MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB),
AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI KWA MWAKA 2017/18
I. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu
lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa
mwaka 2017/18. Bajeti hii inawasilishwa kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 137 ikisomwa pamoja na
Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015 kifungu cha 26.
2. Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba hii, ninawasilisha vitabu
vinne vinavyoelezea kwa kina makadirio ya Bajeti kwa Mafungu. Kitabu cha Kwanza
ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa
Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Kitabu cha Tatu
ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa
Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka
2017 pamoja na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa mwaka 2017 ambayo
ni sehemu ya Bajeti hii.
3. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka
na amani anayoendelea kuijalia nchi yetu na pia kwa kuniwezesha kusimama mbele
ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18.
4. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee napenda nichukue fursa hii kumshukuru
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuendelea kuniamini katika dhamana hii kubwa ya kuongoza wizara
nyeti ya Fedha na Mipango. Aidha, ninamshukuru sana kwa kuniongoza na kunitia
moyo pale mawimbi yalipozidi kuwa makubwa. Maneno yake mazito kwamba aliniteua
ili nipigwe mawe badala yake na badala ya Watanzania maskini na kuwa nimtegemee
Mungu daima, yamekuwa ndiyo nguvu yangu katika kazi. Vile vile, nampongeza
Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake wakuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mheshimiwa Kassim
Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa
jimbo la Ruangwa kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kutuletea maendeleo
Watanzania wote.
5. Mheshimiwa Spika, naomba pia kuwapongeza viongozi wakuu wa
mihimili ya dola, nikianza na wewe mwenyewe Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mbunge wa jimbo la Kongwa, na Mheshimiwa Dkt. Tulia
Ackson (Mbunge) Naibu Spika. Ninawapongeza kwa umahiri na busara zenu katika
kuongoza Bunge hili. Vile vile, ninawapongeza kwa dhati Mheshimiwa Profesa
Ibrahim Juma, Kaimu Jaji Mkuu, kwa kuongoza vyema mhimili wa mahakama katika
kutoa haki.
6. Mheshimiwa Spika, ninawapongeza pia wakuu wa vyombo vya
ulinzi na usalama, nikianza na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo;
Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro; Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt.
Juma Alli Malewa; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala; Mkurugenzi
wa Usalama wa Taifa, Dkt. Modestus Kipilimba; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola; Kamishna
Jenerali wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Bw. Rogers
William Siang’a; na Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji Bw. Thobias
Andengenye, pamoja na makamanda, askari na watumishi wote wa vyombo hivyo kwa
uhodari wao katika kuilinda nchi yetu na kuhakikisha amani, usalama na uhuru
wetu wa kisiasa na kiuchumi vinadumishwa.
7. Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwapongeza Wabunge wapya
walioingia katika Bunge hili mwaka huu wa fedha ambao ni Mheshimiwa Juma Ali
Juma, Mbunge wa Dimani (CCM); Mheshimiwa Mchungaji Dkt. Getrude Pangalile
Rwakatare – Mbunge wa Viti Maalum (CCM); na Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge,
Mbunge wa Viti maalum (CHADEMA). Nawapongeza pia Waheshimiwa Wabunge
walioteuliwa na Rais: Mheshimiwa Abdallah Majura Bulembo (Mb); Mheshimiwa Anne
Kilango Malecela, (Mb); Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete (Mb); na Mheshimiwa
Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb) ambaye pia ni Waziri wa Katiba
na Sheria. Hongera sana kwenu nyote. Sambamba na hilo, niwapongeze Waheshimiwa
Wabunge waliochaguliwa na Bunge hili kuiwakilisha nchi yetu ya Tanzania katika
Bunge la Afrika Mashariki ambao ni: Mhe. Fancy Nkuhi, Mhe. Happiness Legiko,
Mhe. Maryam Ussi Yahya, Mhe. Dkt. Abdallah Makame, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe,
Mhe. Mhandisi Habibu Mnyaa, Mhe. Alhaji Adam Kimbisa, Mhe. Pamela Massay na
Mhe. Josephine Lemoyani. Nawatakia kazi njema na kuwasisitiza wasiyumbe katika
kusimamia maslahi ya kimkakati (strategic interests) ya Taifa letu katika
mijadala ya Bunge hilo la Afrika Mashariki.
8. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kutoa pole
kwa Watanzania waliopatwa na majanga mbalimbali na misiba, nikianza na Bunge
ambalo liliwapoteza wenzetu, Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir aliyekuwa Mbunge wa
Dimani (CCM) na Mheshimiwa Dkt. Elly Marko Macha aliyekuwa Mbunge wa Viti
Maalum (CHADEMA). Aidha, Bunge liliondokewa na Spika mstaafu, Mheshimiwa Samuel
John Sitta, mzee wa kasi na viwango. Vile vile, natoa pole kwa wazazi na ndugu
wa wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vincent
waliofariki kwa ajali ya gari tarehe 06 Mei, 2017 katika wilaya ya Karatu.
Vivyo hivyo, ninatoa pole kwa ndugu wa askari wetu wanane na wananchi wengine
ambao wameuwawa na kundi la kihalifu katika wilaya za Kibiti na Rufiji kwa
nyakati tofauti katika mwaka huu. Mungu azilaze roho za marehemu wote hao
mahala pema peponi. Amina!
9. Mheshimiwa Spika, ninawiwa kuishukuru Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara
Vijijini na makamu wake Mhe. Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kwa
kupitia na kuchambua mapendekezo ya bajeti ninayowasilisha hivi sasa na kutoa
maoni na ushauri uliochangia kuboresha Bajeti hii ya Serikali kwa mwaka
2017/18. Aidha, napenda kuwashukuru wenyeviti wa kamati za kudumu za kisekta na
waheshimiwa wabunge wote kwa ushauri na mapendekezo mliyotoa kwa Serikali
wakati wa kuchambua Bajeti za kisekta. Ninamshukuru pia Mhe. George Mcheche
Masaju (Mb), Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa
Sheria ya Fedha wa mwaka 2017 na Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2017.
10. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba
Kijaji, Mbunge wa Kondoa, ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, kwa
ushirikiano na msaada anaonipatia katika utekelezaji wa majukumu ya wizara
yangu. Aidha, napenda kumshukuru Bwana Doto M. James, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali kwa usimamizi wa kazi za kila siku
za wizara na uratibu mzuri wa maandalizi ya Bajeti hii, akisaidiwa na Naibu
Makatibu Wakuu, Bibi Dorothy Mwanyika, Bibi Amina Kh. Shaaban na Dkt. Khatibu
Kazungu.
11. Mheshimiwa Spika, ninaendelea kumshukuru sana Profesa
Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania kwa kuongoza kwa weledi taasisi
hiyo nyeti yenye jukumu la kusimamia sekta ya fedha na kulinda utulivu na
ukuaji wa uchumi wa Taifa. Aidha, napenda kutambua kazi nzuri ya viongozi wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania katika kukusanya mapato ya Serikali wakiongozwa na
Bw. Charles Kichere, Kamishna Mkuu wa Mamlaka. Pia ninawashukuru Dkt. Oswald
Mashindano, Msajili wa Hazina na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu. Vile vile, ninawashukuru Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya
Mipango, Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara; Wakuu wa idara na vitengo vya
Wizara, pamoja na watumishi wote wa Wizara na taasisi zake kwa kazi kubwa
waliyoifanya katika kukamilisha Bajeti hii.
12. Mheshimiwa Spika, Bajeti hii pia imezingatia mawazo na
mapendekezo ya wadau mbalimbali wakiwemo jumuiya ya wafanyabiashara na
Washirika wa Maendeleo. Nawashukuru wote kwa mawazo na ushauri. Kipekee
niwashukuru wajumbe wa Kikosi Kazi cha Maboresho ya Mfumo wa Kodi (Task Force
on Tax Reforms) ambayo inaundwa na wawakilishi wa sekta binafsi na wataalam wa
kodi kutoka vyuo vikuu na taasisi za utafiti. Aidha naishukuru Kamati ya
Ushauri kwa Waziri wa Fedha kuhusu hatua za mapato (Advisory Committee on
Revenue Measures). Uchambuzi na ushauri wao umechangia kufikia hatua mpya za
kodi nitakazopendekeza hivi punde.
13. Mheshimiwa Spika, hotuba hii inawasilisha Bajeti ya pili ya Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali inaleta Bajeti hii kwa dhamira ya
kuongeza kasi ya kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kupitia
Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 – 2020; Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
2016/17-2020/21; Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu; na Malengo ya Maendeleo
Endelevu 2030.
14. Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge la 11
tarehe 20/11/2015, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania aliwaeleza Watanzania kwamba, vipaumbele vya Serikali
yake kuhusu uchumi ni kuendeleza na kuimarisha misingi imara ya uchumi wa nchi
yetu iliyojengwa katika awamu za uongozi zilizotangulia. Vipaumbele hivyo ni
vifuatavyo:
i. Kuendeleza
ukuaji wa uchumi na kujenga uchumi wa kipato cha kati ambapo sura na maisha ya
Watanzania walio wengi yafananefanane na nchi ya kipato cha kati;
ii. Kuongeza
mapato, kuziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali, kupunguza matumizi yasiyo
ya lazima, na kusimamia sheria za manunuzi ya umma;
iii. Ujenzi
wa miundombinu ya kiuchumi (barabara, reli, usafiri wa anga na wa majini,
umeme) ili kushawishi na kuvutia wawekezaji wa ndani na wa nje;
iv. Kuhakikisha
kwamba madini na maliasili zetu zinatumika kwa manufaa ya Taifa letu;
v. Kuweka
mkazo mkubwa na kusimamia uendelezaji wa viwanda kwa kutambua kwamba sekta
binafsi ndiyo mhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda. Aidha, aina ya
viwanda tunavyotaka ni vile ambavyo vina sifa ya kuzalisha ajira nyingi,
sehemu kubwa ya malighafi husika itatoka ndani, na vile vya kuzalisha bidhaa
zinazotumiwa na watu wengi nchini;
vi. Kuboresha
kilimo cha mazao, mifugo na uvuvi, hususan kuongeza thamani na kuzifanya
shughuli hizi kuwa za kisasa zaidi kwa kutoa mafunzo, pembejeo, zana na
wataalam;
vii. Kuweka
mkazo katika kuendeleza utalii, ardhi na utunzaji wa mazingira;
viii. Kuongeza
ubora wa elimu, huduma za afya, maji na umeme;
ix. Kupambana
na tatizo kubwa la rushwa, ufisadi na madawa ya kulevya; na
x. Kufanya
mabadiliko makubwa ya kiutendaji serikalini ili kupunguza urasimu.
Hivyo, mapitio ya
mwenendo wa uchumi wa Taifa na tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali
katika mwaka 2016/17 yamelenga kutoa picha ya utekelezaji wa vipaumbele hivyo
vya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
15. Mheshimiwa Spika, katika hotuba niliyosoma leo asubuhi,
nilieleza kwa kirefu hali ya uchumi wetu ilivyokuwa katika mwaka 2016 na miezi
minne ya kwanza ya mwaka huu wa 2017. Inatosha nirejee kuwaambia Watanzania
kwamba uchumi wa Taifa umeendelea kuimarika ambapo Tanzania ilikuwa miongoni mwa
nchi tano za Afrika zilizoongoza kwa kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi.
Kwa mujibu wa takwimu za uchumi za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF World
Economic Outlook Database), nchi hizo tano ni Ivory Coast (asilimia 7.9);
Tanzania (asilimia 7.1); Senegal (asilimia 6.6); Djibouti (asilimia 6.5); na
Ethiopia (asilimia 6.5). Aidha, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha
Duniani Bw. Tao Zhang alipotembelea Tanzania kwa mara ya kwanza mwezi Mei 2017,
alitoa tathmini yake kwamba uchumi wa Tanzania umebaki kuwa imara kutokana na
maboresho ya kisera yaliyotekelezwa chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa
Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hasa katika maeneo ya ukusanyaji wa
mapato ya ndani na vita dhidi ya rushwa na ufisadi.
16. Mheshimiwa Spika, jarida la Benki ya Dunia (Tanzania Economic
Update) lililochapishwa Aprili 2017 linabainisha waziwazi kuwa uchumi wa Taifa
ni imara kwa kuangalia viashiria mbalimbali kama ukuaji wa uchumi, mfumuko wa
bei, urari wa biashara, akiba katika fedha za kigeni na thamani ya shilingi, na
naomba kunukuu kwa kiingereza:
“Tanzania’s
economic performance continues to rank among the highest in the region. The
real GDP growth rate has consistently outpaced its EAC peers. The inflation
rate remains relatively low. The current account deficit has significantly
improved, with gross reserves sufficient to cover four months of imports. The
shilling has also remained stable in 2016, following significant depreciation
and volatility in 2015.”
17. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, pamekuwa na
maeneo ambayo yametawala mijadala kuhusu afya ya uchumi wa Taifa, ambayo
napenda kuyaelezea kwa kifupi. Maeneo hayo ni pamoja na ukwasi katika uchumi,
kufungwa kwa biashara, na madai kwamba sekta binafsi imepoteza matumaini na
kujiamini (private sector confidence) kutokana na baadhi ya hatua
zilizochukuliwa na serikali bila ushirikishwaji wa wadau.
