ZIKIWA zimebaki siku mbili kufika Julai 15 ambao ndio ukomo wa leseni ya Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), imeelezwa kuwa hatima yake sasa ipo mikononi mwa Ikulu.
Wakati Ikulu ikisubiriwa kuijibu wizara husika, endapo Julai 15 itapita bila IPTL kuongezwa muda wa leseni yake, haitaweza kuendelea tena na uzalishaji wa nishati hiyo.
Juni 11, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Felix Ngamlagosi, ikiwa ni siku chache tangu mamlaka hiyo itoe taarifa kwa umma ya kuanza kukusanya maoni baada ya ombi la IPTL la kuongezewa leseni ya uzalishaji umeme kwa miezi 55.
Mara baada ya taarifa ya kusimamishwa kazi kwa Ngamlagosi iliyohusishwa na hatua ya Ewura kutoa tangazo kwa umma kuutarifu juu ya kutoa maoni yao kufuatia ombi la IPTL kuongezewa muda wa leseni yao ya uzalishaji umeme, mamlaka hiyo ilitoa taarifa nyingine kwa umma ikitaarufu kusimamisha ukusanyaji huo wa maoni.
“Taarifa inatolewa kwa umma kwamba kufuatia maombi ya kampuni ya uzalishaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) (“Mwombaji”)
kuomba kuongezewa muda wa leseni yake ya kuzalisha umeme kwa kipindi cha miezi 55 kutokea tarehe 15 Julai 2017.
“Ewura zaidi ya hatua nyingine za kiudhibiti, iliwasiliana na Wizara ya Nishati na Madini ili kupata maoni yake kwa mujibu wa kifungu cha 7 (3) cha Sheria ya Ewura, sura ya 414 ya sheria za Tanzania.
“Wizara ya Nishati na Madini imetoa mapendekezo ya kuwapo na mashauriano zaidi kati ya Wizara, Ewura na wadau mbalimbali wa sekta ndogo ya umeme kabla ya kuendelea na mchakato wa maombi ya mwombaji.
“Kutokana na maoni hayo, Ewura inasitisha mchakato wa kushughulikia maombi ya leseni ya mwombaji ikiwa ni pamoja na upokeaji wa maoni/mapingamizi dhidi ya maombi hayo mpaka hapo yatakapotolewa maelekezo mengine,” ilisema taarifa hiyo.
Jana Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo, alipotafutwa na gazeti hili ili kuzungumzia hatima ya IPTL, alisema mashauriano na Serikali bado yanaendelea na ikifika Julai 15 ataweza kuwa na jambo la kusema.
“Kwenye tangazo letu tulisema mashauriano na Serikali yanaendelea na wadau wengine yanaendelea, kwa hiyo kwa sasa siwezi kusema kitu ila subiri hiyo Julai 15 nitakuwa na cha kusema,” alisema Kaguo.
MTANZANIA pia ilimtafuta Kamishina wa Nishati, Innocent Luoga, ili kujua mazungumzo ya suala hilo yalipofikia.
“Natamani kama ningeweza kukujibu, lakini suala hili msemaji wake ni Katibu Mkuu ambaye hayupo, lakini tu nikwambie ukweli kwamba kwa sasa lipo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, kwa hiyo siwezi kusema chochote,” alisema Luoga.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, alipotafutwa ili kuthibitisha kama kweli suala hilo limefika mezani kwa Katibu Mkuu Kiongozi, alisema: “Hili suala ni la Wizara ya Nishati, kama wamewaambia kuwa wamelipeleka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, basi watakachojibiwa watawaeleza.”
Kwa upande wao, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) walipoulizwa baada ya leseni ya IPTL inayozalisha umeme megawati 110 (MW) kwa kutumia mafuata mazito itakapofika kikomo Julai 15 ni hatua gani itafuata, walisema hawawezi kusema lolote kwa sasa.
“Kwa sasa siwezi kuzungumza chochote juu ya suala hilo,” alisema msemaji wa shirika hilo, Leila Muhaji.
Makubaliano ya kuuziana umeme (Purchase Agreement-PPA) kati ya IPTL na Tanesco, yalisainiwa mwaka 1995 kwa miaka 20, huku leseni ya sasa ya IPTL ikiwa imetolewa na Wizara ya Nishati na Madini mwaka 1996 kwa kipindi cha miaka 21.
CHIMBUKO LA IPTL
Chimbuko la IPTL ni uhaba wa umeme mwaka 1994, ilipoonekana kuna uhitaji wa kuwa na umeme wa dharura.
