Monday, October 23

STAMICO SASA KULETA MAPINDUZI KWA WACHIMBAJI WADOGO


Mwenyekiti wa Bodi wa Stamico , Elexender Muganda akizungumza na waandishi habari juu shirika la Taifa la Madini (Stamico) kupata mtambo wa kisasa wa uchorongaji kwa kutumia upepo , jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji wa Stamico, Alex Rutagwelela akitoa ufafanuzi juu ya mtambo wa kisasa wa uchorongaji miamba jijini Dar es Salaam, kushoto ni Meneja Masoko na Uhusiano, Koleta Njelekela.
Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji, Alex Rutagwelela akiangalia mtambo wa uchorongaji wa miamba Bandarini , jijini Dar es Salaam.

Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii.

SHIRIKA la Taifa la Madini (Stamico) limepata mtambo wa uchorongaji kwa kutumia upepo (Air Rotary Drill Rig) wenye thamani dola za Kimarekani milioni 1.3 utakaotumika kupata taarifa za kijiolojia na mashapo kwa wachimbaji wadogo .

Kunufaika kwa wachimbaji wadogo kunatokana na stamico kupata mtambo wa kisasa wa uchorongaji miamba. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi wa Stamico, Elexender Muganda amesema kuwa mtambo umetengenezwa nchini Canada ambapo  mtambo huo utasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa za kjiolojia na mashapo katika maeneo yao kwa gharama nafuu.

Amesema mtambo huo umetolewa na serikali kupitia Wizara ya Madini chiini ya ufadhili wa Benki ya Dunia chini ya mradi wa usimamizi endelevu wa rasilimali ya madini Tanzania (SMMRP).
Muganda amesema huo una uwezo wa kuchoronga miamba kwa kutumia upepo na kwa haraka zaidi kati ya kina mita 30 hadi 200 na kwa gharama ambazo mchimbaji mdogo anamudu na kuchana uchimbaji wa kubahatisha pamoja kuwezesha kupata mikopo katika taasisi za fedha.

Aidha amesema kuwa wachimbaji wadogo wanaohitaji huduma za uchorongaji kwa kutumia upepo wafike katika ofisi za Stamico ili kupata taarifa zaidi.

