Wednesday, March 7

MKURUGENZI WA UNIDO AWASILI TANZANIA KUUNGA MKONO MAENDELEO YA VIWANDA

Serikali imesema kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) limekubali kushirikiana na serikali ya Tanzania katika ukuzaji na uendelezwaji wa viwanda nchini.

Hayo ameyasema Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage wakati akimpokea Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), LI Yong.

Mwijage amesema kwamba katika muda mfupi aliozungumza na Mkurugenzi huyo amesema kwamba yuko tayari kushirikiana na Tanzania katika ukuaji wa viwanda nchini na kuitangaza nchi yetu kimataifa ili kuvutia wawekezaji.

Mwijage amesema kuwa UNIDO imefanya vizuri katika nchi mbalimbali hivyo alichokifanya katika nchi zingine ndicho atakachokifanya Tanzania katika maendeleo ya viwanda vya kuzalisha bidhaa bora na sio mali ghafi.

Amesema kuwa ujio wa bosi wa UNIDO ni sehemu ya kutangaza bidhaa kuweza kupata masoko nje ya nchi na sio wakati wa sasa kupeleka mali ghafi.

Mwijage amesema katika kipaumbele kilichopo ni kuweka viwanda vya kutengeneza mafuta ya kula pamoja na viwanda vya nguo ambapo mali ghafi zote zinapatikana nchini.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, LI Yong amesema kuwa katika ziara hiyo kuna vitu vingi atajifunza kwa nchi ya Tanzania kwa hatua iliyofikiwa katika uendelezwaji Viwanda.

Katika ziara hiyo atafanya mazungumzo na Viongozi wakuu wa Serikali kwa Tanzania bara na Zanzibar pia kufanya mazungumzo na Sekta binafsi nchini ikiwa ni sehemu ya kusukuma maendeleo ya viwanda kwa kasi.
 Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage akizungumza na waandishi habari kuhusiana na ujio wa Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, leo tarehe 7 Machi, 2018 jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya watendaji wa UNIDO pamoja na watendaji wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Mambo ya nje, ushirikiano wa kikanda na kimataifa wakimpokea Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, LI Yong(kushoto) mara baada ya kuwasili.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage(kushoto)  akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, LI Yong(kulia) mara baada ya kuwasili nchini leo.

Mshauri wa Trump kujiuzulu

Gary Cohn
Mshauri wa uchumi wa ngazi ya juu Gary Cohn anaondoka ikulu ya White House baada ya kutofautiana na Rais Donald Trump juu ya sera za biashara, ikiwa ni tukio la karibuni katika mtiririko wa wale waliojiondoa kutoka ofisi hiyo ya rais iliyoko magharibi ya jengo la ikulu.
Cohn, ambaye ni mkurugenzi wa baraza la uchumi la taifa, amekuwa akiongoza wale wanaopinga ndani ya nchi mpango mzima wa Trump wa kuweka ushuru katika uagizaji wa chuma na aluminium.
Pia aliendelea kuhamasisha juhudi za dakika ya mwisho katika siku za karibuni ili kumfanya Trump abadilishe msimamo wake.
Lakini Trump amekaidi juhudi hizo, na kusisitiza Jumanne ataanzisha ushuru katika siku chache zijazo.
Kuondoka kwake Cohn kumekuja katikati ya kipindi ambacho kuna mkanganyo ambao haujawahi kushuhudiwa katika uongozi wa Trump, na wasaidizi wake wana wasiwasi kuwa wafanyakazi zaidi wa Ikulu watajiondosha katika ofisi hiyo.
Tangazo hilo limekuja saa kadhaa baada ya Trump kukanusha kuwa kuna mvurugano ndani ya White House. Trump ameendelea kusema kuwa ikulu ya White House “ina nguvu yakutosha,” lakini maafisa kadhaa wa ikulu hiyo wamesema kuwa Trump amekuwa akiwashauri wasaidizi wake waliokuwa na wasiwasi kuendelea kufanya kazi naye.
“Kila mtu anataka kufanya kazi White House,” Trump amesema wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari akiwa na mgeni wake Waziri Mkuu wa Sweden Stefan Lofven. “Wote hawa wanataka kuwa sehemu ya wafanyakazi wa ofisi ya Rais.”
Katika tamko lake, Cohn amesema ilikuwa ni heshima kubwa kwake kutumikia katika serikali na kuweza kupitisha sheria ya sera za kuboresha uchumi ili kuwanufaisha watu wa Marekani.”
Kwa upande wake Trump amempongeza Cohn pamoja na kuwepo tofauti kati yao juu ya suala la biashara, na kutoa tamko kuwa Cohn “ametumikia nchi yake kwa ufanisi wa hali ya juu.”
Cohn ni mtendaji wa zamani wa Goldman Sachs ambaye alijiunga na ikulu ya White House baada ya kuondoka kutoka kampuni ya Wall Street ambako alipata marupurupu ya dola milioni 285.
Alikuwa na jukumu muhimu la kumsaidia Trump kupitisha sheria ya mabadiliko makubwa katika kodi, na kuratibu suala hilo na wabunge.
Kuondoka kwa Cohen kulitarajiwa lakini kumekuwa ni sikitiko kubwa kwa wabunge na wafanya biashara.

