Tuesday, March 13

Viongozi na wafuasi 20 Chadema washikiliwa na polisi


Mwanza. Takribani watu 20 wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema akiwemo diwani wa Kata ya Mabatini, Deo Mbibo wanashikiliwa na polisi baada ya kukamatwa walipokuwa wameenda kuhani msiba wa mwanachama mwenzao.
Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Leonard Nundi amesema tukio hilo limetokea leo Machi 13, saa kumi jioni ambapo wafuasi hao wakiwa zaidi ya 500 walienda kuhani msiba huo na ghafla polisi waliwavamia na kumtaka mfiwa kuongea naye.
“Chanzo cha vurugu ni baada ya askari hao kuvamia msibani na kumhitaji mfiwa ambaye ni Laurent Chiro kwa ajili ya mazungumzo, waliposhindwa kuelewana walimchukua diwani na viongozi wengine waliokuwa meza kuu na kuwapandisha kwenye gari la polisi,” amesema Nundi.
Amesema wanachama waliokuwa msibani waliogomea kitendo hicho na kuanza kuwarushia mawe polisi ambao nao walianza kujihami kwa kupiga mabomu ili kuwatawanya.
Akizungumzia tukio hilo, kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi pamoja na kudai yuko wilayani Kwimba, lakini amesema wafuasi hao wamekuwa na kawaida kukusanyika na kufanya vikao vyao vya kisiri.
Mmoja wa wanachama aliyekuwa eneo la tukio, Emmanuel Tumbo amesema wafuasi hao wametoka katika kata zote 18 za Jiji la Mwanza ambao wamejiwekea utaratibu wa kuhani misiba inapotokea kwa mwanachama anayefiwa au kufariki dunia.