Hali ya Ukwasi Katika
Uchumi
18. Mheshimiwa
Spika, ukwasi ni kiasi cha
fedha kilichopo katika uchumi kinachojumuisha fedha taslim zilizoko kwenye
mzunguko nje ya mabenki na rasilimali fedha nyingine ambazo zinaweza
kubadilishwa na kuwa fedha taslimu bila kikwazo. Utoshelevu wa ukwasi katika
uchumi hupimwa kwa viashiria mbalimbali vikiwemo ujazi wa fedha, mwenendo wa mikopo
kwa sekta binafsi, kiwango cha mitaji ya mabenki, uwiano kati ya mali inayoweza
kubadilishwa kuwa fedha taslim na amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi
na upatikanaji wa huduma za kifedha.
19. Mheshimiwa Spika, katika kipindi kilichoishia mwezi Machi
2017, hali ya baadhi ya vigezo vya ukwasi inaonyesha kuwa ujazi wa fedha kwa
tafsiri pana zaidi (M3) ambao unajumuisha sarafu na noti zilizoko katika
mzunguko nje ya mabenki, amana za muda mfupi, muda maalum na amana katika fedha
za kigeni zilizopo katika mabenki, uliongezeka na kufikia shilingi trilioni
22.53 kutoka shilingi trilioni 21.65 katika kipindi kama hicho mwaka 2016, sawa
na ongezeko la asilimia 4.1. Aidha, sekta ya kibenki iliendelea kuwa imara na
himilivu, ikiwa na viwango vya mitaji na ukwasi ulio juu ya ukomo unaohitajika
kisheria kama ifuatavyo: kwa kutumia kigezo cha uwiano kati ya mali inayoweza
kubadilishwa kuwa fedha taslim na amana zinazoweza kuhitajika kwa muda mfupi
(Liquid Assets to Demand Liabilities), uwiano huu ulikuwa asilimia 35.9 mwezi
Machi 2017 ikilinganishwa na uwiano wa chini unaohitajika kisheria wa asilimia
20. Vile vile, uwiano wa mtaji wa msingi na rasilimali za benki ulikuwa
asilimia 19.0 ambao uko juu ya kiwango cha chini kinachohitajika kisheria cha asilimia
10. Kadhalika, amana za wateja katika benki za biashara ziliongezeka kwa
asilimia 0.3 kutoka shilingi trilioni 18.84 mwezi Machi 2016 hadi shilingi
trilioni 18.89 mwezi Machi 2017.
20. Mheshimiwa Spika, takwimu pia zinaonesha kuwa ukwasi wa
mabenki ulianza kutetereka kutokana na kuongezeka kwa mikopo chechefu kutoka
asilimia 8.3 mwezi Machi 2016 hadi asilimia 10.9 Machi 2017 ikilinganishwa na
kiwango kinachohitajika cha asilimia 5. Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka
kidogo kwa asilimia 3.7 katika kipindi cha mwaka ulioishia Machi 2017
ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 23.6 katika kipindi kama hicho mwaka
2016. Kupungua kwa kiwango cha ukuaji huo kulitokana kwa kiasi kikubwa na
kuyumba kwa biashara duniani ambako kuliathiri nchi nyingi duniani ikiwemo
Tanzania. Napenda kuchukua fursa hii kuyataka mabenki yote nchini kusimamia
sawasawa taratibu za kibenki katika utoaji wa mikopo.
21. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu imechukua
hatua ikiwa ni pamoja na kupunguza riba ambazo benki za biashara hukopa kutoka
Benki Kuu (Discount Rate) ili kuongeza ukwasi katika benki za biashara na
hivyo kuziwezesha kukopa kwa gharama nafuu zaidi. Riba hiyo imepunguzwa kutoka
asilimia 16.0 iliyokuwa ikitumika tangu mwezi Novemba 2013 hadi asilimia 12.0
ambayo imeanza kutumika rasmi tarehe 6 Machi 2017. Aidha, katika kuimarisha
zaidi soko la fedha nchini, Benki Kuu ilipunguza kiwango cha amana ambacho
benki za biashara zinatakiwa kuhifadhi Benki kuu kama dhamana (Statutory
Minimum Reserve Requirement – SMR) kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0 ili
kuziwezesha benki za biashara kuwa na ukwasi zaidi kwa ajili ya kukopesha sekta
binafsi. Hatua hii imeanza kutumika rasmi mwezi Aprili 2017. Ni matumaini ya
Serikali kuwa hatua hizi zitaziwezesha benki za biashara nchini kuongeza ukwasi
wa kutosha kuwakopesha wananchi kwa riba nafuu.
22. Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, mwaka 2016/17
benki tatu za biashara zilifungwa kutokana na sababu mbalimbali. Benki hizo ni
Benki ya Twiga, FBME Bank Limited; na Mbinga Community Bank. Mnamo tarehe 28
Oktoba 2016, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ilichukua usimamizi wa
benki ya Twiga baada ya kubaini kuwa benki hiyo
ilikuwa na upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na
Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na
kanuni zake. Upungufu huu wa mtaji ulionekana kuhatarisha usalama
wa sekta ya fedha na pia kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa benki ya Twiga
kungehatarisha usalama wa amana za wateja wake. Hata hivyo, baada ya
kukamilika kwa zoezi la kutathmini hali ya kifedha ya benki hiyo, Serikali
iliruhusu baadhi ya huduma za benki hiyo ziendelee huku ikiendelea na mchakato
wa kupitia na kuchambua njia mbadala za kutatua tatizo la mtaji linaloikabili
benki ya Twiga. Kwa sasa Serikali inapitia maombi yaliyoletwa na wawekezaji
mbalimbali wanaotaka kununua hisa na kuongeza mtaji wa benki hiyo.
23. Mheshimiwa Spika, tarehe 8 Mei, 2017 Serikali ilisimamisha
shughuli zote za FBME Bank Limited; kufuta leseni yake ya kufanya shughuli za
kibenki; kuiweka chini ya ufilisi; na kuiteua Bodi ya Bima ya Amana kama
mfilisi. Uamuzi huu ulifikiwa kutokana na mwelekeo wa benki hiyo kuwa
mashakani kufuatia mahakama ya Marekani kukubaliana na ombi la Taasisi ya
Marekani ya Kupambana na Uhalifu wa Kifedha (FinCEN) la kuifungia FBME kutumia
mfumo wa kibenki wa Marekani kutokana na tuhuma za kujihusisha na biashara ya
utakatishaji wa fedha haramu. Naomba tena kupitia hotuba hii ya Bajeti ya
Serikali kwa mwaka 2017/18 kuyaonya mabenki yote yatakayobainika kujihushisha
na biashara ya utakatishaji fedha haramu au kufadhili ugaidi au kwenda kinyume
na sheria za nchi kwamba Serikali itachukua hatua kali za kufuta leseni za
kufanya shughuli za kibenki hapa nchini mara moja na hatua nyingine kwa mujibu
wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake, na hata
sheria za kimataifa.
24. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania
ilichukua hatua nyingine ya kuifunga MbingaCommunity Bank Plc, kusitisha
shughuli zake zote za kibenki na kufuta leseni yake ya biashara ya kibenki
kuanzia tarehe 12 Mei, 2017. Benki hiyo iliwekwa chini ya ufilisi na
kuiteua Bodi ya Bima ya Amana kama mfilisi. Uamuzi huu ulichukuliwa baada ya
Serikali kujiridhisha kuwa MbingaCommunity Bank Plc ina upungufu
mkubwa wa mtaji na ukwasi kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za
Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake. Upungufu huu wa mtaji na ukwasi ungeweza
kuhatarisha usalama wa sekta ya fedha, na wa amana za wateja. Serikali inapenda
kuuhakikishia umma wa Watanzania kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana
katika mabenki yaliyopo nchini kwa lengo la kulinda utulivu katika sekta ya
fedha.
25. Mheshimiwa Spika, wigo wa utoaji huduma za kifedha kwa
wananchi walio wengi zaidi na kwa gharama nafuu umepanuka sana kutokana na
mtandao mkubwa wa mabenki na taasisi nyingine za fedha zipatazo 64 [benki za
biashara 40, benki za maendeleo 3, benki za jumuiya 11, huduma ndogo za kifedha
– (micro finance) 5, taasisi zinazotoa mikopo binafsi (private
credit) 2, na kampuni za huduma za kifedha za kukodisha (lease finance) 3].
Sambamba na hizi, kuna huduma za kifedha na malipo kupitia huduma za benki zinazohamishika
(mobile banking), mawakala na simu za mkononi. Hivi sasa, inakadiriwa
kuwa Watanzania zaidi ya milioni 17 wanafanya miamala kwenye mfumo wa malipo
kupitia simu za mkononi.
Kufungwa kwa Biashara
26. Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo lilikuwa
likizungumzwa sana na wananchi na pia hapa Bungeni ni kuhusu kuongezeka kwa
kasi ya kufunga biashara hususan, eneo la Kariakoo katika Jiji la Dar es salaam
na katika miji mingine. Kwa mujibu wa taarifa zilizofikishwa TRA, katika
kipindi cha kuanzia Julai 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya biashara 7,277
zilifungwa katika mikoa mbalimbali nchini. Mwenendo huu kwa ujumla siyo mzuri
kwa sababu wananchi wanapoteza ajira na kipato, Serikali inakosa mapato ya kodi
na uchumi unadorora. Hivyo, ni muhimu pale wimbi la kufungwa kwa biashara
linapotokea jitihada zifanyike kuelewa aina gani za biashara zinafungwa, kwa
nini zinafungwa na hatua gani zichukuliwe kudhibiti hali hiyo.
27. Mheshimiwa Spika, ziko sababu nyingi zinazoweza kuwa
zimepelekea hali hiyo, ikiwa ni pamoja na ushindani mkali wa kibiashara;
usimamizi dhaifu wa biashara; kuongezeka kwa gharama za kufanya biashara kama
vile usafirishaji, kodi na tozo mbalimbali; na kutozingatia masharti ya kufanya
biashara. Lakini pia, imedhihirika kwamba, wafanyabiashara wengi wameanza
mazoea ya kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mapato mara wanapofunga biashara zao.
Hii ilitokana na elimu iliyotolewa na Mamlaka kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa
ambazo zimewafanya walipa kodi kufahamu kuwa unapofunga biashara bila kutoa
taarifa, kodi inajilimbikiza na wataendelea kudaiwa na TRA.
28. Mheshimiwa Spika, ni vema kutambua kwamba kufunguliwa au
kufungwa kwa biashara ni jambo la kawaida kabisa katika uendeshaji wa biashara.
Napenda kuliarifu Bunge hili kuwa, katika kipindi hicho hicho cha Julai 2016
mpaka Machi 2017, Mamlaka ya Mapato ilisajili biashara mpya zipatazo 224,738.
Hivyo, picha inayotolewa isiwe ya upande mmoja tu. Ni vema pia kujua kwamba
kufungwa kwa biashara sio kwa Tanzania pekee. Ni jambo ambalo linatokea katika
vipindi mbalimbali katika historia za mataifa na kwa viwango tofauti tofauti.
Watu wengi miongoni mwetu tumesoma kuhusu anguko kuu la biashara lililotokea
katika bara la Ulaya na Amerika kati ya mwaka 1929-1939 likijulikana kama “the
Great Depression”. Huko China nako katika miaka 1980 biashara nyingi
zilipigwa na dhoruba ambapo baadhi zilizama lakini nyingine ziliendelea kukua.
Haya yameelezwa vizuri sana katika kitabu cha Tian Tao na wenzake
kinachoitwa Huawei: Leadership, Culture and Connectivity kilichochapishwa
mwaka 2017. Naomba kunukuu kwa lugha ya kiingereza kutoka ukurasa wa 43 wa
kirumi wa kitabu hicho:
“From the 1980s
onward, China was swept up in the largest wave of commercial development in
human history. Businesses at the time were like ships, each raised up and
carried along by the sheer momentum of the wave. Some, however, soon capsized
and were swallowed up, while most drifted along, going with the flow. Others
crashed against barriers in the sea or got stranded on deserted islands. Only a
few rose atop the crest of the wave and survived, eventualy sailed towards new
lands.”
29. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara
na Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara yangu inaendelea kufuatilia kwa karibu
mwenendo wa biashara nchini na itachukua hatua stahiki itakapobidi kufanya
hivyo. Wito wa Serikali kwa wafanyabiashara nchini ni kwamba fanyeni biashara
zenu bila hofu kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu za nchi.
