Friday, September 22

WAZIRI KAIRUKI AZINDUA BODI YA PILI YA UONGOZI INSTITUTE

Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki amesema kuwa wakurugenzi walioteuliwa katika bodi ya Taasisi ya Uongozi  ni watu makini na wenye uzoefu wa muda mrefu katika nafasi mbalimbali ,hivyo watatoa ushauri mzuri kwenye taasisi hiyo.

Waziri Angellah aliyasema hayo katika uzinduzi wa bodi ya pili ya Taasisi  ya Uongozi uliofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini  Dar es Salaam. Amesema bodi ya wakurugenzi wa taasisi hiyo wamepita katika utumishi na wazalendo katika sehemu zao mbalimbali ambapo watakuwa msaada mkubwa kwa taasisi hiyo katika  kutoa ushauri.

Amesema kuwa Uongozi Institute ilianzishwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo viongozi wa Afrika katika kuangalia maendeleo endelevu ya bara la Afrika  hivyo wajumbe wa bodi ni wa kimataifa na wanatambulika.

Angellah amesema kuwa walioteuliwa na Rais Dk.John Pombe Magufuli watatimiza majukumu yao na wataendelea kupewa ushirikiano pamoja na viongozi wengine wa Afrika katika kuwa na ajenda ya kuandaa viongozi.

Amesema uongozi Institute inatakiwa kutimiza mambo matatu moja ni bidhaa ya huduma iliyo na kiwango bora, kuangalia rasilimali  ya kuweza  kufanya taasisi hiyo ikue katika kuangalia vyanzo vya mapato pamoja na kujengea uwezo wa kuendelea kutekeleza ajenda ambazo zimeibuliwa.

Walioteuliwa katika bodi hiyo Mwenyekiti ni Balozi wa Finland Inchini Afrika Kusini, Kari Alanko , Makamu wa Rais Profesa Idris Kikula wengine ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora  Dk. Laureane Ndumbaro,  Katibu Mtendaji wa SADC Dk. Stergomena Tax, Profesa Penina Mlama wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Christina Duarte Waziri wa Zamani wa Fedha , Mipango na Utumishi wa Cape Verde, Mkurugenzi wa Nodic Afrika ya nchini Sweeden Lina Soiri, pamoja Mkurugenzi wa zamani wa shule ya utawala ya nchini Uingereza , David Walker.

Nae Afisa Afisa Mtendaji Mkuu wa Uongozi Institute, Profesa Joseph Semboja  amesema kuwa chombo hicho kilianzishwa katika kuwajengea viongozi wa Afrika ambao waliridhia kuundwa kwa chombo hicho.

Amesema kuwa Taasisi hiyo imetoa mafunzo mbalimbali tangu kuanzishwa kwake na itaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki akizungumza katika uzinduzi wa bodi ya pili ya Wakurugenzi wa Uongozi Institute , uliofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Uongozi Insitute, Profesa Joseph Semboja akizungumza katika uzinduzi wa bodi ya Uongozi Institute  juu ya taasisi hiyo inavyofanya kazi  katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Uongozi Institute ,Balozi wa Finland Inchini Afrika Kusini, Kari Alanko akitoa shukurani kwa Waziri Kairuki  mara baada ya kuzinduliwa  bodi hiyo.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki akigawa vitabu vya miongozo kwa wajumbe wa Bodi hiyo.
 Sehemu watendaji mbalimbali wa serikali waliohudhuria uzinduzi wa bodi ya pili ya oungozi institute.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na bodi ya ya wakurugenzi ya Uongozi Institute, jijini Dar es Salaam.

RAIA WA UHOLANZI AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUISHI NCHINI BILA KIBALI

Raia wa uholanzi, Monique Honsbeek Amanzi, ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, rafiki yake wa kiume ambaye ni askari polisi kitengo cha Trafiki amemchania hati yake ya kusafiria.

Amanzi (28), amedai hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa alifikishwa mahakamani hapo kujibu tuhuma zinazomkabili za kuishi nchini bila ya kuwa na kibali.

Akisomewa mashtaka yake na wakili wa serikali kutoka ofisi za Uhamiaji, Nivatus Mlay amedai, Septemba 11 mwaka huu (2017) katika makao makuu ya ofisi za uhamiaji mshtakiwa huyo, akiwa raia wa Uholanzi alikutwa akiishi nchini bila ya kuwa na kibali.  Baada ya kumaliza kusomewa tuhuma zake hizo. 