Simulizi ya mtoto aliyezuia baba yake kuuza shamba

Mkazi wa Kijiji cha Ngundusi, Ngara, mkoani
Mkazi wa Kijiji cha Ngundusi, Ngara, mkoani Kagera, Petro Magogwa akiwa na watoto wake Anthony (kushoto) na Eliza nyumbani kwake kijijini hapo. Picha na Shaaban Ndyamukama. 
Ngara. Mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Ngundusi wilayani Ngara amemzuia baba yake kuuza shamba la familia.
Anthony Petro (10) amezuia kuuzwa shamba hilo akidai kuona baba yake akisaini barua ya mauzo na hivyo kutoa taarifa polisi.
Akizungumza na mwandishi wetu juzi katika kituo kidogo cha polisi Kabanga, Anthony alisema alizuia shamba hilo lisiuzwe ili yeye na ndugu zake wawili wa kike wasikose sehemu ya kuishi.
Alisema wanaishi maisha ya dhiki wakimtegemea baba yao anayejishughulisha na kilimo na kuokota chupa za plastiki mtaani ili kupata chakula.
“Alitaka kuuza shamba ili sisi tukaishi wapi na tukalime wapi au tutatunzwa na nini? Niliamua kwenda polisi,” alisema mtoto huyo ambaye alisema ili kumsaidia mzazi wake huyo amekuwa akienda kutafuta misaada anapotoka shuleni.
Alisema amekuwa akienda kuomba msaada mji wa Kobero ulioko nchini Burundi umbali wa takriban kilomita nane kutoka wanapoishi na hufika huko kwa kuomba lifti kwenye magari.
Familia ya mtoto huyo iko eneo lililojitenga na makazi ya watu katika shamba lenye miti ya parachichi wakiishi kwenye nyumba chakavu iliyojengwa kwa miti na udongo.
Mkuu wa kituo kidogo cha polisi Kabanga, Bernard Masakia alithibitisha mtoto huyo kutoa taarifa kuzuia baba yake kuuza shamba.
Kutokana na uthubutu wake huo, Masakia kwa kushirikiana na askari wa polisi jamii waliamua kumsaidia baba wa mtoto huyo Sh35,000 kwa ajili ya kununua chakula na mahitaji mengine.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Mukitama, Kijiji cha Ngundusi, Joel Mwasi alisema Petro Magogwa (67) ambaye ni baba wa Anthony alitaka kuuza shamba kutokana na maisha kuwa magumu baada ya kufiwa na wake zake wawili .
Mwasi alisema tayari alishauza sehemu ya shamba hilo na kwamba mama wa mtoto huyo alifariki kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba.
Alisema familia hiyo inaishi mwisho wa kijiji ikipakana na kingine cha Kobero mkoani Muyinga nchini Burundi.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ngundusi, Josia Cleophace alisema Anthony hafanyi vizuri kitaaluma kutokana na mahudhurio yake darasani kuwa ya wastani.
Alisema mwanafunzi huyo amekuwa akienda kwenye vibanda vya wafanyabiashara kuomba misaada ili kupata chakula cha familia.
Wakazi wa Ngundusi, Medard Bilula, Edward Shungu na Generoza Chechelo kwa nyakati tofauti walisema mzazi wa mwanafunzi huyo anaishi kwa shida na watoto wanakosa mapenzi na malezi ya mama baada kufariki wakiwa wadogo.
Michael Nazali ambaye alinunua sehemu ya shamba alisema baba wa mtoto huyo alikuwa akihitaji fedha za matibabu na mahitaji mengineyo ya watoto hao ndipo alipomuuzia eneo mwaka 2000.
Alisema katika siku za hivi karibuni, amekuwa akimpatia msaada mzee huyo kutokana na sadaka zinazokusanywa na waumini kwa watu wasiojiweza na hakuwa na makubaliano ya kununua shamba kama inavyodaiwa na mtoto Anthony.
Mbali ya Anthony, watoto wengine wa Magogwa ni Eliza (9) na Editha (13) ambao wanasoma darasa la pili.
Magogwa alisema alioa jumla ya wake wanne na kuzaa watoto kadhaa huku wengine wakipoteza maisha kwa nyakati tofauti.
Alisema maisha yake yamekuwa duni baada ya kufiwa na wake zake wawili na wengine wawili waliachika na kati yao watatu walikuwa ni kutoka Burundi. Alisema wake wawili walio hai waliondoka na watoto watano.
Alisema wanawe watatu wa kike wameolewa lakini hawana uwezo kiuchumi hivyo anapougua au kuuguza msaada wake ni kukata sehemu ya shamba na kuuza.
“Nikiuza chupa 24 tupu za soda kwa wanaotengeneza pombe wananipatia Sh500 wakati mwingine napata Sh2,000 nanunua unga ili wanangu wasilale njaa,” alisema huku akibubujikwa machozi.
Alisema mara ya mwisho aliuza ardhi kwa Sh120,000 miaka mitatu iliyopita baada ya kuugua muda mrefu pamoja na wanawe.
Magogwa alisema, mkewe wa kwanza walizaa watoto wanane lakini watano wote wa kiume walifariki na kubaki watatu wa kike walioolewa.
Mke wa pili ambaye ni Mtanzania walizaa watoto wanane pia lakini kati yao, saba walifariki na aliyebaki ni msichana anayeishi wilayani Kahama.
Alisema mke wa watatu, raia wa Burundi walizaa watoto watano na wawili wa kiume walifariki na kubaki watatu wa kike ambao baada ya mama yao kufariki dunia, walichukuliwa na mama zao wadogo na wajomba ambao wanaishi Burundi.
Alisema mke wa nne walizaa naye watoto wanne, wawili wa kiume na wawili wa kike. Alisema mama huyo alifariki kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba huku mwanaye mwingine wa kiume akifariki dunia baada ya miezi minane na kubakiwa na watatu akiwamo Anthony.
Alisema eneo la ardhi alilobakiwa nalo lenye miti ya parachichi na mikaratusi ameligawa kwa wanawe chini ya uongozi wa kitongoji ili hata akifa asiwepo wa kuwanyanyasa.

