Thursday, November 2

Marais wa Afrika wammwagia sifa Uhuru Kenyatta


Nairobi, Kenya. Mataifa kadhaa barani Afrika yameelezea kuunga mkono matokeo ya uchaguzi wa marudio nchini Kenya yakisema  hayatarajii kuona Mahakama ya Juu nchini humo ikipinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta kwa mara ya pili katika kipindi cha miezi mitatu.
Wengi wa viongozi hao wamekuwa wakituma salama zao za pongezi kwa rais huyo mteule ambaye kuapishwa kwake kunasubiri kipindi cha siku kadhaa kupisha iwapo kama kuna raia anaweza kwenda mahakamani kupinga ushindi wake.
Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambaye hivi karibuni alichaguliwa kwa asilimia 98 ya kura, ilivyo kwa Rais Kenyatta alisema katika ujumbe wake kuwa ushindi wake (Rais Kenyatta) ni ushahidi tosha kuwa "Wakenya wana imani naye".
Naye Rais wa Uganda, Yoweri Museveni wa Uganda ambaye amekuwa akikosolewa na wapinzani wake kwa kubana demokrasia amesema kuchaguliwa tena kwa Rais Kenyatta ni ishara tosha jinsi wananchi wa Kenya walivyokuwa na imani naye.
“Nakupa pongezi zangu za dhati na uanze kutekeleza uongozi sasa Wakenya wamekupa imani yao. Natumaini utaongoza Wakenya kwa njia ya kuwaunganisha pamoja na kuwatekelezea maendeleo ili uchumi wao ukue,” alisema.
Amesema kuwa anatazamia kuendeleza ushirikiano wa taifa lake na Kenya katika nyanja mbalimbali za kuleta manufaa kwa Wakenya na Waganda.
Rais wa Namibia, Hage Geingob amesema ushindi wa Rais Kenyatta ni mwafaka."Amenidhihirishia kuwa huweka maslahi ya taifa lake mbele,” alisema Geingob.
Nchini Somalia ambako Serikali ya Kenya imetuma vikosi vyake kwa ajili ya kusaidia kuleta amani, rais wake Mohammed Farmaajo ameonyesha kuridhishwa kwake na ushindi wa Rais Kenyatta na kuahidi kuendelea kushirikiana.
“Natumaini kuwa tutaendeleza ushirikiano wetu wa dhati kama mataifa jirani ili tupate ufanisi wa kuridhisha kwa watu wetu,” alisema.
Ushindi huo wa Kenyatta umepingwa na mpinzani wake, Raila Odinga ambaye anasisitiza kutaka kufanyika kwa uchaguzi mwingine.

Deni la Sh 250 milioni kumweka ndani meneja wa Diamond


Dar es Salaam. Meneja wa msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya (Bongo fleva), Abdul Nassib maarufu Diamond Platnum, Hamis Taletale na nduguye Idd Taletale sasa wanachungulia kifungo jela kwa kushindwa kulipa fidia ya Sh250 milioni, ambazo kampuni yao ya Tiptop Connection Limited inadaiwa.
Februari 18 mwaka jana, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliiamuru kampuni hiyo kumlipa fidia ya Sh250 milioni, Mhadhiri wa Dini ya Kiislam, Sheikh Mbonde kwa kutumia mahubiri yake kibiashara bila ridhaa yake, kinyume cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.
Hata hivyo meneja huyo wa Diamond, maarufu kama Babu Tale na nduguye wakiwa wakurugenzi na wanahisa pekee wa kampuni hawakuweza kulipa fidia hiyo wala kuweka wazi mali za kampuni hiyo, hivo Mbonde akalazimika kufungua maombi ya utekelezaji wa hukumu hiyo.
Mahakama hiyo katika uamuzi uliotolewa na Naibu Msajili Wilbard Mashauri Juni 9 mwaka huu iliwaamuru wakurugenzi hao wa kampuni hiyo kuweka wazi mali za zinazomilikiwa na kampuni yao hiyo.
Alisema kuwa iwapo watashindwa kutaja mali za kampuni hiyo basi wao wenyewe watalazimika kulipa kiasi hicho cha fedha au mali zao binafsi kukamatwa na kuuzwa na kwamba iwapo hawatakuwa na mali za kulipa fidia hiyo
“Kama hawana mali, basi watakamatwa na kufungwa gerezani kama wafungwa wa madai kwa mujibu wa masharti ya Amri ya 21 Kanuni ya 38(1) ya CPC (Kanuni za Mashauri ya Madai) Sura ya 33 marejeo ya mwaka 2002.”alisisitiza Naibu Msajili Mashauri.
Katika kutekeleza agizo la Mahakama kwa wakurugenzi hao, kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart & Co Ltd imewapa siku 14 Babu Tale na nduguye kutekeleza uamuzi na agizo hilo la Mahakama.
Taairifa hiyo ya Yono imekabidhiwa leo Alhamisi na Meneja Masoko wa Yono, Kene Mwankenja kwa mjumbe ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mpakani, Kata ya Kwembe, wilayani Ubungo, Wilson John ili kuwafikishia kina Babu Tale
Iwapo hawataweka wazi mali za kampuni hiyo ili zipigwe mnada au walipe fidia hiyo ambayo kampuni yao inadaiwa ama kama hawatakuwa na mali zao binafsi ambazo zinaweza kupigwa mnada, basi wao wenyewe itabidi watupwe jela, kama Mahakama ilivyaomuru.
“Tumewapa notice (taarifa) hiyo ili kuwapa nafasi ya kumaliza suala hilo ndani ya muda huo. Wakilimaliza sawa, lakini wakipuuza basi wajibu wetu ni kutekeleza tulichoelekezwa.” amesema Mwankenja.
Katika hati ya madai ya kesi hiyo namba 185 ya mwaka 2013 na wakati wa usikilizwaji, Juni 6, 2013 Sheik Mbonde aliingia makubaliano na kampuni hiyo, kutumia kazi zake za mawaidha, kwa kuzalisha, kurekodi na kuzisambaza.
Pamoja na mambo mengine, walikubaliana kampuni kulipia gharama za kurekodi masomo na mafundisho ya mihadhara yake, kumnunulia gari, kumjengea nyumba na kugawana faida ya mauzo.
Hata hivyo, baada ya kukamilisha kurekodi masomo saba, maofisa wa kampuni hiyo walimkatia mawasiliano hadi alipobahatika kukutana na mmoja wao, Adam Waziri ambaye alimweleza kuwa wamesitisha mpango wa kuendelea na kazi hiyo.
Hata hivyo, Agosti 9, 2013, wakati mdai akiendesha mhadhara Bahi Dodoma, alibaini kuwa DVD za masomo yake zilikuwa zikiuzwa sokoni Dodoma na katika  mikoa mbalimbali kama vile Mbeya, Tanga na Dar es Salaam, bila ridhaa yake wala makubalino.
DVD hizo kwa mujibu wa hati hiyo zilikuwa ni za masomo mbalimbali aliyokuwa ameyatoa na kwamba makava ya DVD hizo yalikuwa na nembo na namba za simu za maofisa wa mdaiwa.

