Tuesday, December 5

Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya wazinduliwa leo mjini Dodoma


Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Sekta kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), DktAndrew Komba ambaye pia ni mgeni rasmi katika uzinduzi wa Jarida lenye Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya,akizungumza mapema leo mjini Dodoma mbele ya Wadau mbalimbali wa mambo ya Afya,ikiwa ni sehemu ya kuelekea kilele cha uzinduzi wa kampeni ya Unawaji Mikono kwa vituo vya Afya itakayojulikana kwa jina la NIPO TAYARI awamu ya pili,Ambapo katika uzinduzi wa kampeni hiyo itakayozinduliwa rasmi Desemba 7,2017 mkoani Dodoma,Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa  Makamu wa Rais Mama samia Suluh Hassan
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Sekta kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), DktAndrew Komba ambaye pia ni mgeni rasmi akikata utepe kuzindua  Jarida lenye Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya,mapema leo mjini Dodoma,uzinduzi wa jarida hilo ni sehemu ya kuelekea kilele cha uzinduzi wa kampeni ya Unawaji Mikono kwa vituo vya Afya itakayojulikana kwa jina la NIPO TAYARI awamu ya pili,Ambapo katika uzinduzi wa kampeni hiyo itakayozinduliwa rasmi Desemba 7,2017 mkoani Dodoma,Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa  Makamu wa Rais Mama samia Suluh Hassan

Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Sekta kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), DktAndrew Komba akiwaonesha Wanahabari jarida lenye Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya,mapema leo mjini Dodoma

Mratibu wa Kampeni ya Usafi wa mazingira-wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dkt Anyitike Mwakitalima akizungumza jambo mbele ya Wageni waalikwa mbalimbali waliofika kwenye mkutano huo,mapema leo mjini Dodoma,kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa jarida  lenye Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Sekta kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), DktAndrew Komba akimkabidhi Mganga Mkuu wa Mkoa Njombe,Dkt Buru Mwamasage jarida lenye Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya,mapema leo mjini Dodoma
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Sekta kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), DktAndrew Komba akimkabidhi Afisa Afya mkoa wa Dodoma,Edward Ganja jarida lenye Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya,mapema leo mjini Dodoma
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Sekta kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), DktAndrew Komba akimkabidhi Mkurugenzi wa Mipango kutoka shirika la WaterAid -Tanzania Bwa.Abel Dugange  jarida lenye Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya,mapema leo mjini Dodoma
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Sekta kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), DktAndrew Komba akipewa maelezo mafupi kuhusiana na matumizi ya dawa mbalimbali zinazotumika katika usafi wa maeneo mbalimbali ikiwemo ya kunawia mikono na kusafishia vyoo,zilizotengenezwa na wajasiliamali waliokuwepo ukumbini humo wakati wa uzinduzi wa  jarida lenye Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya,mapema leo mjini Dodoma
Mratibu wa Kampeni ya Usafi wa mazingira-wizara ya afya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dkt Anyitike Mwakitalima akipewa maelezo mafupi kuhusiana na matumizi ya dawa mbalimbali zinazotumika katika usafi wa maeneo mbalimbali ikiwemo ya kunawia mikono na kusafishia vyoo,zilizotengenezwa na wajasiliamali waliokuwepo ukumbini humo wakati wa uzinduzi wa  jarida lenye Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya,mapema leo mjini Dodoma.
Wageni waalikwa mbalimbali wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri wakati wa uzinduzi wa jarida lenye Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya,mapema leo mjini Dodoma
Baadhi ya wadau wakiangalia vipeperushi mbalimbali nyenye taarifa za mambo ya Afya na usafi kwa jamii.
Baadhi ya Wawakilishi kutoka shirika la UNICEF wakifuatilia kwa makini yaliyokuwa yakijiri kwenye uzinduzi huo ambao pia uliwajumuisha wadau mbalimbali wa mambo ya Afya


KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA DKT. JUMA MALEWA AMZAWADIA MILIONI MOJA ASKARI WA KIKE KWA UTENDAJI KAZI MZURI KAZINI, JIJINI DAR


Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akimkabidhi zawadi ya Sh. Milioni moja(1,000,000) askari wa kike Sajini wa Magereza, Anna Akuny(katikati) kutokana na utendaji wake mzuri kazini aliouonesha katika Gereza la Wanawake Segerea(wa kwanza kulia) ni Kamishna wa Fedha na Utawala wa Magereza, Gaston Sanga(wa pili kulia) ni Mkuu wa Gereza Segerea, ACP. Godfrey Kavishe. 
Askari wa Kike Sajini Anna Akuny(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(wa tatu toka kulia) mara baada ya kumkabidhi zawadi ya utendaji kazi mzuri kazini. Wengine ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza, Makao Makuu. 