Polisi: Mwanafunzi aliyetoweka ‘alijiteka’


Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na polisi mkoani Iringa limebaini na kujiridhisha kuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo hakutekwa, bali ‘alijiteka’ mwenyewe
Akizungumza leo Jumanne Machi 13, 2018 kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema polisi watachukua hatua za kisheria  kwa kuwa mwanafunzi huyo amewadanganya watu kuwa ametekwa na kusababisha taharuki kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Mambosasa amesema polisi wamefanya uchunguzi na kubaini mwanafunzi huyo hakutekwa bali ‘alijiteka’ mwenyewe ili kutafuta umaarufu wa kisiasa na kusababisha kuzua tafrani kwa jamii.
Amesema Machi 6, 2018 saa sita usiku zilisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Nondo ametekwa na watu wasiojulikana.
Amebainisha kuwa polisi wa kdana hiyo walianza kufuatilia ili kubaini ukweli wa tukio hilo ikiwa pamoja na kufunguliwa jalada la uchunguzi lenye kumbukumbu namba DSM/KIN/CID/P.E/51/2018.
Mambosasa amesema Machi 7, 2018 walipewa taarifa na polisi mkoani Iringa kuwa mwanafunzi huyo ameonekana Wilaya ya Mafinga akiwa na afya njema na mwenye kujitambua akiendelea na shughuli zake.
“Mwanafunzi huyu alionekana Mafinga akiendelea na shughuli zake na wala hakuripoti tukio la kutekwa katika kituo chochote cha polisi hivyo tunaendelea kumshilikia hivyo taratibu ili tumpeleke mahakamani,”amesema Mambosasa.
Amesema upelelezi umebaini mwanafunzi huyo alikwenda kwa mpenzi wake ambaye alikuwa akifanya naye mawasiliano mara kwa mara akiwa njiani kuelekea Iringa.
Mambosasa amesema kuwa pia alivyopimwa alionekana mwenye afya njema, hakupewa dawa yoyote ya kumlevya na hakuwa na majeraha.

Kipi kiwango cha uungwaji mkono wa Magufuli Tanzania kukiwa na uvumi wa maandamano

Serikali ya Tanzania imetoa kauli za kuyazuia maandamano yanayohamasishwa kupitia mitandao ya kijamii yaliyopangwa kufanyika Aprili 26 kufuatia kuwepo na ukosoaji mkubwa wa utawala wa rais John Pombe Magufuli. DW imezungumza na Dr. Onesmo Kyauke wakili wa kujitegemea Tanzania na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, kutaka kujua kiwango cha uungwaji mkono wa Rais Magufuli tokea aingie madarakani.

