Sunday, December 3

Nampenda Raila lakini naguswa sana na Uhuru


Moja ya mambo ambayo hutokea sana kwenye Nyanja za siasa ni ufuasi. Wanasiasa wote wakubwa na wadogo huwa na watu wanaowaunga mkono au kuwapinga. Leo nawafanyia uchambuzi wanasiasa wawili wa Kenya, Raila Odinga na Uhuru Kenyatta. Lengo la makala hii siyo kupitia sifa zao tu, kwa kiasi kikubwa ni kuonyesha namna gani masuala ambayo Raila na Uhuru wanayafanya au kuyasimamia yana mafunzo mengi kwa wanasiasa wa Tanzania na siasa za maendeleo za Afrika Mashariki.
Uhuru na Raila wana historia tofauti, lakini kwa kiasi kikubwa wote wawili wamezaliwa kwenye familia za wazee ambao wamewahi kushikilia madaraka makubwa sana ya kisiasa nchini Kenya. Wote wawili wamewahi kufanya kazi kwenye chama kimoja kama viongozi na wamewahi kufanya kazi kwenye vyama tofauti kama viongozi. Wote wawili wana sifa za kupenda sana demokrasia.
Raila Odinga
Nampenda sana Raila kwa sababu ni mwanasiasa mwenye mafanikio makubwa sana kimsimamo. Masuala ambayo huyasimamia yakitetereshwa hufanya maamuzi ya haraka ya kutengana na msimamo mpya asiouamini. Nimewahi kuandika nikielezea alivyowahi kuhama vyama kadhaa ili kulinda msimamo wake na au mwelekeo wake kisiasa. Katika uhamaji ule kwa kweli Raila hakuwa tu anahama ili kutafuta madaraka – alikuwa anahama pamoja na madaraka lakini ni kujaribu kutaka kupigania kitu ambacho alikuwa anataka kiwe, na hasa masuala ya katiba na haki za Wakenya.
Raila, kila mara alipoona anashindwa kufikia malengo yake mahali, alikwenda mahali pengine na kuongoza mapambano ya kusaka kile anachokisimamia. Wanasiasa wengi wa Tanzania wanapohama kwenye vyama vya zamani kwenda vipya, huenda huko na kukaa kimya, na kufuata kila kilichoko huko – ndiyo, nidhamu za kivyama zinataka sana watu kuzungumza masuala ya chama kwa utaratibu maalum na kwa kiasi kikubwa kutetea chama, hilo linafahamika – lakini chama hakikatazi mwanachama au kiongozi wake kusimamia masuala mema aliyoyaamini.
Mathalani, kama ulikuwa mwanasiasa wa chama cha DP na sasa umehamia UDP, kama ulikuwa unapigania haki za watoto pale DP – kwa nini ukifika UDP unakaa kimya? Kwani haki za watoto zimepatikana? Raila anatufundisha kusimamia ajenda. Raila alipoona chini ya Kanu Kenya haiendi sawa na akajiridhisha kuwa moja ya mambo yanayoirudisha nyuma Kenya ni ukosefu wa katiba mpya na imara – aliendelea na mchakato wa kupigania Katiba mpya ya Kenya hata nje ya Kanu na alifanikiwa kuikwamisha Kanu.
Mapambano ya kudai Katiba itakayoleta uimara wa nchi na utendaji wake ni suala ambalo linamtangaza Raila na kumpa heshima kubwa sana Kenya na duniani. Mwanasiasa huyu ndiye mhimili mkubwa wa demokrasia ya Kenya na amepitia matatizo mengi sana katika kuishi maisha ya kuitafuta Kenya ambayo itaongozwa kitaasisi na amepigana na kufanya hatua zote hizi akiwa katika vyama zaidi ya kimoja, akiwa gerezani na akiwa ndani ya serikali kama kiongozi.
Raila amepata kuwa Waziri Mkuu wa Kenya baada ya machafuko ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 akifanya kazi chini ya Rais Mwai Kibaki kwenye serikali ya umoja wa kitaifa. Bila kujali kuwa alikuwa serikalini na chini ya Kibaki, Raila aliendelea kupaza sauti na kushikilia ajenda yake ya Kenya kuwa na Katiba mpya, demokrasia imara, utawala wa sheria, ulinzi wa haki za binadamau, uwazi na uwajibikaji na utawala bora. Ajenda hizi Raila hajaziacha na nina uhakika hata akifa zitasindikizana naye kaburini.
Somo kubwa analotoa Raila kwa wanasiasa wa Tanzania ni kuenzi misimamo yao hata wanapokuwa kwenye vyama vipya. David Kafulila amehamia CCM mathalani, hapaswi kabisa kuachana na ajenda yake ya kupambana na ufisadi – na awe mkali kama pilipili hata pale anapogundua kuwa chama chake kipya kimeshiriki kwenye ufisadi fulani au kimekalia kimya ufisadi fulani au chama chake cha zamani kimefanya ufisadi fulani au kimeshindwa kuibana serikali kuhusu ufisadi fulani.
Kafulila ni mfano tu lakini lengo ni kuwakumbusha wanasiasa kwamba mambo mazuri waliyowahi kuyapigania na bado yanahitajiwa na taifa letu leo, wanapaswa kuendelea kuyapigania bila kujali wako kwenye chama kipi au wamehamia wapi. Kukaa kimya au kutulizwa unapohamia kwenye chama kipya na kuacha kabisa kusimamia masuala makubwa ya kitaifa kwa sababu yoyote ile, ni usaliti mkubwa kabisa na ndiyo unafanya wanasiasa wanaohama vyama kuitwa wasaliti.
Uhuru Kenyatta
Uhuru Kenyatta amejitanabaisha kama mwanademokrasia. Baba yake, mzee Jomo Kenyatta hatajwi kama mwanademokrasia. Na demokrasia tunayoizungumzia ni ile iliyomo kwenye sheria na katiba zetu na ile ambayo dunia inatarajia kuiona kutoka kwa wanasiasa wote. Yako mambo mengi sana yanayoonyesha kuwa Uhuru siyo mchokozi, ni mtulivu na anapenda sana kuheshimu haki za watu na makubaliano yaliyopo. Uhuru ni mfano halisi wa kiongozi mwenye mamlaka na ambaye bado anaamini wako watu wana haki kushinda hata mamlaka yake.
Naposema hivi kuna watu wanaweza kujiuliza, mbona Uhuru ameyaacha majeshi yake yakawapiga na kuwaumiza waandamanaji hivi karibuni huku akichukua hatua zingine kadhaa za kudhibiti utulivu nchini mwake na zingine zimekuwa na madhara? Jibu ni rahisi sana – walau kwa Kenya, matumizi ya nguvu za polisi yanadhibitiwa kwa kiasi fulani kuliko nchi zingine na uwezekano wa hili kutendeka lazima umuendelee Rais wa nchi.
Uhuru ndiye amiri jeshi mkuu wa majeshi ya Kenya na ndiye anayapa amri. Lakini, sheria na katiba ya Kenya vimeweka utaratibu wa namna ambavyo majeshi yatatekeleza wajibu wao kiweledi na bila kutumia nguvu kubwa sana – na hilo limekuwa likifanikiwa. Hivi karibuni kuna mtoto wa miaka 7 alipigwa risasi na polisi, akauawa! Vitendo vya namna hii haviwezi kumuhusu amiri jeshi mkuu, vinahusu weledi wa polisi wanapokuwa kazini na kwa kweli kama polisi wangekuwa wanataka kuua watu wangeliwaua kwa idadi kubwa zaidi nchini humo.
Kilichofanya watu wengi wasiuawe ni uwezo mkubwa wa kidemokrasia wa Uhuru. Hata polisi wa Kenya walipojaribu kuzuia shughuli za siasa na maandamano ya vyama vya upinzani, Uhuru aliingilia kati na kusisitiza lazima polisi wawalinde waandamanaji hata kama waandamanaji hao wanampinga yeye na kuchaguliwa kwake. Siyo rahisi kwa Afrika kupata marais wenye fikra za kidemokrasia namna hii.
Nchi nyingine za Afrika Mashariki kuna matumizi mabaya sana ya madaraka na kwa kweli marais wa nchi ndiyo hutoa maagizo ya kuzuia shughuli za vyama vingine pamoja na kuwadhibiti wanasiasa wa vyama vingine. Tumekuwa na mifano mingi sana ya udhibiti huo kutoka Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi. Ni rahisi kusema kuwa wakuu wa nchi hizo hawaamini katika demokrasia na wao hawayaishi maisha ya Uhuru Kenyatta.
Pamoja na marais hawa wengine kutoyaishi maisha ya Uhuru Kenyatta, wanalo kubwa la kujifunza. Wao kama alivyo Uhuru wote wameendeleea kuwa wakuu wa nchi na wakiheshimiwa sana ndani na nje ya nchi zao. Uhuru Kenyatta amefanya makosa kadhaa kwenye utawala wake, lakini ameionyesha Afrika kuwa mtu anaweza kuwa na madaraka makubwa kushinda wote katika nchi yake, lakini bado akayatumia madaraka hayo kwa faida ya watu wote.
Katika bara la Afrika, siyo rahisi mtu au watu wakaandamana kupinga kuchaguliwa kwa rais wa nchi yao. Watu hao watakutwa mochwari. Kenya inatuonyesha kuwa kila mtu anaweza kupingwa. Mahakama ya Kenya hivi karibuni ilituonyesha kuwa mhimili wa serikali siyo mkuu kuliko mingine na unaweza kudhibitiwa na mahakama au bunge na ukarudishwa kwenye utaratibu. Lakini yote haya yanawezekana katika dunia ya Kenya, chini ya Uhuru Kenyatta – mwanademokrasia wa mfano katika ukanda wetu.
Raila na Uhuru ni shamba darasa
Natambua Raila na Uhuru watastaafu siasa baadaye, yako mambo mengi wameyaacha na watakumbukwa sana kwa sababu ya mambo hayo. Kama kuna jambo ambalo viongozi wengi wa Afrika husahau wawapo madarakani, ni kuandaa kesho yao. Ni kujiuliza, Je, kesho ntakuwa kama Mandela, Nyerere, Nkrumah?
Wanasiasa wote wa Afrika na hasa Tanzania, wale walioko chama kinachoongoza dola, wanaweza kuendelea kujiuliza, je, kesho ntakuwa Uhuru Kenyatta au Raila Odinga? Je ntakuwa Raila ambaye amepigania mabadiliko ya kimfumo ya Kenya bila kuchoka na kwa kutumia majukwaa tofauti bila kuogopa wala kukata tamaa? Au ntakuwa Uhuru Kenyatta ambaye pamoja na kuwa na madaraka ya mkuu wa nchi, hatujasikia hata akimtishia maisha au kumkamata na kumfunga Raila Odinga.