Lusinde azungumzia kujiuzulu Nyalandu


Dar es Salaam. Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde amezungumzia kujiuzulu kwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu akieleza ni kutokana na kuwepo kwa mfumo ulioanzishwa na Serikali kwa ajili ya kuchunguza utendaji wa viongozi waliopo na waliomaliza muda wao.
Amesema lengo la mfumo huo ni kuchunguza kila kiongozi aliyehusika au kutenda makosa yaliyolisababishia Taifa hasara wakati wa uongozi wake kabla ya kuwachukuliwa hatua za kisheria.
“Sasa hivi Serikali imetengeneza mfumo wa kuchambua sisi viongozi, wale waliokuwa viongozi wa zamani na sisi tuliopo, kujua nani fisadi na alikosea wapi ili wachukue hatua za kuwapeleka mahakamani, sasa nina wasiwasi mheshimiwa Nyalandu alikuwa amepata taarifa,”amesema Lusinde.
“Pengine yupo katika orodha ya uchunguzi, kwa hiyo akaona atumie fursa hii kukimbia ili baadaye atakapokuja kukamatwa au kuanza kuhojiwa asingizie kaanza kuhojiwa kwa sababu ya kwenda upinzani, mimi nina wasiwasi mahali siri zimevuja lakini siyo kwamba ana hoja ya msingi ya kuondoka CCM.”
Lusinde anayezungumza kupitia video inayosambaa mtandaoni amesema tangu alipomfahamu Nyalandu hakuwahi kumsikia akitoa mawazo yake katika kikao chochote cha halmashauri Kuu akimfananisha na mwanasiasa togwa (aliyepoa na asiye na msisimuko) na mwenye bahati ya kushika nafasi za uwaziri pekee.  
“Na ndiyo maana ninasema ni lini tangu ametoka kwenye uwaziri aliwahi kusimama bungeni kutoa hisia zake Spika akamkata, akasema hisia zake Spika akamtoa nje na polisi ni lini? Kwa hiyo kuhama kwake na hoja alizozitoa, hoja sita lakini kubwa kuliko zote ni Serikali kukigandamiza chama na kinashindwa kuisimamia(serikali),”amesema.
Akifafanua hoja hiyo, Lusinde  amesema Serikali anayoituhumu Nyalandu ina toufaui na CCM ya mwaka 1975 ambayo kiutendaji, katibu kata alikuwa mtendaji wa kata, mkuu wa wilaya akiwa Katibu wa CCM wilaya na mkuu wa mkoa akiwa katibu wa CCM mkoa.
“Kwa hiyo hakukuwa na kimbilio, ukikosana naye kwenye chama , unamkuta serikalini, akikuweka ndani serikalini, anakuja kukumaliza kwenye chama, sasa haipo Serikali hiyo, Serikali ya sasa ambayo Nyalandu hakuielewa inajengwa kuondoa siasa za hovyo, majukwaa na kupeleka siasa za kazi, pengine Nyalandu hakuzoea siasa hizi,”amesema.
 Amesema katika hoja sita alizotoa Nyalandu, hakuna hata moja inayogusa mahitaji ya wananchi wa jimboni kwake, akituhumu kuwa ni hoja zake binafsi. 
“Hakuna hata moja, ni wapi aliposema anaondoka CCM kwa sababu haipeleki zahanati, haipeleki barabara, yote yanamuhusu yeye, kwa hiyo kuondoka kwa Nyalandu hakuna pengo isipokuwa kuna fursa,” amesema.

JE WAJUA KUTELEKEZA ARDHI NI PAMOJA NA HAYA.


Image result for ARDHI YETU

NA  BASHIR  YAKUB -

Kuna  mambo ambayo  yafaa  tujihadhari  nayo  sana  hasa  kipindi  hiki. Wengi wamefutiwa  umiliki wa  ardhi. Takwimu  za kufutiwa ni kubwa sana kipindi hiki kama ulikuwa hujui. Kwa  watu  wanaonunua  ardhi  na  kwenda  kuishi  nje  ya  nchi  hili  lawahusu  sana kabla hamjapoteza ardhi zenu.  

Najua  unachojua kuhusu  kutelekeza ardhi  ni pengine  kutokujenga,  au  kutoitumia  kama ilivyopangiwa matumizi, nk. Ni kweli lakini  hiyo ni maana  finyu  ya kutelekeza ardhi. 