Lulu asimulia yaliyomsibu nyumbani kwa Kanumba


Msanii wa fani ya uigizaji filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu Lulu amekana kuhusika kwa namna yoyote na kifo cha msanii mwenzake Steven Kanumba.
Ameieleza Mahakama Kuu kwamba, kama Kanumba asingefariki dunia, basi yeye ndiye angekufa kwa kuwa mpenzi wake huyo alikuwa amelewa na alimshambulia kwa kumpiga kwa ubapa wa panga, huku akimtishia kumuua kutokana na wivu wa mapenzi.
Lulu ameeleza hayo mahakamani leo Oktoba 23,2017 alipotoa utetezi katika kesi ya kumuua bila ya kukusudia inayomkabili. Anadaiwa Aprili 7,2012, nyumbani kwa Kanumba, Sinza Vatican jijini Dar es Salaam alimuua msanii huyo.
Msanii huyo alijitetea baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne na Jaji Samu Rumanyika kutoa uamuzi kwamba ana kesi ya kujibu.
Lulu akiongozwa na wakili Peter Kibatala kutoa ushahidi, amedai alifika nyumbani kwa msanii huyo saa sita au saa sita kasoro usiku baada ya Kanumba kumwita.
Alipofika nyumbani kwa Kanumba amedai alikuta mlango haujafungwa kwa kuwa awali aliwasiliana naye kwa simu na alimweleza anauacha wazi kwa kuwa alikuwa anakwenda kuoga.
Amesema alipofika chumbani kwa Kanumba alikuta akipata nywele mafuta na alikuwa amewekasuper black. Amedai kulikuwa na pombe kali aina ya Jack Danile’s na soda aina ya Sprite ambavyo mpenzi wake huyo alikuwa akinywa.
Lulu amedai akiwa amekaa kitandani, simu ya Kanumba iliita na kupitia mazungumzo alibaini aliyepiga alikuwa msanii wa muziki, Chalz Baba.
Amesema baadaye aliaga kwamba anaondoka kwa kuwa rafiki zake walikuwa wakimsubiri lakini Kanumba alimzuia akimweleza anataka watoke pamoja kwenda kwenye muziki wa dansi lakini alikataa kwa kuwa si mpenzi wa aina hiyo ya muziki aliosema anauona kuwa wa wazee.
Lulu amedai rafiki zake walimpigia simu lakini aliogopa kuipokea kwa kuwa alijua wangemuuliza kwa nini harudi, hivyo aliaga anakwenda kuchukua maji na alipotoka nje ya chumba aliipokea simu.
Amesema alipokuwa akimaliza mazungumzo kwenye korido, Kanumba alifungua mlango na kumuuliza alikuwa anazungumza na nani naye akamjibu kuwa ni rafiki zake.
Amedai alipomfuata alirudi nyuma akihofia kupigwa akidai alipokuwa amelewa Kanumba alikuwa mwenye kukasirika hata kwa vitu vya kawaida na kwa mara kadhaa alikuwa akimpiga kwa sababu hizo hata mbele za watu.
Lulu amedai alifungua mlango akatoka ndani na wakati huo Kanumba alikuwa amevaa taulo pekee, hivyo alijua asingeweza kumfuata.
Hata hivyo, amedai alimfuata na hata alipofungua geti na kukimbia kwenda kujificha kwenye baa ya Vatican bado alimfuata.
Lulu amedai baa hiyo haikuwa ikitumika na kwamba, licha ya giza Kanumba alimuona na alimpiga vibao na kumrudisha ndani nyumbani.
Amedai alikataa kuingia ndani akijua angepigwa zaidi lakini mpenzi wake huyo alimburuza na kumvuta hadi chumbani ambako alifunga mlango, akamtupa kitandani akaendelea kumpiga vibao.
Lulu amedai Kanumba alikuwa akilalamika kuwa alimsikia akizungumza kwa simu na mwanamume mwingine mbele yake na kwamba, alitoa panga uvunguni na kumpiga nalo mapajani kwa ubapa.
Amedai wakati Kanumba akimpiga aliziba uso kwa mikono yake na alisikia panga likianguka na sauti kama ya mtu aliyekabwa.
Lulu amedai alipoondoa mikono usoni alimwona Kanumba akiwa amejigonga ukutani na alijaribu kuinuka lakini akajigonga tena.
Amedai alikimbilia chooni ili kujiokoa, ambako alijifungia na akawa anapiga kelele  kuomba msaada.
Akiwa chooni, amedai alisikia kishindo cha mtu aliyeanguka au aliyebamiza mlango na kisha kimya kikitawala.
Lulu amedai alidhani Kanumba alitoka ndani na kubamiza mlango kwa hasira, hivyo akaamua kutoka ili akimbie lakini alimuona Kanumba akiwa amelala chini kimya.
Amedai alidhani Kanumba alijifanya kazimia baada ya yeye kupiga kelele kuomba msaada. “Nilimwambia kuwa hata kama ukijifanya kuzimia akija mtu nitamwambia kuwa umenipiga na ulitaka kuniua,” amedai Lulu.
Amesema baada ya kuona kimya aliingia bafuni alikochukua maji na kumwagia Kanumba ambaye hakuamka, ndipo alipokwenda kumweleza Seth, ambaye ni mdogo wa Kanumba.
Lulu amedai Seth alipomuangalia Kanumba alimwita daktari wake ambaye alimwambia amfuate. Amedai Seth alimtaka abaki pale lakini  alikataa kwa sababu alihisi akipata fahamu angeweza kumkata kwa panga, hivyo Seth alipoondoka naye akaondoka.
Lulu amesema alipokamatwa kwa msaada wa daktari wa Kanumba alipelekwa kituo cha polisi ambako alifanyiwa mahojiano katika vyumba vinne tofauti.
Amedai Aprili 8,2012 aliamka na kuhisi maumivu ya kipigo hivyo polisi walimpeleka katika Hospitali ya Mwananyama ambako alipatiwa matibabu.
Alipouliwa na wakili Kibatala kuhusu shtaka linalomkabili la kumuua Kanumba bila kukusudia au kusababisha kifo chake, Lulu alikana akisema hajawahi kusababisha kifo bali yeye ndiye alikuwa anashambuliwa kwa panga na asingeanguka basi huenda yeye ndiye angeuawa.
Lulu alipoulizwa na Wakili wa Serikali, Faraja George ni kwa nini hakuomba msaada kwa watu wengine katika nyumba hiyo na badala yake alikimbia nje, alijibu pamoja na kujiepusha pia alitaka kumfichia mpenzi wake aibu.
Baada ya Lulu kumaliza kutoa ushahidi, Jaji Rumanyia aliahirisha kesi hiyo hadi kesho Oktoba 24,2017 itakapoendelea kwa upande wa utetezi na kisha majumuisho ya hoja za mwisho za mawakili.
Lulu ambaye yupo nje kwa dhamana pia anatetewa na mawakili Fulgence Massawe na Omary Msemo.

