Wednesday, August 23

DKT. KALEMANI AITAKA TANESCO KUUNGANISHA NGUVU KUKAMILISHA MIRADI YA UMEME YA KURASINI NA KIMBIJI

NA K-VIS BLOG/Khalfan Said

NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani,(pichani anayeongea), amelitaka Shirika la Umeme Tanzania TANESCO kuunganisha nguvu ili kuhakikisha wanakamilisha mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza na kusamabaza umeme kinachotarajiwa kujengwa huko Kimbiji wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kalemani ametoa maelekezo hayo leo Agosti 22, 2017, wakati alipofanya ziara kukagua miradi ya umeme kwenye kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Kurasini, Kigamboni na eneo panapotarajiwa kujengwa kituo kingine cha kupoza na kusambaza umeme huko Kimbiji wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam.

“Hakikisheni mradi wa uejenzi wa kituo hiki cha Kimbiji unakamilika ifikapo Machi 30, mwakani,(2018), na kuwaondolea adha ya upatikanaji wa umeme wananchi wa Kigamboni, chukueni mafundi waliokamilisha kazi ya kujenga kituo cha umeme kule Mtwara waje hapa, muwaache wale wanaojenga transition (njia ya kusafirisha umeme) wajenge, lakini wale mafundi wengine waleteni hapa ili mradi huu ukamilike.” Alifafanua.
 
Akiwa kwenye kituo cha kupoza na kusamabza umeme cha Kurasini jijini Dar es Salaam, Dkt. Kalemani aliipongeza TANESCO kwa juhudi kubwa walizofanya kwa hatua ujenzi waliyofikia ambapo sasa wameanza kufunga mashine kubwa. Kituo cha Kurasini ndicho kinachotegemewa sana na watu wa Mbagala, Kurasini na Kigamboni.

Ongezeko la haraka la wakazi kwenye maeneo ya Mbagala, na Kigamboni kumepelekea uhitaji mkubwa wa umeme ambapo umeme unaopatikana kwa sasa umekuwa haukidhi mahitaji ya wakazi wa maeneo hayo.

“Naomba niwaambie, mradi huu umechelewa sana, hivyo basi ongezeni kasi ili ifikapo Agosti 30, mwaka huu, mradi ukamilike nataka watu wa Mbagala, watu wa Kurasini, na watu wa Kigamboni wanaondokana na kero hii ya umeme, na mimi nitawaambia washeshimiwa wabunge wa Kigamboni Mheshimiwa Ndungulile (Dkt. Faustin Ndungulile) na Mheshimiwa Mangungu (Murtaza Magungu) Mbunge wa Mbagala kuhusu habari hii ili wawaambie wananchi wa maeneo haya wawe wavumilivu kwani mradi huu sasa utakamilika.” Alisema.

Dkt. Kalemani pia aliwaagiza viongozi wa TANESCO, kuhakikisha wanakusanya nguvu kwa maana ya vifaa kutoka ofisi zote za TANESCO mkoa wa Dar es Salaam, ili kuhakikisha wananchi wote wa Kigamboni wanaofikia 350 waliolipia ada za kuunganishiwa umeme wawe wamepelekewe umeme ifikapo mwisho wa mwezi huu wa Agosti.Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka, aliwaambia waandishi wa habari kuwa maelekezo ya Mheshimiwa Naibu waziri yatafanyiwa kazi kwa haraka ili kuhakikisha kero hiyo inaondoka.
 
Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia miradi, Mhandisi Khalid James,(kulia), akimpatia maelezo Naibu waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme Kurasin jijini Dar es Salaam. 

Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia miradi, Mhandisi Khalid James,(kulia), akimpatia maelezo Naibu waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme Kurasin jijini Dar es Salaam.
 
Dkt. Kalemani (katikati), akitoa maagizo kwa wakandarasi wanaotekeleza mradi huo wa Kurasini. 
 
Meneja Mwandamizi wa TANESCO Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Mhandisi Mahende Mgaya, (watatu kushoto), akimpatia maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa kituo cha umeme cha Kigamboni, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, (wapili kushoto).
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka, (kulia), akiwa na Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO anayeshughulikia miradi, Mhandisi Khalid James, (kushoto), akiongea na waandishi wa habari.



Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Mhandisi Jahulula akifafanua baadhi ya mambo kwenye eneo ambalo patajengwa kituo cha kupoza na kusambaza umeme huko Kimbiji, Kigamboni jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani.
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Mhandisi Jahulula, (wapili kulia), akifafanua baadhi ya mambo kwenye eneo ambalo patajengwa kituo cha kupoza na kusambaza umeme huko Kimbiji, Kigamboni jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani(katikati).

Fundi wa TANESCO akiwa kazini pale Kigamboni

Mhandisi Jahulula, (kushoto), akionyesha mahala mpaka wa eneo hilo la mradi unapoishia. 

Dkt. Kalemani (katikati), na viongozi wa TANESCO wakiwa kwenye eneo hilo la Kimbiji

Nyumba ya Lissu kupekuliwa tena


Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema polisi wamemchukua mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu na kwenda naye nyumbani kwake kwa ajili ya kumpekua.
Msafara wa magari ya maofisa wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam umeongozana na Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki na mawakili wake.
"Wamemchukua hapo kituoni na kuelekea naye hadi nyumbani, lengo ni kumkagua.Mawakili wanaomsaidia Lissu wameshaondoka muda huu ili kujua ni kitu gani atapekuliwa," amesema Mrema.
Kaimu Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum Lucas Mkondya alipotakiwa kuzungumzia taarifa hizo alikata simu baada ya kuulizwa kuhusu upekuzi huo.
Jana  Agosti 22,Lissu alinyimwa dhamana baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kumkashifu Rais John  Magufuli na uchochezi.
Hii ni mara ya pili maofisa wa Jeshi la Polisi kwenda kumpekua Lissu nyumbani kwake ikiwa ni ndani ya wiki kadhaa.
Julai 21, mwaka huu Chadema inasema Polisi ilimpekua Lissu nyumbani kwake na kuchukua CD 6 zinazohusiana na utafiti alioufanya mwaka 1999 katika sakata la mgodi wa Bulyanhulu.

JAPAN YAISAIDIA TANZANIA SHILINGI TRILIONI 74 KUTEKELEZA MIRADI KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MITANO



Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan –JICA, Bw. Shinichi Kitaoka (kushoto), akielezea namna Shirika lake lilivyojipanga kuendeleza ushirikiano na Tanzania alipokutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri wa Fedha na Mipango. Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), (wa kwanza kulia), Jijini Dar es Salaam.



Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango. Bi. Amina Khamis Shaaban (kushoto), akisikiliza kwa makini mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Mipango. Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) na Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan –JICA, Bw. Shinichi Kitaoka, (hawapo pichani), walipokutana Jijini Dar es Salaam.



Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango. Dkt. Dkt. Khatibu Kazungu (kulia), na James Andindilile (kutoka Wizara ya Nishati na Madini) wakisikiliza kwa makini mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Mipango. Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) na Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan –JICA, Bw. Shinichi Kitaoka, (hawapo pichani), walipokutana Jijini Dar es Salaam.



Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Shogholo Msangi na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara hiyo Bi. Susana Mkapa, wakiangalia moja ya nyaraka zilizowekwa mezani wakati wa mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan-JICA, Bw. Shinichi Kitaoka, Jijini Dar es Salaam.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (BU), Prof. Adolf Mkenda (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt, Khatibu Kazungu, wakisikiliza kwa makini mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) na Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan-JICA, Bw. Shinichi Kitaoka, Jijini Dar es Salaam.



Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake, Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan-JICA, Bw. Shinichi Kitaoka (wa tatu kulia), baada ya kumaliza mazungumzo yao kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika hilo, Jijini Dar es Salaam.



Balozi wa Japan nchini Tanzania, Bw. Masaharu Yoshida (kulia) akieleza jambo nje ya viunga vya Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa mazungungo kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan-JICA Bw. Shinichi Kitaoka.

Benny Mwaipaja, WFM-Dar es Salaam

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amelishukuru Shirika la Maendeleo la Japan-JICA, kwa uwekezaji mkubwa uliofikia kiasi cha Shilingi trilioni 74.93 katika miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Dkt. Mpango ametoa shukrani hizo Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika hilo, aliyepo katika ziara ya kikazi hapa nchini, Bw. Shinichi.

Kiasi hicho cha fedha kinahusisha ruzuku asilimia 76.0, mikopo yenye masharti nafuu asilimia 3.8 na usaidizi wa kiufundi asilimia 20.1.

Amemwomba Rais huyo wa JICA, kuongeza ufadhili kwenye miradi ya nishati ya umeme, miundombinu, afya, kilimo na uvuvi kusaidia kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kukuza uchumi wa viwanda.


