Dar es Salaam. Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ameingia kwenye mjadala kuhusu hali mbaya ya elimu, lakini akijikita zaidi kwa kuangalia Bara la Afrika.
Suala la hali mbaya ya elimu limeibua mjadala tangu Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kupendekeza kuanzishwa kwa mjadala wa kitaifa kuhusu sekta ya elimu kutokana na matokeo mabaya ya shule za Serikali.
Lakini Kikwete aliangazia suala hilo katika wigo mpana zaidi wakati alipokuwa akizungumza kwenye kongamano lililopewa jina la “Mageuzi ya Afrika Katika Karne ya 21” lililoandaliwa na Taasisi ya Masomo ya Afrika ya Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani.
Kikwete, ambaye alikuwa mmoja wa wasemaji wakuu wanne kwenye kongamano hilo, alisema Afrika inaweza kuwa inapiga hatua katika kuendeleza elimu, lakini inahitaji kuongeza juhudi hasa kutoka elimu ya msingi hadi sekondari.
“Kwa kuangalia takwimu, Afrika ni bara la wahitimu wa elimu ya msingi,” alisema Kikwete katika mada yake kwenye kongamano hilo na kukaririwa na tovuti ya africanews.com.
“Ni asilimia 20 ya vijana wanaweza kwenda shule za sekondari. Kibaya zaidi, hata hao wachache wanaofanikiwa kwenda sekondari hawafanyi vizuri.
“Kwa wastani katika nchi nyingine duniani, karibu asilimia 30 ya wanafunzi wa elimu ya juu ya sekondari, wanakwenda vyuo vya ufundi stadi; barani Afrika ni chini ya asilimia 20.”
Wazungumzaji wengine katika kongamano hilo walikuwa John Agyekum Kuffor ambaye alikuwa Rais wa Ghana, Olesegun Obasanjo (Rais wa mstaafu wa Nigeria) na Carlos Verga (Waziri Mkuu mstaafu wa Cape Verde).
Kikwete pia alisisitiza haja ya kuweka mkazo katika kuwapa elimu wasichana wadogo, akisema, “Wakati wasichana wadogo wanapoolewa, wananyimwa fursa sawa ya kupata elimu.”
Rais huyo mstaafu alisema kuna haja ya kuweka mkazo katika teknolojia kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya Afrika kwa kuwekeza zaidi katika masomo ya teknolojia ya sayansi, uhandisi na hisabati (Stem).
Kikwete aliangazia zaidi matatizo ya elimu barani Afrika, lakini hoja kwamba hata hao wachache wanaovuka elimu ya msingi kwenda sekondari hawafanyi vizuri inalingana na kauli ya Rais mstaafu Mkapa na mkuu wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Casmir Rubagumya ambao wanaona janga hilo la elimu kwa kuangalia ubora wa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu na matokeo ya shule za Serikali.
Mkapa ambaye ni mkuu wa Udom, alisema kuna janga katika elimu nchini na kushauri kuitishwa kwa mdahalo wa wazi wa kitaifa utakaoshirikisha makundi yote ya jamii.
Mkapa alikuwa akizungumzia suala hilo kwa mara ya pili baada ya Novemba 11, 2017 kuwaambia washiriki wa kongamano la wanataaluma Udom, kwamba Tanzania haijaweka msukumo katika kutafakari upya mfumo wa elimu.
“Tunahitaji kufanya mapinduzi kwenye elimu,” alisema Mkapa.
“Ninaamini kabisa kwamba tuna crisis (janga). Ninasoma katika magazeti, ninaletewa presentation (mawasilisho) kutoka sekta binafsi, walimu, private university (vyuo binafsi). Napata pia minong’ono kutoka vyuo vya umma kwamba kuna crisis katika elimu.”
Mkapa alisema njia moja ya kujua mwenendo wa mambo ni kusoma barua za wasomaji, akitumia uzoefu wake wa uhariri katika magazeti ya Uhuru, Mzalendo, Daily News na Sunday News.
