Wednesday, September 13

Siasa zetu Zifuate utandawazi wenye sura ya ubinadamu


Tunapigana vita ya uchumi, tukiwa kwenye dunia ya leo ambayo ni ya utandawazi. Ni dunia ambayo inatanguliza faida kuliko ubinadamu. Ni wazi ili tufanikiwe ni muhimu kuwa wapole kama njiwa na wajanja kama nyoka.
Wale wenye kupata nafasi ya kumsogelea Rais wetu John Magufuli na kuongea naye, ni muhimu wayajadili haya. Wasipende kumfurahisha, bali wamsaidie kutafakari, kwamba tunahitaji furaha ya taifa zima, zaidi ya furaha ya mtu mmojammoja.
Vita ya uchumi na hasa kwenye dunia ya utandawazi ni pana na ina wadau wengi, hivyo kuna mambo mengi ya kufanyika na tunahitaji nguvu za pamoja.

Mashirika ya kimataifa yanayouongoza utandawazi (Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Biashara Duniani (WTO) ni lazima yabadilishe mfumo wake vinginevyo yanaielekeza Tanzania, kwenye utumwa.
Utumwa ni kitu kibaya. Tulipokuwa watoto tulikuwa tukiimba wimbo wa “Utumwa ni kitu kibaya, tuliuzwa kama samaki, samaki wa kwetu wanono si kama wale wa Amerika...” Wimbo wenyewe hasa ulikuwa: Afrika nakutamani nikikumbuka sifa zako, ingawa niko nchi za mbali, furaha haishi moyoni. Ni wazi hizi zilikuwa nyimbo za watumwa.
Utumwa ni hali ya mtumishi asiyelipwa chochote na ambaye amefungwa, hana sauti, hana uhuru na huweza kutendwa lolote na bwana wake.  Utumwa hauna sura ya ubinadamu.
Siwezi kupendekeza Tanzania tuachane na utandawazi pamoja na hali hii mbaya inayojitokeza ya kutuelekeza kwenye utumwa. Hatuwezi kuutupilia mbali utandawazi na tukaendelea kuishi kwenye ‘kijiji kimoja’ na mataifa mengine ya dunia hii. 
Hali ya sasa hivi inaonyesha kwamba tunauhitaji utandawazi na ‘utandawizi’ unatuhitaji. Jambo la kuzingatia ni kwamba tunauhitaji utandawazi wenye sura ya ubinadamu.
Tunauhitaji utandawazi wenye uwezo wa kusukuma mbele gurudumu la uwajibikaji, uwazi, ukweli, kujitegemea, demokrasia na maendeleo. Utandawazi unaoweza kuisaidia Tanzania, kubadilika: Maisha ya watu maskini yakawa bora, kila raia akapata elimu bora, huduma bora ya afya na mambo mengine muhimu kama maji, umeme, chakula na mawasiliano.
Tunahitaji utandawazi unaotanguliza huduma za kijamii. Usafiri wa umma ulio bora na si kama sasa hivi ambavyo usafiri wa umma umewekwa mikononi mwa watu binafsi ambao wanaangalia kutengeneza faida zaidi ya kutoa huduma. Ukiangalia daladala zetu zote zinazotoa huduma ndani ya Jiji la Dar es Salaam, zipo tu kumtafutia mwenye mali fedha na wala si huduma na kuhakikisha mteja anasafiri kwa raha na furaha. Hali ni mbaya kiasi kwamba Watanzania wanaamini kwamba usafiri wa umma ni lazima kubanana na kusukumana wakati wa kuingia kwenye daladala.
Wakati mwingine mvua ikinyesha hakuna tofauti ya kuwa kwenye gari na kuwa nje, maana daladala nyingine hazina madirisha na nyingine zinavuja. Viti vimechoka na karibia kila kitu kimechoka na wakati mwingine ajali zinazotokea zinasababishwa na hali ya magari yenyewe kutofanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.
Nchi nyingine duniani, usafiri wa umma unabaki mikononi mwa Serikali. Ili jamii ipate huduma nzuri ya usafiri ni lazima Serikali itoe ruzuku. Kwa kigezo kwamba Serikali haitangulizi faida wakati wa kutoa huduma za kijamii, bali inamtanguliza mwananchi. Kinyume na watu binafsi wakiendesha sekta hii ya usafiri wa umma, wanatanguliza faida na mwishoni ndio wanaangalia huduma.
Kwa njia hii, usafiri wa umma hapa Tanzania utaendelea kuwa mbaya. Tungekuwa na usafiri wa umma mzuri, hata msongamano wa magari ungepungua. Watu wangeyaacha magari yao na kupanda usafiri wa umma. Lakini hali ilivyo sasa hivi kupanda usafiri wa umma ni kuishiwa au kuonekana mtu wa chini katika jamii.
Hoja hapa si kuupinga utandawazi, bali ni kuonyesha ukweli kwamba mfumo wake hauna sura ya ubinadamu. Ni mfumo wa kuangalia kutengeneza faida, kabla ya kuangalia huduma. Na mbaya zaidi wale wanaotufundisha utandawazi, walihakikisha kwanza huduma zote za kijamii zinakuwa nzuri, na mpaka sasa kuna huduma ambazo hawakubali kuziweka mikononi mwa watu binafsi zinabaki chini ya Serikali. Sisi tunataka kila kitu kiwe mikononi mwa watu binafsi.
Mfumo wa sasa wa utandawazi unawaruhusu watu wachache, nchi chache na kampuni chache kutajirika kupindukia wakati mamilioni ya watu duniani wanaogelea kwenye dimbwi la umaskini.
Itakuwa ni ndoto kutupilia mbali ukweli wa ugumu uliopo wa kuibadilisha hali ya sasa. Mabadiliko ni kitu kigumu na kina gharama zake. Kila mtu anaweza kujipima mwenyewe  inavyokuwa vigumu kubadilisha tabia moja na kukumbatia nyingine; kuacha ubinafsi na kuwahudumia watu wengine, kuacha ukabila na kuyakumbatia makabila na mtaifa mengine, kukubali maoni ya watu wengine, kuwakubali watu wengine jinsi walivyo nk, ni vigumu na inaumiza kubadilika.
Mashirika ya kimataifa yanalazimika kuchukua uamuzi ambao ni mgumu na wa kuumiza  wa kubadilisha mifumo yake ili mchango wake uweze kujenga utandawazi wenye sura ya ubinadamu. Kinyume chake ni kushindwa kujenga dunia yenye sura ya ubinadamu.
Ugaidi ni matokeo ya utandawazi usiokuwa na sura ya ubinadamu. Hili linahitaji makala yanayojitegemea.

