Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.
MHASIBU wa Shule ya Sekondari ya St Joseph Cathedral, Elizabeth Asenga leo amehukumiwa kulipa faini ya Sh Milioni tano au kwenda jela miezi 12 baada ya kukutwa na hatia ya kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais Dk, John Magufuli.
Mhasibu huyo anadaiwa kumuita Rais Magufuli kilaza kupitia mtandao wa WhatsApp.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amesema mshtakiwa amepatikana na hatia baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na pande wa Jamuhuri kwa kuleta mashahidi saba na kumuona mshitakiwa ana hatia.
"Upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa umetenda kosa hivyo mahakama inakutia hatiani kwa makosa uliyoshitakiwa nayo"
Akimsomea adhabu yake amesema "utatakiwa kulipa faini ya Sh Milion tano au kutumikia kifungo cha miezi 12 jela," alisema Hakimu Shaidi.
Kabla ya kutolewa adhabu, mshitakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa mama yake mzazi ni mzee anamtegemea na ana watoto wanaomtegemea.
Hata hivyo, mshtakiwa amelipa faini na amefanikiwa kukwepa kwenda jela
Katika kesi ya msingi, inadaiwa Agosti 6, mwaka jana mshtakiwa huuo aliwasilisha maneno kinyume cha sheria kupitia mtandao wa WhatsApp katika group la wafanyakazi la STJ kwa nia ya kumtusi Rais.
Mshtakiwa alinukuliwa kuwa "Habari za asubuhi humu hakuna rais kilaza kama huyu wetu duniani angalia anavyompa Lissu umashuhuri, fala yule picha yake ukiweka ofisini nuksi tupu ukiamka asubuhi ukikutana na picha yake kwanza siku inakua ya mkosi mwanzo mwisho."