Waziri aagiza mkandarasi akamatwe


Naibu Waziri Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso ameviagiza vyombo vya dola mkoani Ruvuma kumsaka mkandarasi (jina tunalo) kwa tuhuma za kulipwa Sh500 milioni na kuondoka.
Agizo hilo alilitoa wilayani Tunduru jana baada ya kupokea taarifa ya mradi mkubwa wa maji unaogharimu Sh1 bilioni uliopo Mironde, Kijiji cha Matemanga.
Naibu Waziri Aweso alisema kwamba Serikali haitamvumilia mkandarasi yeyote atakayekula pesa ya mradi wa maji na kuwataka waliokula pesa hizo kujiandaa ‘kuzitapika.’
Naibu Waziri aliwaagiza wakuu wa idara na wakurugenzi wa halmashauri kuacha kutoa tenda kwa ushemeji au mtoto wa mjomba.
Awali, mhandisi wa maji wa halmashauri ya Tunduru, Emmanuel Mfoi alisema mradi huo ulianza kujengwa mwaka 2013 na ulitakiwa kukamilika mwaka 2014 lakini umekuwa ukisuasua.
Alisema kwamba mkandarasi alikuwa akiongezewa muda mara kwa mara na kutakiwa akabidhi mradi huo kwa halmashauri kabla ya Novemba 27 mwaka huu lakini kashindwa.
Mkazi wa kijiji cha Matemanga, Said Hamis alimweleza Naibu Waziri kuwa wananchi wanateseka kutokana na kutopata huduma ya maji.
“Tunashukuru umefika kiongozi wetu, huduma ya maji hapa hakuna kabisa hali ni mbaya na hatuna matumaini ya kupata majisafi na salama, tunaomba Serikali itutatulie kero hii ya muda mrefu,” alisema Hamis.

