Wednesday, September 13

SERIKALI KUNUNUA MASHINE ZA DNA KWENYE MAABARA ZA KANDA


Serikali imedhamiria kununua mashine tatu za vipimo vya vinasaba (DNA) ili zitumike katika maabara za Kanda na hivyo kusogeza huduma karibu na wananchi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto Dkt. Hamis Kigwangala wakati akijibu swali la Mbunge wa Chumbuni Mhe. Ussy Pondeza kuhusu ucheleweshwaji wa matokeo ya uchunguzi wa sampuli ikiwemo sampuli za makosa ya jinai.

Dkt Kigwangala amesema kuwa Serikali ina mkakati wa kuongeza mashine hizo ili kuwezesha uchunguzi kufanyika kwa wakati kwa vielelezo vya makosa ya jinai ikiwa ni pamoja na vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto.

" Sampuli za uhalali wa watoto kwa wazazi zinafanyika kwa wepesi zaidi kuliko sampuli za makosa ya jinai kwani sampuli hizo zinachukuliwa moja kwa moja toka kwa wahusika hivyo kurahisisha uchunguzi wake endapo wahusika wa uchukuaji watachukua kwa umahiri na uhifadhi utafanyika kwa namna stahili" amefafanua Dkt. Kigwangala.

Aidha, Dkt. Kigwangala amesema kuwa sampuli za uchunguzi wa makosa ya jinai zinachukuliwa toka maeneo ya matukio hivyo uchunguzi wake unaweza kuchukua muda zaidi kutegemeana na aina ya sampuli na eneo zilipotoka.

Vilevile Dkt. kigwangala aliongeza kuwa Serikali inampango wa kuanzisha kituo cha kupima vinasaba (DNA) Mkoani Mbeya kwa lengo la kupunguza ucheleweshaji wa matokeo ya uchunguzi.

Mbali na hayo akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Vijijini Mhe. Hawa Ghasia kuhusu Serikali kuagiza tohara kuwa lazima kwa wanaume nchini, Dkt. kigwangala amesema kuwa si rahisi kwa Serikali kuagiza tohara  kuwa lazima japo kuwa inafaida kiafya kwa wananchi.

" Tohara inasaidia kupunguza maambukizi ya Saratani ya shingo ya Uzazi kwa wanawake pamoja na maambukizi ya virusi vya Ukimwi" ameongeza Dkt. kigwangala.

Aidha, amesema kuwa elimu kuhusu tohara imefikishwa kwa wananchi kwa kiasi kikubwa ambapo Serikali kwa kushirikiana na wadau katika Mikoa ya kipaumbele  imekuwa ikitoa elimu kabla na baada ya huduma ya tohara katika vituo vya kutolea huduma za afya.

YALIYOJIRI BUNGENI MJINI DODOMA



 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ngugai  akisisitiza jambo wakati wa Kikao cha Bunge leo mjini Dodoma.



 aziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi akilieleza Bunge leo mjini Dodoma kuhusu mkakati wa Serikali kukamilisha ujenzi wa nyumba elfu kumi za makazi kwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania  (JWTZ )  ambapo kati ya hizo zaidi ya elfu sita zimeshakamilika.



 Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir Ali Maulid (wakwanza  kulia)  akifuatilia kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo mjini Dodoma wakati wa ziara yake .



 Mbunge wa Mtwara Vijijini Mhe . Hawa Ghasia akichangia hoja Bungeni leo mjini Dodoma kuhusu maboresho katika sekta ya Afya hasa suala la tohara kwa wanaume ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza  maambukizi ya virusi vya ukimwi.



Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju akisisitiza jambo mara baada ya kuwasilisha muswaada wa sheria ya marekebisho ya Sheria mbalimbali  namba 3 wa mwaka 2017 leo Bungeni mjini Dodoma.



Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia  Katiba na Sheria Mhe.  Mohamed Mchengerwa (Mb) akiwasilisha maoni ya Kamati hiyo kuhusu  muswaada wa sheria ya marekebisho ya Sheria mbalimbali  namba 3 wa mwaka 2017 leo Bungeni mjini Dodoma



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi,  Ajira, Vijana na Wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza jambo kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi.
( Picha zote na Frank Mvungi- Maelezo Dodoma ).