“Sekta ya viwanda haiwezi kuendelea kama hakutakuwa na uwekezaji mkubwa kwa upande wa nishati ya umeme pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara” alisisitiza Dkt. Mpango.

Amesisitiza pia umuhimu wa Shirika hilo kuisaidia Tanzania kuboresha sekta ya afya kwa kujenga Hospitali zitakazo hudumia magonjwa makubwa kama ya moyo na mengine mengi pamoja na kuweka vifaa vya kisasa kwa kuwa Japan inafanya vizuri katika masuala hayo.

“Eneo lingine tunaloona ni muhimu ni kusaidia kutoa ufadhili wa masomo ya ujuzi wa aina mbalimbali kwa vijana wetu ili waweze kusaidia nchi katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi” aliongeza Dkt. Mpango.

Kwa upande wake, Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan-JICA, Bw. Shinichi Kitaoka, ameahidi kuwa shirika lake litaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutatua changamoto zinazokwaza maendeleo yake.

Amesema kuwa pamoja na kuendelea kusaidia ujenzi wa miundombinu, Shirika lake litaangalia namna ya kusaidia Sekta ya afya kwa kuboresha lishe kwa watoto ili kujenga kizazi imara na chenye nguvu.

Bw. Shinichi Kitaoka ameahidi kwenda kuwahamasisha wawekezaji mbalimbali kutoka nchini mwake kuja kuwekeza Tanzania kwa kuwa kuna fursa nyingi za kiuchumi.

Japan, kupitia Shirika lake la Maendeleo-JICA, inatarajia kutekeleza miradi mipya maendeleo hapa nchini ukiwemo awamu ya pili ya ujenzi wa barabara kutoka Moroco hadi Mwenge Jijini Dar es Salaam, utakayogharimu shilingi bilioni 1.38, ambao mkataba wake utasainiwa majuma mawili yajayo.

Mradi mwingine ni upanuzi na uboreshaji wa barabara ya kuanzia makutano ya eneo la Kamata na barabara ya Kilwa, unaotarajiwa kuanza wakati wowote baada ya masuala ya changamoto za kiufundi kukamilika, utakao gharimu shilingi bilioni 24.2.

Aidha, Japan, imefadhili mradi wa ujenzi wa Barabara ya Arusha hadi Holili utakaogharimu Dola milioni 269.8 utakapo kamilika huku mradi mwingine unaoendelea ni ule wa ujenzi wa barabara za juu katika eneo la TAZARA, Jijini Dar es Salaam.

Kuhusu biashara kati ya Tanzania na Japani, imeendelea kuimarika ambapo kati ya mwaka 2015/2016 nchi hiyo imeingiza bidhaa nchini zenye thamani ya Dola milioni 363.0 hadi kufikia Dola milioni 371, sawa na ongezeko la asilimia 2.2

Katika kipindi hicho Tanzania haikufanya vizuri ambapo kiwango cha mauzo ya bidhaa nje ya nchi kilishuka kutoka Dola za Marekani milioni 229.7 hadi Dola milioni 138.5 sawa na asilimia 39.7 hali iliyosababishwa na ushindani mdogo wa wazalishaji wa Tanzania ikilinganishwa na wenzao wa Japani.

SERIKALI KUONDOA KABISA MFUMO WA ZAMANI WA MALIPO YA KODI YA ARDHI NCHI NZIMA



Maafisa kutoka Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa wakijifunza jinsi ya kutumia Mfumo wa GePG katika malipo ya Kodi ya aedhi.

Na. Hassan Mabuye
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikishirikiana na Wizara ya Fedha, imesambaza maafisa wake katika halmashauri 169 kote nchini.

Maafisa hawa wanaotoa mafunzo katika vituo vyote vya makusanyo ya kodi ya ardhi na tozo nyingine kwa kutumia simu ya mkononi ili kuondoa kabisa mfumo wa zamani wa malipo.

Zaidi ya maafisa 170 kutoka makao makuu ya Wizara ya Ardhi, Wizara ya Fedha na kutoka kanda nane za ardhi wameanza kutoa elimu hiyo katika halmashauri na vituo vyote vya makusanyo ya kodi ya ardhi ili kurahisisha ulipaji kodi ya ardhi kwa wananchi kwa kutumia simu zao na kuondoa usumbufu.

