Wednesday, March 14

Maadili ya uchaguzi na migogoro katika uchaguzi


“Migogoro ya uchaguzi ni asili ya chaguzi. Changamoto katika uchaguzi, mwenendo au matokeo yake, haipaswi kuonekana kama udhaifu wa mfumo wa uchaguzi, bali ni uthibitisho wa nguvu na uwazi wa mfumo wa kisiasa.
“Kwa hiyo kuongezeka kwa aina na idadi ya migogoro inayohusiana na uchaguzi hutokea kwa kiasi kikubwa kutokana na ongezeko la umma kuelewa mchakato wa kurekebisha mambo.”
Haya ni maneno ya Mwanasheria kutoka Ofisi ya Taasisi za Kidemokrasia na Haki za Binadamu (ODIHR) ya nchini Poland, Denis Petit aliyoyaandika kwenye andiko lake “Kutatua migogoro ya uchaguzi.”
Maneno haya ya Denis Petit yanathibitisha historia ya kuanzishwa kwa Maadili ya Uchaguzi katika uchaguzi hapa nchini ambayo moja ya malengo yake ilikuwa ni kutatua migogoro inayojitokeza katika chaguzi.
Migogoro ya uchaguzi ni hali ya kutoelewana na malalamiko yanayoibuka kabla, wakati na baada ya uchaguzi baina ya mgombea wa chama kimoja na mgombea wa chama kingine au baina ya chama kimoja na chama kingine.
Msingi wa migogoro ya uchaguzi ni ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi na ufanyaji wa vitendo vilivyokatazwa katika uchaguzi kwa makubaliano baina ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Serikali, vyama vya siasa na wagombea.
Historia ya Maadili ya Uchaguzi ilianza kutokana na changamoto zilizojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 kati ya wagombea wa vyama tofauti na kati ya chama na chama kingine.
Hali hiyo iliifanya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuandaa mapendekezo ya Mwongozo wa Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2000 ili kuweka msingi wa mazingira sawa ya ushindani.
Lengo mahususi la kuandaa maadili hayo ni kuhakikisha chaguzi zinafanyika katika mazingira ya usawa, haki na amani, hivyo kusaidia katika kujenga demokrasia imara katika chaguzi.
Mapendekezo hayo yalijadiliwa na wawakilishi wa vyama vya siasa na Serikali Julai 31, 2000 na hatimaye Tume, vyama vya siasa na Serikali walitia saini Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2000.
Hata hivyo, maadili haya hayakuwa na nguvu ya kisheria kwa kuwa yalitumika kama mwongozo tu wa mambo yanayoruhusiwa na yanayokatazwa kufanywa wakati wa uchaguzi ambao uliandaliwa baada ya Tume, Serikali, vyama vya siasa na wagombea kukubaliana na kusaini maadili hayo.
Maadili haya yamekuwa yakifanyiwa mabadiliko na kuboreshwa kila ifikapo Uchaguzi Mkuu kutokana na changamoto mpya zinazojitokeza uchaguzi mbalimbali.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, marekebisho ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 yalifanyika na Kifungu cha 124 A kiliundwa kuyapa nguvu ya kisheria Maadili ya Uchaguzi.
Kifungu hicho kiliipa Tume jukumu la kuandaa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi na kuzichapisha kwenye Gazeti la Serikali, baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa na Serikali.
Kanuni hizo zilielekeza kuandaliwa maadili ya vyama vya siasa na Tume wakati wa kampeni na wakati wa uchaguzi na mbinu za utekelezaji wa kanuni hizo.
Pamoja na kuilazimisha Tume na Serikali kutekeleza kifungu hicho, kila chama cha siasa na mgombea hushurutishwa kukubali kufuata maadili hayo wakati wa kuwasilisha fomu ya uteuzi wa mgombea katika uchaguzi.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, vyama vya siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Serikali, walikubaliana Maadili ya Uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2015 kwa kutoa tamko kwamba:
“Sisi vyama vya siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa pamoja, tumekubaliana kuwa na uchaguzi huru, wa haki, uwazi na wa kuamika.
“Na kwamba amani, ustawi wa nchi, usalama wa raia, uhuru wa vyama vya siasa na utii wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ndio msingi wa uchaguzi ulio huru, haki na wenye kuzingatia ushiriki wa makundi yote ya jamii katika uchaguzi.
“Tunajipa na tunakubaliana kuwajibika kuyatekeleza maadili haya yanayotokana na kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 1985 (Sura ya 343).
“Tutafanya jitihada za wazi kuhakikisha maadili haya yanajulikana na kuheshimiwa na wagombea na wanachama wote wa vyama vya siasa”
Makubaliano haya yalikubaliwa na kuahidi kutekelezwa na Katibu Mkuu Dk Florens Turuka kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume Jaji Damian Lubuva Julai, 27 2015.
Wengine waliokubali maadili hayo na kuahidi kuyatekeleza ni viongozi wa vyama vyote 22 vya siasa vilivyokuwa na usajili wa kudumu, kupitia makatibu wakuu au Naibu wake, wenyeviti au makamu wao.
Maadili hayo ambayo tutayachambua katika makala zinazofuata, hutumika katika Uchaguzi Mkuu na katika chaguzi ndogo zinazofuata baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka husika.
Kila chama cha siasa na mgombea huwajibika kusaini maadili hayo wakati wa uchaguzi na chama ambacho hakitasaini kitazuiliwa kushiriki kampeni za uchaguzi na mgombea atakayekataa kusaini ataondolewa kushiriki katika uchaguzi.

No comments:

Post a Comment