Kenya yasema haina fedha

Waziri wa Fedha Henry Rotich (kushoto)
Waziri wa Fedha wa Kenya Henry Rotich amesema kuwa serikali inakabiliwa na matatizo kadhaa katika kufadhili baadhi ya miradi yake ya maendeleo.
Rotich ameweka bayana pendekezo la kupunguza matumizi ya mabilioni ya fedha zilizokuwa zimetengwa kwa kaunti kadhaa ambazo ni kati ya shilingi bilioni 15 na shilingi bilioni 17.
Wakati akiongea mbele ya kamati ya fedha na bajeti ya Baraza la Seneti Jumatano, Rotich amesema hali hiyo inatokana na mamlaka ya mapato Kenya kushindwa kukusanya kodi kwa kufikia malengo waliopewa katika makadirio ya ukusanyaji wa kodi yaliyopitishwa.
“Tumezungumza na KRA juu ya njia bora ya kufikia udhibiti wa ukusanyaji kodi kamili kwa pato la ndani ya nchi na pato la bidhaa zinazoingia nchini,” Rotich ameiambia kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Mandera Mohamed Maalim Mahamud.
Waziri ameongeza kuwa; “tunahitaji kulizungumzia suala hili pamoja (maseneta) na magavana kwamba kiwango cha mapato tunachojadili siyo rahisi kukusanya kutokana na changamoto nilizozielezea.”
Katika mwaka wa fedha 2018, shilingi bilioni 302 zilikuwa zimetengwa kwa kaunti za serikali 47 katika uwiano uliosawa wa mapato yaliyokusanywa, ikimaanisha kuwa katika hali mbaya kabisa ya kiuchumi, mgawanyo huo ungeweza kupungua kufikia shilingi bilioni 285.
Kwa mujibu wa waziri wa fedha, upungufu huo wa ukusanyaji mapato kama ulivyokuwa umekadiriwa mwezi Machi 2017 wakati bajeti hiyo iliposomwa mapema mwaka 2017 ili kuwezesha uchaguzi mkuu kufanyika Agosti 8, umesababishwa na kipindi kirefu cha kuandaa uchaguzi na ukame uliokuwa unaikabili Kenya.
Waziri anasema kuwa hili liliathiri ukusanyaji wa mapato kwani ilizorotesha shughuli za biashara nchini.