Somo kutoka Ghana kwa Akufo, ‘wilaya moja kiwanda kimoja’


Alipokuwa kwenye kampeni za urais mwaka 2015, Dk John Magufuli alijinadi kuwa anataka kuielekeza nchi kwenye uchumi wa viwanda. Ahadi hiyo ilipewa jina la “Tanzania ya Viwanda.”
Ni sawa ana ilivyokuwa Ghana. Katika Uchaguzi Mkuu Desemba 2016, Rais Nana Akufo-Addo kutoka NPP, aliomba ridhaa ili atawanye viwanda kila kona ya nchi hiyo, ahadi iliyobatizwa jina la “Wilaya Moja, Kiwanda Kimoja”.
Rais Magufuli aliapishwa Novemba 5, 2015 sasa ametimiza miaka miwili madarakani. Oktoba 2020, akitaka atarejea kwa wapigakura kuomba ridhaa ya kuongezwa kipindi cha pili.
Rais Akufo-Addo alikula kiapo cha kuiongoza Ghana kwa miaka minne Januari 17. Katika uchaguzi huo Akufo-Addo alimshinda Rais aliyekuwa madarakani, John Mahama.
Tanzania na Ghana ni nchi ambazo katika miaka ya 6, ziliweka mkazo mkubwa wa sera ya viwanda kwa lengo la kuyaelekeza mataifa hayo kwenye uchumi unaotokana na uzalishaji kuliko makusanyo ya kodi. Tanzania ilikuwa chini ya Mwalimu Nyerere, Ghana chini ya Kwame Nkrumah.
Kama ilivyotokea Ghana, sera ya viwanda kutofanikiwa na vilivyokuwepo kufa kwa sababu ya ukosefu wa uongozi sahihi, ndivyo na Tanzania ambavyo viwanda vingi viliingiza hasara badala ya faida, mwisho vikabinafsishwa kwa watu ambao baadhi wameshindwa kuviendeleza.
Tofauti na utekelezaji wa miaka ya sitini na sabini kwa nchi zote mbili kuwa chini ya Serikali, awamu ya sasa sekta ya viwanda siyo ya umma, bali watu binafsi, hivyo Serikali ina wajibu wa kuandaa mazingira yenye kuvutia na kuirahisishia sekta binafsi kuwekeza kwenye viwanda.
Kutokana na mkazo wa sera hiyo kwa nchi zote mbili na mafanikio ambayo Ghana imeanza kuyapata ndani ya muda mfupi wa utawala wa Akufo-Addo, inapendeza kuishauri Tanzania ione cha kujifunza.
Walichofanya Ghana
Akufo-Addo amebobea katika fani ya sheria, hivyo hajabobea sana katika uchumi. Hata hivyo, kwenye kutimiza malengo ya kiuchumi kwa nchi, anayo bahati ya kuwa na Dk Mahamudu Bawumia, mshirika wake ambaye ni makamu wa rais aliye nguli wa uchumi.
Buwamia ni bingwa wa uchumi ambaye shahada yake ya uzamivu inampambanua kama mbobezi wa uchumi kivitendo, kimuundo, kitabia na kiuamuzi. Pia ni mtaalamu asiyetiliwa shaka katika Uchumi wa Kimataifa, Uchumi wa Maendeleo na Sera ya Fedha.
Kabla ya NPP kumteua Buwamia kuwa mgombea mwenza wa Akufo-Addo, alikuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu Ghana, hivyo sera za kiuchumi na maendeleo ya kibenki kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa nchi, zimelala kwenye kichwa chake.
Hiyo ndiyo sababu masuala mengi ya kiuchumi yanasimamiwa moja kwa moja na Buwamia. Na kwa usimamizi huo, Serikali ya Akufo-Addo iliona umuhimu wa kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika biashara nyingi, ushuru, Kodi ya Ongezeko la Mtaji ili kuifanya sekta binafsi ipumue, ifanye biashara na ipate fedha.
Machi 12, mwaka huu, katika mkutano wa kutiliana saini makubaliano ya kutokutoza kodi mara mbili kwa bidhaa ziingiazo na kutoka kati ya Ghana na Mauritius, uliofanyika Mauritius, Buwamia alisema, bajeti mpya Ghana kwa mwaka 2017-2018, kodi nyingi zimefutwa ili kuipa uhai sekta binafsi.
“Lengo letu ni kuifanya Ghana kuwa nchi rafiki zaidi kibiashara na uchumi Afrika. Nchi rafiki kibiashara na uchumi wa watu Afrika. Ndiyo maana tumeondoa VAT kwenye uwekezaji wa biashara zisizohamishika. Tumefuta ushuru kwenye uingizaji wa mitambo yenye kutumika kutengeneza viwanda,” alisema Buwamia.
Alisema kuwa kodi nyingine zilizofutwa ni VAT katika usafiri wa ndani wa ndege, huduma za kifedha, ushuru wa uingizaji wa malighafi za viwandani na vipuri vya aina zote, vilevile wamepunguza VAT kwa wafanyabiashara wadogo kutoka asilimia 17 mpaka asilimia 3.
Msingi wa kuondoa kodi na ushuru kwa sehemu kubwa Ghana, upo kwenye maeneo makuu mawili, kwanza ni kuiondoa nchi kwenye uchumi wa kodi kisha kujielekeza kwenye uchumi wa uzalishaji. Ulimwengu wa leo, uzalishaji unafanywa na sekta binafsi, hivyo ni lazima ipewe nguvu.
Pili sera ya ‘wilaya moja, kiwanda kimoja’ ni ya Serikali lakini inatekelezwa na sekta binafsi kwa asilimia 100. Hivyo, Serikali inapaswa kuandaa, kutengeneza na kuboresha mazingira kwa wafanyabiashara, lakini muhimu zaidi ni kuwajengea vivutio ili wavutiwe kuwekeza kwenye viwanda.