Maana  ni  zaidi ya hiyo,  na  hapa tutaona  ili  ujihadhari na  uwezekano wa  kupoteza  ardhi  yako.

1.MAMBO  AMBAYO  UKIFANYA  UTAHESABIKA  KUTELEKEZA  ARDHI.

Mambo  haya  yameelezwa   na  Sheria  Namba  4  ya  ardhi  ya  1999 kifungu  cha  51(1).

( a ) Kutokulipa  kodi, tozo  au  ushuru  wowote  ambao  upo  kisheria  kwa  ajili  ya  ardhi  ni  kutelekeza  ardhi  kwa  mujibu  wa  sheria hiyo.  Mnazijua  kodi  za  majengo,  kodi  za  ardhi  nk.  Hizi  ni  muhimu  sana  na  kimsingi  ndizo  zinazoeleza  uhai  wa  ardhi  yako.

Ikiwa hulipi  hizi  hata  kama  eneo  hilo  umejenga  kiwanda  kinachofanya  kazi  saa  24  siku  7  za  wiki  bado  mbele  ya  macho  ya  sheria  unahesabika  kutelekeza  ardhi.  Dawa  ya  kuepuka  hili  ni  ndogo.  Lipa  hizo  kodi  na  tozo  kwa  mujibu  wa  sheria. Yamkini  hizi  huwa si  pesa  nyingi  sana ya  kumshinda  mmiliki  kulipa.

( b ) Jengo  ndani  ya  ardhi  kuwa  gofu  ni  kutelekeza  ardhi  kwa  mujibu  wa  sheria.  Lakini  pia   katika eneo  hilo  sheria  imetumia  neno “disrepair”.  Maana   yake  kutokufanya  ukarabati.  Kwa  tafsiri  hii  ni  kuwa  kumbe  hata  kutokufanyia  majengo  yetu ukarabati  nako ni  kutelekeza  ardhi.

Utaona  katikati  ya  miji  yetu  majengo ya  zamani machafu,  yaliyopauka. Japo  ndani  mwake  watu  wanaishi  na  maofisi  yamo  bado kwa tafsiri  ya  neno  “disrepair”  ni  kuwa  jengo  hilo  limetelekezwa.  Na  sheria  imeeleza  zaidi  kuwa itakuwa  mbaya  zaidi  ikiwa  jengo  hilo  linahatarisha  afya  au maisha  ya  watumiaji  wake , majirani  au  hata  wapita  njia.

( c )  Sheria  inasema  ikiwa  mmiliki  ardhi  ameondoka  nchini  na  hakuacha  mtu  yeyote  hapa  nchini  wa  kuangalia  ardhi  ile  kwa  ajili  ya  kuilinda  na  kutekeleza  masharti  yote  yanayohitajika kisheria  kwa  ardhi  hiyo basi atakuwa ametelekeza ardhi hiyo.  Sheria  imetaja  kabisa  maneno  mtu  “aliyeondoka  nchini”.  Hii  maana  yake  ni  maalum  kwa  Watanzania  wanaoishi  nje  ya  nchi.

Unayemuachia  ardhi  kazi  yake  kubwa   si  kukaa  kama  mlinzi kwenye  ardhi  hiyo. Laa hasha,  bali  kazi  yake  kubwa ni  kuhakikisha  anatekeleza  masharti  ya  umiliki  wa  ardhi  kwa mujibu  wa  sheria  kwa  niaba  yako.  

Na kama  kuna  mambo  ambayo yatahitaji  sahihi  yako  basi  ni  kuhakikisha  yanakufikia  na  kuyatia  sahihi  kama  inavyohitajika.

Wengi  walio  nje  wamefutiwa  umiliki  wa  ardhi   kwa  kukosa hili. Usimamizi  wa  ardhi  zao. Hata hiyvo  kifungu  hicho kimeeleza utaratibu  wa  kumtaarifu  Kamishna  wa rdhi  kuhusu  ardhi  yako  kabla  hujaondoka kwenda nje. Hii  inaweza  sana  kukuweka  salama.

 ( d ) Pia   ardhi  kuacha  kutumika  kwa manufaa, au  ardhi  kuwa imeharibiwa  kwa maana  ya  uharibifu  wa  mazingira nako ni kutelekeza ardhi. Unaweza kuwa  uharibifu   uliosababisha  wewe  au  wa  asili.

2.  IPI  ADHABU  YA  KUTELEKEZA  ARDHI.

Adhabu  ya  kutelekeza ardhi  ni kufutiwa  umiliki   kwa  mujibu  wa  kifungu  cha  49  cha  sheria  hiyo.  Ukifutiwa  umiliki  ardhi yako  atapewa  mtu  mwingine  au  itaingia  kwenye hifadhi  ya  ardhi ya serikali  inayosubiri kugawiwa. Ni  kitu  kibaya  sana.

Makala  nyingine  nitaeleza  taratibu  zinazotakiwa kufuatwa  kabla hujafutiwa umiliki wa ardhi  ili  ujue  kama  umeonewa  iwapo  limekutokea hili  au  kama  halijakutokea   ujue  kuwa  kwa  dalili  hizi  sasa  naanza   kufutiwa  umiliki.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com

WAZIRI MKUU MAJALIWA AZUNGUMZA NA BAADHI YA WATANZANIA WAISHIO NCHINI CANADA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waishio Canada wadumishe mshikamano wao na wawe na uzalendo kwa Taifa lao.

Ametoa wito huo jana (Jumanne, Oktoba 31, 2017) wakati akizungumza na Watanzania waishio Toronto, Canada.

