Wednesday, May 22

BUNGE lisitishwa jioni hii kutokana na hali tete ya mtwara



Spika ameahirishwa bunge hadi kesho kutokana na hali ya Mtwara. Spika kasema amepokea hali ya vurugu mtwara, hivyo bunge limeahirishwa ili kutoa fursa kwa kamati ya bunge kujadili suala hilo na serikali imetakiwa kutoa majibu katika kikao cha kesho.
Spika kasema kuwa wabunge wangependa kujadili hali ya Mtwara leo  lakini watajadili nini wakati hata wao wabunge wamepata taarifa hizo  kwenye vyombo vya habari? Hivyo, akaiagiza serikali kuleta majibu sahihi kesho bungeni na kuwaomba wabunge kuwa na subira hadi kesho na kisha akaahirisha bunge.
Akahitimisha kwa kusema kamati ya bunge inakwenda kujadili suala hilo sasa hivi.

Breaking News: Vurugu za Mtwara


Askari wanne na Wananchi Kadhaa Wameuawa. Hadi kufikia saa hii (3:00 pm) kuna taarifa kwamba ofisiza CCM (maeneo ya Mdenganamadi na Majengo) zimechomwa moto; askari wanne wameuawa pamoja na wananchi kadhaa. Wananchi wanatumia baruti za kulipulia samaki kuwalipua majengo na askari.Hatari iliyopo ni kuchomwa kwa jengo la ofisi za mkuu wa mkoa. Yote haya ni kupinga bomba la gesi kujengwa kuelekea DSM.
Habari zilizofika muda huu zinaripoti kwamba hali sio nzuri huko Mtwara, kwa ufupi hali ni tete na hakuna amani, mabomu ya machozi yanarindima muda huu na huduma zote za kijamii zimefunngwa hakuna usafiri, masoko, maduka na bar zote zimefungwa, daladala, Taxi na Bodaboda hazifanyi kazi. Kwa ujumla kinachoendelea ni mapambano makali kati ya Jeshi la polisi na wananchi wenye hasira wanaopinga vikali kuendelea kwa mchakato wa gesi ilihali nchi ikiwa haina sera inayosimamia nishati hiyo.
Kufuatia Kambi ya Upinzani kuukataa mpango wa serikali wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara Mpaka Dar es salaam ilihali Waziri wa Nishati akisoma hotuba yake kwa hisia kali na mbwembwe na kusema bomba la gesi linajengwa kutoka Mtwara kwenda Dar es salaam Wananchi wa Mtwara wacharuka!
Daraja la Mikindani limevunjwa hakuna mawasiliano Mtwara na Dar es salaam.
Baadhi ya Wananchi wamepora Silaha na wanazitumia kujibu mashambulizi ya Jeshi la Polisi (habari haijathibitishwa rasmi)
Jengo la Ofisi ya CCM saba saba limechomwa moto.
Nyumba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi), Hawa Ghasia yachomwa moto.
Lodge/Hotel (Shengena) inayoaminika kwamba ndiyo waliyofikia Askari wa Jeshi la Polisi (FFU) kutoka mikoa ya jirani kwaajili ya operation inayoendelea imechomwa moto.
Milio ya risasi na mabomu ndicho kinachosikika.
Nyumba kadhaa za watumishi wa Serikali zimechomwa maeneo ya Shangani. (habari haijathibitishwa rasmi)
Ni magari ya FFU ndio yaliyopo barabarani nayo yanapata wakati mgumu kupita kwasababu ya mawe na magogo makubwa yaliyowekwa na Wananchi.
Askari kadhaa wamekufa (habari hii haijathibitishwa rasmi)
Baadhi ya watu kadhaa wamechukuliwa na askari kwakuwa wamepita jirani na gari yao.
Yadaiwa askari wengi waliokuja si wa Mtwara, wengi wametoka Masasi na Lindi.
Ving'ora vinalia hovyo. Watoto wamefungiwa mashuleni walimu wamekimbia.
Vituo vya Redio vya Mtwara havizungumzii hali hii ya hatari bali vinapiga Muziki pengine vinakusanya matukio na habari ya majanga haya ili Wananchi wayapate.
Mabomu yanapigwa mfululizo maeneo ya Magomeni-Mtwara, mpaka sasa takriban mabomu 20 na ushee yameshapigwa.
Wakati waziri wa Nishati akisoma hotuba yake kwa hisia kali na mbwembwe na kusema bomba la gesi linajengwa kutoka Mtwara kwenda Dar Kauli mbiu ya Wananchi wa Mtwara ni "Gesi haitoki hata kwa bomba la peni"
Wananchi walalamikia kituo cha Television na Radio TBC kuzuia na kukata mawimbi yake kutoonekana wala kusikika katika Mkoa wa Mtwara kwa muda. Hatimaye hivi Punde matangazo yarejea.
Hili linaendelea wakati bajeti ya nishati na madini ikiendelea kujadiliwa muda huu Bungeni.

