Tuesday, November 14

Mbarawa amjia juu Saada Mkuya


Serikali imemjia juu waziri wa zamani wa Fedha, Saada Mkuya kwa kutoa mapendekezo ya kutaka ajira kwa shirika la mawasiliano la simu kwa upande wa Zanzibar ziwe kwa Wazanzibar.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema alitegemea hoja ya aina hiyo ingezungumza na watu vijijini huko Pemba au vijiweni huko darajani Zanzibar na siyo Mkuya.
Profesa Mbarawa aligeuka mbogo leo Jumatatu jioni wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia Muswada wa Shirika la Mawasiliano wa 2017, uliowasilishwa na Profesa Mbarawa.
“Utaratibu wa ajira TTCL ni Mtanzania yeyote anafanya kazi TTCL. Tunachoangalia sisi muhimu ni uwezo wa mtu na sifa za mtu. Jambo alilolisema Saada Mkuya limenisikitisha sana,” amesema.
“Sikutegemea maneno hayo yangetoka kwa kiongozi kama Saada ambaye alikuwepo serikalini. Hasa kwa kiongozi ambaye ana uzoefu mkubwa,” amesema Profesa Mbarawa na kuongeza kuwa;
“Nilitegemea mawazo au maoni kama yale yazungumzwe na watu wa kijijini kule Pemba. Nilitegemea mawazo kama yale yazungumzwe na watu wa kijiweni pale Darajani,”
“Nilitegemea yeye kama kiongozi na sisi kama Tanzania katika kujenga umoja wetu tuseme kila Mtanzania afanye kazi mahali popote Tanzania,”
“Mheshimiwa Naibu Spika hivi tunavyoongea leo, Meneja wa TTCL Zanzibar ni Mzanzibar anaitwa Mohamed Mohamed. Meneja wa TTCL Pemba ni Mnzanzibar anaitwa Ngwali Hamis,”
“Naomba nimpe taarifa mheshimiwa Saada ambaye hazijui kiutendaji.  Mtendaji Mkuu wa TTCL mwaka 2010 hadi 2012 alikuwa Injinia Said Ameir ni Mzanzibar,”
“Sasa sikutegemea nasema ni kitu kimeniuma sana. Nilitegemea kama Mtanzania unatoka Lindi kama kuna fursa TTCL Zanzibar unaenda. Kama Mzanzibar ameona fursa Kibondo aende.”
“Hii ndio Tanzania tunayoitaka. Hii ndio Tanzania ambayo Watanzania kule nje wanaitaka. Nikienda zaidi TTCL tuna TTCL Pesa ina watendaji watano waandamizi. Watatu ni wanzanzibar”
Jitihada za Saada kutaka kumpa Profesa Mbarawa taarifa ziligonga mwamba baada ya Naibu Spika kumweleza kuwa kikanuni waziri akiwa amesimama kwa hatua ya jana, hakuna taarifa.

Dk Shika asema nyumba za Lugumi bado zinahitajiwa na kampuni yake



Dar es Salaam. 'Bilionea' wa nyumba za Lugumi, Dk Louis Shika ameachiwa na kwenda kupanda daladala kuelekea nyumbani huku akisema mpango wake wa kununua nyumba za Lugumi uko palepale.
Baada ya kuachiwa na polisi leo Jumanne jioni amesema kwamba bado mpango wake wa kununua nyumba hizo uko palepale.
Amesema anachosubiri sasa ni fedha kuingizwa kwenye akaunti yake na kulipa asilimia 25 anayodaiwa.
"Siku nikipeleka fedha nataka Yono na TRA waite waandishi wa habari waone na wautangazie umma," amesema.
Amesema vyombo vya habari vimetoa taarifa zake lakini vitaumbuka siku akienda kupeleka fedha hizo.
Ameendelea kusisitiza kwamba nyumba hizo zinahitajiwa na kampuni yake ambayo hakuitaja.
Njiani wakati akielekea kwenye kituo cha daladala cha Mnazi Mmoja, Dk Shika alikuwa kivutio kwa watu aliokuwa akipishana nao.
Alipopanda daladala la Tabata Mawenzi, kondakta alimkaribisha kwa kumweleza karibu mzee Shika.
Kauli hiyo iliwaamsha abiria ambao walikuwa na hamu ya kumwona.
Dk Shika alipanda daladala na kusimama huku akionyesha tabasamu lisiloisha.

