Monday, July 31

WAZIRI MKUU AWAASA WATUMISHI WANAOFANYAKAZI VIWANDANI


WAZIRI MKUU  Mhe. Kassim Majaliwa amewasihi Watanzania wanaofanya kazi katika viwanda mbalimbali nchini kufanya kazi kwa bidii na kuwa waaminifu.
Amesema Tanzania imedhamiria kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda hivyo ni vema watakaopata fursa ya ajira katika viwanda hivyo kuwa waadilifu.
Ameyasema hayo Jumapili, Julai 30, 2017 wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha gesi cha Ikama kilichoko wilayani Rungwe.
Waziri Mkuu amesema wakati Serikali ikiendelea kuwakaribisha wawekezaji nchini, wananchi walioajiriwa kwenye maeneo hayo wawe waaminifu.

“Mnatakiwa muwe waaminifu, msibebe kitu chochote ndani ya kiwanda bila ya ridhaa ya wamiliki kwa kuwa mtaonyesha taswira mbaya kwa wawekezaji.”
Amesema uaminifu wao ndio utawezesha Watanzania wengi kupata ajira kwenye viwanda hivyo ambavyo vimejengwa katika maeneo yao.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na kampuni ya TOL Gases, Mhandisi Harold Temu alisema kiwanda kinauwezo wa kuzalisha tani 46 kwa siku.

Alisema gesi inayozalishwa kiwandani hapo ni ya Carbon Dioxide ambayo inauzwa nchini na nchi jirani za Zambia, Malawi, Zimbabwe na Congo.

Mhandisi Temu alisema wateja wakubwa wa gesi hiyo ni viwanda vya kutengenezea soda, bia na pia hutumika katika kuhifadhia chakula na kwenye vifaa vya kuzimia moto.

Mapema Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kuchakata majani ya chai cha Katumba, ambapo alisema Serikali inaimarisha Ushirika wa zao hili ili wakulima waweze kupata tija. 

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa umma wa wilaya ya Rungwe Julai 30, 2017. Kulia ni Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson na kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Mbeya  Mhe. Amos Makalla. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wa kiwanda cha gesi cha TOL Gases Limited kilichopo katika kijiji cha Ikama wilayani Rungwe Baada ya kuwasili kiwandani hapo Julai 30, 2017 Kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana viongozi wa kiwanda cha chai cha Katumba wilayani Rungwe alipowasili kiwandani hapo kukagua shuguli za kiwanda hicho Julai 30, 2017. 
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akitembelea kiwanda cha chai cha Katumba wilayani Rungwe Julai 30, 2017. Kulia ni Mkuu wa mkoa wa Mbeya  Mhe. Amos Makalla na kushoto ni Meneja Uzalishaji wa kiwanda hicho, Bw. Ramadhani Kampasili. 
Waziri Mkuu  Mhe. Kassim Majaliwa akitazama chai iliyosindikwa na kufungashwa tayari kwa kuuzwa wakati alipotembelea kwianda cha chai cha Katumba wilayani Rungwe Julai 30, 2017.  
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Tukuyu Wilayani Rungwe baada ya kutembelea kiwanda cha Chai cha Katumba Julai 30, 2017. 
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Ufundi, Bw. McJohn Mbiri (kulia Kwake) kuhusu mitambo ya kuzalisha gesi ya hewa ya ukaa wakati alipotembelea kiwanda cha TOL Limited kilichopo katika kijiji cha Ikama wilayani Rungwe Julai 30, 2017. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makalla. 
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na wazee wa kijiji cha Busokelo baada ya kuwasili kwenye uwanja wa michezo wa Kandete katika jimbo la Busokelo kuhutubia mkutano wa hadhara Julai 30, 2017. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia ngoma ya asili ya Kimyakyusa iitwayo "Ndigala" baada ya kuwasili kwenye uwanja wa michezo wa Kandete katika jimbo la Busokelo mkoani Mbeya kuhutubia mkutano wa hadhara 
Sehemu ya watumishi wa umma wa wilaya ya Rungwe wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipozungumza nao leo Julai 30, 2017. 