Huwezi kuwa unataka mfanyabiashara awekeze kwenye viwanda wakati mazingira ya kibiashara ni magumu. Mfanyabiashara anabanwa hata kukuza mtaji, kwani anakatwa kodi kadiri anavyoongeza mtaji. Na viwanda vinahitaji mtaji mkubwa. Anafikaje huko?
Tanzania inaweza kujifunza kwanza kwa Ghana kutokana na mazingira ambayo Serikali imetengeneza kufanikisha sera yake ya ‘wilaya moja, kiwanda kimoja. Mazingira yenye kushawishi wafanyabiashara kuwekeza kutokana na unafuu mkubwa wa kodi ambao umewekwa.
Matokeo ya Ghana
Unadhani baada ya Ghana kufuta kodi maeneo mengi ili kuwarahisishia wafanyabiashara kuwekeza kwenye viwanda, mapato ya nchi yameporomoka? La! Ripoti ya Benki ya Dunia inaipata jeuri kuwa sera zake za kiuchumi kuelekea uchumi wa viwanda kila wilaya ni bora na ni mwafaka.
Ukuaji wa sekta ya viwanda ni wa kishindo, kwani imepanuka kwa asilimia 11.5, wakati ukuaji wake ulikuwa asilimia 1.8 mwaka jana. Katika eneo hilo, unaweza kuona kasi ya Ghana kuyafikia malengo ya uchumi wa viwanda kabla ya Serikali ya Akufo-Addo haijatimiza mwaka mmoja.
Sekta ya kilimo imekua kwa asilimia 7.6 kutoka asilimia 5. Hii inatokana na ukweli kwamba ukuaji wa viwanda siku zote huchochea kukua kwa kilimo kwa sababu uzalishaji wa bidhaa hutegemea malighafi ambazo nyingi hutoka shambani. Upande mwingine mfumuko wa bei umeshuka kufika asilimia 11.9 Julai mwaka huu, kutoka asilimia 12.4 Desemba mwaka jana.
Juni mwaka huu, mzani wa biashara kwa maana ya uwiano wa thamani ya fedha kati ya mauzo nje ya nchi na uagizaji wa bidhaa kutoka nje umekuwa chanya, kwa maana mauzo ya nje yamezidi kwa dola 1.43 bilioni (Sh3.2 trilioni), sawa na asilimia 3.1 ya Pato la Ndani la Taifa (GDP), wakati mwaka jana mzani ulikuwa na nakisi ya asilimia 3.3.
Matokeo hayo ya mzani wa biashara kuwa chanya, kwa maana ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi kuwa na thamani kubwa kuliko yale ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kufukia nakisi ya mwaka jana, kisha kuleta ziada ya Sh3.2 trilioni, ni kipimo chenye kuwasha taa ya kijani kuhusu mwanzo mzuri wa uchumi wa uzalishaji.
Matokeo mengine ni kuwa akiba ya fedha za kigeni imepanda kutoka dola 4.9 bilioni (Sh11 trilioni) Desemba mwaka jana mpaka kufikia dola 5.9 bilioni (Sh13.3 trilioni) Julai mwaka huu. Hiki ni kipimo kingine chenye kuashiria uimara wa nchi kibiashara.
Matokeo zaidi
Oktoba 3, mwaka huu, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Ghana, Robert Lindsay, alifanya mahojiano katika kipindi cha Citi Breakfast Show cha redio Citi Fm ya Accra, na kueleza uelekeo wa utekelezwaji wa sera ya ‘Wilaya moja, kiwanda kimoja’ kwamba mafanikio ni makubwa.
Lindsay alisema, mazingira bora ambayo Serikali ya Ghana imeyaweka kwa ajili kuirahisishia sekta binafsi kufanya biashara yamewezesha mpaka sasa kuwa na viwanda 173 ambavyo vinaendelea kujengwa, huku maombi mengi zaidi yakiendelea kufanyiwa kazi.
“Kwa muda sasa, tumeendelea kupokea maombi ya wafanyabiashara kujenga viwanda, wenye kuomba ni wafanyabiashara wa ndani na nje ya Ghana. Tumeshapokea maombi 600 ya kujenga viwanda na mipango ya biashara ya kuwekeza kwenye viwanda tuliyopokea mpaka sasa ni 457,” alisema Lindsay.
Alichokisema Lindsay kinaakisi moja kwa moja takwimu za Benki ya Dunia kuhusu matokeo ya ukuaji wa kiuchumi wa Ghana tangu kuingia kwa Serikali ya Akufo-Addo na makamu wake, Dk Buwamia. Inaonekana dhahiri kuwa wawekezaji wanakimbilia Ghana, kwani wanaona ni fursa iliyorahisishwa.
Ghana ina wilaya 216, hivyo kama viwanda vyote 173 alivyosema Lindsay vitakamilika ndani ya mwaka mmoja mpaka miwili, maana yake kutakuwa na upungufu wa viwanda 43 tu. Na ukifuata maombi na mipango ya uwekezaji, ni wazi inawezekana kufikisha hata viwanda vitatu kila wilaya.
Kizuri zaidi kwa Ghana ni kuwa mipango yao ya kujenga viwanda inafuata aina ya malighafi kwenye wilaya. Busara hiyo inasaidia kuchangamsha sekta nyingi, kwamba wakati nchi ikizalisha bidhaa, inawezesha maendeleo ya kibiashara kuwa makubwa na soko la wakulima kuwa la uhakika.
Hayo ndiyo mambo ambayo yanavutia kwa Ghana na yanaweza kuifaa Tanzania. Kutoa unafuu wa kodi na kuweka mazingira rahisi kwa wafanyabiashara ili kukuza mitaji yao na kuwekeza. Mazingira ya kibiashara yakiwa magumu ni vigumu mfanyabiashara kuvutiwa kujenga kiwanda. Na izingatiwe kwamba Serikali haijengi viwanda.