Kampuni inayounda viatu vya ngozi ya kiboko na mbuni Zimbabwe

Courteney Boot Company boots
Hewa ni nzito hapa na harufu ya viatu vipya wakati kikundi cha wabunifu 16 wakitengeneza mabuti aina ya Safari.
Kila pea ya viatu huchukua wiki mbili kutengeneza mpaka kumaliza, huwezi kuishutumu Courteney Boot Company kwa kurashiarashia vitu.
Badala yake ni biashara, moja kati ya chapa kubwa ulimwenguni, hivi sasa hutengeneza pea 18 za buti na viatu kwa mikono yao kila siku.
Ilianzishwa mwaka 1991 Bulawayo, Zimbabwe, Courtney inaendelea kuwa biashara chache zenye hadithi ya mafanikio katika nchi ambayo uchumi wake umesuasua kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita
Wakitumia ngozi za wanyama isivyo kawaida, ngozi kama ya mamba, swara, kiboko na mbuni, mabuti yao yanaendelea kuhitajika mno duniani kote.
Courteney Boot Company boots
Image captionJina la kampuni hiyo linatokana na mpelelezi wa karne ya 19 kutoka Uingereza Frederick Courteney Selous
Gale Rice
Image captionGale Rice ameisimamia biashara hiyo kivyake tangu mwaka 2012 mumewe John alipofariki
John alianza kutengeneza viatu nchini Uingereza mwaka 1953 akiwa na miaka 15, alianza kufanya kazi kwenye Kampuni ya Uingereza ya kutengeneza viatu Clarks, kazi yake hiyo ilimpeleka Afrika Kusini, kabla ya kwenda Zimbabwe.
Wawili hao waliendesha biashara kwa miaka 21 mpaka John alipofariki mwaka 2012.
Tangu wakati huo Gale ameongoza Kampuni hiyo akiwa peke yake.
Katika miaka ya nyuma ya Courteney anasema yeye na John walibuni namna ya kutangaza biashara yao .
''Mwanzo kabisa tulitengeneza mabuti kwa wale waratibu wa Safari nchini Zimbawe na Afrika Kusini bure na tulivisafirisha sisi wenyewe," alisema Gale.
''Waratibu wa safari walivaa buti walipokuwa kwenye vichaka na wateja wao wa ng'ambo na walitutangazia biashara kwa mdomo tu''.
Courteney Boot Company boots
Image captionKampuni hiyo huwa haina pupa katika kutengeneza viatu vyake
Wageni nao walikuwa wakitafuta maduka nchini Zimbawe na Afrika Kusini kwa ajili ya kununua viatu vya Courteney kwa ajili ya kwenda navyo nyumbani baada ya likizo.
Kisha huwapa motisha marafiki zao nao wakaagiza wakiwa nchi za ng'ambo.
Wakulima wakubwa wa nchini Zimbabwe, wa asili ya weupe nao walikuwa wakinunua mabuti.
Gale anaongeza: ''tulikuwa na wateja wakuu watatu-wawindaji, wakulima na watalii''.
Kampuni ilikua na nguvu mpaka pale hali ya uchumi na siasa ilipoanza kuyumba nchini Zimbabwe mwaka 2000.
Kampuni lipoteza wateja wake wengi wa ndani.Kwanza, wakulima Wazungu waliondoka nchini,na watalii wakaacha kuingia nchini.
Kwa ajili ya kuendeleza Kampuni, Gale alilazimika kuongeza nguvu kwa kuuza nje zaidi, ambayo ilikua kutoka 50% mpaka sasa 85% ya mauzo ya jumla.
A Courteney Boot Company worker
Image captionKampuni hiyo imeajiri watu 16
''Tangu mwanzo wakati wote tulidhamiria kujaribu kutengeneza buti zetu ziweze kupatikana kwenye soko duniani," alisema
''Tangu mwaka 2000 Zimbabwe ilikuwa na hali mbaya kiasi cha kutaka kuanguka kabisa''
''Ni muda sasa tumekuwa tunachagua ama tukauze nje au Kampuni ife kabisa''.
Hivi sasa Gale anasema 70% ya mauzo yake yamefanyika kwa njia ya mtandao, 20% ya kiasi hicho ni kwa kupitia mtandao wa Courteney.
Kila pea ya Buti ya dola 145-492 za Marekani zinatengenezwa kwa kuagizwa kutoka kwenye duka dogo la Kampuni na Gale amesema kuwa Kampuni haitaongeza uzalishaji zaidi ya pea 30 kwa siku, kwa ajili ya kuimarisha ubora wa bidhaa, ''naendelea na mbinu hiyo''.
''Ningesema kuna mambo kadhaa ya mafanikio yetu kwenye kusafirisha nje,lakini la muhimu ni kuhakikisha tunatengeza bidhaa nzuri,yenye kuridhisha na zenye kudumu''.
John RiceHaki miliki ya pichaCOURTENEY BOOT COMPANY
Image captionJohn Rice alikuwa akitengeneza viatu tangu akiwa na miaka 15
''Changamoto wanazokabiliwa nazo, wauzaji wa bidhaa kuelekea nje ya nchi zinatokana na kuwa Zimbabwe ni nchi kavu, lakini kama una wateja karibu nusu duniani unapaswa kuzalisha kwa uhakika zaidi.
''Wakati mwingine hata mara tatu au nne zaidi ya kiasi kilicho kwenye makubaliano ya kwenye karatasi''.
Bwana Tarirah anaongeza kuwa ''mtandao wa Intaneti pia umebadili mwenendo wa biashara kwa wasafirishaji kutoka nchi kama Zimbabwe''.
''sasa ni rahisi kwa watengenezaji kuzalisha kwa kuzingatia mtindo ulio hivi sasa, tofauti na kuwa na bidhaa iliyohifadhiwa isiyoweza kutumika kwa miezi mitatu, sita mpaka tisa''.
''Inawapa fursa ya kuwika kwenye masoko ambapo kwa kawaida wasingeweza kufikia''.
A Courteney Boot Company worker
Image captionMfanyakazi katika kampuni ya Courteney
Gale anasema "bila shaka siri yetu ya kuwa na mafanikio ni tabia.''
Anaongeza: ''Kusafirisha kwa njia ya maji kunategemea mawasiliano mengi na uvumilivu''.
Wakati uuzaji wa ndani ukianza kukua tena taratibu tangu aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Robert Mugabe kujiuzulu, Gale anasema bado si rahisi kufanya biashara Zimbabwe.
''Maisha ni magumu hapa, lakini tunachagua kuwa na mawazo chanya na kufikiria nini cha kufanya''.