Na Lucas Mboje, Jeshi la Magereza

Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa ametowa zawadi ya utendaji kazi mzuri kwa askari wa Jeshi hilo Sajini Anna Akuny wa Gereza la Wanawake Segereza leo Desemba 5, 2017 katika Makao Makuu ya Magereza Jijini Dar es Salaam. Askari huyo Sajini Anna amekabidhiwa Sh. milioni moja (1,000,000) na Kamishna Jenerali wa Magereza kutokana na kuonesha utendaji wake mzuri pamoja na nidhamu kazini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa amemtaka askari huyo kutokubweteka na mafanikio hayo bali iwe chachu ya kufanya kazi kwa bidii zaidi. Jenerali Malewa ametoa wito kwa Maafisa na Askari wa Jeshi hilo kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na miongozo inayotolewa mara kwa mara na Uongozi wa Jeshi hilo.

Hafla ya kukabidhi zawadi kwa askari huyo imehudhuriwa na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza Makao Makuu, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, DCP. Augustine Mboje pamoja na Mkuu wa Gereza Segerea, ACP. Godfrey Kavishe.

Ronaldo kumfikia Messi kwa tuzo


Paris. Ufaransa. Cristiano Ronaldo ‘atapokea tuzo ya tano ya  Ballon d’Or akiwa juu ya mnara wa Eiffel uliopo jijini Paris, Ufaransa Alhamisi hii’
Kwa mujibu wa picha zilizosambaa mtandaoni mwezi uliopita zilisema mpinzani wake kutoka Barcelona, Lionel Messi ndiye atakayetwaa tuzo hiyo.
Lakini taarifa kutoka Hispania sasa zimethibisha kuwa  Ronaldo atapokea tuzo hiyo Paris, kauli iliyoungwa mkono na rais wa Bernabeu, Florentino Perez.
Mreno huyo yupo katika msimu ambao hatousahau katika kikosi cha Real Madrid.
Siyo tu kwa mafanikio yake binafsi, lakini akiwa mafanikiwa kufunga mabao mawili katika mashuti 68 aliyopiga, mbaya zaidi Real kwa sasa ipo nyuma kwa point inane kwa vinara wa La Liga, Barcelona.
Ni msimu mbaya kwa vijana Zinedine Zidane katika ligi ya Hispania tangu 2008.
Hata hivyo, Ronaldo aliingoza klabu hiyo kuweka historia ya kutetea ubingwa wa Ligi ya Mabingwa.
Taarifa ya gazeti la Mundo Deportivo limedai David Ginola ndiye atakayemkabidhi Ronaldo tuzo hiyo na kulingana na Messi kwa kutwaa tuzo hiyo mara tano.

Kabudi ataka kutumiwa wasaidizi wa kisheria

       Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa
       Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi       
Dar es Salaam. Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi ametoa wito kwa jamii kuwatumia wasaidizi wa sheria ili kupata ushauri kwa kuwa hivi sasa wanatambulika kisheria.
Akifungua maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja jana, Profesa Kabudi alisema kuwatumia wasaidizi wa sheria kutapunguza muda unaotumika mahakamani.
“Nitoe rai kwa wananchi kutumia fursa hii mliyopewa na sheria kupata msaada wa kisheria kupitia wananchi wenzenu waliojitolea kwa moyo kutoa ushauri,” alisema katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema.
Alisema kutokana na kada hiyo kuwa ngeni nchini, watu wengi hasa wanasheria na mawakili wamekuwa na mtizamo hasi na hata kufikia kuwapiga vita.
Profesa Kabudi alisema kwa kutambua umuhimu wa kusogeza huduma karibu na wananchi, sheria imeweka wasajili wasaidizi katika ngazi za halmashauri ambao watakuwa wakishirikiana na wasaidizi wa kisheria maeneo hayo.
Naye mwakilishi wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), John Seka alisema jukumu la chama hicho ni kutoa msaada wa kisheria kwa jamii.
Aliwataka wananchi kuzitumia ofisi za chama hicho zilizopo mikoa mbalimbali nchini kupata msaada wa kisheria. “Tumekuwa tukitoa msaada wa kisheria ikiwamo kutoa mawakili ili kuwasaidia wananchi wasio na uwezo,” alisema.     