Aliulizwa kama ni kweli au la, ndipo Amanzi akadai kuwa, alikuwa na hati yake ya kusafiria ambayo rafiki yake huyo wa kiume trafki aliyemtaja kwa jina la Letiko Kulwa wa Makumbusho Victoria aliichana na hivyo kumfanya asijue kama visa yake ilikuwa imeisha.

Amedai, alikuja nchini akitokea uholanzi akiwa na mumewe Ibrahim Abasa, na watoto wao wawili lakini baadae waliachana ndipo akampata trafiki huyo ambaye walizaa nae mtoto mmoja lakini alifariki.

Amedai ameishatoa taarifa katika kituo cha polisi miaka miwili iliyopita juu ya kuchanwa kwa hati yake lakini RB aliyopewa ameipoteza. Pia alishaenda kutoa taarifa Uhamiaji lakini hakupata msaada wowote.
Kesi hiyo itatajwa Septemba 27 mwaka huu.

SHEIKH HAMID JONGO AWATAKA WANAFUNZI NA WALIMU WA SHULE YA VUCHAMA KUJIPANGA KATIKA USHINDANI WA KITAALUMA

Mjumbe wa baraza la Ulamaa BAKWATA taifa, ambaye pia ni Imamu Mkuu wa Msikiti wa Manyema jijini Dar es salaam, Sheikh Hamid Jongo akizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi wa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Vuchama iliyopo Ugweno, Mwanga Mkoani Kilimanjaro, katika mahafali ya kuwaaga wanafunzi wa kidato cha nne.
Meneja wa shule ya sekondari ya Vuchama, Alhaj Yusuph Mfinanga, akizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi wa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Vuchama iliyopo Ugweno, Mwanga Mkoani Kilimanjaro.
Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Vuchama, Mwalimu Juma A. Juma akizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi wa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Vuchama iliyopo Ugweno, Mwanga Mkoani Kilimanjaro,katika mahafali ya kuwaaga wanafunzi wa kidato cha nne.

Na Mwamvua Mwinyi, Kilimanjaro

MJUMBE wa baraza la Ulamaa(BAKWATA)Taifa,ambae pia ni Imamu mkuu wa msikiti wa Manyema jijini Dar es salaam, Sheikh Hamid Jongo, amewataka wanafunzi wa shule za taasisi za kielimu za kidini kusoma kwa bidii na kuwa watiifu badala ya kuwa wajeuri na mafedhuri.

Ameeleza watoto wanapaswa kujipanga kitaaluma ya ahera na kidunia ili kukua katika misingi iliyo na maadili mema ya kidini na kitaifa. Aidha sheikh Jongo,ameziasa taasisi hizo waache kufundisha uhasi bali zijiongeze,kubuni mbinu mbadala zitakazowezesha kwenda pamoja na ushindani wa kitaaluma kwa lengo la kufaulisha hasa kidato cha nne na cha sita pasipo kushika mkia.

Aliyaelezea hayo, wakati akizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi katika shule ya kiislamu ya sekondari ya VUCHAMA ,iliyopo Ugweno,wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro,kwenye mahafali ya kuwaaga wanafunzi wa kidato cha nne. Sheikh Jongo,alisema elimu ni silaha ya maisha na msingi wa kimaendeleo hivyo ,wanafunzi hao wajitahidi kuondokana na ujinga kwa manufaa yao ya baadae .
Alifafanua kwamba,walimu wa shule hizo wawafundishe wanafunzi wao utiiifu ili kuishi vizuri na kuwa wazalendo na nchi yao.

“Ikiwa tunapita mashuleni na kuwasomesha masomo ya dini na miongoni wa maeneo tunayowapa yakiwa ni ya uhasi hilo ni suala baya sana, kitawagharimu waislamu kweli, kwani matokeo yake kuna vijana wamekuwa wajeuri ,mafedhuri hata kwa mashehe zao”

“Kijana wa aina hiyo mnatarajia awe kiongozi wa baadae wa kiroho kwelii?hawa ndio wanaohangaisha hata nchi,hivyo ,walimu tujitahidi kufundisha maadili mema ya kidini na kimaisha kijumla”alisema sheikh Jongo.