Vijana wasema Jenerali wa jeshi hana nguvu zozote Zimbabwe

Jenerali wa jeshi la Zimbabwe Constantino ChiwengaHaki miliki ya pichaAFP
Image captionJenerali wa jeshi la Zimbabwe Constantino Chiwenga
Vugu vugu la vijana wa chama tawala cha Zimbabwe limemkosoa jenerali wa jeshi mwenye cheo cha juu zaidi nchini humo kufuatia kauli aliyoitoa kwamba jeshi linajiandaa kuingilia kati kumaliza mzozo wa ndani wa chama tawala cha Zanu-Pf..
Ameambia vyombo vya habari mjini Harare kwamba mkuu huyo wa jeshi haungwi mkono na jeshi lote.
Tayari chama cha upinzani nchini Zimbabwe MDC kimepuuzilia mbali kauli hiyo ya jenerali wa jeshi kikimtaja kuwa asiye na nguvu zozote.
Matamshi hayo yanajiri kufuatia hatua ya Chimwenga kutishia kufanya mapinduzi iwapo chama cha Zanu-PF hakitasita kuwafurusha wapiganaji wa uhuru katika chama hicho ambao wametofautiana na rais Robert Mugabe na mkewe Grace Mugabe.
Msemaji wa MDC Kuraoune Chihwaye alinukuliwa akisema:
''Hana nguvu zozote kumzuia Grace kuwatukana wapiganaji wa uhuru wa zamani''.
Rais Robert Mugabe na mkewe Grace MugabeHaki miliki ya pichaAFP
Image captionRais Robert Mugabe na mkewe Grace Mugabe
Jumatatu, jeneral Constantino Chiwenga alisema kuwa mvutano juu ya askari wa zamani lazima usitishwe.
Kauli hiyo ilipokelewa na wengi kama iliyomlenga Emmerson Mnangagwa, ambaye alifutwa kazi kama makamu wa rais wa Zimbabwe wiki iliyopita .
Taarifa zilizotolewa kwenye mitandao ya kijamii ya habari zinaelezea kuwa magari ya kivita yalionekana yakielekea katika mji mkuu Harare.
Sasa inadhaniwa kuwa ni magari ya kivita yanayosafiri kutoka kwenye kambi za kijeshi kuelekea kwenye kambi ya walinzi wa rais nje ya mji mkuu.

HRW inadai wafanyikazi wa nyumbani kutoka Tanzania wananyanyaswa Uarabuni

HRW inadai wafanyikazi wa nyumbani kutoka Tanzania wananyanyaswa UarabuniHaki miliki ya pichaHRW
Image captionHRW inadai wafanyikazi wa nyumbani kutoka Tanzania wananyanyaswa Uarabuni
Mamlaka nchini Tanzania imezuia uzinduzi wa ripoti kuhusu unyanyasaji wa wafanyikazi wanawake kutoka taifa hilo wanaofanya kazi katika mataifa ya Uarabuni.
Shirika la Human Wrights Watch limedai katika matokeo yake kwamba wafanyikazi wa nyumbani kutoka nchini Tanzania walikuwa wakibakwa , kuteswa na kulipwa mishahara duni na waajiri wao katika mataifa ya Uarabuni.
Ripoti yenye kurasa 100 inayodai kuteswa kwa wafanyikazi wa nyumbani wa Tanzania nchini Oman na muungano wa mataifa ya Emirata UAE ilitarajiwa kutolewa leo kwa waandishi wa habari mbele ya waathiriwa lakini hilo halikufanyika.
Katika hatua isiokuwa ya kawaida ,afisa mmoja kutoka shirika linalofadhiliwa na serikali la Sayansi na Teknolojia COSTEC William Kindekete alifutilia mbali mkutano huo katika mji mkuu wa Dar es Salaam akisema kuwa wanaharakati wa shirika hilo la haki za kibinaadamu hawakufuata sheria katika kufanya utafiti wao.
Hatahivyo matokeo ya utafiti huo wa HRW unaonyesha kuwa takriban wanawake 50 walihojiwa wakati wa utafiti huo ambao wanadai kwamba walilazimishwa kufanya kazi kwa kati ya saa 15 na 21 kwa siku huku wakipokonywa pasipoti zao na waajiri wao punde tu walipowasili katika mataifa hayo.
Afisa wa shirika la Human Rights Watch
Image captionAfisa wa shirika la Human Rights Watch
Ripoti hiyo ilibaini zaidi kwamba zaidi ya nusu yao hawakulipwa huku wengine wakisema kuwa hawakulipwa kabisa.
Wawili kati ya watano walidai kupigwa mbali na kunyanyaswa kijinsia.
Ripoti hiyo ya HRW pia inasema kwamba balozi za Tanzania katika eneo la Ghuba hazikutoa usaidizi wowote kwa waathiriwa wakati walipotaka usaidizi .
Juhudi za kupata majibu kutoka kwa serikali ya Tanzania hazikufanikiwa kwa kuwa maafisa wengi hawakuwa tayari kuzungumzia swala hilo.

