Monday, July 20

Benard Membe Atangaza Kuachana Na Siasa.......Asema Hatagombea Wadhifa Wowote Mwaka Huu

Waziri wa Mambo ya Nje na  ushirikiano wa kimataifa, Bernard Membe, amesema hatogombea wadhifa wowote kwenye uchaguzi mkuu wa  mwaka huu na kwamba anapanga kujishughulisha na masuala yake ya kibinafsi.

Membe ambaye alikuwa akitafuta tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuwania urais mwezi Oktoba lakini akashindwa kufikia lengo hilo, amesema kuwa, hatotafuta nafasi ya ubunge katika jimbo lake la Mtama.

Hata hivyo amesema ataendelea kukiunga mkono chama chake cha CCM na atampigia debe mgombea urais aliyeteuliwa na chama hicho, Bw. John Magufuli.

Awali kulikuwa na tetesi kwamba Membe angegombea ubunge baada ya kukosa nafasi ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM.

Huku hayo yakijiri, chama cha Mapinduzi  (CCM) kinaendelea kupata pigo baada ya baadhi ya wabunge wake kutangaza kuwa hawatogombea tena nafasi zao kupitia chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Tayari madiwani 20 wa CCM katika jimbo la Monduli wametangaza kuhamia Chadema na kumtaka mbunge wao, Edward Lowassa kufuata mkondo huo.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda Akataa Kugombea Tena Ubunge

Waziri mkuu Mizengo Pinda amekataa ombi la wananchi wa  jimbo lake la uchaguzi la Katavi la kumtaka agombee tena ubunge katika jimbo hilo ili kuendeleza mipango mbalimbali ya maendeleo aliyoianzisha. 
 
Akizungumza baada ya Ibada ya Jumapili katika kigango cha Kanisa Katoliki cha Kibaoni wilayani Mlele (Jumapili, Julai 19, 2015), Waziri Mkuu Pinda amesema anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia Taifa akiwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na anaamini wakati umefika wa yeye kuwaachia wengine nafasi ya ubunge wa jimbo la Katavi.

Amesema yeye ataendelea kuwa karibu na wananchi wa Katavi wakati wote  na kwa vile atakuwa na muda wa kutosha atashiriki kikamilifu katika mikakati mbalimbali ya kuwaletea maendeleo wananchi ili waweze kujikwamua kutoka kwenye umaskini. 
 
Mheshimiwa Pinda aliwaasa wananchi wa jimbo la Katavi wawe makini katika kuchagua mbunge na madiwani na kamwe watoa rushwa na wabadhirifu wasipewe nafasi katika uchaguzi ujao. 
 
Akimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, Paroko wa Parokia ya Usevya wilayani Mlele, Padri Aloyce Nchimbi aliwaasa wananchi wa Wilaya ya Mlele kumuenzi Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hata atakapokuwa amestaafu kwani bado watahitaji busara na uzoefu wake katika kujiletea maendeleo. 
 
Waziri Mkuu yuko kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mlele kwa ajili ya mapumziko mafupi. 
 
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Lembeli: Sitagombea ubunge kupitia CCM


Mbunge wa Kahama, James Lembeli ameiweka njiapanda CCM baada ya kutangaza kutogombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho.
 
Uamuzi wa Lembeli umekuja wakati wanachama kutoka sehemu mbalimbali wakitangaza uamuzi wao wa kujiengua CCM na kujiunga na vyama vya upinzani, hasa Chadema ambayo imesomba asilimia kubwa ya wahamaji hao.
 
Akizungumza  jana baada ya kuzagaa kwa taarifa katika mitandao ya kijamii kuwa amekihama chama chake na kuhamia Chadema, Lembeli alisema taarifa hizo ni uvumi uliozagaa jimboni kwake, lakini hajajiunga na chama chochote.
 
“Ni uvumi tu na uvumi wenyewe umechangiwa na swali nililoulizwa leo na wananchi kwamba ‘mbona toka mchakato wa kuchukua fomu umeanza hatujakuona’ na mimi nikawajibu kuwa ‘sitachukua fomu’,”alisema.
 
Lembeli (pichani) alisema amechukua uamuzi huo kutokana na rafu inayoendelea jimboni humo na maneno ya baadhi ya wanachama, wakiwemo viongozi kuwa hatakiwi na vigogo ndani ya CCM.
 
