Wednesday, November 1

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUJIUZULU NDG. LAZARO NYALANDU

MAHAKAMA YAPOKEA HATI YA UKAMATWAJI ILIYOJAZWA KATIKA UPEKUZI ULIOFANYIKA NYUMBANI KWA WEMA SEPETU


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepokea hati ya ukamatwaji iliyojazwa katika upekuzi uliofanyika nyumbani kwa muigizaji maarufu wa filamu nchini, Wema Sepetu  kama kielelezo kwa upande wa mashtaka na kutupilia mbali hoja za upande wa utetezi zilizowasilishwa mahakamani hapo na wakili Peter Kibatala.

Uamuzi huo umetolewa leo, Novemba 1, 2017 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kusema kuwa upekuzi huo ulifanywa nyumbani kwa Wema na siyo Maungoni mwake kwani kama upekuzi ungefanyika maungoni mwake basi ni lazima angepekuliwa na askari wa kike.

Awali upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula uliiomba mahakama ipokee hati ya ukamataji Mali uliofanyika nyumbani kwa Wema kama kielelezo huku upande wa utetezi ukipinga.

Kesi hiyo sasa itaendelea Novemba 16, mwaka huu. Huku Hakimu Simba akiagiza mashahidi wote wa upande wa mashtaka wafike siku hiyo.

Katika upekuzi uliofanyika nyumbani kwa Wema panadaiwa kuwa palikutwa na  misokoto inayodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya bangi.

Katika ushahidi uliotolewa na Inspekta Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Wille (43) kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi  wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya  Dar es Salaam yeye alidai katika upekuzi huo walifanikiwa kukuta misokoto inayodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya bangi.

Wema anashtakiwa pamoja na wafanyakazi wake wawili, Angelina Msigwa  na Matrida Seleman Abbas. Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.

Urusi kujenga viwanda viwili vya nishati ya nyuklia Nigeria

Urusi imetia saini mkataba wa kujenga viwanda viwili vya nishati ya nyuklia nchini Nigeria ili kukabiliana na uhaba mkubwa wa umeme
Image captionUrusi imetia saini mkataba wa kujenga viwanda viwili vya nishati ya nyuklia nchini Nigeria ili kukabiliana na uhaba mkubwa wa umeme
Urusi imetia saini mkataba wa kujenga viwanda viwili vya nishati ya nyuklia nchini Nigeria huku taifa hilo lenye uchumi mkubwa barani Afrika likiweka mikakati ya kumaliza matatizo yake ya umeme.
Kampuni inayomilikiwa nchini Urusi Rosatom itajenga kituo kimoja kusini na chengine katikati kulingana na duru katika tume ya nishati nchini Nigeria.
Thamani ya makubaliano hayo haijulikani, ijapokuwa ripoti zinasema kuwa huenda inakaribia $20bn.
Ni mojawapo ya viwanda vya kinyuklia ambavyo kampuni hiyo ya Urusi imekuwa ikilenga kujenga barani Afrika.
Kampuni hiyo pia imeanza mazungumzo ya kujenga vituo kama hivyo nchini Ghana na Afrika Kusini.
Makubaliano ya wali ya kampuni hiyo kujenga kituo kama hicho nchini Afrika Kusini yalikataliwa na mahakama ya taifa hilo mapema mwaka huu.
Makubaliano hayo nchini Nigeria yaliafikiwa baada ya muda mrefu wa majadiliano huku mataifa hayo mawili yakitia saini makubaliano ya kwanza ya ushirikiano wa kinyuklia kati ya serikali mbili 2009.
Nigeria inatumai kiwanda hicho ambacho opersheni zake zitaendeshwa na Rosatom kabla kukabidhiwa serikali ya Nigeria kitasaidia kukabiliana na uhaba wa umeme wa taifa hilo.
Kulingana na takwimu za benki ya dunia, zaidi ya asilimia 40 ya taifa hilo halikuwa na umeme 2014.
Nigeria ndio taifa lenye utajiri mkubwa wa mafuta barani Afrika lakini utajiri wake wa mafuta umetumiwa vibaya kwa miaka mingi.
Ufisadi umeliwacha taifa hilo bila fedha na kutoa kiwango kidogo cha umeme ambacho raia milioni 180 wa taifa hilo wamekuwa wakihitaji.
Ujenzi wa kiwanda hicho kipya unatarajiwa kuanza katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Mahakama ya juu yasitisha uchaguzi wa rais Liberia