ZANZIBAR KUIMARISHA KANUNI ZA KUKATAZA MATUMIZI YA TUMBAKU KATIKA KULINDA AFYA ZA WANANCHI


 Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Zanzibar Dkt Ghirmay Andemichael akitoa maelezo ya Shirika hilo kwenye warsha ya siku tatu ya kuimarisha kanuni za kupambana na matumizi ya tumbaku inayofanyika Hoteli ya Golden Tulip Malindi Mjini Zanzibar.
 Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Jamala Adam Taib akifungua warsha ya kuimarisha kanuni za mapambano ya matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku katika Hoteli ya Golden Tulip Malindi Mjini Zanzibar.
 Dkt. William Maina kutoka WHOAFRO akitoa maelezo ya Azimio la WHO na sheria za kimataifa dhidi ya mapambano ya matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku katika warsha ya kuimarisha kanuni za mapambano hayo katika Hoteli ya Golden Tulip Malindi.
 Baadhi ya washiriki wa warsha ya kumiarisha mikakati ya kanuni za kupiga vita matumizi ya tumbaku inayofanyika Hoteli ya GoldenTulip Malindi Mjini Zanzibar.
Picha ya pamoja ya mgeni rasmi na washiriki wa warsha ya kuimarisha mikakati ya kupiga vita matumizi ya tumbaku inayofanyika Hoteli ya Goden Tulip Malindi Mjini Zanzibar.Picha na Makame Mshenga.

Tume ya Mufti yakabidhi ripoti


 Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir akimkabidhi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi Ripoti ya Tume ya Mufti ofisini kwa Waziri.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi amekutana na Mufti Sheikh Abubakar Zubeir pamoja ujumbe wake wa Tume ya Mufti iliyoundwa kuhakikisha kwamba mali za waislam zinazomilikiwa na BAKWATA zinarejeshwa.

Waziri Lukuvi amepokea ripoti hiyo ikiwa ni kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli la kumtaka Waziri Ardhi afuatilie kwa makini maeneo yote ya waislam yanayomilikiwa na BAKWATA na yaliyomilikiswa watu kinyume cha utaratibu yanatafutiwa ufumbuzi.

Katika ujumbe huu Mufti ameongozana na Kaimu Katibu Mkuu wa BAKWATA Mwalimu Salim Abeid, Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Sheikh Ally Ngeruko, Makamu mwenyekiti wa Tume ya Mufti na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Sheikh Issa Othman Issa na Katibu wa Tume ya Mufti Alhaj Omary Igge.

Baada ya kukabithi ripoti hii Mufti Sheikh Abubakar Zubeir amemshukuru Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi kwa kupokea Ujumbe wake wa Tume ya Mufti na kumuomba achunguze na kuchambua kwa makini maeneo yote ya Bakwata yanayohusiana na migogoro ya ardhi.

Tume hii ya Mufti ya Kuhusu urejeshaji wa mali za waislam iliundwa na Mufti Sheikh Abubakar Zubeir mara baada ya kukukutana Mheshimiwa Rais na kumuomba awasaidie kuhakikisha kwamba mali za waislam zinazomilikiwa na BAKWATA zinarejeshwa BAKWATA.

Mara baada ya kupokea ripoti hii Waziri Lukuvi amemuahidi Mufti Sheikh Abubakar Zubeir kwamba atatekeleza agizo hilo la Mheshimiwa Rais na ataifanya kazi hii katika muda mfupi ujao na kusimamia kikamilifu kwa kufuata sheria.



 Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir akiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi akimsisitiza kufuatilia kwa makini maeneo yote ya waislam yanayomilikiwa na BAKWATA na yaliyomilikishwa watu kinyume cha utaratibu yanatafutiwa ufumbuzi kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais.



 Ujumbe wa Tume ya Mufti ukiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi ofisini kwake.



 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi akimsikiliza Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir mara baada ya kupokea Ripoti ya Tume ya Mufti ofisini kwake, kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu wa BAKWATA Mwalimu Salim Abeid na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Sheikh Ally Ngeruko.



 Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir akiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi baada ya kumkabidhi Ripoti ya Tume ya Mufti.

DC KILOLO AWATAKA WAZAZI KUWASOMESHA WATOTO WAO


Mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah akiwa katika ziara ya kuzitembelea shule za msingi za kata ya Bomalang'ombe na kujionea jinsi gani shule hizo zinavyoongozwa na kuzitambua changamoto zinazowakabili walimu,wanafunzi,wanachi na viongozi wanaozizunguka shule hizo lengo likiwa ni kuboresha utoaji wa elimu bora kwa wanafunzi wa wilaya ya kilolo.
Mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Bomalang'ombe.


Na Fredy Mgunda,Iringa

Wanachi wa kijiji cha mwatasi wamekuwa kikwazo cha wanafunzi kufanya vizuri katika masomo ya shule ya msingi kutokana na wazazi kutowatimizia mahitaji muhimu watoto wao pindi waendepo shule.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika shule hiyo mwalimu mkuu wa shule ya msingi mwatasi Seth Mfikwa alisema kuwa wazazi wengi wa kijiji hicho wamekuwa kikwazo cha maendeleo ya wanafunzi kwa kuwakatisha tamaa juu ya umuhimu wa elimu.

“Hapa kijijini wazazi wengi hawapendi watoto wao kwenda kusoma kwa kuwa watakuwa wanapunguza nguvu kazi zao mashambani ndio maana hawawapatii mahitaji muhimu ya kuwasaidia wanafunzi kusoma kwa uhuru” alisema Mfikwa

Mfikwa alimuomba mkuu wa wilaya ya kilolo Asia Abdallah kutafuta wataalam wa saikolojia kuja kuwapa elimu wazazi wa kijiji cha Mwatasi ili kukuza taaluma kwa wanafunzi wa kijiji hicho.