Serikali kuajiri walimu 11,000


Serikali imepanga kuajiri walimu 11,000 wa shule za msingi na sekondari katika mwaka wa fedha wa 2017/18.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleiman Jafo alisema katika mpango huo, walimu 7, 000 watakuwa wa shule za msingi na 4,000 wa sekondari.
“Hadi kufikia Desemba 31, walimu 2,700 watakuwa wameshaajiriwa,” alisema Jaffo
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma wakati wa kurekodi kipindi cha Tujadiliane kinachoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kurushwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari, Jafo alisema ajira hizo zitapunguza upungufu wa walimu unaotokana na ongezeko la wanafunzi tangu Sera ya Elimu Bure ya Msingi ianze kutekelezwa.
Tangu mwaka jana, Serikali inatekeleza sera hiyo inayoligharimu Taifa zaidi ya Sh20 bilioni kila mwezi, huku idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa katika shule za msingi na wale wanaojiunga na za sekondari ikiongezeka kwa zaidi ya wanafunzi milioni moja.
Miundombinu shuleni
Kuhusu miundombinu shuleni alisema kwamba Serikali imetenga zaidi ya Sh37 bilioni za ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari za umma 148.
Akifafanua, Jafo alisema zaidi ya Sh21 bilioni zimetumika kujenga mabweni 85 katika awamu ya kwanza ya mpango huo, huku awamu ya pili ya kujenga mabweni 65 iliyoanza kutekelezwa Agosti ikitarajiwa kugharimu Sh16 bilioni.
Kuhusu matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa,
Waziri Jafo alisema Serikali imetenga zaidi ya Sh246 bilioni kukabiliana na upungufu wa matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa katika shule za umma.
“Theluthi moja ya fedha hizo, sawa na Sh82 bilioni zitatumika kukamilisha miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo inayotekelezwa kwa nguvu za wananchi,” alisema.
Sekta ya afya
Waziri Jafo alisema kuwa Serikali imepanga kujenga vituo vya afya 172 kwa fedha kutoka Benki ya Dunia (WB), Serikali ya Canada na wadau wengine kupitia mfuko wa pamoja wa kuendeleza Sekta ya Afya (Basket Fund).
“Lengo ni kutekeleza sera ya zahanati kila kijiji na kituo cha afya katika kila kata ili kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma za afya,” alisema Jafo.
Alifafanua kuwa hivi sasa ni kata 530 pekee kati ya 3,900 zilizopo nchini ndizo zenye vituo vya afya.
Kuhusu upatikanaji wa dawa na vifaatiba, alisema Serikali imeongeza bajeti hadi kufikia Sh269 bilioni kwa ajili hiyo.
“Tunazo pia zaidi ya Sh127 bilioni za Basket Fund zitakazoelekezwa kwenye utatuzi wa changamoto ya upungufu wa dawa na vifaa tiba kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma,” alisema.
Akizungumzia upungufu wa watumishi katika sekta ya afya iliyochangiwa na uhakiki wa vyeti feki, Waziri Jafo alisema tayari Serikali imeajiri watumishi 2,058 huku wengine zaidi wakitarajiwa kuajiriwa.
Suala la uhakiki wa vyeti lililoendeshwa na Serikali mwaka jana liliwanasa zaidi ya watumishi 19, 000 ambao ajira zao zilisitishwa, huku sekta ya afya na elimu zikiathirika zaidi.

Wahitimu Veta kupata fursa mradi bomba la mafuta Tanga


Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) linafanya utafiti wa kujua namna ya kuwatumia wanafunzi wanaohitimu katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) mkoani Tanga katika mashirika yatakayowekeza kwenye miradi mbalimbali ikiwamo bomba la mafuta, imeelezwa.
Kaimu mkuu wa Veta mkoa wa Tanga, Amenya Ntibai alitoa taarifa hiyo jana katika mahafali ya 22 ya wahitimu 246 wa fani mbalimbali katika chuo hicho yaliyofanyika jijini hapa.
Alisema kupitia utafiti huo, Veta inaamini kuwa wanafunzi wanaosoma na kuhitimu chuoni hapo watapata ajira na kuongeza ujuzi zaidi kupitia miradi hiyo ya uwekezaji.
Ntibai alisema wanafunzi wanaopita chuoni hapo wanatoka wakiwa wameiva kiufundi na wanaweza kumudu ushindani wa soko la ajira la nchi za Afrika Mashariki, hivyo hakutakuwa na haja ya wawekezaji kuleta mafundi wa fani mbalimbali kutoka nje ya nchi.
“Mbali ya kuwapika ili wajiajiri, lakini Veta tunawaandaa vijana kumudu ushindani wa soko la ajira la nchi za Afrika Mashariki na tunaamini wanatoka hapa wakiwa na ujuzi mkubwa,” alisema Ntibai.
Kaimu mkuu wa wilaya ya Tanga, Selemani Zumo aliutaka uongozi wa Veta kuweka kumbukumbu sahihi za wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mafunzo kwa vitendo katika kila fani ikiwamo kujua wapi waliko ili itakapopatikana fursa iwe rahisi kuwatafuta.
“Moja ya sifa za fundi kuchukuliwa na mradi wowote wa uwekezaji naamini itakuwa ni cheti cha Veta. Hivyo ni vyema kuwa na kumbukumbu za wanafunzi waliofanya vizuri na kujua wapi waliko, Serikali itahakikisha wanapewa kipaumbele,” alisema Zumo.
Mwanafunzi aliyehitimu mafunzo ya ufundi umeme wa magari katika chuo hicho, Yusuph Idd alisema katika miaka miwili aliyosoma amepata ujuzi utakaomuwezesha kujiajiri na kuajiri vijana wengine.
Veta mkoa wa Tanga ilianzishwa mwaka 1977 na hadi mwaka huu imeshatoa mafunzo kwa vijana 13,987.

Dk Shein: CCM ina uwezo mkubwa


Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) kina uzoefu wa kufanya mageuzi ya kifikra, itikadi, sera na mabadiliko ya kimaendeleo kwa kufuata misingi imara iliyoachwa na waasisi wa Taifa hili.
Dk Shein alisema hayo jana katika Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja uliokwenda sambamba na uchaguzi wa viongozi chama kimkoa.
Alisema CCM si chama cha mtu mmoja kama vilivyo vyama vingine vya siasa vinavyoendelea kupoteza mwelekeo na kusambaratika kwa kukosa uzoefu wa kihistoria.
Dk Shein ambaye mkoa huo ndiyo wake kichama alisema ni vyema kwa wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha viongozi watakaowachagua wanaielewa itikadi ya chama hicho na sera zake na wapo tayari kuzilinda, kuzisimamia na kuzitekeleza kwa vitendo.
Aliwataka viongozi watakaochaguliwa wawe makini, kama ilivyo kawaida kwa viongozi wa CCM.
“Chama chetu kinapendwa, kinawavutia wananchi na kina uwezo mkubwa na wa kipekee wa kurejesha na kujenga matumaini mapya kwa wanachama wake na wananchi wote hivyo hapana shaka tuna nafasi nzuri ya kuendelea kushika dola kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisisitiza Dk Shein.
Pia, alisema ushindi wa kishindo ambao CCM imeupata katika uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika Novemba 26 kwenye kata 43 nchini ni ishara kwamba ilipitisha viongozi wenye sifa, uwezo, nia njema na waliokubalika kwa wananchi kugombea nafasi hizo.
Alisema ushindi mkubwa uliopatikana katika maeneo ambayo wapinzani walidhani ni ngome yao ni uthibitisho kuwa wananchi wanaendelea kuiamini CCM.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alisema wajumbe wanapaswa kuchagua viongozi wa kukiimarisha chama hicho ili kiendelee kupata ushindi katika chaguzi zijazo.