TTCL kufutwa na kuja shirika jingine

Dodoma. Serikali iliwasilisha Muswada wa Sheria ambao unaiua rasmi Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na kuanzisha shirika jipya la mawasiliano Tanzania ambalo litamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100.
Muswada huo, umewasilishwa bungeni  leo Jumanne na  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa huku wabunge wakipinga baadhi ya vifungu vya muswada huo.
Akiwasilisha muswada huo, Profesa Mbarawa amesema madhumuni yake ni kuanzisha shirika hilo kwa ajili ya kulinda usalama wa nchi, kukuza uchumi na kutoa huduma kwa jamii.
Profesa Mbarawa amesema sheria hiyo mpya itaiwezesha TTCL kutekeleza majukumu yake kama shirika la umma la mawasiliano likijulikana kama Tanzania Telecommunication Corporation.
Amesema mambo muhimu ya kuzingatiwa katika muswada huo ni kuwa unakwenda kuifuta TTCL na kuanzisha shirika jipya.
Sheria hiyo ambayo itaumika Tanzania bara na Zanzibar, ilipendekeza muundo wake na mtendaji mkuu na wajumbe watano ambapo  upande wa Tanzania Zanzibar utakuwa na mjumbe mmoja.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, inaelekeza kwamba ili mtu awe na sifa ya kuteuliwa kuwa mkurugenzi mkuu ni lazima awe na uzoefu wa miaka nane katika ngazi ya juu ya utawala.
Hata hivyo wabunge waliungana kutaka Zanzibar iwe na wajumbe wawili badala ya mmoja katika bodi ya wakurugenzi na wakataka pia na uzoefu wa mtendaji mkuu uwe miaka mitano badala ya saba.
Mbali na suala la uwakilishi wa Zanzibar, lakini wabunge hao wa CCM na wale wa upinzani, waliungana pia kutaka waziri asiwe na madaraka makubwa ya kuingilia uendeshaji wa shirika hilo.
Wabunge karibu wote waliochangia pamoja kambi rasmi ya upinzani bungeni, wakapendekeza Zanzibar ipewe nafasi mbili kati ya tano badala ya moja, ili kuleta sura halisi ya muungano.
Hata hivyo, Naibu Spika Dk Tulia Ackson alitahadharisha mwelekeo wa mjadala huo akisema hilo si shirika la kwanza la muungano, hivyo wasije wakaanzisha utaratibu mpya kwenye mashirika.

Viongozi wa taasisi ya mikopo watiwa mbaroni


Dodoma. Viongozi wa  Taasisi ya Kusaidia Jamii ( TSSF) ambayo ilitangaza kuwa inatoa mikopo ya elimu ya juu wamekamatwa na polisi baada ya kugundulika kuwa ni matapeli.
Wakurugenzi hao wamekamatwa leo Jumatatu jioni mara tu baada ya mkutano wa waandishi wa habari na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha wa kuelezea kuhusu uchunguzi uliofanyika baada ya Mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Cosato Chumi kuomba mwongozo bungeni.
Chumi ametaka ufafanuzi kuhusu uhalali wa taasisi hiyo baada ya kutangaza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kulipa Sh 30 000 kama ada ya maombi ya kusajiliwa kuomba mkopo.
Hata hivyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema  Serikali haitambui taasisi hiyo na kuahidi kufanya uchunguzi.
Akizungumza leo Jumanne, Ole Nasha amesema baada ya uchunguzi huo wamebaini kuwa taasisi hiyo haina uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi 50,000 ambao ilitangaza kutoa.
Amesema katika mahojiano na taasisi hiyo viongozi hao walisema kuwa fedha za kuwakopesha wanafunzi hao watazipata kutoka nje ya nchi baada ya kupeleka kiasi cha fedha.
Hata hivyo, amesema mkataba wa taasisi hiyo na wafadhili hao unaonyesha kuwa wamefikia makubaliano ya kufanya utafiti wa jinsi wanavyoweza kukusanya fedha na si kuwapa fedha kwa ajili ya kutoa mikopo.
Amesema tayari taasisi hiyo imekusanya fedha kwa wanafunzi 600 na imepeleka wanafunzi 198 katika vyuo mbalimbali nchini kwa makubaliano ada zao wangelipa Desemba mwaka huu.
Hata hivyo, amesema hakuna uthibitisho kama wana fedha kweli za kuwalipia wanafunzi hao ada ingawa wanadai kuwa katika akaunti zao za benki wana fedha kati ya Sh 600 milioni na 700 milioni.
Amesema kufuatia hilo wanaagiza vyombo vya dola kuchunguza jambo hilo na wakati wakifanya hivyo ni marufuku kwa vyuo kuwapokea wanafunzi wanaopewa mikopo na taasisi hiyo.
Pia ameagiza akaunti zao zote kufungiwa hadi hapo watakapomaliza uchunguzi sambamba na taasisi hiyo kutojihusisha na shughuli yoyote.
Baada ya kumaliza mkutano huo polisi kutoka makao makuu ya polisi waliingia ndani ya ukumbi wa mkutano na kuwaeleza wako chini ya ulinzi.
Polisi hao mmoja akiwa na sare na mwingine akiwa na nguo za kiraia waliwakamata na kuondoka nao.