Lembeli, mmoja wa wabunge waliokuwa mstari wa mbele wakati wa kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, alisema sababu za kutotakiwa huko zinatokana na dhana potofu ya baadhi ya viongozi kwamba michango yake ndani na nje ya Bunge inaivua nguo Serikali.
 
“Tangu mchakato wa uchukuaji wa fomu umeanza baadhi ya wanachama wengi tu wameitwa kwenye vikao visivyo halali karibu kata zote wakiwa na kadi zao na kuorodheshwa na kupewa maagizo ya kunikataa kwenye kura ya maoni na wengine wanapewa Sh5,000,”alisema 
 
Lembeli alidai kuwa mbaya zaidi ni kwamba zipo kadi mpya za CCM zinazotolewa kiholela bila kufuata utaratibu na licha ya kulalamikia hali hiyo hakuna hatua zilizochukuliwa.
 
Alisema kutokana na yote hayo, aliwahi kusema kwenye mkutano wa hadhara kuwa kuna njama hizo, lakini badala ya CCM kufanyia kazi madai hayo, wakamuita mbele ya Kamati ya Maadili.
 
“Kwenye kamati ya maadili nilituhumiwa kuwa nakidhalilisha chama na kutakiwa niwataje nani walioniambia sitakiwi. Niliwajibu, tena kwa maandishi na kuwapa orodha, lakini mpaka leo kimya ina maana mimi bado ni mtuhumiwa,” alidai.
 
“Mimi siyo mtoto mdogo. Naelewa nini kinaendelea na ndiyo maana nimesema sitachukua fomu ya kugombea ubunge kwa mazingira haya. Bado sijatangaza kuhama CCM”.
 
Wakati Lembeli akisisitiza suala la kuhama kwake ni fununu tu, habari nyingine zilidai huenda akagombea ubunge kwa tiketi ya Chadema kutokana na kutokubaliana na mchakato huo anaodai ni batili.
 
Lembeli anaonekana kuwa mwiba ndani ya Serikali ya CCM baada ya kuiongoza Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ya Bunge katika uchunguzi wa uendeshaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili na kuibuka na taarifa iliyoonyesha kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
 
Mawaziri hao ni Balozi Hamis Kagasheki, Dk. David Mathayo, Dk. Emmanuel Nchimbi, Shamsi Vuai Nahodha na Ezekiel Maige.
 
Lembeli pia nusura ajikute nje ya mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2010 wakati alipopigiwa simu na katibu mkuu wa CCM wa wakati huo, akiambiwa achukue fomu za kuwania ubunge wa jimbo jipya la Ushetu.
 
Wakati huo, Lembeli alidokezwa siku ya mwisho na ofisa mmoja wa Tume ya Uchaguzi kuwa hakukuwapo na jimbo hilo na kulazimika kufanya jitihada katika muda mfupi kuchukua fomu kwenye Jimbo la Kahama na kufanikiwa kushinda kiti hicho.
 
Hivi karibuni, Lembeli alitofautiana na taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ya kuwasafisha mawaziri na katibu wa wizara waliowajibika kutokana na kashfa ya escrow na Operesheni Tokomeza.
 
Lembeli alisema kitendo cha kuwasafisha viongozi hao ni kuipeleka nchi gizani.
 
“Yuko hapa (waziri mkuu wa zamani, Edward)Lowassa. Japo mimi sipendi wizi na ufisadi, katika kashfa ya Richmond nilikuwa mmoja wa waliopiga kelele awajibike. Lakini wengine wamesafishwa, kwanini naye asisafishwe,” alisema baada ya taarifa hiyo ya Ikulu.
 
“Kama ni kusafishana tusafishwe wote, tuanze upya ndipo nchi hii itatawalika, vinginevyo huko mbele kuna giza nene.”