Bibi aeleza sababu za kumfanyia ‘unyama’ mjukuu wake Moshi


Bibi wa mwanafunzi wa darasa la tano anayesoma Shule ya Msingi Kilimanjaro wilayani Moshi, Costansia Lyimo amesema si mara ya kwanza kuwaadhibu wajukuu zake.
Bibi huyo aliagiza mjukuu wake kufungwa kwenye mti na kupigwa jambo ambalo lilisababisha maumivu makali kwa mwanafunzi huyo (jina tunalihifadhi kimaadili).
Akizungumza na Mwananchi jana baada ya juzi picha kusambaa zikionyesha mwanafunzi huyo akiwa amefungwa kwenye mti, Costantina alisema amekuwa akiwaadhibu wajukuu zake kwa namna hiyo ya kufungwa kamba na kutwishwa tofali kichwani huku akiwa amefungwa miguu na kunyanyua mikono juu ili liwe fundisho.
Alisema adhabu ambayo mwanafunzi huyo alipewa juzi ni kutokana na ukorofi wake kiasi ambacho wameshindwa kuvumilia na kwamba mara kwa mara akienda kuogolea huwa anakaa kuanzia asubuhi mpaka jioni.
“Yaani huyu mtoto anaweza kuondoka nyumbani asubuhi hadi jioni ndio anaonekana, kwa kweli baada ya kaka yake kufunga shule na kurudi nyumbani nilimwomba anisaidie kumwadhibu maana ameshindikana,” alisema bibi huyo
Hata hivyo, mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Grace Mushi aliyekamatwa juzi jioni na kufikishwa katika kituo kidogo cha Polisi Majengo alisema mtoto huyo amekuwa akimsumbua kila mara kutokana na ukorofi wake.
Alisema mwanaye huyo amekuwa akimsababishia matatizo mengi (hakuyataja) kutokana na tabia chafu aliyonayo.
“Huyu mtoto anaweza kwenda Mto Karanga na kukaa huko kuanzia asubuhi hadi jioni hata shule haendi, kwa kweli huyu mtoto ananiumiza kichwa,” alisema mama huyo.
Mwanafunzi huyo, alikiri kuwa huwa anapigwa na bibi yake huyo kila mara na kudai kuwa juzi ilikuwa si mara ya kwanza kupigwa ila kipigo kilizidi siku nyingine.
“Napigwa kila mara, lakini jana (juzi) nimepigwa zaidi, siku nyingine napigwa tu kawaida,” alisema mtoto huyo.
Jirani aliyeshuhudia tukio hilo, Emmanuel Shirima alisema mtoto huyo alifungwa zaidi ya saa tano huku akiadhibiwa vibaya.
Alisema kitendo ambacho mtoto huyo anafanyiwa kila mara si kizuri hata kidogo katika jamii maana ni unyama.
Aliongeza kuwa hata kama ni adhabu asingestahili kupewa kipigo hicho kutokana na umri wake kuwa bado mdogo.
“Kitendo cha kupigwa kwa mtoto huyo tulishindwa kuvumilia ilibidi twende kutoa taarifa katika kituo kidogo cha Polisi Longuo KCMC, ndipo baada ya muda kidogo askari kutoka kituo cha polisi Majengo walikuja kumchukua mtoto huyo pamoja na mama yake,” alisema shuhuda huyo.
Hata hivyo baada ya askari kumchukua mama wa mwanafunzi huyo kumpeleka kituo cha polisi alikaa muda kidogo na kuachiwa.

