Tuesday, October 3

Tahadhari yatolewa kwa Watanzania juu ya ugonjwa wa tauni

Wizara ya Afya imetoa tahadhari kuhusu kuwepo ugonjwa wa tauni katika nchi ya Madagascar ulioibuka Agosti.
Imeelezwa kuwa, kati ya wagonjwa 104 walioripotiwa, 20 wamefariki dunia.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne na Ofisa Habari wa wizara hiyo, Catherine Sungura imesema Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza nchini Madagascar mikoa minane  imeripoti kuwepo wagonjwa ukiwemo mji mkuu wa nchi hiyo, Antananarivo.
Ugonjwa huo ulianza kuripotiwa Agosti 23 hadi Septemba 28.
“Wengi walioripotiwa wameonyesha kuwa na uhusiano kwa njia moja au nyingine na mgonjwa wa kwanza jambo linalothibitisha yapo maambukizi ya ugonjwa wa tauni kati ya binadamu na binadamu. Hivyo, kwa mujibu wa WHO, ipo hatari ya wastani (moderate risk) ya ugonjwa huo kusambaa katika nchi jirani na Madagascar,” imesema taarifa hiyo.
Wizara imesema tahadhari hiyo inatolewa kwa kuzingatia kwamba, Madagascar haiko mbali sana na Tanzania na inawezekana kukawa na mwingiliano kati ya wananchi wa nchi hizi mbili.
“Serikali inasisitiza kuwa mpaka sasa ugonjwa wa tauni haujaingia nchini. Kwa kuwa magonjwa hayaangalii mipaka, tunahitaji kuchukua tahadhari madhubuti ili kuzuia ugonjwa huu usiingie nchini. Hivyo, wananchi wanahimizwa kuzingatia kanuni za afya za kuzuia ugonjwa huu, pia wanatakiwa kuripoti haraka kwenye vituo vya huduma za afya waonapo dalili zozote za ugonjwa huu,” imesema wizara.
Sungura amesema hatua zilizochukuliwa baada ya kupata taarifa ya tahadhari ya WHO Septemba 29 ni kusambaza barua za tahadhari ya ugonjwa huo kwa makatibu tawala wa mikoa yote ya Tanzania Bara.
Makatibu tawala katika barua hizo wametakiwa kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa katika viwanja vya ndege, mipakani na bandari ili kubaini wagonjwa waingiao nchini wakiwa na dalili za ugonjwa huo.
“Kupitia kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya, wizara inatoa maelekezo ya kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na utambuzi wa magonjwa katika vituo vya kutolea huduma,” amesema.
Pia, wizara itatoa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa huo.

Kuhusu tauni
Ugonjwa huu husababishwa na bakteria anayejulikana kitaalamu “Yersinia pestis” ambaye hupatikana katika baadhi ya wanyama wadogo kama vile panya, paka, mbwa na viroboto.
Taarifa hiyo imezitaja njia kuu tatu ambazo mtu anaweza kupata maambukizi kuwa ni kung’atwa na viroboto vyenye maambukizi ya bakteria hao kutoka kwa wanyama kama vile mbwa na paka ambao huweza kubeba viroboto.
“Kugusana bila kuwa na kinga mwili na majimaji yenye vimelea vya bakteria kutoka kwa mtu/mnyama aliyeathirika kwa njia ya kugusa sehemu zenye vimelea zilizochafuliwa na mgonjwa/mnyama na kisha mtu huyo kujigusa mdomoni au puani,” imesema taarifa hiyo.
Njia nyingine ni kugusana na majimaji yanayotoka kwa mgonjwa kwa njia ya kukohoa au kupiga chafya bila ya mgonjwa kufunika pua au mdomo.

No comments:

Post a Comment