HABARI Habari Wavuvi wapamba mapokezi ya Dk Magufuli Sengerema 33 MINUTES AGO Msigwa asimamisha shughuli Iringa 52 MINUTES AGO Lembeli akataa kubadili msimamo 1 HOUR AGO Vita kali ya ubunge CCM, Chadema BIASHARA Biashara MICHEZO Michezo MAKALA Makala SWAHILI HUB Swahili Hub AJIRA VIDEO MONDAY, JULY 20, 2015 Vita kali ya ubunge CCM, Chadema

Baada ya mchakato wa kuwania urais, sasa vita ya Uchaguzi Mkuu imehamia kwenye ubunge na udiwani hasa kutoka katika vyama vikubwa vya CCM kinachotawala na Chadema kinachoongoza upinzani.
Hadi jana, ambayo ilikuwa ni siku ya mwisho kwa vyama hivyo kuchukua na kurejesha fomu, jambo moja lilijidhihirisha katika baadhi ya majimbo kwa upande wa CCM; baadhi ya majina makubwa katika siasa za ubunge yanachuana hivyo kufanya mchakato wa kumpata mteule mmoja kuwa mgumu.
Mchuano huo na kuimarika kwa Chadema mikoani hasa kutokana na majeraha ya mchakato wa urais ndani ya CCM, vinaufanya upinzani wa kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kuwa sawa na vita.
Nzega Vijijini
Makada wawili wa chama hicho, Lucas Selelii na Dk Hamisi Kigwangalla wamechukua fomu kuwania ubunge wa Nzega Vijijini.
Katika uchaguzi uliopita wa 2010, makada hao walivaana katika Jimbo la Nzega lakini wote wakaangushwa na Hussein Bashe aliyeibuka wa kwanza akifuatiwa na Selelii.
Hata hivyo, matokeo hayo yalibatilishwa na Halmashauri Kuu ya CCM na kumchukua Dk Kigwangalla aliyekuwa mshindi wa tatu.
Mgawanyo wa majimbo uliofanywa wiki iliyopita na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), umerahisisha mpambano wa makada hao, hivyo wawili hao wakamwachia Bashe Nzega Mjini. 
Akichukua fomu hiyo jana, katika ofisi za CCM za Wilaya ya Nzega, Dk Kigwangalla akiwa ameambatana na wazee wa jimbo hilo, alisema shinikizo la kugombea Nzega Vijijini limetoka kwa wananchi wanaotambua umuhimu wake.
Selelii aliyekuwa Mbunge wa Nzega kwa miaka 15 hadi 2010, alichukua fomu kimyakimya bila kuzungumza na vyombo vya habari.
Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega,  Empimark Makuya alithibitisha kuwa kada huyo alishachukua fomu. Wawili hao watakabiliana na upinzani mkali kutoka kwa wengine wawili waliochukua fomu, John Dotto na Paul Kabelele.
Maiga aibukia Iringa
Baada ya kukwama katika harakati za kuwania urais kupitia CCM, Balozi Dk Augustine Mahiga amejitokeza kuwania ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini.
Dk Mahiga aliyechukua fomu jana na kurudisha, atapambana na Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Jesca Msambatavangu, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Frederick Mwakalebela na mwandishi wa habari, Frank Kibiki ambao tayari wamechukua na kurejesha fomu zao.
Mchuano katika jimbo hilo unatarajiwa kuwa mkali wakati na baada ya kura za maoni ndani ya CCM hasa ikizingatiwa kwamba Mwakalebela alikuwa amechukua namba moja katika kura za maoni za chama hicho mwaka 2010 kabla ya jina lake kukatwa na NEC.