Sumu yakwamisha Afrika kupenya Ulaya

     Mkurugenzi wa usalama wa chakula wa
     Mkurugenzi wa usalama wa chakula wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Raymond Wigenge      
Dar es Salaam. Inakadiriwa mwaka 2014 nchi za Afrika zilipata hasara ya Dola 670 milioni za Marekani kwa kushindwa kuuza vyakula katika Jumuiya ya Ulaya (EU), kutokana na sumu kuvu.
Hayo yalibainishwa jana na mkurugenzi wa usalama wa chakula wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Raymond Wigenge kwenye kongamano la udhibiti wa sumu kuvu kwa kushirikina na wadau kutoka umoja wa Afrika kupitia programu ya udhibiti wa sumu kuvu (PACA).
Wigenge alisema uwapo wa sumu kuvu katika vyakula unaosababishwa na baadhi ya fangasi wanaoingia ikiwamo mahindi, imekuwa changamoto kubwa hivyo huathiri ukuaji wa biashara ya vyakula.
Alisema inakadiriwa watu milioni 208 katika bara la Afrika wanategemea mahindi kama chakula kikuu, hivyo kupata mbinu mwafaka za udhibiti wa sumu kuvu kutapunguza tatizo hilo.
Wigenge alisema nchi 16 kati ya 22 zinategemea mahindi duniani zimeathirika.
Pia, alisema inakadiriwa asilimia 30 ya wagojwa wa kansa ya ini barani Afrika, wanapata tatizo hilo kupitia ulaji wa vyakula vyenye sumu kuvu hivyo jitihada zaidi zinahitajika kuhakiisha hali hiyo inadhibitiwa.
Alisema tatizo hilo linaweza kusababisha baadhi ya watoto kupata ugonjwa wa udumavu, hivyo hatua za udhibiti zinatakiwa kuanzia kwa wakulima.
Naye mshauri wa sumu kuvu kutoka Umoja wa Afrika wa Udhibiti wa Sumu Kuvu (Paca), Profesa Martin Kimanya alisema tatizo ni kubwa kwa sababu linahusu maisha ya binadamu kila siku.
Profesa Kimanya alisema mahindi yanapobanguliwa shambani kunakuwa na fangasi ambao wanaingia kwenye mbegu, hivyo kusababisha madhara kwa watumiaji.
Alisema asilimia 30 ya watumiaji wa mahindi kwa nchi za Kenya na Tanzania, wanakabiliwa na hatari ya kupata athari zitokanazo na sumu hiyo.
Pia, alisema lazima Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wahakikishe tatizo hilo linadhibitiwa. “Vyama vya wakulima, watafiti, wataalamu wa kilimo na wa lishe tushirikiane kuondoa tatizo hili mapema,” alisema.    