Waziri Mkuu ambaye yuko Canada kwa ziara ya kikazi, alisema kila Mtanzania anapaswa ahubiri utaifa wake. “Tembea huku ukiringia nchi yako, wakati wote ringia nchi yako, unapotakiwa kuisemea nchi yako, isemee vizuri kama ambavyo wengine wanasemea vizuri nchi zao licha ya matatizo waliyonayo.”

Aliwataka wakumbuke kuweka akiba na wanapopata fursa watume fedha zao nyumbani ili zisaidie kuleta maendeleo. “Ukipata kitu kidogo, rusha nyumbani; ukipata mtu anayeweza kuleta tija, mlete nyumbani, nasi tutawapokea wewe na yeye,” alisisitiza. 

“Tunawasisitiza muitangaze nchi yetu kwa mataifa mengine ili nao waone Tanzania ni mahali pa fursa, na akitaka kuwekeza ajue kuwa anawekeza mahali ambapo ni salama,” alisema.

Alisema Serikali inasisitiza wananchi waishio nje ya nchi, wawe wazalendo na washirikiane kuhakikisha wanazitumia vizuri fursa za kimaendeleo kwa manufaa ya nchi yao.

Awali, Balozi wa Tanzania nchini Canada, Mhe. Jack Nzoka, alitumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania waishio nchini humo wazingatie sheria za nchi hiyo.“Wote sisi tunawatambua kama mabalozi katika nafasi zenu hapa Canada. Tunawashauri muwe raia wema, na muishi kwa kufuata sheria na taratibu za nchi hii na msisahau mlipotoka, kwani hakuna mahali pazuri kama nyumbani,” alisisitiza.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMATANO, NOVEMBA MOSI, 2017.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na baadhi ya watanzania waishio nchini Canada, kwenye hoteli ya The Ritz-Carlton Toronto Oktoba 31, 2017
Watanzania waishio nchini Canada,wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipo kutana nao kwenye hoteli ya The Ritz-Carlton Toronto Oktoba 31, 2017.Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

HITILAFU YA MFUMO WA KUPOKELEA GESI KINYEREZI I, TATHIMINI YAONYESHA MATENGENEZO MAKUBWA YANAHITAJIKA, MAFUNDI WAKO KAZINI: TANESCO


Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, TANESCO


NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
TATHMINI iliyofanywa na Wahandisi wa Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), kufuatia mfumo wa kupokea gesi asili kwenye mitambo ya kufua umeme, Kinyerezi I jijini Dar es Salaam kupata hitilafu, imebaini matengeenzo makubwa yanahitajika kufanyika ili kuhakikisha mfumo unarudi katika ubora wake..
Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka, iliyosambazwa kwa vyombo vya habari leo Novemba 1, 2017, imesema kufuatia mfumo huo kupatwa na hitilafu majira ya mchana Oktoba 32, 2017, hatua ya kwanza iliyochukuliwa na wataalamu wa TANESCO ni kuzima mitambo ili kuruhusu kazi ya usafishaji kuondoa gesi hiyo kufanyika.
”Baada ya usafishaji wa Mitambo kukamilika, matengenezo yalianza usiku wa kuamkia leo Novemba 1, 2017, kwa kutumia wataalamu wa ndani wa Shirika pamoja na Mkandarasi wa kampuni ya JACOBSEN ELEKTRO AS.” Taarifa hiyo ya TANESCO ilisema.
Taarifa hiyo iliendelea kusema, “Kutokana na ukubwa wa matengeenzo na uangalifu wa hali ya juu unaotakiwa katika kazi hii hususan suala la usalama wa mitambo pamoja na watumishi wa Shirika waliopo katika eneo la mitambo, hatua za tahadhari zimechukuliwa.” Taarifa hiyo ilisema.
Aidha taarifa imefafanua kuwa kutokana na Mitambo hiyo kuzimwa ili kuruhusu kazi ya marekebusho ya hitilafu hiyo kukamilika kwa wakati, kutakuwa na upungufu wa umeme katika maeeno mbalimbali ya nchi.
“Uongozi wa Shirika unawaomba radhi wateja wake na wananchi kwa ujumla kwa maeneo ambayo bado yanakosa huduma ya umeme katika kipindi hiki cha matengenezo hayo na tutaendelea kuwaarifu wananchi jinsi kazi ya matengenezo inavyoendelea hadi kukamilika kwake.” Taarifa hiyo ilisema

MPANGO WA UENDESHAJI WA KIJINSIA KWA AJILI YA MWITIKIO WA UKIMWI TANZANIA BARA WATAMBULISHWA RASMI KWA MKOA WA SINGIDA

ratibu wa Jinsia kutoka TACAIDS Jacob Kayombo na Afisa Jinsia kutoka TACAIDS Judith Luande wakijadili baadhi ya maoni, maswali na mapendekezo ya wajumbe ambao ni timu ya kudhibiti Ukimwi ya Mkoa wa Singida wakati wa Mafunzo juu ya mpango wa uendeshaji wa kijinsia.
Mjumbe wa mafunzo juu ya mpango wa uendeshaji wa kijinsia Afisa wa Serikali za Mitaa Hussein Mwatawala akipitia fomu zitakazotumika katika kukusanya taarifa za masuala ya Kijinsia mkoani Singida.


Serikali kupitia Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) imeandaa Mpango wa uendeshaji wa Kijinsia kwa ajili ya mwitikio wa Masuala ya Ukimwi ambao umetambulishwa rasmi kwa timu ya Kuthibiti Ukimwi Mkoani Singida.

Mratibu wa Jinsia Kutoka TACAIDS Jacob Kayombo ameongoza mafunzo hayo kwa timu ya kuthibiti Ukimwi Mkoa wa Singida ambapo amewaeleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuratibu na kutoa dira katika utekelezaji wa program mbalimbali za Ukimwi kwa ngazi ya Mkoa.