Mshindi atakuwa na wakati mgumu kukabiliana na kishindo cha upinzani hasa kutoka Chadema ambako Mchungaji Peter Msigwa aliyeshinda katika uchaguzi uliopita, jana alipokewa na umati mkubwa wa watu alipowasili mjini hapo.
Profesa Maghembe na Thadayo tena
Mshikemshike mwingine unatarajiwa kuibuka katika Jimbo la Mwanga ambako Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe anatarajiwa kupambana tena na hasimu wake mkubwa katika kiti hicho, Joseph Thadayo.
Katika uchaguzi wa 2010, Profesa Maghembe alimshinda Wakili huyo ambaye alionekana kuungwa mkono na wanasiasa wengine wenye nguvu katika jimbo hilo. Mbali yao wengine waliojitokeza ni Aminieli Kibali na Karia Magaro.
Wasira, Bulaya wavaana
Mchuano mwingine mkali unatarajiwa kuwapo katika Jimbo la Bunda Mjini ambako Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira atavaana na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya.
Wabunge hao wa CCM wamekuwa wakitambiana muda mrefu na wakati mwingine waliwahi kurushiana maneno hadi bungeni, lakini mwisho wa tambo zote ni kwenye kura za maoni.
Mamia warejesha fomu
Hadi muda wa mwisho wa kurejesha fomu unakamilika saa 10 jioni jana, mamia ya makada wa Chadema na CCM walikuwa wamejitokeza na kudhihirisha kuwa mchuano utakuwa mkali katika kura za maoni na hata kwenye uchaguzi wenyewe.
Kawe 22: Elias Nawera, Dk Walter Nnko, Jumaa Muhina, Kippi Warioba, Atulinda Barongo, Tegemeo Sambili, Kiganga George, Edmund Lyatuu, Charles Makongoro Nyerere, Mtiti Butiku, Yusuf Nassoro, John Mayanga, Dickson Muze, Dk Wilson Babyebonela, Colman Massawe, Amon Mpanji, Amelchiory Kulwizira, Gabriel Mnasa, Abdallah Majura na Jerry Murro, wote wakikabiliana na Halima Mdee aliyejitokeza pekee Chadema, hasa iwapo atasimama pekee kupitia Ukawa.
Kinondoni 12: Idd Azan, Wagota Salum, Tonny Kalijuna, Goodchange Msangi, Emmanuel Makene, Lusajo Willy, Mage Kimambi, Mussa Mwambujule, Stevew Nengere (Steve Nyerere), Joseph Muhonda, Michael Wambura na Macdonald Lunyiliga.
Ubungo 12: Vincent Mabiki, Timoth Machibya, Jordan Baringo, Emmanuel Mboma, Zangina Zangina, Kalist Ngalo, Hawa Ng’umbi, Jackson Millengo, Didas Masaburi, Joseph Massana, wote wa CCM wakitarajiwa kumkabili John Mnyika wa Chadema.
Ilala watatu: Mussa Azzan Zungu, Mrisho Gambo na Waziri Kindamba.
Ukonga 16: Jerry Silaa, Jacob Katama, Hamza Mshindo, Frederick Rwegasira, Anthony Kalokola, Ramesh Patel, Peter Majura, Amina Mkono, Edwin Moses, Robert Masegese, John Bachuta, Edward Rabson, Nickson Tugale, Elly Ballas, Asia Msangi, Lucas Otieno, Fredrick Kabati, Mwanaidi Maghohe, Mwita Waitara, Deogratius Munishi, Deogratius Kalinga, Deogratius Mramba, Salanga Kimbaga, James Nyakisagana, Lameck Kiyenze na Gaston Makweta.
Segerea 13: Zahoro Lyasuka, Apruna Humba, Bona Kalua, Nicholaus Haule, Baraka Omary, Benedict Kataluga, Dk Makongoro Mahanga na Joseph Kessy.