Hata hivyo Sheikh Jongo ,aliwaomba waislamu wamuogope mwenyezi mungu,waendelee kukubaliana na imani ya kiislamu na kuwaomba baadhi yao kuacha fikra potofu ya imani za itikadi za kisiasa ama siasa kali. Alibainisha,watu wenye itikadi kali hata mtume S.A.W hajawahi kukubaliana nao katika enzi hizo,hivyo kumcha mungu ukiwa na siasa kali utakuwa na kasoro.
Sheikh huyo,alitoa rai kwa watanzania kijumla kuishi kwa amani na utulivu ili kuendelea kujenga heshima ya taifa. Wakati huo huo meneja wa shule ya kiislamu ya sekondari ya Vuchama,alhaj Yusuph Mfinanga,aliwasihi wahitimu wa kidato cha nne shuleni hapo kwenda kuyaendeleza mazuri na heshima waliyoipata wakiwa shule.

Alisema shule hiyo ina chumba cha kufundishia TEHAMA chenye computer 30 itakayowasaidia watoto kuondoka wakiwa na uelewa juu ya masuala ya mitandao,chumba cha maabara ya masomo ya sayansi na maktaba. Alhaj Mfinanga alitoa ofa kwa mwanafunzi atakaefaulu na amekuwa akitoa motisha mbalimbali kwa walimu .

Alisema kwasasa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa msikiti ambapo kwasasa wanasalia ndani ya madarasa ,:”Inatakiwa sh.mil.105 ili kukamilihsa msikiti wanaotarajia kuanza kuujenga. Nae mkuu wa shule ya kiislamu ya sekondari ya Vuchama,Juma .A.Juma,aliishauri serikali kuiangalie kuwapelekea mafungu ya wilaya ya kuendeleza shule kama zimefanya vizuri.
Alisema shule za binafsi zimekuwa ni moja ya shule zinazofanya vizuri lakini zimekuwa hazipewi mafungu hayo hali ambayo imemsukuma aombe wizara ya elimu kuliona hilo. Shule ya kiislamu ya sekondari ya Vuchama,imesajiliwa mwaka 2014,kwa wanafunzi wa kidato cha I hadi IV. Ilianza rasmi mwaka 2015 ikiwa na wanafunzi wawili na sasa ina wanafunzi 267 kati yao wanaohohitimu kidato cha nne ni 33.

Shule ya Vuchama ni moja ya shule zinazomilikiwa na mfanyabiashara Yusuph Mfinanga,ambapo ana chuo cha masuala ya utalii Njuweni Institute,hotel ya Njuweni na shule ya msingi Kibaha Independent-KIPS zilizopo Kibaha mkoani Pwani .

BARAZA LA TAIFA LA UJENZI NI MUHIMU KATIKA KUTOA TAARIFA MBALIMBALI ZA SEKTA YA UJENZI NCHINI –PROFESA MBARAWA

Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii
Serikali  imesema kuwa Baraza la Taifa la Ujenzi ni muhimu kwa taifa pamoja na kwa wananchi katika kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu  sekta ujenzi nchini.

Hayo ameyasema leo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa wakati akifungua warsha ya Baraza la Taifa la Ujenzi kujadiliana la maboresho ya baraza hilo, uliofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere leo jijini Dar es Salaam, Profesa Mbarawa amesema kuwa hakuna mtu ambaye anajua gharama ya mraba wa mita moja ambapo kazi hiyo ilitakiwa kufanywa na baraza hilo.

Amesema kuwa wakati mtu anataka kujenga nyumba anaweza kupata gharama katika baraza la ujenzi na kuachana na ujenzi wa mazoea ambao unachukua gharama kubwa.

Mbarawa amesema  bidhaa zinaingia nchini lakini hakuna anayejua gharama na ubora na kutofautisha na bidhaa zingine za ambapo kazi hiyo baraza la taifa la ujenzi linatakiwa kufanya.

Amesema kuwa kama mambo hayaendi sawa kutokana na sheria yuko tayari kubadilisha sheria  ili baraza lifanye kazi yake kwa maendeleo ya taifa.

Aidha Mbarawa amesema warsha hiyo italeta mapendekezo ya kina kutokana na wadau waliopo katika sekta ya ujenzi ili iweze kuleta matokeo chanya.

