Tuesday, October 3

Makocha walia upendeleo Mwanza


Huenda waamuzi wanaochezesha mechi kwenye Uwanja wa Nyamagana siyo wazalendo kutokana na lawama wanazopewa na makocha wa timu ngeni.
Jana,  Jumatatu, mechi kati ya Pamba FC ya jijini Mwanza na Biashara ya mkoani Mara ilimalizika kwa suluhu, lakini bado kocha wa Biashara alishusha mvua ya lawama kwa waamuzi wa mchezo huo.
Kocha msaidizi wa Biashara FC, Amani Josiah, alimtupia lawana mwamuzi wa mchezo huo huku akitolea mfano baadhi ya nafasi na makosa yaliyopuzwa wakati wa pambano.
“Mchezo umekuwa ni mgumu sana, vijana wangu wamejituma kadri wawezavyo lakini mwamuzi wa leo amewanyima ushindi ambao ulikuwa wa wazi kabisa. Kipenga cha mwamuzi huyu kimekolea sana kwa upande wetu. Hata mngewasikiliza mashabiki wa Pamba wenyewe walikuwa wanamshabikia mwamuzi badala ya mchezo,” alisema Josiah.
Hata hivyo alishukuru kwa kupata pointi muhimu ugenini na pia kufahamisha kwamba hiyo ndio historia ya mpira wa miguu na zaidi ya yote akaridhia matokeo.
Kocha wa Pamba, Mathias Wandiba alisema wapinzani wao walikuwa na ‘rafu’ nyingi na ndio maana mwamuzi akawa anajaribu kutenda haki.
Aidha matokeo hayo yalimsikitisha kocha huyo kwani hakutarajia kutoka sare ya 0-0 akiwa nyumbani ingawa mpira wa miguu hautabiriki hadi kipenga cha mwisho.
Awali kwenye mchezo wa Trans Camp na Toto Africans uliopigwa uwanjani hapo juma lililopita, kocha mkuu wa Trans Camp, Nevelin Kanza alimlaumu mwamuzi wa mchezo huo kwamba alikuwa na mapendeleo ya wazi. Shirikisho la mpira wa miguu nchini liliangalie hili.
“Kiukweli mwamuzi ametumaliza kabisa. Imetulazimu kunyamaza ili kuheshimu sheria za soka lakini amekuwa kikwazo,” alisema kocha Kanza.
Kwenye mchezo huo, Toto Africans walipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Trans Camp uwanjani Nyamagana.

No comments:

Post a Comment