Kayombo amesema Mafunzo hayo yamelenga kuutambulisha mpango huo pamoja na fomu zitakazotumika katika ukusanyaji wa taarifa zihusuzo jinsia na Ukimwi.“Mafunzo haya tunayotoa yamejikita katika kuufafanua mpango huu utakavyotumika pamoja na namna ambavyo fomu hizi zitatumika kukusanya taarifa za jinsia na Ukimwi kwa Mkoa wa Singida na jinsi ambavyo taarifa hizo zitasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu masuala ya Ukimwi”, amesema Kayombo.

Ameongeza kuwa matarajio yanayotegemewa baada ya mafunzo hayo kutolewa ni kuona masuala yote ya kijinsia yanapewa kipaumbele katika program mbalimbali za Ukimwi.Kayombo amesisitiza kuwa mpango huu utakuwa ni mwongozo wa wadau wa masuala ya Ukimwi ili waweze kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia usawa wa kijinsia hasa katika kuweka mikakati ya kuthibiti Ukimwi yenye uelekeo wa Usawa wa kijinsia.

Amebainisha kuwa mpango huu ambao umedumu katika kipindi cha mwaka 2016 mpaka 2018 una mwelekeo mpya wa program za ukimwi wenye kuzingatia masuala ya kijinsia pamoja na kuondoa changamoto zitokanazo na mila na desturi potofu za masuala ya kijinsia.

Naye Mjumbe wa mafunzo hayo Afisa wa Serikali za Mitaa Hussein Mwatawala amesema mafunzo hayo yametoa mwanga na mwelekeo utakawaosaidia katika kusimamia wadau wanaotekeleza shughuliza Ukimwi ili wazingatie usawa wa kijinsia mkoani hapa.

Mwatawala amesema maafisa waliopata mafunzo hayo wamepewa elimu ya kutosha juu ya mpango na wameufahamu vema kazi iliyobaki ni kuhakikisha masuala ya usawa ya kijinsia yanapewa kipaumbele katika kila program ya Ukimwi inayotekelezwa na wadau mkoani hapa.Mpango wa uendeshaji wa masuala ya Kijinsia 2016-2018 umeanzishwa kwa lengo la kutoa mwongozo kwa wadau wa masuala ya Ukimwi ili watekeleze program zao katika mtazamo wa usawa wa kijinsia.

Mpango huu unashughulikia tofauti za kijinsia zikiwemo ukatili wa kijinsia, unyanyapaa na ubaguzi ili kulinda haki za watu wote wakiwemo wanaume,wanawake,wasichana na wavulana ili wapate huduma za uzuiaji wa maambukizi ya VVU, tiba, matunzo na msaada.

Aidha mpango huu unahusianishwa na Mkakati wa tatu wa taifa wa kuthibiti Ukimwi 2013-2018 na Mkakati wa tatu wa kuthibiti VVU na Ukimwi wa Sekta ya Afya 2013-2017 ambapo mikakati hiyo ina kanuni ambazo zinajumuisha usawa wa kijinsia na ulinzi wa haki za binadamu.

SERIKALI YATAIFISHA NG’OMBE 6648 MISENYI KAGERA


Akiwa katika muendelezo wa ziara zake za oparation kamata mifugo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina Ameagiza kukamilisha taratibu za Uhamiaji na Mahakama kupitia mwanasheria mkuu wa Serikali wa Wilaya ya Misenyi Pamoja na Uhamiaji, ili kuweza kupigwa mnada kwa idadi ya ng’ombe 6648 walioingia nchini kinyemela toka nchi jirani ya Uganda na kukamatwa.

Waziri mpina alisema uvamizi wa kundi kubwa kama hilo la wanyama linaweza kusabisha madhara makubwa katika mazingira kama vile mmomonyoko wa ardhi, kuharibifu wa vyanzo vya maji, kumaliza malisho ya mifugo iliyoko nchini, kusababisha migogogoro ya mara kwa mara kwa wakulima na wafugaji na hata kuleta maambukizi ya magonjwa ya wanyama. “Sisi kama Serikali hatuwezi kuruhusu hali hii iendelee na mimi kama Waziri Mwenye dhamana nina jukumu la kuhakikisha tunalinda lasimali hii ya malisho” Alisema Mpina.

Mpina alisema suala hili haliingiliani na Ushirika wa Afrika Mashariki kwani Ushirika huo upo kisheria hivyo wavamizi wanaoingiza mifugo kinyemela nchini toka nchi jirani ni wahalifu kama wahalifu wengine. “Kwa hiyo naangiza ng’ombe hawa 6648 waliokamatwa hatua ziendelee na ambao hawajakamatwa wakamatwe na wataifishwe na Serikali.”Alisisitiza Waziri Mpina.

Kwa upande wa upande wake mkuu wa Wilaya ya Misenyi Kanali Denis Mwila alisema kuwa zoezi la kutathmini ng’ombe katika wilaya yake bado linaendelea na taratibu za kisheria zinafuatwa.

Alipokuwa Mkoani Kagera Mapema Leo Mpina alitembelea mabwawa ya mradi wa samaki yaliyopo Wilayani Muleba katika kijiji cha Luhanga na kusema Serikali ina nia ya kukomesha kabisa uvuvi haramu ikiwa ni pamoja na kuwasaka wavuvi haramu kule waliko na kuwa na nyenzo.

Aidha, akiwa Bukoba Mjini Mpina alitembelea kiwanda cha kuchakata samaki cha Suprime Fish Ltd na kuagiza wamiliki wa viwanda vya samaki nchini kuhakikisha wanachukua hatua za haraka kufufua viwanda hivyo na kuongeza uzalishaji kwani Serikali imeshaanza kuchukua hatua ya kuhakikisha samaki wanapatikana kwa wingi nchini. 