Serikali, mabenki kupiga mnada mali za Rwigara


Familia ya Rwigara iliyokuwa na ukwasi mkubwa wa mali nchini, siku chache zijazo huenda ikajikuta haina makazi ikiwa mamlaka zitaendelea na mpango wa kupiga mnada mali zao ili kupata faranga 5 bilioni (dola za Marekani 6 milioni) inazodaiwa.
Mamlaka za Rwanda zinawashutumu kina Rwigara kwa ukwepaji kodi na huenda jengo la kifahari lililopo eneo la Kiyovu, Kigali likaorodheshwa kuwa miongoni mwa mali za kukamatwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo, ikiwa ni nyongeza kwa kampuni ya sigara ya Premier Tobacco, ardhi, magari na mali nyingine.
"Ikiwa watashindwa kulipa kodi hadi mwishoni mwa Novemba, tutaanza kuweka mali zao kwenye mnada," amesema Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kodi ya Rwanda (RRA), Richard Tusabe.
Tusabe aliongeza kwamba mnada huo utasitishwa tu ikiwa akina Rwigara watakuja hapa na mpango unaoeleweka wa kulipa deni.
Vyanzo kutoka ndani ya sekta ya fedha vimeliambia gazeti la The EastAfrican kwamba benki zilizoikopesha familia ya Rwigara zinatarajia kukamata mali za familia hiyo na kuziuza kwa mnada.
Lakini familia hiyo imesisitiza kwamba mashtaka dhidi yao yamechochewa kisiasa na yana lengo la kuwanyamazisha ili wasiendelee kuikosoa na hivyo kuwafilisi.
Katika kikao cha mahakama mwezi uliopita, mwakilishi wa familia hiyo ya wafanyabiashara Anne Rwigara, dada wa Diane Rwigara aliyekosa sifa za kugombea urais Agosti, aliwaambia majaji kuwa maofisa wa mamlaka ya mapato walijaribu kumlazimisha kutia saini mpango wa malipo ambayo aliona ni vigumu kutekeleza.

Kigali, Rwanda. Familia ya Rwigara iliyokuwa na ukwasi mkubwa wa mali nchini, siku chache zijazo huenda ikajikuta haina makazi ikiwa mamlaka zitaendelea na mpango wa kupiga mnada mali zao ili kupata faranga 5 bilioni (dola za Marekani 6 milioni) inazodaiwa.
Mamlaka za Rwanda zinawashutumu kina Rwigara kwa ukwepaji kodi na huenda jengo la kifahari lililopo eneo la Kiyovu, Kigali likaorodheshwa kuwa miongoni mwa mali za kukamatwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo, ikiwa ni nyongeza kwa kampuni ya sigara ya Premier Tobacco, ardhi, magari na mali nyingine.
"Ikiwa watashindwa kulipa kodi hadi mwishoni mwa Novemba, tutaanza kuweka mali zao kwenye mnada," amesema Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kodi ya Rwanda (RRA), Richard Tusabe.
Tusabe aliongeza kwamba mnada huo utasitishwa tu ikiwa akina Rwigara watakuja hapa na mpango unaoeleweka wa kulipa deni.
Vyanzo kutoka ndani ya sekta ya fedha vimeliambia gazeti la The EastAfrican kwamba benki zilizoikopesha familia ya Rwigara zinatarajia kukamata mali za familia hiyo na kuziuza kwa mnada.
Lakini familia hiyo imesisitiza kwamba mashtaka dhidi yao yamechochewa kisiasa na yana lengo la kuwanyamazisha ili wasiendelee kuikosoa na hivyo kuwafilisi.
Katika kikao cha mahakama mwezi uliopita, mwakilishi wa familia hiyo ya wafanyabiashara Anne Rwigara, dada wa Diane Rwigara aliyekosa sifa za kugombea urais Agosti, aliwaambia majaji kuwa maofisa wa mamlaka ya mapato walijaribu kumlazimisha kutia saini mpango wa malipo ambayo aliona ni vigumu kutekeleza.