George Weah (L) and Joseph Boakai (R)Haki miliki ya pichaREUTERS/ EPA
Image captionGeorge Weah (kushoto) na makamu wa Rais Joseph Boakai
Mahakama ya juu zaidi nchini Liberia imeamrisha maandalizi ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais kusitishwa kufuatia madai ya udanganyifu kutoka kwa mgombea aliyeondolewa kutoka kinyanganyiro hicho.
Mcheza soka wa zamani George Weah na makamu wa Rais Joseph Boakai wanatarajiwa kukutana katika duru hiyo ya pili ya tarehe 7 Novemba.
Lakini mgombea wa chama cha Liberty Charles Brumskine, ambaye alichukua nafasi ya tatu amepinga matokeo hayo.
Uchaguzi wa mwezi uliopita ndio wa kwanza huru kufanyika tangu kukamilika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2003.
Mahakama imeamrisha chama cha Liberty na tume ya uchaguzi nchini humo kupeleka kesi zao ifikapo Alhamisi.
Lakini msemaji wa tume ya uchaguzi Henry Flomo aliambia BBC kuwa hajajulishwa rasmi kuhusu amri hiyo ya mahakama.
Waangalizi wa kimataifa wakiwemo wale kutoka muungano wa Ulaya hahawajaelezea hitilafu yoyote wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi.

Watumishi 71 wafutwa kazi kutokana na rushwa


Watumishi 71 wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wanaofanya kazi katika kitengo cha mizani wamefukuzwa kazi kwa tuhuma za rushwa.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale amesema watumishi hao wanadaiwa kupokea rushwa ili kuruhusu magari yanayozidisha uzito kupita kwenye mizani bila kutozwa faini. Amesema watumishi wengine saba wanachunguzwa kwa tuhuma hizo.
Mfugale amesema hayo leo Jumatano Novemba Mosi, 2017 katika mkutano wa tisa wa baraza la wafanyakazi wa Tanroads unaofanyika mjini Kigoma.
“Hatua hizi zimechukuliwa kati ya Januari na Oktoba,2017, tutaendelea kuchukua hatua kwa wote wanaojihusisha na vitendo hivyo,” amesema Mfugale.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga amewataka watumishi wa umma kujiepusha na vitendo vya rushwa. Ameonya watakaobainika watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.
“Bila kudhibiti magari yanayozidisha uzito, barabara zetu zinazojengwa kwa gharama ya mabilioni ya fedha za umma hazitadumu,” amesema Anga.
Mkuu wa wilaya ametoa mfano wa miradi ya ujenzi wa barabara zinazogharimu mamilioni ya fedha za umma kuwa za Nyakanazi-Kakonko na Kasulu -Kidahwe zinazounganisha Kigoma na mikoa mingine.
Mwenyekiti wa Bodi ya Tanroads, Hawa Manga amewaasa watumishi kuzingatia sheria, kanuni na maadili.

Mahakama yamwachia huru Malima



Siku sita baada ya Adam Malima kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mahakama imemfutia kesi ya shambulio iliyokuwa ikimkabili.
Rais John Magufuli, Alhamisi Oktoba 26,2017 alifanya uteuzi mbalimbali ukiwemo wa wakuu wa mikoa.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatano Novemba 1,2017 imeifuta kesi dhidi ya Malima na mwenzake.
Malima ambaye amesharipoti mkoani Mara hakuwepo mahakamani wakati uamuzi huo ukitolewa.
Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage ameifuta kesi hiyo na kuwaachia huru washtakiwa baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kuomba ifutwe.
Chini ya kifungu cha 91 (1) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Mutalemwa ameomba shauri lifutwe kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi ya washtakiwa.

Baada ya ombi hilo kuwasilishwa, Hakimu Mwijage alimuhoji Mutalemwa iwapo kuna sababu ya kuifuta kesi hiyo na kama hana hataifuta.
Wakili Mutalemwa alisoma kifungu hicho akisema kinampa mamlaka DPP kuiondoa kesi mahakamani wakati wowote anapoona inafaa na pia, kinamruhusu kuirudisha mahakamani.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mwijage alikubali kuwaachia huru washtakiwa.
Shauri hilo lilikuwa katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Waliposomewa maelezo ya awali, Malima na mshtakiwa mwenzake Ramadhani Kigwande walikubali maelezo yao binafsi, siku ya tukio walikuwepo Masaki, walikamatwa na kushtakiwa.
Walikana maelezo mengine kuhusu mashtaka yanayowakabili.
Katika kesi hiyo, Malima aliyewahi kuwa naibu waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne na mbunge wa zamani wa Mkuranga alidaiwa Mei 15,2017 katika eneo la Masaki kwa makusudi alimzuia ofisa wa polisi Konstebo Abdu kufanya kazi yake halali.
 Malima alidaiwa kumzuia askari huyo kumkamata Ramadhani Kigwande kwa kosa la kumshambulia Mwita Joseph.
Kigwande alidaiwa Mei 15,2017 eneo la Masaki wilayani Kinondoni akiwa na nia ya kumzuia Mwita Joseph, ambaye ni ofisa operesheni wa kampuni ya Priscane Business Enterprises alipokuwa akimkamata kwa kupaki vibaya gari alimshambulia na kumsababishia maumivu.
Waliposomewa mashtaka, washtakiwa walikana na walikuwa nje kwa dhamana  kwa kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja ambaye alisaini bondi ya Sh5 milioni.