Aliyeshika Samakai aina ya Sato ni Waziri Mpina alipotembelea Mradi wa Mabwawa ya Samaki wa Luhanga Wilayani Muleba.
Waziri Mpina katika Picha akivua samaki aina ya kambale alipotembelea Mradi wa mabwawa ya samaki wa Luhanga Wilayani Muleba.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina akiiongea na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Misenyi mara baada ya zoezi la kutaifisha ng'ombe.
Katika Picha ni sehemu ya ng'ombe 6638 waliotaifishwa na serikali baada ya kuingia nchini kinyemela kutoka nchi jirani ya uganda ng'ombe hao wanasubiri maamuzi ya Mhakama kwa ajili ya Kupigwa mnada.

DC WILAYA YA NYANG'WALE ASEMA BILA YA KUWEPO USALAMA WA CHAKULA NCHINI HAKUNA KITAKACHOWEZA KUFANYIKA

 Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'wale mkoani Geita
 Mkuu wa Wilaya ya Nyang'wale Mkoa wa Geita,  Hamim Buzohera Gwiyama (katikati), akizungumza na watafiti wa kilimo kutoka  Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Ukiriguru Mwanza, Ilonga mkoani Morogoro na Waandishi wa Habari kabla ya kukabidhiwa mbegu bora za mahindi na mhogo kwa ajili ya kuzipanda kwenye mashamba darasa katika vijiji vinne wilayani humo leo hii. Kulia ni Diwani wa Kata ya Nyugwa, Ndozi Manual na kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Fabian Sospeter ambaye alikabidhiwa mbegu hizo na kuhutubia wananchi kwa niaba ya mkuu huyo wa wilaya.
 Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa uzinduzi wa upandaji wa mbegu katika mashamba darasa uliofanyika Kata ya Nyugwa wilayani humo.
 Diwani wa Kata ya Nyugwa, Ndozi Manual, akizungumza katika uzinduzi huo.
 Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Fabian Sospeter, akihutubia wananchi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo.
 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi, akimkabidhi mbegu ya mhogo aina ya Mkombozi Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Fabian Sospeter kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo.
 Mtaalamu wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula, akiwaelekeza wananchi wa Kata ya Nyugwa jinsi ya upandaji wa mbegu ya mhogo aina ya Mkombozi kwenye shamba darasa.
 Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Fabian Sospeter akipanda mbegu ya mhogo aina ya Mkombozi kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo.
 Mtafiti kutoka  Kituo cha Utafiti wa Kilimo  cha Ilonga, mkoani Morogoro, Ismail Ngolinda akitoa maelekezo kwa wakulima wa Kijiji cha Kakora  jinsi ya upandaji wa mbegu ya mahindi aina ya Wema 2109 yanayostahimili ukame. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Kilimo wa Wilaya ya Nyang'wale,Gudala Kija Tabu na katikati ni mkulima wa kijiji hicho.
 Wananchi wa kijiji cha Kakora wakiwa wamesimama mbele ya shamba la mahindi ambalo mahindi yake ni duni kutokana na mimea yake kushambuliwa na wadudu.
 Mkulima Pendo Sangoma akishiriki kupanda mbegu ya Wema katika shamba darasa katika Kijiji cha Kakora wilaya humo. Kushoto ni Ofisa Ugani, David Makabila kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
 Watoto, Michael  na Getruda Bundala wa Kijiji cha Kakora wakiwa wamebeba mbegu ya mahindi aina ya Wema wakati wa uzinduzi wa shamba darasa katika kijiji hicho.
 Ofisa Ugani wa Kijiji cha Nyang'wale, akitoa maelekezo kwa watafiti wa kilimo kuhusu masuala ya kilimo.
Mshauri wa Jukwaa la Matumizi ya Bioteknolojia katika Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange, akizungumza na viongozi wa Kijiji cha Kanegele, maofisa ugani na watafiti kabla ya kupanda mbegu ya mhogo katika shamba darasa kwenye kijiji hicho. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa kijiji hicho, Makoye Malikwisha.

Na Dotto Mwaibale, Nyang'wale, Geita

MKUU wa Wilaya ya Nyang'wale Mkoa wa Geita Hamim Buzohera Gwiyama amesema bila ya kuwepo kwa usalama wa chakula nchini bado kutaendelea kuwepo na changamoto nyingi za maendeleo na kuwa pasipo chakula hakuna kitakachoweza kufanyika.

Hayo yalisema na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Fabian Sospeter  kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo, Hamim Gwiyana wilayani humo jana wakati akipokea mbegu bora za mahindi aina ya Wema na mhogo aina ya Mkombozi kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB) kwa ajili ya kuanzisha mashamba darasa ya mbegu katika vijiji vya Kakora, Nyang'wale, Kanegele na Nyugwa.

"Bila ya kuwepo kwa chakula cha kutosha hakuna kitu kitakachoweza kufanyika kwani shughuli zote zitasimama hivyo ni muhimu kuhimizana katika kilimo chenye tija kama tunavyo himizwa na wataalamu wetu kutoka COSTECH, Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ukiriguru Mwanza na Maruku mkoani Kagera" alisema Gwiyama.

Alisema usalama wa kujilinda na adui hauna shida kwani mtu anaweza kuandaa jeshi lake la kukabiliana na adui huku akiwa na silaha nzito lakini sio usalama wa chakula ambao unahitaji maandalizi ya kutosha na watu kujituma na kufanya kazi kwa bidii hasa za kilimo chenye tija.

Alisema kukosekana kwa chakula mara nyingi kunachangiwa na tabia za baadhi ya watu kuharibu mazingira kwa kukata miti hovyo hivyo kusababisha mvua kushindwa kunyesha  na maeneo mengi kuwa na ukame.

