Tuesday, December 25

"MZIKI WA BONGO FLEVA NI WA KIJINGA"....TID


Inaonekana bado mambo hayamwendei poa Top In Dar licha ya kuwa na hit ya ‘Kiuno’ hewani ambayo imeendelea kufanya poa.Hiyo ni baada ya nyota huyo ambaye jina lake halisi ni Khalid, kuamua kutumia Facebook kutoa maoni yake jinsi muziki huo unavyoenda.
“This Bongo Fleva Music is so stupid yaani kiasi kwamba we don’t even sell it only adios get sponsorship to play it lakini sisi tuko majalala,” aliandika TID.
Ujumbe huo ulivuta hisia za Chidi Benz ambaye aliamua kuchangia kwa kuandika: "Uoga. Unazaa vijana wanataka ustaa so wanakubali chochote. Wakongwe wanataka maisha so wanahitaji kuongezwa chochote. Vitu vinagongana vitu havieleweki."
Chidi aliongeza,”Watangazaji na wadau wamekua mameneja. Haikatazwi. Ila kama wewe si line yake atakupa vipi na asimpe msanii wake. We utapita vipi? Ujinga unajizaa kwa style ya mapacha."
TID naye aliongeza, “now watangazaji sasa hivi wanatutukana and they can do anything to anyone wanaweza wakasema TiD amecopy wimbo bila ya research yoyote yaani anaweza kufanya kila kitu hana limit.”

Mume wa ofisa wa Takukuru ampa jukumu Dk Hoseah

MUME wa aliyekuwa Ofisa Uchunguzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), marehemu Bhoke Ryoba ambaye aliuawa juzi kwa kupigwa risasi amesema kifo cha mkewe kimegubikwa na utata mwingi.
Akizungumza na jana, mumewe huyo, Charles Gibore, pamoja na mambo mengine alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo kubaini ukweli.
“Mke wangu aliuawa na mfanyakazi mwenzake na tukio hilo limegubikwa na utata ambao Takukuru na Polisi ndiyo pekee wanaoweza kutupa ukweli,” alisema Gibore nje ya chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.
Gibore alieleza kuwa mkewe huyo aliuawa usiku wa kuamkia Jumapili katika tafrija ya kuagana na kupongezana na baadhi ya wafanyakazi wenzake wa Takukuru waliokuwa wamepandishwa vyeo, tafrija ambayo Bhoke alipewa zabuni ya kupika chakula.
Alisema pia mkewe aliombwa pia awapatie wenye sherehe hiyo, vijana wawili wa kuwachomea nyama... “Vijana hao walikwenda asubuhi ukumbini ili kuandaa eneo la kuchomea nyama, huku Bhoke akiwa bado nyumbani akiandaa chakula,” alisema Gibore na kuongeza:
“Wale vijana walinieleza kwamba baadaye saa 8:30 mchana, Bhoke na wenzake walifika ukumbini na kuwakuta vijana wawili wanaofanya nao kazi wakinywa pombe, huku wakichezea silaha aina ya bastola kujaribu shabaha.”
“Vijana hao walifyatua risasi juu na ndipo muuaji alipompiga kichwani marehemu katika jicho na mauti yalimfika muda mfupi,” alisema.
Alisema baada ya hapo muuaji huyo alitoweka kisha kujisalimisha mwenyewe katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Temeke, Chang’ombe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Engelbert Kiondo alithibitisha mtuhumiwa huyo kujisalimisha na kisha kushikiliwa kituoni hapo na kueleza kuwa amekuwapo hapo Jumamosi iliyopita.Kamanda Kiondo alisema pamoja na mtuhumiwa huyo kujitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa Takukuru, polisi wanaendelea kuchunguza ili kubaini ukweli wa taarifa hizo.
“Tunaendelea kumshikilia hapa na uchunguzi utakapokamilika tutamfikisha mahakamani kwa taratibu nyingine za kisheria,” alisema Kiondo.
Marehemu Bhoke Ryoba alizaliwa Juni 18, 1978 katika Kijiji cha Kiterere, Wilaya ya Tarime mkoani Mara na anatarajiwa kuzikwa kesho kijijini kwao.
Ameacha watoto watatu; Doloresy (10), Dolrisy (4) na Dolrick Gibore ambaye ana mwaka mmoja.

Mwekezaji atiwa mbaroni kwa ujangili

MENEJA wa Hoteli ya Kitalii ya Tree Top, iliyoko katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, wilayani Monduli ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kukutwa na ngozi za chui nyumbani kwake, akiwa katika harakati za kuisafirisha kinyemela kwenda nje ya nchi.
Habari zilizothibitishwa na Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Paschal Shelutete, zilisema mtuhumiwa huyo anayeaminika kuwa ni raia wa Afrika Kusini alikotarajia kupeleka ngozi hiyo, alikamatwa saa 11 jioni ya Desemba 21, mwaka huu.
Kwa mujibu wa habari hizo, kabla ya kutiwa mbaroni, Kikosikazi kinachoundwa na askari kutoka Tanapa, Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA), kilifanya upekuzi nyumbani kwa meneja huyo baada ya kupokea taarifa za siri kuwa anajihusisha na ujangili na kuuza isivyo halali, nyara za Serikali.
“Ni kweli mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya kikosikazi chetu kupata taarifa kuwa anamiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria na kweli baada ya upekuzi alikutwa na ngozi ya chui,” alisema Shelutete kwa njia ya simu jana.
Alisema suala hilo tayari limefikishwa polisi katika Kituo cha Mto wa Mbu, wilayani Monduli kwa ajili ya uchunguzi na hatua zaidi za kisheria kabla ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani.
Habari zaidi zilidai kuwa mtuhumiwa aliyepelekwa katika Kituo cha Polisi cha Karatu ambako ndiko yalipo makao makuu ya Kikosikazi cha kupambana na ujangili katika Hifadhi za NCAA, Manyara na Tarangire.
Inasemekana hata hivyo aliachiwa kwa dhamana baada ya kudhaminiwa na mfanyakazi mmoja wa Hoteli za Sopa Lodges inayomiliki msururu wa hoteli kwenye mbuga za wanyama katika Mikoa ya Arusha na Mara.
Katika nyumba ilimokutwa nyara hizo za Serikali, inasemekana nyara zilikutwa zikiwa zimefungwa kwenye mfuko maalum tayari kusafirishwa huku jina na anwani ya mpokeaji ikiwa pia imeandikwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas aliyezungumza kwa njia ya simu akiwa njiani akitokea Moshi kwenda Arusha, aliahidi kulifualia suala hilo na kulitoa ufafanuzi suala hilo baada ya kufika ofisini.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la matukio yanayohusishwa na vitendo vya ujangili hatua ambayo inahatarisha usalama wa baadhi ya nyara za Serikali. Wiki iliyopita Serikali ilitangaza kutia mbaroni mtandao wa ujangali uliokuwa ukijihusisha na biashara haramu ikiwemo wa pembe za ndovu

JWTZ: Tunamsaka askari aliyepiga picha na Lema

WAKATI Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), likihaha kumtafuta aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akiwa amevaa sare za jeshi hilo, mtu huyo ameibuka na kusema yuko tayari kufukuzwa kazi kuliko kuacha kuishabikia Chadema.
Kauli hiyo ya JWTZ imekuja baada ya jana, gazeti la mwananchi kuchapisha picha ya mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni askari wa JWTZ akiwa amepiga picha na Lema pamoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, huku akiwa amenyoosha vidole viwili alama inayotumiwa na Chadema.
Baada ya taarifa hiyo, JWTZ lilitoa taarifa likieleza kushtushwa na tukio hilo na kusema kwamba linamtafuta mtu huyo kwa udi na uvumba ili kujiridhisha kama kweli ni askari wake.
‘‘Kimsingi Jeshi linafanya uchunguzi wa kumtambua mtu huyo kama kweli ni askari,’’ ilisema sehemu ya taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya jeshi hilo ambayo iliyatilia shaka mavazi aliyokuwa amevaa mtu huyo kama ndiyo yanayotumiwa na jeshi hilo sasa.
Taarifa hiyo ya JWTZ, ilisema ingekuwa rahisi kumtambua mtu huyo kwa kuangalia paji la uso lakini alilifunika ili asitambulike.
‘‘Pamoja na hayo, jeshi linamtafuta ili kumchukulia hatua za kinidhamu kutokana Kanuni za Majeshi ya Ulinzi likisema Sheria namba Nne ya Mabadiliko ya Nane katika Katiba ya Nchi ya mwaka 1992, Ibara ya 147(3), mwanajeshi yeyote hatakiwi kujihusisha na masuala ya kisiasa,’’ ilisema taarifa hiyo.
Mbali ya taarifa hiyo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema endapo itabainika kuwa aliyevaa sare hizo ni mwanajeshi, moja ya hatua dhidi yake ni kufukuzwa kazi mara moja.
Mbali na hatua hiyo, Kanali Mgawe alisema kuanzia sasa, Jeshi limepiga marufuku mtu yeyote kuvaa sare zake katika mikutano yote ya siasa na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Kuhusu kitendo cha askari huyo kupiga picha na Lema, Kanali Mgawe alisema moja ya masharti muhimu ya askari anapiojiunga na jeshi ni kutambua na kutii sheria inayomzuia kujihusisha na masuala ya siasa na kwamba kitendo cha mtu huyo kimemshangaza na kumfanya amtilie shaka kama kweli ni askari aliyekamilika.
Msimamo wa mtuhumiwa
Kwa upande wake, mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni askari wa Kikosi cha Chuo cha Mafunzo Monduli (TMA), mkoani Arusha, alisema ni bora afukuzwe kazi kuliko kunyimwa kujiunga na Chadema.
Akizungumza jana kwa sharti la kutotajwa jina akiwa Mirerani, Simanjiro mtu huyo alisema Chadema ni chama makini chenye uwezo wa kuongoza nchi kwani kinatetea wanyonge na kujali masilahi ya jamii.
Alisema kwa kuwa Katiba ya nchi hairuhusu wanajeshi kujihusisha na vyama vya siasa, yuko tayari kufukuzwa kazi ili aendelee kukishabikia chama hicho.
Alisema ruhusa ya kikatiba kwa wanajeshi ya kupiga kura kuchagua madiwani, wabunge na Rais haitoshi na kwamba ameamua kujiunga kabisa na chama. Askari huyo alipiga picha na Lema baada ya mbunge huyo kuhutubia mkutano uliofanyika huko Mirerani. Katika mkutano huo wa hadhara, Lema alisema: “Ninapoongoza maandamano ya makamanda ninakuwa natetea masilahi yenu mkiwamo polisi ambao mnanipiga mabomu.
Sisi hatuangalii wake zetu wamevaa hereni za dhahabu ila tunaandamana kudai haki, mishahara mizuri kwa madaktari, walimu, askari na maisha bora kwa Watanzania.”
Raymond Kaminyoge, Patricia Kimelemeta, Dar na Joseph Lyimo, Simanjiro.