MAVUNDE ASISITIZA KUWA NA NGUVU KAZI YA VIJANA WENYE UJUZI KATIKA UJENZI WA UCHUMI WA TAIFA


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi,Vijana na Ajira) Mh. Anthony Mavunde leo ametembelea Chuo cha Ufundi Don Bosco kilichopo mkoani Kilimanjaro na kukagua maendeleo ya Vijana ambao wanasomeshwa hapo na Serikali kupitia mpango wa Ukuzaji Ujuzi Nchini.

Akizungumza na Vijana hao ambao wanasomea masomo ya Komputa,Mavunde amewataka Vijana hao kuutumia ujuzi watakaoupata hapo chuoni kujiajiri kwa  kuunda vikundi na Makampuni ili wapate nafasi ya kuwezeshwa kupitia mifuko ya uwezeshwaji wananchi kiuchumi nchini na hivyo kusaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa Ajira kwa Vijana.

Mavunde pia amewaeleza Vijana hao kwamba watambue siku zote wao ndio moyo wa Taifa  na hivyo ndio nguvu kazi inayotegemewa kwa kiasi kikubwa ndio maana Serikali inaona umuhimu wa kuwekeza katika Mpango huu wa ukuzaji Ujuzi ili kuhakikisha Taifa linakuwa na nguvu kazi yenye ujuzi stahiki katika kuelekea nchi Uchumi wa Viwanda na ya kipato cha kati.

Kwa upande wao Vijana hao wanufaika na Mpango huu wameishukuru serikali kwa kutekeleza mpango huu wa ukuzaji ujuzi ambao utawasaidia kupata ujuzi na baadaye kuweza kujiajiri na Kuajiri Vijana wengine.

Mpango huu wa ukuzaji ujuzi unatarajia kuwanufaisha Vijana 3445 ambao serikali itagharamia mafunzo yao katika kozi za Tehama,Umeme,Ushonaji,Useremala,Uchomeleaji,Kuweka vigae,Ufundi bomba,Upigaji chapa na Ufundi Magari.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi,Vijana na Ajira) Mh. Anthony Mavunde akikagua maendeleo ya Vijana ambao wanasomeshwa na Serikali kupitia mpango wa Ukuzaji Ujuzi Nchini katika Chuo cha Ufundi Don Bosco kilichopo mkoani Kilimanjaro.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi,Vijana na Ajira) Mh. Anthony Mavunde akizungumza na vijana katika Chuo cha Ufundi Don Bosco kilichopo mkoani Kilimanjaro.

IGP SIRRO ATAKA JESHI LA POLISI KUDUMISHA MICHEZO

Na Jeshi la Polisi.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amewataka Maofisa na Askari Polisi kote nchini kushiriki michezo ili kujenga Afya,ukakamavu na urafiki baina ya wenyewe kwa wenyewe na raia.

IGP Sirro ameyasema hayo jijini Dar Es Salaam wakati hafla fupi ya kuwapongeza wachezaji wa TAEKWONDO waliofanya vizuri katika michezo ya Taekwondo Pumsae (kucheza Kata), Taekwondo Gyeokpa ( kuvunja kibao kwa kuruka Juu) na Taekwondo Gyeorugi (Mapigano) iliyomalizika hivi karibuni ambapo timu ya Polisi iliibuka na ushindi wa kwanza  katika timu 17 zilizoshiriki.

Sirro alisema Jeshi la Polisi litaendelea kutilia mkazo michezo ya aina mbalimbali na atahakikisha Askari na Maofisa wanapata fursa ya kushiriki michezo kwakuwa kwakufanya hivyo kutasaidia pia kulitangaza Jeshi la Polisi na kujenga mahusiano na jamii."Hakikisheni hamrudi nyuma,tutawapa sapoti ya kila namna ili tusiwe wasindikizaji bali tuweze kutoa ushindani na kufanya vyema na ni jambo linalowezekana kwa kuwa ari na morali ipo"Alisema Sirro.