Kigaila ahojiwa polisi, akosa dhamana


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam 'limemtupa' rumande Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Kigaila Benson.
Kigaila anayetuhumiwa kutoa lugha za kichochezi Oktoba 12 katika mkutano wake na waandishi wa habari, alikutana na kadhia hiyo jana aliporipoti kituoni kituo kikuu cha kanda hiyo.
Mwanasheria wa Kigaila, Frederick Kihwelo akizungumza na waandishi wa habari nje ya kituo hicho leo Jumatatu amesema hatima ya dhamana ya mkurugenzi huyo itaamuliwa kesho Jumanne.
''Amehojiwa kwa masaa 3 kuanzia saa 7 hadi saa 10  na amehojiwa kwa makosa aliyoyafanya katika mkutano wake wa Oktoba 12 na wamekataa kutoa dhamana labda hadi kesho,'' amesema Kihwelo.
''Lakini makosa yake yana dhamana ila wametueleza wanaoweza kuamua ama kupata dhamana au kukosa hawapo ofisini,"
Mwanasheria huyo amesema katika mkutano huo alizungumza mambo mengi ikiwamo kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na kutekwa kwa Ben Saanane ambaye ni msaidizi wa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Mwananchi imezungumza na kaimu kamanda wa kanda hiyo, Benedict Kitalika ambaye amesema upepelezi kwa sehemu kubwa umekamilika.

Mwigamba aeleza sababu za kutohudhuria kikao ACT -Wazalendo


Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa ACT -Wazalendo, Samson Mwigamba ametaja sababu mbili zilizomfanya kukataa wito wa kikao cha Kamati ya Uongozi ya chama hicho kwa ajili ya mahojiano.
Jumamosi Oktoba 21,2017 Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliwaeleza waandishi wa habari kwamba Kamati ya Uongozi ya chama hicho, ilimwita Mwigamba ili atoe maelezo baada ya kukituhumu chama hicho kukiuka misingi yake lakini hakufika.
Zitto alisema kamati hiyo baada ya kukutana na kujadiliana ilibaini hakuna misingi iliyokiukwa.
Mwigamba aliyekihama chama hicho na kujiunga na CCM, leo Jumatatu Oktoba 23,2017 amesema hakuona jambo jipya litakalojadiliwa dhidi yake katika kikao cha Kamati ya Uongozi kwa kuwa mengi aliyoyalalamikia alishayatolea ufafanuzi kwenye barua yake ya kujiuzulu.
Amesema jambo lingine lililomfanya kutohudhuria kikao hicho ni Kamati ya Uongozi kuwa na wajumbe 12 badala ya watano waliopo kwa mujibu wa Katiba ya ACT-Wazalendo.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa chama hicho, Ado Shaibu amesema hawana muda wa kulumbana na Mwigamba na wanaheshimu uamuzi wake wa kujiuzulu, hivyo wanamtakia kila la kheri kwenye safari yake ya kisiasa.