Wapangaji wadai fedha zao kwa wenye nyumba zinazobomolewa Dar


Wamiliki wa nyumba zilizowekwa alama ya X kutoka Kimara hadi Ubungo wamegoma kurudisha pesa kwa wapangaji wao walioanza kuondoka kwenye nyumba hizo.
Nyumba hizo zilizowekwa alama ya X Novemba 20 mwaka huu kupisha ujenzi wa barabara ya Morogoro zitaanza kubomolewa siku nne kabla ya sikukuu ya Krismasi.
Wapangaji hao wamelalamikia gharama za usafiri huku wengine wakiwataka wenye nyumba kuwarudishia japo gharama hizo za usafiri.
Wakizungumza na Mwananchi baadhi yao walisema walilipa kodi ya miezi sita na wengine miezi 12, hivyo wanastahili kurudishiwa fedha za miezi iliyobaki.
Mkazi wa Kimara Baruti, Victoria Charles alisema ameishi katika nyumba aliyopanga kwa mwezi mmoja tu.
“Nilikuja hapa mwishoni mwa Oktoba na wakati nakuja nililipia miezi sita, haya leo nyumba inawekwa alama X najuta kwa nini nililipa kiasi hicho cha pesa nilicholipa,” alilalamika Victoria.
Alisema alijaribu kumuomba mwenye nyumba amrudishie kodi iliyobaki lakini alimwambia kuwa hali ni ngumu kwa sasa.
“Tulijaribu kumueleza kuhusu kodi zetu alisema hana, yaani hapa usafiri tu natakiwa nitoe laki na nusu,” aliongeza.
Mkazi wa Ubungo, Abbas Mustafa alisema ameamua kuhama mapema ili kuondoa usumbufu na kuepusha vitu vyake kuharibika ubomoaji utakapoanza.
“Nakumbuka wenzetu Kimara waliathirika, vitu vyao vilivunjwavunjwa na kusababisha hasara, hivyo mimi naondoka mapema,” alisema Mustafa.
Alisema muda uliopo ni mdogo kwa wao kupata vyumba hata hivyo aliongeza kuwa hali ni ngumu kifedha na mwenye nyumba hakuwaeleza chochote juu ya malipo yao.
“Hii ni kama taarifa ya kushtukiza kwetu, ukizingatia hatujamaliza hata miezi mitatu tangu tumekuja kupanga hapa, lakini hatuna jinsi tutaenda kujisitiri kwa ndugu hadi hapo tutakapo pata pesa kwa ajili ya kupanga sehemu nyingine,” aliongeza.
Pascal Lameck aliyepangisha wapangaji tisa alisema wote wamehama na kila mpangaji alihitaji kurudishiwa pesa.
Alisema wakati anapokea pesa zao hakujua kama nyumba yake ingewekwa alama ya X jambo alilodai ni uonevu.
“Kinachonikosesha raha ni wapangaji kutaka niwarudishie pesa zao, hivi kwa maisha haya ndugu mwandishi naipata wapi pesa hiyo,” alisema.
Alisema mara kadhaa alipelekwa katika ofisi za kata ili alipe kodi alizochukua pamoja na kupewa muda wa kurudisha lakini alidai hana uwezo wa kulipa.
“Hata mimi roho inaniuma sana, sipendezwi na tuhuma hizi, lakini sina jinsi kwani hapa nilipo ninakosa raha maana nilikuwa nategemea wapangaji kuendesha maisha yangu,” alisema.
“Mimi kwa kweli uwezo wa kulipa sina na ili kunusuru maisha yao waondoke tu ili mwezi ujao Tanroads wasije kuharibu mali zao,”aliongeza.
Diwani wa Kata ya Kimara, Pascal Manota alisema amekuwa akipokea kesi mbalimbali za wapangaji kudai kutapeliwa na wenye nyumba.
“Unakuta mtu anakuja hapa anasema anataka kurejeshewa pesa yake kwa kuwa nyumba aliyopanga imewekwa alama ya X,” alisema Manota.
Alisema katika vikao vyao na wananchi waliwaambia wasilipe pesa nyingi kutokana na bomoabomoa hiyo.
“Baadhi ya wenye nyumba bado wanaendelea kuchukua kodi za wapangaji ila kwa sasa tumetoa agizo kwa viongozi wa serikali za mitaa kuwa mikataba yote ya upangishaji vyumba au nyumba ipitie huko ili tuwaonyeshe wananchi maeneo sahihi ya kupanga,” aliongeza.
Bomoabomoa yazua taharuki Dodoma
Mjini Dodoma, Kampuni ya Miliki ya Raslimali za Reli (Rahco) imezua taharuki baada ya kutangaza bomoabomoa kwa wafanyabiashara zaidi ya 1,000 waliojenga majengo na vibanda vya biashara katika hifadhi ya reli.
Juzi jioni, gari la matangazo lilipita likiwatangazia wafanyabiashara hao kuwa Rahco ingeendesha bomoabomoa kuanzia saa 12:00 jana asubuhi.
Wafanyabiashara wanaotakiwa kubomoa majengo yao ni wale waliojenga kandokando ya stendi ya daladala ya Jamatini, soko la Sarafina, kituo cha mafuta, mama lishe na vibanda vya kukatia tiketi za mabasi yaendayo mikoani.
“Waliojenga eneo la hifadhi ya reli, wanaofanya biashara eneo la hifadhi ya reli waondoke kabla ya kesho (jana) sasa 12.00 asubuhi. Ikifika asubuhi hujaondoka hutaruhusiwa kuchukua kitu chochote ndani,” alisema.
Hata hivyo, baada ya matangazo hayo wafanyabiashara walijikusanya na kuwaita viongozi mbalimbali wa mkoa akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge.
Wakizungumza katika mkutano huo, wafanyabiashara hao walisema wako tayari kuondoka kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kupisha ujenzi huo, lakini wakaomba kupatiwa maeneo mbadala na muda wa kuondoka katika hilo.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Sakina Said alisema hawapingani na kauli ya Serikali juu ya kupisha maeneo hayo kwa ajili ya maendeleo ya Taifa bali wanaomba kupatiwa eneo jingine na muda wa kujiandaa kuondoka.
“Mkuu wa mkoa tunaiheshimu na kuitii Serikali yetu tukufu chini ya uongozi wa jemedari mkuu Rais Dk John Magufuli, tunachokuuomba tupatiwe muda na tuonyeshwe maeneo ambayo tutafanyia biashara zetu,” alisema.
Mfanyabiashara mwingine Jonath Jonathan alisema wengi wa wafanyabiashara wamechukua mikopo benki ambayo wanatakiwa kurejesha kwa wakati na kuomba Serikali kuwafikiria kuwapa muda na kuwatafutia eneo mbadala.
Akizungumza katika hadhara hiyo, Dk Mahenge aliwataka wafanyabiashara hao kutii amri ya kuondoka kwenye maeneo hayo ili kupisha ujenzi wa reli mpya ya kisasa.
Alisema mkandarasi ameshawekeana mkataba na Serikali na kwamba kazi ya ujenzi wa reli hiyo inatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.

Diallo akerwa Takukuru kumpekua


Mwenyekiti wa CCM mkoani Mwanza, Anthony Diallo amedai kukerwa na kitendo cha maofisa wa Takukuru kusimamisha gari lake na kulipekua, wakati alipokuwa kwenye harakati za kampeni wilayani Ukerewe.
Mfanyabiashara huyo maarufu Kanda ya Ziwa anatetea nafasi yake katika uchaguzi uliofanyika jana.
Hali hiyo, imekuja wakati uchaguzi wa viongozi wa CCM ukiwa umefikia ngazi ya mkoa huku katika baadhi ya mikoa kukiwa na malalamiko mengi ya rushwa.
Akizungumza wakati akiomba kura jana, Diallo alisema amesikitishwa na kutofurahishwa na kitendo cha maofisa hao.
“Kitendo hiki (cha gari kupekuliwa), hakikuwa cha kiungwana,” alisema Diallo ambaye anamiliki kampuni ya Sahara Media inayomiliki kituo cha televisheni na redio.
“Hata mimi najua rushwa ni adui wa haki na nimeahidi kupambana na rushwa kwa ahadi na imani ya mwana CCM.”
Mbali na kupekua gari la waziri huyo wa zamani, Takukuru iliwahoji baadhi ya wagombea na wanachama mkoani Simiyu kwa tuhuma za rushwa.
Wakati mkuu wa Takukuru mkoani Mwanza, Ernest Makale akithibitisha kupekuliwa kwa gari la Diallo, mwenzake wa Simiyu, Adili Elinipenda amesema taasisi yake inawashikilia viongozi na wanachama kadhaa kwa mahojiano.
Wakuu hao wawili wamethibitisha matukio hayo walipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana.
Kuhusu gari la Diallo kupekuliwa, Makale alisema tukio hilo lilitokea wilayani Ukerewe baada ya maofisa wa Takukuru kupata taarifa kuwa kiongozi huyo aliyekuwa wilayani humo kufanya kampeni alikuwa akijihusisha na vitendo vya rushwa.
“Hata hivyo, baada ya kulisimamisha gari yake na kufanya upekuzi, hatukukuta ushahidi wowote na kumuachia kuendelea na kampeni zake,” alisema Makale.
Diallo aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Nne, ni miongoni mwa wagombea waliopitishwa na Halmashauri Kuu kutetea nafasi yake.
Katika tukio la Simiyu, Elinipenda alisema Takukuru inaendelea kuwahoji baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM lakini hakuwa tayari kuwataja.
“Nitatoa taarifa na kutaja majina ya tunaowahoji baada ya zoezi la kuwahoji kukamilika,” alisema Elinipenda.