Kwa Upande wake Mkuu wa Michezo wa Jeshi la Polisi,Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Philip Kalangi alisema ushindi wa timu hiyo ni chachu katika kujiandaa na michezo ya majeshi ya EAPCCO itakayofanyika hapa nchini mwakani ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji.

mashindano hayo yaliyoandaliwa na ubalozi wa Jamhuri ya korea ukishirikiana na Chama cha Walimu wa Taekwondo kutoka korea (Korean Taekwondo Masters Association) ambayo ni mashindano ya Taekwondo ya kitaifa yaliyofanyika tarehe 21/10/2017 ambayo yalishilikisha vilabu 17 vya Taekwondo kutoka  nchi nzima ambavyo ni Makongo Juu, Kariakoo,Shark TKD,Twiga Triple A,HTC DSM, KILI, Vingunguti,Arusha Morden,TCC,AICC,UAUT pamoja na vilabu vya Polisi ambavyo ni DPA, MPA na ZPA.
  Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akiwa na viongozi wa Jeshi la Polisi  Sambamba na Askari Polisi walioshiriki na kujinyakulia medali mbalimbali katika mashindano ya mchezo wa Taekwondo iliyo andaliwa na Ubalozi wa Jamuhuri ya Korea ukishirikiana na Chama cha walimu wa Taekwondo kutoka Korea. (Korean Taekwondo Masters Association)
 Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akiwa na askari wa jeshi hilo wanaounda timu ya Taekwondo ambao walishiriki na kujinyakulia medali mbalimbali katika mashindano ya Taekwondo yaliyo andaliwa na Ubalozi wa Jamuhuri ya Korea ukishirikiana na Chama cha walimu wa Taekwondo kutoka Korea. (Korean Taekwondo Masters Association) yaliyoshirikisha vilabu 17 vya Taekwondo kutoka nchi nzima.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simoni Sirro akimvisha medali askari Polisi ambaye ni miongoni mwa askari waliojinyakulia medali katika mashindano taekwondo iliyo andaliwa na Ubalozi wa Jamuhuri ya Korea ukishirikiana na Chama cha walimu wa Taekwondo kutoka Korea. (Korean Taekwondo Masters Association). Picha zote na Jeshi la Polisi

RC MAKONDA AOKOA BILLION 1.11 KUFUFUA MAGARI MENGINE YA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA YALIYOKUFA



Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akikaribishwa na viongozi wa jeshi wakati alipokwenda kukabidhi Mabasi 10 chakavu ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kampuni ya Dar Coach kwa ajili kufufuliwa upya na kuwa ya kisasa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda leo amekabidhi Mabasi 10 chakavu ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kampuni ya Dar Coach kwa ajili kufufuliwa upya na kuwa ya kisasa.

Mabasi hayo 10 chakavu yanatoka kwenye Vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ Magari 3, Jeshi la Polisi Magari 4 pamoja na Jeshi la Magereza Magari 3 ambapo yote kwa pamoja Matengenezo yake yameokoa kiasi cha Shilingi Billion 1,110,000,000 ya Serikali.

Makonda amesema kuwa Gari hizo zitatengenezwa na kukamilika ndani ya Siku 90 hadi 120 ambapo ameipongeza Kampuni ya Dar Coach kwa kujitolea kukarabati Magari hayo bila kutumia pesa ya Serikali.

Aidha Makonda amesema Magari hayo yatafungwa Vifaa vya Kisasa ikiwemo Kiyoyozi (AC), Mfumo wa Chaji ya Simu kila Seat, Runinga, Radio, Viti vya kisasa, Vyoo vya Ndani, Bodi mpya pamoja na mwonekano mzima wa Gari ili ziwe za kisasa.

Amesema mpango wake wa kuendelea kuongezea nguvu Vyombo vya Ulinzi na Usalama hautokoma kwakuwa lengo lake ni kuwatumikia Wananchi na Askari wajivunie kufanyakazi chini ya Mkuu wa Mkoa mwenye kuwapenda na kuwajali.

Amemuagiza Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa kuhakikisha Ving'ora vya Jeshi la Polisi vinakuwa tofauti na kampuni za Ulinzi na Usalama, Magari ya Wagonjwa ili kupunguza Mkanganyiko kwa wananchi na kujengea heshima Jeshi la Polisi.

Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na usalama akiwemo Kamanda wa Polisi Dar es Salaam Lazaro Mambosasa, Mkurugenzi wa usafirishaji JWTZ Kanal RAajab Mwenyumbu, Mnadhimu wa Jeshi la Magereza ACP. Noel James ambapo wote kwa pamoja wamempongeza mkuu wa mkoa kwa hatua kubwa anayoifanya ya kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira mazuri.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda akimkabidhi Mabasi 10 chakavu ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Dar Coach kwa ajili kufufuliwa upya na kuwa ya kisasa wakishuhudiwa na  Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaviva,Kamanda wa Polisi Dar es Salaam Lazaro Mambosasa, Mkurugenzi wa usafirishaji JWTZ Kanal RAajab Mwenyumbu, Mnadhimu wa Jeshi la Magereza ACP. Noel James.
Mabasi 10 chakavu yakiwa yanatoka katika Chuo cha Polisi Kilwa Road kuelekea Mkuranga kwenye ofisi za Kampuni ya Dar Coach kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho na kuwa ya kisasa zaidi.
Mkuu wa Mkoa Paul Makonda akiwa ndani ya basi la Magereza.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaviva,Kamanda wa Polisi Dar es Salaam Lazaro Mambosasa, Mkurugenzi wa usafirishaji JWTZ Kanal RAajab Mwenyumbu, Mnadhimu wa Jeshi la Magereza ACP. Noel James wakati wa kukagua mabasi 10 chakavu kabla ya kupelekewa kwenye gereji ya Dar Coach kwa ajili ya matengenezo.Picha zote na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

