Wakizungumza leo Machi 14, 2018 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Hisabati Duniani, wadau hao wamesema ufaulu mdogo wa somo hilo imekuwa kilio ambacho bado hakijapata suluhisho la dhati.
Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati nchini (Mat/Chahita), Dk Said Sima amesema takwimu za ufaulu katika miaka kumi iliyopita katika mitihani ya hisabati kitaifa ni asilimia 17.63 kwa shule za sekondari na asilimia ya 31.86 kwa shule za msingi.
Amesema utafiti uliofanywa kwa baadhi ya shule zilizoshikilia nafasi za mwisho kitaifa kwenye mitihani hiyo jijini Dar es Salaam, uhaba wa walimu ni kati ya sababu za ufaulu mdogo.
Amesema ipo dawa ya kupambana na uhaba wa walimu wa masomo ya hisabati kwa Serikali kuajiri walimu waliohitimu vyuo mapema wanapomaliza badala ya kusubiri muda mrefu.
"Hii ya kusubiri muda mrefu inawafanya walimu kwenda kuajiriwa kwenye sekta nyingine na inapokuwa hivyo inakuwa vigumu kuwapata tena,"amesema.
Alitaja mbinu nyingine kuwa ni kuajiri wahitimu wa shahada za sayansi kwa kuwapa mafunzo maalumu ya ualimu na baadae kusomea kabisa taaluma hiyo.
Ameshauri kuwapo kwa mpango maalumu kwa vyuo vya ualimu na vyuo vikuu kusaidia kufundisha kwa kutumia wanafunzi waliopo vyuoni hasa nyakati za likizo na mwisho wa wiki.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk Leonard Akwilapo amesema wapo tayari kupokea ushauri wa wadau hao kwa kuwa ni ukweli usiopingika kwamba kiwango cha ufaulu wa hisabati kinaanguka.
Amesema kuhusu suala la walimu, Serikali inaendelea kupambana nalo kwa kuwaajiri na kutilia mkazo wa ufundishaji wa masomo hayo ili kuongeza ufaulu na kuendelea kuzalisha walimu wa kutosha.
Awali, Ofisa Viwango Mwandamizi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Hamis Sudi amesema hakuna taaluma yoyote anayoweza kusomea mtu bila kuhusisha hesabu.
"Hesabu ni maisha, kila kitu kinafanywa kwa kutumia hisabati," amesema.
No comments:
Post a Comment