Saturday, July 15

RC SHINYANGA ATEMBELEA KIWANDA CHA MAFUTA YA MCHELE KIZUMBI SHINYANGA

Ijumaa Julai 15,2017,Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack ametembelea kiwanda cha kutengeneza mafuta ya mchele kinachomilikiwa na kampuni ya Mwekezaji kutoka nchi ya China Jielong Holding kilichopo katika kijiji cha Nhelegani kata ya Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga.

Mkuu huyo wa mkoa aliyekuwa ameambatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Shinyanga na maafisa mbalimbali mkoa huo amejionea jinsi kampuni hiyo ilivyodhamiria kuzalisha mafuta ya kupikia yanatokana na mapumba laini ya mpunga “Mchele”.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Telack alisema kiwanda hicho ni cha pekee nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla na kitasaidia wamiliki wa mashine za kukobolea mpunga pamoja na wakulima kunufaika na zao la mpunga kwani wataweza kuuza mapumba kwa ajili ya kutumika kama malighafi kuzalishia mafuta hayo.

“Niwapongeze wawekezaji hawa kwa ubunifu huu wa kiwanda cha aina yake, serikali ya mkoa wa Shinyanga inaunga mkono jitihada za kuhakikisha tunakuwa na uchumi wa viwanda,tushirikiana kuwahamasisha wananchi kulima mpunga kwa wingi na wale wenye mpunga basi wauze mapumba yao ili wajipatie kipato”,alieleza Telack.

“Naamini watu wenye mashine za kukobolea mpunga wataongeza kipato kwa kuuza mabaki ya mpunga kwa ajili ya kuendeshea kiwanda hiki ambacho pia kinazalisha nishati ya umeme kwa kutumia mapumba”,alieleza Telack.

Aidha aliwahamasisha wamiliki wa kampuni ya Jielong Holding kununua mapumba ya mchele kwani katika maeneo mbalimbali mkoani Shinyanga ili kiwanda hicho kianze kufanya kazi mara moja.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Kampuni ya Jielong Holding, Qi Shuwei aliiomba serikali kuendelea kushirikiana na kampuni hiyo na pale panapojitokeza mapungufu basi serikali iwape ushauri kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.

“Tunaishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa viwanda,lengo kampuni yetu inayojihusiha na mazao hususani uzalishaji wa mafuta ya alizeti,pamba na mchele na kutengeneza sabuni ni kuwainua kiuchumi wananchi kupitia mazao wanayolima”,alisema Shuwei.

Hata hivyo alisema kiwanda hicho kimekwama kuanza uzalishaji wa mafuta ya mchele kutokana na uhaba wa malighafi kwani zinatakiwa tani 500 za mapumba kwa ajili ya kuanzisha uzalishaji lakini kiwango hicho hakijafika.

Angalia picha za matukio yaliyojiri wakati wa ziara hiyo kutembelea viwanda mbalimbali ikiwemo kiwanda cha kutengenezea mafuta ya Mchele,alizeti,pamba na sabuni vinavyomilikiwa na kampuni ya Jielong Holding 
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack (kulia) akitembelea kiwanda cha kutengeneza mafuta ya mchele kinachomilikiwa na kampuni ya Mwekezaji kutoka nchi ya China Jielong Holding kilichopo katika kijiji cha Nhelegani kata ya Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga.Kulia kwake ni Mkalimani katika kampuni hiyo Joseph Warioba akifuatiwa na Mwenyekiti wa kampuni Jielong Holding,Qi Qi Shuwei.Wengine ni wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Shinyanga na maafisa kutoka mkoa huo. 
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiwa ndani ya kiwanda cha Jielong Holding.

Qi Shuwei akiongoza msafara wa mkuu wa mkoa wa Shinyanga kuangalia uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na mazao yanayolimwa na wakulima.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiteta jambo na Mwenyekiti wa kampuni Jielong Holding,Qi Qi Shuwei.

Kulia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Jielong Holding, Qi Shuwei akimweleza mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack kuhusu kiwanda cha mafuta ya mchele walichokianzisha ambapo watakuwa wananunua mapumba ya mpunga ili kupata mafuta ya kupikia.