BASHE AUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS DKT MAGUFULI KATIKA KUSIMAMIA RASIMALI,KUFUNGA MIANYA YA RUSHWA NA KURUDISHA NIDHAMU YA KAZI KWA WATUMISHI WA UMMA

Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Mhe. Hussein Mohammed Bashe amekua na mkutano wa wazi na wananchi uliojikita katika kuelezea mafanikio na changamoto za miaka miwili ya kipindi cha ubunge wake.

Aidha Malengo makubwa ya mkutano huo yalikuwa ni:
1. Kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa uwazi ili kuongeza nafasi ya ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika mijadala ya maendeleo.

2. Kueleza juhudi za kuleta maendeleo zilizokwishafanywa na Ofisi ya Mbunge katika kipindi cha miaka miwili (2)

3. Kutambulisha miradi mikubwa ya Elimu, Afya na Maji inayoendelea ndani ya Jimbo la Nzega Mjini;
Elimu
- Ujenzi wa Shule ya kwanza ya wanawake
- Utoaji wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wote wanaofaulu Jimboni kupitia Bashe Scholarship Awards 
- Ugawaji wa Vifaa vya shule na madaftari 37,000 
- Ujenzi wa Shule ya Kwanza ya Kidato cha Tano na Sita 
- Ujenzi wa zaidi ya vyumba vya madarasa 32 ya Shule za Msingi  kwenye kata 10 jimboni

Afya
- Ujenzi wa Nyumba za waganga 
- Ujenzi wa Zahanati kwenye kila Kata
- Ugawaji wa Vitambulisho vya Matibabu kwa wazee 
- Upanuzi wa kituo cha Afya cha Zogolo kuwa na hadhi ya Hospitali

4. Kuelezea miradi ya uwezeshaji kwa akina mama na vikundi vya wajasiriamali ambayo imefanywa na Ofisi ya Mbunge ikiwemo;
 - Utoaji wa mikopo kwa vijana
- Utoaji wa mikopo kwa wanawake
- Utoaji wa pikipiki kwa vijana

5. Kuelezea mradi mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria ambao tayari umeshaanza utekelezaji wake hivyo kuwahamasisha wananchi kulinda mali na kuwa tayari kupisha maeneo ambayo mradi utapita ili kuweza kutatua kanisa shida ya Maji Nzega.

6. Upatikanaji wa fedha za Maendeleo zaidi ya Bilioni Moja na Milioni Mia Tank nje ya Bajeti.
(a)  259,000,000 - Ujenzi Shule ya Bweni ya Kwanza Nzega ya Kidato cha Tano na Sita
(b) 384,000,000 - Ujenzi wa Shule ya Kwanza ya wasichana Nzega Kidato cha Kwanza hadi Sita 
(c) 400,000,000 - Uboreshaji wa Miundombinu ya Maji. Fedha hizi amezitoa Mhe. Dr. John Pombe Magufuli baada ya kumuomba alipotembelea kwa nyakati tofauti Nzega na Tabora.
(d) 500,000,000 - Ujenzi na Upanuzi wa Kituo cha Afya cha Zogolo kuwa na hadhi ya hospitali.

7. Kuelezea mafanikio na maendeleo makubwa ya ukuaji wa sekta ya elimu ndani ya Jimbo la Nzega Mjini kwa kipindi cha miaka miwili tangu amekua Mbunge kama ifuatavyo;
Ufaulu Elimu ya Msingi Nzega
2014 - 48%
2015 - 54%
2016 - 74%
2017 - 90.66%

Ufaulu Elimu Sekondari IV
2014 - 59%
2015 - 72%
2016 - 77%
2017 - 82%

Ufaulu Elimu Sekondari II
2015 - 79%
2016 - 81%
2017 - 87%

Mwisho; Mhe Hussein Bashe ameunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli katika kusimamia rasilimali; kufunga mianya ya rushwa na kurudisha nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma.

Kwa upande mwingine Mhe. Bashe amemshukuru Rais Dr. John Pombe Magufuli kwa Namna ambavyo amekua bega kwa bega katika kushirikiana na wananchi wa Jimbo la Nzega Mjini kutatua changamoto mbalimbali.