Nae  Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano-Ujenzi, Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema warsha hiyo watajadili  katika kuborseha baraza hilo.

Amesema kuwa wadau wa sekta ya ujezi watakuwa huru na wazi katika uchangiaji masuala mbalimbali ikiwa na malengo ya kuborsesha sekta ya ujenzi.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Profesa Mayunga Mkunya amesema kuwa kufanyika kwa baraza hilo ni matokeo kile kitachojadiliwa kuwezesha katika kujenga baraza.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano , Profesa Makame Mbarawa akizungumza katika ufunguzi wa warsha ya kujadili mabaoresho ya baraza la taifa la Ujenzi lililofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano-Ujenzi, Mhandisi Joseph Nyamhanga akizungumza juu ya baraza la Taifa la Ujenzi linavyofanya kazi leo katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Ujenzi,  Profesa Mayunga Mkunya akizungumza juu warsha hiyo itavyoleta matokeo yaliyotokana na majadiliano na wadau leo katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
 Sehemu ya wadau ya wakiwa kwenye Warsha ya Baraza la Taifa la Ujenzi kujadiliana maboresho ya baraza hilo, iliofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa warsha ya baraza la Taifa la Ujenzi leo katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere leo jijini Dar es Salaam.  

IN MEMORY OF MWALIMU CLARA GASPAR MAREALLE


04 AUGUST 1930 – 22 SEPTEMBER 2009

Days, weeks, months and years came and gone. It is now 8 years since you left us, desolate and bereft. Mama your bountiful, unconditional and unwavering Love and support to your husband, children, grandchildren and family members gardened you unprecedented admiration from the Marealle and Lyimo Clans, then and always! You left a foot print in this earthly world of ours. We loved you Mama, and will forever Love You.

Rest in Eternal Bliss Mama.

WAFANYAKAZI WASHAURIWA KUPIMA AFYA MARA BAADA YA KUSTAAFU.

Na: Lilian Lundo – MAELEZO Dodoma.

Wafanyakazi nchini wameshauriwa kupima afya zao mara tu wanapostaafu ili kujihakikishia ikiwa hawajaathirika na kazi ambazo wamekuwa wakizifanya.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Eric Shitindi alipokuwa akifungua semina ya viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi juu ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, leo Mjini Dodoma.

“Kumekuwa na mazoea kwa wafanyakazi kupima Afya pale tu wanapoajiriwa na kutotilia maanani upimaji afya zao mara wanapostaafu ili kujua ikiwa kazi wanazozifanya zimewaathiri kwa kiasi gani,” amesema Shitindi.

Ameendelea kwa kusema kuwa, upimaji wa afya mara baada ya kustaafu utasaidia watumishi kujua afya zao na ikiwa watakuwa wameathirika upitia kazi walizokuwa wakizifanya basi mwajiri atawajibika mkulipa fidia mtumishi huyo.

Aidha amesema kuwa licha ya juhudi za Serikali katika kusimamia Usalama na Afya maeneo mengi ya kazi sio ya kuridhisha kutokana na waajiri wengi kutokuzingatia sheria na kanuni mbalimbaliza Usalama na Afya.

Hivyo basi kutokana na waajiri hao kutofuata sheria na kanuni hizo kumesababisha maeneo mengi ya kazi kulalamikiwa kutokana na ukiukwaji wa sheria hizo.

