Kwa mujibu wa barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Ameir A. Ameir kwenda kwa Mwenyekiti wa ZATI, Seif Masoud Miskiry, mkutano huo hautaweza kufanyika kwa vile suala hilo halikuwa miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa na kikao cha Baraza la Mawaziri la SMZ.
Mkutano huo uliOkuwa ufanyike chini ya Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Maudline Castico, umezua malalamiko kutoka kwa wawekezaji na wafanyakazi wa sekta binafsi ambao hadi sasa hawajui hatima yao.
Mkutano huo ungetoa fursa kwake kushughulikia masuala yaliyowasilishwa na ZATI serikalini katika kikao cha siku mbili Julai 26-27 kutafuta ushauri na mwongozo wa kumwezesha ilikuweza kupata ufumbuzi masuala hayo.
“Ningependa kukufahamisha kwamba suala letu halikuwepo katika ajenda za kikao cha Baraza la Mawaziri na hivyo halikujadiliwa katika tarehe ile. Kutokana na hali hiyo, Mheshimiwa waziri anaahirisha mkutano hadi itakapotangazwa tena baadaye,” alieleza Ameir katika barua yake
Kutokana na uamuzi huo Ameir alisema kwamba anasikitishwa kufutwa kwa mkutano huo, anatarajia utapangwa tena wakati mwafaka.
Mapema wiki hii MTANZANIA ilimtafuta Waziri Castico ili kupata kauli ya Serikali ambapo mwandishi alipopiga simu yake na kujitambulisha kwa waziri huyo kuwa anahitaji kupata ufafanuzi wa suala hilo alikata simu bila kujibu lolote.
Waziri Castico ambaye alipigiwa kwa simu yake ya kiganjani namba 0652…348 ambapo baada ya kuulizwa swali kuhusu madai hayo ya wawekezaji hao alikataa simu na baada ya kutumiwa ujumbe kwa njia ya simu aliizima kabisa.
Pamoja na hali hiyo MTANZANIA ilimtumia ujumbe mfupi kwa njia simu uliosomeka “Habari mheshimiwa Waziri ….ni mwandishi wa gazeti la MTANZANIA nahitaji kupata kauli ya Serikali juu ya malalamiko yaliyotolewa na Jumuiya ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI),” ulisema ujumbe huo waliotumiwa Waziri Castico ambao ulionesha ameusoma na lakini na alipogiwa simu iliita na kuizima hadi tunakwenda mitamboni.
Kutokana na hali hiyo gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Abood, ambapo naye alisema kuwa kwa sasa hana mamlaka ya kuzungumzia suala hilo zaidi ya Waziri husika.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI), Seif Masoud Miskry, alisema wanashangazwa kupewa lawama za wao kukwamisha kutolipwa mishahara mipya kwani wao waliwasiliana na Waziri mwenye dhamana (Castico) na kuwaambia waendelee kulipa mishahara ya zamani.
Alisema licha ya Waziri Castico kutangaza kima kipya cha mhshara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi hakuna sehemu yoyote wao kama wadau waliposhirikishwa zaidi ya uamuzi binafsiwa kiongozi huyo.
Naye Mlezi wa ZATI ambaye pia ni Mwakilishi wa Tunguu, Simai Mohamed Said (CCM), alimwomba Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein aingilie kati sakata hilo kuokoa sekta ya utalii nchini.
Kutokana na hali hiyo alisema wageni hao Zanzibar hushindana na nchi kama Thailand, Tunisia, Morocco, Spain, Visiwa vya Ugiriki kama Crete, Mexico, Cuba, St. Lucia pamoja visiwa vyengine.
Alisema wanaouza nafasi za hoteli kwa Zanzibar kwa nchi za Ulaya tayari tayari wanaanza kuona Zanzibar ni bei ghali hasa ikiwa mishahara itapanda kupindukia na wao itawafanya wapandishe bei ina maana katika mapumziko ya mwaka 2018 wataiondoa Zanzibar katika mabango ya kuitangaza hasa kwenye mitandao ya kununua likizo hizo.
Mabadiliko hayo yamefanyika kwa mujibu chini ya kifungu cha 97 (1) cha sheria ya Ajira nambari 11 ya mwaka 2005 ambapo kima cha chini kwa wafanyakazi kimeongezeka kutoka Sh 145,000 hadi 180,000 huku kwa wenye mikataba ikingezwa kutoka kiwango cha sasa cha Sh 145,000 hadi 300,000.
Huku kwa vibarua wa kutwa wenye ujuzi, kimeongezwa kutoka Sh 10,000 hadi 30,000 kwa siku na kwa vibarua wa kutwa wasio na ujuzi, kimeongezwa kutoka Sh 7000 na kufikia 25,000.