Bandari D’Salaam yapoteza Sh3 trilioni kwa mwaka


Dar es Salaam. Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikilikosesha taifa Dola 1.8 bilioni za Marekani (Sh2.8 trilioni) kwa mwaka, kutokana na kukosa ubora wa biashara.
Kutokana na hali hiyo, wataalamu wameeleza kuwa bandari hiyo inahitaji kufanyiwa maboresho muhimu ya hali ya juu, ili fedha hizo zisaidie nchi kuacha kutegemea misaada ya maendeleo.
Kwa mujibu wa ripoti iliyopo kwenye kitabu cha Opening the Gates: How the port of Dar es Salaam can transform Tanzania, licha ya Bandari ya Dar es Salaam kuwa sehemu nzuri, imekosa uwezo hivyo usimamiaji sera bora za kuiboresha zinatekelezwa taratibu. Ripoti hiyo inaeleza kuwa, mwaka 2012 pekee bandari hiyo ilikosesha taifa kiasi hicho cha fedha, huku ikizikosesha nchi jirani Sh1.3 trilioni.


“Fedha hizo ni sawa na asilimia saba ya pato la taifa, kitu ambacho kinawaathiri wanunuzi, wafanyabiashara na wakala mbalimbali wa Serikali,” inaeleza.
Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia (WB), Jacques Morisset ameihimiza Tanzania kuifanya bandari hiyo kuwa moja ya vipaumbele vyake vya juu kwa ajili ya kukua kwa uchumi.
“Watumiaji Bandari ya Dar es Salaam wanalipa fedha nyingi kwa wasimamizi wa bandari na wakala mbalimbali, kwa ajili ya huduma zao kuliko Mombasa,” alisema Morisset.
Akizungumzia ripoti hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alisema Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha bandari hiyo, lakini kazi ya ziada inahitajika kuifanya iweze kushindana na nyingine.


“Tunahitaji nchi jirani ziendelee kuitumia bandari yetu, bado tuna kazi kubwa ya kufanya ndiyo maana niko hapa, tunahitaji kuimarisha Kitengo cha Operesheni na maeneo mengine,” alisema Dk Mwakyembe.

Maalim Seif: Nitaomba kuwania tena urais mwaka 2015

Dar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad amesema ataomba tena kugombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha runinga cha ITV, Maalim Seif alisema kuwa anachoomba tu Mwenyezi Mungu ampe afya njema.
“Ni uamuzi wa wananchi na wanachama wenyewe wa CUF lakini kama Mwenyezi Mungu akinipa afya na uzima bado nia ipo,” alisema Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Alisema hivi sasa chama hicho kimekuwa kikijiimarisha visiwani huko kwa kufanya mikutano Pemba na Unguja ili kuhakikisha kinaendelea kukubalika kwa wananchi.
Kauli hiyo ya Maalim Seif ambaye amekuwa akiwania nafasi hiyo tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi, ilipokewa kwa hisia tofauti ambapo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Bashiru Ali alisema vyama vya siasa ni lazima viwe vinatayarisha viongozi wa baadaye ambao watafahamu kwamba uongozi ni dhamana wanayopewa na wananchi.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema Maalim Seif kama mwanachama wa chama hicho anaruhusiwa kwa mujibu wa Katiba kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa dola.