Forbes: Trump ashuka orodha ya matajiri duniani 2018

Donald TrumpHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Rais wa Marekani Donald Trump ameshuka nafasi 222 katika orodha ya kila mwaka ya watu tajiri zaidi duniani ambayo hutolewa na jarida la Forbes.
Mali yake imeshuka thamani kutoka $3.5bn (£2.5bn) hadi $3.1bn.
Jarida hilo limesema kushuka kwa utajiri wa Trump kumetokana zaidi na kushuka kwa thamani ya nyumba na vipande vya ardhi New York na pia kushuka kwa mapato kutoka kwa viwanja vyake vya kuchezewa mchezo wa gofu.
Anayeongoza orodha ya matajiri wa kupindukia ni mmiliki wa kampuni ya Amazon, Jeff Bezos.
Utajiri wa Bezos umepanda na kufikia $112bn kutoka takriban $39.2bn mwaka jana.
Kuimarika kwa utajiri wa Bw Bezos ndiko kwa juu zaidi katika historia.
Amemuondoa mwanzilishi wa Microsoft Bill Gates kutoka uongozini kwenye orodha hiyo.
Utajiri wa Gates unakadiriwa kuwa $90bn mwaka huu kutoka $86bn, na ndiye anayeshikilia nafasi ya pili.
Bw Gates ameongoza orodha hiyo kwa miaka 18 kati ya miaka 24 iliyopita.
Forbes wanasema kuna mabilionea 2,208 (kwa kutumia dola za Marekani) ambao walishirikishwa katika orodha ya 32 ya kila mwaka ya jarida hilo.
Matajiri hao kwa pamoja wana utajiri wa $9.1 milioni.
Miongoni mwao, kuna mabilionea 259 wapya ambao walijipatia utajiri wao kutoka wka biashara za aina nyingi zikiwemo nguo za harusi, wanasesere wa kuchezewa na watoto na magari yanayotumia umeme.
Mwekezaji mmarekani Warren Buffett ndiye wa tatu utajiri wake ukiwa $84bn. Utajiri wake umepanda kutoka $75.6bn mwaka uliotangulia.
mtu tajiri zaidi Ulaya ndiye wa nne kwenye orodha hiyo, ambaye ni mmiliki wa kampuni ya bidhaa za kifahari ya LVMH, Bernard Arnault, ambaye utajiri wake ni $72bn.
Matajiri
'Kupanua pengo'
Marekani ndiyo nchi iliyo na mabilionea wengi duniani, ambapo ina mabilionea 585, ikifuatwa na China. Jimbo la California pekee lina mabilionea 144, zaidi kushinda mataifa yote isipokuwa Marekani na China.
Ujerumani ndiyo nchi inayoongoza Ulaya ikiwa na mabilionea 123.
India ina mabilionea 119 nayo Urusi mabilionea 102.
Kuna mabilionea 53 kutoka Uingereza kwa mujibu wa Forbes na idadi hiyo imeshuka kutoka 54 mwaka 2017.
Luisa Kroll na Kerry Dolan kutoka kwa Forbes Media alisema: "Watu matajiri kupindukia wanazidi kupanua mwanya kati yao wenyewe, na pia kati yao na watu wengine."
Orodha ya mabilionea ya Forbes inatumia takwimu za kufikia Februari 9, 2018.
Jarida hilo hutumia bei ya soko la hisa na ubadilishanaji wa fedha za kigeni ya siku hiyo kutoka kila pembe duniani kuandaa orodha hiyo.