“Ukiangalia hali ya ufaulu wa shule hii sio mzuri kutokana na wazazi kutokujua umuhimu wa elimu lakini tunaendelea kuwaelimisha kidogo kidogo hivyo kwa kuwa mkuu leo umefika kwenye shule yetu tunaomba msaada wako wa kutoa elimu kwa wazazi ili kukuza elimu kwa wanafunzi wa kijiji hiki” alisema Mfikwa.

Aidha Mfikwa alisema kuwa wamekuwa wakiitisha mikutano ya mara kwa mara lakini bado tatizo kubwa hivyo jitihada zinahitajika kukomesha tabia hiyo kwa kuwa bila hivyo watoto wa kijiji hichi wataendelea kuwa wafanyakazi za ndani tu.

Anderson Mdeke ni diwani wa kata ya Bomalang’ombe alikiri kuwa wazazi wa kijiji cha mwatasi hawana elimu juu ya umuhimu wa kujua dhamani ya elimu katika maendeleo ya familia zao na taifa kwa ujumla.

“Kweli kabisa wazazi wa kijiji cha mwatasi wamekuwa wakiwaambia watoto wasifanye mitihani vizuri ili wasifaulu kwa kuwa wakifaulu watakuwa na gharama kubwa ya kuwasomesha hivyo wakifeli wataenda kuwafanya kazi za ndani na dio furaha kwa wazazi wa kijiji cha Mwatasi” alisema Mdeke

Mdeke alisema kuwa uongozi wa kata ya bomalang’ombe utaendelea kutoa elimu kwa wazazi hao ili kurudisha morali ya kuendelea kuwapa mahitaji muhimu yanayohitajika shuleni kwa kwa lengo la kuboresha maisha ya watoto hao.

“Zana potofu zimekuwa kikwazo kikubwa sana katika maendeleo ya wananchi wa kijiji cha Mwatasi hivyo tukiondoa zana hiyo elimu itakuwa kwa wanafunzi wa kijiji hichi” alisema Mdeke

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah aliahidi kulifanyia kazi tatizo hilo kwa kuzungumza na wazazi ili kuwaelimisha juu ya umuhimu wa elimu kwa wananchi wa kijiji hiki cha Mwatasi.

“Tangu nianza ziara katika wilaya ya kilolo leo ndio nimekutana nah ii changamoto ya wazazi kuwarudisha nyuma kielimu hivyo nitatenga muda muafaka wa kuja kuongea na wazazi wa kijiji cha Mwatasi kwanza swala hili limenishtua sana kwakweli lazima nilitafutee ufumbuzi haraka sana”alisema Abdallah

Aidha mkuu wa wilaya hiyo Asia alisema anatakiwa kujifunza tabia za wananchi wa kijiji cha Mwatasi kwanini wanafanya hivyo kwa kuwa changamoto hiyo ni kubwa na inatakiwa kutatuliwa mapema.

“Unajua lazima nijue chanzo cha kuwakatisha tamaa watoto wao wasiendelee na masomo ni nini hivyo nikijua tatizo ni nini naweza kutatua tatizo hilo kwa urahisi kabisa maana elimu ni kitu mhimu sana kwa maendeleo ya watoto yao” alisema Abdallah 

Abdallah alisema licha ya changamoto hiyo ya wazazi hata walimu wa shule wanamatatizo kwani haiwezekani kuwa na walimu wengi hivi lakini ufaulu bado upo chini lazima kukaa chini na hawa walimu kujua tatizo ni nini.