 
Sikiliza sauti02:43

Kesi kuhusu kuminya uhuru wa habari yaanza kusikilizwa Tanzania

Mzee akisoma gazetiHaki miliki ya pichaAFP
Image captionMzee akisoma gazeti
Sheria mpya ya vyombo vya habari nchini Tanzania ambayo ilipitishwa na rais wa nchi hiyo mnamo Novemba 2016, imeanza kusikilizwa rasmi leo katika mahakama ya Afrika Mashariki huko, Arusha, Kaskazini mwa Tanzania.
Kesi hiyo ilifunguliwa mwezi Januari 2017 na wanaharakati pamoja na wataalamu katika tasnia hio ya habari, wakiwa wanaamini kwamba sheria hio inakiuka mkataba wa Afrika Mashariki kwa kuminya uhuru wa habari na uhuru wa watu kujieleza katika nchi hio.
Madai ambayo wameyaainisha na wanaona kuwa sheria hiyo imekeuka ni kwa jinsi ambavyo Waziri amepewa mamlaka ya kuvifungia vyombo vya habari na kuwepo kwa ugumu kwa wageni kupata vibali vya kuja kuandika taarifa zao nchini humo.
Mkataba wa Afrika mashariki unataka kila nchi lazima ikuze demokrasia na uhuru wa kujieleza.Ingawa wanaamini kuwa hakuna uhuru ambao hauna mipaka lakini sheria hii inafanya uhuru usiwepo.
Aidha baraza la habari nchini Tanzania na wanaharakati wa haki za binadamu wanasema sheria mpya ya habari imetoa vifungu vinavyokandamiza tasnia hiyo ya habari katika kutoa taarifa.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa rasmi kwa njia ya maandishi kwa sasa ili kiini cha mgogoro uweze kupatikana.
Wadau wa habari walidahi kuwa walitoa maoni yao wakati sheria hiyo ikiwa inaandaliwa lakini wanadhani kuwa ushauri wao haukuzingatiwa hivyo inabidi irekebishwe tena.
Serikali ya Tanzania yalifungia gazeti la mwanahalisi kwa miaka 2
Image captionSerikali ya Tanzania ilifungia gazeti la Mwanahalisi kwa miaka 2
Mwaka jana, magazeti manne ya Tanzania Daima , Mawio, Mwanahalisi, na Raia Mwema yalifungiwa kwa muda wa kati ya siku 90 hadi miaka miwili.
Miaka ya hivi karibuni, sekta ya habari Tanzania imekua kwa kasi kubwa, lakini pia vyombo vya habari vimekuwa vikimulikwa kwa karibu sana na serikali huku sheria na kanuni zikiwa zimepatiwa mamlaka kuwazuia waandishi na mashirika ya habari kwa misingi ya usalama wa taifa na maslahi ya umma.

Novichok: Mambo muhimu kuhusu sumu kali ya Urusi iliyotumiwa kumshambulia jasusi

Investigators in Winterslow, near Salisbury on 12 March 2018Haki miliki ya pichaPA
Image captionWachunguzi waliondoa gari hili kutoka kwa kijiji karibu na Salisbury Jumatatu
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May Jumatatu alisema jasusi wa zamani wa Urusi na binti yake walipewa sumu kali ambayo ni sehemu ya kundi la kemikali za sumu kwa jina Novichok.
Sergei Skripal na binti yake Yulia bado wamo katika hali mahututi hospitalini kufuatia jaribio hilo la kuwaua eneo la Salisbury mnamo 4 Machi.
Kemikali hiyo ilitambuliwa na wataalamu katika maabara ya ulinzi na sayansi Porton Down.
Tunafahamu nini kuhusu kundi hili la kemikali zenye sumu?
1) Ziliundwa katika Muungano wa Usovieti
Jina Novichok maana yake ni "mgeni" kwa lugha ya Kirusi.
Ni jina linalotumiwa kurejelea kemikali za sumu ambazo hushambulia mfumo wa neva mwilini.
Kemikali hizo ziliundwa na Muungano wa Usovieti miaka ya 1970 na 1980.
Zilifahamika kama silaha za kemikali za kizazi cha nne na zilistawishwa chini ya mpango wa silaha za Muungano wa Usovieti uliofahamika kama "Foliant".
Mwaka 1999, maafisa wa ulinzi kutoka Marekani walisafiri hadi Uzbekistan kusaidia kuvunja na kusafisha moja ya eneo kubwa zaidi lililotumiwa kufanyia majaribio silaha za kemikali na Muungano wa Usovieti.
Kwa mujibu wa afisa mmoja wa ngazi za juu ambaye alitorokea Marekani, maafisa wa Usovieti walitumia kiwanda kilichokuwa eneo hilo kuunda na kufanyia majaribio sampuli za kemikali ya Novichok. Kemikali hii iliundwa mahsusi kutoweza kugunduliwa na wakaguzi wa silaha na sumu katika mataifa mengine.
Sergei Skripal and his daughter YuliaHaki miliki ya pichaEPA/ YULIA SKRIPAL/FACEBOOK
Image captionSergei Skripal, 66, na Yulia, 33, wamo katika hali mahututi hospitalini
2) Ni sumu yenye nguvu kuliko sumu nyingine
Moja ya kemikali hizi zinazofahamika kama Novichok - A-230 - inadaiwa kuwa na nguvu mara 5-8 zaidi ya sumu nyingine hatari kwa jina VX.
"Hii ni sumu hatari na changamano kushinda sumu aina ya sarin au VX na pia huwa vigumu zaidi kuitambua," anasema Prof Gary Stephens, mtaalamu wa kemikali katika Chuo Kikuu cha Reading.
Sumu ya VX ndiyo iliyotumiwa kumuua ndugu wa kambo wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un mwaka jana, kwa mujibu wa Marekani.
Aina mbalimbali za kemikali hii ya A-230 zimekuwa zikitengenezwa, na aina moja inadaiwa kuidhinishwa na jeshi la Urusi itumike kama silaha ya kemikali.
3) Aina mbalimbali za Novichok
Ingawa baadhi ya aina za sumu hii ya Novichok huwa majimaji, kuna aina nyingine ambazo ni yabisi (gumu au isiyokuwa majimaji).
Ni kemikali ambayo pia inaweza kugeuzwa kuwa poda laini.
Baadhi ya sumu hizi pia hudaiwa kutumiwa kama "silaha za ngazi mbili". Hii ina maana kwamba sumu hii huhifadhiwa mara nyingi kama kemikali aina mbili ambazo zikiwa kando kando si hatari. Zinapochanganywa, huingiliana na kutengeneza sumu.
Hii huifanya rahisi sana kwa viungo vya kemikali hii kusafirishwa kwani huwa sumu tu zikichanganywa.
"Moja ya sababu ambayo hufanya sumu hizi kuandaliwa ni kwa sababu viungo vyenyewe havijapigwa marufuku," anasema Prof Stephens.
"Hii ina maana kwamba kemikali hizi ambazo huchanganywa huwa rahisi sana kusafirishwa bila kuwa hatari kwa anayezisafirisha."
Theresa May addressing Commons on 12 March 2018
Image captionBi May akihutubia wabunge baada ya Mkutano wa Baraza la Usalama wa Taifa
4) Zinaweza kuathiri mtu haraka sana
Mtu anapopumua sumu ya Novichok, au hata ikigusa ngozi yake, basi huanza kumuathiri upesi.
Dalili zake zinaweza kuanza kujionesha katika kipindi cha muda mfupi hivi, sekunde 30 hadi dakika mbili.
Hata hivyo, sumu hii ikiwa kama poda huchukua muda zaidi kuanza kuathiri mtu.
Dalili kali zinaweza kuanza kujionesha saa 18 baada ya mtu kukumbana na sumu hiyo.