Nassari aeleza uvamizi ulivyofanyika kwake


Joshua Nassari, mbunge wa Arumeru Mashariki kwa tiketi ya Chadema, amesema watu wasiojulikana wamevamia nyumbani kwake na kufyatua risasi moja iliyomuua mbwa wake katika tukio ambalo amelihusisha na upinzani wa kisiasa uliotokana na uchaguzi mdogo wa madiwani.
Nassari amefafanua kuwa aliwajibu watu hao kwa kupiga risasi tano hewani, huku wenyewe wakipiga risasi kama 12 hivi, huku moja ikimpata mbwa wake.
Tukio hilo limetokea takriban miezi miwili baada ya mbunge mwingine wa Chadema, Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi akiwa ndani ya gari lililoegeshwa nje ya makazi yake mjini Dodoma.
Nassari, ambaye chama chake kinaongoza kwa idadi ya madiwani jimboni mwake, amesema anahisi shambulio hilo lilifanywa na watu ambao wamekuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu.
“Kwa sababu kwa muda wa zaidi ya siku nne sikuwepo nyumbani na baada ya kurejea ndipo tukio hilo likatokea,” alisema Nassari.
Alisema, juzi alifika nyumbani kwake majira ya saa 5:00 usiku akitokea katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya vijana wa nchi za Afrika Mashariki zililofanyika kwenye taasisi ya MS TCDC iliyopo Usa River. “Nataka niamini taarifa nilizopewa kuwa nimekuwa nikifuatiliwa hata kabla ya uchaguzi mdogo kwa lengo la kunidhuru,” alisema Nassari.
“Kwa sababu mimi si mfanyabiashara (hivyo) hawana cha kuiba, zaidi ni sababu za kisiasa tu na Mungu amenisaidia sana.”
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema waliona kwenye mtandao wakawa wanamtafuta Nassari kwa kuwa baada ya tukio alitakiwa kwenda kuripoti polisi na ameshafanya hivyo.
Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo. Polisi walifika nyumbani kwa Nassari jana baada ya kuripoti tukio hilo akiwa na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Nassari hakueleza sababu za watu hao kumfuatilia na kutaka kumdhuru kutokana na uchaguzi mdogo wa madiwani ambao chama chake kilijitoa.
Hata hivyo, mbunge huyo alitoa tuhuma za madiwani waliokuwa wa Chadema kuhongwa fedha na kuahidiwa mafao yao iwapo wangehamia CCM.
Baada ya madiwani hao kuhamia CCM, Nassari aliwaonyesha waandishi wa habari video za jinsi kiongozi wa wilaya alivyowashawishi na kuwaahidi fedha. Tayari Nassari amewasilisha video hizo Takukuru.
Nassari alisema jana kuwa tangu awasilishe vielelezo vya ushahidi Takukuru, maisha yake yamekuwa hatarini.
Akizungumzia tukio la juzi usiku, Nassari alisema baada ya kufika nyumbani, takriban nusu saa baadaye alisikia hali isiyo ya kawaida ndani ya uzio wa nyumba yake na baadaye kusikia milio ya risasi kisha mbwa wake kunyamaza, hali iliyomfanya achukue silaha yake kujihami.
“Baada ya kusikia milio ya risasi, nikajua niko kwenye hatari nikafungua mlango wa nyuma nikaanza kurusha risasi kuelekea walipo,” alisema.
“Nilipiga risasi tano, wenyewe nadhani zimefika 12 kisha kukawa kimya nikaenda kuwaamsha vijana wanaonisaidia hapa nyumbani kuwaeleza tukio lililotokea kisha nikaondoka.”
Alisema alitaka kutoa taarifa polisi usiku huo, lakini baadaye akasita kutokana na kuwa na wasiwasi wa usalama wake kwa kuhofia wangemvamia akiwa njiani.
Alisema waliotekeleza tukio hilo hawakujua kama ana silaha kwa sababu mwaka 2014 wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa silaha yake aina ya bastola ilichukuliwa na polisi na hadi leo hajarudishiwa, hivyo kuwa na silaha nyingine kulimsaidia kujibu mapigo.
Mfanyakazi wake, Geofrey Joshua alisema alisikia milio ya risasi, lakini hawakuweza kutoka kwa sababu hakuwa na silaha na baada ya muda Nassari alitoka na kuwaelezea tukio zima kisha wakamuona mbwa mmoja kati ya wawili akiwa amekufa kwa kupigwa risasi.
Kaimu katibu wa Chadema wa mkoa, Elisa Mungure alisema tukio la kuvamiwa nyumbani kwa Nassari ni mwendelezo wa vitisho kabla na baada ya uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika jumapili iliyopita.
Mkazi wa eneo hilo, Dominick Mungure alisema tangu Novemba 25 mwaka huu siku moja kabla ya uchaguzi wa marudio hali ya usalama imekuwa tete huku baadhi ya watu wakishambuliwa na hakuna hatua zilizochukuliwa licha ya taarifa kutolewa na wahusika kutajwa.
“Hatujui hatma yetu kwa ujumla, hofu imetanda kwa kila mwananchi fikiria kama mbunge anaweza kuvamiwa hivi sisi wananchi itakuaje,” alisema Mungure.

Dk Mahanga aeleza kushawishiwa kurejea CCM


Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, katika Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Makongoro Mahanga ambaye ni mwanachama wa Chadema amedai kuwashawishiwa kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM).
Dk Mahanga alihama CCM Agosti 2,2015 baada ya kushindwa katika kura ya maoni kwa nafasi ya ubunge jimbo la Segerea.
Mbunge huyo wa zamani wa Segerea alijitoa CCM akisema ni kwa sababu utaratibu uliotumika haukuwa sahihi na uligubikwa na vitendo vya rushwa na njama zilizofanywa na viongozi wa kitaifa wa chama hicho tawala.
Akizungumza na MCL Digital leo Jumapili Desemba 3,2017 Dk Makongoro amesema mara kwa mara amekuwa akifuatwa na watu tofauti wakiwamo ndugu zake wakimshawishi arejee kwenye chama hicho tawala.
Amesema, “Nawaambia hivi sirudi huko. Huwa nina ishi kwa ninachokiamini  na hakuna kinachoweza kunishawishi kubadili imani na dhamira yangu ya Agosti 2 mwaka 2015.”
Awali, kupitia akaunti ya mtandao wa kijamii wa Facebook Dk Mahanga aliwataka wahusika kuacha kuwatuma rafiki zake na ndugu zake ili kumshawishi kurejea CCM.
“Imani yangu, utu wangu na msimamo wangu huwa hauna bei. Kamwe sitorudi CCM acheni kuhangaika,” amesema Dk Mahanga katika ukurasa huo.