Thursday, May 23

VURUGU ZA MTWARA ZAUA WANAJESHI WANNE NA KUJERUHI 20


Katika tukio lingine askari wanne wa jeshi la wananchi kikosi cha 41 KJ wamefariki dunia na wengine 20 kujeruhiwa baada ya gari lao kupinduka eneo la Kilimani hewa Nachingwea njiani kuelekea Mtwara kuongezea nguvu jeshi la polisi kufuatia vurugu zilizotokea mkoani humo


Mtu mmoja amefariki dunia na kadhaa kujeruhiwa katika vurugu zilizoibuka mkoani Mtwara baada ya bajeti ya wizara ya nishati na madini kusomwa ambapo pia ofisi za CCM wilaya ya Mtwara vijijini imeteketezwa moto pamoja na nyumba nyingine nne ikiwemo nyumba ya mbunge na mwandishi wa habari wa TBC



Nyumba ya mwandishi wa habari wa tbc yachomwa moto huku mabomu yakirindima huko mtwara


Hali imezidi kuwa mbaya katika Mji wa Mtwara na hivi punde watu wanaendelea kufanya uharibifu katika maeneo mbalimbali ya mji huo.
Jengo moja ambalo linadaiwa kumilikuwa na CCM limechomwa moto katika eneo la Majengo na daraja linalounganisha Lindi na Mtwara limevunjwa.
Mbali na hayo pia nyumba ya mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC)imechomwa moto.
Katika Mji wa Mtwara milio ya mabomu na risasi ndio inayosikika kila kona. Jeshi la Polisi linajaribu kuwadhibiti vijana na watu wengine ambao wanafanya vurugu hizo.

Kwa mujibu wa - freebongo.blogspot.com

Umefika wakati wa kubadili muundo wa Tanesco


ahitaji ya umeme kwa wateja wake ni Megawati 906, lakini uwezo wake ni kuzalisha 705 tu. Megawati hizo zinazalishwa kupitia mabwawa ya Kidatu (204), Kihansi (180), Mtera (80), Pangani (68), Hale (21) na Nyumba ya Mungu (8).
Jana bungeni, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka huu wa fedha na ndani ya hotuba yake alielezea hali mbaya ya Tanesco akisema inadaiwa zaidi ya Sh900 bilioni.
Haishangazi kusikia Tanesco ina hali mbaya kifedha, kwa sababu tangu shirika hilo lianzishwe mwaka 1964, limeshindwa kutoa huduma ya umeme kwa walau nusu ya Watanzania, hata hao waliounganishiwa, hawapati umeme wa uhakika.
Wizara inayoisimamia Tanesco imeshaongozwa na mawaziri 21 na makatibu wakuu 18. Hoja za baadhi yao ni shirika hilo kuzidiwa kimajukumu, ikiwamo mzigo wa madeni.
Katibu Mkuu aliyepita, David Jairo hakutafuna maneno aliposema hali ya Tanesco ni mbaya, mapato yake ya mwezi hayazidi Sh30 bilioni, wakati kwa siku inatumia Sh566 milioni kuwalipa Songas na IPTL.
Kwa mfano, mahitaji ya umeme kwa wateja wake ni Megawati 906, lakini uwezo wake ni kuzalisha 705 tu. Megawati hizo zinazalishwa kupitia mabwawa ya Kidatu (204), Kihansi (180), Mtera (80), Pangani (68), Hale (21) na Nyumba ya Mungu (8).
Umeme mwingine ni wa nguvu za mitambo iliyopo katika Vituo vya Tanesco vya Ubungo, Megawati 100 na Tegeta 45. Wakati uzalishaji wa umeme ni megawati 705, mahitaji ya Dar es Salaam pekee, ni Megawati 455. Profesa Muhongo ambaye ni waziri wa 21 katika wizara inayoongoza Tanesco, kwenye hotuba yake ya kwanza kwenye Bunge la Bajeti la mwaka jana, alizungumzia hoja ya kuinusuru Tanesco kwa kuipa ruzuku. Hata hivyo, msaada wa ruzuku ya Serikali kwa Tanesco umeonekana kutofua dafu.
Profesa Muhongo ameshawahi kukaririwa akitaka marekebisho makubwa katika shirika hilo, hoja ambayo inaungwa mkono na wananchi wengi. Kwa mfano, wananchi wa Wilaya ya Bunda, Mara wakizungumza kwenye mkutano wa wadau wa umeme walitamka bayana kuwa shirika hilo limezidiwa. Walisema limebeba mzigo mkubwa wa kuzalisha umeme, kuuza na kusambaza.
Ufanisi wa Tanesco umegubikwa na ‘umwinyi’ unaochangia kulidhoofisha, wateja wanaoomba kuunganishiwa umeme hawapewi huduma hiyo kwa wakati, kumekuwa na ulegevu wa ufuatiliaji madeni kwa wateja na hujuma nyingine zinafanywa na wafanyakazi wenyewe.
Kumekuwa na mianya mingi ya hujuma za mapato ya Tanesco, kumekuwa na tatizo la ‘vishoka’ wa kuunganisha umeme na wanaouza Luku na wote hao wana uhusiano na baadhi ya wafanyakazi wa Tanesco.
Pamoja na kuiona Tanesco kwamba imekuwa mzigo, bado kuna waliolifikisha shirika hilo hapo, Serikali na taasisi zake ni mojawapo na kwa kiasi kikubwa hawawezi kukwepa lawama.
Siyo siri, Serikali imekuwa mdaiwa mkubwa wa Tanesco na kutolipa hayo kumechangia kulidhoofisha shirika hilo kimapato.
Tunadhani kwamba hakuna haja ya kuendelea kuibebesha Tanesco mzigo wa kuzalisha umeme, kuuza na kusambaza. Ni wakati sasa kwa Serikali kulivunja shirika hilo ili kulipunguzia mzigo wa majukumu lakini pia kuongeza ufanisi kwa kuleta ushindani katika sekta ya nishati.
Wakati mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini ukiendelea bungeni, tungependa kuwashauri wabunge kuishauri Serikali kubadili muundo wa shirika hilo ili Watanzania wengi ambao ni zaidi ya milioni 40 waweze kunufaika na huduma ya umeme.