Mfano IMF, isikazanie tu uimara wa uchumi katika nchi zinazoendelea, bila kuangalia upatikanaji wa ajira katika nchi hizo. Watu wengi wanapoteza kazi kutokana na mashinikizo na masharti ya IMF na Benki ya Dunia. Hawa watu watashughulikiwa vipi?
Ni tatizo na mzigo mkubwa wa nchi zinazoendelea. Watashindwa kuendesha maisha yao, watakuwa majambazi na kujiingiza kwenye biashara ya dawa za kulevya, biashara ya kuwatorosha watu na kuwapeleka kwenye nchi zilizoendelea ili kuwatumikisha na kuuza miili yao, watajiingiza kwenye matendo ya ugaidi na kuivuruga dunia nzima.
IMF isikazanie ushuru, kwamba nchi zinazoendelea zikusanye kwa nguvu zote ushuru katika nchi zao, bila kuangalia uboreshwaji wa sera ya umilikaji wa ardhi katika nchi zinazoendelea. Katika nchi hizi watu wachache wanamiliki ardhi au wana uwezo wa kuiendeleza ardhi na walio wengi wanabaki kuwa  vibarua.
Shinikizo na ubinafsishaji na uwekezaji linalowekwa na IMF katika nchi zinazoendelea, linachangia watu maskini kuendelea kunyong’onyea na kupoteza uwezo wa kutumia na kumiliki ardhi.
IMF, inakazana kutoa mikopo kufuatana na ushauri wa wataalamu wake wa nchi zilizoendelea bila kufuata matakwa ya nchi husika kama kuboresha elimu na afya.
IMF, inajua fika kwamba nchi yenye Serikali fisadi na viongozi wala rushwa haiwezi kuendesha vizuri zoezi zima la ubinafsishaji.
Viongozi walewale walioshindwa kusimamia vizuri uendeshaji wa mashirika ya umma ndio haohao wanaosimamia kuyauza mashirika hayo. Matokeo yake mashirika yanauzwa kwa bei ndogo, kwa upendeleo,  na mara nyingi kwa wawekezaji wa kutoka nje ya nchi ambao wako tayari kutoa chochote (rushwa) kwa viongozi.
Matokeo ya zoezi hili ni kuweka uhai wa uchumi mikononi mwa wawekezaji kutoka nchi za nje, ambao kazi yao kubwa ni kulinda maslahi yao. Nchi isipotawala uchumi wake, inakuwa si huru tena.
Utandawazi usiokuwa na sura ya ubinadamu unayaruhusu makampuni makubwa kama Coca-cola, Pepsi na Unilever kutawala soko la dunia nzima la vinywaji baridi. Hii inaua kabisa jitihada za viwanda vidogo katika nchi zinazoendelea. Utandawazi usiokuwa na sura ya ubinadamu unazalisha maskini wengi. Si ukweli kwamba maskini ni wavivu na hawafanyi kazi. Na maskini wengine wanafanya kazi sana na wakati mwingine katika mazingira magumu, wengi wao wanajikuta katika mzunguko wa maisha magumu yasiyokuwa na mwisho: Bila chakula cha kutosha na chenye kiwango kinachokubalika kimataifa, mtu hawezi kuwa na afya bora ya kumwezekesha kufanya kazi kwa masaa yanayokubalika kimataifa, bila kufanya kazi kwa masaa yanayokubalika kimataifa ni vigumu kupata kipato cha kukidhi mahitaji muhimu kama kulipa karo ya watoto, bila kulipa karo, watoto hawawezi kupata elimu. Ni Watanzania wangapi sasa hivi wataweza kumudu kusomesha watoto wao hadi chuo kikuu? Mfumo mpya wa kulipia gharama za chuo kikuu, ni wangapi wanaweza kuukabili? Matokeo watoto watabaki bila elimu na watalazimika kuishi kwenye umaskini. Hivyo umaskini unakuwa ni kitu cha kurithi kizazi hadi kingine.