Sumu aina ya Novichok

Mara 5 hadi 8
hatari zaidi ya sumu ya VX
  • 2 kemikali ambazo hazina sumu zinazoweza kuchanganywa na kuunda sumu hii
  • Sekunde 30 Muda ambao unatosha kwa dalili za sumu kuanza kujionesha
  • 1970 Kipindi ambacho sumu hii iliundwa na Muungano wa Usovieti
EPA
5) Dalili zake ni sawa na za sumu nyingine za neva
Sumu aina ya Novichok huwa na madhara sawa na ya sumu nyingine zenye kushambuliwa mfumo wa neva.
Hii ina maana kwamba huwa zinafanya kazi kwa kuzuia ujumbe au mawasiliano kati ya mfumo wa neva na misuli, na pia kusambaratisha shughuli nyingi muhimu za mifumo mwilini.
Dalili zake ni pamoja na macho kuwa na rangi nyeupe, huku mboni za macho zikiminyika, mtukutiko wa maungo, na mtu kuonekana kupumbaa. Wakati mwingine, mtu hupoteza fahamu, kushindwa na kupumua na kufariki.
Sumu hizi kimsingi hufanya moyo kupunguza mapigo yake na kubana njia zinazotumiwa na mwili kupumua na mwishowe mtu kufariki kutokana na mtu kukosa hewa ya kutosha.
Baadhi ya aina za sumu hii ya Novichok zimeundwa mahsusi kuhakikisha dawa za kawaida za kupoza nguvu ya sumu haziwezi kufanikiwa.
Iwapo mtu amepewa sumu huu, anafaa kuvuliwa mavazi yake na ngozi yake kuoshwa vyema kwa maji na sabuni.
Macho yake yanafaa pia kuoshwa vyema kwa maji na apewe hewa ya oksijeni.
What nerve agents do to the body