Vile vile amesema kuwa baadhi ya waajiri na wafanyakazi wana uelewa mdogo  kuhusu kuzingatia maelekezo ya Usalama na Afya Mahali pa kazi ikiwemo matumizi sahihi ya vifaa kinga.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Khadija Mwenda amesema kuwa, wameamua kuandaa semina hiyo kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi hapa nchini ili na wao wakatoe elimu hiyo kwa wafanyakazi wote nchini kutokana na wafanyakazi hao kutokuwa na uelewa mzuri juu ya masuala ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.
 Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) Bi. Khadija Mwenda akiongea na Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania(TUCTA) na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wakati wa Ufunguzi wa Semina kuhusu masuala ya usalama na afya mahala pa kazi Leo Mjini Dodoma.Kulia ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw.Qambos Sule
 Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Bw. Eric Shitindi akiongea na Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania(TUCTA) na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wakati wa Ufunguzi wa Semina kuhusu masuala ya usalama na afya mahala pa kazi ambapo aliwashauri wafanyakazi nchini kupima afya mara wanapostaafu ili kujihakikishia kama hawajaathirika na kazi walizokuwa wanafanya.Katikati ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw.Qambos Sule na Kushoto ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) Bi. Khadija Mwenda 
 Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw.Qambos Sule akiongea naViongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania(TUCTA) na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wakati wa Ufunguzi wa Semina kuhusu masuala ya usalama na afya mahala pa kazi, kulia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Bw. Eric Shitindi na kushoto ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) Bi. Khadija Mwenda
 Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw.Qambos Sule (KUSHOTO) na Katibu Mkuu Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw. Jones Majura(KULIA) wakiteta jambo na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Bw. Eric Shitindi baada ya ufunguzi wa Semina kuhusu masuala ya usalama na afya mahala pa kazi leo Mjini Dodoma
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Bw. Eric Shitindi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Semina kuhusu masuala ya usalama na afya mahala pa kazi Leo Mjini Dodoma. PICHA NA IDARA YA HABARI-MAELEZO,DODOMA

SSRA Yatakiwa kusimamia Michango ya Wanachama


Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Alli Karume  akipata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na SSRA kutoka kwa Afisa Uhusiano wa Mamlaka Bw. Sabato Kosuri alipotembelea banda hilo  wakati wa maadhimisho ya siku ya Bahari Duniani yaliyofanyika mkoani Kigoma.

Na. Zawadi Msalla. 

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mh. Alli Karume ameitaka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kusimamia kwa ukaribu michango ya Wanachama kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii  ili itumike kwa malengo yaliyokusudiwa kwa mujibu wa Sheria zilizoanzisha mifuko hiyo. 

Wito huo umetolewa jana mjini Kigoma na Waziri Karume alipotembelea banda la SSRA kwenye maonesho ya wiki ya Bahari duniani yanayoendelea kwenye viwanja vya shule ya msingi Mlole Mkoani humo.

Waziri Karume alisema SSRA inawajibu mkubwa wa kumlinda mwanachama wake ili kuhakikisha hapati matatizo pale anapotakiwa kupata mafao yake.Pia alisisitiza kuwa Itakuwa ni jambo la kuumiza sana inapotokea mwanachama mwenye matumaini ya kupata mafao yake atakapoambiwa mfuko umefilisika na hivyo mafao anayoyatarajia hawezi kuyapata.

Aidha Mhe. Karume aliipongeza SSRA kwa elimu wanayoendelea kuitoa kwa jamii juu ya umuhimu wa kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na  jinsi wanavyo simamia maboresho mbalimbali yanayoendelea katika sekta hiyo. 
Hata hivyo alisema bado SSRA inawajibu mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii ili kushawishi wananchi kuona umuhimu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwani wapo wananchi wengi wasio fahamu umuhimu wa  mifuko hiyo na wengi wao hupata shida inapofikia kipindi cha uzeeni.

Awali akitoa maelezo ya shughuli za SSRA Afisa Uhusiano na Uhamasishaji wa Mamlaka hiyo  Bw. Sabato Kosuri alimhakikishia Mhe. Waziri usalama wa  michango ya wanachama kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Bw.Kosuri alisema  tayari SSRA imeweka miundombinu imara ya kusimamia eneo hilo ikiwa ni pamoja na miongozo ya uwekezaji pamoja na kaguzi za mara kwa mara ili kuhakikisha mifuko inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria kanuni na taratibu na hivyo kuwahakikishia usalama wachangiaji wote kwenye mifuko ya hifadhi ya  jamii.

Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii iliundwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, Sura ya 135 (Toleo la 2015) kwa lengo la kusimamia na kudhibiti Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa manufaa ya Wanachama na Taifa kwa ujumla. Mamlaka ilianza kazi rasmi mwishoni mwa Mwaka 2010.

Mamlaka ina jukumu la msingi la kuhakikisha kwamba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inakuwa endelevu, inaendeshwa kwa kufuata kanuni, taratibu na kisheria, wanachama wanapata taarifa za Mifuko/michango yao, na mafao yaliyobora. 

WANAFUNZI WANG’ARA SHINDANO LA GENIUS CUP.