UJIO WA RAIS OBAMA NCHINI TANZANIA

Rais wa Marekani Bw. Baraka Obama na Mkewe wanatarajia kufanya ziara ya nchi tatu barani Afrika itakayojumuisha nchi za Senegal, Afrika ya Kusini na Tanzania, Kuanzia tarehe 26 Juni hadi tarehe 3 Julai.

Katika ziara yake hiyo, Rais atawekea mkazo umuhimu ambao Marekani inauweka katika ushirikiano wetu wa kina na unaoendelea kuimarika na nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia mipango mbalimbali ikiwemo ile ya kuimarisha ukuaji wa uchumi, uwekezaji na biashara, uimarishaji wa taasisi za kidemokrasia na uwekezaji katika kizazi kipya cha viongozi wa Kiafrika.

Rais atakutana na viongozi mbalimbali wa kiserikali, sekta binafsi na jumuiya huru ya kiraia ikiwemo vijana ili kujadili ubia wetu wa kimkakati katika ushirikano wetu rasmi na masuala mengine ya kimataifa.

Ziara hii itadhihirisha dhamira ya dhati ya Rais ya kupanua na kuimarisha ushirikiano kati ya Marekani na watu wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara katika kuimarisha amani na ustawi katika kanda hii na duniani kote kwa ujumla

Lissu abadili mbinu uzinduzi kampeni

Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anna Kilango akizozana na mnadhumu wa kambi ya upinzani, Tundu Lissu nje ya ukumbi wa Bunge jana baada ya Spika kuahirisha Bunge akiagiza hotuba ya kambi ya upinzani kuhusu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kufanyiwa marekebisho.Picha na Emmanuel Herman 

Ikungi. Mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni ya uzinduzi wa nafasi ya udiwani Kata ya Iseke Tarafa ya Ihanja, Wilaya ya Ikungi, Tundu Lissu, juzi alishindwa kuuza sera za Chadema, na badala yake alitumia muda mwingi kuhimiza ‘sera ya kuwakataza’ wananchi kuchangia maendeleo yao .
Tundu ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia chama hicho, alipanda jukwaani huku akiwa amebeba makabrasha ya michanganuo ya Bajeti ya Serikali ya kuanzia mwaka wa fedha wa 2010/11 hadi 2013/14.

“Mimi leo sitaki kabisa kuzungumzia habari za Amosi Mghenyi ambaye ametusaliti kwa kuhama Chadema na kurejea CCM. Amosi kisiasa ni mfu, kwa hiyo siwezi kupoteza muda wangu kuzungumiza mambo ya mfu”,alisema na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo uliofanyika katika kijiji cha iseke.
Alisema ufunguzi wake utajikita zaidi katika kuwaelimisha wananchi wa Kata ya Iseke kwamba Serikali inazo fedha nyingi na za kutosha kugharamia maendeleo ya wananchi.
Akijenga hoja yake hiyo, alisema kwa mfano katika mwaka wa fedha wa mwaka 2010/11, Mkoa wa Singida, ulipewa zaidi ya Sh903 milioni za undeshaji wa shule, lakini zilizotumika ni Sh464 milioni na kubaki Sh438.2.
Alisema fedha hizo zaidi ya Sh438.2 milioni zilizobaki, hazijaainishwa zilipelekwa wapi. “Kwa vyo vyote zitakuwa zimeishia kwenye matumbo ya mgambo na watendaji wa Serikali ya CCM”.
Lissu ambaye pia ni mwanasheria kitaaluma, aliwataka wakazi wa Kata ya Iseke, kumchagua Emmnuel Jackson Jingu awe diwani wao.
ili waondokane na manyanyaso ya michango kama walivyojikomboa wakazi wa Jimbo la Singida Mashariki.
Wagombea wengine wa nafasi ya udiwani Kata ya Iseke, ni Amosi Munghenyi wa CCM na Abdallah Kinyenje maarufu kwa jina la Petro wa CUF.

