Saturday, October 7

Siku za Tillerson zinahesabika


Washington, Marekani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson, mkurugenzi wa zamani wa kampuni ya mafuta ambaye aliteuliwa na Rais Donald Trump kusimamia masuala ya kimataifa anatajwa na maofisa wa utawala kuwa anaelekea kuondoka.
Sababu za Tillerson kutajwa kuwa siku zake katika nafasi hiyo zinahesabika zimechochewa wiki hii na ripoti mpya kali baina ya watu hao, ambapo inadaiwa Tillerson alihoji uwezo wa kufikiri wa Trump alipozungumza na maofisa wengine.
Kisa hicho kimemkera rais huyo na alichukizwa kuona kwamba mtu aliyedhaniwa ni mdogo kicheo alikuwa akimtusi kwa marafiki zake. Habari zinasema hali hiyo imezidisha taswira ya Tillerson kama mshirika asiyekubali sera za Trump kuhusu ajenda ya sera ya mambo ya nje, maeneo ambayo watu wawili hao wameshindwa kukubaliana hadharani.
Vyanzo zaidi ya dazani kutoka ndani ya utawala na nyanja za kidiplomasia vinasema kuwa uhusiano kati ya Tillerson na Trump uko chini sana. Watu wawili hao wameshindwa kukuza uhusiano wa karibu ambao Trump anaufurahia kutoka kwa mawaziri wengine.
Tofauti za kihaiba kati ya Tillerson na Trump zimewaingiza katika msuguano na dharau.
Habari zinasema Tillerson amewaambia marafiki zake kwamba anakusudia kushikilia nafasi hiyo kwa angalau mwaka mmoja, mstari aliojichorea kisaikolojia kwamba utamwezesha, kwa hiari yake moyoni, kuondoka kwa heshima.
Lakini kukirihika kwa bosi wake kukichanganywa na kukerwa kwake kumesababisha wakati fulani kuyumba. Tillerson alionyesha ishara wiki hii kwamba ataendelea na kazi zake walau kwa sasa, ikiwa ni pamoja na kuonekana hadharani kumuunga mkono Trump.
Chanzo kinachofahamu vizuri mzozo unaomzingira Tillerson kinasema “hakuna dalili” kuwa kibarua chake kiko hatarini walau siyo kwa sasa.

No comments:

Post a Comment