Panga la JPM haliwezi kuacha mawaziri salama


“Inawezekana ukawa ni mzuri wa sura, mchapakazi lakini kama utakuwa umetajwa katika ripoti yoyote inayoonyesha Taifa kuingia hasara, utaondoka na sifanyi hivi kwa kumwonea mtu.” Ni kauli ya Rais John Magufuli baada ya kupokea ripoti za uchunguzi wa uchimbaji na biashara za almasi na tanzanite.
Kauli hiyo inaakisi utaratibu wake aliojiwekea katika utendaji wa Rais Magufuli katika awamu yake.
Ripoti hizo ziliwasilishwa na kamati mbili zilizoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kuangalia uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa almasi na tanzanite.
Baada ya ripoti hizo kuwasilishwa, Waziri katika Ofisi ya Rais Tamisemi George Simbachawene amelazimika kujiuzulu baada ya kutajwa kwamba akiwa Waziri wa Nishati na Madini, aliwahi kuridhia mabadiliko katika mauzo ya kampuni uchimbaji Tanzanite na utoaji wa leseni kinyume na utaratibu.
Mwingine ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Edwin Ngonyani naye aliandika barua ya kujiuzulu baada ya kamati ya almasi kusema aliwahi kuzuia Serikali kununua mgodi wa almasi kwa dola milioni 10 na kuikosesha Serikali zaidi ya dola milioni 300, fedha ambazo zilienda kwa kampuni iliyonunua hisa.
Mtikisiko huo umekuja wakati vumbi la Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo halijatua. Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Muhongo baada ya kudaiwa kusababishia taifa kukosa mapato yake kupitia biashara ya usafirishaji wa makinikia ya dhahabu.
Hawa wote wameondolewa katika nafasi hizo, kwa makosa waliyohusishwa nayo katika uongozi wa wizara hiyo.
Wahenga walisema ukiona mwenzio ananyolewa na wewe tia maji. Msemo huo unawagusa mawaziri wengine wanaoongoza wizara nyingine na hata wale waliowahi kuziongoza wizara hizo, kwamba wakati wowote kaburi litakapofukuliwa, hakuna atakayebaki salama.
Mzimu wa Nishati na Madini
Kumbukumbu zinaonyesha ni Simbachawene pekee ndiyo alikuwa ameshikilia rekodi ya kuondoka Wizara ya Nishati na Madini bila mawaa, lakini baada ya kujiuzulu siku nne zilizopita, wizara hiyo imefuta rekodi hiyo tangu uongozi wa awamu ya tatu, nne na tano madarakani.
Simbachawene aliyeongoza wizara hiyo kwa kipindi cha miezi 10 tu, tayari amejiuzulu baada ya kutajwa na ripoti ya Kamati  maalum ya Bunge kuhusisha katika kashfa ya biashara ya Tanzanite. Simbachawene amefanya wizara hiyo kufikisha idadi ya mawaziri sita walioingia na kutoka kwa kashfa wizara hiyo.
Hii inatokana na ukweli kwamba kwa miaka ya karibuni mawaziri wote wa Nishati madini tangu uongozi wa awamu ya nne 2005, Dk Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi, William Ngeleja, Profesa Sospeter Muhongo, George Simbachawene wote wameondoka kwa kashfa za umeme.
Pia yupo Daniel Yona aliyekuwapo wizarani hapo katika awamu ya mwisho ya uongozi wa Rais Benjamini Mkapa, kabla ya Rais Jakaya Kikwete kuchaguliwa 2005.
Yona aliyedumu kwa miaka miwili baadaye aliishia jela kwa kashfa ya zilizohusu mikataba na Kampuni ya MS Alex Stuwart iliyopewa zabuni ya kuhakiki malipo tanzania iliyostahili kutokana na mauzo ya madini.
Waliofuata
Kwa mujibu wa kumbukumbu katika wizara hiyo, Januari hadi Oktoba 2006, Wizara hiyo iliongozwa na Dk Ibrahim Msabaha ambaye baadaye alihusishwa na kashfa ya Richmond na kulazimika kujiuzulu.
Oktoba mwaka 2006 hadi 2008, wizara hiyo ikawa chini ya Nazir Karamagi ambaye alikutana na joto la kashfa ya Richmond.
Kuanzia mwaka 2008 hadi 2012, kibarua cha wizara hiyo kikakabidhiwa kwa William Ngeleja lakini naye aliondolewa katika nafasi hiyo na sakata la mawaziri mizigo, na baadaye akiwa nje akakutwa na mgawo wa James Rugemalira kwenye sakata ya Tegeta Escrow.
Nafasi hiyo kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2014 ilijazwa na Profesa Sospeter Muhongo aliyeondolewa kwa mara ya kwanza kwa kuhusishwa kwenye mzimu wa Escrow.
Januari mwaka 2015, Rais Kikwete alimteua George Simbachawene kabla ya kurejeshwa Rais John Magufuli kumrejesha Profesa Muhongo, lakini akalazimika kumwondoa tena katika sakata la Makinikia.