Wanafunzi Tanzania hawaamini uchunguzi wa Polisi

Abdul NondoHaki miliki ya pichaNONDO FACEBOOK
Image captionAbdul Nondo ,aliyedaiwa kujiteka
Mtandao wa wanafunzi nchini Tanzania (TSNP) umesema usingeweza kupuuza taarifa za hatari ya usalama iliyokuwa ikimkabili mwenyekiti wao Abdul Nondo.
Taarifa za kupotea kwa Bwana Nondo katika mazingira ya kutatanisha ziliibuka tarehe 6 Machi baada ya Nondo kutuma ujumbe kwa mmoja wa marafiki zake usiku wa manane akisema kuwa usalama wake uko hatarini.
Hali hiyo ilipeleka taharuki miongoni mwa wanafunzi wenzake na jamii kwa ujumla huku wengi wakidhani kuwa bwana Nondo alikuwa ametekwa.
Akizungumza na BBC mapema hii leo, msemaji wa TSNP Helllen Sisya amesema taarifa za nini hasa kilichomsibu bwana Nondo zinakinzana
"Sisi bado hatuamini Uchunguzi uliofanywa na polisi kwa kuwa hatujamsikia Nondo akiongea na kile tulichoelezwa na polisi mkoani Iringa na hiki tulichokisikia leo kwa polisi Dar es Salaam haviendani", alisema Sisya.
Mtandao wa wanafunzi
Image captionMtandao wa wanafunzi(TSNP)
Mtandao wa Wanafunzi Tanzania ambao ulitoa taarifa kwa Umma kuhusu kupotea kwa Abdul Nondo,hawakubaliani na taarifa hiyo ya polisi kwa kudai kuwa inakanganya,Polisi wanadai kuwa alipatikana akiendelea na shughuli zake za kawaida alipoenda kumtembelea mpenzi wake na wakati wao walipata taarifa kutoka kwa jeshi la polisi wa Iringa kuwa Nondo alifika kituoni hapo akiwa hajitambui.
Mapema leo Jeshi la polisi nchini Tanzania lilizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam,Abdul Nondo aliyedaiwa kupotea katika mazingira ya kutekwa ulikuwa uzushi.
Kamanda wa Polisi,Lazaro Mambosasa amedai kuwa taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii na kuzua taharuki mnamo tarehe 6,Machi kwa madai kuwa mwanafunzi huyo ametekwa na watu wasiojulikana si za kweli kwa kuwa uchunguzi wa jeshi la polisi umebaini kwamba mwanafunzi huyo alikutwa akiendelea na shughuli zake za kawaida na wala hakutekwa au kutoa taarifa kuwa ametekwa.
Mambosasa
Image captionAfande Lazaro Mambosasa
Upelelezi umebaini kuwa alikuwa anafanya mawasiliano na mpenzi wake wakati yuko safarini kutoka Dar es salaam kuelekea Iringa hata baada ya muda aliodaiwa kutuma ujumbe kuwa yuko hatarini.
Lakini jeshi hilo la polisi halikuishia kwenye mawasiliano ya simu tu bali lilienda kumpima afya yake na kubaini kuwa ni mzima wa afya na hana tatizo la akili.
Aidha jeshi la polisi limedai kuwa litaendelea kumshikilia mpaka atakapopelekwa mahakamani kusikiliza kesi yake kuhusu uzushi na imetoa onyo kwamba haitamhurumia mtu yeyote atakayesambaza taarifa za namna hiyo.
Viongozi wa mtandao wa wanafunzi wametakiwa kufika kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi.
Hata hivyo hivi karibuni nchini Tanzania kumekuwepo na visa vya mauaji na kutoweka kwa watu bila kujua kiini cha kutoweka kwao.