Julai 29, 2005, Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa alihutubia kwa mara ya mwisho Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Rais, ikiwa ni hotuba ya kuaga na kulivunja Bunge la Nane, baada ya kuliongoza taifa kwa miaka 10, tangu mwaka 1995-2005.
Katikati ya hotuba yake, Mkapa alisimulia kisa kimoja cha wazazi wa makamo na mtoto wao ambaye alishakuwa kijana mkubwa wa kiume, lakini akawa haeleweki anataka kufanya kazi ya aina gani, kwa hiyo ikabidi wamjaribu kwa mtihani ambao wao waliamini ungewapa majibu.
Mtihani gani ambao wazazi walimpa mtoto wao? Mkapa alisimulia: “Wazazi walichukua vitu vitatu, noti ya Sh10,000, Biblia na chupa ya pombe aina ya whisky, wakaviweka mlangoni ili kijana wao akifungua mlango tu avione. Baada ya hapo wazazi wakajificha waone itakuwaje.”
Wakiwa wamejificha, baba wa yule kijana alimwambia mkewe: “Kijana wetu akichukua fedha, atakuwa mfanyabiashara, akichukua Biblia bila shaka atakuwa padri na Mungu apishie mbali akichukua chupa ya whisky atakuwa mlevi.”
Kweli, haukupita muda mrefu, kijana akawa amerudi nyumbani kutoka matembezini. Akafungua mlango na kukuta vile vitu vitatu. Wazazi wakawa wanachungulia kupitia tundu la ufunguo. Wakawa na shauku kubwa kuona kijana wao atachagua nini.
Wazazi wakiendelea kuchungulia, walimshuhudia kijana wao akichukua noti ya Sh10,000. Akaiangalia vizuri halafu akaielekeza kwenye mwanga kujiridhisha kama ni halali, kisha akaitia mfukoni. Wakadhani angeishia hapo ili kukamilisha tafsiri ya kuwa mfanyabiashara.
Mshangao ukafuata baada ya kuweka noti mfukoni, hakuishia hapo, yule kijana alichukua na Biblia, akaifungua na kutazama kurasa kadhaa, halafu nayo akaitia mfukoni. Wazazi wakapigwa na butwaa kwa uchaguzi ule wa mtoto wao lakini hawakuchanganyikiwa.
Wazazi walitaka kuuona mwisho wa kijana wao, wakaendelea kuchungulia kwa umakini mkubwa. Wakamuona anashika na ile chupa ya whisky na kuifungua, akaonja ili kujiridhisha ubora wake, kisha nayo akaitia mfukoni. Akaenda chumbani kwake na vitu vyote vitatu.
Mkapa alisimulia kuwa kwa kitendo cha yule kijana kuchukua vitu vyote vitatu, wazazi wake walibaki wameduwaa. Kisha baba wa yule kijana alijipiga kofi kwenye paji la uso na kumwambia mkewe: “Sasa nimejua, mtoto wetu bila shaka atakuwa mwanasiasa.”
Tafsiri ya kisa hicho mpaka hitimisho lake ni kuwa mwanasiasa ama huwa haeleweki anataka nini, kwani anabeba kila sifa au anaweza kutosha maeneo yote, mfanyabiashara yeye, vilevile mtumishi wa Mungu lakini wakati huohuo akawa mlevi.
Hata hivyo, Rais Mkapa alionya kuwa hiyo si sifa ambayo angependa wanasiasa wakashifiwe nayo. Kwani naye ni mwanasiasa. Kwamba haitakiwi siasa zimpe sifa mbaya mwenye kushughulika nayo. Hata hivyo, visa vya wanasiasa mara nyingi huvunja mbavu na kukupa tabasamu.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika Awamu ya Nne, Lawrence Masha alihama CCM na kujiunga na Chadema. Masha alihama katika wimbi la waliomfuata Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyehamia Chadema.
Lowassa ambaye ni kada wa muda mrefu wa CCM, sababu ya kuhama kwake inatambulika kuwa ilikuwa kusaka nafasi ya kugombea urais, baada ya kutoswa kwenye chama chake, huku akiwa amejipanga kwa maandalizi makubwa na uwekezaji wa kiwango cha juu kupita yeyote yule.
Matarajio ya Lowassa kushinda yalikuwa makubwa hata baada ya kuhama CCM, ndiyo ikawa sababu kukawa na wimbi la wanaCCM ambao waliamua kujiunga na Chadema, mmoja wapo akiwa ni Masha ambaye alipoteza ubunge tangu 2010.
Tabasamu na Masha; hivi karibuni alirejea CCM baada ya kudumu na uanachama wa Chadema kwa miaka miwili. Sababu za kuhama alieleza kuwa hakuna mipango ya kuchukua dola. Hiyo sababu aliyotoa si tatizo, kwani kila mwanasiasa huwa na kipimo chake cha kubaki au kuhama chama.
Mfano wa tabasamu ni kwamba Aprili 4, mwaka huu, Chadema waliwasilisha bungeni kwa upendeleo majina mawili kwa ajili ya nafasi mbili za ubunge wa Afrika Mashariki. Majina hayo moja ni la Masha na lingine la Mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekia Wenje.