Kigamboni 10: Aron Othman, Kiaga Kiboko, Abdallah Mwinyi, Dk Faustine Ndugulile, Ndahaye Mafu, Flora Yongolo, David Sheba, Mohammed Ally Mchekwa, Khatib Zombe na Adili Sunday.
Mbagala 23: Lucas Malegeli, Mindi Kuchilungulo, Kazimbaya Makwega, Adadius Richard, Tambwe Hiza, Issa Mangungu, Ingawaje Kajumba, Siega Kiboko, Peter Nyalali, Mwinchumu Msomi, Dominic Haule, Aman Mulika, Banda Sonoko, John Kibasso, Ally Makwiro, Alvaro Kigongo, Maesh Bolisha, Kivuma Msangi, Deus Sere, Abdulrahim Abbas, Salum Seif Rupia, Ally Mhando, Fares Magessa, Stuwart Matola.
Moshi: Priscus Tarimo, Amani Ngowi, Patrick Boisafi, Davis Mosha, Buni Ramole, Halifa Kiwango, Michael Mwita, Daud Mrindoko, Shanel Ngunda, Innocent Siriwa, Edmund Rutaraka, Omari Mwariko, Basil Lema, Jaffar Michael na Wakili Elikunda Kipoko.
Busokelo:  Suma Mwakasitu , Dk Stephen Mwakajumilo, Ezekiel Gwatengile, Mwalimu Juma Kaponda, Ally Mwakibolwa, Issa Mwakasendo, Aden Mwakyonde na Lusubilo Mwakibibi.
Kilombero: Kanali mstaafu Harun Kondo, Vitus Lipagila, Abdullah Lyana, Oscar Mazengo,  Japhet Mswaki, Paul Mfungahema, John Guninita, Abubakari Asenga na Abdul Mteketa.
Mlimba: Dk Frederick Sagamiko, Senorina Kateule, Godwin Kunambi, Augustino Kusalika, George Swevetta, Castor Ligallama, Profesa Jumanne Mhoma, Fred Mwasakilale, Dismas Lyassa.
Namtumbo: Edwin Ngonyani, Edwin Milinga, Mwinyiheri Ndimbo, Vita Kawawa, Anselio Nchimbi, Julius Lwena, Fitan Kilowoko, Balozi Salome Sijaona, Mussa Chowo, Salum Omera, Ally Mbawala na Charles Fussi.
Tunduru Kaskazini: Mhandisi Ramo Makani, Omary Kalolo, Michael Matomola, Hassan Kungu, Issa Mpua, Rashid Mandoa, Athuman Mkinde, Shaban Mlono na Moses Kulawayo.
Tunduru Kusini: Abdallah Mtutura, Daim Mpakate na Mtamila Achukuo.
Nyasa: Christopher Chale, Bethard Haule, Adolph Kumburu, Alex Shauri, Frank Mvunjapori, Dk Steven Maluka, Stella Manyanya, Cassian Njowoka, Jarome Betty na Oddo Mwisho.
Serengeti: Dk Stephen Kebwe, Dk James Wanyancha, Juma Kobecha na Mabenga Magonera.
Sumbawanga Mjini: Aeshi Hilaly, Anyosisye Kiluswa, Fortunata Fwema, Mathias Koni, Gilbert Simya, Frank Mwalembe, Selis Ndasi, Mbona Mpaye, Sospeter Kansapa, Paschal Sanga na Victor Vitus.
Korogwe Vijijini: Stephen Ngonyani (Profesa Majimarefu), Cesilia Korassa, Allan Bendera, Ali Mussa Moza, Abdallah Nyangasa, Christopher Shekiondo, Andrew Matili, Edmund Mndolwa, Ernest Kimaya, Peter Mfumya na Stephen Shetuhi.
Kilindi: Beatrice Shellukindo, Abdallah Kidunda, Fikirini Masokola na Dk Aisha Kigoda.
Bariadi Mashariki: Masanja Kadogosa na Joram Masaga.
Mbulu: Mary Margwe amechukua fomu ya kugombea ubunge wa viti maalumu
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye na yule wa Kilosa Kati, Mustafa Mkulo hawakujitokeza kuchukua fomu.
Imeandikwa na Julius Mathias,  Bakari Kiango, Godfrey Kahango, Ngollo John, Salim Mohammed, Joseph Lyimo, Faustine Fabian, Joyce Joliga, Daniel Mjema, Burhani Yakub, Antony Mayunga, Mussa Mwangoka na Mustapha Kapalata