Alisema katika wilaya yake njaa imechangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kuwa watoro na kushindwa kumaliza shule na kuwa kukosekana kwa chakula kwa watu ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.


Diwani wa Kata Nyugwa, Ndozi Manual akizungumza kwa niaba ya wananchi wa vijiji hivyo aliwata wananchi kuyatunza mashamba darasa hayo kwa kuwa ni mali yao baada ya kuletewa na COSTECH na OFAB na kuwa baada ya kupata mbegu bora wanatarajia kupata mavuno mengi.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, alisema kuwa kazi kubwa ya COSTECH ni kuishauri serikali katika masuala yote yanayohusu  Sayansi na Teknolojia na kusimamia tafiti zote za kisayansi katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha matunda ya tafiti hizo yanawafikia walengwa.

Alisema mbegu hizo walizozikabidhi ikiwamo ya mahindi yanayostahimili ukame ya Wema 2109 na mhogo zimefanyiwa utafiti na zitapandwa katika mashamba darasa na baadae kusambazwa kwa wakulima wengine ili kuondoa changamoto ya kukosekana kwa mbegu bora kutokana na wakulima kukabiliwa na mbegu ambazo zilikuwa na magonjwa. 

Dk. Bakari aliwataka wakulima na maofisa ugani kuyatunza mashamba darasa hayo ili kazi kubwa iliyofanyika isipotee bure na baada ya muda mfupi watarudi kuangalia maendeleo yake.