Mwenyekiti wa Kampuni ya Jielong Holding, Qi Shuwei akionesha mapumba malaini yaliyoanza kutengenezwa ili kupata mafuta ya kupikia.



Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akishika mapumba laini ya mpunga 'mchele' ambayo tayari yapo katika hatua za awali kwa ajili ya kutengeza mafuta ya kupikia.

Mapumba ya mpunga yakiwa kiwandani.

Mkuu wa mkoa,waandishi wa habari na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Shinyanga wakiangalia moto mkali ndani ya kiwanda hicho unaotokana na mapumba/mabaki ya nafaka ambayo yanatumika kutengeneza nishati ya umeme katika kiwanda cha Jielong Holding.Kulia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Jielong Holding, Qi Shuwei.

Dirisha dogo lililofunguliwa kuonesha moto mkali.

Mwenyekiti wa Kampuni ya Jielong Holding, Qi Shuwei akimweleza jambo mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack wakati akimbelea viwanda vya kampuni hiyo.

Mkalimani katika kiwanda cha Jielong Holding,Joseph Warioba akitoa maelezo kwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack kuhusu malighafi mbalimbali zinazotumika katika kiwanda hicho cha kutengeneza mafuta ya alizeti,pamba,mchele na sabuni.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiangalia zoezi la utengenezaji wa madumu ya plastiki kwa ajili ya kuwekea mafuta yanayotengenezwa katika kiwanda cha Jielong Holding.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiangalia mitambo ya kutengenezea vifungashio vya plastiki/madumu ya mafuta.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiwa ndani ya kiwanda cha Jielong Holding.



Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiangalia ndoo ya plastiki iliyotengenezwa katika kiwanda hicho kwa ajili ya kuwekea mafuta ya alizeti.





Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akingalia shughuli ya uzalishaji mafuta ya alizeti inavyofanyika.





Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiangalia mafuta ambayo yako tayari kwa ajili matumizi ya binadamu.





Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiwa ndani ya kiwanda hicho.





Mwenyekiti wa Kampuni ya Jielong Holding, Qi Shuwei akimweleza jambo mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack.





Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiangalia mitambo ndani ya kiwanda.





Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiendelea kuangalia mitambo.





Mfanyakazi wa kiwanda cha Jielong Holding,Joseph Warioba akionesha mitambo ya kutengenezea mafuta mbalimbali.





Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiangalia sabuni ya gwanji iliyotengenezwa katika kiwanda cha sabuni cha Jielong Holding.





Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiangalia sabuni.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack na Afisa Uhamiaji mkoa wa Shinyanga Anna Maria Yondani wakiangalia miche ya sabuni.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akikagua mazingira nje ya viwanda

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiangalia shimo la majitaka.

Kulia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Jielong Holding, Qi Shuwei akizungumza baada ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack kutembelea viwanda vinavyomilikiwa na kampuni ya Jielong Holding.Kushoto ni Mkalimani wa kampuni hiyo Joseph Warioba akitafsiri lugha ya Kichina na Kiswahili.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akizungumza baada ya kutembelea viwanda,

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa,maafisa mkoa na wafanyakazi wa kampuni ya Jielong Holding wakijadiliana namna ya kufanya ili viwanda viwanufaishe wananchi,wawekezaji na serikali. 

Naibu Waziri Dk. Kigwangalla aagiza uboreshaji wa huduma za Afya Tunduru


Naibu waziri wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto Dk. Hamisi Kigwangalla ametoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tunduru kuhakisha wanaboresha huduma za Afya katika Wilaya hiyo hasa kituo cha Afya Mkasale ambacho kimebainika kuwa na huduma mbovu huku pia kikiwa na uchakavu kwenye majengo yake hali ambayo inaweza kuhatarisha usalama na afya za watumishi na wagonjwa wanaohudumiwa hapo.