Agosti 19, 2014, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mechmar, iliyokuwa ikimiliki asilimia 70 ya hisa za IPTL, Datuk Baharuden Majid, aliongoza ujumbe kutoka Malaysia kuja kuzungumza na Serikali ya Tanzania.
Septemba 1994, Mkataba wa Maelewano (MOU) ulifikiwa, licha ya tahadhari kutoka kwa washauri wa Tanesco ambao ni kampuni za Acres (Canada) na Hunton and Williams (Uingereza), kwamba uwekezaji huo ulikuwa ni janga kwa sekta ya umeme na kwa uchumi wa taifa.
Kampuni hiyo ambayo wamiliki wake ni Mechmar ya Malaysia mwenye asilimia 70 na VIP ya Tanzania yenye asilimia 30 ilisaini mkataba wa miaka 20 (1995-2015) na Serikali ya Tanzania.
7.92 kwa mwezi kama ada ya huduma za mtambo. Mwaka 2002 IPTL ikaanza kuiuzia umeme Tanesco, lakini ilipofika 2004 ikabainika kuwa ilidanganya kuhusu mtaji.
Awali IPTL ilisema asilimia 30 ya mtaji ilikuwa nao sawa na Dola milioni 36 na kwamba asilimia 70 ilikopa.
Baada ya ukaguzi ikabainika IPTL haikuweka dola milioni 36 kama mtaji, bali iliweka dola 50 ambazo kwa wakati huo zilikuwa sawa na Sh 50,000.
Kutokana na kasoro hiyo, Tanesco ikataka gharama ya umeme ishuke.
Mabishano yakaendelea hadi mwaka 2006, ikaamuliwa kufunguliwa kwa akaunti maalumu (Tegeta Escrow) ili Tanesco iwe inaweka huko fedha hadi pale mwafaka utakapopatikana.
Mwaka 2008, IPTL ilishindwa kujiendesha, hivyo ikawekwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA).
Hukumu ya Mahakama Kuu iliyotoka Septemba 2013 chini ya Jaji John Utamwa, iliamua IPTL iondolewe chini ya usimamizi wa Rita na mali zake zote ipewe Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Ltd (PAP) ya Harbinder Singh Sethi.
Hukumu hiyo ilitoka huku mmiliki wa asilimia 70 ya IPTL (Mechmar) akiwa mufilisi nchini Malaysia na zaidi ICSID kukiwa na kesi inayohusu mgogoro wa IPTL na Serikali uliofunguliwa na Standard Chartered Bank, ambayo ilinunua deni la kampuni hiyo mwaka 2005 na ikaruhusiwa kuishtaki Serikali ya Tanzania kwenye baraza hilo lenye mamlaka ya mwisho.
Februari 2014, ICSID ilifanya uamuzi wa awali kwamba ni kweli IPTL inaitoza zaidi Tanesco na kuelekeza pande mbili zikafanye hesabu upya ndani ya siku 90 zilizoisha Mei 2014 kwa lengo la kujua ni kwa kiasi gani kampuni hiyo imelipunja shirika hilo katika bei tangu 2002 hadi 2013.
Hata hivyo, Tanesco na Serikali hawakutoa ushirikiano ndani ya siku hizo 90 kutekeleza uamuzi huo.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu ukaguzi wa Akaunti ya Tegeta Escrow na umiliki wa Kampuni ya IPTL iliyowasilishwa bungeni Novemba 2014, ilionyesha kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Sh bilioni 306 na zilitakiwa kurudishwa Tanesco.
Kutokuwapo kwa umakini kwa Serikali kulisababisha Kampuni ya PAP kujimilikisha fedha za IPTL kwa asilimia 70 bila kuwa na ushahidi wowote kwamba iliinunua IPTL ikiwamo malipo ya kodi kama ilivyofanya kwa VIP yenye asilimia 30 za hisa.
IPTL INAVYOINYONYA TANESCO
Moja ya taarifa za Ewura kuhusu kampuni zinazoiuzia Tanesco umeme, zinaonyesha kuwa IPTL inaiuzia kila uniti kwa Dola za Marekani senti 23.1 na kila mwezi inalipwa Capacity Charge ya Dola za Marekani 2,655,786.
Ukikokotoa kiasi hicho kwa wastani wa kila Dola moja kwa Sh 2,238, inafanya kila mwezi IPTL kulipwa Sh bilioni Sh bilioni 5.943 ambayo kwa mwaka inakuwa wastani wa Sh bilioni 71.316.