Wizara ya Fedha na Mipango imetiliana saini na Kampuni ya ujenzi wa barabara ya Reynolds kandarasi ya ujenzi wa barabara ya kutoka Kidatu hadi Ifakara mkoani Morogoro, yenye urefu wa kilometa 67 kwa kiwango cha lami utakaojengwa kwa shilingi bilioni 101, kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya, Marekani na Uingereza.
Mkataba huo umesainiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Shaaban kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Bw. Dan Yzhak Shahn, Bw. Benjamin Arbit ambaye ni Mkandarasi kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Reynolds.
Kiasi hicho cha fedha ni sawa na Euro milioni 40.4 ambapo Euro milioni 29.6 zimetolewa kwa ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na Shirika la Misaada la Uingereza-UK-AID, huku kiasi kinachobaki cha Euro milioni 10.8 kikitolewa na Shirika la Misaada la watu wa Marekani- USAID.
Akizungumza mara baada ya kutiwa saini kwa kandarasi hiyo, Bi. Amina Khamis Shaaban, amesema ujenzi wa barabara hiyo utakaohusisha pia ujenzi wa daraja katika Mto Ruaha Mkuu, utasaidia wakulima wadogo kupitia Program ya Uendelezaji Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania-SAGCOT, walioko katika Bonde la Mto Kilombero, kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao.
“Kuimarika kwa kipande hiki cha barabara kutaongeza uzalishaji wa nafaka na bidhaa nyingine hatimaye kupunguza gharama za chakula na umasikini wa wananchi” aliongeza Bi. Shaaban
Bi Shaaban amewashukuru wadau hao wa maendeleo kwa msaada huo utakao fungua milango ya kiuchumi kwa Watanzania kupitia Program hiyo ya kuendeleza Kilimo katika Ukanda huo wa Kusini-SAGCOT, unaohusisha pia kuboresha masuala ya nishati ya umeme.
“Ujenzi wa miundombinu unalengo la kuchochea maendeleo ya kilimo cha kibiashara kwa kuwa itasaidia kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara na wakulima”. Aliongeza Bi Shaaban.
Aidha amesema uboreshwaji wa miundombinu utachochea uwekezaji ambao ndio chachu ya maendeleo ya biashara za watu wa chini, hivyo kuinua kiwango cha maisha yao.
“Barabara ya Kidatu hadi Ifakara ndiyo inayounganisha Wilaya za Kilombero na Ulanga na ni barabara kuu itokayo Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zambia, Malawi na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) hivyo kuwa na tija katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi jambo ambalo ndio lengo kubwa la Wahisani hao”. alifafanua Bi Shaaban.
Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) hapa nchini, Roeland van de Geer ameahidi kuwa EU, UKAID na USAID, zitaendelea kushirikiana kwa kiwango cha juu na Serikali ya Tanzania katika kuboresha Sekta ya ujenzi na miundombinu kwa ujumla lakini pia atahakikisha wanachangia katika kupata soko la uhakika la mazao ya kilimo.
Sekta ya kilimo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania mbapo zaidi asilimia 70 ya wakazi wake hutegemea kilimo na kuna uwezekano mkubwa wa kuongeza uzalishaji, kipato na kukuza ajira, hususan kwa wanawake na vijana ikiwa miundombinu inayochangia ukuaji wa Sekta hiyo itazidi kuimarika.