Gavana mteule asema anatambua changamoto za wadhifa huo



Profesa Florens Luoga
Profesa Florens Luoga 
Dar es Salaam. Gavana mteule wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga amesema amepokea kwa heshima kubwa dhamana aliyopewa na Rais John Magufuli na anatambua changamoto za nafasi hiyo.
Profesa Luoga ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) - Taaluma, amesema leo Jumatatu Oktoba 23,2017 kuwa atatumia wataalamu wa BoT kufanya kazi.
Amesema anahitaji ushirikiano wa kila mtu katika kufanikisha kazi aliyopewa.
“Nimepokea kwa heshima dhamana niliyopewa nikitambua kwamba zipo changamoto. Nitakwenda kujifunza zaidi kwa sababu sijawahi kuwa Gavana, nitatumia wataalamu waliopo katika kutekeleza majukumu yangu,” amesema Profesa Luoga.
Rais Magufuli Julai 11,2017 alimteua Profesa Luoga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akichukua nafasi ya Bernard Mchomvu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa Novemba mwaka jana na bodi hiyo kuvunjwa.
Profesa Luoga ni mtaalamu katika masuala ya sheria za kodi na amefundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tangu mwaka 1986 kabla ya kupandishwa cheo na kuwa profesa mshiriki (Associate Professor) mwaka 2005.
Ameshika nafasi mbalimbali chuoni hapo ikiwa ni pamoja na mwenyekiti wa kamati ya misaada ya kisheria katika kitivo cha sheria mwaka 1993 - 1995, mkurugenzi wa masomo ya shahada za awali (2005 - 2009), katibu wa baraza la chuo kikuu (2009 - 2013) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma (2013 hadi sasa).
Profesa Luoga aliyezaliwa mwaka 1958 ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Alihitimu shahada ya kwanza ya sheria UDSM mwaka 1985. Baadaye alikwenda kusoma Shahada ya Uzamili (LLM) katika chuo cha Queen’s University cha Canada (1988).
Mwaka 1988 alihitimu Shahada ya Uzamili ya Sheria za Kimataifa (MIL) katika Chuo cha Lund University cha Sweden (1991) na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Warwick cha Uingereza mwaka 2003.

Watetezi wasema mkutano uliingiliwa bila ya sheria Tanzania

Raia wa Uganda ambaye alihojiwa na vyombo vya habari akisema kuwa anahofia usalama wake kutokana na kuwa ni shoga alipokuwa Nairobi, Kenya, Aug. 7, 2014.
Mawakili wa utetezi wa haki za binadamu (LHR) wenye makao yao makuu Afrika Kusini, wameshtushwa na kitendo cha kukamatwa kwa wanaharakati wa haki za binadamu 13 wakiwemo raia wawili wa Afrika Kusini, nchini Tanzania.
Sanja Bornman wa LHR- Progamu ya Usawa wa Kijinsia amesema, “ Hakuna msingi wa sheria yoyote uliotumika katika kuwakamata watu hawa, na pia kuwapa dhamana na baadae kuifuta.
Ameongeza, "Hili linaonyesha ni jaribio la kuwadhibiti na kuwatishia watu na mawakili wanaotetea haki za binadamu, ambao kisheria walikuwa wanapata maelekezo kutoka kwa wateja wao kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria."
"Jambo hili halikubaliki na ni kinyume na majukumu ya kulinda haki za kibinadamu katika nchi ya Tanzania na kimataifa. Hivyo tunataka vyombo vya serikali kuwaachia huru wale wote waliokamatwa wakiwemo wanaharakati wenzetu wa Afrika Kusini," amesisitiza Bornman.
Polisi nchini Tanzania wanadaiwa kuwa waliingilia kati mkutano wa ushauri wa kisheria uliokuwa unafanyika kuanzisha mkakati wa mchakato wa kisheria Afrika (Isla) na huduma za afya ya jamii na uhamasishaji, huko katika jiji la Dar es Salaam.
Watu hao waliokamatwa mwanzoni waliachiwa kwa dhamana lakini baadae dhamana hiyo ilifutwa. Leo Jumatatu ombi la dhamana yao litapelekwa upya.
Taarifa ya LHR inasema kuwa kukamatwa kwa watu hao kunadaiwa kuwa kulisababishwa na ukweli wa kuwa wanaharakati hao walikuwa “wakihamasisha ushoga.”
Lakini LHR wanaamini kuwa sababu hizi ni dhaifu, na siyo za kweli kutokana na polisi wa Tanzania walikuwa wanashikilia agenda na maandiko ya mkutano huo.
Nyaraka walizonazo polisi zinaonyesha wazi kuwa mkutano huo ulioitishwa na Isla, ulikuwa na lengo la kuchukua maelekezo ya kisheria kwa kinachowezekana katika kukabiliana na changamoto za katazo la serikali katika kufunga vituo ambavyo vinawahudumia watu hasa ambao wanakabiliwa na hatari za Ukimwi.
Polisi pia waliwakamata watu 20 kati yao wanane ni wanaume na 12 wanawake kwa makosa ya ushoga katika kisiwa cha Zanzibar mwezi uliopita.
Mwezi Februari, Tanzania ilikosolewa na Marekani baada ya kutangaza kufunga vituo vya afya kadhaa vinavyoshughulikia kuelimisha watu kujilinda na Ukimwi, ikidai kuwa vilikuwa ni vituo vya kuhamasisha ushoga.
Serikali Dar es Salaam iliahidi kuwaondoa nchini raia wa kigeni wote wanaofanya kampeni kutaka mashoga wapewe haki zao.
Ushoga kwa kukutana kimwili wanaume unaadhibiwa kwa kifungo kati ya miaka 30 hadi maisha katika Sheria za Tanzania. Hakuna katazo kama hilo kwa kosa la mapenzi baina ya wanawake.
Kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binadamu Amesty International, ushoga ni kinyume cha sheria katika nchi 38 kati ya nchi za Kiafrika 54 na adhabu yake ni kifo huko Mauritania, Somalia na Sudan.
Uganda in 2014 tried to impose the death penalty on those found guilty of being homosexual, however the controversial law was later repealed.
Uganda mwaka 2014 ilijaribu kuweka adhabu ya kifo kwa wale watakao kutinakana na kosa la kujihusisha na ushoga , lakini sheria hiyo tata iliondolewa kabisa siku za usoni.

