Katibu
Mkuu Kiongozi wa Serekali ya Mapinduzi Zanzibar Dk. Abdulhamid Yahya
Mzee, akionesha ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa kuzama kwa Meli ya MV
Skagit katika bahari ya Zanzibar ikitokea Dar-es- Salaam, ripoti hiyo
tayari imeshakabidhiwa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu Zanzibar. Katibu Mkuu Kiongozi
amesema ripoti hiyo itakuwa katika Makumbusho ya Nyaraka za Kale
Kilimani.
Na RAMADHANI ALI-HABARI MAELEZO
Tume
iliyoundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
kuchunguza ajali ya meli ya MV. Skagit iliyotokea tarehe 18.7.2012
ilipokuwa ikitokea Dare s Salaam kwenda Zanzibar imependekeza
kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu watu saba kwa makosa mbali
mbali yaliyochangia kutokea kwa ajali hiyo ili kuhakikisha kunakuwepo
uwajibikaji kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wa baharini na watendaji
wa Taasisi zinazosimamia suala hilo na kuepusha ajali za mara kwa mara.
Akitoa
taarifa ya Tume hiyo kwa Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara ya
Habari Maelezo Mnazimmoja, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu
Kiongozi Abdulhamid Yahya Mzee amewataja watu waliopendekezwa
kuchukuliwa hatua za kisheria ni mmiliki wa MV.Skagit ambaye ni
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Seagull Sea Transport Said Abdul-rahman
Juma, Nahodha wa meli hiyo Makame Mussa Makame na Meneja wa Kampuni hiyo
tawi la Dar es salaam Omar Hassan Mkonje.
Amesema
kutokana na matendo yao ya kuwa karibu mno na sababu zilizopelekea
kutokea kwa ajali hiyo, Tume imependekeza watu hao washtakiwe kwa kosa
la kusababisha vifo kutokana na uzembe.
Mmiliki
wa kampuni hiyo amefanya kosa la kufanya biashara ya usafiri wa
baharini kwa kutumia chombo ambacho hakikusajiliwa kwa mujibu wa sheria
na kutumia chombo ambacho hakikutimiza masharti ya ukaguzi kwa mujibu wa
sheria ya usafiri wa baharini Zanzibar namba 5 ya mwaka 2006, kumuajiri
nahodha bila ya kuwa na cheti cha umahiri cha daraja la tano na
kuruhusu meli kupakia idadi kubwa ya abiria kinyume na uwezo wake.
Abdulhamid
amesema taarifa hiyo imesema Nahodha Makame Mussa ametenda kosa la
kuendesha meli akiwa hana cheti, kushindwa kuwaandaa abiria kujiokoa
wala kutoa taarifa ya dharura, kuendesha meli hali ya kuwa si salama na
kuruhusu kupakia abiria 431 badala ya 250 iliyoainishwa kwenye cheti cha
abiria.
Watu
waliopendekezwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ni aliekuwa Mkaguzi wa
meli na Kaimu Mrajisi wa meli kutoka Mamlaka ya usafiri wa baharini
Zanzibar Juma Seif Juma, Mkaguzi wa kujitegemea Capt. Saad Shafi Adam na
Maafisa wa usalama wa bandari ya Dar es Salaam Johari Mikidadi
Ndumbati na Peter Ndimbwa Mwasi kwa kushindwa kudhibiti uingizaji wa
abiria katika meli ya MV. Skagit siku iliyopata ajali ikiwa ni kinyume
na majukumu yao ya kazi.
Taarifa
hiyo imetoa mapendekezo ya kuimarisha Sheria na kanuni za usafiri wa
baharini namba 5 ya 2006 kwa kuvifanyia marekebisho baadhi ya vifungu
ikiwemo kuweka utaratibu wa kisheria utakaowalazimisha wafanyabiashara
wa usafiri wa baharini kuwa na utaratibu wa kuuza tiket za safari pamoja
na kutengeneza urodha ya wasafiri kwa njia ya electroniki na kuweka
utaratibu wa kisheria unaowalazimisha uongozi wa kampuni unaoendesha
biashara ya usafiri wa baharini kuwa na taaluma ya masuala ya usafiri wa
baharini.
Aidha
Abdulhamid amesema Tume hiyo imependekeza Kampuni kuwalipa fidia abiria
wote waliokuwemo ndani ya meli. Kwa waliofariki walipwe thamani ya
kiwango cha mshahara wa chini cha muda wa miezi 80 na walionusurika na
kupata ulemavu walipwe asilima 75 ya kiwango cha waliofariki na watu
wengine walionusurika bila ya kupata majeraha yoyote walipwe asilimia 50
ya kiwango walicholipwa waliofariki.
Katika
ajali hiyo watu 81 wakiwemo raia watatu wa kigeni walifariki na maiti
zao zilipatikana na kuzikwa, 212 walipotea na 154 waliokolewa wakiwa
hai wakiwemo raia 15 wa kigeni.
Katibu
Mkuu Kiongozi amesema Tume imeeleza sababu za kutokea ajali hiyo kuwa
ni upepo mkali, muundo wa meli ilioruhusu abiria wengi kukaa juu, mwendo
wa kasi, nahodha kukosa ujuzi na umahiri na abiria kuwa wengi kupita
kiwango chake.
Amesema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekubaliana na mapendekezo yote
yaliyotolewa na Tume hiyo iliyokuwa na wajumbe 10 chini ya mwenyekiti
wake Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Abdulhakim Ameir Issa.