Mkurugenzi wa shule ya Feza Ibrahim Yunus kushoto na kulia Mwalimu Mkuu wa Feza Boys, Saimon Albert  wakiwa kwenye picha ya pamoja na mshindi wa kwanza hadi watatu wa mashindano hayo. Wa kwanza kushoto ndiye Perfect Ndyetabura  aliyeibuka mshindi wa kwanza kutoka shule ya msingi Hazina  na Hamza Azaeli mwenye miwani aliyeibuka mshindi wa pili naye akitokea shule ya Hazina na watatu anatoka shule ya Feza.

WANAFUNZI wa shule ya Msingi Hazina ya jijini Dar es Salaam, wameibuka washindi kwenye mashindano ya Genius CUP, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza  kwenye mashindano hayo ni Hamza Azaeli na Perfect Ndyetabura ambao wote wanatoka shule ya msingi Hazina.

 Mashindano hayo yaliyoshirikisha shule mbalimbali nchini yaliandaliwa na  shule ya Feza na kushirikisha shule kutoka mikoa na kuitaja baadhi ya mikoa iliyoshiriki kuwa ni Tanga, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Mtwara, Pwani, Arusha na Zanzibar.

Mratibu wa mashindano hayo kutoka shule ya Feza, Ashrak Habibu, alisema wanafunzi hao walionyeshana umwamba kwenye masomo ya sayansi na hisabati.

Katika hafla ya kukabidhi vyeti hivyo, iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Kimataifa ya Feza, Salasala jijini Dares Sallam, Mkurugenzi wa shule hiyo, Ibrahim Yunus alisema mashindano hayo ya kimasomo yajulikanayo kama Genius Cup, yaliandaliwa kwa pamoja na shule hizo kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Tume ya Sayansi na Teknolojia.

“Lengo letu ni kuwaandaa wanafunzi ili watakapomaliza masomo yao wawe na taaluma ya kisayansi, hasa kwa kuwa nchi inaelekea katika uchumi wa viwanda, hivyo inahitaji vijana wanasayansi na mashindano haya hufanyika kila mwaka hapa nchini,” alisema mkurugenzi huyo.

 Mbali na kupewa vyeti, wanafunzi watatu waliofanya vizuri zaidi katika masomo ya Hisabati walitunukiwa kiasi cha fedha 200,000 kwa mshindi wa kwanza (150,000) mshindi wa pili na laki moja kwa mshindi wa tatu.

Akizungumzia  mafanikio ya wanafunzi hao, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,  Patrick Cheche, alisema wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakifanya vyema kwenye mashindano mbalimbali kutokana na maandalizi mazuri wanayoyapata.


 “Walimu wanafanyakazi kwa moyo sana, wazazi wa wanafunzi wamekuwa wakitoa ushirikiano mzuri sana kwa shule na uongozi wa shule unawajali sana walimu, hayo kwa pamoja yamekuwa yakisaidia wanafunzi wetu kufanya vizuri kwenye mashindao mengi,” alisema Mwalimu Patrick

RAIS ABBAS: AIDHA UHURU AU HAKI KAMILI KWA WOTE, KATIKA NCHI YA PALESTINA YA KIHISTORIA


Rais wa Palestina “Mahmoud Abbas” amesisitiza kuwa uhuru  wa nchi yake upo karibu hauepukiki na kwamba uvamizi wa Israeli unafikia mwisho, akisema: "Aidha upatikane uhuru au haki kamili ya wote katika nchi ya Palestina ya kihistoria."

Rais Abbas Jumatano jioni akihutubia Mkutano wa 72 wa Umoja wa Mataifa, ameongeza kusema kwamba, imepita miaka ishirini na minne tangu kusainiwa kwa Mikataba ya mpito ya Oslo, ambayo ilionesha ukomo wa uvamizi wa Israeli na kuwapa matumaini Wapalestina, ya kuanzishwa kwa Dola yao huru, huku akihoji " Tuko wapi sasa na matumaini haya?."

Amesema:"Tumekubali uwepo wa Dola ya Israeli  kupitia mipaka ya mwaka 1967, lakini Israeli kutokubali uwepo wa Dola ya Palestina kunatupa maswali mengi. Badala ya kuzingatia sababu, inafanya juhudi kuteka misimamo ya kimataifa kwa masuala yasiyo na uzito wowote, yatokanayo na sera zake za kikoloni. Tunapoitaka na kutakiwa na jumuiya ya kimataifa kukomesha uvamizi wake, inadai ni uchochezi na kukosekana  ushiriki wa Palestina na kuwekwa kwa masharti yasiyowezekana."

