CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema mafanikio kinayopata yanatokana na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa kutoa siri kwao.
Kauli hiyo imetolewa juzi mjini hapa na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu), wakati akihutubia mkutano wa hadhara kwenye Viwanja vya Ruanda, Nzovwe.
Alisema hatua ya nchi kuyumba, inatokana na Serikali kutowajali maofisa wa Idara hiyo, hali inayowalazimu kuvujisha siri kwao.
Mbilinyi, alitoa siri hiyo baada ya kudai wamepata taarifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupeleka vijana 300 kambini katika Shule ya Sekondari Chimala, wilayani Mbarali, kwa ajili ya mafunzo ya kuvuruga mikutano ya CHADEMA.
“CCM imepasuka na ndiyo maana tunapata siri zote na popote palipo na maofisa usalama zaidi ya watatu, mmoja wao ni wa CHADEMA na walipo maofisa watatu au wanne wa Polisi, wawili ni wetu,” alisema Mbilinyi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa, alisema kutokana na taarifa hiyo, ameagiza kukutana na vijana wake wa kikosi cha Red Brigade kwa ajili ya kukabiliana na vijana wa CCM.
Alisema wamepata taarifa kuwa Serikali inataka kutumia jopo la waganga wa kienyeji kuwashughulikia wapinzani, lakini yeye hawatamuweza, kwa sababu ni mganga wa jadi ambaye anatoka Karatu.
Kutokana na kauli hiyo, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Mbeya, ulilazimika kuitisha mkutano wa waandishi wa habari kukanusha tuhuma hizo.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mbeya, Aman Kajuna, alisema chama hicho kimepeleka vijana wasiozidi 280 kwenye makambi kwa ajili ya kutoa mafunzo ya halaiki ya sherehe za miaka 37 ya CCM, zitakazofanyika kitaifa mkoani hapa.
Hata hivyo, baadhi ya waandishi wa habari mkoani Mbeya, walitembelea kambi hiyo baada ya mkutano wa Chadema uliofanyika karibu na Shule ya Chimala na kukuta vijana hao, wakifanya mazoezi ya kuimba nyimbo nyingi za kuzaliwa CCM.
>>Mtanzania
No comments:
Post a Comment