IGP SIRRO AMALIZA ZIARA YAKE MIKOA YA KANDA YA ZIWA KWA KISHINDO


Na Jeshi la Polisi Nchini 

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, amemaliza ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa pamoja na mkoa wa Singida, huku akiacha morali kwa watendaji wa Jeshi hilo hatua ambayo italiwezesha ieshi hilo kufanyakazi zake kwa weledi katika kukabiliana na matishio ya uhalifu na wahalifu. 

IGP Sirro, amefanya ziara hiyo ikiwa ni mkakati wake aliojiwekea tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi hilo kwa lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari na maofisa ili kujua namna wanavyotekeleza majukumu yao ya kazi za Polisi. 

Katika mazungumzo yake IGP Sirro, amewataka askari na maofisa kutimiza wajibu wao kwa kutenda haki na bila uwoga wala kumuonea mtu muhali jambo ambalo litarahisisha upatikanaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu katika jamii. 

Hata hivyo, katika mabaraza ya kuzungumza na askari na maofisa baadhi ya hoja kadhaa ziliibuliwa kwa baadhi ya askari waliopata nafasi ya kutoa mawazo yao, ambapo IGP Sirro aliahidi kuzishughulikia mapema ili kuzidisha morari katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. 

Aidha, katika ziara yake IGP Sirro, alipata fursa ya kukutanana Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama ya mkoa huku masuala kadhaa ya kiusalama na mbinu na mikakati ikijadiliwa katika kamati hizo na kuahidi kutoa ushirikiano utakaowezesha kukabiliana na matishio mbalimbali ya kiuhalifu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akizungumza na baadhi wa  Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Singida, wakati alipofika katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa huo kwa lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari na maofisa wa Jeshi hilo pamoja na kujua changamoto wanazokutananazo wakitekeleza majukumu yao. Picha na Jeshi la Polisi. 

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akizungumza na askari na maofisa wa Jeshi hilo na kuwataka wafanyekazi kwa kutenda haki na kusimamia misingi ya sheria na taratibu, IGP Sirro yupo mkoani Singida kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari na kujua changamoto wanazokutananazo wakitekeleza majukumu yao. Picha na Jeshi la Polisi. 
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akizungumza na kikosi cha Polisi wanawake baada ya kukagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili yake alipowasili mkoani Singida, kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari na kujua changamoto wanazokutananazo wakitekeleza majukumu yao. Picha na Jeshi la Polisi. 

DED ILEJE AINGIA DARASANI KUFUNDISHA



Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ileje Mkoani Songwe, Haji Mnasi akiwa darasani kufundisha wanafunzi huku wanafunzi wakiwa makini kusikiliza nini wanachofundishwa na Mkurugenzi hiyo.
Na Fredy Mgunda,Ileje

Katika hali isiyozoeleke kwa watumishi wengi wa Idara ya Elimu wilayani Ileje mkoani Songwe kwa Mkurugenzi Mtedaji wa Halmsahauri ya wilaya hiyo kwa kuingia kwenye baadhi ya shule za msingi na kufundisha.

Mkurugenzi huyo Ndugu Haji Mnasi ambaye kitaaluma ni mwalimu aliamua kufanya hivyo katika ziara ya kushtukiza aliyoifanya kweye shule za Nyerere,Rungwa na Itumba zilizopo katika kata za Itumba na Isongole Tarafa ya Bulambya.

Akiwa katika shule ya Msingi Nyerere aliweza kufundisha masomo ya Kiiingeriza,Hisabati na Kiswahili, pia aliweza kupima uelewa wa wanafunzi pamoja na kutoa maswali machache ya kuandika.

Ziara hiyo iliweza pia kumfikisha katika Shule ya Msingi Rungwa ambapo aliweza kuzungumza na walimu akiwapa moyo katika kuwapatia elimu bora wanafunzi akiwapa moyo wa utendaji kazi akiwataka kuzingatia maagizo mbalimbali ya serikali.