Kambi ya Lowassa sasa rasmi Chadema

Sasa ni rasmi kwamba kambi ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Edward Lowassa imeamua kuachana na chama hicho baada ya madiwani 18 kutangaza kuhamia Chadema, huku mratibu wa wanachama wanaomuunga mkono kada huyo wa CCM kuamua kujiunga na vyama vinavyounda Ukawa.
Matukio hayo yametokea ikiwa ni mwendelezo wa wimbi la wanachama wa CCM kutangaza kuhamia vyama vya upinzani, hasa Chadema baada ya madiwani tisa pamoja na wanafunzi 28 wa vyuo vikuu kutangaza kuhamia Chadema ambayo ni chama kikuu cha upinzani.
Wote wameeleza sababu ya kuhama CCM ni kutokubaliana na uamuzi wa Kamati Kuu wa kukata jina la Lowassa wakati wa mchujo wa wagombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala mwishoni mwa wiki iliyoishia Julai 12.
Akizungumzia kuhama kwa madiwani hao, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema hawezi kujibu lolote kwa madai kuwa hana taarifa rasmi na kutaka waulizwe viongozi wa chama wa mkoa.
“Madiwani hao siwajui na sina taarifa rasmi ninaweza kutoa maoni yangu, lakini kesho ikabainika kuwa hazikuwa taarifa rasmi juu ya kuhama kwao?” alihoji.
Nape alisisitiza kuwa hakuna kanuni zilizokiukwa wakati wa kumsaka mgombea urais kama wanachama hao wanavyodai.
Nape pia alizungumzia kitendo cha mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru cha kuilaumu Kamati ya Maadili na Kamati Kuu akisema kinaweza kukigawa chama hicho.
“Kama wakiendelea CCM kitaitisha mkutano na kuwajibu. Lakini kwa sasa tunawataka tu wawasilishe malalamiko yao sehemu husika maana huo utaratibu wanaujua,” alisema
Jana, mkoani Arusha, madiwani hao, walioongozwa na viongozi wa kijadi wa jamii ya Kimasai wanaofahamika kwa jina la Malaigwanan, walipokewa jana na aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema kwenye hafla fupi iliyofanyika mjini Monduli.
Mwenyekiti wa CCM wa mkoa, Onesmo ole Nangole alisema chama chake hakina uwezo wa kuzuia mtu kuondoka CCM.
“Tumepata taarifa za kuondoka madiwani na viongozi wetu na kuchomwa kadi lakini hatuwezi kuzuia uamuzi wa watu kufanya wanachotaka,” alisema.
Alisema tayari wameanza kufuatilia kinachoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali mkoani Arusha ili kujua athari za matukio hayo kwa CCM.
Viongozi hao waliohamia Chadema ni 10 wakati Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ina kata 20. Awali, halmashauri hiyo ilikuwa na kata 15 kabla nyingine tano kuongezwa mwaka huu.
Akisoma tamko la kujiengua CCM na kuhamia Chadema, mwenyekiti wa madiwani hao, Julius Kalanga ambaye ni diwani wa Kata ya Lepurko, alisema hatua hiyo imetokana na kuchoshwa na vitendo alivyoviita vya hila, uonevu, ubaguzi na unyanyasaji vinavyofanywa ndani ya chama hicho tawala.
“Tumetafakari usalama wetu ndani ya CCM kwa umoja wetu tumeshindwa kuuona… CCM iliyokuwa ikiongozwa kwa Katiba, kanuni na miongozo hivi sasa inaongozwa kwa matakwa ya familia chache kwa jinsi watakavyoona inawapendeza wao,” alisema Kalanga.
Alisema mchakato wa CCM wa kumpata mgombea urais uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma ni miongoni mwa ishara za wazi za chama hicho kukosa maadili kuanzia kwenye vikao vya Kamati ya Maadili alichodai kilikosa maadili hadi kukatwa kwa majina ya wagombea akiwemo Lowassa.
Kalanga, mmoja wa wasaidizi wa karibu wa Lowassa katika shughuli zake za kisiasa, alisema wana-CCM wamepoteza haki na uwezo wa kuchagua viongozi wanaowataka kutokana na kunyimwa uwezo wa kufikiri kwa sababu uamuzi hauzingatii utaratibu wa vikao.
“Tunakataa kuwa watumwa katika misingi hii na ndiyo maana leo tunaondoka sisi viongozi wote na kuamua kujiunga Chadema,” alisema Kalanga.
“Tunamwomba Mheshimiwa Lowassa aungane nasi katika safari yetu hii inayoendelea. Awe na moyo wa ujasiri na kufanya uamuzi mgumu maana hakuna busara nyingine inayoweza kutumika zaidi ya kuondoka CCM,” alisisitiza Kalanga.
