Wednesday, January 29

JE! UNAYAFAHAMU MAVAZI YASIYORUHUSIWA OFISI ZA UMMA


Wizara ya utumishi wa umma imetuma waraka unaotoa mwongozo wa mavazi kwa watumishi wote wa ofisi za umma na wananchi wote wanaohitaji huduma ktk ofs hizo.

Waraka huo namba 3 wa mwongozo wa mavazi wa mwaka 2007 unawatka wafanyakazi wote wa ofisi za umma na wananchi wote kutokuvaa mavazi yafuatayo:-
-Jeans
-Nguo zenye maandishi yoyote
-Nguo zinazobana mwili wako
-Nguo zilizo juu ya magoti (sketi/gauni)
-Kaptula
-Pedo
-Jezi za timu za mpira
-Nguo za chama chochote cha siasa
-Suruali ambazo hazijapindwa
-Blauz zinazoacha kifua/mgongo wazi
-Kuvaa mlegezo
Waraka huo ulikuwepo ila uekelezaji haukufanyika,hivyo kwanzia mwaka huu utaanza kutumika nchi nzima.
Wananchi usiende ofisi za umma ukiwa umevaa mavazi tajwa hapo juu,utaishia kufukuzwa bila kuhudumiwa…
@Jamii Forum
Soma sehemu ya waraka huo hapa chini:-
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA OFISI YA RAIS
Kumb. Na. EG.45/86/01/”A”/2 12/9/2007
WARAKA WA UTUMISHI WA UMMA NA 3 WA MWAKA
2007 KUHUSU MAVAZI KWA WATUMISHI WA UMMA
Utangulizi:
Waraka wa Utumishi Na. 1 wa mwaka 1971 unaohusu mavazi ulitokana na mwongozo uliotolewa na Chama cha TANU kuhusu mavazi. Madhumuni ya waraka huo ilikuwa kuimarisha heshima ya Taifa kwa kuhakikisha kuwa watumishi wa Serikali wanavaa mavazi ya heshima wanapowahudumia wananchi. Waraka huo uliainisha baadhi ya mifano ya mavazi ambayo yalionekana hayafai na yale yanayofaa kwa wanawake na wanaume, utengenezaji wa nywele unaofaa na usiofaa na vipodozi visivyokubalika.
Hali ilivyo sasa:
2. Tangu waraka huo ulipotolewa kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya mitindo ya mavazi, nywele na vipodozi. Mabadiliko ya mitindo ya mavazi ni jambo lisiloepukika. Hata hivyo baadhi ya mitindo hiyo ya mavazi inashusha heshima na hadhi ya utumishi wa umma kama itaendelea
kuvaliwa na ni kinyume na kifungu cha 2 (e) cha kanuni za Maadili ya utendaji katika utumishi wa umma za mwaka 2005 Hata hivyo kumekuwepo na tatizo la kutokuwepo na tafsiri inayoeleweka juu ya mavazi gani ni ya heshima au yanayokubalika na yasiyokubalika mahali pa kazi.
2
Uamuzi wa Serikali:
Tafsiri ya mavazi ya heshima hutegemea mila na desturi ya jamii husika. Katika utumishi wa umma mavazi ya heshima kwa mtumishi wa umma ni yale ambayo yanazingatia mila na desturi za taifa letu ambayo yanapovaliwa hayaonyeshi sehemu ya maungo ya mwili ambayo hayakuzoeleka kuachwa wazi, hayabani na ambayo hayana michoro au maandishi ya kudhalilisha wengine au yanayoonyesha ushabiki wa kitu fulani. Kwa hiyo waraka huu unatoa ufafanuzi kuhusu mavazi nadhifu yanayopaswa kuvaliwa kazini kwa kutoa mifano michache ya mavazi ambayo siyo ya heshima na ambayo hayakubaliki katika utumishi wa umma kwa jinsi zote mbili.
Utekelezaji:
3. Ufuatao ni ufafanuzi wa mavazi yasiyokubalika mahali pa kazi ambayo pia yameonyeshwa kwa picha kwenye kiambatisho A na B. Nguo kama “Jeans” na fulana zinaweza kuvaliwa na watumishi ambao wanalazimika kufanya kazi za nje ya ofisi.
3.1 Kwa Wanawake
(i) Baadhi ya mavazi yasiyofaa:
• Nguo zinazobana,
• Nguo fupi ambazo zinaacha magoti wazi.
• Nguo ambazo zinaacha sehemu ya mwili wazi kama
vile kitovu na kifua,
• Nguo ambazo zina picha, michoro, na maandishi ambayo hayaendani na shughuli za serikali,
• Kaptura aina yoyote ile kama vile pedo na pensi,
• Nguo zinazoonyesha maungo ya mwili (transparent).
• Suruali za “Jeans”,
• Suruali yoyote iliyoachwa bila kupindwa,
• Fulana – “T-Shirts” (Hizi zivaliwe tu wakati wa shughuli maalum inayotambulika),
• Nguo ambazo ni za kazi maalum – michezo, kazi za nje au burudani. Hizi zivaliwe mahususi wakati wa utekelezaji wa shughuli hizo,
• Nguo yenye maandishi ya chama chochote cha siasa au ushabiki wa kitu fulani,
• Nguo yeyote inayopingana na maadili ya utumishi wa umma.
(ii) Nywele zisizofaa:
• Nywele chafu na ambazo hazikutengenezwa vizuri.
(iv) Viatu visivyofaa
• Kandambili,
• Viatu vya michezo (isipokuwa wakati wa shughuli
maalum za michezo),
3.2. Kwa Wanaume
(i) Baadhi ya mavazi yasiyofaa:
• Nguo ambazo ni za kazi maalum kama vile michezo (Hizi zivaliwe wakati wa shughuli hiyo tu).
• Nguo ambazo zina michoro, maandishi na picha ambazo haziendani na shughuli za serikali.
• Nguo zinazobana,
• Kaptura ya aina yoyote.
• Suruali yoyote inayoachwa bila kupindwa.
• Suruali za “Jeans” na Fulana “T-shirts” (Hizi zivaliwe tu wakati wa shughuli maalum inayotambulika).
• Kikoi au msuli
• Nguo zenye maandishi ya chama chochote cha siasa na yenye kuonyesha ushabiki wa kitu fulani.
• Nguo yeyote inayopingana na maadili ya utumishi wa
umma.
(iii) Nywele zisizofaa:
• Nywele chafu na ambazo hazikutengenezwa vizuri.
• Nywele zilizosukwa mitindo ya aina yoyote ile
• Ndevu zisizotunzwa vizuri.
(iv) Viatu visivyofaa:
• Kandambili,
• Viatu vya michezo( Labda wakati wa shughuli maalum
za michezo).
Mwisho:
4. Kwa waraka huu waajiri wote wanapaswa kuwaelimisha watumishi kuhusu mavazi yasiyokubalika na kusimamia kikamilifu suala la mavazi kwa watumishi wa umma .
5. Waraka huu unafuta Waraka wa Utumishi Na.1 wa mwaka 1971 na unaanza kutumika mara moja.
George D. Yambesi
KATIBU MKUU
(MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA)

No comments:

Post a Comment