Pia Mkurugenzi huyo,aliyekuwa amefuatana na mmoja wa viongozi wa Idara ya Elimu Msingi akiwa Rungwa aliweza kuzungumza na mafundi waliokuwa wakiendelea na ujenzi ambapo aliwataka kumaliza kazi kwa wakati wakifuata viwango vinavyotakiwa.

Ziara yake kwa siku hiyo ilishia katika shule ya Msingi Isongole ambako alipata fursaa kufuwatathimini wanafunzi wa Darasa la Saba ambao walikuwa wametoka kumalizia mtihani wa Moko ya Wilaya.

Mara baada ya kumalizia ufundishaji kwa masomo ya Hisabati,Kiswahili na Kiingereza Mkurugenzi huyo aliwapongeza walimu wa shule hiyo kwa jinsi walivyowaanda wanafunzi wao ambao wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Taifa siku chache zijazo.

Walimu kwa upande wao walimpongeza mwajiri wao kwa kuweza kutembelea shule yao na kuzungumza nao wakisema hali hiyo imewapaa ari ya kufanya kazi wakishauri ziara hiyo iendelee na kwa shule zingine

Mwalimu Denis Umbo alisema kuwa ,kitendo cha mwajili wao kuingia darasani hakijawatia moyo wa kufanya kazi tu bali ameitendea haki taaluma yake na kujionea hali halisi ilivyo mashuleni badala ya kusubiri taarifa za mezani.

Si hayo tu yaliyojili katika shule hiyo pia Mkurugenzi alibahatika kuzungumza na wananchi waliokuwa kwenye mkutano ambao pamoja na mambo mengine walitarajia kujadili masuala mbalimbali ya shule likiwemo la chakula cha mchana kwa wanafunzi na taaluma.

Mnasi aliwataka wazazi hao kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano juu ya utoaji elimu bure kwa watoto wote hapa nchini.

TASWIRA MBALIMBALI KUTOKA KISIWANI PEMBA



















JUMUIYA YA WATANZANIA READING- BERKSHIRE YAPATA VIONGOZI WAPYA

Jumuiya ya Watanzania wa Reading {Tanzania Reading - Berkshire Association- } imepata viongozi baada ya kufanyika uchaguzi huru wa kidemokrasia Kwa mujibu wa Katiba yake halali siku ya Jumamosi ya tarehe 29 July 2017 katika jiji la Reading.
Zoezi la Uchaguzi lilisimamiwa kikamilifu Kwa mujibu wa Katiba halali ya Jumuiya na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi 2017 Ndugu Bernard Chisumo pamoja na timu yake chini ya Makamu Mwenyekiti na Kaimu Mwenyekiti Mstaafu Ndugu Hussein Chang'a.
Katika hotuba yake fupi Ndugu Chang'a alisisitiza umuhimu wa wajumbe kuheshimu muongozo wa Jumuiya na kufanya shughuli zote za kwa kufuata muongozo waliojiwekea na kutokukubali kuyumbishwa na watu wachache wenye malengo binafsi.
 *Mgeni rasmi alikua ni Mwenyekiti wa TZUK {Great Britain & Northern Ireland}, Ndugu Abraham Sangiwa. ambaye alisindikizwa na Makamu Mwenyekiti TZUK, Bi. Mariam Seif
Katika wosia wake kwa Watanzania wa Reading Ndugu Sangiwa alisisitiza kuwa na umoja na mshikamano kwa Watanzania wote wanaoishi Reading- Berkshire na kuelezea kwa ufasaha jinsi TZUK inavyofanya shughuli zake kwa kushirikiana na jumuiya zote za mikoa hapa UK.
Ndugu Sangiwa alielezea juhudi mbalimbali zinazofanyika kwa kushirikiana na Jumuiya mbalimbali za Watanzania wanaoishi nje katika nchi mbalimbali duniani kupendekeza sera ya Diaspora kwa pamoja itakayotoa majibu katika masuala mbalimbali yanayowagusa Watanzania Ughaibuni na mchango wao mkubwa kwa nchi yao mama "TANZANIA", unavoweza kuwa katika mfumo utakaoleta manufaa makubwa kwa nchi katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo na huduma kwa jamii.
"Tunahitaji kulinda na kutangaza utamaduni wetu na vivutio vya utalii kwa kuhakikisha vizazi vyetu ughaibuni vinanapata misingi muhimu na mafunzo kuhusu Tanzania. Ni muhimu sana kujenga "Model" itakayofanya TAIFA letu kufaidika na vizazi hivi vitakavokuwa na " Exposure " ya kimataifa katika nyanja mbalimbali zenye manufaa makubwa kwa nchi yetu, alisisitiza Ndugu SANGIWA.