 Umaskini unazaa unyonge na kutojiamini. Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia 2000, katika zoezi lililoitwa “the voice of the poor” (sauti ya maskini tafsiri ni yangu) ulibainisha kwamba maskini wanajihisi kutokuwa na sauti, wananyanyaswa na hawana uwezo wa kuendesha mambo yao wenyewe. Wanafunikwa kwa nguvu za uchumi zilizo juu ya uwezo wao kuzidhibiti. Kwa maneno mengine wanaishi katika utumwa.
 Utandawazi wenye sura ya ubinadamu ungesambaza mazuri ya utandawazi. Nchi zilizoendelea zimefika zilipo kwa kusaidiwa na kuwepo kwa Serikali bora na viongozi imara na wenye mwelekeo.
Mafanikio haya yalisukumwa na demokrasia, elimu, uwazi, ukweli na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari. Mfano nchini Marekani, demokrasia, elimu, uwazi, ukweli na uhuru wa vyombo vya habari si zawadi ya serikali kwa wananchi, bali ni haki ya kila raia wa Amerika.
Je, Amerika, imezisaidiaje nchi zinazoendelea kama Tanzania, kiasi kwamba kila Mtanzania akatambua kwamba demokrasia, uwazi, ukweli, elimu na uhuru wa vyombo  vya habari, uhuru wa kutoa maoni ni haki yake? 
La kusema hapa ni kwamba hata demokrasia Tanzania, bado ni kitendawili.
Mtu kuwa kwenye chama cha upinzani ni kama kufanya dhambi ya mauti. Nimesikia kwamba kuna baadhi ya viongozi wa dini wanaofundisha kwamba upinzani wa kisiasa ni dhambi.
Wanawalinganisha wapinzani  wa kisiasa na wapinzani waliokuwa wakijitokeza kwenye dini zao katika historia. Tumeshuhudia vituko vingi wanavyofanyiwa watu waliojitenga na CCM na kujiunga na vyama vya upinzani, hadi wanapiga magoti kuomba msamaha wa kurudishwa ndani ya kundi.
Wakati tunayashinikiza mashirika ya kimataifa kubadilisha mifumo yake na kuyataka kutuletea utandawazi wenye sura ya ubinadamu, ni lazima na sisi tuanze kubadilika. Tujifunze kuwajibika, tujifunze kuwa wazi, tujifunze kusema ukweli, tujifunze kulitanguliza taifa letu kuliko kutanguliza sifa, tamaa na maslahi binafsi. Ni lazima sisi pia tuonyeshe utayari wa kupokea utandawazi wenye sura ya ubinadamu. Vinginevyo tunajiingiza kwenye Utumwa, na utumwa daima hauna sura ya ubinadamu.
Tunapompongeza Rais wetu Magufuli, kwa kazi kubwa anayoifanya. Ni muhimu pia kumkumbusha dunia yetu.  Ni muhimu  kutambua kwamba pamoja na mabadiliko tunayoyafanya kama taifa, hatuwezi kuishi nje ya dunia hii ya utandawazi. Tuwe wapole kama njiwa, lakini wajanja kama nyoka. Ni muhimu kujenga taifa imara ndani ya utandawazi wenye sura ya ubinadamu. Utandawazi unaolinda uhai na heshima ya kila Mtanzania.

Padri Privatus Karugendo.

No comments:

Post a Comment