Akiwa katika ziara ya kikazi ya ukagazi wa utekelezajiwa agizo la uboreshaji wa vituo vya afya katika kila Kata nchini lilitolewa Desemba 2016, Dk. Kigwangalla akikagua kituo hicho cha Mkasale , aliweza kujionea mazingira hayo ambapo licha ya kupewa taarifa alitaka mara moja Uongozi wa Halmashahuri

hiyo kushughulikia suala ndani ya miezi mitatu ikiwemo Mkandarasi wa Maji kuhakikisha anaingiza mifumo ya maji ndani ya kituo hicho, pia aliagiza uongozi wa kijiji kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira yanayozunguka kituo hicho cha Mkasale.

Awali akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Tunduru baada ya ziara hiyo ya kukagua vituo vya Afya na Hospitali ya Wilaya, Dk Kigwangalla amesema Serikali inaendelea na uboreshaji wa huduma za afya na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma zenye ubora na kwa wakati na lengo la serikali ya awamu ya tano ni kupunguza kwa asilimia kubwa changamoto zinazoikabili wilaya ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, kukamilisha maboma yote ya vituo vya afya, zahanati na hospitali ambazo hazijakamilika, na kuhakikisha kuwa vifaa tiba na dawa zinapatikana za kutosha.

“Hata hivyo nawasihi wananchi tumuunge mkono Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kwa vita aliyoianzisha ya kulinda rasilimali za nchi yetu, kwani taifa limekuwa likiibiwa kwa muda mrefu sana ila umefika muda kuhakikisha kuwa rasimali za nchi zinatunzwa na kulindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.” Alieleza Dk. Kigwangalla wakati akiwahutubia wananchi hao.

Aliendelea kusema kuwa ili mwananchi aweze kushiriki katika shughuliza uzalishaji ni lazima awe na afya njema na ili awe na afya njema ni lazima wananchi kwa kushirikiana na serikali kuboresha vituo vya kutoa huduma za afya na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

“Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha kuwa dawa zinakuwepo za kutosha katika hospitali na vituo vya afya na katika mwaka wa fedha 2017/2018 serikali imetenga bajeti ya kutosha kuhakikisha kuwa vifaa tiba vinakuwepo katika vituo vya afya na hospitali zote nchini” Alieleza Dk. Kigwangalla katika mkutano huo.

Samabamba na hayo serikali inahakikisha kuwa huduma za mama na mtoto zinatolewa bure kwenye hospitali za umma zote nchi ili kupunguza vifo vya wamama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Dk Kigwangalla aliuagiza uongozi wa kijiji cha mkasale na mkotamo kutengeza barabara ya kuelekea katika kituo cha afya mkasale kutoka na barabara hivyo kuwa chafu sana hali inayoweza kuleta madhara kwa watumiaji hasa kwa wadudu kama nyoka.

"Nakuagiza mwenyekiti wa kijiji mara baada ya kumaliza kikao hapa upange ratiba na wananchi wako namna bora ya kuweza kutengeza barabara inayokwenda katika kituo cha afya mkasale na pia mupange ratiba ya kufanya ausafi katika kituo kwani kazi ya usafi ni ya wananchi"alisema Dk kigwangalla.

Aidha, katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma zilizo bora uongozi wa wilaya umeagizwa kufanya kuhakikisha vituo vyote vya afya vilivyopo wilayani Tunduru, vinajenga vyumba vya upasuaji katika vituo vyote vya afya, kukarabati maabara zote, na kuhakikisha kunakuwepo na mfumo wa maji safi wenye uhakika katika vituo vyote vya afya, kufanya matengenezo kwa vifaa vilivopata hitilafu ili kuboresha huduma.
Naibu waziri wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto Dk. Hamisi Kigwangalla akilakiwa na wananchi wa Kijiji cha Mkasale wilayani Tunduru, Mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake hiyo 
Naibu waziri wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto Dk. Hamisi Kigwangalla akimsabahi mmoja wa watoto waliofika na wazazi wake wakati wa kumpokea katika Kijiji cha Mkasale wilayani Tunduru, Mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake hiyo.
Naibu waziri wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza katika mkutano huo wa wazi kwa wananchi wa Halmashauri ya Tunduru, Mkoani Ruvuma

TRA YAANZA KUVIFUNGULIA VITUO VINAVYOTIMIZA MASHARTI YA KUFUNGA MASHINE ZA KIELEKTRONIKI


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imevifungulia vituo vya mafuta vipatavyo vitatu jijini Dar es Salaam baada ya kutimiza masharti ya kufunga mashine za kielekitroniki zinazotoa risiti moja kwa moja kutoka kwenye pampu ya mafuta (Automatic EFD).