Coca Cola kutengeneza kinywaji chenye kileo kwa mara ya kwanza

Ni mara ya kwanza kwa Coca Cola kutengeneza kinywaji chenye kilevi katika historia ya miaka 125 ya Kampuni hiyoHaki miliki ya pichaAFP/GETTY IMAGES
Image captionNi mara ya kwanza kwa Coca Cola kutengeneza kinywaji chenye kilevi katika historia ya miaka 125 ya Kampuni hiyo
Coca-Cola imetangaza mpango wa kutengeneza kinywaji chenye kilevi kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 125 ya Kampuni hiyo nchini Japan kwa kutumia bidhaa tamu lakini yenye kileo.
Bidhaa hiyo ya muundo wa alcopop itakuwa na kiwango cha kileo cha ujazo wa 3% na 8%
Rais wa Coca Cola nchini Japan Jorge Garduno amesema ''hatujawahi kujaribu bidhaa kama hiyo yenye kileo kidogo, lakini ni mfano wa namna ambavyo tunavyotumia fursa nje ya mipaka yetu''.
Haijafahamika bado kama kinywaji hicho kitauzwa nje ya Japan.
Chu-Hi ni kifupi cha Shochu highball ambacho ni mbadala wa bia, maarufu sana kwa wanywaji wanawake.
Kampuni kubwa za vinywaji nchini Japan ikiwemo Kirin, Suntory na Asahi zina aina mbalimbali za vinywaji na wameendelea kufanya majaribio na mamia ya ladha.
Lakini mwezi Novemba mwaka jana ilikisiwa kuwa Coca Cola itaanza kutengeneza vileo.
Neno alcopop lina maana ya vinywaji vyenye sukari lakini vyenye kileo, na miaka ya 1990 bidhaa za UK kama vile Hooch, Reef, Smirnoff Ice na Bacardi Breezer zilikuwa maarufu sana.
Lakini zilileta mkanganyiko, zikidaiwa zinawafanya vijana kutumia kinywaji chenye kileo kingi kwa kiasi kikubwa kwa kuwa zilikuwa rahisi kutumia.

Hivi unafahamu umri sahihi wa kuanza kufanya mapenzi nchini mwako?

