Saturday, December 2

Uchaguzi wa marudio watia hofu wasomi kuelekea 2020


 Wasomi na wanasiasa wameeleza hofu yao kuhusu mustakabali wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 endapo kasoro zilizojitokeza kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani hazitafanyiwa kazi.
Hofu hiyo imejitokeza katika uchambuzi wa wasomi waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti kuhusu matokeo na malalamiko yaliyojitokeza katika uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita na CCM kushinda kwa asilimia 97.
Miongoni mwa malalamiko yaliyojitokeza ni mawakala wa baadhi ya vyama vya upinzani kukamatwa na polisi na wengine kutimuliwa huku wengine na viongozi wao wakishambuliwa na kujeruhiwa.
Hata hivyo wakati upande mmoja wa upinzani ukilia kwa hujuma na kuambulia kata moja, upande mwingine wa chama tawala unachelea kwa ‘ushindi wa kishindo’ wa kata 42 kati ya 43, unaotajwa kuwa salamu za mwaka 2020.
Vurugu zilizotokea
Katika baadhi ya maeneo kulikofanyika uchaguzi huo, hali haikuwa tulivu bali yaliripotiwa matukio ya watu kupigwa, kukatwa mapanga, magari kuvunjwa vioo, wagombea kuzuiwa kutembelea vituo, wanachama kupigana, madai yaliyosababisha Chadema kujitoa katika kata tano za mkoa wa Arusha.
Hata hivyo, licha ya kujitoa katika kata za Ngabobo, Leguruki, Makiba, Maroroni na Mbureni, matokeo yalitangazwa na CCM kuibuka kidedea.
Matukio ya mawakala kuondolewa yaliripotiwa katika kata kadhaa, zikiwamo za Saranga (Dar es Salaam), Makiba (Arumeru) na Nyabubinza (Maswa).
Alipotafutwa kuzungumzia madai hayo jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhan simu iliita bila kupokewa badala yake alituma ujumbe mfupi kuuliza anapigiwa na nani.
Alipotajiwa anayeuliza na swali kuhusu malalamiko yaliyotokea kuhusu uchaguzi huo likiwamo suala la mawakala kutolewa kwenye vyumba vya kupigia kura na wengine kukamatwa, hakujibu hadi gazeti linakwenda mtamboni.
Hata hivyo, Kailima alikaririwa na gazeti moja Novemba 27 akisema uchaguzi umekwenda vizuri kwa asilimia 100.
“Vituo vyote kufikia saa 10.30 jioni hali ilikuwa nzuri na kura zilikuwa zinahesabiwa. Kumekuwapo na kasoro ndogo, kwa mfano kule Mwanza kuna vijana wa Chadema walikuwa wakiwazuia watu kwenda kupiga kura Nyakato. Dar es Salaam kila kitu kimekwenda vizuri, Lushoto kulikuwa na mawakala walitaka waruhusiwe bila kuwa na kiapo cha uwakala, lakini wakazuiwa,” alisema Kailima.
Maoni ya wachambuzi
Katika uchambuzi wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse alisema, “hii haiashirii jambo jema, kama uchaguzi mdogo umeleta shida namna hii, itakuwaje katika uchaguzi mkubwa wa mwaka 2020, hali itakuwa mbaya zaidi,” alisema Dk Jesse.
Alisema swali la kujiuliza ni kwa nini kunakuwa na matukio kama hayo kila wakati wa uchaguzi ilihali nchi ni ya kidemokrasia.
Alisema kibaya zaidi waliokuwa wakikamatwa ni wa upinzani zaidi, huku baadhi yao wakipigwa pia, “suala hili haliashirii mwanga mwema huko twendako. Uchaguzi ni suala la kisheria na kikatiba, kwanini linagubikwa na mambo yasiyofuata misingi hiyo, hakuna maana kukubali vyama vingi huku wagombea wa upande mmoja wakikamatwa,” alisema.
Msomi huyo alisema lazima kuwepo na malalamiko ya uonevu, wajibu wa Serikali ni kuhakikisha inasimamia uwanda mpana wa usawa wa kisiasa badala ya hali ilivyo sasa,” alisema Dk Jesse.
Alisema matukio hayo yakiachwa yaendelee yanaweza kutishia amani kwa sababu yanajenga chuki miongoni mwa wananchi.
“Pamoja na ushindi uliopatikana, sisiti kusema wazi kuna maeneo hawakushinda kihalali na hapakuonyesha hali ya kidemokrasia hata kidogo,” aliongeza Dk Jesse.
Kuhusu kauli ya mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla kuomba msamaha kwa sababu ya mkoa wake kukosa kata moja ya Ibhigi, msomi huyo alisema hilo linahitaji majibu kutoka kwake, lakini linaibua maswali.
“Inawezekana walipewa masharti lazima washinde, inawezekana walishindwa kwa uzembe, hawakusimamisha mgombea anayekubalika, hawakufanya kampeni, hawakuiba kura, hawakufanya fitina vya kutosha. Hizi zote ni hisia na mawazo kutokana na kauli ile, hivyo bado ana nafasi ya kufafanua sababu ya kuomba msamaha, kwa sababu kwenye uchaguzi wa kidemokrasia kuna matokeo mawili kushindwa na kushinda, hivyo kama kilichotokea ni demokrasia kwanini aombe msamaha,” alihoji Dk Jesse.
Maoni ya Dk Jesse hayaachani sana na ya Profesa George Shumbusho, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, aliyesema, “nachelea kusema kila kitu moja kwa moja kwa sababu sioni mwanga huko tuendako, kauli ya Makalla nayo inaleta maswali mengi je, aliambiwa lazima ashinde?
“Kama hivyo ndivyo basi itakuwa bahati mbaya sana kwa demokrasia ya nchi, hata hivyo hakupaswa kusema hadharani ili kuepusha maswali kama haya, hata kama lilikuwa ni agizo,” alisema.
Hata hivyo, Profesa Shumbusho alisema ni ngumu kutoa tathmini ya uchaguzi kama hujafanya tafiti, lakini kupitia vyombo vya habari, matukio kadhaa ambayo hayaashirii hali nzuri ya kidemokrasia yaliripotiwa.
“Ninachofahamu kwenye uchaguzi huru na wa haki na wa kidemokrasia, matokeo ni mawili kushinda na kushindwa, inashangaza kusikia wanaoshindwa wanapaswa kuomba msamaha, why (kwanini),’’ alisema Profesa na kuhoji.
Alisema kama kusingekuwa na kamatakamata ya wapinzani na mawakala wao ilikuwa rahisi kusema CCM imeshinda kwa mafanikio.
Alipoulizwa ushauri gani anatoa kwa wapinzani, alisema kama uchaguzi ungekuwa huru wananchi wangemchagua wanayemtaka, hivyo kungekuwa na nafasi ya kuwaambia wapinzani wafanye nini, lakini kwa hali ilivyokuwa hakuna cha kuwaambia.
Kuhusu namna ya kuondokana na hali hiyo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Omari Mbura alisema kuna haja ya kuziangalia dosari zilizojitokeza kwa kina.
Alisema pia wananchi na watawala wanapaswa kutambua katika uchaguzi kuna kushindwa na kushinda na wasipende kutamani kushinda wakati wote.
“Sidhani kama kuna aliyeonewa kwa sababu polisi wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria na wanafuata sheria, si rahisi kuacha kuwakamata watu wanaofanya fujo kwa sababu ni upinzani au chama tawala. “Wanachotakiwa kuzingatia ni kufanya kazi bila kupata maelekezo ya mtu au kwa ushabiki wa vyama,” alisema Dk Mbura.

No comments:

Post a Comment