Uchaguzi 2017: Mabalozi wa Magharibi wawaonya wanasiasa Kenya

Karatasi za kuraHaki miliki ya pichaAFP
Image captionTume imeendelea na maandalizi ya uchaguzi huo wa Alhamisi
Mabalozi kutoka nchi za Magharibi nchini Kenya wamewataka wanasiasa nchini humo kuachana na "tabia hatari" huku hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda kabla ya uchaguzi wa marudio kufanyika Alhamisi.
Katika taarifa yao wanadiplomasia hao wamesisitiza kuwa uchaguzi wa urais unafaa kufanyika kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.
Mabalozi hao, wakiongozwa na balozi wa Marekani Robert Godec aidha wamewataka wanasiasa kutoa wito kwa wafuasi wao kutowashambulia maafisa wa tume ya uchaguzi.
Wamemtaka rais Uhuru Kenyatta kutotia saini marekebisho ya sheria za uchaguzi ambayo yalipitishwa hivi majuzi na Bunge linalodhibitiwa na chama chake cha Jubilee.
"Suluhu ya changamoto za sasa Kenya lazima zipatikane kwa kufuata katiba, sio nje ya katiba. Ni katiba pekee inayohakikisha haki kwa wote, na sio kwa wenye mali na mamlaka pekee.
"Uchaguzi huu ni sharti ufanyike kwa kufuata Katiba na sheria, kama zilivyofasiriwa na mahakama.
"Majaribio la kubadili sheria dakika za mwisho hayatasaidia, na kwa mara nyingine tunamhimiza Rais Kenya kutotia saini marekebisho ya sheria za uchaguzi."
KenyattaHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Image captionRais Kenyatta alikutana na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati mapema laoe
Katika mkutano wake na mkuu wa tume ya uchaguzi IEBC hivi leo, Rais Kenyatta ameendelea kuisisitiza kuwa tume hiyo iandae uchaguzi uliopangwa kufanyika 26 Oktoba.
Tayari kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga alishatangaza kutoshiriki uchaguzi huo na badala yake amewataka wafuasi wa muungano wake wa National Super Alliance (Nasa) kuandamana siku hiyo.
Bw Godec amesema walisikitishwa sana na hatua ya Bw Odinga na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka kujiondoa kutoka kwenye uchaguzi na kwamba wamekuwa wakijaribu kuwashawishi kukubali kushiriki uchaguzi huo na "tunaendelea kutumai kwamba watafanya hivyo ukizingatia hatua zilizopigwa na IEBC na kujitolea kwetu kwa pamoja kufanikisha uchaguzi huru wa kidemokrasia."
OdingaHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Image captionOdinga amesisitiza kuwa hatashiriki uchaguzi huo
Mabalozi hao, wakiwemo Nic Hailey wa Uingereza, Jutta Frasch wa Ujerumani na Stefano A. Dejak wa Umoja wa Ulaya pia wametoa wito kwa polisi kutotumia nguvu kupita kiasi wakikabili waandamanaji.
Muungano wa upinzani Nasa umekuwa ukiandaa maandamano ya mara kwa mara kushinikiza mageuzi katika tume ya uchaguzi.
Baada ya kuyaahirisha kwa muda, wakuu wa muungano huo wametangaza kwamba maandamano yataanza tena Jumanne katika miji mikubwa nchini humo.

Uchaguzi Kenya: Kenyatta akutana na mwenyekiti wa IEBC, asema yuko tayari kwa uchaguzi

Wafula Chebukati na Uhuru KenyattaHaki miliki ya pichaUHURU KENYATTA / TWITTER
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amekutana na mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) huku uchaguzi wa marudio ambao umekumbwa na utata ukiendelea kukaribia.
Rais amekutana na Bw Wafula Chebukati katika afisi ya Bw Kenyatta katika jumba la Harambee, Nairobi.
Mwenyekiti huyo wa tume alikuwa amekutana na mgombea wa upinzani Bw Raila Odinga Ijumaa.
Bw Odinga alijiondoa kutoka kwenye uchaguzi huo wa Alhamisi akisema hana imani uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki.
Uchaguzi huo wa 26 Oktoba unaandaliwa baada ya Mahakama ya Juu kufuta uchaguzi wa kwanza uliofanyika tarehe 8 Agosti ikisema kulikuwa na kasoro nyingi.
Bw Chebukati wiki iliyopita alikuwa ameitisha mkutano wa wagombea wote wa urais lakini baadaye akauahirisha na baadaye akakutana na Bw Odinga kivyake.
Alidokeza kwamba anapanga kuwakutanisha Bw Odinga na Bw Kenyatta baadaye baada kukutana na rais huyo.
Taarifa kutoka ikulu imesema Rais Kenyatta amemwambia mwenyekiti huyo kwamba yuko tayari kwa uchaguzi huo wa marudio na hana masharti yoyote kwa tume hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Naibu Rais William Ruto pia amehudhuria mkutano huo.
"Tumeweka wazi kwamba hatuna masharti wala matakwa yoyote kwa kuhusu suala hili. Tumetoa fedha za kutumiwa na IEBC kufanya kazi yake. Sasa wanafaa kfuanya kazi hiyo," amesema Rais Kenyatta.
"Tunasisitiza tu kwamba uchaguzi ufanyike tarehe 26 Oktoba, huo ndio wakati uliowekwa na IEBC kwa mujibu wa matakwa yaliyoambatana na kufutwa kwa uchaguzi wa tarehe 8 Agosti."
Odinga: Hakutakuwa na uchaguzi Kenya 26 Oktoba
Mahakama ya Juu, kwenye uamuzi wake ilikuwa imeagiza uchaguzi mpya ufanyike kwa kufuata katiba na sheria kikamilifu katika muda wa siku 60.
IEBC awali ilikuwa imetangaza uchaguzi mpya ufanyike tarehe 17 Oktoba lakini baadaye ikaahirisha tarehe hiyo hadi 26 Oktoba baada ya moja ya kampuni zilizokuwa zikitoa huduma muhimu kwa ajili ya uchaguzi huo kusema hazingekuwa tayari wakati huo.
Bw Odinga amekuwa akiitaka IEBC kuahirisha uchaguzi huo na ametangaza kwamba tarehe hiyo "hakutakuwa na uchaguzi".
Kumekuwa na utata kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo hasa baada ya kujiuzulu kwa mmoja wa makamishna wa tume hiyo Dkt Roselyn Akombe wiki iliyopita.
Dkt Akombe alisema anaamini tume hiyo haina uwezo wa kuandaa uchaguzi huru na wa haki Alhamisi.
Lakini maandalizi ya uchaguzi huo yamekuwa yakiendelea.
Shehena ya kwanza ya karatasi za kupigia kura iliwasili Jumamosi na shehena nyingine inatarajiwa kufika Nairobi baadaye leo.

Wakuu wa IEBC

Mwenyekiti: Wafula Chebukati
Naibu Mwenyekiti: Consolata Nkatha Maina
Makamishna:
  • Boya Molu
  • Paul Kibiwott Kurgat
  • Abdi Guliye
  • Margaret Wanjala Mwachanya
Afisa Mkuu Mtendaji/Katibu: Ezra Chiloba

Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilimtangaza Rais Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, akiwa mbele ya mpinzani wake Raila Odinga wa muungano wa upinzani Nasa kwa zaidi ya kura 1.4 milioni.
Bw Odinga alipinga matokeo hayo mahakamani na Mahakama Kuu ikaamua ulijaa kasoro nyingi na kuagiza uchaguzi mpya ufanyike katika kipindi cha siku sitini.