Mfumo wa ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa njia ya simu ya mkononi ni mfumo wa kielektroniki wa Government electronic Payment Gateway (GePG) katika makusanyo ya kodi ya pango la ardhi ambao utamrahisishia mwananchi kulipia popote walipo kwa kutumia simu zao kwa urahisi zaidi.



Afisa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bwana Haruna Kiyungi akitoa mafunzo kwa maafisa Ardhi Manispaa ya Nyamagana jinsi ya kutumia Mfumo wa ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa njia ya simu ya mkononi/kielektroniki.

Mwananchi yeyote anayemiliki kiwanja au shamba lililopimwa na kupatiwa hati, ataweza kutumia simu yake ya mkononi kujua kiasi cha kodi ya pango la ardhi anachodaiwa na kukulipa kwa kutumia simu yake ya mkononi.

Ili kujua unadaiwa kiasi gani cha kodi ya pango la ardhi kwa kutumia simu ya mkononi bonyeza *152*00# au kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi yaani sms halafu unatuma kwenda namba 15200 na baada hapo unaweza kulipia kwa njia ya Mpesa, Tigo Pesa au kulipia tawi lolote la benki ya NMB na CRDB.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza rasmi kutumia mfumo huu wa kielektroniki wa GePG katika makusanyo ya kodi ya pango la ardhi pamoja na tozo nyingine zinazotokana na sekta ya ardhi nchini na kuondoa kabisa mfumo wa zamani.

Mfumo huu utamrahisishia mwananchi kulipa kodi ya pango la ardhi popote alipo, ikiwa ni pamoja na kulipia tozo nyingine mbalimbali za sekta ya ardhi. Mmiliki wa kipande cha ardhi ataweza kujua anadaiwa kiasi gani cha kodi ya pango la ardhi na kulipia popote alipo bila kusumbuka kufuata huduma hizo katika vituo vya makusanyo.



Maafisa Ardhi kutoka Manispaa ya Nyamagana, Mwanza wakifuatilia kwa makini jinsi ya kutumia Mfumo wa ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa njia ya simu ya mkononi/kielektroniki.

Kwa majaribio ya ukusanyaji kodi ya pango la ardhi kwa kutumia mfumo wa kielektroniki yalifanywa katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na baada ya mafanikio makubwa kuonekana elimu ikatolewa kwa watendaji wote wa sekta ya ardhi katika Halmashauri zote za mkoa wa Dar es salaam kabla ya zoezi hilo kuhamishiwa mikoani.

Kwa zile huduma nyingine za sekta ya ardhi ambazo zinahusisha malipo kama vile upekuzi katika daftari la msajili (official search), mwananchi atapaswa kutembelea ofisi za Wizara ya ardhi zilizo katika eneo lake na kupatiwa makadirio ya kulipia huduma husika pamoja na namba ya malipo itakayomuwezesha kulipia aidha kwa njia ya benki au simu ya mkononi.

Kwa sasa kikosi kazi kinachotoa mafunzo juu ya matumizi ya mfumo huu kimeshaanza kuelemisha mikoa mingine baada ya kupata mafanikio mazuri katika mkoa wa Dar es Salaam. Lengo kubwa la kutumia mfumo huu ni kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali pamoja na kurahisisha ulipaji kodi ya pango la ardhi nchini.

RAZA AMWAGA ZAWADI MICHEZO YA MASKULI MIKOA


Mkurugenzi Idara ya Michezo na Utamaduni katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Hassan Khairalla Tawakal, akimtambulisha Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi wa wizara hiyo Omar Ali Bhai kwa Mwenyekiti wa kampuni ya ZAT Mhe. Mohammedraza Hassanali.
Mwenyekiti wa ZAT ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mhe. Mohammedraza Hassanali akimkabidhi kalkuleta Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Omar Ali Bhai kwa ajili ya washindi wa mashindano ya mpira wa miguu kwa skuli za mikoa yote ya Unguja na Pemba inayotarajiwa kuanza Septemba 12, 2017 katika uwanja wa Amaan Mjni Unguja. 
Mkurugenzi Idara ya Michezo na Utamaduni Hassan Khairalla Tawakal akitoa shukurani kwa Mhe. Raza kwa msaada alioutoa kuwazawadia washindi wa michuano ya mpira wa miguu kwa skuli za mikoa ya Zanzibar itakayofanyika mwezi ujao mjini Zanzibar.Picha na Makame Mshenga.