Mtoto aliyeolewa
Ufaransa inatarajia kuweka sheria maalum ya umri wa kuanza kufanya mapenzi kuwa ni miaka 15. Hivyo kufuatia mapendekezo hayo mtu yeyote atakayebainika kufanya mapenzi chini ya umri huo atakuwa amebaka.
Maamuzi haya yamekuja nchini humo mara baada ya madaktari na wanasheria kutoa ushauri wao kuhusiana na umri mtu anaostahili kuanza kufanya mapenzi.
Mabadiliko haya yamekuja kufuatia kesi mbili za hivi karibuni nchini Ufaransa zilizohusisha wanaume waliofanya mapenzi na wasichana waliokuwa na umri wa miaka 11.
Katika sheria ya sasa, kama mtu amekutwa na kosa la kufanya mapenzi na mtu chini ya miaka 15 iwe kwa hiari ama makubaliano, mshtakiwa atahukumiwa kwa kosa la kujamiana na mtoto lakini sio kosa la ubakaji.
Kosa hilo litamlazimu mshtakiwa kutoa kiasi cha dola 87,000 kama sehemu ya adhabu na kwenda jela miaka mitano.
Hukumu ni sawa kwa wanaofanya unyanyasaji kwa watu wazima na watoto lakini kosa la ubakaji huwa lina adhabu kubwa zaidi.
MacronHaki miliki ya pichaAFP
Image captionRais Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron anaunga mkono mpango huo wa kuweka kiwango cha umri wa kuanza kufanya mapenzi.
Mwishoni mwa mwaka jana, mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 30 alikutwa hana hatia baada ya ushahidi kueleza kuwa aliyefanyiwa vitendo hivyo hakuwa amelazimishwa wala kupewa vitisho vyovyote.
Hata hivyo wakati msimamo huo ukitolewa huko nchini Ufaransa hali ni tofauti katika maeneo mengine barani Ulaya. Sheria ya kujihusha na mapenzi inaruhusu katika umri tofauti;

Ulaya

Austria,Ujerumani,Italia ni miaka 14
Ugiriki, Poland, Sweden ni miaka 15
Ubeligiji, Netherland, Spain, Urusi na Uingereza ni miaka 16

Barani Afrika

Miaka 12; Angola
Miaka 13; Burkina Faso, Comoro, Niger
Miaka 14; Botswana (wanaume), Cape Verde, Chad (wasichana), Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (wasichana), Lesotho (wanaume), Madagascar na Malawi
Miaka 15; Guinea, Morocco
Miaka 16; Algeria, Botswana (wanawake), Cameroon, Ghana, Guinea Bissau, Lesotho (wanawake), Mauritania, Mauritius, Mozambique, Namibia, Senegal, Afrika kusini, Swaziland, Togo, Zambia, Zimbabwe.
Miaka 18; Benin, Burundi, Afrika ya kati,Ivory Coast, DRC (wanaume), Djibouti, Equatorial Guinea, Eritrea, Ethiopia, Gabon, Gambia, Kenya, Liberia, Mali, Nigeria, Republic of Congo, Rwanda, Seychelles, Sierra Leone, Somalia, South Sudan, Tanzania, Uganda.
Miaka 20; Tunisia
Wakati ukatili wa kimapenzi kwa watoto ni kosa la jinai katika nchi nyingi za Afrika bado katiba za nchi hizo zimetoa mwaya kutokana na mila na desturi na kupelekea kuendelea kuwepo kwa mimba za utotoni na ndoa za utotoni.
Kwa mfano nchini Tanzania, ni hatia kwa mtu kujihusisha na mapenzi chini ya umri wa miaka 18 na kutajwa kuwa ni unyanyasaji kwa watoto na kinyume cha sheria.
Huku kuna mkanganyiko ambapo kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inaruhusiwa mtu kufunga ndoa akwa na umri wa miaka 14.
ukatili wa kimapenzi kwa watoto ni kosa la jinai katika nchi nyingi za AfrikaHaki miliki ya pichaAFP
Image captionUkatili wa kimapenzi kwa watoto ni kosa la jinai katika nchi nyingi za Afrika
Nchini Kenya umri sahihi wa kuanza kujihusisha na mapenzi ni miaka 18 na yeyote aliye chini ya umri huo anatambuliwa kuwa ni mtoto. Ingawa ndoa pia inawezekana kufungwa katika umri huo, sheria haijaweka wazi.
Katika vigezo hivyo vya umri, Angola ikiwa ni nchi pekee ya barani Afrika iliyoweka umri mdogo zaidi ya watu kujihusisha na ngono, wa miaka 12.
Mara nyingi nchi nyingi barani Afrika huwa hawaweki wazi suala hili la umri wa kuanza kujihusisha na mapenzi kutokana na mila na desturi pamoja na imani za dini.
Na kwa upande wa Umoja wa mataifa hakuna sheria au muongozo maalum kuhusu umri ambao unaruhusu mtu kuanza kufanya tendo hilo, licha ywa kwamba kuna haki za kumlinda mtoto.