VIONGOZI WAPYA WALIOCHAGULIWA KUONGOZA JUMUIYA YA WATANZANIA READING - BERKSHIRE NI KAMA IFUATAVYO:

MWENYEKITI NI NDUGU JOE J.E WARIOBA, MAKAMU MWENYEKITI  NI Bi. LAURA BANDUKA, KATIBU MKUU NI  Bi. Raya Walker, NAIBU KATIBU {KAIMU}, Bw.   Peter Owino, MTUNZA HAZINA ni  Bi. FLORA DICKSON, wakati MTUNZA HAZINA MSAIDIZI ni   Ndugu Elijah Mwamunyange.

WAJUMBE SITA NI Peter Owino, MOHAMMED Upete, Paul Onyango, Geofrey Mumu, Evelyne Furzei na Dorine White, wakati Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu (AUDITOR) ni Eliud Mwijarubi. 
Pia kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania Diaspora Community United Kingdom of Great Britain &  kila jumuiya za matawi zinatakiwa kuchagua wawakilishi wawili (2) katika Baraza (The Council) la Tanzania Diaspora UK. Wajumbe watachaguliwa hapo baadae.
Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza sana katika hatua hio kubwa na ya muhimu katika ujenzi wa Umoja wa Watanzania UK
Asanteni sana

Uongozi: TA READING -  BERKSHIRE*Kwa kushirikiana na
Tanzania Diaspora Community/Association - United Kingdom of Great Britain & Northern Ireland

 Makamu mwenyekiti mpya Bi. Laura Noe akinadi sera zake
 Bi. Raya Walker akijinadi na kuomba kura kwa wanachama
 Hussein Chang'a

 Katibu Bi. Raya Walker na Mwenyekiti Ndugu Joe J.E Warioba wakibadilishana mawazo
 Ndugu Mohamed Upete akitimiza haki yake ya kupiga kura
 Makamu na Kaimu Mwenyekiti Mstaafu ndg Hussein Chang'a akitimiza haki yake ya kupiga kura kama mwanachama hai
 Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TA READING- BERKSHIRE Ndugu Bernard Chisumo pamoja na Katibu wa TZUK Ndugu Gerald Lusingu wakifuatilia mambo kadhaa katika Mkutano Mkuu wa Jumuiya.
 Masanduku ya kura yakisubiri kula kura 

 Wajumbe na Wanachama wakiwa makini
 Meza kuu na Wajumbe na Wanachama
 Makamu na Kaimu Mwenyekiti Mstaafu Ndugu Hussein Chang'a akimpongeza Mwenyekiti Mpya wa TA Reading- Berkshire aliyechaguliwa Ndugu Joe J.E Warioba. Kushoto ni Katibu mpya Bi Raya Walker na kulia ni Makamu mwenyekiti mpya Bi. Laura Noel
 Ndugu Hussein Chang'a Makamu na Kaimu Mwenyekiti Mstaafu akikabidhi Uongozi Mpya taarifa zote muhimu za Jumuiya kwa Katibu Mpya Bi. Raya Walker
Mtunza Hazina Bi. Flora Dickson akimkabidhi ripoti ya Fedha na Akaunti ya Jumuiya Mwenyekiti Mpya wa TA READING BERKSHIRE Ndugu Joe J.E Warioba
 Wanakamati na Viongozi wa wapya wa Jumuiya
 Viongozi wa TZUK na TA READING BERKSHIRE
Baadhi ya Viongozi wa Kamati ya Uchaguzi TA READING- BERKSHIRE na Uongozi wa TZUK

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MHANDISI RAMO MAKANI, AMUAGIZA MKUU WA WILAYA YA MUHEZA KUSHUGHULIKIA MGOGORO WA HIFADHI YA MSITU WA DEREMA WILAYANI HUMO


Na Hamza Temba - WMU - Muheza, Tanga

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga kukutana na wakulima 879 wa vijiji vitano katika Tarafa ya Amani Wilayani humo kwa ajili kufanya uhakiki wa malipo ya fidia ya mazao waliyolipwa na Serikali ili kupisha eneo la hifadhi ya msitu wa Derema.

Mhandisi Makani ametoa agizo hilo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Msasa IBC, Tarafa ya Amani, Wilayani Muheza kufuatia malalamiko ya wananchi hao kupunjwa malipo yao wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 15 baina Serikali na wananchi wa vijiji hivyo vya Kisiwani, Kwemdim, Msasa IBC, Antakae na Kambi.

Akisoma risala ya wakulima hao mbele ya Naibu Waziri Makani, Mwenyekiti wa Kamati ya wakulima hao, Mohammed Rama Shesha alidai kuwa jumla ya wakulima 1,128 wa vijiji hivyo wanailalamikia Serikali kwa kuwalipa viwango pungufu vya malipo ya fidia ya mazao yao tofauti na viwango vilivyolipwa na Serikali mwaka 2002 kupitia mradi wa FINIDA. Aidha, alidai kuwa kuna baadhi ya mazao pia hayakulipiwa kabisa fidia hizo.

Akizungumzia viwango vya fidia hizo Shesha alisema wananchi walilipwa Shilingi 28,800 kwa mche mmoja wa iliki na Shilingi 11,000 kwa mche mmoja wa mgomba. Alidai viwango hivyo vilibadilika kuanzia mwaka 2005 ambapo walilipwa Shilingi 3,315 kwa kila mche mmoja badala ya Shilingi 5,100 kama ilivyoainishwa kwenye viwango vya Serikali hivyo akaomba walipwe kiasi kilichobakia cha shilingi 1,785.

Akitolea ufafanuzi wa malalamiko hayo, Naibu Waziri Makani alisema idadi kamili ya wananchi waliohakikiwa katika eneo hilo ni 879 na sio 1,128 kama alivyodai mwenyekiti huyo. Aidha, alisema viwango vilivyotumiwa kuwalipa wananchi hao mwaka 2002 sio vya Serikali na kwamba vilitumiwa na mradi wa FINIDA uliofadhiliwa na Serikali ya Finland kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wa mpakani na hifadhi hiyo ili kufanikisha zoezi la kuanisha mpaka wa hifadhi hiyo na kusaidia Serikali kutimiza azma ya kuhifadhi eneo hilo.

Alisema viwango halali vya Serikali vilivyopo kisheria kwa ajili ya kulipa fidia ya mimea hiyo ni kuanzia Shilingi 5,100 kwa kiwango cha juu kwa mmea uliokoma kufikia kiwango cha uzalishaji, Shilingi 3,315 kwa mmea wenye mwaka mmoja na Shilingi 2,040 kwa mmea wenye mwezi mmoja. Alisema viwango vingine vya malipo kwa kiwango cha chini ni Shilingi 204, Shilingi 102 na Shilingi 51.

Alisema Serikali iliamua kulipa kiwango cha Shilingi 3,315 kwa mazao yote ikiwemo yale yaliyostahili kulipwa kiwango cha chini kabisa cha Shilingi 51 ili kuweka uwiano na kurahisha zoezi hilo la malipo. Alihoji kama kuna mwananchi yeyote aliyelipwa chini ya kiwango hicho japokuwa kulikuwepo na wengine mazao yao yalistahili kulipiwa viwango hivyo, hakuna aliyejitokeza.

Kufuatia ufafanuzi huo aliuagiza uongozi wa Wilaya ya Muheza kutumia kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo Jumatatu kuonana na wakulima hao ili kuhakiki malipo yao na hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kama kuna yeyote aliyezulumiwa apewe haki yake. 

"Kwa wale ambao tayari wana kumbukumbu zao vizuri wazilete mbele ya Serikali, kupitia wao pengine tunaweza kupata picha ya jumla pengine kulikua na mapungufu kwenye malipo. Kuanzia jumatatu ijayo Mhe. DC tulitekeleze hilo la kukusanya nyaraka kwa wale walizonazo tuweze kuzilinganisha na zile tulizokua nazo Serikalini tujadiliane nao kwamba ni kitu gani kimebaki tofauti katika maeneo yale yale mliyofanyiwa uhakiki", alisema Mhandisi Makani.

Alisema kwa wale ambao wamepoteza nyaraka zao za malipo wataandaliwa utaratibu maalum wa uhakiki kwa kuwa kumbukumbu zote za malipo zipo kwenye Kompyuta za halmashauri ya Wilaya ya Muheza.

Alisema lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inamaliza kabisa migogoro ya ardhi nchini. “Tutahakikisha tunaboresha zaidi usimamizi wa uhifadhi wa rasilimali zetu za misitu, wanyamapori na nyinginezo kuhakikisha migogoro hiyo inapungua kwa kasi kuelekea kwenye sifuri, zero rate", alisema Makani.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanaisha Tumbo alisema, Serikali ya Wilaya imepokea maelekezo hayo na itayafanyia kazi na kwamba maafisa wa Halmashauri watafika katika kila kijiji siku ya Jumatatu na Jumatano kwa ajili ya kuendesha zoezi hilo la uhakiki.

Akizungumzia zoezi la fidia Mkuu huyo wa Wilaya alisema pamoja na wananchi hao kulipwa fidia za mazao yao ambayo yalilipwa kwa awamu tatu, asilimia 50 mwaka 2005, asilimia 25 mwaka 2006 na asilimia 25 mwaka 2008, pamoja na asilimia 23 kama fidia ya ucheleweshaji wa deni, Serikali pia itawapa maeneo ya fidia ambapo kila mwananchi aliyeathirika eneo lake atapewa ekari tatu.

Alisema eneo ambalo limeanishwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi hao ni lililokuwa shamba la mkonge Kibaranga ambalo lina ukubwa wa hekta 1370 sawa na ekari 3425 na lilikua likimilikiwa na Bodi ya Mkonge, eneo hilo lilitolewa tamko ya kufutiwa umiliki wake na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli mwezi Julai, 2016.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (katikati), akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Msasa IBC wilaya ya Muheza mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili kutatua mgogoro wa hifadhi ya msitu wa Derema. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanaisha Tumbo. 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (katikati), akimuonesha mwenyekiti wa kamati ya wakulima wa vijiji vitano vya tarafa ya Amani, Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, Mohammed Ramadhani Shesha viwango halali vya serikali vya kulipia fidia za mazao kwa wananchi waliondolewa katika eneo la hifadhi ya msitu wa Derema wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo jana kwa ajili ya kutatua migogoro wa hifadhi hiyo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanaisha Tumbo.  
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia), akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Msasa IBC wilaya ya Muheza mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili kutatua mgogoro wa hifadhi ya msitu wa Derema.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani, (wa tatu kushoto), akiangalia eneo la Msitu wa hifadhi ya Derema na viongozi wa wilaya ya Muheza Muheza wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo jana kwa ajili ya kutatua mgogoro wa hifadhi hiyo. 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia), akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Msasa IBC wilaya ya Muheza Mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili ya kutatua mgogoro ya hifadhi ya msitu wa Derema. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kushoto), akimuonesha mwenyekiti wa kamati ya wakulima wa vijiji vitano vya tarafa ya Amani, Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, Mohammed Ramadhani Shesha (kulia) viwango halali vya serikali vya kulipia fidia za mazao kwa wananchi waliondolewa katika eneo la hifadhi ya msitu wa Derema wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo jana kwa ajili ya kutatua migogoro wa hifadhi hiyo.