“Nimeendelea kusoma magazeti sana mpaka mke wangu ananilalamikia. Lakini (barua za wasomaji) nyingi zinalalamika zinasema hivyohivyo. Zinasema elimu yetu ina mushkeli,” alisema.
Alisema wapo watu wanaolalamika kuhusu lugha, ratiba, ushirikiano, lakini pia kuhusu ushirikishwaji wa wahitimu, wanaofanya kazi na wazazi ili kuamua Taifa linakwendaje katika elimu siku zijazo.
“Katika (shule) kumi za kwanza (katika matokeo ya mitihani ya kitaifa), ukiangalia unaweza kuwa na uhakika kuwa nane si za Serikali ni za watu binafsi. Kama Serikali ndio mhimili mkuu wa elimu, kuna kasoro gani?” alihoji.
Alishauri kuitishwa kwa mdahalo wa kitaifa ambao utashirikisha makundi yote na kusikia maoni yao badala ya kuwaachia wanataaluma pekee ambao alisema wanaegemea kwenye ujuzi wao.
Maoni kama hayo kuhusu hali mbaya ya kielimu pia yalitolewa na Profesa Rubagumya.
Katika habari iliyotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, Profesa Rubagumya anasema uzoefu wake wakati akiwa mkuu wa Udom ulimfungua macho kuhusu hali ya elimu nchini.
“Kipindi changu nikiwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma kilinifungua macho kujua hali ya elimu nchini inavyozidi kuwa mbaya. Kiwango cha wanafunzi tunaowapokea kutoka shule za sekondari kilikuwa kibaya zaidi ya nilichokiona Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” anasema Profesa Rubagumya katika ukurasa huo wa Facebook.
“Kila mwaka tulipokea mazao mabaya zaidi ya mwaka uliotangulia. Wanafunzi walikuwa hawawezi kuwasiliana vizuri ama kwa Kiswahili au Kiingereza. Tatizo halikuwa lugha pekee, bali kutokuwa na uwezo wa kufikiria vizuri kwa kutumia lugha yoyote.
“Wanafunzi pia walikuwa hawana ufahamu wa mambo ya kawaida ya msingi kuhusu dunia na hata kuhusu Tanzania. Siku moja nilistushwa baada ya kujua kwamba mwanafunzi wa mwaka wa pili wa chuo kikuu hakuwa akijua hata jina la Makamu wa Rais, kitu ambacho mtoto hata wa darasa la pili angetegemewa kuwa anakifahamu.”
Profesa anasema katika tukio jingine, mwanafunzi wa mwaka wa mwisho wa chuo kikuu ambaye masomo yake yalijikita katika Kiswahili, aliandika barua ambayo haikuwa inaeleweka.
“Hiki ni kitu ambacho mtu hawezi kukitatua chuo kikuu. Ni dalili za tatizo kubwa zaidi na la kimsingi zaidi katika mfumo mzima wa elimu nchini,” anasema.
“Na si tatizo linalokikabili Chuo Kikuu cha Dodoma pekee. Katika jukumu langu kama msimamizi wa mtihani wa nje, nilibaini tatizo hilohilo katika vyuo vikuu vingine.”
Anasema wanafunzi wa sasa ni wa kizazi tofauti ambao hawapendi maisha ya kisomi na wengi wao wanataka njia za mkato kupata vyeti.
“Mtindo huo unahusisha kuhonga wakati wa kutoka daraja moja kwenda jingine kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu. Kwa bahati mbaya, baadhi ya walimu na wazazi ni sehemu ya mchezo huu mchafu, ambao unaonyesha sababu za kuwa na vyeti vingi vya kughushi katika madaraja tofauti,” anasema.
“Pia tuna wanafunzi ambao wanawalipa watu wawaandikie tasnifu (dissertations). Hayo yote ni dalili zinazotia wasiwasi kuwa mfumo wa elimu haufanyi kazi vizuri.”