Madai ya Kuwa Sekta
Binafsi Imepoteza Kujiamini (Private Sector Confidence)
30. Mheshimiwa Spika, yamekuwepo madai ya kuwa wafanyabiashara
wamepoteza kujiamini kutokana na matamshi ya viongozi na hatua zilizochukuliwa
na Serikali bila kuwashirikisha wafanyabiashara ambazo zimezua hofu. Napenda
niwahakikishie wafanyabiashara kuwa, Serikali ya awamu ya tano inaamini kwa
dhati kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi na inathamini sana na kupongeza
mchango mkubwa sana wa wafanyabiashara katika uchumi na maendeleo ya Taifa kwa
ujumla. Ni ukweli ulio dhahiri kwamba, sehemu kubwa ya uzalishaji wa bidhaa na
huduma mbalimbali kwa ajili ya matumizi nchini na mauzo nje yanayotupatia fedha
za kigeni unafanywa na sekta binafsi. Lakini pia sekta binafsi ndiyo mwajiri
mkuu na chanzo kikuu cha mapato ya Serikali. Hivyo, sekta binafsi ndiyo mbia
mkuu wa Serikali katika kazi ya kuharakisha maendeleo nchini.
31. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu mkubwa wa sekta
binafsi na wafanyabiashara, Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kujenga
mazingira mazuri ya kufanya biashara. Katika kuboresha mazingira ya biashara na
uwekezaji, Serikali iliendelea na jitihada za kuimarisha utulivu wa uchumi
jumla, kupunguza urasimu, kuharakisha maamuzi, kuimarisha ulinzi na usalama na
kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu imara na huduma bora zikiwemo umeme wa
uhakika na mikopo kwa sekta binafsi. Hayo yote ni maeneo ambayo Serikali
iliyapa na itaendelea kuyapa kipaumbele. Aidha, Serikali bado ina dhamira ya
dhati kuendeleza mashauriano na wafanyabiashara kupitia utaratibu wa mikutano
ya Baraza la Taifa la Biashara, Taasisi ya Sekta Binafsi na makongamano
mengine.
32. Mheshimiwa Spika, tumeanza kuona viashiria bora zaidi
katika eneo hili la kuboresha mazingira ya biashara. Taarifa ya Benki ya Dunia
ya mwaka 2017 ilionesha kuwa, Tanzania ilikuwa nchi ya 132 kwa urahisi wa kufanya
biashara ikiwa imepiga hatua kwa nafasi 12 kutoka nafasi ya 144 mwaka 2016.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya “Fahirisi ya Uwekezaji Afrika ya mwaka 2016”
(Africa Investment Index, 2016) iliyotolewa na taasisi ya “Quantum Global
Research Lab” ya Uingereza, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza miongoni mwa
nchi za Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji na ya nane kwa Afrika, ikiwa
imepiga hatua kutoka nafasi ya 19 mwaka 2015.
33. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuzungumza na
wafanyabiashara ili kupata maoni na ushauri wao kuhusu sera mbalimbali na
mwenendo wa uchumi kwa ujumla na kutatua kero zao. Nia ya Serikali ni
kuhakikisha wanafanya biashara katika mazingira mazuri yanayotabirika ili
biashara hizo zikue na kushamiri, ajira ziongezeke na Serikali ipate kodi
stahiki kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na huduma za jamii.
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania itaendelea kuboresha mfumo wa kodi
na kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na kuwawezesha kufanya biashara
zao kwa urahisi. Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na taasisi
nyingine za Serikali itaendelea na jitihada za kuelimisha umma juu ya umuhimu
wa kurasimisha shughuli zao za kiuchumi. Pamoja na kutoa elimu, napenda
kusisitiza kuwa, kulipa kodi ni wajibu wa msingi wa kila raia kwa maendeleo ya
Taifa. Lazima Watanzania tulipe kodi. Serikali hii haitavumilia uporaji wa
rasilimali za nchi na ukwepaji kodi kwa kivuli cha kulinda imani (confidence)
ya wafanyabiashara.
34. Mheshimiwa Spika, napenda nitumie pia fursa hii
niwakumbushe watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwamba, kodi zinatozwa kwa
kuongozwa na sheria na kanuni zake. Matumizi ya vitisho na unyanyasaji kwa
walipa kodi, kuwadai rushwa au kuwazidishia makadirio ya kodi ili kuwakomoa ni
mambo ya hovyo na hayakubaliki hata kidogo! Wale watumishi wa TRA, ambao
naamini ni wachache tu, wanaojihusisha na vitendo hivyo, wakome kabisa kufanya
hivyo. Wale tutakaowabaini tutawachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria za
utumishi wa umma. Aidha, natoa rai kwa wafanyabiashara wetu na wananchi
wazalendo kutupatia taarifa za ukweli kuhusu mwenendo mbaya wa mtumishi yeyote
wa TRA ili zifanyiwe kazi na Serikali. Nawaomba pia mfanye hivyo hivyo
kutupatia taarifa kuhusu wafanyabiashara wanaokwepa kodi ili tuwashughulikie
ipasavyo.
II. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA
2016/17
Mapato
35. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2016 hadi
Aprili 2017, mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia shilingi bilioni 20,710.5, sawa
na asilimia 70.1 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 29,539.6.
Mchanganuo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo:
i. Mapato ya
kodi yalifikia shilingi bilioni 11,644.6 sawa na asilimia 77.1 ya lengo la
mwaka la kukusanya shilingi bilioni 15,105.1;
ii. Mapato
yasiyo ya kodi yalifikia shilingi
bilioni 1,611.0 sawa na asilimia 59.8 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 2,693.0;
iii. Mapato ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa
yalikuwa shilingi bilioni 399.3 sawa na asilimia 60.0 ya lengo la kukusanya
shilingi bilioni 665.4 kwa mwaka;
iv. Mikopo kutoka vyanzo vya ndani ilifikia
Shilingi bilioni 4,715.6, sawa na asilimia 87.7 ya shilingi bilioni 5,374.3
zilizotarajiwa kukopwa kwa mwaka kutoka katika chanzo hiki; na
v. Misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka
nje iliyopokelewa hadi Aprili 2017 ni shilingi bilioni 2,340.1 sawa na asilimia
65.0 ya lengo la shilingi bilioni 3,600.8 zilizoahidiwa na Washirika wa
Maendeleo kwa mwaka 2016/17.
36. Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/17, Serikali
ilipanga kukopa kiasi cha shilingi bilioni 2,100.9 kutoka kwenye vyanzo vya
kibiashara ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo lakini haikuweza
kukopa kutokana na hali ya soko la fedha la kimataifa kutokuwa nzuri. Hata
hivyo, Serikali inakamilisha majadiliano na wakopeshaji ambapo kiasi cha dola
za Marekani milioni 500 kinatarajiwa kupatikana kabla ya mwisho wa mwezi huu wa
Juni 2017.
Kudhibiti upotevu wa
mapato
37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17, Serikali
imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kudhibiti upotevu wa mapato. Katika
kutekeleza azma hii, baadhi ya taasisi zimeanza kutumia mifumo ya kielektroniki
katika kukusanya mapato. Mfano, Halmashauri zinatumia Mfumo wa Ukusanyaji wa
Mapato wa Serikali za Mitaa (Local Government Revenue Collection System -
LGRCS) na Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Dar es Salaam linatumia Mfumo wa
Udhibiti wa Vyombo vya Moto Barabarani (Traffic Management System).
Aidha, Serikali imekamilisha mfumo wa kielektroniki (Government e-Payment
Gateway System-GePGs) utakaotumika katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Mfumo utasaidia Serikali kuwa na uhakika wa mapato ya nayokusanywa kutoka
katika vyanzo mbalimbali kwa wakati na kurahisisha ulipaji wa kodi, tozo na ada
mbalimbali. Aidha, tarehe 01 Juni, 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alizindua Mfumo mpya wa
ukusanyaji mapato kwa mjia ya kielektroniki. Mfumo huo unalenga kupata taarifa
sahihi za mlipakodi na mtoa huduma hususan makampuni ya simu, mabenki na
televisheni.
Ukusanyaji wa Kodi ya Majengo
38. Mheshimiwa Spika, Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 iliyopitishwa
na Bunge lako Tukufu inaipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jukumu la
kukusanya kodi ya majengo kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa zote nchini kuanzia
mwaka 2016/17. TRA ilipewa jukumu hili kutokana na kuwa na ufanisi katika
ukusanyaji na mtandao mpana ulioenea nchi nzima. Uamuzi huu haukuwa na maana ya
kupora chanzo hiki cha mapato kutoka katika halmashauri, bali kuongeza ufanisi
katika ukusanyaji wa kodi kutoka katika chanzo hiki.
39. Mheshimiwa Spika, baada ya kupitishwa kwa Sheria hiyo,
hatua iliyofuata ilikuwa ni kutolewa kwa Tangazo la Serikali No. 276 la tarehe
30 Septemba 2016 lililoitaka TRA kuanza zoezi hilo kwa Halmashauri 30 za awali.
Jukumu la kukusanya kodi ya majengo katika halmashauri zilizobaki liliendelea
kubaki katika halmashauri husika. Katika kipindi hicho, Serikali kupitia TRA
ilifanya maandalizi ya taratibu na mifumo ya ukusanyaji. Maandalizi hayo
yalihusisha kutengeneza kanuni za ukusanyaji, kutengeneza mfumo wa ukusanyaji
wa kodi hii, kuunda kitengo, kuweka wafanyakazi na vitendea kazi kabla ya
kuanza ukusanyaji.
40. Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa taratibu hizo,
TRA ilianza rasmi kukusanya Kodi ya Majengo tarehe 1 Oktoba, 2016 katika
majiji, manispaa na miji 30. Hadi Mei, 2017, TRA imekusanya jumla ya Shilingi
milioni 15,134.2. Ni matumaini ya Serikali kwamba kwa mwaka 2017/18, TRA
itafanya vizuri zaidi katika ukusanyaji wa kodi hii ya majengo. Maboresho ya
kukusanya kodi hiyo nitayaeleza baadae. Natoa rai kwa wadau wote wakiwemo
wamiliki wa majengo, viongozi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na Mamlaka ya
Mapato Tanzania kushirikiana bega kwa bega kuhakikisha wanafanikisha
zoezi hili la ukusanyaji wa kodi ya majengo kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa
ujumla.
Matumizi
41. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi
Aprili, 2017 jumla ya shilingi bilioni 20,036.5 zilitolewa kwa Wizara, Idara
zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kati ya
kiasi hicho, shilingi bilioni 15,480.9 zilizotolewa kwa ajili ya matumizi ya
kawaida sawa na asilimia 87.4 ya lengo la mwaka na shilingi bilioni 4,555.5
zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 38.5 ya lengo la
shilingi bilioni 11,820.5 zilizotengwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo kwa
mwaka. Fedha za maendeleo zilizotolewa zinajumuisha fedha za ndani shilingi
bilioni 3,647.7 na fedha za nje shilingi bilioni 907.8. Hata hivyo, baadhi ya
fedha za nje za kugharamia miradi ya maendeleo hazikujumuishwa kwenye matumizi
kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo: kuchelewa kupata thamani halisi ya
vifaa vilivyopelekwa moja kwa moja kwenye miradi kutokana na baadhi ya
Washirika wa Maendeleo kuendelea kupeleka fedha moja kwa moja kwenye miradi
bila kupitia mfumo wa malipo wa Serikali.
42. Mheshimiwa Spika, baadhi ya mahitaji yaliyopewa kipaumbele
katika utoaji wa fedha za matumizi ya maendeleo kati ya Julai, 2016 hadi
Aprili, 2017 ni pamoja na:-
i. Ujenzi
na ukarabati wa barabara kuu za Mikoa na Halmashauri (Mfuko wa Barabara)
shilingi bilioni 675.9;
ii. Miradi
ya ujenzi wa barabara ikiwemo ulipaji wa madeni ya wakandarasi na wahandisi
washauri shilingi bilioni 540.3;
iii. Miradi
ya uzalishaji wa umeme, uboreshaji wa njia za kupitisha umeme na usambazaji wa
umeme vijijini shilingi bilioni 421.5;
iv. Mikopo
kwa wanafunzi wa elimu ya juu shilingi bilioni 393.2;
v. Malipo
ya awali ya ujenzi wa reli kwa kiwango cha ‘standard gauge’ awamu ya kwanza
katika eneo la Dar – Morogoro (Km 205) shilingi bilioni 300;
vi. Ununuzi
wa ndege mbili na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege nne shilingi bilioni
234.9;
vii. Usambazaji
wa maji mijini na vijijini shilingi bilioni 186.4; na
viii. Uboreshaji
wa huduma za afya katika ngazi zote shillingi bilioni 170.6 ikiwemo ununuzi wa
dawa na vifaa tiba shilingi bilioni 156.1.
43. Mheshimiwa Spika, utoaji wa fedha za matumizi ya kawaida
unajumuisha shilingi bilioni 5,320.3, sawa na asilimia 80.6 ya lengo la mwaka
kwa ajili ya kugharamia mishahara; shilingi bilioni 7,775.5, sawa na asilimia
97.2 ya lengo la mwaka kwa ajili ya kulipia Deni la Taifa na shilingi bilioni
2,385.1, sawa na asilimia 76.5 ya lengo la mwaka kwa ajili ya kugharamia
matumizi mengineyo.
44. Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyopewa kipaumbele katika
utoaji wa fedha za matumizi mengineyo ni pamoja na:
i. Kugharamia
shughuli za vyombo vya ulinzi na usalama shilingi bilioni 591.3;
ii. Elimu
msingi bila malipo shilingi bilioni 203.0;
iii. Uendeshaji
wa mitihani ya kitaifa shilingi bilioni 69.9;
iv. Mfuko
wa Bunge shilingi bilioni 69.1;
v. Kugharamia
balozi zetu nje ya nchi shilingi bilioni 68.7;
vi. Posho
ya madaktari wanafunzi shilingi bilioni 15.3;
vii. Ruzuku
ya pembejeo shilingi bilioni 15.0;
viii. Ruzuku
ya vyama vya siasa shilingi bilioni 14.2; na
ix. Ununuzi
wa chakula cha hifadhi ya Taifa shilingi bilioni 13.0.
Kudhibiti matumizi
45. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2016/17, Sera za Matumizi ya
Serikali zililenga kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa
kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015, Sheria ya Usimamizi wa Fedha
za Umma SURA 348, Sheria ya Fedha ya Mamlaka za Serikali za Mitaa SURA 290,
Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2013 SURA 410 na Kanuni husika, pamoja na
miongozo mbalimbali ya Serikali. Lengo kuu lilikuwa ni kupunguza matumizi
yasiyo na tija, kuziba mianya ya ufujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi
kikubwa cha fedha kwenye maeneo ya kipaumbele.
46. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Serikali imeendelea
kudhibiti matumizi katika maeneo mbalimbali ikiwemo: kupunguza safari za nje
kwa kuhakikisha kuwa vibali vinatolewa kwa safari zenye manufaa kwa Taifa;
kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara;
na kuendelea kudhibiti gharama za uendeshaji wa magari ikiwa ni pamoja na
matengenezo, mafuta na vilainishi. Aidha, utaratibu wa kufanya mikutano na
makongamano katika kumbi za Serikali na taasisi za umma umeongeza udhibiti wa
matumizi ya Serikali.
Malimbikizo, uhakiki na
ulipaji wa Madai
47. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Juni, 2016 madai
yaliyokuwa yamewasilishwa na taasisi mbalimbali yalikuwa jumla ya shilingi
bilioni 2,934.4 ambapo jumla ya shilingi bilioni 1,997.9 sawa na asilimia 68.1
zilithibitika kuwa madai halali baada ya uhakiki. Kati ya madai yaliyohakikiwa,
Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 796.5 hadi mwezi Machi, 2017 na
hivyo kubakia na madai ya shilingi bilioni 1,201.4. Kati ya madai hayo
yaliyolipwa, shilingi bilioni 632.1 ni kwa ajili ya wakandarasi na wahandisi
washauri; shilingi bilioni 78.9 kwa ajili ya wazabuni wa huduma na bidhaa
ikiwemo shilingi bilioni 11.2 za Bohari Kuu ya Madawa (MSD); shilingi bilioni
67.6 kwa ajili ya malimbikizo ya madai ya watumishi; na shilingi bilioni 17.9
ni kwa ajili ya watoa huduma mbalimbali.
48. Mheshimiwa Spika, kati ya
Julai hadi Desemba 2016, malimbikizo ya madai mapya kutoka kwenye taasisi
mbalimbali yalikuwa jumla ya shilingi bilioni 899.55. Hivyo, hadi Desemba 2016,
madai yote yalifikia shilingi bilioni 2,100.90. Madai hayo yamegawanyika kama
ifuatavyo: shilingi bilioni 910.30 wakandarasi; shilingi bilioni 890.16 ni
wazabuni wa huduma na bidhaa; shilingi bilioni 159.10 ni madai ya
watumishi mbalimbali; shilingi bilioni 75.45 ni ankara za maji,umeme na simu;
na shilingi bilioni 65.89 ni pango la ofisi. Aidha, kati ya madai ya wazabuni
wa huduma na bidhaa, lipo deni la MSD ambalo ni shilingi bilioni 145.89
linalotokana na malimbikizo ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba vilivyochukuliwa
na taasisi mbalimbali za serikali na havikuwa vimelipiwa.
Deni la Taifa
49. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia Deni la Taifa
kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134. Ili kuhakikisha
kuwa deni la Taifa linaendelea kusimamiwa ipasavyo, Bunge lako Tukufu
lilipitisha marekebisho ya Sheria hiyo mwezi Novemba, 2016. Baadhi ya maeneo
yaliyorekebishwa ni pamoja na: kuongeza masharti kwa Taasisi na Mashirika ya
Umma yanayoomba dhamana ya Serikali ili kudhibiti utoaji wa dhamana hizo;
kuweka utaratibu maalum wa kisheria ambao unahakikisha kwamba fedha zilizokopwa
na Serikali ya Muungano kwa lengo la kugharamia miradi ya maendeleo Zanzibar
inafika kama ilivyokusudiwa; na kuongeza wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Deni la Taifa.
50. Mheshimiwa Spika, Hadi Machi 2017, deni la Taifa lilifikia
shilingi bilioni 50,806.5. Kati ya kiasi hicho, deni la Serikali ni shilingi
bilioni 42,883.6 na deni la sekta binafsi ni shilingi bilioni 7,922.9. Deni la
Serikali limeongezeka kwa asilimia 9.2 kutoka shilingi bilioni 39,274.6 Machi, 2016 hadi shilingi bilioni 42,883.6
Machi, 2017. Ongezeko la deni la Serikali lilitokana na mikopo mipya na
ya zamani iliyopokelewa katika kipindi cha mwaka 2016/17 kutoka vyanzo vya
masharti nafuu na ya kibiashara, malimbikizo ya riba ya deni la nje kwenye nchi
zisizo wanachama wa kundi la Paris ambazo zinatakiwa kutoa msamaha wa madeni
lakini bado hazijatoa pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola
za Marekani.
51. Mheshimiwa Spika, deni la Serikali linajumuisha deni la ndani
la shilingi bilioni 12,073.7 sawa na asimilia 28.1 na deni la nje la shilingi
bilioni 30,809.9 sawa na asilimia 71.9. Deni la nje linajumuisha mikopo ya
masharti nafuu kutoka kwenye mashirika ya fedha ya kimataifa, sawa na asilimia
56.8, mikopo kutoka nchi wahisani ilifikia asilimia 16.3 na mikopo kutoka
mabenki ya kibiashara ya kimataifa ilifikia asilimia 26.9 ya deni lote la
nje. Mikopo hiyo ilitumika kugharamia miradi ya maendeleo hususan katika
sekta za ujenzi (barabara na reli), nishati, uchukuzi, elimu na maji.
Tathmini ya Uhimilivu wa
Deni la Taifa
52. Mheshimiwa Spika, matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa deni
iliyofanyika mwezi Novemba, 2016 yalibainisha kuwa Deni la Taifa ni himilivu
kwa muda mfupi, wa kati na mrefu. Katika tathmini hiyo, viashiria vinaonesha
kuwa: thamani ya sasa ya jumla ya Deni la Taifa (Present Value of Total Public
Debt) kwa Pato la Taifa ni asilimia 34.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia
56; thamani ya sasa ya Deni la nje (Present Value of External Debt) kwa
Pato la Taifa ni asilimia 19.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; thamani
ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 97.7 ikilinganishwa
na ukomo wa asilimia 150; na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mapato ya ndani
ni asilimia 145.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 250. Viashiria hivyo
vinapima uwezo wa nchi kukopa bila kuathiri uhimilivu wa deni (solvency
indicators).
53. Mheshimiwa Spika, kutokana na tathmini ya uhimilivu wa
deni la Taifa, ambayo inapima uwezo wa nchi kulipa deni, uwiano wa ulipaji wa
deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani umefikia asilimia 11.5 ikilinganishwa
na ukomo wa asilimia 20 na uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo
ya bidhaa nje ni asilimia 7.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20. Kwa
kuzingatia viashiria hivyo, ambavyo vipo chini ya ukomo unaokubalika kimataifa,
Tanzania bado ina uwezo wa kuendelea kukopa kutoka ndani na nje ya nchi ili
kugharamia shughuli zake za maendeleo na pia ina uwezo wa kulipa mikopo
inayoiva kwa kutumia mapato yake ya ndani na nje.
III. SERA ZA BAJETI KWA MWAKA 2017/18
54. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa makubaliano ya nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, dhima ya Bajeti ya mwaka 2017/18
ni “kujenga uchumi wa viwanda utakao chochea ajira na ustawi endelevu
wa jamii”. Hii inaendana na msisitizo na vipaumbele vya Serikali ya
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kujenga Tanzania ya viwanda.
Shabaha za Uchumi Jumla
55. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa bajeti ya 2017/18 unalenga
kufikia shabaha za uchumi jumla kama ifuatavyo:
i. Pato
halisi la Taifa kukua kwa asilimia 7.1 mwaka 2017 kutoka asilimia 7.0 mwaka
2016;
ii. Kuendelea
kudhibiti mfumuko wa bei katika wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 5.0 na
asilimia 8.0 mwaka 2017;
iii. Mapato
ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri kufikia asilimia 15.8 ya Pato la
Taifa mwaka 2016/17, na kuendelea kuongezeka kufikia asilimia 16.5 ya Pato la
Taifa mwaka 2017/18;
iv. Mapato
ya kodi yanakadiriwa kuongezeka kufikia asilimia 14.2 ya Pato la Taifa mwaka
2017/18 kutoka matarajio ya asilimia 13.3 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17;
v. Matumizi
ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka kufikia asilimia 26.2 ya Pato la Taifa
mwaka 2017/18 kutoka matarajio ya asilimia 23.7 ya Pato la Taifa mwaka
2016/17;
vi. Nakisi
ya bajeti inatarajiwa kupungua kufikia asilimia 3.8 ya Pato la Taifa kutoka
asilimia 4.5 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17;
vii. Nakisi
katika urari wa malipo ya kawaida inatarajiwa kuwa asilimia 7.0 ya Pato
la Taifa mwaka 2017/18; na
viii. Kuwa
na akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na
huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.
Sera za Mapato
56. Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuongeza na
kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutekeleza sera zifuatazo:
i. Kuendelea
kusimamia kikamilifu matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika
ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato;
ii. Kuendelea
kupanua wigo wa walipa kodi ikiwa ni pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi
ili iweze kuingia katika mfumo wa kodi;
iii. Kuimarisha
ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi na kuboresha usimamizi wake;
iv. Kuendelea
kufanya uthamini wa majengo na kusimamia ulipaji ili kuongeza mapato yatokanayo
na kodi ya majengo;
v. Kurasimisha
miliki za ardhi kwa lengo la kuongeza mapato; na
vi. Kuendelea
kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija.
57. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2017/18, Serikali itaendelea kupanua soko la fedha la ndani ili kuwa na
washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi kwenye soko watakaowezesha Serikali
kupata fedha za kuziba nakisi kwenye bajeti kwa riba nafuu. Serikali
itahakikisha kuwa, mchakato wa upatikanaji wa fedha za mikopo yenye masharti ya
kibiashara unaharakishwa kwa kuzingatia maslahi ya Taifa na kuhakikisha fedha
zitakazopatikana zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.
58. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za Serikali kutaka
kuimarisha ushirikiano kati yake na Washirika wa Maendeleo, na kuhakikisha
fedha zinazoahidiwa zinatolewa kwa wakati, Serikali na Washirika wa Maendeleo
walitafuta Washauri Elekezi Huru. Timu hiyo iliongozwa na Dkt. Donald P.
Kaberuka, aliyekuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. Washauri Elekezi
walipewa kazi ya kutathmini na kutoa mapendekezo ya kuimarisha ushirikiano kati
ya Serikali na Washirika wa Maendeleo na muundo wa utoaji fedha.
59. Mheshimiwa Spika, baadhi ya mapendekezo ya Washauri Elekezi
katika kuimarisha ushirikiano yanajumuisha:
i. Kuanzisha Majadiliano Thabiti: Majadiliano hayo yanalenga kufanya
mapitio na kuimarisha Mchakato wa Mapitio ya Matumizi ya Umma (PER), kupata
matokeo kwenye ngazi ya kisekta pamoja na namna ya kushughulikia masuala nyeti
pasipo kuathiri mchakato wa Bajeti.
ii. Kujenga Uwezo wa Kitaasisi: Lengo ni kujenga ujuzi wa kiwango cha
juu kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo namna ya kufanya majadiliano ya kuvuna
maliasili, masuala ya usimamizi wa fedha, sera za biashara, usimamizi wa deni
la nje na utafiti na uchambuzi wa sera.
iii. Kugharamia Azma ya Serikali Kuleta Maendeleo: Hii itahusisha kutafuta fedha kupitia ubia
kati ya sekta binafsi na sekta ya Umma. Misaada na Mikopo ya Kibajeti (GBS)
bado inaweza kutumiwa katika maeneo mahsusi kama vile kulipia madeni ya
Serikali.
60. Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kufanyia kazi
mapendekezo ya Washauri Elekezi kwa kukamilisha Mwongozo wa Ushirikiano kati ya
Serikali na Washirika wa Maendeleo. Mwongozo huu unaainisha masuala mbalimbali
ikiwemo: Misingi ya ushirikiano; muundo wa majadiliano; na mifumo ya misaada
inayoendana na mahitaji ya nchi. Ni matarajio ya Serikali kwamba, hatua hii
itasaidia kuimarisha ushirikiano na hivyo kuwawezesha Washirika wa Maendeleo
kutimiza ahadi zao kwa kutoa fedha kwa wakati.
Sera za Matumizi
61. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali
itaendelea kuhakikisha kuwa fedha zinaelekezwa kwenye maeneo ya vipaumbele ili
kutekeleza kikamilifu Mpango wa Maendeleo wa Mwaka. Nidhamu ya hali ya juu
katika matumizi lazima isimamiwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha thamani ya
fedha inapatikana. Ili kufikia azma hiyo, Serikali itafanya yafuatayo:
i. Kuendelea
kuhakikisha kuwa Mashirika ya Umma yaliyoundwa kwa lengo la kujiendesha
kibiashara, yanajiendesha kwa faida bila kutegemea ruzuku ya Serikali;
ii. Kuhakikisha
mikataba inayoingiwa na Serikali na Taasisi zake inakuwa katika shilingi za
Kitanzania isipokuwa kwa mikataba inayohusisha biashara na huduma za
kimataifa;
iii. Kuendelea
kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia
zinazopunguza gharama katika matumizi hayo;
iv. Kuendelea
kudhibiti ulipaji wa mishahara kwa kulipa watumishi wanaostahili; na
v. Kutumia
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kufanikisha mawasiliano
katika shughuli za Serikali.
62. Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti ulimbikizaji wa madeni, Serikali itachukua
hatua zifuatazo:
i. Kutokufanya
matumizi pasipokuwa na kasma iliyoidhinishwa kwenye bajeti ya Fungu husika;
ii. Kuhakikisha
kuwa uagizwaji wa bidhaa unafanyika baada ya kutolewa kwa hati ya ununuzi (LPO)
kwenye mfumo rasmi wa malipo (IFMS);
iii. Kuhakikisha
kuwa ahadi (Commitment) inafanyika baada ya kupatikana kwa fedha na kutoingia
mikataba bila kuwa na ridhaa ya matumizi; na
iv. Kuhakikisha
kuwa makubaliano ya kukopa yanafanyika baada ya kupata kibali cha maandishi
kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya
Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 pamoja na marekebisho yake.
Maeneo ya vipaumbele kwa
mwaka 2017/18
63. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka
2017/18 ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka
Mitano, 2016/17 – 2020/21. Kama nilivyoeleza kwenye hotuba ya Hali ya
Uchumi kwa mwaka 2016, maeneo ya kipaumbele yanaakisi Mpango wa Miaka Mitano,
hususan:
i. Kukuza
uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda;
ii. Kufungamanisha
uchumi na maendeleo ya watu;
iii. Kujenga
mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji; na
iv. Kuimarisha
usimamizi wa utekelezaji wa Mpango.
64. Mheshimiwa Spika, Mpango huu umeweka msisitizo katika
kufanikisha utekelezaji wa Miradi Mikubwa ya Kielelezo, ambayo
ni:- Ujenzi wa Reli ya
Kati kwa kiwango chaStandard Gauge; Kuhuisha Shirika la Ndege Tanzania;
Miradi ya Chuma Liganga na Makaa ya Mawe Mchuchuma – Njombe; Uanzishwaji wa
Kanda Maalum za Kiuchumi; Mradi wa Gesi Kimiminika (Liquefied Natural Gas
- LNG); Kituo cha Biashara cha Kurasini; Shamba
la Kilimo na Uzalishaji Sukari Mkulazi; na Kusomesha Vijana wa Kitanzania kwa
wingi kwenye fani na ujuzi maalum kwa ajili ya maendeleo ya watu na viwanda na
kukuza sayansi, teknolojia na ubunifu.
IV. HATUA ZA MAPATO NA MABORESHO YA MFUMO WA KODI,
ADA NA TOZO MBALIMBALI
A. Hatua za Kisera na Kiutawala
65. Mheshimiwa
Spika, Serikali
itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera na kiutawala ili kuimarisha na
kurahisisha ukusanyaji mapato. Hatua hizo ni pamoja na:-
i. Kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa
kutumia vifaa na mifumo ya kielektroniki ili kuzuia uvujaji wa mapato ya
Serikali. Mfumo uitwao “Government e-payment Gateway System” uko tayari
kwa ajili ya matumizi ya Wizara, Idara na Taasisi za Serikali. Wizara, Idara na
Taasisi zote za Serikali zinaagizwa zianze kutumia mfumo huu;
ii. Serikali imezindua mfumo mpya wa ukusanyaji
mapato kwa njia ya kielektroniki (Electronic Revenue Collection System (e-RCS))
ambao utadhibiti udanganyifu unaofanywa na maafisa wa Serikali kwa kushirikiana
na walipa kodi katika kukadiria kodi sahihi. Aidha, mfumo huu utawasaidia
walipa kodi kwa kuwa na uhakika wa kiasi cha kodi wanayopaswa kulipa. Mfumo huo
wa e-RCS utaanza rasmi katika mwaka huu wa fedha kwa usimamizi wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa upande wa
Bara na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRB) kwa upande wa Zanzibar;
iii. Katika mwaka wa fedha 2017/18,
Serikali itaendelea na ukusanyaji wa kodi ya majengo (yaliyothaminiwa na
yasiyothaminiwa) kwenye halmashauri zote nchini. Jukumu hili litasimamiwa na
Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania. Serikali
itatoza Kodi ya Majengo kwa nyumba zote kwa viwango vitakavyopangwa na Waziri na
Fedha na Mipango. Nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini zitatozwa kwa kiwango
maalum (flat rate) cha shilingi elfu kumi (10,000) kwa nyumba na
shilingi elfu hamsini (50,000) kwa nyumba za ghorofa kwa kila ghorofa;
iv. Kuwatambua rasmi wafanyabiashara
wadogo wadogowasio rasmi na wanaofanyia biashara katika maeneo yasiyo
rasmi mfano mama lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza mazao ya kilimo wadogo
kama mboga mboga, ndizi, matunda, na kadhalika kwa kuwapatia
vitambulisho maalum vya kazi wanazozifanya;
v. Kuendelea kusimamia na kuhimiza matumizi
ya mashine za kielektroniki (EFDs) kwenye Wizara, Idara, Taasisi za
Serikali na kwa wafanyabiashara;
vi. Serikali
itafungua akaunti maalum (Escrow Account) kuanzia mwezi Julai 2017 ili
kurahisisha na kuhakikisha kwamba marejesho ya Ushuru wa Forodha wa ziada
(Additional Import Duty) wa asilimia 15 unaolipwa na waagizaji wa sukari ya
viwandani yanafanyika kwa wakati. Hatua hii itaiwezesha Mamlaka ya Mapato
kufanya marejesho kwa wakati kwa wazalishaji wanaotumia sukari hiyo katika
kuzalisha bidhaa mbalimbali; na
vii. Serikali kutoruhusu usafirishaji wa madini
kutoka migodini na kupeleka moja kwa moja nje ya nchi. Aidha, Serikali
itaanzisha maeneo maalum (clearing houses) katika viwanja vya kimataifa,
migodini, na kadhalika ambapo madini hayo yatathibitishwa na kupewa kibali cha
kusafirisha madini hayo ambacho kitatozwa ada ya asilimia moja (clearing fee)
ya thamani ya madini hayo.
B. Maboresho ya Mfumo wa Kodi, Ada na Tozo
Mbalimbali
66. Mheshimiwa
Spika, pamoja
na hatua za kisera na kiutawala za kuboresha ukusanyaji wa mapato, napenda
kuwasilisha mapendekezo ya kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ikiwemo
kurekebisha baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada chini ya sheria mbalimbali.
Aidha, marekebisho haya yanalenga pamoja na mambo mengine, kuongeza mapato ya
Serikali; kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya viwanda,
kilimo, usafirishaji na kukuza ajira. Aidha, kama nilivyoeleza awali,
marekebisho haya hayataathiri kwa kiwango kikubwa utulivu na utabirifu wa mfumo
wa kodi. Marekebisho hayo ni pamoja na Sheria zifuatazo:-
a. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA
148;
c. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
d. Sheria ya Usalama Barabarani, SURA 168;
e. Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, SURA
290;
f. Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya mwaka 2004;
g. Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya
Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali;na
h. Marekebisho ya Ada na Tozo mbalimbali
zinazotozwa naWizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea.
a) Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA
148
67. Mheshimiwa
Spika, napendekeza
kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148 kama
ifuatavyo:-
i. Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye
bidhaa za mtaji (capital goods) ili kupunguza gharama za ununuzi/uagizaji
wa mashine na mitambo ya kuzalishia na hivyo kuvutia uwekezaji katika sekta ya
viwanda. Aidha, hatua hii itahusisha viwanda vya mafuta ya kula, nguo, ngozi,
madawa ya binadamu na mifugo. Lengo la hatua hii ni kuvutia uwekezaji katika
sekta za viwanda, kilimo cha mazao na mifugo, na kukuza ajira na uchumi wa
nchi. Aidha, hatua hii itawezesha viwanda vidogo na vya kati kupata unafuu wa
gharama za kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa mashine na mitambo
watakayonunua kwa ajili ya kusindika na kutengeneza bidhaa mbalimbali. Mitambo
na mashine zote zitakazosamehewa Kodi ya Ongezeko la Thamani zitaainishwa kwa
kutumia HS Codes;
ii. Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango
cha asilimia sifuri katika huduma zinazotolewa kwenye usafirishaji wa
bidhaa/mizigo nje ya nchi (ancillary transport services). Lengo la
hatua hii ni kupunguza gharama za usafirishaji katika bandari zetu
kwa kuifanya Tanzania kuwa njia bora zaidi ya kupitisha bidhaa
zinazotoka nje ya nchi kwenda nchi nyingine hususan zisizo na
bandari (landlocked countries). Hatua hiiitahamasisha wasafirishaji kutoka
nchi jirani kupitisha mizigo yao kwa wingi kwenye bandari zetu na hivyo
kukuza uchumi wa nchi kutokana na kuongezeka kwa mapato ya bandari. Vile
vile kukua kwa sekta ya bandari kutachangia kuongezeka kwa ajira nchini;
iii. Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye
vyakula vya mifugo (compounded animal feeds) vinavyotengenezwa hapa nchini
vinavyotambulika kwenye HS Code 2309. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama
za kununua vyakula hivyo kwa wafugaji; na
iv. Kufanya marekebisho kwenye sehemu ya kwanza ya
jedwali la misamaha ya kodi kipengele cha 3(13) ili kusamehe Kodi ya Ongezeko
la Thamani kwenye mayai ya kutotolesha vifaranga (fertilized eggs for
incubation). Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji wa vifaranga
na kukuza sekta ndogo ya ufugaji ili iweze kuongeza mchango wake katika pato la
Taifa.
Hatua hizi zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake
zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi
milioni 48,034.1.
b) Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
68. Mheshimiwa
Spika, napendekeza
kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kama
ifuatavyo:-
i. Kufanya marekebisho kwenye aya ya nne ya
Jedwali la Kwanza la Sheria ya Kodi ya Mapato ili kurekebisha muda uliotolewa
katika kutoza kodi mbadala (Alternative Minimum Tax) kwa kampuni zinazopata
hasara kwa miaka mitatu mfululizo badala ya miaka mitano mfululizo. Lengo la
hatua hii ni kuoanisha na aya ya nne ya kifungu cha nne cha sheria hiyo
kinachotamka kwamba kodi hiyo inatozwa kwa miaka mitatu mfululizo;
ii. Kufanya marekebisho kwenye Jedwali la Tatu la
Sheria ya Kodi ya Mapato ili kuongeza kiwango cha juu kinachotumika kama
gharama ya kukokotoa uchakavu wa magari yasiyo ya
kibiashara (non-commercial motor vehicles) kutoka shilingi milioni 15
hadi shilingi milioni 30. Lengo la hatua hii ni kufanya/kuhuisha gharama
za magari hayo ziendane na gharama za halisi za soko.Marekebisho haya
yamezingatia kwamba kiwango chasasa cha shilingi milioni 15 ni cha
muda mrefu na hakiakisi bei halisi ya magari kwa sasa katika soko;
iii. Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi
ya Mapato ili kupunguza kiwango
cha Kodi ya Mapato ya Makampuni(Corporate Income
Tax) kutoka asilimia 30 mpakaasilimia 10 kwa miaka mitano kuanzia mwaka mwekezajiatakapoanza uzalishaji,
kwa waunganishaji (assemblers) wa magari,
matrekta na boti za uvuvi. Lengo la
hatua hiini kuongeza ajira, kuongeza mapato ya Serikali na pia
kuhamasisha uhaulishaji wa teknolojia (technology
transfer). Aidha, Serikali itaingia mkataba wamakubaliano na utekelezaji (Performance
Agreement) nakila muunganishaji ambao utaainisha wajibu wa kilaupande; na
iv. Kuanza kutoza Kodi ya Zuio (Withholding Tax)
kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye bei ya kuuzia (total market value) ambayo itakua
ni Kodi ya Zuio ya mwisho (final Withholding Tax) kwa wachimbaji wadogo wadogo
wa madini ya aina zote. Lengo la hatua hii ni kuiwezesha Serikali kupata
mapato stahiki kutoka katika sekta ya madini.
