Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Polisi Tarime, Rorya, Sweetbert Njewike akizungumza kwa simu akiwa Shirati wilayani Rorya, amesema hana taarifa hiyo ofisini kwake.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyantira, James Chacha amesema tukio hilo lilitokea kati ya Juni 7, 8 na 9 na kuzua taharuki kijijini hapo kutokana na aina ya vifo vya wanafamilia hao watatu kufariki kwa kufuatana.
Amewataja waliofariki kuwa ni Kerato Nyangerela (70), Regina Kerato (50) na Samwel Kerato (12) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi Nyantira.
Chacha amesema, "Juni 7 tulizika mzee baada ya kumkimbiza Kituo cha Afya, Muriba, baada ya saa 12 akafariki, tukamleta nyumbani kuzika, tulipomaliza maziko mtoto naye akawa kwenye hali mbaya, tukamkimbiza kituoni, akafa siku tunazika akaanza mama naye akafa pia," alisema.
Ameongeza kuwa kufariki kwa watu hao kwa mfuatano kijiji kumeibua hali ya wasiwasi na huzuni hasa kwa kuwa wameacha watoto wadogo.
Akizungumzia vifo hivyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Tarime, Mkumbo Odari alisema,"asali kama asali haina madhara kwenye mwili wa binadamu isipokuwa pale inapokuwa imechanganyika na sumu ndipo inapoweza kuleta madhara, na ndiyo maana asali inatumiwa kama dawa, kwenye chakula na kupaka kwenye mikate," alibainisha Odari.
Naye Diwani wa Kata ya Nyansicha, Sunday Magacha alisema hadi sasa chanzo cha vifo vya wanafamilia hao hakijajulikana na uchunguzi bado unaendelea ili kufahamu chanzo licha ya kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa na kituo cha afya Muriba ulionyesha kuwa walikuwa wamekula sumu.
Alisema tukio hilo lilikuwa la kwanza na la aina yake ambalo limewaacha wananchi wakiwa wameathirika kisaikolojia.