Na Salum Vuai, MAELEZO

MKURUGENZI wa kampuni ya usafiri wa anga na huduma za viwanja vya ndege Zanzibar (ZAT) Mohammedraza Hassanali, ametoa wito kwa kampuni na taasisi mbalimbali kuunga mkono juhudi za serikali kuimarisha michezo maskulini.

Akizungungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vitu mbalimbali kwa ajili ya zawadi za washindi kwenye mashindano ya mpira wa miguu mikoa ya Unguja na Pemba iliyofanyika nyumbani kwake Kibweni, Raza alisema ni wajibu wa kila Mzanzibari kusaidia sekta ya michezo.

Alifahamisha kuwa, iwapo wafanyabiashara wa Zanzibar wataunganisha nguvu kwa lengo la kuinua michezo kuanzia ngazi ya skuli ambako ndiko kwenye msingi wa vipaji vizuri, nchi hii itafika mbali kimichezo na kulitangaza vyema jina la Zanzibar. 

“Hii ninchi yetu sote, tuna wajibu kusaidia juhudi za serikali, na nimpongeze Mhe. Rais kwa kuteua Mkurugenzi makini na mwenye jitihada kuongoza Idara ya Michezo na Utamaduni,” alieleza Raza.

Raza ambaye pia ni Mwakilishi wa jimbo la Uzini, alisema hatachoka kutoa msukumo katika sekta ya michezo na misaada mingine ya kijamii, na vitu hivyo alivyotoa ni kutimiza ahadi yake aliyoitoa kabla mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi huyo alikabidhi vityu mbalimbali kwa Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Omar Ali Bai kwa ajili ya zawadi za washindi na washirikiwenmgine wa mashndano hayo yaliyopangwa kuanza Septemba 12, 2017 katika uwanja wa Amaan.

Mkurugenzi Bai aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa wizara yake Bi. Khadija Bakari Juma, akimshukuru Mhe. Raza, alisema kuwekeza katika michezo maskulini ni jambo muhimu kwa kuinua ufahamu wa wanafunzi masomoni.

Alisema dhana za watu wanaodhani mchezo inarejesha nyuma maendeleo ya masomo sio sahihi, kwani ushahidi duniani unaonesha wanafunzi wengine mahodari wamekuwa wakijikita kucheza michezo mbalimbali.

“Akili nzuri hutoka kwenye mwili wenye afya ambao kujengeka kwake kunatokana na mtu kujishughulisha katika michezo ambayo wataalamu wanasema ni sehemu bora kwa makuzi ya watoto”, alieleza.

Alimuahidi mfadhili huyo kwamba vitu vyote alivyovitoa vitafika kwa walengwa, huku akiwaomba wananchi wengine wenye uwezo, makampuni na wafanyabsiahara mbalimbali kushirikiana ili Zanzibar irejeshe hadhi yake michezoni ambayo kwa miaka ya karibuni imeonekana kutetereka.

Mapema, Mkurugenzi wa Idara ya Michezo na Utamaduni katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, alimshukuru Raza kwa moyo wake wa uzalendo, na kuwa tayari kutumia mali zake katika kujenga ustawi wa nchi.

Alisema kuwa Rais Dk. Shein amepania kwa dhati kuendeleza michezo kama anavyofanya katika mambo mengine, na akamsifu Raza kwa kuwa kiungo kizuri kati ya idara yake wanafunzi na watu wengine katika kuhakikisha michezo nchini inapiga hatua. 

Katika hafla hiyo, Raza alikabidhi kalkuleta za kisasa, madishi ya kuhifadhia chakula na kalamu huku akiahidi kufanya mambo mengine makubwa kwa ajili ya kuwashajiisha washiriki wa mashindano hayo ya mikoa sita ya Unguja na Pemba.