Akizungumza mara baada ya kufungua vituo hivyo, Kamishina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere amewashukuru wamiliki wa vituo hivyo kwa kuonyesha ushirikiano kwa serikali kwa kutimiza masharti waliyopewa ya kufunga mashine hizo na kusisitiza kuwa hakuna kituo kitakachofunguliwa kama hakitatimiza masharti. 

"Niwaombe wamiliki wa vituo vilivyofungiwa kuwa kwa sasa hakuna kitakachofunguliwa bila kutimiza mashart, timiza masharti tuje tukague na tukufungulie uanze biashara yako," amesema Kamishna Kichere. 

Amesema vituo vilivyofunguliwa leo ni GBP kilichopo eneo la Majumba Sita, Simba Oil kilichopo eneo la Sitakishari, Ukonga na PETRO kilichopo eneo la Kigamboni. 

"Kitendo cha kuunganisha mashine hizi na pampu za mafuta ni cha muda mfupi sana na wala hakichukui muda mrefu, angalia huyu tulimfungia siku ya jumanne tarehe 11 Julai na leo Ijumaa Julai 14 ameshafunga mashine na anaanza kufanya biashara bila kugombana na serikali;" amesema Kamishna Kichere. 

Mpaka sasa vituo zaidi ya 40 vimefungiwa nchi nzima ikiwemo jijini Dar es Salaam kwa kosa la kushindwa kufunga mashine za kielekitroniki zinazotoa risiti moja kwa moja kutoka kwenye pampu ya mafuta (Automatic EFD).  Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Edward Kichere akikata utepe katika kituo cha mafuta cha Kigamboni jijini Dar es Salaam baada ya kutimiza masharti ya kufunga mashine za kielekitroniki zinazotoa risiti moja kwa moja kutoka kwenye pampu ya mafuta. 
Mfanyakazi wa kituo cha mafuta cha Kigamboni akitoa risiti mara baada ya kuuza mafuta. 
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Edward Kichere akikagua risiti mara baada ya kuuza mafuta.

 Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Edward Kichere akiuza mafuta katika kituo cha GBP kilichopo uwanja wa ndege mara baada ya kukifungulia. 

CHUO CHA AFYA CHA TUMAINI JIPYA MAFINGA KINATANGAZA NAFASI ZA MASOMO


MKUU WA CHUO CHA AFYA CHA  TUMAINI JIPYA MAFINGA ANA FURAHA KUWATANGAZIA KUWA CHUO KIMEANZA KUPOKEA MAOMBI YA MASOMO KWA MWAKA WA MASOMO 2017/18.

KOZI ZIFUATAZO: 
1. CERTIFICATE IN CLINICAL MEDICINE YAANI TABIBU MSAIDIZI KWA MIAKA MIWILI

  • Sifa za mwombaji: Awe na ufaulu wa kidato cha nne kwa angalau alama D nne yakiwemo masomo ya sayansi yaani Fizikia (Physics), Kemia (Chemistry) na Baolojia (Biology)


2. CERTIFICATE IN COMMUNITY HEALTH (Uhudumu wa afya ngazi ya jamii) MWAKA MMOJA

  • Sifa za mwombaji: Awe na ufaulu wa kidato cha nne kwa angalau D nne likiwemo somo la Baolojia (Biology)


MUHULA MPYA UTAANZA MWEZI SEPTEMBA, 2017.
YOTE HAYO YANAZINGATIA MWONGOZO WA WIZARA YA AFYA NA NACTE.

CHUO KIMESAJILIWA KWA USAJILI WA KUDUMU KWA NAMBA 144.
ADA ZETU NI NAFUU NA ZINALIPWA KWA AWAMU.