Shahidi: Mshtakiwa alijaribu kutoroka

Washtakiwa katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa
Washtakiwa katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mfanyabiashara wa madini marehemu, Erasto Msuya wakiwa chini ya ulinzi wa askari wakipelekwa kwenye chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Moshi,n jana  mkoani Kilimanajro. Picha na  Dionis Nyato 
Moshi. Koplo Derick ambaye ni shahidi wa tatu katika kesi ndani ya shauri la mauaji ya bilionea Erasto Msuya, ameiambia Mahakama Kuu Kanda ya Moshi kuwa mshtakiwa wa pili, Shaibu Jumanne alikuwa na afya njema wakati wakimtoa mahabusu na alijaribu kuwatoroka polisi eneo la King’ori mkoani Arusha wakati akiwapeleka askari kuonyesha silaha aina ya SMG alikokuwa ameificha.
Kesi hiyo iliibuka Ijumaa iliyopita wakati shahidi wa 11 upande wa mashtaka, Koplo Seleman Faraji alipotaka kutoa maelezo ya kukiri makosa ya mshtakiwa huyo kama kielelezo.
Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Majura Magafu walipinga kutolewa kwa maelezo hayo yaliyochukuliwa na Koplo Seleman Agosti 16, 2013 akisema mshtakiwa aliteswa na polisi.
Wakili Magafu alidai kuwa mteja wake alimweleza kuwa siku hiyo alikuwa hajakamatwa na Agosti 18 aliteswa na kulazimishwa kusaini maelezo ambayo hayafahamu.
Pia, Wakili Magafu alieleza kuwa baada ya mshtakiwa kuteswa na kuumizwa, polisi waliingiwa hofu kuwa angeweza kufa katika Kituo Kikuu cha Polisi Moshi hivyo Agosti 21, 2013 wakampeleka hospitali.
Akitoa ushahidi wake jana katika shauri hilo, koplo Derick alidai kuwa Agosti 18, 2013 majira ya asubuhi akiwa ofisini kwake aliitwa na afande Chiluba akimtaka kumpeleka mshtakiwa mkoani Arusha.
Shahidi huyo akiongozwa na wakili wa Serikali, Omar Kibwana akisaidiana na Abdallah Chavula, Kassim Nassir na Lilian Kyusa, aliieleza mahakama hiyo mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo kuwa lengo la kumpeleka mshtakiwa Arusha lilikuwa ni kuwaonyesha silaha.
Koplo Derick alidai kuwa mshtakiwa alikuwa katika hali nzuri na alifungwa pingu na kwamba wakiwa kwenye gari walipofika eneo la King’ori kulikuwa na foleni na gari lilipunguza mwendo ghafla mshtakiwa aliruka.
Alieleza kuwa baada ya kuruka kwenye gari alianza kukimbia huku akichechemea hivyo polisi waligonga gari kutoa ishara kwa dereva asimame na walianza kumkimbiza na kumkamata.
Koplo Derick alieleza kuwa baada ya kumkamata afande Chilumba alimuamuru dereva kugeuza gari kurudi Moshi na walipofika walimrudisha mahabusu na kuendelea na majukumu mengine.
Baada ya kumaliza kuongozwa na wakili Kibwana, ilikuwa zamu ya mawakili wa utetezi wakiongozwa na Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emmanuel Safari na John Lundu.
Wakili Ndusyepo: Agosti 18, 2013 ulipangiwa kazi gani?
Shahidi: Nilikuwa nikifanya shughuli nyingine za ofisi ambazo ni za kipelelezi.
Wakili Ndusyepo: Shaibu umemuona mara ngapi?
Shahidi: Nilimuona siku hiyo nilipomtoa Kilimanjaro kwenda Arusha.
Wakili Ndusyepo: Kitu gani kimekufanya umtambue Shaibu?
Shahidi: Kitendo cha kufanya jaribio la kutaka kutoroka chini ya ulinzi wa polisi ni jambo linalohatarisha kazi yangu.
Wakili Ndusyepo: Je, mlifungua taarifa za mshtakiwa Shaibu kutaka kutoroka chini ya ulinzi wa polisi?
Shahidi: Sikumbuki kwani nilikuwa na kiongozi wangu Inspekta Chilumba.
Wakili Ndusyepo: Unakubali kuwa wewe ni shuhuda wa tukio hilo?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili Ndusyepo: Uliandika maelezo ya tukio unalolizungumzia?
Shahidi: Sikufungua.
Wakili Ndusyepo: Kwa nini haukuandika?
Shahidi: Kwa sababu sikuwa peke yangu na zaidi ya yote nilikuwa na incharge (msimamizi) wangu Inspekta Chilumba.
Wakili Ndusyepo: Mahakama hii itaamini vipi kulikuwa na jaribio la kutaka kutoroka?
Shahidi: Mlalamikaji ndiye alitakiwa kuandika maelezo.
Baada ya maelezo hayo Wakili Magafu anaanza kumhoji.
Wakili Majura: Shahidi ieleze mahakama hii umesoma hadi darasa la ngapi?
Shahidi: Hadi darasa la saba
Wakili Majura: Shule gani?
Shahidi: Shule ya Msingi Kizuka.
Wakili Majura: Ulijiunga na jeshi lini?
Shahidi: Mwaka 2007.
Wakili Majura: Unaweza kukumbuka Shaibu alikamatwa lini?
Shahidi: Siwezi kwa sababu sikuwapo siku akikamatwa.
Wakili Majura: Wakati mnamchukuwa mlimtoa wapi?
Shahidi:Tulimtoa lockup (mahabusu) ya polisi.
Wakili Majura: Nani alikwenda kumtoa mahabusu?
Shahidi: Mimi na mwenzangu.
Wakili Majura: Unajua mshtakiwa kutoroka chini ya mikono ya polisi ni kosa la jinai?
Shahidi: Sijui.
Wakili Majura: Kwa hiyo ndiyo maana hukuona umuhimu wa kuandika maelezo ya mshtakiwa kuruka kwenye gari la polisi?
Shahidi: Inspekta Chilumba ndiye alipaswa kuandika maelezo.
Wakili Majura: Mshtakiwa alikuwa amekaa upande gani?
Shahidi: Upande wa kushoto karibu na kebini.
Wakili Majura: Unao uzoefu wa miaka mingapi kusindikiza watuhumiwa kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine?
Shahidi: Karibia miaka 11.
Wakili Majura: Uliwahi kusikia kama mtuhumiwa alichukuliwa kwenda kuhojiwa kutokana na tukio alilolifanya la kutoroka?
Shahidi: Ndiyo
Wakili Majura: Nani alikwambia alihojiwa ?
Shahidi: Inspekta Chilumba.
Wakili Majura: Utakubaliana na mimi hakuna tukio la namna hii lilishawahi kutokea?
Shahidi: Hapana.
Wakili Majura: Lini ulipewa taarifa ya kuja kutoa ushahidi?
Shahidi: Wiki iliyopita.
Wakili Majura: Ulipewa samansi kutoka mahakamani au kwa maneno?
Shahidi: Kwa mdomo.
Wakili Majura: Uliambiwa na nani?
Shahidi: Afande RCO (mkuu wa upelelezi mkoa) Dotto.
Wakili Majura: Alikwambia unakuja kutoa ushahidi kuhusu nini?
Shahidi: Nilijulishwa kuwa nahitajika mahakamani.
Wakili Majura: Nani alikupa taarifa ya kuja kutoa ushahidi wa aliyeruka kwenye gari?
Shahidi: Wakili wa Serikali.
Wakili Majura: Wakili yupi?
Shahidi: Wakili (Abdallah) Chavula.
Wakili Majura: Wakili wa Serikali alijuaje wewe ulikuwa na mshtakiwa kwenye gari?
Shahidi: Sijui yeye alijuaje.
Wakili Majura: Ni kweli hujawahi kuandika statement (maelezo).
Shahidi: Kweli.
Wakili Majura: Nikikwambia ulihusika kumchukua mshtakiwa na kumpeleka kwenye mateso utasemaje?
Shahidi: Siyo mimi.
Wakili Majura: Unasema baada ya kusimamisha gari, mshtakiwa aliruka?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili Majura: Na alikuwa ameumia sana?
Shahidi: Alikuwa ameumia ndiyo, aliumia mguuni na kuchubuka sana.
Wakili Majura: Alikuwa anaweza kutembea mwenyewe baada ya kumkamata?
Shahidi: Tulikuwa tunamshikilia na kumuingiza kwenye gari.
Wakili Majura: Je, aliruka umbali gani mpaka mkamkamata?
Shahidi: Kama mita mia moja hivi.
Wakili Majura: Kwenye gari mlikuwa mnajua ni mshtakiwa wa mauaji ya Erasto Msuya, kweli au si kweli?
Shahidi: Kweli.
Wakili Majura: Ulimwadhibu kidogo?
Shahidi: Hakupigwa.
Wakili Majura: Baada ya yeye kuumia, uliwahi kujua alichukuliwa na kupelekwa kwenye matibabu?
Shahidi: Hapana.
Wakili Majura: Kuna mwenzako mlikuwa naye kwenye gari ambaye aliwahi kuhojiwa, ametoa taarifa za mshtakiwa kuruka kwenye gari?
Shahidi: Mimi sijui.
Wakili Majura: Mtu akikamatwa na kupelekwa kituoni na kuwekwa mahabusu, anawekwa kwenye lockup register (rejista ya mahabusu) lazima usaini, wewe ulisaini?
Shahidi: Ndiyo.
Bilionea Msuya aliuawa Agosti 7, 2013 Mijohoroni wilayani Hai, Kilimanjaro. Kesi hiyo inawakabili washtakiwa saba; Shaibu Said, Sadiki Jabir, Karim Kihundwa, Ally Mussa au Majeshi, Jalila Said na Sharifu Athuman.