Mheshimiwa Bashe amesema ya kuwa  ...."Mwaka 2015 katika viwanja hivi vya parking nikiwa na Mgombea urais wakati huo Mhe. John Pombe Magufuli nilimuahidi kuwa Mimi sitakua mbunge wa ndio Mzee ila nitamsaidia sana katika kuishauri serikali, kuitetea na pia kuikosoa pale inapobidi ili kuboresha ufanisi wa serikali na Chama cha Mapinduzi."
 Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Mhe. Hussein Mohammed Bashe akiwahutubia wananchi jimboni kwake katika mkutano wa wazi na wananchi,Mh Bashe alijikita katika kuelezea mafanikio na changamoto za miaka miwili ya kipindi cha ubunge wake.

 Baadhi ya Wananchi wa Nzega wakimsikiliza Mbunge wao,Mh bashe alipokuwa akiwahutubia katika mkutano wa wazi.

WATAALAM JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI WAIBUA CHANGAMOTO SEKTA YA NISHATI


Watalaam wa Masuala ya Nishati wakifuatilia taarifa kuhusu masuala ya umeme wakati wa Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Asteria Muhozya, Arusha

Wataalam wa Masuala ya Nishati wanaoshiriki Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Jumuiya ya Afrika Mashariki unaondelea jijini Arusha wameibua masuala kadhaa katika mkutano huo ambayo yanalenga kuharakisha utekelezaji wa miradi ya Nishati iliyokubaliwa na Jumuiya hiyo. Hayo yalibainika katika siku ya Pili ya mkutano wa Timu ya Wataalam kutoka Jumuiya hiyo ulioanza tarehe 30 Oktoba, 2017. Mkutano wa Wataalam umefanyika kabla ya kikao cha Makatibu Wakuu kitakachofanyika tarehe 2 Oktoba, 2017 na kitafuatiwa na kikao cha Mawaziri wa Nishati kinachotarajiwa kuhitimisha mkutano huo tarehe 3 Oktoba,2017.

Baadhi ya miradi ya umeme iliyojadiliwa ni pamoja na ile ya ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha Umeme inayounganisha nchi na nchi ambayo imeelezwa kuwa na kasi ndogo katika utekelezaji wake. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa Miundombinu ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 wa Singida- Arusha- Namanga, mradi wa kV 220 wa Rusumo- Nyakanazi na mradi wa kV 400 wa Iringa- Mbeya - Tunduma. Pia, Wataalam hao wamejadili masuala ya kodi kwa vifaa vya umeme jua, miradi ya umeme ya mipakani ikiwemo miradi ya Murongo/Kigagati na Nsogezi pamoja na Sera ya Usalama wa Nishati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Baadhi ya Wataalam kutoka Tanzania wakijadiliana jambo wakati wa mkutano huo.

Aidha, katika siku mbili za majadiliano, Watalaam kutoka Jumuiya hiyo pia wamejadili masuala kadhaa yakiwemo yanayohusu nishati jadidifu, gesi asilia na mafuta. Kikao cha Makatibu Wakuu, kitakachofanyika tarehe 2 Oktoba, kitatanguliwa na kikao cha Kamati ya Nishati cha Baraza hilo kinachofanyika leo tarehe 1 Oktoba, 2017 ambapo hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Wataalam hao zitajadiliwa katika kikao hicho.

Awali, akifungua mkutano wa Baraza hilo kwa upande wa Wataalam tarehe 30 Oktoba, 2017 Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki upande wa Sekta za Kijamii na Uzalishaji, Christophe Bazivamo alieleza umuhimu wa nchi husika kuongeza kasi ya upatikanaji wa Nishati miongoni mwa nchi wananchama ili kuwezesha mapinduzi ya Viwanda na kusisitiza kuwa, miongoni mwa maeneo ya kipaumbele ya Jumuiya hiyo ni Nishati.
Wataalam kutoka nchi mbalimbali wakijadiliana kuhusu masuala ya mafuta na gesi asilia wakati wa Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Bazivamo aliongeza kuwa, ili nchi hizo ziendeleee kiviwanda zinahitaji nishati kwa kuwa ndiyo kichocheo kikuu cha maendeleo na kwamba, bado idadi kubwa ya wananchi wa jumuiya hiyo haijaunganishwa na nishati ya umeme. Pia, aliongeza kuwa, ukosefu wa nishati hiyo siyo tu unadidimiza maendeleo ya watu pia unaathiri sekta ya elimu kwa kuwa, kukosekana na nishati kunasababisha wanafunzi hususani waishio vijijini kutumia muda mwingi kutafuta nishati ya kuni kwa ajili ya kupikia badala ya kujikita na masomo.

Nchi zinazoshiriki mkutano huo ni pamoja na Tanzania, Uganda, Rwanda, Uganda na Kenya. Aidha, Tanzania inawakilishwa na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maji, Mazingira na Nishati ya Zanzibar, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Wakala wa Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta , Zanzibar (ZURA). Mwenyekiti wa Mkutano wa 12 wa Baraza hilo ni nchi ya Uganda na Katibu ni nchi ya Rwanda.
Baadhi ya Wataalam kutoka nchini Kenya wakijadiliana jambo.

