Tuesday, May 19

Wabunge 200 watoro



Hali ya utoro kwenye vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano sasa imekithiri baada ya ofisi ya chombo hicho cha kutunga sheria kusema kina taarifa za wabunge 15 tu walioomba ruhusa kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Bunge hilo, linalotakiwa kuwa na wabunge 357, lilishindwa kupitisha miswada mitatu kutokana na upitishwaji wake kuhitaji theluthi mbili ya wabunge wa kila upande wa Muungano.
Jana, wakati wa mjadala wa muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa ambao uliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), Jenister Mhagama kulikuwa na idadi ya wabunge 81 tu bungeni, jambo linalomaanisha kuwa takriban wabunge 250 hawakuwamo ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.
Hali ilikuwa mbaya zaidi juzi. Wakati kikao cha Bunge kikianza kujadili Muswada wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi, kulikuwa na wabunge 29 tu ukumbini, hali inayomaanisha kuwa zaidi ya wabunge 320 hawakumo ndani kujadili suala hilo nyeti.
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge,  John Joel aliiambia Mwananchi jana kuwa ni wabunge 15 tu ndiyo ambao wana ruhusu ya Spika ya kutoshiriki kwenye vikao vinavyoendelea na kwamba wengine wote wanapaswa kuwa bungeni.
“Wabunge 15 tu ndiyo wenye ruhusa, wengine wapo lakini wanaingia na kutoka bungeni. Kutokuwepo kwao kunaathiri sana wakati wa kupitisha miswada kutokana na kutotimia kwa akidi.”
Idadi ya wabunge walio na ruhusa ni ndogo sana kulinganisha na viti vingi vinavyokuwa vitupu wakati wa mijadala mbalimbali kwenye vikao vya Mkutano wa 19 vinavyoendelea mjini hapa, jambo ambalo ofisi ya Bunge imeleza kuwa inathiri shughuli mbalimbali za Bunge zinazotakiwa kufanyika. Kwa mpangilio wa viti bungeni, kawaida safu tatu tu za eneo moja huweza kuwa na viti zaidi ya 15.
Wawakilishi hao wa wananchi wanalipwa Sh300,000 kwa siku, ikiwa ni fedha za posho ya “Ukiingia bungeni unakuta ukumbi mtupu kabisa, lakini ukitoka nje unakutana na wabunge wengi wakizurura. Kanuni zinasema kuwa ili muswada upitishwe inatakiwa kuwe na wabunge walau nusu,” alisema Lissu.
Lissu alisema huenda kukosekana kwa wabunge hao kukawa kunachangiwa na Uchaguzi Mkuu, kwani wengi wamejikita majimboni.
“Pia wapo ambao wamekwenda safari za kibunge, lakini si wengi kufanya Bunge liwe tupu.”
Wabunge wengi hawaonekani bungeni, lakini wamekuwa vinara wa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii katika majimbo yao hasa kipindi hiki, kitu kinachoonekana kuwa ni kujiweka karibu na wananchi.
Wengi wanajishughulisha na kuchangia masuala ya maendeleo pia kuendesha au kudhamini mashindano mbalimbali ya mpira wa miguu katika majimbo yao.
Mbali na kutoonekana bungeni kutokana na kujikita kuweka mikakati ya ushindi majimboni, baadhi ya wabunge pia wamekuwa watoro wa kuhudhuria vikao vya Bunge, kama wakionekana asubuhi, jioni ni nadra kuwaona.
Baada ya kujadili muswada wa Uhamiaji juzi, Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohamed Habib  Mnyaa aliomba mwongozo wa Spika kuhusu idadi ya wabunge kuwa ndogo.
 Mbunge huyo alisema kwa idadi hiyo itakuwa kinyume na kanuni kama Bunge litapitisha muswada na kusisitiza kuwa ili muswada uweze kupitishwa inatakiwa wawepo wabunge si chini ya 176.
“Ninavyofahamu mimi, ili tuweze kupitisha muswada huu wabunge tunaotakiwa kuwemo humu ndani ni kuanzia 176, lakini nikitizama idadi yetu hata 100 hatufiki, kutokana na suala hili naomba mwongozo wako,” alisema Mnyaa.
Akijibu suala hilo Spika Makinda alisema: “Naona kuna watu wapo kwa ajili ya kukwamisha vitu tu. Haya tuendelee.”
Baada ya majibu ya Spika, idadi ya wabunge iliongezeka kidogo na kufikia 139.
Licha ya idadi kuwa ndogo mjadala uliendelea na hatimaye muswada huo ukapitishwa.na vikao, kiwango ambacho kwa kuzidisha kwa idadi ya wabunge 357 inafanya jumla ya Sh107.1 milioni kutumika kwa siku moja.
Tangu kuanza kwa vikao vya Mkutano wa 19 wa Bunge  Machi 17 mwaka huu hadi jana mchana, idadi ya wabunge imekuwa ndogo ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge uliokuwa na mahudhurio makubwa kutokana na kujadili sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Katika mkutano wa 18 ulioisha Februari mwaka huu wabunge wengi walikuwa wakichangia hoja, walijikita katika kuzungumzia matatizo ya majimbo yao na kuacha mjadala uliokuwa mezani, jambo ambalo lilimfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwataka wajikite kwenye hoja za msingi na si kuzungumzia masuala ya majimbo yao.
Katika mkutano wa 19 unaoendelea hivi sasa wabunge wamekuwa ni wachache, hali ambayo hulalamikiwa na baadhi ya wabunge hasa ukifika muda wa kupitisha miswada mbalimbali.
Jana, kaimu kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema kuwa utoro wa wabunge unakwamisha mambo mengi ya msingi bungeni, huku akibainisha kuwa miswada haiwezi kupitishwa huku kukiwa na idadi ndogo ya wabunge na kwamba kufanya hivyo ni kukiuka kanuni.
Akizungumzia muswada huo, Lissu aliliambia gazeti hili kwamba itakuwa vigumu kupitishwa kwa sababu unatakiwa kupigiwa kura na theluthi mbili ya wabunge wa Tanzania Bara na theluthi mbili ya wabunge wa Zanzibar.
“Sijui kama muswada huu utaweza kupita maana ukitizama idadi ya wabunge si rahisi kupata theluthi mbili kutoka Zanzibar na Tanzania Bara,” alisema Lissu.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan alisema kuwa utoro huo hautoi picha nzuri kwa wananchi kwani wabunge ni wawakilishi wa wananchi na wanatakiwa kuhudhuria vikao vya Bunge.
“Miswada inawasilishwa bungeni na kitendo cha wabunge kutohudhuria ni wazi kuwa maoni yao kuhusu miswada husika inakosekana na pengine ingeweza kuisaidia Serikali,” alisema Azzan.
“Wapo ambao wapo katika majimbo maana huu ni mwaka wa uchaguzi. Binafsi nawashauri wahudhurie bungeni tu kwa sababu hayo majimbo yapo tu,” alisema.
 Mbunge wa Songwe (CCM), Philipo Mulugo alisema: “Kukosekana kwa mbunge kuna sababu nyingi, wapo walioomba ruhusa kutokana na kuwa na sababu maalumu na pia wapo waliopo majimboni. Ila binafsi naona ushiriki wetu bungeni ni jambo muhimu.”