Bajeti Nishati kupoza kiu ya Wanamtwara?

Profesa Sospeter Muhongo 

Dodoma/Mtwara. Wakati mjadala mkali ukitarajiwa kuibuka bungeni leo wakati Serikali itakapokuwa ikiwasilisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, joto limezidi kupanda mkoani Mtwara ikielezwa kuwa wananchi wamehamasishana kwa mara nyingine kuacha shughuli zote ili kusikiliza kama hotuba hiyo italinda masilahi yao.
Hotuba hiyo ambayo itasomwa leo mara baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni na Waziri wa wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo, inatarajiwa kuibua mengi yakiwamo yanayohusu suala la gesi ya Mtwara.
Mjini Mtwara vipeperushi vinavyopingana vilisambazwa kuhamasishana ‘kuacha shughuli zao zote na kubaki nyumbani ili kufuatilia matangazo ya televisheni wakati Profesa Muhongo atakapotangaza bajeti hiyo, huku vingine vikipinga.
Ahadi za matumaini
Licha ya kampeni hizo za watu wa Mtwara, Serikali nayo imeweka matangazo katika vyombo vya habari likiwemo gazeti hili ikieleza namna mikoa ya Mtwara na Lindi itakavyonufaika na utafutaji na uendelezaji wa Gesi Asilia.
Tangazo lililotolewa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania limeainisha faida za gesi hiyo kwa Mkoa wa Mtwara ukiwamo umeme utakaotokana na gesi asilia. Pia imeelezwa jinsi mafunzo kwa vijana juu ya matatizo ya gesi asilia yaliyodhaminiwa na Wizara ya Nishati na Madini na kampuni mbalimbali kuanzia mwaka 2010.
Vilevile imeelezwa jinsi uboreshaji wa huduma za jamii kama ujenzi wa shule, hospitali na ujenzi wa viwanda kama kile cha saruji cha Dangote na mitambo ya kusafishia gesi utakavyowanufaisha wakazi wa mkoa huo.
Gesi hiyo ambayo pia inachimbwa katika Kisiwa cha Songosongo inatajwa kwamba itawanufaisha wakazi wa Mkoa wa Lindi kwa kupata umeme, kunufaika na kodi ya wawekezaji wa gesi na udhamini wa mafunzo kutoka kampuni mbalimbali na wizara.
Wiki iliyopita Profesa Muhongo alijigamba kuwa bajeti ya wizara yake atakayosoma leo itakuwa ya karne ya 22 itakayomaliza tatizo la umeme nchini kwa kuwa imetoa vipaumbele kwa sekta binafsi kusaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Wabunge wapania
Dalili za kuibuka mjadala mkali katika bajeti ya leo zilianza kujitokeza mwishoni mwa wiki wakati wa semina ya wabunge kuhusu masuala ya gesi ambapo wizara hiyo ilibanwa juu ya mambo ya mikataba.
Hata hivyo, semina hiyo ilitafsiriwa kuwa ililenga kuwapoza wabunge na kupunguza hasira zao huku wizara ikijipanga namna ya kuwashawishi waikubali bajeti baada ya kuona mwelekeo wao.
Wasiwasi Mtwara
Hali ya wasiwasi imeanza tena kutanda mkoani hapa hasa kutokana na vipeperushi vinavyokinzana na ujumbe tofauti kwa njia ya simu unaosambazwa.
Hali hiyo imejirudia tena huku ikionekana dhahiri kuwa na kauli kutoka makundi tofauti zinapishana katika vipeperushi hivyo huku wengine wakitaka mwendelezo wa kusitisha huduma ufanyike na wengine wakipinga.
Mojawapo ya kipeperushi kilisisitiza huduma zote zisitishwe kuanzia bajaji, bodaboda, masoko na magari yote yaendayo mikoani na wilayani yasiingie wala kutoka.
Huku vipeperushi vingine vikipinga: “Tunafahamu gesi ni mali yetu wote Wanakusini na tunafahamu kunyanyasika kwetu na Serikali ya nchi yetu na Mei 17 tuliunga mkono kufunga maduka na biashara zote, lakini hatukunufaika na chochote.
“Sasa Jumatano tena tusifanye biashara. Tuache ujinga Wanakusini wenzetu wengine hawana kazi wala gesi. Kampeni zitafanya tuwe maskini zaidi. Tarehe 22.05.2013 hatufungui duka wala hoteli, hata soko,” kilisomeka kimoja kati ya vipeperushi hivyo.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Linus Sinzumwa aliwataka wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku bila kujali vitisho hivyo kwa kile alichokidai kuwa ulinzi umeimarishwa.
ya za Tandahimba, Masasi, Newala na Nanyumbu waliendelea na shughuli za uzalishaji bila bughudha