JPM: MAJIZI CCM YANAKIMBILIA CHADEMA


RAIS Dk. John Magufuli amesema yalikuwapo majizi CCM kuliko hata ya Chadema na wengine wametoka kwenye chama hicho tawala na kukimbilia chama hicho cha upinzani.
Alisema pia kuwa wapo waliopo Chama cha Wananchi (CUF) wengine ni wabaya sana.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Mkuyuni jijini Mwanza.
“Ndiyo maana tumeamua kuijenga reli ya umeme na sio ya kuendeshwa na dizeli kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma kwa fedha za ndani za Watanzania Sh trilioni 7, nataka niwaambie kwamba hata kama itachukua miaka 10 itafika Mwanza na speed (mwendo kasi) yake ni kilomita 160 kwa saa.
“Tunataka Tanzania mpya, hilo ndiyo lengo langu na ndiyo maana nilipofika hapa sikusema CCM oyee kwa sababu yapo yaliyokuwepo CCM yalikuwa majizi sana kuliko hata ya Chadema.
“Ndiyo maana mimi niko hapa sijasema Chadema oyee, kwa sababu yalikuwepo majizi CCM yakakimbilia Chadema, ndiyo maana sijasema CUF oyee, kwa sababu wapo waliopo CUF wengine ni wabaya sana, mimi nataka maendeleo, nasema Tanzania oyee, kwa sababu Tanzania inatakiwa kujengwa na Watanzania,” alisema Rais Magufuli.

AWATAKA WAWEKEZAJI KUJITATHMINI
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli wakati akizindua kiwanda cha kuzalisha dawa za binadamu cha Prince Pharmaceutical Ltd kilichopo eneo la Buhongwa mkoani Mwanza, alitoa wiki mbili kwa wawekezaji wa viwanda vya Keko Pharmaceutical Ltd na Tanzania Pharmaceutical Ltd vya Dar es Salaam, ambavyo pia Serikali ni mbia, kujitathmini  juu ya kusuasua kwa uzalishaji wake na wakishindwa watanyang’anywa na kugawiwa kwa wawekezaji wengine.
Agizo la Rais Magufuli lilitokana na kauli ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, aliyewataka wawekezaji hao kuonana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Elisante ole Gabriel kumweleza mikakati yao kabla ya Serikali kuchukua uamuzi wake.
“Tanzania ina viwanda 13 vya kutengeneza dawa za binadamu, lakini vinavyofanya kazi ni vitano. Kati ya hivyo vitano, viwili vinasuasua, tena ndivyo ambavyo vina ubia na Serikali, hivyo natoa mwezi mmoja kwa mwekezaji kama atashindwa kuchukua hatua, Serikali itavichukua, kama nguo imekubana ni vema ukaivua na kumpa mdogo wako.
“Kabla ya kuchukua hatua hizo, wawekezaji hao nendeni mkaonane na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Elisante ole Gabriel na kumpa mikakati yenu kabla ya Serikali kuchukua uamuzi,” alisema.
Aidha, Mwijage alidokeza kuwa kuna wawekezaji watano wameonyesha nia ya kuwekeza nchini na katika kipindi cha miezi 18, lazima kutakuwa na viwanda vitatu vitakuwa vimejengwa na wawekezaji hao, pia  ndani ya miezi 12 lazima kuwepo na kiwanda cha kuzalisha matone maji (drip) kwani Serikali inatumia Sh bilioni moja kuagiza nchini Uganda.

JPM ASHANGAZWA MAJI YA DRIP KUAGIZWA NJE
Akizungumza jana, Rais Magufuli alishangazwa na kutokuwapo na hata kiwanda cha drip, mabomba ya sindano na pampas hapa nchini, huku vyote  vikiagizwa kutoka mataifa mengine.
“Hata mimi mwenyewe najua kutengeneza maji ya drip, wanafunzi wa chuo waliosoma kemia kwa kidato cha nne na sita wanajua kutengeneza, kwanini tusitengeneze maji ya drip badala yake tunanunua Uganda? Tunashindwaje kuwatumia wanafunzi au wahitimu wa kemia kutengeneza?” alihoji.
Pia alitoa angalizo kwa mwekezaji wa Kiwanda cha nguo cha Mwatex kilichopo Mwanza, kuhakikisha kinaongeza uzalishaji na kuacha visingizio na kama ameshindwa ni vema kukiachia ili kukabidhiwa mtu mwingine.
Rais Magufuli alionyesha pia kushangazwa na mwekezaji wa kiwanda hicho, kupewa kingine Mbeya na sasa hakifanyi kazi ipasavyo.