Hatua hizi za Kodi ya Mapato kwa ujumla wake zinatarajiwa
kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni88.5.
c) Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
69. Mheshimiwa
Spika, napendekeza
kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 kama ifuatavyo:
-
i. Kufanya
marekebisho ya viwango maalum vya ushuru (specific duty rates) vinavyotozwa
kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa kiwango cha mfumuko wa bei cha asilimia 5.
Sababu yake ni kuwa pale ambapo Ushuru wa Bidhaa unatozwa kwa viwango maalum
(specific rates) ushuru huo hauakisi mfumuko wa bei na hivyo hupunguza mapato.
Njia bora inayotumika kuondoa mapungufu hayo ni kurekebisha viwango maalum vya
ushuru ili kuendana na kiwango cha mfumuko wa bei. Utaratibu huu ni tofauti na
pale ambapo Ushuru wa Bidhaa hutozwa kwa kiwango cha asilimia ya thamani ya
bidhaa (advalorem rates) ambapo hapana sababu ya kurekebisha viwango vya ushuru
kwa kuwa thamani ya bidhaa inazingatia mfumuko wa bei. Aidha,
marekebisho haya ninayopendekeza ni kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa
Kifungu cha 124(2) inayoelekeza kuwa marekebisho ya viwango vya ushuru yanaweza
kufanyika kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine
vya uchumi jumla. Hata hivyo, kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa kukuza uchumi
wa viwanda, baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini hazitafanyiwa marekebisho
hayo. Mabadiliko ninayopendekeza ni kama ifuatavyo:-
a. Ushuru
wa Bidhaa kwenye vinywaji baridi kutoka shilingi 58 kwa lita hadi shilingi 61
kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 3 kwa lita;
b. Ushuru
wa Bidhaa kwenye maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa yaliyoagizwa kutoka
nje kutoka shilingi 58 kwa lita hadi shilingi 61 kwa lita ikiwa ni ongezeko la
shilingi 3 kwa lita. Aidha, Ushuru wa Bidhaa kwenye maji yanayozalishwa nchini
utabaki kuwa shilingi 58 kwa lita;
c. Ushuru
wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda
yanayozalishwa hapa nchini (local juices) utashuka kutoka shilingi 9.5 kwa lita
na kuwa shilingi 9.0 kwa lita;
d. Ushuru
wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda ambayo
hayazalishwi hapa nchini (imported juices) kutoka shilingi 210 kwa lita hadi
shilingi 221 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 11 kwa lita;
e. Ushuru
wa Bidhaa kwenye bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo
haijaoteshwa (Beer from Local
Unmalted Cereals) kutoka
shilingi 429 kwa lita hadi shilingi 450 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi
21 kwa lita;
f. Ushuru
wa Bidhaa kwenye bia nyingine zote kutoka shilingi 729 kwa lita hadi shilingi
765 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 36 kwa lita;
g. Ushuru
wa Bidhaa kwenye bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu
kutoka shilingi 534 kwa lita hadi shilingi 561 kwa lita ikiwa ni ongezeko la
shilingi 27 kwa lita;
h. Ushuru
wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi
kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, utashuka kutoka shilingi 202 kwa lita na
kuwa shilingi 200 kwa lita;
i. Ushuru
wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa
kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi 2,236 kwa lita hadi shilingi
2,349 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 113 kwa lita;
j. Ushuru
wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyoagizwa kutoka nje kutoka shilingi 3,315
kwa lita hadi shilingi 3,481 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 166 kwa
lita. Aidha,Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyozalishwa nchini
utabaki kuwa shilingi 3, 315 kwa lita;
k. Ushuru
wa Bidhaa kwenye sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku
inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka
shilingi 11,854 hadi shilingi 12,447 kwa kila sigara elfu moja, ikiwa ni
ongezeko la shilingi 593 kwa kila sigara elfu moja;
l. Ushuru
wa Bidhaa kwenye sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku
inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka
shilingi 28,024 hadi shilingi 29,425 kwa kila sigara elfu moja, ikiwa ni
ongezeko la shilingi 1,401 kwa kila sigara elfu moja;
m. Ushuru
wa Bidhaa kwenye sigara zenye sifa tofauti na (k) na (l) kutoka shilingi 50,700
hadi shilingi 53,235 kwa kila sigara elfu moja ikiwa ni ongezeko la shilingi
2,535 kwa kila sigara elfu moja;
n. Ushuru
wa Bidhaa kwenye tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler)
kutoka shilingi 25,608 hadi shilingi 26,888 kwa kilo, ikiwa ni ongezeko la
shilingi 1,280 kwa kilo; na
o. Ushuru
wa Bidhaa wa ‘cigar’ unabaki kuwa asilimia 30.
ii. Kufuta Ada ya Mwaka ya Leseni ya Magari (Annual Motor
Vehicle Licence Fee) iliyokuwa inalipwa hata kwa magari ambayo hayatumiki
ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu, badala yake ada hiyo itatozwa kwa
magari yanayotembea tu, kwa sababu hiyo, Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya
petroli, dizeli na taa utaongezeka kwa kiasi cha shilingi 40 kwa lita moja
kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 339 kwa lita hadi shilingi 379 kwa lita
kwa mafuta ya petroli, kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 215 kwa lita hadi shilingi
255 kwa lita kwa mafuta ya dizeli na kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 425
kwa lita hadi shilingi 465 kwa lita kwa mafuta ya taa. Lengo la hatua hii ni
kuwaondolea wananchi usumbufu wa kudaiwa ada hii hata kwa magari ambayo
hayatumiki.
Hatua za Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa
ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi
milioni 27,801.8.
d) Sheria ya Usalama Barabarani, SURA 168
70. Mheshimiwa
Spika, napendekeza
kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usalama Barabarani, Sura 168 kama
ifuatavyo;
i. Kufuta Ada ya Mwaka ya Leseni ya Magari (Annual Motor
Vehicle Licence Fee) ili ada hii ilipwe mara moja tu gari linaposajiliwa
na baada ya hapo iendelee kulipwa kupitia Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya
petroli na dizeli kwa kuongeza Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya petroli,
dizeli na taa kama ilivyoainishwa katika aya ya 69(ii). Aidha, Serikali inatoa msamaha wa kodi, riba na
adhabu zinazoambatana na madeni yote (Tax Amnesty) ya ada hiyo yaliyolimbikizwa
kwa miaka ya nyuma.
Inapendekezwa pia kuongeza Ada ya Leseni ya Magari wakati wa
usajili mara ya kwanza (Annual Motor Vehicle Licence Fee on first
registration). Ongezeko la Ada ya Leseni ya Magari wakati wa usajili ni kama
ifuatavyo;
a. Gari lenye ujazo wa injini ya 501-1500 cc
kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 150,000 hadi shilingi 200,000, ikiwa ni
ongezeko la shilingi 50,000;
b. Gari lenye ujazo wa injini ya 1501-2500 cc
kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 200,000 hadi shilingi 250,000, ikiwa ni
ongezeko la shilingi 50,000; na
c. Gari lenye ujazo wa injini ya 2501 cc na zaidi
kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 250,000 hadi shilingi 300,000, ikiwa ni
ongezeko la shilingi 50,000.
Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali
kwa kiasi cha shilingi milioni 77,603.5.
e) Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, SURA 290
71. Mheshimiwa
Spika, napendekeza
kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290 ili
kupunguza Ushuru wa Mazao (Produce Cess) unaotozwa na Halmashauri za Wilaya
kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 5 ya thamani ya mauzo (Gross Value) hadi
asilimia 3 kwa mazao ya biashara na asilimia 2 kwa mazao ya chakula. Aidha Mtu
anayesafirisha mazao yake kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine yasiyozidi tani
moja (1) asitozwe Ushuru. Lengo la hatua hii ni kuwawezesha wakulima kulipwa
bei stahiki ya mazao yao na hivyo kuboresha mapato yao. Hatua hii inatarajiwa
kuhamasisha uzalishaji wa mazao.
f) Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Masharikiya mwaka 2004
72. Mheshimiwa
Spika, Mawaziri
wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya kikao cha maandalizi ya
Bajeti tarehe 6 Mei, 2017 mjini Arusha, Tanzania. Kikao hicho kilipendekeza
kufanya marekebisho ya viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha (EAC- Common
External Tarrif “CET”) na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC
Customs Management Act, 2004) kwa mwaka wa Fedha 2017/18. Mapendekezo hayo
yanalenga kwa kiwango kikubwa katika kukuza viwanda ndani ya Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa lengo la kuongeza ajira na kunufaisha watu
wote.
73. Mheshimiwa
Spika, maeneo
yaliyopendekezwa kufanyiwa marekebisho kwenye viwango vya Ushuru wa Pamoja wa
Forodha ni kama ifuatavyo:-
i. Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwa
mwaka mmoja kwenye ngano inayotambuliwa katika HS Code 1001.99.00 na HS Code
1001.99.90. Hatua hii itahusu viwanda vinavyotumia bidhaa hii katika
uzalishaji (duty remission). Aidha, imezingatia kwamba uzalishaji wa bidhaa hii
katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mdogo na hivyo
hautoshelezi mahitaji. Pia inatoa unafuu kwa viwanda na wazalishaji wa bidhaa
na vyakula vinavyotumia ngano na kuimarisha utulivu wa bei wa bidhaa
zinazozalishwa kwa kutumia ngano hiyo;
ii. Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwenye malighafi
inayotumika katika kutengeneza sabuni (LABSA) inayotambuliwa katika HS Code
3402.11.00; HS Code 3402.12.00 na HS Code 3402.19.00 kwa kipindi cha mwaka
mmoja. Hatua hii itahusu viwanda vinavyotumia malighafi hii katika
uzalishaji (duty remission). Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu wa gharama za
uzalishaji kwa viwanda vidogo na vya kati vya kutengeneza sabuni na hivyo
kuweza kuongeza uzalishaji na ajira;
iii. Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 25 kwa
mwaka mmoja kwenye viunganishi vya pikipiki. Hatua hii itahusu viwanda
vinavyotumia viunganishi hivyo katika kuunganisha pikipiki (duty
remission for Motorcycle Assemblers). Lengo la hatua hii ni kuendelea
kuhamasisha uunganishaji wa pikipiki katika Nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki, wakati wataalam wanaanda orodha ya viunganishi ambavyo vitastahili
kupata msamaha wa Ushuru wa Forodha na ambavyo havitastahili. Baada ya
kuainisha orodha ya viunganishi visivyostahili kupata msamaha wa Ushuru wa
Forodha, waunganishaji watahamasishwa kuvitengeneza ndani ya Nchi Wanachama wa
Jumuiya;
iv. Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye mafuta ghafi ya kula
(crude palm oil) yanayotambulika katika Hs Code 1511.10.00 kwa
mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kuhamasisha kilimo cha mbegu
za mafuta hapa nchini na kukuza viwanda vya kutengeneza mafuta ya kula. Aidha,
inazingatia mkakati maalum wa kuendeleza na kulinda viwanda vya kuzalisha
mafuta ya kula yanayotokana na mbegu zinazozalishwa hapa nchini na kutumia
fursa ya soko kubwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tanzania ina nafasi
kubwa ya kuweza kuongeza uzalishaji wa mbegu za mafuta;
v. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au
kiwango maalum cha dola za kimarekani 250 kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa
kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma (Flat rolled Iron
or non alloy Steel) kwa mwaka mmoja zinazotambuliwa katika
HSCodes: 7210.41.00; 7210.49.00; 7210.61.00; 7210.69.00; 7210.70.00;
7210.90.00; 7212.30.00; 7212.40.00; 7212.50.00; na 7212.60.00. Hatua hii
inalinda uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya ndani
dhidi ya ushindani wa bidhaa za aina hiyo zinazoingizwa kutoka nje ya nchi;
vi. Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 200 kwa kila tani
moja ya ujazo (metric ton) kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za
chuma (Steel Rods and Bars and Hot rolled Angles, Sections) zinazotambuliwa
katika HS Codes 7213.10.00; 7213.20.00; 7214.10.00; 7214.20.00; 7214.30.00;
7214.91.00; 7214.99.00; 7216.10.00; 7216.21.00; 7216.22.00; na 7216.50.00.
Hatua hii inatekelezwa ili kulinda uzalishaji wa bidhaa hizo za chuma kutokana
na ushindani unaosababishwa na uingizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Aidha, hatua hii inahamasisha uwekezaji na kuongeza ajira;
vii. Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 badala ya asilimia 25 au dola za
kimarekani 200 kwa tani ya chuma (HS Code 7228.20.00) kutegemea kiwango kipi ni
kikubwa kwa wazalishaji wa springi za magari (leaf spring). Hatua hii itahusu
viwanda vinavyotumia bidhaa hii katika uzalishaji (duty remission).