Mhasibu wa Takukuru akwama mahakamani


Dar es Salaam. Mahakama imegoma kumfutia shtaka la utakatishaji fedha mhasibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai.
Gugai anayedaiwa kuwa na utajiri wa kutisha usiolingana na kipato chake, aliiomba mahakama kumfutia shtaka hilo na kujikuta likitupiliwa mbali.
Gugai na wenzake watatu, George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera wanakabiliwa na mashtaka hayo ambayo hayana dhamana pamoja na mengine ya jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Novemba 16, na kusomewa mashtaka 43 yakiwamo 20 ya kutakatisha fedha.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, kupitia kwa jopo la mawakili wao lilioongozwa na Alex Mgongolwa waliiomba mahakama kuwafutia mashtaka ya utakatishaji fedha, pamoja na mambo mengine wakidai hayajakidhi vigezo vya kisheria.
Maombi na hoja za mawakili wa washtakiwa hao, zilipingwa vikali na upande wa mashtaka ulioongozwa na Simon Wankyo baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliiahirisha hadi jana kwa uamuzi wa ama kuyafuta mashtaka hayo au la.
Hata hivyo, hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba anayesikiliza kesi hiyo katika uamuzi wake alitupilia mbali maombi na hoja za mawakili wa washtakiwa hao.
Akisoma uamuzi wake, Simba alitupilia mbali maombi na hoja hizo akisema hazina msingi wa kisheria na hati ya mashtaka ipo sawa haina kasoro za kisheria.
Baada ya kusoma uamuzi huo, wakili wa Serikali mkuu, Vitalis Peter aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Simba aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 18, litakapotajwa kwa ajili ya upande wa mashtaka kueleza hatua ya upelelezi ulipofikia.
Awali, akiwasilisha maombi ya kufutwa kwa mashtaka hayo, Mgongolwa alidai mashtaka hayo hayakidhi vigezo vya kisheria vilivyotajwa katika sheria ya utakatishaji fedha.
Alidai maelezo ya makosa hayo hayaelezi kosa la utakatishaji fedha na kwamba, lazima makosa hayo yaonyeshe uhalisia ili kumwezesha mshtakiwa kutengeneza utetezi wake.
Aliendelea kuwa msingi wa mashtaka ya utakatishaji wa fedha ni fedha, lakini katika mashtaka yote hayo ya utakatishaji hakuna sehemu iliyotajwa fedha na kwamba kinachoonekana ni udanganyifu wa kiwango cha mali anazomiliki mshtakiwa.
Maombi hayo yalipingwa na upande wa mashtaka ambao waliiomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo, kwa kuwa hayana msingi kisheria.
Gugai kwa upande wake anakabiliwa na shtaka la kumiliki mali ambazo hazina maelezo.
Anadaiwa kuwa kati ya Januari 2005 na Desemba 2015, katika mkoa wa Dar es Salaam, akiwa ofisa wa umma aliyeajiriwa na Takukuru, alikutwa anamiliki mali zenye thamani ya Sh. 3,634,961,105.02 ambazo haziendani na kipato chake cha sasa wala cha nyuma. 

Kumbusho aachiwa baada ya kuhojiwa polisi


Dar es Salaam. Mbunge wa serikali ya wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Kumbusho Dawson ameachiwa baada ya kuhojiwa na polisi wa kitengo cha makosa ya mtandao.
Kumbusho alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi leo Jumanne Desemba 5,2017 akitokea Oysterbay alikokwenda kuripoti asubuhi baada ya kuachiwa kwa dhamana jana usiku.
Wakili Alex Masaba anayewakilisha Kumbusho amesema polisi wamemuachia baada ya mahojiano na wanaendelea na upelelezi hivyo wakimuhitaji watamwita.
Masaba amesema mteja wake amekamatwa kwa kosa la kusambaza picha zinazoonyesha nyufa kwenye jengo la  mabweni ya chuo hicho. Hata hivyo, amesema anaamini kilichofanyika si jinai.
"Kosa la kusambaza picha zilizopigwa si jinai hata polisi nimewaeleza kwa kitendo kilichofanyika inabidi apongezwe," amesema Masaba.

Mtoto aliyezaliwa ubongo ukiwa nje afanyiwa upasuaji


Dar es Salaam. Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) imefanya upasuaji mkubwa wa kurudisha ubongo wa mtoto mwenye umri wa miezi minne aliyezaliwa ukiwa kwenye mfuko nje ya kichwa.
Upasuaji huo uliofanyika kwa mafanikio ni wa kwanza nchini wa kurudisha ubongo uliokuwa kwenye mfuko nje ya kichwa (occipital encephalocele).
Imeelezwa upasuaji huo uliwahusisha madaktari bingwa kutoka nchini kwa gharama ya Sh4 milioni badala ya kati ya Sh25 milioni na Sh30 milioni kama ungefanika nje ya nchi.
Daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo wa Moi, Nicephorus Rutasibwa amesema leo Jumanne Desemba 5,2017 kuwa upasuaji huo umefanywa kwa zaidi ya saa nne.
Dk Rutasibwa amesema upasuaji umefanyika baada ya utafiti wa miezi miwili kujua namna bora ya kumsaidia mtoto huyo ili kuokoa maisha yake.
“Tathmini ya uchunguzi ilionyesha uvimbe au mfuko ulikuwa umefunika sehemu kubwa ya ubongo na mishipa ya damu inayolisha ubongo, hivyo kuhatarisha maisha yake. Upasuaji ulihitaji umakini wa hali ya juu na vifaa vya kisasa,” amesema.
Dk Rutasibwa amesema upasuaji huo ulifanywa bila kuathiri utendaji kazi wa ubongo ambao wakati wote wa upasuaji ulikuwa unafanya kazi.
Hata hivyo, amesema walikabiliana na changamoto wakati wa maandalizi ya upasuaji ya upatikanaji wa mishipa ya damu ya mtoto kwa kuwa ilikuwa midogo.
“Baada ya upasuaji mtoto aliendelea vizuri na aliweza kunyonya, tangu alipozaliwa ilikuwa vigumu kumbeba lakini sasa mama anaweza kumbeba mwanaye. Mtoto amepata nafasi ya kuendelea na maisha,” amesema.
Mama wa mtoto huyo ambaye hakupenda kutajwa jina amesema awali alikata tamaa ya mwanaye kupona kutokana na uvimbe uliokuwa ukimuelemea.
“Nawashukuru madaktari bingwa kwa kufanikishwa upasuaji huu, nilishakata tamaa na sikujua kama leo ningeweza kumnyonyesha mwanangu akiwa mzima,” amesema.