DKT. PALLANGYO AONGOZA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI ZIARA KATIKA MIRADI YA GESI LINDI


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (katikati) akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, mara baada ya kuwasili katika eneo la Kiwanda cha Kuzalisha vigae (tiles) cha Goodwill Ceramic kilichopo Mkuranga kwa ajili ya kuanza ziara hiyo
Msimamizi wa Uzalishaji na Ujenzi katika Kiwanda cha Kuzalisha vigae (tiles) cha Goodwill Ceramic kilichopo Mkuranga mkoani Pwani, Said Ngongoki akielezea jinsi uzalishaji unavyofanyika kiwandani hapo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (katikati) pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti mara walipofanya ziara kiwandani hapo
Meneja Rasilimaliwatu kutoka katika Kiwanda cha Kuzalisha vigae (tiles) cha Goodwill Ceramic kilichopo Mkuranga mkoani Pwani, Msafiri Figa ( wa kwanza kulia) akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti katika eneo la uzalishaji la kiwanda hicho.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (katikati) akibadilishana mawazo na mwakilishi kutoka Idara ya Biashara katika Kiwanda cha Kuzalisha vigae (tiles) cha Goodwill Ceramic kilichopo Mkuranga mkoani Pwani, Emily Wu (kulia) katika eneo la uzalishaji la kiwanda hicho.
Mtaalam kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Dominick Ngunyali (kulia) akitoa ufafanuzi juu ya jinsi gesi inavyopokelewa katika Kiwanda cha Kuzalisha vigae (tiles) cha Goodwill Ceramic kilichopo Mkuranga mkoani Pwani kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti katika eneo la kupokelea gesi hiyo
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (mbele kulia) akiongoza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwenye ziara katika eneo la Kiwanda cha Kuzalisha vigae (tiles) cha Goodwill Ceramic kilichopo Mkuranga mkoani Pwani.
Meneja Rasilimaliwatu kutoka katika Kiwanda cha Kuzalisha vigae (tiles) cha Goodwill Ceramic kilichopo Mkuranga mkoani Pwani, Msafiri Figa (kushoto) akielezea jinsi udongo wa aina mbalimbali unavyochanganywa katika hatua za awali za maandalizi ya utengenezaji wa vigae (tiles) kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia) akitoa maelekezo kwa Mhandisi wa Mitambo katika Kituo za Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Gesi cha Somangafungu kilichopo mkoani Lindi, Edwin Konyani katika ziara hiyo.
Msimamizi wa Bomba la Gesi Upande wa Umeme katika Kituo cha Kupokea Gesi kutoka Songosongo na Madimba Joseph Msafiri (katikati) akielezea jinsi  gesi inavyopokelewa katika kituo hicho kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti katika ziara hiyo.
Sehemu ya Kituo cha Kupokea Gesi kutoka Songosongo na Madimba kilichopo Somangafungu mkoani Lindi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo ameongoza Kamati y Kudumu ya Bunge ya Bajeti katika maeneo mbalimbali yenye miradi ya gesi katika mkoa wa Lindi lengo likiwa ni kuona utekelezaji wa miradi hiyo. 

Kati ya maeneo waliyotembelea ni pamoja na Kiwanda cha Kuzalisha vigae (tiles) cha Goodwill Ceramic kilichopo Mkuranga mkoani Pwani, Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa kutumia Gesi Asilia cha Somangafungu, Makutano ya Bomba la Gesi Asilia (Somangafungu) mkoani Lindi pamoja na eneo linalotarajiwa kujengwa Mitambo ya Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) lililoko katika Manispaa ya Lindi.

MAHUJAJI WA TANZANIA WAANZA KUWASILI SAUDI ARABIA

Na Mwandishi Maalum, Riyadh, Saudi Arabia.
Mahujaji kutoka Tanzania wameanza kuwasili nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kutekeleza nguzo ya tano ya dini ya kiislamu ya kuhiji Makkah inayofanywa na watu mbalimbali duniani, wakiwamo Waislamu kutoka Tanzania.



Baadhi ya mahujaji wakionekana Uwanja wa Ndege baada ya kuwasili nchini Saudi Arabia kwa ajili ya swala ya Hija.



Mahujaji kutoka Tanzania wakiwa wamewasili nchini Saudi Arabia.



Baadhi ya Waislamu wanaoendelea kuwasili nchini hapa wakionekana pichani.



Ibada ya Hijja mwaka huu inatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Agosti hadi mwanzoni mwa mwezi Septemba, huku jumla ya mahujaji 977 kutoka Tanzania wameshawasili katika miji ya Madina na Jeddah. Mahujaji hao waliwasili katika viwanja vya ndege vya Madina na Jeddah na kupokelewa na maafisa wa Ubalozi wa Tanzania.

Tanzania kwa mwaka huu inataraijiwa kupeleka mahujaji wapatao 2,700. Indonesia ndiyo nchi inayoongoza kwa kupeleka mahujaji wengi mwaka huu inatarajiwa kuwa na mahujaji wapatao 168,000. Mwaka huu Saudi Arabia inatarajiwa kupokea mahujaji zaidi ya 2,000,000 kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni.