Kilichotokea Kenya Septemba Mosi 2017 ni mshtuko wa zaidi ya mripuko wa bomu. Ni tukio la kihistoria ambalo litakuwa na nafasi katika vitabu vya sheria za kikatiba duniani.
Ijumaa iliyopita Mahakama ya Juu ya nchi hiyo ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8, mwaka huu yaliomtangaza Rais Uhuru Kenyatta (55) kuwa mshindi wa urais.
Majaji wanne wa jopo la watu saba likiongozwa na Jaji Mkuu David Maraga walisema uchaguzi huo haujaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na sheria, hivyo Kenyatta hatakuwa rais halali.
Waliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya(IEBC), iandae uchaguzi mpya ndani ya siku 60.
Imekuwa ni tabia kwa uchaguzi unaofanyika katika nchi mbalimbali za Afrika kwamba upinzani unapotangazwa umeshindwa hukataa kuyatambua matokeo na huenda mahakamani kuyabishia. Pia, huko mahakamani hushindwa. Hali hiyo husababisha wananchi kupoteza imani kwa taasisi za “kidemokrasia”, ikiwamo mahakama katika nchi zao.
Wananchi hujiuliza, ikiwa wizi wa waziwazi wa kura unafanywa na Tume za Uchaguzi na Mahakama zinafumbia macho, ina maana gani kwa wananchi kwenda kupiga kura?
Mara kadhaa matokeo ya uchaguzi katika Afrika yanakuwa tayari yameshajulikana hata kabla ya kutangazwa na hata kabla ya chaguzi zenyewe. Inakuwa tu ni suala la kumtangaza na kumtawaza mtawala ambaye tayari ameshapangwa na walio na nguvu katika nchi.
Kenya sasa imejaribu kuuvunja mduara huu wa kikaragosi usiokuwa na haya wala aibu. Majaji huko Nairobi, japokuwa walimuona Rais Kenyatta hana makosa katika mchakato wa uchaguzi huo, lakini waliiona Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo imekwenda kinyume na Katiba na sheria.
Swali linazuka, ilikuwaje kwamba makamishna wa tume hiyo wakaachilia kwa kujua au labda kwa dharau, uchafu uliofanyika katika zoezi zima la uchaguzi uliomfaidisha Kenyatta?
Yawezekana wafanyakazi wa IEBC kwa kujipendekeza kwa Kenyatta walifanya hayo walioyatenda bila ya yeye mwenye kuwaamrisha kufanya hivyo.
Mara nyingi tumeona kwamba kwenye nchi zenye taasisi dhaifu za Serikali maofisa, hata bila ya kushawishiwa na wanasiasa walioko madarakani, hujipendekeza kwa wanasiasa hao na kutenda mambo yaliyo kinyume na viapo vyao vya utumishi wa Serikali.
Isisahaulike pia katika mifumo ya tawala za kidikteta utumishi wa Serikali ulio huru ni nadra. Mtumishi wa Serikali hutakiwa kwa uwazi awe si tu mtiifu wa Serikali, lakini hata pia kada wa chama tawala.
Udanganyifu iliofanywa katika uchaguzi wa Kenya na kuanikwa wazi mahakamani haujaupiku ule uliofanywa mwaka jana katika nchi ya Afrika Magharibi ya Gabon. Agosti 2016, Rais Ali Bongo katika kuwania urais wa nchi hiyo kwa mara ya pili, alishinda kwa shida kwa kupata asilimia 49.8 ya kura dhidi ya mpinzani wake, Jean Ping, aliyepata asilimia 48.2.
Wakati wote ambapo kura zilikuwa zikihesabiwa Ping alikuwa anaongoza, akiwa na asilimia 59 ya kura, wakati Ali Bongo akiambulia asilimia 37. Hadi karibu ya mwisho pale kura za jimbo anakotokea Ali Bongo zilipohesabiwa.
Kwa mshangao mkubwa ilitangazwa Bongo amepata asilimia 99.93 ya kura katika jimbo hilo, na watu waliojitokeza kupiga kura katika jimbo hilo walifikia asilimia 95.46. Udanganyifu uliofanyika ulikuwa wazi kabisa. Ghasia na fujo zikazuka mitaani na damu ikamwagika.
Mahakama Kuu ya Gabon ilimtangaza Bongo kuwa mshindi, akatawazwa na anabaki anatawala hadi leo. Pia, huko Kenya mwaka 2013, licha ya kuwa na sababu zaidi za kimsingi, upinzani, ukiongozwa na mgombea yuleyule Raila Odinga (72), haujaweza kufua dafu katika jaribio la kuishawishi mahakama itengue ushindi wa Kenyatta.
Hata mwaka huu kiongozi huyo wa Muungano wa Nasa, Raila Odinga hajawa na tamaa kubwa kwamba mahakama ingempa haki. Hasa alipungukiwa na tamaa pale jumuiya mbili zisizokuwa za kiserikali ambazo zilitaka kuishtaki IEBC kwa kuendesha uchaguzi ovyo zilipotishiwa kupigwa marufuku. Mara hii mahakama ya Kenya imekwenda mbali zaidi kuliko vile mahakama za nchi nyingine za Afrika zilivyowahi kufanya – si tu kusema kulikuwapo dosari hizi na zile katika zoezi la uchaguzi, lakini kuwa na ujasiri wa kusema kwamba dosari hizo ni kubwa mno kufanya matokeo ya uchaguzi mzima kuwa batili na matokeo yake yasitambuliwe.
Kabla ya matokeo ya uchaguzi wa Kenya kutangazwa, waangalizi wa kigeni wa uchaguzi huo walikuwa tayari wanataja kwamba uchaguzi huo uliendeshwa kwa haki na namna iliyo sawa. Kati ya waangalizi hao walikuwapo Taasisi ya Jimmy Carter ya Marekani, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Swali linaloulizwa ni je, imekuwaje waangalizi hao wa kimataifa wakafikia uamuzi huo ambapo Mahakama ya Juu nchini Kenya imeona vingine?
Japokuwa uangalizi wa kutoka nje ni jambo zuri na la kukaribishwa, lakini jambo hilo lichukuliwe kwa tahadhari. Waangalizi hao wanakuwa wachache mno kuweza kusimamia kila kituo cha kupigia kura, si wajuzi waliobobea na siasa za undani za Afrika na hukaa siku chache kabla na baada ya uchaguzi, hivyo si rahisi kutoa makadirio ya kina.
Uchaguzi mtu hashindi tu katika siku ya kupiga kura, bali hushinda kwa kupitia zoezi zima, tangu uandikishaji wa wapiga kura, upigaji na kuhesabiwa na kusafirisha kura kutoka kwenye vituo pamoja na kutangazwa matokeo. Pia, yasidharauliwe masuala ya usalama wakati wa kampeni za uchaguzi na uhuru waliokuwa nao wagombea wakati wa kampeni zao. Kwa hivyo, inafaa tuwe waangalifu, tusiamini kila kitu kinachosemwa na waangalizi wa nje.
Swali jingine linaloulizwa ni kama IECB itaweza kuutayarisha uchaguzi mpya ndani ya siku 60 kama mahakama ilivyotaka. Mabishano yameshaanza kati ya Jubilee na Nasa.
Odinga na muungano wa Nasa hawana imani na IEBC na wanataka viongozi wa tume hiyo waliochangia katika uchakachuaji uliofanywa wafikishwe mahakamani.
Wangepanda uchaguzi mpya usimamiwe na chombo kingine na si IEBC, labda Umoja wa Mataifa. Kenyatta na Jubilee wanataka uchaguzi huo usimamiwe na IEBC ileile na tarehe ya uchaguzi itangazwe kwa haraka kama inavyowezekana. Wanasema wao wako tayari na mara hii watashinda zaidi kuliko hapo kabla.
Mashambulizi kwa mahakama
Jambo la kushtua ni kwamba Rais Kenyatta na makamu wake ambaye pia ni mgombea wake mwenza, William Ruto wameushambulia vikali uamuzi wa Mahakama Kuu ya Kenya na kuwavurumishia matusi majaji waliotoa uamuzi huo.
Kufanya hivyo inaonesha vipi wanasiasa hao wawili wasivyostahamili jambo lolote ambalo haliambatani na matakwa yao; ni harufu ya udikteta.
Wanasahau kwamba mahakama ni muhimili wa tatu huru katika demokrasia yeyote ile. Haitakiwi kutishwa na rais na makamu wake. Cha kushtusha zaidi ni kwamba Jubilee wamewasingizia majaji hao mambo ya uongo na kuitisha mahakama, hiyo kwamba itaona cha mtema kuni siku zijazo.
Ni Kenyatta huyohuyo aliyemshawishi Odinga baada ya uchaguzi uliopita wa Agosti 8 akalalamike mahakamani kama kaonewa na si kwenda barabarani.
Odinga amefanya hivyo, na sasa Kenyatta analalamika na kuwaita majaji “wakora.” Ni Kenyatta huyohuyo aliyeisifu mahakama hiyo mwaka 2013 pale ilipoamua na kuhakikisha kwamba yeye ni mshindi wa uchaguzi wa urais wa mwaka huo, naye Odinga akatoka patupu.
Leo Kenyatta anataka kuilazimisha mahakama ipigie magoti matakwa yake. Hii ni aibu ya hali ya juu na yaonesha kuna wanasiasa wanaopiga porojo tu pale wanapozungumzia juu ya uhuru wa mahakama na utawala wa sheria chini ya Serikali zao.
Kwa “kufunguka kisanduku cha uchawi huko Kenya”, sasa yamechomoza matumaini kwa Afrika. Bila ya kujali ikiwa Kenyatta atamshinda Odinga katika uchaguzi mpya - mara hiyo labda kwa njia safi- muhimu ni kwamba sheria katika Kenya si kitu kilichopotea kabisa.
Mahakama ya Kenya, kama alivyosema Odinga, imeinusuru hadhi ya Afrika na kwamba Afrika sasa haitakamata mkia linapokuja suala la haki. Kenya imeweka mfano mzuri kwa nchi nyingine za Afrika, tena bila mbwembwe.
Mwakani watawala wa muda mrefu katika Afrika, Paul Biya wa Cameroon na Robert Mugabe wa Zimbabwe, watataka wachaguliwe tena. Wao ni wazoefu na maarufu linapokuja suala la wizi wa kuchakachua katika uchaguzi na pia majeshi yao ni hodari katika kuwapiga mikong’oto wapinzani.
Kutokana na mambo yalivyochomoza huko Nairobi, wazee hao wawili sasa hawatakuwa tena na “mambo poa tu” katika chaguzi zijazo nchini mwao.