Mara nyingi jamii inapojadili hali ya elimu Zanzibar kila mtu au kikundi huwa na lake linalotafautiana na la mwenzake.
Huyu humlaumu yule na yule humkosoa mwingine. Kwa ufupi unachosikia ni masikitiko na lawama.
Ukitafakari utaona ari ya kusomesha na kuwajibika kwa walimu wengi imeshuka na walimu nao kuwa na malalamiko mengi ya maslahi na mazingira ya kazi.
Maadili ya hii taaluma yameshuka. Wapo walimu, kama Rais Ali Mohamed Shein alivyoeleza, wamezigeuza shule vituo vya ujasiriamali vya kuuzia bagia, mbatata za urojo, chapati na maandazi.
Walimu wachache wasiojali maadili yao ya kazi hushughulika zaidi kuuza biashara walizotoka nazo majumbani kwao badala ya kukamata chaki kusomesha.
Taarifa zinaonyesha hata walimu wanaoishi karibu na shule walizopangiwa wamekuwa wakipokea mishahara wakati hawaendi kusomesha.
Mwishowe unabaki kujiuliza kama hali ndiyo hivi nini kifanyike ili masikitiko yaondoke na jamii iridhike na kiwango cha elimu.
Miongoni mwa yanayosikika ni uhaba wa walimu na miongoni mwa waliopo hawana sifa za taaluma hii, madarasa yamefurika (mengine yanao wanafunzi 70 au zaidi) na mazingira ya shule nyingi sio rafiki.
Pia, upo uhaba mkubwa wa vifaa vya kufundishia, kama vile vya maabara, nidhamu kupungua, wazazi kutofuatilia mahudhurio na maendeleo ya watoto wao na ushirikiano wao mdogo na walimu.
Vilevile hatuwezi kusahau uduni wa maslahi ya walimu na mengi wanayoahidiwa lakini hayatekelezwi.
Ni muhimu yote yaliyoelezwa, kujadiliwa hadharani na si pembeni na kutolewa maoni ya nini kifanyike.
Kwa bahati nzuri yote, ya kufurahisha na ya kusikitisha, yaliwekwa wazi hivi karibuni katika mkutano mkuu wa sita wa walimu uliofanyika Zanzibar.
Hali ya elimu si nzuri na ni haki ya kila mzalendo mkweli kuilalamikia, lakini lawama pekee hazitoshi. Kila mtu ajiulize anatoa mchango gani kusaidia kuondoka hapa tulipo.
Kazi ya kulaumu ni rahisi na nyepesi, bali ile ya kuondoa tatizo lililopo ndiyo mbinde.
Matokeo ya mtihani ya karibuni ya kitaifa sio ya kuridhisha, ijapokuwa wapo wanaokingia kifua na kusema sio mbaya sana.
Ni vizuri walimu kujitathmini na kukosoana na kurekebishana. Mwenendo wa baadhi yao kuchukua mishahara wakati hawaendi kusomesha au kutumia muda mwingi nje ya shule kwa shughuli binafsi au kujihusisha na bishara badala ya kusomesha ni wizi wa mchana.
Walimu kama hawa wanapaswa sio tu kufukuzwa kazi bali kushtakiwa kwa kupata fedha kwa kutumia hadaa.
Mtindo wa walimu kwenda shule na vikapu vya maandazi na visheti badala ya vitabu lazima ukomeshwe. Shule ni vituo vya elimu na si biashara.
Serikali nayo itimize wajibu wake na sio kila siku kutoa ahadi zisizotekelezwa juu ya madai halali ya walimu kama ya nyongeza za mihashara, posho za usafiri na likizo ambazo zimeainishwa kisheria, lakini hawazipati.
Si haki kumlaumu mwalimu kwa kutotimiza wajibu wakati Serikali inashindwa au haitaki kuwawekea mazingira yatakayopelekea kuona kazi yao inaheshimiwa na kuthaminiwa.
Kwa muda mrefu walimu wamesema wanashangazwa kuona wafanyakazi wa sekta nyingine za Serikali wanapata nyongeza za mishahara, posho na marupurupu bila ya bughudha, lakini kwao wao inakuwa nongwa.
Huu ni unyonge ambao hakuna anayeweza kuuvumilia na lazima uondolewe.
Lililonisikitisha ni kumsikia Rais wa Zanzibar akishangaa kuambiwa agizo lake la mwaka jana kwa Hazina ya Zanzibar na Wizara ya Elimu kuwalipa walimu malimbikizo yao ya malipo ya miaka mitatu halijatekelezwa.
Huu ni uzembe usiokubalika kwa sababu wahusika wameshindwa hata kutoa taarifa kwa nini hili halikutimizwa na ilikuwaje hata malimbikizo ya watumishi wengi wa Serikali au wajumbe wa Baraza la Wawakilishi hayawekwi kiporo kama tunavyoona kwa walimu.
Serkali inapaswa kuhakikisha inaweka mfumo mzuri wa ukaguzi wa shule zetu.
Nilishangaa siku moja kumsikia mwalimu mmoja anasema wanajitayarisha kuwapokea wakaguzi wa shule yao.
Ukaguzi sahihi huwa wa kushtukiza ili ionekane hali halisi ya shule. Pakiwepo taarifa ya awali lini ukaguzi utafanyika ni sawa na kumwambia mwizi weka nyumba yako sawa tunakuja kesho kukupekua.
Tatizo la madawati na msongamano katika madarasa ni la zaidi ya miaka 30 sasa na kila siku tunasikia juhudi zinafanyika kulimaliza.
Hii ni dosari na haihitaji tena ahadi, kinachotakiwa ni vitendo vya marekebisho.
Tusisahau kuwa aliyezoea kuandika akiwa amekaa kwenye sakafu hupata shida kufanya mtihani akikaa juu ya kiti na meza.
Hali hii inachangia watoto kupata maradhi ya mgongo kuokana na kujipinda wanapoandika wakiwa wamekaa chini.
Vilevile msongamano wa wanafunzi unampa taabu mwalimu kusomesha. Katika mfumo unaokubalika, darasa halitarajiwi kuwa na kuzidi wanafunzi 40. Fikiri hali inakuwaje kama darasa lina wanafunzi 100?
Hatua ya Serikali ya kutangaza elimu bure ni nzuri na inasaidia wanyonge, lakini gharama zake ni kubwa.
Hii inajidhihirisha wazi katika matokeo ya mtihani ambapo watoto wa shule binafsi zinazotoza ada hufanya vizuri zaidi kuliko wenzao wa shule za serikali.
Labda baada ya kuliona hili ndiyo mawaziri, viongozi wengi wa Serikali na makampuni na wafanya biashara wanawapeleka watoto wao kusoma shule binafsi nchini na nje.
Wanaobaki katika shule za Serikali ni watoto wa pangu pakavu na kauka nikuvae. Nitafurahi kupewa orodha ya viongozi wa serikali na zaidi wa Wizara ya Elimu ambao watoto wao wanasoma katika shule za serikali. Tuache kudanganyana.
Rais Shein alitoa takwimu kuonyesha bajeti ya Wizara ya Elimu Zanzibar imekuwa ikiongezeka kila mwaka. Hivi ndivyo inavyohitajika kufanyika kama kweli tunataka maendeleo.
Lakini suala ni kiwango gani cha fedha za bajeti zinazoidhinishwa na Baraza la Wawakilishi hutolewa kwa Wizara ya Elimu?