Rais Abbas ameongeza kusema kuwa,anaelea machafuko ni Utawala wa kivamizi wa Israeli katika ardhi yetu,uvamizi ambao umefikia zaidi ya nusu karne,huku zaidi ya miaka kumi sasa tumekubaliana  kuunda kamati ya pande tatu ambazo ni Marekani,Israeli na Palestina, ili kumaliza suala la uchochezi.Kamati  imefanya kazi kwa muda, lakini tumekuwa tunatoa wito wa kufufuliwa wa kamati hiyo hatupati mrejesho. Hivi ni nani anaekaribisha hilo na kufanya juhudi ya kulifanya liwepo?.

Amesema pia,kuendelea kwa uvamizi ni aibu kwa Israeli na Jumuiya ya Kimataifa,ni wajibu wa Umoja wa Mataifa kumaliza uvamizi huo ili kuwezesha jamii ya Palestina kuishi kwa uhuru na ustawi katika ardhi yake,huku mji mkuu wake ukiwa ni Jerusalemu ya Mashariki.

"Kukomesha uvamizi na vitendo vyake vya kidhalimu, vitakuwa na athari kubwa mno katika kupambana na udaidi pia mashirika yake kukosa karatasi muhimu ambazo huzitumia kwa kuuza fikra zao."Tunatilia mkazo la kukaliza uvamizi ili kukamilisha juhudi zetu katika kukabiliana na mashirika hayo ya kigaidi,kwani Wapalestina wapo dhidi ya ugaidi wa ndani,kikanda na wa kimataifa.

"Tuliwasilisha mpango wa amani wa Kiarabu  unaoitaka Israeli kuondoka katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kimabavu tangu  mwaka 1967 lakini Israeli haikujibu,kama ilivyoufanyia ule mpango ujulikanao kama “Road Map” uliowasilishwa na pande nne na kupitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,hali inayoonekana kana kwamba Israeli ipo juu ya sheria. Vilevile ukaja mpango wa amani wa Ufaransa ukifuatiwa na mkutano husika mjini Paris,lakini juhudi zote hizi zilikataliwa na kupigwa na Israeli."

Ameongeza kusema:”Tulimuomba Waziri Mkuu wa Israeli akubali ufumbuzi wa dola mbili, kisha tukae kuzungumzia suala la mipaka akakataa,licha ya jitihada zetu kufikia amani ya kweli, lakini Israeli inaendelea kuvuruga na kuendeleza ujenzi wa makazi ya walowezi Ukingo wa Magharibi na kila mahali, hatimae hakuna tena nafasi kwa ajili ya taifa la Palestina.

"Vitendo viovu vya Israeli katika mji mtakatifu, vitachochea hisia za uadui wa kidini, ambao unaweza kugeuka mgogoro mkubwa wa kidini, tumeiomba serikali ya Israeli kuheshimu sheria na historia ya sehemu hizo takatifu lakini Israel tangu ilipoikalia kimabavu Jerusalemu mwaka 1976, imekuwa ikiihodhi kwa azimio la upande mmoja.

Rais Abbas amesema kuwa, “Jerusalemu imekaliwa kimabavu na hatua zote za Israeli ni batili kama ilivyo katika ujenzi wake wa makazi ya walowezi Jerusalemu ya Mashariki na maeneo mengine ya Palestina. Ieleweke wazi kuwa,ubadilishaji wa historia ya Jerusalemu na kuuchafua Msikiti wa Aqswa ni kuchezea hatari,pia ni kushambulia majukumu ya Palestina na yale ya Jordan.Tunaitahadharisha hilo, isijaribu kusababisha vita vya kidini wakati mgogoro wetu ni wa kisiasa”.

"Chaguo letu kama Waarabu na chaguo la dunia ni sheria za kimataifa, uhalali wa kimataifa na uwepo wa dola huru ya Palestina kwa mujibu wa mipaka ya 1967.Tutatoa ushirikiano wote katika kufanikisha hilo la kihistoria,ili tupate kuishi kwa amani pamoja na Israeli. Lakini kama ufumbuzi wa dola mbili utaharibiwa na kuimarisha dola moja yenye serikali mbili,hapatakuwa na linguine kwetu wala kwenu ila mapambano na kutaka kupata haki zetu kamili ndani ya Palestina ya kihistoria. Hivi si vitisho ila ni kutaka haki zetu kama wapalestina”.