Kutokana na nafasi za Chadema kuwa mbili na majina kuwasilishwa mawili, ilibidi zipigwe kura za Ndiyo au Hapana. CCM kikiwa ndicho chama chenye idadi kubwa ya wabunge, kiliwakataa Masha na Wenje kwa kuwapigia kura nyingi za Hapana, hivyo kukosa ubunge.
Kanuni zilikuwa wazi kwamba katika wabunge tisa wa Tanzania, lazima Chadema kiwe na viti viwili, CUF kimoja, CCM sita, na kwa sababu wagombea wawili wa Chadema walikuwa wamekataliwa, ilibidi chama hicho kipendekeze majina mengine ya kupigiwa kura.
Katika kukwepa usumbufu wa mwanzo, Chadema mara ya pili kiliwasilisha majina sita ya Masha, Wenje, Salum Mwalimu, Profesa Abdallah Safari, Josephine Lemoyan na Pamela Maasay. Uchaguzi wa pili ulifanyika Mei 10, mwaka huu, Josephine na Pamela wakachaguliwa.
Kimsingi, Masha alikataliwa na CCM kuwa mbunge wa Afrika Mashariki, wakati Chadema walijaribu kumpendelea aipate nafasi hiyo, ila ameamua kujiunga na chama ambacho kilimkataa na kumnyima fursa ya kuitumikia nchi, ameachana na chama kilichompendelea.
Hilo ndilo eneo la kukufanya uduwae kuhusu wanasiasa. Hata hivyo, unaweza kuweka maneno yangu kichwani kuwa mwanachama ambaye hana kinachomzuia kuhama, kwa maana ya cheo au masilahi mengine ambayo huyakusudia, kumzuia kuondoka huwa kazi ngumu mno.
Mfano wa pili; Masha alipohamia Chadema mwaka 2015 alikutana na misukosuko ya polisi mara mbili. Agosti 2015 alitupwa mahabusu kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam, akidaiwa kuwatolea lugha mbaya polisi, alipokwenda kuwawekea dhamana vijana wa Chadema waliokamatwa.
Tukio la pili ni Oktoba 20, 2015 alipokamatwa Mpanda, Rukwa, akituhumiwa kufanya kampeni kwenye kambi za wakimbizi. Masha akatupwa rumande. Utetezi wa Masha ni kuwa alikuwa akionewa kwa sababu amehamia upinzani. Alilaumu kwamba Serikali inatumia vibaya nguvu zake za dola dhidi ya wapinzani.
Hata hivyo, Masha baada ya kuhama, hivi karibuni alipokuwa anahutubia mkutano wa kampeni za udiwani, Mbweni, Dar es Salaam, alimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kuwalinda wanachama wa CCM, kwani alipokuwa waziri pia yeye aliwalinda CCM.
Ni Masha huyohuyo aliyelalamika mwaka 2015 kuwa CCM inatumia vibaya polisi ndiyo maana wapinzani wanakamatwa kiholela. Akiwa CCM anaona sawa kutamba CCM walindwe na polisi kwani naye aliwalinda alipokuwa waziri.
Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila ambaye baada ya kushindwa ubunge 2015, alihamia Chadema Desemba mwaka jana, hivi karibuni amehamia CCM. Kabla ya kuwa NCCR-Mageuzi Kafulila alikuwa Chadema.
Aliposhindwa ubunge mwaka 2015, alifungua kesi mahakamani kudai aliibiwa kura na CCM. Tafsiri baada ya kuhamia CCM ni kuwa sasa anaungana na wale ambao alilalamika na kuwashtaki mahakamani kwa kumpora ubunge wake.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, Kafulila alisema kuwa asingejiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu maudhui ya chama hicho ni kugawa kura za upinzani kwa kutumiwa na CCM, maneno ambayo yalibeba tafsiri ya kumponda Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Miaka miwili baada ya Kafulila kutoa maneno hayo, amekuwa mwanachama wa CCM, huku Zitto na chama chake ambacho kiliitwa tawi la CCM, kikiwa kimewasha taa ya mapambano kisiasa, kikichuana vilivyo na CCM kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani.
Mabadiliko hayo ya rangi ya wanasiasa yasikuchanganye, bali yakujengee tabasamu. Kwamba Kafulila alimdhihaki Mbunge wa zamani wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, aliyegombea ubunge kwa tiketi ya ACT-Wazalendo mwaka 2015, kisha kuhamia CCM mwaka jana, mwaka huu ameungana naye CCM.
Mfano wa Rais Mkapa kuhusu wazazi wa makamo na kijana wao ukupe tabasamu zaidi na kukuondolea maswali ya mvurugiko wa wanasiasa kulamba matapishi yao, bali shusha pumzi kuwa Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ameteuliwa balozi na Rais John Magufuli.
Dk Slaa ataapishwa na Rais Magufuli ambaye miaka iliyopita alimbebea bango kwa kukosa uadilifu wa mali za umma kwa kuuza kiholela nyumba za Serikali.
Ni sawa tu aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu ambaye alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alishambuliwa kweli na wabunge wa Chadema kwa ufisadi sekta ya utalii na ugawaji wa vitalu vya uwindaji lakini leo Nyalandu ni Chadema, na ni kamanda wao. Tabasamu.