Akizungumzia hali hiyo, Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti (Repoa), Dk Abel Kinyondo anasema tatizo linalojitokeza katika wizara hiyo ni unyeti wa rasilimali zake kuwa chini ya uamuzi wa kiongozi mmoja.
Anatoa mfano akisema mikataba inayoingiwa katika sekta ya madini, ni ya muda mrefu na hivyo kushawishi mwekezaji na waziri mwenye dhamana kutumia njia za kona.
“Waziri anaingia wizarani akijua hataweza kukaa milele, na yeye ni binadamu anayeweza kuingiwa na tamaa, anajikuta ameshawishika kuingia mikataba itakayomnufaisha kwanza yeye,” anasema.
Dk Kinyondo anasema udhaifu katika wizara hiyo unachagizwa na Katiba na sheria zinazotoa mamlaka makubwa kwa waziri mwenye dhamana badala ya kuweka mfumo utakaokuwa na taasisi mbalimbali zinazoshiriki katika upitishaji wa maamuzi ya mwisho.
“Norway hakuna kiongozi mmoja anayeweza kubadilisha au kupitisha maamuzi ya mwisho ndani ya kampuni ya usimamizi wa rasilimali. Ujerumani hakuna mwanasiasa anayeweza kuingia taasisi ya fedha na kufanya jambo fulani, hata sisi ilitakiwa waziri awe sehemu tu ya uamuzi wa mwisho, yaani tuwe na hatua mbalimbali za uhakiki wa mikataba, sheria zinazopitishwa na maamuzi ya mwisho,” anasema.
Dk Kinyondo anasema katika mazingira ya mfumo huo, hakuna waziri au kiongozi atakayeweza kuingiza udhaifu katika usimamizi, uthibiti na uendeshaji wa rasilimali za nchi.
Msingi anaoweka JPM
Mkurugenzi wa Taasisi ya Fordia, Bubelwa Kaiza anasema usafi anaouzungumzia Rais Magufuli hauishii kwa mawaziri waliopo madarakani, bali hata kwa mawaziri wastaafu na wabunge wa chama hicho atawajibishwa.
“Ndiyo maana akasema hata Bunge liangalie vizuri kanuni zake kwa wale wanaotajwa tajwa, ili Bunge litoe mapendekezo na chama chake kitaangalia namna ya kuwachuja.
Kaiza anasema ni jambo jema kujiwekea viwango na utaratibu wa viongozi anaofanya nao kazi. Mwanaharakati huyo katika sekta ya rasilimali za madini anasema kinachomsaidia ni mfumo alioanza kuweka kupitia sheria mpya ambazo zitalazimisha viongozi na mawaziri wapya wanaokuja wasiweze kumwangusha.
“Kwa mfano, Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba 7 ya mwaka 2017 imeondoa mamlaka kwa waziri, katibu mkuu na kamishna wa madini katika usimamizi na udhibiti wa madini na badala yake mamlaka hayo imepewa Kamisheni ya madini itakayokuwa na wataalamu kutoka sekta mbalimbali. Hii ni hatua nzuri inayoondoa tamaa za kiongozi mmoja ndani ya wizara ya madini kuamua kwa maslahi yake,” anasema.
Hata hivyo, Kaiza anasema changamoto ilijitokeza katika mfumo uliokuwapo ambao ulikuwa wa kujinufaisha kwa viongozi wengi.
“Rais alijua wapya hawatamletea matatizo, ndiyo maana alitumia muda mrefu kuchuja wale wenye dosari na kuchukua wasiojulikana,” anasema.
Kuhusu hatma ya mawaziri wa zamani, mchambuzi huyo anasema itakuwa ni vigumu kupona endapo Rais atapita kila wizara kwa kipindi cha miaka mitatu aliyobakiza.
Kila wizara na kaburi lake
Kwa sasa ziko wizara 18 na kila moja tunaweza kusema ina kaburi lake ambalo likifukuliwa hatujui nani atakayepona.
Matatizo haya yamekuwa yakiibuliwa na mara nyingi na ripoti ya Ofisi Mdhibiti  na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na nyingine za kamati zinazoundwa na Bunge kuchunguza masuala mahususi.
Mathalan, licha ya kuondolewa kwa kashfa ya ulevi bungeni, wakati huohuo lilikuwa sakata la Lugumi lililoibua shinikizo la kung’olewa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga baada ya wizara yake kuhusishwa na zabuni tata ya mradi wa ufungaji wa vifaa vya mawasiliano kwenye vituo vua polisi.
Aidha, ripoti ya mwaka 2014/ 2015 iliyowasilishwa Aprili mwaka jana CAG Mussa Juma Assad iliibua uozo zaidi kwenye halmashauri, taasisi za Serikali na mashirika ya umma, ikibainisha kuwa nchi ina tatizo kubwa, zaidi ya watu wachache ambao wamekuwa wakishughulikiwa na Serikali ya Rais Magufuli.
Ripoti hiyo iligusa taasisi zilizowahi kuwa chini ya Wizara ya Elimu, Afya, Ardhi, Ujenzi, Mambo ya Nje na nyinginezo kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Pia ripoti hiyo inabainisha kuwa mapendekezo mengi ambayo CAG amekuwa akiyatoa kwa takribani miaka saba sasa, hayatekelezwi. Cha kujiuliza ni je, hivi yakitekelezwa nani atabaki salama?