Tatizo letu kwa utawala wa kivamizi wa Israeli sio Uyahudi kama dini, kwani hiyo ni dini ya Mungu kama Uislamu na Ukristo.Tumebeba majukumu yetu katika Ukanda wa Gaza,ambayo haiwezekani kuwepo Palestina bila hiyo,ninafarijika leo kuona kufikiwa kwa makubaliano mjini Cairo kufuatia juhudi nzuri za Misri.Yamekomesha vitendo vya Hamas vilivyoleta mgawanyiko na hatimae kufanyika kwa uchaguzi mkuu,hatimae serikali yetu mwisho wa wiki ijayo itakwenda Ukanda wa Gaza ili kufanya kazi huko.

"Ukimya wa jumuiya ya kimataifa juu ya vitendo dhalimu vya Israeli,ndio uliohamasisha vitendo hivyo tangu awali hadi inakiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa tangu kuanzishwa kwake, uko wapi Umoja huo na maazimio yake?Vipi unatendea mataifa kwa viwango tofauti? Basi huu ni wajibu wa Umoja wa Mataifa." Aidha ameuomba kumaliza uvamizi wa Israeli ndani ya muda maalumu,kwani haiwezi tena kutoa data huru kuhusu mpango wa amani wa kiarabu,hasa kuhusiana na faili wakimbizi kwa mujibu wa azimio la Umoja wa Mataifa 194,huku akiashiria kuwa maazimio ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kupuuzwa na Israeli”.

Rais Abbas amesisitiza haja ya kusitisha shughuli za ujenzi wa makazi ya walowezi katika maeneo ya Palestina,kwani hatuna uwezo wa kulinda raia zetu chini ya utawala wa mabavu,Umoja wa Mataifa uitake Israeli kutambua mipaka Palestina ya mwaka 1967 na kupunguza mpaka na kuomba wajumbe wote wa Umoja wa Mataifa kutangaza kwamba kutambuliwa kwao kwa msingi wa mipaka ya 1967,pia wanachama wote wa Umoja huo kutambua mipaka hiyo ili kutilia mkazo maazimio ya sheria za kimataifa.

Amesema:"Iko wapi mipaka ya Israeli mlioitambua wakati Israeli yenyewe haijaikubali,sheria za kimataifa zinaitaka dunia kuweka hiyo mipaka". Aidha Rais ametoa wito kwa nchi zote duniani kutoshiriki katika ujenzi wa makazi ya kikoloni ulio kinyume na sheria,huku zikichukua hatua stahiki dhidi yake kama ilivyofanya jumuiya ya kimataifa dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika ya kusini na tunataka kutangaza habari mbaya za mashirika ambayo yanafanya kinyume cha sheria na makazi."

Hivyo, amezihimiza nchi wanachama kuitambua dola ya Palestina kwa mujibu wa mipaka ya mwaka 1967,huku akitilia mkazo kuwa hatua hiyo haitoathiri mpango wa amani,hasa hasa ikiwa Wapalestina wanaitambua dola ya Israeli. Tunauhimiza Umoja wa Mataifa kuikubali Palestina kama mwanachama wake kamili,huku tukiiomba jumuiya ya kimataifa kuendelea kuisaidia kiuchumi na kifedha ili iweze kujitegemea na kujiamini.  

Aidha Rais Abbas, ametahadharisha juhudi za kutaka kubadilisha majukumu ya shirika la misaada  UNRWA na kanuni zake,pia kufuta kipengele cha saba katika Baraza la haki za binaadamu au kuzuia kutoa orodha chafu ya mashirika yanayofanya kazi katika makazi ya walowezi wa Israeli nchini Palestina inayokaliwa kimabavu. 

Rais Abbas amehitimisha hotuba yake kwa kutilia mkazo msimamo wa nchi yake,katika kuheshimu haki za binaadamu na kutekeleza mikataba ya Umoja wa Mataifa na ile yote iliyosaini,kwani Palestina ni sehemu ya jumuiya ya kimataifa na si vingine. Huku nchi yake pia itaandaa matakwa hayo kwa maazimio yatayokwenda sambamba na misingi husika,kisha kuyawasilisha kwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.