FOMU ZINAPATIKANA CHUONI TUMAINI JIPYA MAFINGA – IRINGA AU KWENYE WEBSITE YA CHUO.www.tumainijipya.ac.tz Kwa maulizo tafadhali wasiliana na chuo kwa namba 0755535301 AU 0625716530 AU 0754444151.

Mrithi wa Mghwira Act-Wazalendo kufanya ziara mikoa saba

Kaimu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Yeremia
Kaimu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Yeremia Maganja, 
Dar es Salaam. Kaimu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Yeremia Maganja, anatarajia kufanya ziara katika mikoa saba nchini kwa ajili ya kukagua uhai wa chama na maandalizi ya uchaguzi wa ndani ya chama katika ngazi ya mitaa.
Taarifa iliyotumwa na kitengo cha mawasiliano cha ACT-Wazalendo, leo imeeleza kuwa ziara hiyo itaanza Julai 17 na mkoa wa kwanza utakuwa ni Mara.
“Katika ziara hiyo, Maganja atafuatana na katibu wa kamati ya kampeni ya uchaguzi Mohamed Massaga, pia watakutana na kamati ya uongozi ya mkoa na majimbo yote ya mkoa” imesema
Mikoa mingine itakayofikiwa katika ziara hiyo ni Simiyu (Julai 19), Shinyanga (Julai 20),Mwanza(Julai 21),Manyara (Julai 23),Arusha(Julai 24) na Kilimanjaro (Julai 25)
“Baada ya ziara hiyo na itakayofuatiwa na tathmini ya kina Mwenyekiti Maganja atamalizia mikoa iliyosalia ya Tanzania bara kabla ya kuelekea mikoani kwa ajili ya kujitambulisha rasmi,” imesema
Taarifa hiyo imesema ziara hiyo  itakuwa ni ya kwanza kwa kiongozi huyo ambaye alipokea kijiti cha uongozi kutoka kwa Mama Anna Mghwira, aliyeondolewa katika nafasi hiyo na kamati ya uongozi ya chama baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mkuu wa  mkoa wa Kilimanjaro.

Wasichana wafunika matokeo kidato cha sita

Matokeo ya kidato cha sita nchini  yametolewa leo Jumamosi, Julai 15, yameonyesha kuwa wasichana wameongoza kwa ufaulu ambapo  kati ya wasichana 28,731 (38 asilimia) waliofanya mtihani, waliofaulu ni ni 27,577 (sawa na asilimia 97.21).
Jumla ya watahiniwa 75, 116, walifanya mtihani huo Mei mwaka huu.
Kwa upande wa watahiniwa wavulana,  waliofaulu walikuwa ni 42,975 (sawa na asilimia 95.34) kati ya  46,385.
 Taarifa iliyotolea inaonyesha kuwa watahiniwa 58,556 (asilimia 93.72) walipata daraja la kwanza hadi la tatu. Kati ya hao, wasichana ni 22, 909 na wavulana ni 35,647.
 “Mchanganuo wa ufaulu katika madaraja unaonyesha kuwa watahiniwa walipata daraja la 1-11  umepanda  kwa asilimia 0.59 kutoka asilimia 93.13 mwaka 2016 hadi 93.72 mwaka huu,” imesema taarifa hiyo na kuongeza;
 “Pia, ufaulu katika madaraja kwa upande wa wasichana umepanda ikilinganishwa na wavulana. Ubora wa ufaulu kwa wasichana ni asilimia 94.07 ikilinganishwa na asilimia 93.49 ya wavulana.”
 Ufaulu wa masomo
Kadhalika taarifa hiyo imeonyesha kuwa ufaulu kwa watanikiwa wa shule kwa upande wa masomo, ya Sayansi, Biashara, Lugha na Sanaa, haukuonyesha tofauti kubwa ukilinganisha na mwaka jana.
Hata hivyo, ufaulu katika somo la General Studies umeshuka kwa asilimia 7.54 kutoka asilimia 71. 24 hadi 63.70.