Waliofukuzwa kazi na madiwani warejeshwa


Watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, ambao walifukuzwa kazi Mei mwaka jana wamerejeshwa kazini.
Hatua hiyo inatokana na watumishi hao kushinda rufaa waliyokata kwenye vyombo vya juu vya utumishi.
Watumishi hao ni Mhandisi  Edwin Magiri, Ofisa Elimu Shule za Msingi, Beth Mlaki na Kaimu Ofisa Ununuzi Eliada Msana ambao walifukuzwa kazi na baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa makosa tofauti.
Baraza la madiwani chini ya mwenyekiti wake, Mwalingo Kisemba lilifikia uamuzi wa kuwafukuza kazi baada ya kujiridhisha na ripoti ya kamati ilizounda kuchunguza tuhuma dhidi yao.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla  ametangaza leo Jumanne uamuzi wa kuwarejesha kazini watumishi hao kwenye kikao cha baraza la madiwani ili kutoa mrejesho wa hatua iliyochukuliwa na  vyombo vya juu vilivyosikiliza rufaa zao chini ya Tume ya Utumishi.
Amesema vyombo hivyo vimebaini utaratibu uliotumiwa na madiwani ulikuwa na kasoro, hivyo wamerejeshwa kazini na watalipwa stahiki zao zote tangu walipofukuzwa.

Siasa zetu Zifuate utandawazi wenye sura ya ubinadamu


Tunapigana vita ya uchumi, tukiwa kwenye dunia ya leo ambayo ni ya utandawazi. Ni dunia ambayo inatanguliza faida kuliko ubinadamu. Ni wazi ili tufanikiwe ni muhimu kuwa wapole kama njiwa na wajanja kama nyoka.
Wale wenye kupata nafasi ya kumsogelea Rais wetu John Magufuli na kuongea naye, ni muhimu wayajadili haya. Wasipende kumfurahisha, bali wamsaidie kutafakari, kwamba tunahitaji furaha ya taifa zima, zaidi ya furaha ya mtu mmojammoja.
Vita ya uchumi na hasa kwenye dunia ya utandawazi ni pana na ina wadau wengi, hivyo kuna mambo mengi ya kufanyika na tunahitaji nguvu za pamoja.

Mashirika ya kimataifa yanayouongoza utandawazi (Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Biashara Duniani (WTO) ni lazima yabadilishe mfumo wake vinginevyo yanaielekeza Tanzania, kwenye utumwa.
Utumwa ni kitu kibaya. Tulipokuwa watoto tulikuwa tukiimba wimbo wa “Utumwa ni kitu kibaya, tuliuzwa kama samaki, samaki wa kwetu wanono si kama wale wa Amerika...” Wimbo wenyewe hasa ulikuwa: Afrika nakutamani nikikumbuka sifa zako, ingawa niko nchi za mbali, furaha haishi moyoni. Ni wazi hizi zilikuwa nyimbo za watumwa.
Utumwa ni hali ya mtumishi asiyelipwa chochote na ambaye amefungwa, hana sauti, hana uhuru na huweza kutendwa lolote na bwana wake.  Utumwa hauna sura ya ubinadamu.
Siwezi kupendekeza Tanzania tuachane na utandawazi pamoja na hali hii mbaya inayojitokeza ya kutuelekeza kwenye utumwa. Hatuwezi kuutupilia mbali utandawazi na tukaendelea kuishi kwenye ‘kijiji kimoja’ na mataifa mengine ya dunia hii. 
Hali ya sasa hivi inaonyesha kwamba tunauhitaji utandawazi na ‘utandawizi’ unatuhitaji. Jambo la kuzingatia ni kwamba tunauhitaji utandawazi wenye sura ya ubinadamu.
Tunauhitaji utandawazi wenye uwezo wa kusukuma mbele gurudumu la uwajibikaji, uwazi, ukweli, kujitegemea, demokrasia na maendeleo. Utandawazi unaoweza kuisaidia Tanzania, kubadilika: Maisha ya watu maskini yakawa bora, kila raia akapata elimu bora, huduma bora ya afya na mambo mengine muhimu kama maji, umeme, chakula na mawasiliano.