Kiwango cha asilimia 25 au dola za kimarekani 200 kiliwekwa mwaka 2016/17
kulinda wazalishaji wa bidhaa za vyuma hapa nchini wakati wazalishaji wa
springi za magari walikuwa wanahitaji kutumia bidhaa hizo kama malighafi;
viii. Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola za kimarekani 125 kwa tani moja ya
ujazo kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za chuma (Flat-rolled
products of iron or non alloy steel of a width of 600mm or more, cold rolled or
cold reduced) kwa mwaka mmoja zinazotambuliwa chini ya HS Codes 7209.15.00;
7209.16.00; 7209.17.00; 7209.18.00; 7209.25.00; 7209.26.00; 7209.27.00;
7209.28.00 na 7209.90.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vyetu kutokana
na ushindani wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
ix. Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 kwenye malighafi za kutengeneza
chujio za hewa za magari (air filters). Hatua hii itahusu viwanda vyote
vinavyotumia bidhaa hii katika uzalishaji wa chujio hizo (duty remission)
katika Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo la hatua hii ni
kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa hiyo na kukuza ajira;
x. Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye Gypsum
Powder inayotambuliwa chini ya HS Code 2520.20.00 kwa mwaka mmoja.
Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo hapa nchini na
kuhamasisha wawekezaji watumiegypsum inayopatikana hapa nchini
katika kuzalishagypsum powder na kwa kufanya hivyo tutaongeza ajira
na mapato;
xi. Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya kuongeza kiwango
hicho hatua kwa hatua hadi kufikia asilimia 25 mwaka 2018/19 kwenye sukari
inayotumika viwandani. Hatua hii itahusu viwanda vyote vinavyotumia sukari hiyo
katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali (duty remission). Hatua ya kutoongeza
Ushuru wa Forodha imezingatia kuwa sukari inayotumika viwandani ni malighafi ya
maana katika kuzalisha chakula, vinywaji na madawa ambavyo ni muhimu kwa
mahitaji ya binadamu;
xii. Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwenye mashine za kielektroniki
za kukusanya mapato ya hazina (Electronic Fiscal Devices) zinazotambuliwa chini
ya HS Code 8470.50.90 kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha
wafanyabiashara na walipa kodi kutumia mashine hizo katika kufanya mauzo na
kuongeza ufanisi katika usimamizi na udhibiti wa kodi;
xiii. Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwenye bidhaa za
karatasi zinazotambulika chini ya HS Codes 4804.11.00; 4804.19.90;
4804.21.00; 4804.29.00; 4804.31.00; 4804.29.00; 4804.41.00; 4804.51.00;
4804.59.00; 4805.11.00; 4805.12.00; 4805.19.00; 4805.24.00; 4905.25.00;
4805.30.00; 4805.91.00 na 4805.92.00. Hatua hii imeendelea kutekelezwa ili
kuvilinda viwanda vya ndani vinavyozalisha karatasi hizo kutokana na ushindani
wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi;
xiv. Kutoza
Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwenye
malighafi na vifaa vinavyoagizwa nje ya nchi kwa ajili ya kuunganisha na
kutengeneza vifaa (inputs for assembling of equipments) ambavyo ni mahsusi kwa
ajili ya matumizi ya walemavu. Aidha, hatua hii itahusu waunganishaji wa vifaa
hivyo tu (duty remission). Hivyo waunganishaji (assemblers) wa vifaa hivyo
watanufaika na punguzo la ushuru huo. Aidha, lengo la kuchukua hatua hii ni
kuhamasisha uwekezaji katika kuzalisha vifaa hivyo muhimu ndani ya Nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki na kukuza ajira;
xv. Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 0 kwenye muundo wa
aluminiamu (aluminium structure) inayotambuliwa kwenye HS Code 7610.90.00 kwa
mwaka mmoja. Hatua ya kuweka kiwango hiki cha Ushuru inalenga katika
kutofautisha vifaa vyenye kufanana lakini vina ubora tofauti (steel and
aluminium) hali ambayo inasababisha ukwepaji kodi;
xvi. Kufanya
marekebisho katika uandishi wa HS Code 4911.99.20 ili kujumuisha karatasi
zinazotumika kwenye Shule katika kujibu maswali (examination answer sheet) ili
nazo ziweze kutozwa Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 kama vile karatasi za
maswali (question papers) zinavyotozwa. Hatua hii itapunguza gharama za kutoa
elimu nchini; na
xvii. Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 kwenye vifaa vinavyotumika katika ujenzi na
uunganishaji wa meli (inputs for use in the manufacture/assembling of ships).
Hatua hii itawahusu wajenzi na waunganishaji wa meli (duty remission). Lengo ni
kutoa unafuu wa gharama katika kutengeneza meli au kuunganisha. Aidha hatua hii
itahamasisha uvuvi, kuimarisha usafiri wa majini na kuongeza ajira.
74. Mheshimiwa
Spika, Mawaziri
wa Fedha wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya pia
marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-
Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo:-
i. Kufanya
marekebisho katika kifungu B cha Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufuta aya ya 25 ili kuondoa msamaha wa Ushuru
wa Forodha kwenye taa zinazojulikana kama Compact Fluorescent Bulbs (CFL) na
Light Emitting Bulbs (LEI). Hatua hii imezingatia kwamba msamaha huo hauna tija
hivi sasa kwa kuwa bidhaa hizo ni zile ambazo zimetengenezwa kwa kiwango
kilicho kamilika kwa matumizi (finished goods) na hivyo zinastahili kutozwa
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25;
ii. Kufanya
marekebisho katika sehemu ya 203 ya Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuongeza adhabu (fine) kutoka dola za kimarekani
10,000 hadi dola za kimarekani 20,000 au asilimia 50 ya kodi iliyostahili
kulipwa kutegemea kiwango kipi ni kikubwa. Lengo ni kuweka adhabu kali kwa
makosa (offences) yanayofanywa na waagizaji mizigo kama vile kuwasilisha
nyaraka zisizo sahihi, taarifa zisizo sahihi, kukwepa kodi kwa njia ya
kughushi, na kadhalika. Hatua hii imezingatia adhabu ya juu inayotozwa hivi
sasa ni dola za kimarekani 10,000 ambazo ni ndogo na haziwezi kupunguza makosa
ya namna hiyo;
iii. Kufanya
marekebisho katika kifungu cha 218 cha Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ili kumpa mamlaka Kamishna wa Forodha kumrejeshea mlipa kodi bidhaa
ambazo zilikuwa zimezuiliwa badala ya utaratibu wa sasa unaotoa mamlaka hayo
kwa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
iv. Kufanya
marekebisho katika aya ya 30 ya Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki ili kuongeza “usambazaji wa mafuta na gesi” katika misamaha
inayotolewa kwenye miradi ya gesi na mafuta. Hatua hii ina lengo la kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye miradi ya mabomba ya mafuta inayotekelezwa
na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hatua hizi za Ushuru
wa Forodha kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi chashilingi
milioni 16,053.9.
g) Marekebisho madogo madogo katika baadhi
ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali
75. Mheshimiwa
Spika, napendekeza
kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika sheria
mbalimbali za kodi pamoja na sheria nyingine mbalimbali ili ziwe sanjari na
azma ya kurahisisha utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika
Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 na Matangazo ya Serikali (Government
Notices).
h) Marekebisho ya Ada na Tozo mbalimbali
zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea
76. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbalimbali zinazotozwa na
Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi
ya ukuaji wa uchumi. Aidha, marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa
Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).
Marekebisho hayo yatajumuisha:-
i. Kufuta ada ya ukaguzi wa viwango, ada ya
ukaguzi wa mionzi na ada ya wakala wa vipimo kwenye mbolea inayotozwa na
Shirika la Viwango Tanzania, Tume ya Mionzi Tanzania na Wakala wa Vipimo
Tanzania. Lengo la hatua hii ni kuwapunguzia wakulima gharama za pembejeo na
hivyo kuongeza tija katika uzalishaji;
ii. Kufuta ada ya ukaguzi wa viwango kwa mazao ya
biashara kama pamba, chai, korosho na kahawa inayotozwa na Shirika la Viwango
Tanzania. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji kwa viwanda
vinavyosindika mazao haya na pia kuongeza mapato kwa wakulima;
iii. Kufuta Ushuru wa Huduma (Service Levy) kwenye
nyumba za kulala wageni ambazo zinatozwa Guest House Levy;
iv. Kufuta Ushuru wa Mabango kwa mabango
yanayoelekeza mahali huduma za jamii (Shule na Hospitali au Zahanati) zinapopatikana.
Aidha, kuanzia tarehe 1 Julai, 2017 Mamlaka ya Mapato Tanzania itaanza
kukusanya Ushuru wa Mabango ya Matangazo kwa nchi nzima;
v. Kufuta ada ya vibali vinavyotolewa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa mfano vibali vya machinjio (isipokuwa ada ya machinjio na
ada ya ukaguzi wa nyama), ada ya vibali vya kusafirisha mifugo na ada ya vibali
vya kuanzisha maduka ya dawa;
vi. Kufuta ada ya makanyagio minadani; na
vii. Kufanya marekebisho ya kiwango cha faini kwa
makosa ya watakaoenda kinyume na masharti ya Sheria ya Fedha za Serikali za
Mitaa kutoka kiasi kisichozidi shilingi 50,000 na kifungo kisichozidi miezi 12
hadi kiasi kisichopungua shilingi 200,000 na kisichozidi shilingi 1,000,000 au
kifungo kisichopungua miezi 12 na kisichozidi miaka miwili.
77. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kufanya uchambuzi na
tathmini ya tozo na ada zinazotozwa na mashirika, taasisi na wakala mbalimbali
ili kuendelea kuweka mazingira bora ya kufanya biashara/kuwekeza na kuondoa
kero kwa wananchi. Hii itajumuisha kupitia upya na kuvisawazisha viwango vya
tozo na ada hizo na pia kuondoa tozo na ada za usumbufu.
i) Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi
78. Mheshimiwa Spika, hatua
hizi za kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2017,
isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.
V. SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2017/18
79. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha na sera za bajeti
kwa mwaka 2017/18, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya shilingi
bilioni 31,712.0 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika
kipindi hicho. Jumla ya mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri
yanatarajiwa kuwa shilingi bilioni 19,977.0, sawa na asilimia 63.0 ya bajeti
yote. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla
ya shilingi bilioni 17,106.3 sawa na asilimia 85.6 ya mapato ya ndani. Aidha,
mapato yasiyo ya kodi ni shilingi bilioni 2,183.4 na mapato kutoka vyanzo vya
Halmashauri ni shilingi bilioni 687.3.
80. Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa
kuchangia shilingi bilioni 3,971.1 ambayo ni asilimia 12.5 ya bajeti yote.
Misaada na mikopo hii inajumuisha miradi ya maendeleo shilingi bilioni 2,473.8;
mifuko ya pamoja ya kisekta shilingi bilioni 556.1; na misaada ya kibajeti (GBS)
shilingi bilioni 941.2.
81. Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kukopa shilingi
bilioni 7,763.9 kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara. Mikopo
ya ndani inatarajiwa kuwa shilingi bilioni 6,168.9, ambapo shilingi bilioni
4,948.2 ni kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zinazoiva (rollover) na
shilingi bilioni 1,220.7 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni mikopo mipya
kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Ili kuongeza kasi katika ujenzi wa
miundombinu, Serikali inatarajia kukopa shilingi bilioni 1,595.0 kutoka soko la
nje.
82. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali itaongeza
jitihada za ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na mikopo ya ndani na nje ili
kutekeleza miradi ya maendeleo. Miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo awamu
zinazofuata za ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, na
uboreshaji wa bandari mbalimbali nchini, vitatekelezwa kulingana na mpangokazi
kutegemea mwenendo wa mapato ya ndani na nje utakaojidhihirisha baada ya
kufanya mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha Julai hadi Desemba
2017. Aidha, mara baada ya ridhaa ya Serikali kupatikana, utaratibu wa kutoa
hatifungani maalum (special non-cash bond) utatekelezwa ili kusaidia kupunguza
madeni yaliyohakikiwa ya Serikali kwa mifuko ya hifadhi ya jamii.
83. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali inapanga
kutumia jumla ya shilingi bilioni 31,712.0. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 19,712.4 zimetengwa kwa
ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha shilingi bilioni 7,205.8 za mishahara
na shilingi bilioni 9,461.4 kwa ajili ya kulipia deni la umma na huduma
nyinginezo. Aidha, matumizi ya maendeleo yatakuwa shilingi bilioni 11,999.6
sawa na asilimia 38 ya bajeti yote, ambapo shilingi bilioni 8,969.7 ni fedha za
ndani na shilingi bilioni 3,029.8 ni fedha za nje. Kiwango hiki kimezingatia
wigo wa asilimia 30 hadi asilimia 40 ya bajeti yote iliyoidhinishwa katika
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/17 – 2020/21.
84. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama
nilivyoeleza, sura ya bajeti kwa mwaka 2017/18 ni kama inavyooneshwa
katika Jedwali A.