Polisi yamwachia Dk Shika


Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefikia uamuzi wa kumuachia  Dk Louis Shika ‘bilionea wa nyumba za Lugumi’ baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kujidhamini yeye mwenyewe baada ya kukosa mtu yeyote aliyejitokeza kwenda kutaka kumwekea dhamana.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Novemba 14, Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema “uchunguzi wa tuhuma dhidi yake unaendelea lakini mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyefika kutaka kumwekea dhamana, yaani anaishi kama mtu wa nyikani.”
Mambosasa ameongeza, “nimeagiza watendaji wangu wamwachie kwa dhamana yaani ajidhamini yeye mwenyewe na awe anakuja kuripoti,” amesema Mambosasa
Kamanda huyo ametoa kauli hiyo mara baada ya Mwananchi kumtafuta kutaka kujua hatima ya Dk Shika ambaye ameshikiliwa tangu Novemba 9 akituhumiwa kuvuruga mnada wa nyumba za kifahari za mfanyabishara Said Lugumi
Dk Shika tangu siku hiyo amekuwa gumzo sehemu mbalimbali kutokana na kile alichokifanya siku ya mnada alipokuwa akipandisha bei dhidi ya washindani wake na moja ya kauli zake zinaendelea kutumika hadi sasa ni ‘Mia 900 itapendeza.’

Masha aiacha Chadema


Aliyekuwa mwanachama CCM, ambaye baadaye alihamia Chadema, Lawrance Masha amejivua uanachama katika chama hicho akidai  upinzani wa sasa umeridhika na hali ya kuendelea  kuwa wakosoaji ili kukisaidia chama tawala kujirekebisha.
Pia amesema, “Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa upinzani wa sasa nchini hauna nia wala sababu ya kutafuta fursa ya kuunda Serikali kupitia falsafa, sera na uongozi mbadala.”
Masha ameeleza hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo Jumanne Novemba 14.
Masha ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, katika Serikali ya awamu nne, amesema upinzani hauwezi kutegemea kushika dola kwa kutegemea madhaifu ya CCM badala uwezo wake kama mbadala.
Amesema  kazi kubwa ya chama chochote cha siasa ni kujiandaa na hatimaye kushinda uchaguzi ili uweze kuunda na kuendesha Serikali na dola kama njia ya maono yaliyo kwenye ilani ya uchaguzi kwa lengo la kuleta maendeleo na ustawi katika nchi.
“Nilijivua uanachama CCM mwaka 2015 na kujiunga Chadema nikiamini nitashiriki kukifanya chama hiki kikomae na kufikia hatua ya kuwa mbadala kifalsafa, kisera na uongozi. Hata hivyo uzoefu wangu wa miaka miwili ndani ya Chadema umenionyesha chama hiki kina safari ndefu kisiasa na kuwa chama mbadala cha kuunda Serikali.
“Mpaka sasa chama hiki kimendelee kujikita katika kukosoa na kuonyesha madhaifu ya Serikali hasa Rais John Magufuli binafsi. Natambua kwamba kukosoa ni kazi muhimu ya chama cha upinzani, kazi hii haikifanyi chama kuwa mbadala cha kuunda Serikali,”amesema Masha katika taarifa hiyo.
Masha ambaye aliwani kuwa Mbunge wa Nyamagama mwaka 2005-10, amesema siyo sahihi kwa vyama vya upinzani kuwekeza katika kumpinga Rais Magufuli ambaye ni mkuu wa nchi pekee anayetekeleza kwa vitendo mambo ambayo upinzani ilikuwa ikiyapigia kelele kwa miaka mingi, na kuwashinda viongozi wa CCM  waliomtangulia.
“Nimejivua uanachama kuanzia leo, nina imani uamuzi huu utanipa fursa ya kutafakari kwa kina safari yangu ya kisiasa ndani ya nchi hii. Nawashukuru viongozi wa Chadema kwa miaka miwili ya kufanya kazi pamoja nao nawatakiwa kila la kheri,” amesema Masha ambaye alikuwa ni miongoni mwa watu walioshirikia kampeni za uchaguzi za mwaka 2015 kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Vifaru vyarandaranda jijini Harare