Diwani wa Kata ya Mererani, Edward Lenana ambaye ni mmoja wa waliotimkia Chadema alisema yeye na wenzake watazunguka kwenye majimbo yote ya jamii ya Wamaasai kuhamasisha jamii hiyo kutochagua wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais.
Akizungumza baada ya kuwakabidhi viongozi hao kadi za Chadema, Lema aliwataka kuingia kazini kukijenga chama chao kipya ili kufanikisha ushindi katika uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba 25.
“Ndani ya Chadema hakuna mheshimiwa, kiongozi wala mwanachama mdogo. Wote ni makamanda wanaopaswa kupambana dhidi ya uovu na ukandamizaji. Kuanzia leo ninyi nyote ni makamanda. Hakuna kamanda mgeni wala mwenyeji, bali sote ni wapiganaji wenye lengo moja la ushindi mwezi Oktoba,” alisema Lema.
Mwenyekiti wa Chadema wa mkoa, Amani Golugwa aliwataka wanachama hao wapya kujifunza na kuishi katika misingi ya uadilifu, unyenyekevu na utumishi kwa umma aliosema ndiyo miongoni mwa imani kuu ya Chadema.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na wa viti maalumu, Joyce Mukya waliwahakikishia viongozi hao fursa ya kuendelea kuwatumikia wananchi katika kata zao wakiwa Chadema kwa sababu wapigakura ni wale wale, bali kilichobadilika na jukwaa la kusimamia kuwatumikia.
Wengine Dar wajiengua
Jijini Dar es Salaam, wanachama waliokuwa kundi la 4U Movement linalomuunga mkono Lowassa, walitangaza kuihama CCM chama hicho na kujiunga na Ukawa, kutokana na kile walichodai kuchukizwa na mchakato wa kumpata mgombea urais.
Mratibu wa wanachama hao, Hemed Ally alisema wamefikia uamuzi wa kujiunga na Ukawa inayoundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, NLD na CUF, kwa ajili ya “kutafuta mabadiliko nje ya CCM”, kutokana na kushindwa kuyapata wakiwa ndani ya chama hicho tawala.
Wadai njama zimewatoa
Wanachama hao wanaodai wana wafuasi wapatao milioni 10 ambao wengi ni vijana, walitangaza uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari, huku wakisisitiza kuwa kulikuwa na njama za kuhakikisha kuwa Lowassa anaenguliwa huku wakinukuu maneno yaliyosemwa na kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru ambaye naye alikilalamikia chama hicho kutomtendea haki Lowassa, ambaye ni mbunge wa Monduli.
Makada wa CCM waliopitishwa kuwania nafasi ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 walikuwa 38, huku Dk John Magufuli akiibuka kidedea.
Waliongia tano bora walikuwa Dk Magufuli, Bernard Membe, Balozi Amina Salum Ali, Asha-Rose Migiro na January Makamba.
Wanachama hao walisema kwa pamoja wamekubaliana kutumia kura zao kuking’oa CCM madarakani katika uchaguzi wa mwaka huu.
Ally alisema kulikuwepo na ukiukwaji mkubwa wa kanuni katika uteuzi, jambo linalowafanya waamini kuwa Kamati ya Maadili ilikosa maadili.
“Tunaomba ieleweke wazi hatuna nia ya kumpinga Magufuli ila upatikanaji wake ulijaa maovu hivyo tumeamua hatutaiunga mkono CCM na kura zetu tutazipeleka upinzani.
“Lowassa hakutendewa haki na kila mmoja anatambua hilo, sisi tumeamua kutoka kwa sababu tulikuwa tunamuunga mkono yeye tukiamini atatuletea mabadiliko lakini kwa mtindo huu tunaona kiu yetu haiwezi kutimizwa ndani ya CCM,” alisema Ally.
Alivitaka vyama vya upinzani kuunganisha nguvu kwa pamoja na kushirikiana nao kuindoa CCM kwa demokrasia ya upigaji kura. Kwa mujibu wa Ally, wafuasi hao wamegawanyika katika makundi kadhaa ambayo ni 4 U Movement, Lowassa for Presidency, Team Lowassa, Umoja wa Waendesha Bodaboda na Shirikisho la Walimu.
“Upinzani ukijipanga vizuri tunaweza kuindoa CCM madarakani ikizingatiwa kura zetu zote tutazielekeza upande huo kumuunga mkono mgombea yoyote watakayemsimamisha,” alisema.
Katibu wa Shirikisho la Walimu Wafuasi wa Lowassa, Maulid Nkungu alisema kama vijana hawana sababu ya kukubaliana na utaratibu ambao hata wakongwe wa chama hicho hawajaridhishwa nao.
“Tuliipenda sana CCM, lakini imeonyesha kutopenda mabadiliko hilo ndilo linalotuondoa tumechoka kuonewa tunataka kulinda heshima na kuwakomboa wanaonyanyaswa,” alisema.