Saturday, April 28

Wabunge wahoji kufungiwa magazeti, nyimbo za wasanii

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza 

Dodoma. Wakati wabunge wakihoji sababu za Serikali kufungia magazeti, kutoweka kwa mwandishi wa habari na kufungia nyimbo za wasanii, Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeitaka kueleza lini itakamilisha kutunga kanuni za Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ili itekelezwe kikamilifu.
Walisema hayo jana bungeni mjini Dodoma wakichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka 2018/19 ambapo wizara imeomba kuidhinishiwa Sh33.3 bilioni.
Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Devotha Minja alisema kufungiwa kwa magazeti na Serikali kuanza utaratibu wa kusajili magazeti kila mwaka, si jambo sahihi na linalenga kudhoofisha vyombo vya habari nchini. “Katiba ya nchi inasema ni haki ya kila Mtanzania kupata taarifa, sasa kwa nini mnakuja na vigezo kuwa kila mwaka gazeti lisajiliwe upya. Hili ni makusudi tu kwamba yale ambayo yatakuwa hayaimbi mapambio ya Serikali mwaka unaofuata hayatapewa usajili. Rwanda ndio wenye utaratibu huu,” alisema Devotha ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari.
Alisema wakati magazeti hayo yakifungiwa, Bunge limekuwa likichagua picha za video za vikao vya Bunge kwa ajili ya vyombo vya habari na kubainisha kuwa video hizo zinakatwa katika maeneo ambayo wabunge wameikosoa Serikali.
Kuhusu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuanza kuzibana televisheni, ikiwa ni pamoja na kuzitoza faini alisema ni mwendelezo kama wa kufungia magazeti na hilo litasababisha wawekezaji kukimbia nchini.
Devotha pia alizungumzia matukio ya waandishi wa habari kupotea, kutekwa na kutishiwa maisha akihoji sababu za Serikali kutotoa matamko ya kulaani vitendo hivyo. Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku maarufu Musukuma alisema wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini wanaitangaza nchi lakini mwenendo wa kufungia nyimbo zao, huenda ukashusha juhudi zao.
“Kipindi cha hivi karibuni kumeibuka fungiafungia. Msanii anafanya kazi yake nzuri ikitokea akakosea kidogo kwa kuonyesha mpasuo anafungiwa. Mnafungia nyimbo kwa sababu ya mpasuo wakati mnakaa na kutazama nyimbo za akina Rihanna kwenye Youtube,” alisema Musukuma.
“Mnataka wasanii wetu wavae madera? Waziri ukiangalia wasanii wanafanya kazi nzuri, wanatumia gharama kubwa na wakikosea tu mpasuo wanafungiwa, lakini ukienda kule Samora mbona kuna wanawake wanavaa nguo zenye mipasuo na hawafungiwi,” alisema.
“Mngetafuta muda wa kuwapatia semina badala ya kuwaacha wanafanya kazi nzuri wanatumia gharama kubwa na wakikosea mnawafungia,” alisema Musukuma.
Majibu ya mawaziri
Akijibu hoja za wabunge kuhusu kufungiwa kwa baadhi ya nyimbo za wasanii, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza alisema baadhi ya wahusika hawazipeleki Basata kukaguliwa licha ya kuwapo kwa kanuni zinazowataka kupeleka kazi zao kabla ya kuzitoa. “Serikali haina ugomvi na wasanii, ina ugomvi na mmomonyoko wa maadili uliopo katika nyimbo zao,” alisema Shonza.
Aliwataka wasanii kuzingatia jambo hilo, akiwataka kuhakikisha wanapeleka nyimbo zao Basata kabla ya kuziachia katika vyombo mbalimbali vya habari.
Akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti hiyo, Dk Mwakyembe alisema kuwa kanuni za sheria mpya ya habari zimeshatungwa na tayari zimeanza kutumika.
Kuhusu kuanzisha Bodi ya Ithibati na Baraza Huru la Habari alisema uanzishwaji wake unategemea zaidi vyombo vya habari na kubainisha kuwa Serikali haiwezi kuanzisha kwa kuepuka watu kusema kuwa ni vya Serikali. “Lengo ni kutaka vyombo vya habari kujiendesha vyenyewe,” alisema.
Akizungumzia magazeti kusajiliwa kila mwaka, alisema husajiliwa mara moja tu na kwamba kila mwaka huwa zinatolewa leseni kwa kuwa yako mengi lakini mengine hayafanyi kazi.
Akijibu swali kuhusu vyombo vya habari kufungiwa, hasa magazeti, Dk Mwakyembe alisema Sheria ya Huduma za Habari inaeleza makosa ambayo vyombo vya habari vinaweza kufungiwa vikikiuka na vinapomaliza adhabu wahusika hujifunza na kutii sheria hiyo.

1 comment:

  1. Thanks for sharing, nice post! Post really provice useful information!

    Hương Lâm chuyên cung cấp máy photocopy và dịch vụ cho thuê máy photocopy giá rẻ, uy tín TP.HCM với dòng máy photocopy toshiba và dòng máy photocopy ricoh uy tín, giá rẻ.

    ReplyDelete