amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu vijana Mhe. Rais Magufuli amewataka kuendelea kujielimisha katika Nyanja mbalimbali, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza na kuwakabidhi vyeti wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa walioongozwa na Amour Hamad Amour kwa kukimbiza mwenge huo kwa siku 195 katika mikoa yote 31 na Halmashauri 195, ambapo jumla ya miradi 1,512 yenye thamani ya jumla ya Shilingi Trilioni 1.1 imepitiwa. Na pia ameahidi kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika kusababisha dosari katika miradi 19 ambayo viongozi wa mwenge wamebaini.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Makama wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Seif Ali Idd, Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Janeth Magufuli, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein na viongozi wengine wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akipokea Mwenge wa uhuru wakati wa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa na Wiki ya Vijana katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar leo Oktoba 14, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akipokea ripoti ya miradi mbalimbali kutoka kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru wakati wa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa na Wiki ya Vijana katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar leo Oktoba 14, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwnyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein wakiteta jambo wakati wa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa na Wiki ya Vijana katika uwanja wa Amaan mjini Zanzib
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akihutubia wakati wa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa na Wiki ya Vijana katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar leo Oktoba 14, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akisalimiana na mwakilishi wa familia ya Mwalimu, Mhe. Makongoro Nyerere wakati akiwasili kwenye sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa na Wiki ya Vijana katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar leo Oktoba 14, 2017.
Vijana shupavu sita waliokimbiza mwenye wa Uhuru mwaka 2017.