UJUMBE KWA WAFANYABIASHARA
Pia Rais Magufuli aliwatumia ujumbe wafanyabiashara, kwamba wasilalamike pesa kukosekana mifukoni badala yake watumie fursa ya Tanzania ya viwanda kuwekeza ili Serikali iweze kuwapatia zabuni na hatimaye watapata fedha kwa urahisi.
“Pesa zipo nyingi, lakini za bure hazipo na hazitakuja kamwe, lazima mzitafute kwa kufuata mkondo mzuri ambao ni kuwekeza kwenye viwanda na masoko yapo likiwamo la Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki lenye watu  milioni 165, pia kuna soko la nchi za Jumuiya ya Nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC), ambalo lina watu milioni 400, hivyo ukiwekeza kwenye viwanda utapata wateja wengi huko,” alisema.
Rais Magufuli aliwaonya wafanyabiashara wa dawa kutotumia fursa ya soko la ndani kupandisha bei ya bidhaa hizo, badala yake ziwe nafuu ili Serikali iweze kuangalia kuongezea Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa zile zinazotoka nje ya nchi na kuwaondolea wazalishaji wa ndani.

WAZIRI UMMY
Kwa upande wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema Kiwanda cha Prince Pharmaceutical kitaokoa zaidi ya asilimia 80 ya dawa zilizokuwa zikiagizwa nje ya nchi.
Alisema Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD), wameanzisha mpango wa kununua dawa kutoka kwa wazalishaji wa ndani.
Waziri Ummy alisema tayari zabuni imetangazwa na mikataba 10 kwa wazawa imetolewa yenye thamani ya Sh bilini 20.6 hadi Oktoba mwaka huu.
“Kwa bahati nzuri, MSD imeteuliwa na SADC kuwa mnunuzi wa dawa za nchi 15 ambazo zitanunuliwa katika viwanda vya hapa Tanzania, kikiwamo hiki cha Prince, pia tuna mpango wa kujenga kiwanda kinachozalisha bidhaa za pamba mkoani Simiyu.
“Pia Global Fund wameahidi kutusaidia magari 190 ya kusambaza dawa nchi nzima na yatakuwa yakionekana mara kwa mara kama ilivyo magari ya Coca Cola, vile vile si kwamba tunaendelea kununua drip nje ya nchi, mpango wetu ni kujenga hapa hapa,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Prince Pharmaceutical, Hetal Vetalan, alisema kiwanda hicho kinazalisha aina 26 za dawa na moja ya glucose na wamepata zaidi ya Sh bilioni 222.5 kutoka serikalini baada ya kuanza kununua dawa kiwandani hapo.
Awali, Rais Magufuli alifungua kiwanda cha kutengeneza bidhaa za plastiki cha Victoria Moulders & Polybags kilichopo Igogo, ambako alimpongeza mwekezaji kwa kuzalisha bidhaa ambazo zinauzwa hapa nchini na nje ya nchi.
Pia alimtaka mwekezaji huyo kukitanua kiwanda hicho ili kuboresha masilahi kwa wafanyakazi.

AUNGA MKONO JUHUDI ZA WANANCHI
Akiwa kiwandani hapo, alitoa Sh milioni tatu kwa lengo la kununulia mifuko 100 ya saruji kwa shule mbili zilizopo ndani ya kata hiyo.
Rais Magufuli alimkabidhi fedha Diwani wa Kata ya Igogo, John Minja, akiunga mkono juhudi za wananchi wa kata hiyo katika kuboresha miundombinu.
Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula, alimweleza Rais Magufuli kuwa wananchi wa kata hiyo wamechanga Sh milioni 15.8 kujenga matundu ya vyoo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuwa aliwahi kuishi ndani ya kata hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Kiwanda cha Victoria Moulders & Polybags, Manjist Singh, alisema bidhaa zinazozalishwa hapo zinauzwa Uganda, Rwanda, Burundi na ndani ya nchi na kuongeza kuwa alikianzisha kutokana na uwepo wa shughuli za kilimo na madini.
Hata hivyo, aliomba Serikali kupunguza matatizo yaliyopo soko la ndani kwa kuondoa utegemezi wa bidhaa za nje kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji wa ndani.

Meya aibuka kwa JPM
Katika hali isiyotarajiwa baada ya jana kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa saa sita, Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire, alipongeza jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli na kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania katika sekta ya afya, elimu na miundombinu.
Hata hivyo, wakati akizungumza, minong’ono na vicheko vya chini chini vilitawala, hasa kwa madiwani wenzake, huku wananchi wakimshangilia.
Bwire alimweleza Rais Magufuli kwamba amepokea maelekezo yake ya kuwataka kukaa meza moja na kutatua matatizo yao ya ndani.
Alisema binafsi ameridhia kukaa na anaamini wenzake wamemwelewa Rais Magufuli.
Hata hivyo, alimwomba Rais Magufuli pale atakapopata muda kama itampendeza, kumpa nafasi ya kumwona kwani ana jambo binafsi la kumsimulia na asingeweza kuliongea hadharani.