JK: Lowasa jembe


Dodoma/Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amemwagia sifa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hatua ambayo inaweza kutafsiri mengi katika medani ya siasa nchini.
Akizungumza na wabunge wa CCM kwenye Ukumbi wa White House Dodoma juzi, Rais Kikwete ambaye pia mwenyekiti wa chama hicho, alisema nguvu za Lowassa pekee zinatosha kushinda uchaguzi mdogo wa kiti cha udiwani Kata ya Makuyuni kilichoko wilayani Monduli.
Kata ya Makuyuni iko wilayani Monduli, ambako Lowassa amekuwa mbunge wake tangu mwaka 1995.
Habari za kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa Rais Kikwete alitoa kauli hiyo kuhusu kampeni za uchaguzi huo wa Makuyuni, baada ya kuwa ametoa ruksa kwa makada wa chama hicho wanaotaka urais kuanza kujipitisha pitisha miongoni mwa wanachama wa chama hicho. Lowassa anatajwa kuwa miongoni mwa wanaCCM wanaotaka kumrithi Rais Kikwete kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
“Sina tatizo na pale Makuyuni, najua muscles (misuli) za Mzee Lowassa zinatosha kutupa ushindi; au vipi mzee?” alidokeza mmoja wa wabunge wa CCM akimnukuu Rais Kikwete.
Uchaguzi wa Udiwani Kata ya Makuyuni unaotarajiwa kufanyika Juni 16, mwaka huu, utakuwa wa ushindani mkali kati ya CCM na Chadema ambao historia yao kisiasa mkoani Arusha ni ya uhasama.
Katika uchaguzi huo, unaofanyika baada ya kifo cha Abdillah Warsama (CCM), chama hicho kitatetea nafasi yake kwa kumsimamisha Godluck Lerunya na Chadema ni Japhet Sironga.
Mbali na Kata ya Makuyuni, uchaguzi wa udiwani mkoani Arusha utafanyika pia katika Kata za Kaloleni, Themi, Kimandolu na Elerai, kutokana na waliokuwa madiwani wa kata hizo (Chadema), kufukuzwa na chama chao.
“Mnaweza kuchafuana leo, kesho mkapata mgombea mwenye nundu nyingi na mabandeji kila mahala, halafu mkapata shida kumnadi,” alisema.
Siyo mara ya kwanza kwa Kikwete kumsifia Lowassa kwani aliwahi kufanya hivyo mwaka jana huko Longido wakati akikabidhi ng’ombe.
Pia aliwahi kumsifia wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2010 wakati Kikwete alipomwelezea Lowassa kama Mbunge makini na kuwaomba watu wa Monduli kumchagua tena.
Hata hivyo, alipoulizwa kama baada ya kuruhusiwa kuanza kujipitisha kwa wanaCCM kama anataka kuwania urais, Lowassa alijibu kupitia watu wake wa karibuni kuwa asingependa kuzungumzia suala hilo hasa baada ya Rais kutoa kauli hiyo.
Kutangaza nia ruksa
Rais Kikwete aliwaeleza wabunge hao kuwa si kosa kwa watu kutangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ikiwamo urais mwaka 2015.
“Wabunge na mawaziri wenye nia ya kutangaza nia ya kugombea urais wawe huru, kwani hiyo ni haki yao, isipokuwa wafanye kwa wema bila kukivuruga chama na kuwagawa wanaCCM katika makundi. Sioni tatizo watu kujipitisha. Sisi sote hapa tulijipitisha. Lakini tufanye hivyo kistaarabu bila kuvurugana.”
Aliwaagiza wabunge wa chama hicho kwenda majimboni mwao kusikiliza kero za wananchi badala ya kusubiri wakati wa uchaguzi.
Membe
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye naye anatajwa kuwa miongoni mwa wagombea amewataka waandishi waache kuandika kila siku habari za urais na badala yake waandike mambo ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kukutana na mabalozi wa nchi zinazoendelea kuhusu Mkutano wa Smart Partnership, unaotarajiwa kufanyika nchini, Membe alisema ni vizuri yakaandikwa mambo ya maendeleo na si kila wakati kuandika mambo ya urais.
“Mkutano kama huu nchi kama Kenya watauripoti vizuri na kwa undani hivyo mfanye hivyo si kila kitu urais 2015,” alisema Membe. Mkutano huo utaanza Mei 28, hadi Juni Mosi na utajadili jinsi gani sayansi na teknolojia vinaweza kutumika kuzikwamua kiuchumi.
Imeandikwa na Kizitto Noya, Habel Chidawali na Boniface Meena.