Jedwali A: Mfumo wa Bajeti ya Mwaka 2017/18
Shilingi Milioni
|
||
Mapato
|
2017/18
|
|
A.
|
Mapato ya
Ndani-Serikali Kuu
|
19,289,695
|
(i) Mapato ya Kodi
(TRA)
|
17,106,336
|
|
(ii) Mapato yasiyo
ya kodi
|
2,183,359
|
|
B.
|
Mapato ya
Halmashauri
|
687,306
|
C.
|
Mapato na Mikopo
nafuu kutoka nje
|
3,971,103
|
(i) Misaada na
Mikopo nafuu -GBS
|
941,258
|
|
(ii)Misaada na
Mikopo nafuu ya Miradi
|
2,473,770
|
|
(iii)Misaada na
Mikopo nafuu ya Kisekta
|
556,075
|
|
D.
|
Mikopo ya Ndani na
Nje yenye Masharti ya Kibiashara
|
7,763,882
|
(i) Mikopo ya Nje
|
1,594,985
|
|
(ii) Mikopo ya Ndani
|
1,220,668
|
|
(iii)Mikopo ya
Ndani- Rollover
|
4,948,229
|
|
JUMLA YA MAPATO YOTE
(A+B+C+D)
|
31,711,986
|
|
Matumizi
|
||
E.
|
Matumizi ya Kawaida
|
19,712,394
|
o/w (i) Deni la
Taifa
|
9,461,433
|
|
-Malipo ya Riba Ndani
|
1,025,546
|
|
-Malipo ya Mtaji Ndani (Rollover)
|
4,948,229
|
|
-Malipo ya Mtaji Nje
|
1,182,651
|
|
- Malipo ya Riba Nje
|
673,492
|
|
- Michango ya Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi za Jamii
|
1,195,882
|
|
-Matumizi Mengine ya Mfuko Mkuu
|
435,633
|
|
(ii) Mishahara
|
7,205,768
|
|
(iii)Matumizi Mengineyo (OC)
|
3,045,193
|
|
- Matumizi yanayolindwa (protected
expenditure)
|
1,985,245
|
|
- Matumizi ya Halmashauri
|
274,922
|
|
-
Matumizi Mengine ya kuendesha ofisi
|
785,025
|
|
F.
|
Matumizi ya
Maendeleo
|
11,999,592
|
(i) Fedha za Ndani
|
8,969,747
|
|
o/w Matumizi ya Halmashauri
|
412,384
|
|
(ii)Fedha za Nje
|
3,029,845
|
|
JUMLA YA MATUMIZI
YOTE (E+F)
|
31,711,986
|
|
NAKISI YA BAJETI
(ASILIMIA YA PATO LA TAIFA)
|
3.8%
|
VI. HITIMISHO
85. Mheshimiwa Spika, hatua zilizopendekezwa kwenye bajeti hii
zinalenga kujenga msingi madhubuti wa uchumi wa viwanda na kupanua fursa za
ajira na biashara. Dhamira yetu sote ni kufikia kiwango cha uchumi wa kipato
cha kati ifikapo 2025. Ili kushiriki katika mafanikio hayo, ni lazima kila
mmoja wetu ashiriki katika shughuli halali ya uzalishaji na afanye hivyo kwa
juhudi na maarifa ili kuleta tija.
86. Mheshimiwa Spika, kufanikiwa kwa Bajeti hii kunahitaji
nidhamu ya hali ya juu katika usimamizi wa mapato na matumizi. Ili kufikia azma
hii, juhudi za pamoja kati ya Serikali na wadau wote zinahitajika ikiwa ni
pamoja na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi kwa kuwekeza
zaidi katika maeneo ya kipaumbele. Natoa rai kwa kila Mtanzania kutimiza wajibu
wake ili Bajeti hii iweze kutekelezwa kama ilivyopangwa.
87. Mheshimiwa Spika, mojawapo ya masharti ambayo nchi yetu
haina budi kuyatimiza ili Tanzania ifanikiwe kufanya mapinduzi ya kiuchumi na
kijamii kwa haraka, ni pamoja na kuwa na viongozi wenye sifa za kuleta na
kusimamia mabadiliko. Sifa za viongozi wa aina hiyo ni zifuatazo:
i. Wanafanya
jitihada kuwa binadamu wema, wanaojali na kusaidia watu wengine hasa wanyonge,
wenye maadili mema, waaminifu na kutenga muda wao kutafakari juu ya utumishi
wao kwa umma;
ii. Wanakuwa
na dira kuhusu wapi pa kuipeleka nchi kutoka ilipo sasa na kujiwekea malengo
makubwa;
iii. Wanaweka
viashiria vya mafanikio kwa kila programu na mradi utakaotekelezwa;
iv. Wanasimamia
kidete muda wa utekelezaji;
v. Wanatoa
maamuzi magumu na maelekezo thabiti kwa kutambua kuwa hakuna mchezo usio na
maumivu sambamba na kuandaa na kuwawezesha viongozi watakaopokea kijiti; na
vi. Wanateua
kwa umakini na kufanya kazi pamoja na timu hiyo madhubuti ya ushindi.
88. Mheshimiwa Spika, mimi naamini, na Bunge lako Tukufu na
Watanzania walio wengi watakubaliana nami kuwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anazo sifa zote hizi.
Ni kiongozi mzalendo, anayependa na kujivunia nchi yake ya Tanzania; ni
kiongozi ambaye amejielekeza kuijenga Tanzania mpya; ana moyo thabiti, nia
njema na kujifunga kuwatumikia Watanzania wote na hasa wanyonge; ana msimamo
thabiti usioyumba; anayo dhamira ya dhati ya kusimamia utendaji uliotukuka;
anachukia rushwa, ubadhirifu, ufisadi na wizi wa rasilimali za umma; ana
uthubutu wa kufanya mambo mapya tofauti, yenye maslahi kwa Taifa kinyume na
mazoea, hata kama hayawapendezi baadhi ya watu.
89. Mheshimiwa Spika, sasa Watanzania wote tumeanza kuona matokeo.
Ndani ya kipindi kifupi cha miezi 18 ya uongozi wake, Mheshimiwa Rais amefanya
mambo mengi makubwa sana! Mengi yamefufua matumaini na ari ya wananchi walio
wengi lakini kwa wachache yamekuwa machungu. Naomba niyarejee baadhi kama
ifuatavyo: Kutengua uteuzi wa viongozi mbalimbali ambao aliona hawaendi
na dhamira na kasi yake; Kukamata makontena yaliyoondolewa bandarini bila
kulipa kodi stahiki; Kuondoa Serikalini watumishi wasio na sifa/vyeti halali na
wanafunzi hewa; Kuimarisha matumizi ya fedha za umma; Kudhibiti mishahara na
madai hewa; Kuerejesha nidhamu kwa Wizara, Idara na taasisi za Serikali kulipa
madeni ya umeme, maji na huduma nyingine; Kugharamia elimu msingi bila malipo;
Kuongeza ukusanyaji wa kodi kutoka wastani wa shilingi bilioni 800 kwa mwezi hadi
wastani wa shilingi trilioni 1.2; kuthubutu kutekeleza uamuzi wa muda mrefu wa
kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma; Kumtaka kila Mtanzania afanye kazi;
Kuanza utekelezaji wa kujenga Standard Gauge Railway (SGR);
Kununua ndege mbili mpya na kufanya malipo ya awali kwa ndege nyingine nne ili
kufufua shirika la ndege na kuinua utalii; Kushawishi Serikali ya Uganda
kuridhia mradi mkubwa wa bomba la mafuta lijengwe kutoka Hoima - Uganda hadi
bandari ya Tanga katika mazingira ya ushindani mkali; Kuendelea na ujenzi na
ukarabati wa barabara mbalimbali nchini ikiwemo flyover pale
TAZARA, interchangeUbungo; na ujenzi wa miradi ya miundombinu ya
umeme, maji, na meli mpya mbili katika Ziwa Nyasa. Aidha, katika uongozi
wake agenda ya kujenga uchumi wa viwanda imepata mwitikio mkubwa wa sekta
binafsi nchini na hususan ukanda wa Pwani.
90. Mheshimiwa Spika, ninafurahi kuwaambia Watanzania wenzangu
kuwa hatua hizo ni uwekezaji wa lazima na wa busara (sensible investment).
Bajeti hii ya 2017/18 itaendelea kuimarisha matokeo haya na kuchukua hatua
zaidi ili tuende mbele. Ukiona vinaelea, ujue vimeundwa! Rai yangu kwa
Watanzania wenzangu, na hasa sisi viongozi na wananchi wote ni lazima tujitoe
kuijenga Tanzania, tumuunge mkono Rais wetu kwa vitendo kwa kila mtu kufanya
kazi kweli kweli tukijielekeza kutekeleza Dira na malengo ya Serikali ya awamu
ya tano ya kujenga ustawi wa uchumi imara unaotengeneza ajira, fursa mpya na
mgawanyo wa haki na usawa wa rasilimali za Tanzania kwa wananchi wote. Tulinde
umoja na amani yetu kama mboni ya jicho na tena, letu liwe moja katika masuala
yote yenye maslahi kwa taifa letu. Naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya
Serikali kuwashukuru na kuwapongeza kwa dhati kabisa wananchi wote ambao
wanalipa kodi stahiki ambao ndiyo wamefanikisha maendeleo hayo niliyoyataja.
Serikali inawaahidi kutumia vizuri mapato yatokanayo na kodi zenu kuwaletea
maendeleo. Wale mnaojaribu kukwepa kodi, mkono wa sheria utachukua mkondo wake.
91. Mheshimiwa Spika, ninapokaribia kumaliza hotuba hii,
naomba kuwatambua na kuwashukuru Washirika wetu wa Maendeleo wanaotarajia
kuchangia Bajeti ya Serikali jumla ya shilingi bilioni 3,971.1 kwa mwaka
2017/18 kama ifuatavyo, (kiasi walichoahidi kuchangia katika bajeti ya
2017/18 kikiwa katika mabano):Benki ya Maendeleo ya Afrika (shilingi bilioni
410.9); Abu Dhabi/OPEC (shilingi bilioni 20); AFD/French (Shilingi bilioni
27.3); Badea (shilingi bilioni 10); Ubelgiji (shilingi bilioni 13.7); Denmark
(shilingi bilioni 47); DFID (Shilingi bilioni 364.4); Jumuiya ya Ulaya
(shilingi bilioni 150.3); Finland (shilingi bilioni 25.7); Ujerumani (shilingi
bilioni 58.4); Global Fund (shilingi bilioni 431.2); IFAD (shilingi bilioni
45.3); India (shilingi bilioni 80); Ireland (shilingi bilioni 18.3); JICA/Japan
(shilingi bilioni 57.4); Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (shilingi bilioni 20);
Norway (shilingi bilioni 22.3); OPEC Fund (shilingi bilioni 8.5); Poland
(shilingi bilioni 61.1); Sweden (shilingi bilioni 172.5); Korea ya Kusini
(shilingi bilioni 20); Uswisi (shilingi bilioni 12.1); UNICEF (shilingi bilioni
27.2); USAID (shilingi bilioni 3.4); na Benki ya Dunia (shilingi bilioni
1,862.3). Fedha zilizoingizwa kwenye Bajeti hii zinazingatia historia ya utoaji
wa fedha za kugharamia miradi kutoka kwa Washirika wetu wa Maendeleo.
92. Mheshimiwa Spika, napenda pia kutambua uhusiano mzuri tulionao
na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) chini ya Mpango wa Ushauri wa Kisera
(Policy Support Instrument - PSI). Ni matumaini yetu kuwa Bodi ya Shirika la
Fedha Duniani itakubali kuendeleza awamu nyingine ya mpango wa PSI baada ya
mwezi Desemba 2017. Rai yangu kwa marafiki wote wa nchi yetu ni kuwa: Endeleeni
kuiunga mkono Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hususan
katika azma yake ya kujenga uchumi wa viwanda. Watanzania wamesikia kiasi cha
fedha mlizoahidi na nawaomba mtimize ahadi zenu kwa wakati nasi tunawaahidi
kutumia michango yenu adhimu kwa ufanisi na uwazi.
93. Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, naomba nihitimishe kwa
kumshukuru kwa namna ya pekee kabisa, mke wangu na rafiki yangu mpenzi, mama
Mbonimpaye Mpango pamoja na watoto na wajukuu wetu wote kwa kunitunza na
kuniombea kwa Mungu kila siku ili niweze kutekeleza vema dhamana niliyopewa ya
kuwatumikia Watanzania. Aidha, kwa heshima kubwa, ninawashukuru sana ndugu
zangu, wana wa Wilaya ya Buhigwe na wananchi wa mkoa wa Kigoma kwa ujumla kwa
upendo na kunitakia heri ili niendelee kutekeleza wajibu wangu ipasavyo.
Mlinilea na kunifundisha kupenda kufanya kazi. Nami nawaahidi kuwa nitakuwa
mwaminifu, sitawaangusha! Asanteni sana Waheshimiwa Wabunge, viongozi na
wananchi wote kwa kunisikiliza.
MUNGU IBARIKI
TANZANIA!
94. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.