Tunahitaji utandawazi unaotanguliza huduma za kijamii. Usafiri wa umma ulio bora na si kama sasa hivi ambavyo usafiri wa umma umewekwa mikononi mwa watu binafsi ambao wanaangalia kutengeneza faida zaidi ya kutoa huduma. Ukiangalia daladala zetu zote zinazotoa huduma ndani ya Jiji la Dar es Salaam, zipo tu kumtafutia mwenye mali fedha na wala si huduma na kuhakikisha mteja anasafiri kwa raha na furaha. Hali ni mbaya kiasi kwamba Watanzania wanaamini kwamba usafiri wa umma ni lazima kubanana na kusukumana wakati wa kuingia kwenye daladala.
Wakati mwingine mvua ikinyesha hakuna tofauti ya kuwa kwenye gari na kuwa nje, maana daladala nyingine hazina madirisha na nyingine zinavuja. Viti vimechoka na karibia kila kitu kimechoka na wakati mwingine ajali zinazotokea zinasababishwa na hali ya magari yenyewe kutofanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.
Nchi nyingine duniani, usafiri wa umma unabaki mikononi mwa Serikali. Ili jamii ipate huduma nzuri ya usafiri ni lazima Serikali itoe ruzuku. Kwa kigezo kwamba Serikali haitangulizi faida wakati wa kutoa huduma za kijamii, bali inamtanguliza mwananchi. Kinyume na watu binafsi wakiendesha sekta hii ya usafiri wa umma, wanatanguliza faida na mwishoni ndio wanaangalia huduma.
Kwa njia hii, usafiri wa umma hapa Tanzania utaendelea kuwa mbaya. Tungekuwa na usafiri wa umma mzuri, hata msongamano wa magari ungepungua. Watu wangeyaacha magari yao na kupanda usafiri wa umma. Lakini hali ilivyo sasa hivi kupanda usafiri wa umma ni kuishiwa au kuonekana mtu wa chini katika jamii.
Hoja hapa si kuupinga utandawazi, bali ni kuonyesha ukweli kwamba mfumo wake hauna sura ya ubinadamu. Ni mfumo wa kuangalia kutengeneza faida, kabla ya kuangalia huduma. Na mbaya zaidi wale wanaotufundisha utandawazi, walihakikisha kwanza huduma zote za kijamii zinakuwa nzuri, na mpaka sasa kuna huduma ambazo hawakubali kuziweka mikononi mwa watu binafsi zinabaki chini ya Serikali. Sisi tunataka kila kitu kiwe mikononi mwa watu binafsi.
Mfumo wa sasa wa utandawazi unawaruhusu watu wachache, nchi chache na kampuni chache kutajirika kupindukia wakati mamilioni ya watu duniani wanaogelea kwenye dimbwi la umaskini.
Itakuwa ni ndoto kutupilia mbali ukweli wa ugumu uliopo wa kuibadilisha hali ya sasa. Mabadiliko ni kitu kigumu na kina gharama zake. Kila mtu anaweza kujipima mwenyewe  inavyokuwa vigumu kubadilisha tabia moja na kukumbatia nyingine; kuacha ubinafsi na kuwahudumia watu wengine, kuacha ukabila na kuyakumbatia makabila na mtaifa mengine, kukubali maoni ya watu wengine, kuwakubali watu wengine jinsi walivyo nk, ni vigumu na inaumiza kubadilika.
Mashirika ya kimataifa yanalazimika kuchukua uamuzi ambao ni mgumu na wa kuumiza  wa kubadilisha mifumo yake ili mchango wake uweze kujenga utandawazi wenye sura ya ubinadamu. Kinyume chake ni kushindwa kujenga dunia yenye sura ya ubinadamu.
Ugaidi ni matokeo ya utandawazi usiokuwa na sura ya ubinadamu. Hili linahitaji makala yanayojitegemea.