Hali ya sintofahamu imejitokeza katika jiji la Harare baada ya vifaru kuonekana vikielekea mjini ambako vilitumika kufunga barabara kubwa za kuingia na kutoka nje.
Aidha vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kwamba msafara mkubwa wa wanajeshi wenye silaha ulizingira kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali ZBC. Kadhalika Shirika la Reuters limesema vifaru vinne vilionekana mitaani.
Baadhi ya watu walianza kusambaza picha za magari ya kijeshi kwenye mitandao ya kijamii. Baadhi walisema (mapinduzi) lakini gazeti la Independent la Uingereza limeshindwa kuthibitisha ukweli wa picha hizo na msafara wa magari hayo ya kijeshi.
Hata hivyo, tukio hilo limekuja siku moja baada ya Mkuu wa Jeshi Jenerali Constantino Chiwenga kutishia kuingilia kati na akaagiza “kusitishwa” mara moja ufukuzaji wanachama kutoka chama cha Zanu PF cha Rais Robert Mugabe kufuatia kufutwa kazi kwa Makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa.
Jenerali Chiwenga akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliohudhuriwa na walau makamanda 90 wa ngazi ya juu kwenye makao makuu ya jeshi, Jumatatu alisema: "Ufukuzaji huu unaolenga wanachama wa chama wenye uhusiano na harakati za ukombozi lazima ukome mara moja."
Ripoti zinasema kwamba jeshi limekuwa likimuunga mkono Mnangagwa kumrithi Mugabe, 93, lakini mke wa mzee huyo Grace ameibuka na kuwa mshindani mwenye nafasi kubwa.
Mnangagwa alifukuzwa serikalini na kwenye chama wiki iliyopita baada ya kushutumiwa kwamba alikuwa anapanga njama za kumwondoa mamlakani Mugabe. Mnangagwa amekimbilia uhamishoni.
Waziri wa Elimu ya Ufundi Jonathan Moyo amemkemea Jenerali Chiwenga lakini umoja wa vijana wa Zanu PF umesema “uko tayari kufa” ili kuitetea serikali ya Rais Robert Mugabe.
"Sisi kama vijana wa Zanu-PF ni simba aliyesimama imara na mwenye sauti, kwa hiyo hatutalemaa na kukunja mikono yetu wakati vitisho vikitolewa dhidi ya Mugabe," ilisema taarifa ya Katibu mkuu wa vijana wa  Zanu-PF Kudzai Chipanga.

Mbowe azungumzia watakachofanya sheria mpya vyama vya siasa


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema iwapo Sheria Namba Tano ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 itawasilishwa bungeni wa ajili ya kupitishwa watakuwa tayari kufa kuliko kukubali ipitishwe.
Akizungumza leo Jumanne jioni wakati wa kumnadi Mgombea Udiwani wa Kata ya Ibhigi, iliyopo Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Emmanuel Simba, Mbowe amesema kama kuna wakati wanaume wanatakiwa kusimama wahesabiwe ni wakati huo.
Amesema kupitisha sheria hiyo maana yake ni kuingiza ubatili walioufanya ili uwe sheria kamili, kwamba hakuna mikutano ya vyama vya siasa, hakuna majadiliano ya mustakabali wa nchi.
"Wanaanda mkakati wa kubadilisha sheria ya vyama  vya siasa taarifa tunayo,  wanataka kuiingiza sheria hiyo kwa nguvu, Sugu(Joseph Mbilinyi) tunaanzia bungeni, wakati huo ukifika wakituua watuue, wakitunyonga watunyonge hatutakubali tutaandamana mahali popote," amesema Mbowe.
Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai amesema watalikataa hilo ili watoto watakaokuja kesho na keshokutwa wajue baba na mama zao walipambana kulipigania Taifa lao.
Amesema Watanzania kwa umoja wao wasilikubali hilo kwa sababu litawanyima haki  kukutana na kujadili wanataka nini kifanyike na watakuwa wamekubali kurudi nyuma miaka mitano.
Kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyokutana juu na wawakilishi wa vyama vya siasa , ambapo ilitoa tamko kuwa katika  kampeni za uchaguzi wa marudio ya udiwani, wasijadili masuala ya siasa nje ya kata, jambo ambalo ni la kipuuzi.
Amesema "tusipokuwa makini na haya matamko ipo siku tutaambiwa wake zetu walale upande huu na sisi upande huu”
"Wanataka mimi mwenyekiti wa chama Taifa nije kujadili masuala ya kata, halafu masuala ya Taifa atajadili nani," amehoji Mbowe.
Amesema wamezuiliwa kuzungumza na wananchi kwa miaka miwili sasa ndiyo nafasi pekee waliyopata kuzungumza nao, "Haya ni makatazo ya kipuuzi," amesema.
Mbowe pia alizungumzia kashfa zinazodaiwa kufanywa na  aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, amesema kama wana uhakika na tuhuma hizo wampeleke mahakamani.
"Ilianza kwa Edward Lowassa alipohamia Chadema, ikaja kwa Fredrick Sumaye na sasa Nyalandu, kila anayehamia upinzani anaitwa fisadi, sisi hatuogopi Mahakama kwa sababu tunajiamini, wawachunguze na wawapeleke mahakamani.
" Nimezungumza na Nyalandu asubuhi ya leo, nikamuuliza kuhusu tuhuma hizo atachomoa, akasema hilo ni jambo dogo atadili nalo na halimpi shida," amesema Mbowe.

Mkuu wa Mkoa Dodoma apiga marufuku kuzungumzia ukame



Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge 
Chemba. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amepiga marufuku wakazi wa mkoa huo kutamka habari ya ukame.
Dk Mahenge amesema kutamka ukame ni kisingizio cha uvivu na ni sawa na watu wasiokuwa na maono.
Akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Chemba leo Jumanne katika mfululizo wa ziara zake, Dk Mahenge amesema haiingii akilini kutaja habari za ukame ilihali mkoa unafaa katika kilimo cha mazao mengi.
"Hata katika nchi ambazo ni jangwa lakini chini yake wana mafuta, hapa kwetu ukame tunauita sisi wenyewe," amesema Dk Mahenge.
Amewataka watumishi kubadilika kifikra ili wawape elimu wakulima wao watakaoweza kulima mazao yanayostahili katika maeneo ya mvua chache kama ilivyo mkoani humo.
Amewaagiza wakuu wa wilaya kuhakikisha wanashughulikia matatizo mengine lakini isiwe katika suala la njaa.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga amesema wilaya yake imeweka mikakati ya kujitosheleza kwa chakula na  kumaliza migogoro ambayo hupunguza muda wa uzalishaji.
Odunga amesema Chemba imejidhatiti kupambana na upungufu wa chakula na wanayo ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo.
"Hata hivyo tumeainisha mazao yanayotakiwa kulimwa kwa kila kata kutokana na mtawanyiko wa mvua za msimu," amesema Odunga.
Hata hivyo mkuu huyo amesema kuwa tofauti na maeneo mengine, Chemba wameendelea kukaribisha mifugo kwa kuwa ndiyo fursa kwao katika kuchangia maendeleo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Rehema Madenge amesema mambo mengi yatafanikiwa ikiwa watumishi watafuata utaratibu na kutimiza wajibu wao.
Kwa mujibu wa Madenge bila ya kufuata utaratibu mzuri wa kiusimamizi hakuna kinachoweza kubadilika mkoani humo.

Dhuluma wanazopitia uarabuni wafanyakazi wa nyumbani kutoka Tanzania

Wafanyakazi wa nyumbani kutoka Tanzania wanadhulumiwa uarabuniHaki miliki ya pichaHRW
Image captionWafanyakazi wa nyumbani kutoka Tanzania wanadhulumiwa uarabuni
Wafanyakazi wa kike wa nyumbanni kutoka nchin Tanzania walio nchini Oman na milki ya nchi za kiarabu UAE, wanadhulumiwa kimwili na kingono, wakiwa wanafanya kazi masaa mengi na wakilipwa mishahara midogo, kwa mujibu wa shirika la kitetea haki za binadamu, Human Rights Watch (HRW).
Kwenye ripoti iliyotelewa leo, HRW ilisema kuwa kuna maelfu ya wafanyakazi wa nyumbani kutoka Tanzania wako nchini Oman na UAE.
Watafiti wake waliwahoji 50 kati yao na kugundua kuwa karibu wote walipokonywa pasipoti zao walipowasili na kulazimiswa kufanya kazi hadi masaa 21 kwa siku bila kupumzika.
Wafanyakazi waliotoroka waajiri dhalimu na maajenti walisema kuwa polisi au balozi zao ziliwalazimisha kurudi la sivyo wangekosa mishahara yao hali iliyowachukua muda mrefu kutafuta pesa za kuwawezesha kurudi nyumbani.
Walisema kuwa walilipwa pesa kidogo kuliko zile waliahidiwa, au walikosa kulipwa kabisa, wakalazimishwa kula chakula kulichooza au mabaki ya chakula na kutukanwa kila siku, na pia kudhulumiwa kingono.

Mama Kanumba asema Lulu atatoka, Kanumba hatarudi tena


Dar es Salaam.  Siku moja baada ya Elizabeth Michael ‘Lulu’ kuhukumiwa kifungo cha kutumikia jela miaka miwili kwa kosa la kuuua bila kukusudia, mama mzazi wa marehemu Steven Kanumba, Flora Mutegoa amesema wanaombeza kwa kuishukuru Mahakama wamuache kwa hakuna mwenye uchungu zaidi yake.
Jana baada ya Mahakama Kuu kumtia hatiani mwigizaji huyo na kumpa adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela, Mama Kanumba aliishukuru Mahakama akisema imetenda haki jambo ambalo lilizusha gumzo wengi wakisema hakupaswa kufurahia adhabu hiyo.
Akihojiwa na waandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam jana Jumatatu baada ya hukumu kutolewa alisema anashukuru kwa kuwa haki imetendeka na kwamba atakwenda kumzika rasmi mtoto wake.

Hata hivyo, Mwananchi leo Jumanne amesema asibezwe kwa kauli hiyo kwa kuwa hakuna anayeujua uchungu anaoupata kila siku.
“Mimi sijui kama ninafurahia kama wanavyodai, waulize kwamba, yeye (Lulu) alipokufa mwanangu Kanumba alifurahia? Mimi ni mkristo, sipendi kuona baya likimfika binadamu mwenzangu, lakini Lulu ameenda miaka miwili jela na atarudi, je, mwanangu atarudi lini? nitamwona wapi tena? Amehoji.

Macho yote kwa Jaji Maraga


Nairobi, Kenya. Mahakama ya Juu inatarajiwa kufanya mkutano wa usikilizwaji wa awali leo wa kesi tatu za kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta zilizofunguliwa hivi karibuni kabla ya kuanza rasmi kibarua cha kusikiliza na kutoa hukumu.
Kesi zilizofunguliwa; ya kwanza ilipelekwa kortini na aliyekuwa Mbunge wa Kilome John Harun Mwau, ya pili iliwasilishwa na viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali Njonjo Mue na Khelef Khalifa ilhali ya tatu ilifunguliwa na Taasisi ya Demokrasia na Usimamizi (IDG) kupitia kwa wakili Kioko Kilukumi.
Katika kikao hicho kilichotarajiwa kuanza saa 5:00 asubuhi majaji na mawakali wa pande wote wanatarajia kukubaliana juu ya kanuni za kuongoza usikilizwaji wa kesi hadi hukumu. Jaji Mkuu David Maraga, mtu ambaye huzingatia sana matumizi ya muda ataupatia kila upande muda wa kuwasilisha hoja.
Walalamikaji watapewa muda mrefu zaidi wa kuwasilisha madai yao. Baada ya wajibu maombi kutoa hoja zao, walalamikaji watapewa tena fursa ya kuweka msisitizo katika hoja zao kwa mujibu wa sheria.
Katika usikilizwaji wa awali shughuli nyingine itakayofanywa na mahakama leo ni kusikiliza maombi ya wanaotaka kushirikishwa katika kesi hiyo dhidi ya Rais Kenyatta. Ombi la kwanza ni la mwanasheria mkuu, Profesa Githu Muigai kisha la aliyewania kiti hicho cha urais, Dk Ekuru Aukot.
Profesa Muigai ameeleza mahakama kuwa ni mshauri mkuu wa Serikali katika masuala yote ya sheria wakati Dk Aukot anasema katika ombi lake kwamba ana ushahidi utakaowezesha mahakama kufikia uamuzi wa haki.
Hii ni mara ya pili ushindi wa Rais Kenyatta unawekwa katika mikono ya Mahakama ya Juu baada ya kesi ya kwanza iliyofunguliwa na muungano wa vyama vya upinzani (Nasa) kupinga uchaguzi wa Agosti 8, 2017.
Septemba Mosi mahakama ilikubaliana na madai ya mlalamikaji kiongozi wa Nasa, Raila Odinga kwamba uchaguzi haukuwa huru na wa haki hivyo ikaubatilisha ushindi wa Rais Kenyatta.