Mfano IMF, isikazanie tu uimara wa uchumi katika nchi zinazoendelea, bila kuangalia upatikanaji wa ajira katika nchi hizo. Watu wengi wanapoteza kazi kutokana na mashinikizo na masharti ya IMF na Benki ya Dunia. Hawa watu watashughulikiwa vipi?
Ni tatizo na mzigo mkubwa wa nchi zinazoendelea. Watashindwa kuendesha maisha yao, watakuwa majambazi na kujiingiza kwenye biashara ya dawa za kulevya, biashara ya kuwatorosha watu na kuwapeleka kwenye nchi zilizoendelea ili kuwatumikisha na kuuza miili yao, watajiingiza kwenye matendo ya ugaidi na kuivuruga dunia nzima.
IMF isikazanie ushuru, kwamba nchi zinazoendelea zikusanye kwa nguvu zote ushuru katika nchi zao, bila kuangalia uboreshwaji wa sera ya umilikaji wa ardhi katika nchi zinazoendelea. Katika nchi hizi watu wachache wanamiliki ardhi au wana uwezo wa kuiendeleza ardhi na walio wengi wanabaki kuwa  vibarua.
Shinikizo na ubinafsishaji na uwekezaji linalowekwa na IMF katika nchi zinazoendelea, linachangia watu maskini kuendelea kunyong’onyea na kupoteza uwezo wa kutumia na kumiliki ardhi.
IMF, inakazana kutoa mikopo kufuatana na ushauri wa wataalamu wake wa nchi zilizoendelea bila kufuata matakwa ya nchi husika kama kuboresha elimu na afya.
IMF, inajua fika kwamba nchi yenye Serikali fisadi na viongozi wala rushwa haiwezi kuendesha vizuri zoezi zima la ubinafsishaji.
Viongozi walewale walioshindwa kusimamia vizuri uendeshaji wa mashirika ya umma ndio haohao wanaosimamia kuyauza mashirika hayo. Matokeo yake mashirika yanauzwa kwa bei ndogo, kwa upendeleo,  na mara nyingi kwa wawekezaji wa kutoka nje ya nchi ambao wako tayari kutoa chochote (rushwa) kwa viongozi.
Matokeo ya zoezi hili ni kuweka uhai wa uchumi mikononi mwa wawekezaji kutoka nchi za nje, ambao kazi yao kubwa ni kulinda maslahi yao. Nchi isipotawala uchumi wake, inakuwa si huru tena.
Utandawazi usiokuwa na sura ya ubinadamu unayaruhusu makampuni makubwa kama Coca-cola, Pepsi na Unilever kutawala soko la dunia nzima la vinywaji baridi. Hii inaua kabisa jitihada za viwanda vidogo katika nchi zinazoendelea. Utandawazi usiokuwa na sura ya ubinadamu unazalisha maskini wengi. Si ukweli kwamba maskini ni wavivu na hawafanyi kazi. Na maskini wengine wanafanya kazi sana na wakati mwingine katika mazingira magumu, wengi wao wanajikuta katika mzunguko wa maisha magumu yasiyokuwa na mwisho: Bila chakula cha kutosha na chenye kiwango kinachokubalika kimataifa, mtu hawezi kuwa na afya bora ya kumwezekesha kufanya kazi kwa masaa yanayokubalika kimataifa, bila kufanya kazi kwa masaa yanayokubalika kimataifa ni vigumu kupata kipato cha kukidhi mahitaji muhimu kama kulipa karo ya watoto, bila kulipa karo, watoto hawawezi kupata elimu. Ni Watanzania wangapi sasa hivi wataweza kumudu kusomesha watoto wao hadi chuo kikuu? Mfumo mpya wa kulipia gharama za chuo kikuu, ni wangapi wanaweza kuukabili? Matokeo watoto watabaki bila elimu na watalazimika kuishi kwenye umaskini. Hivyo umaskini unakuwa ni kitu cha kurithi kizazi hadi kingine.
 Umaskini unazaa unyonge na kutojiamini. Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia 2000, katika zoezi lililoitwa “the voice of the poor” (sauti ya maskini tafsiri ni yangu) ulibainisha kwamba maskini wanajihisi kutokuwa na sauti, wananyanyaswa na hawana uwezo wa kuendesha mambo yao wenyewe. Wanafunikwa kwa nguvu za uchumi zilizo juu ya uwezo wao kuzidhibiti. Kwa maneno mengine wanaishi katika utumwa.
 Utandawazi wenye sura ya ubinadamu ungesambaza mazuri ya utandawazi. Nchi zilizoendelea zimefika zilipo kwa kusaidiwa na kuwepo kwa Serikali bora na viongozi imara na wenye mwelekeo.
Mafanikio haya yalisukumwa na demokrasia, elimu, uwazi, ukweli na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari. Mfano nchini Marekani, demokrasia, elimu, uwazi, ukweli na uhuru wa vyombo vya habari si zawadi ya serikali kwa wananchi, bali ni haki ya kila raia wa Amerika.
Je, Amerika, imezisaidiaje nchi zinazoendelea kama Tanzania, kiasi kwamba kila Mtanzania akatambua kwamba demokrasia, uwazi, ukweli, elimu na uhuru wa vyombo  vya habari, uhuru wa kutoa maoni ni haki yake? 
La kusema hapa ni kwamba hata demokrasia Tanzania, bado ni kitendawili.
Mtu kuwa kwenye chama cha upinzani ni kama kufanya dhambi ya mauti. Nimesikia kwamba kuna baadhi ya viongozi wa dini wanaofundisha kwamba upinzani wa kisiasa ni dhambi.
Wanawalinganisha wapinzani  wa kisiasa na wapinzani waliokuwa wakijitokeza kwenye dini zao katika historia. Tumeshuhudia vituko vingi wanavyofanyiwa watu waliojitenga na CCM na kujiunga na vyama vya upinzani, hadi wanapiga magoti kuomba msamaha wa kurudishwa ndani ya kundi.
Wakati tunayashinikiza mashirika ya kimataifa kubadilisha mifumo yake na kuyataka kutuletea utandawazi wenye sura ya ubinadamu, ni lazima na sisi tuanze kubadilika. Tujifunze kuwajibika, tujifunze kuwa wazi, tujifunze kusema ukweli, tujifunze kulitanguliza taifa letu kuliko kutanguliza sifa, tamaa na maslahi binafsi. Ni lazima sisi pia tuonyeshe utayari wa kupokea utandawazi wenye sura ya ubinadamu. Vinginevyo tunajiingiza kwenye Utumwa, na utumwa daima hauna sura ya ubinadamu.
Tunapompongeza Rais wetu Magufuli, kwa kazi kubwa anayoifanya. Ni muhimu pia kumkumbusha dunia yetu.  Ni muhimu  kutambua kwamba pamoja na mabadiliko tunayoyafanya kama taifa, hatuwezi kuishi nje ya dunia hii ya utandawazi. Tuwe wapole kama njiwa, lakini wajanja kama nyoka. Ni muhimu kujenga taifa imara ndani ya utandawazi wenye sura ya ubinadamu. Utandawazi unaolinda uhai na heshima ya kila Mtanzania.

Padri Privatus Karugendo.