Wafanyabiashara wapandishwa kizimbani kwa uhujumu uchumi


Dar es Salaam. Wanandoa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Minda Mfamai na mkewe Fatuma Mpondi ambao ni wafanyabiashara wamepandishwa kizimbani pamoja na mwenzao Oswini Mango wakidaiwa kusafirisha gramu 375.20 za dawa za kulevya aina ya heroin.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri; wakili wa Serikali, Adolf Mkini amedai Novemba 22,2017 katika maeneo ya Chamazi kwa Mkongo, Dar es Salaam washtakiwa walisafirisha dawa hizo.
Baada ya kusomewa shtaka leo Jumanne Desemba 5,2017 washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu.
Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 19,2017.
Mahakama imeamuru mshtakiwa Minda akatibiwe baada ya kulalamika kuwa alipigwa akiwa polisi.

Mahakama kutoa uamuzi wa dhamana kesho


Morogoro. Wabunge Susan Kiwanga na Peter Lijualikali waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro pamoja na washtakiwa wengine 36 wamerejeshwa rumande.
Mahakama iliyokuwa itoe uamuzi wa dhamana leo Jumanne Desemba 5,2017 imekwama kufanya hivyo kutokana na kuibuka hoja za kisheria.
Upande wa mashtaka na ule wa utetezi unavutana kuhusu hati ya kiapo ya kupinga dhamana iliyowasilishwa mahakamani hapo.
Kutokana na mvutano wa kisheria, hakimu Ivan Msack ameahirisha kesi hiyo hadi kesho Jumatano Desemba 6,2017 ili kutoa fursa kwa pande zote mbili kujibu hoja kuhusu hati hiyo.
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka nane likiwamo la kuchoma moto ofisi ya Kata ya Sofi iliyopo wilayani Malinyi.
Washtakiwa wanatetewa na mawakili Peter Kibatala, Ignas Punge, Fredrick Kiwelo na Bartholomew Tarimo. 
Upande wa mashtaka unawakilishwa na mawakili wa Serikali, Edga Bantulaki na Sunday Hyera. 
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Frederick Sumaye walihudhuria mahakamani.
Wengine waliofika mahakamani ni mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na wa Viti Maalumu, Devota Minja.

JWTZ yaandaa mazoezi ya kijeshi ya pamoja EAC



Dar es Salaam. Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeandaa mazoezi ya pamoja ya kijeshi kwa maofisa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Mazoezi hayo yaliyopewa jina ‘Ushirikiano imara’ yanawashirikisha wanajeshi na maofisa wa Serikali kutoka Tanzania, Uganda, Burundi, Kenya na Rwanda.
Mkuu wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi, Brigedia Jenerali Alfred Kapinga amesema leo Jumanne Desemba 5,2017 kuwa watu 300 wanashiriki wakiwamo makamanda wa jeshi na maofisa wa juu kutoka wizara zaidi ya tatu ikiwamo ya Katiba na Sheria.
Amesema kwa Tanzania wanaoshiriki ni makamanda na maofisa watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Brigedia Jenerali Kapinga amesema kwa upande wa Tanzania washiriki ni 107 na kwamba, mazoezi yameanza jana Desemba 4,2017 na yatazinduliwa Desemba 7,2017 na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.
“Mazoezi yanafanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Kunduchi, Dar es Salaam na yamejikita katika mambo makuu manne,” amesema.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni operesheni katika ulinzi wa amani; kupamba na ugaidi; kupambana na uharamia wa aina yoyote ndani ya Bahari ya Hindi; na majanga na maafa.
Amesema lengo la mazoezi hayo ni kuwaandaa na kuwapa uwezo washiriki katika kupanga na kutekeleza majukumu ya operesheni za ulinzi wa amani katika kupambana na ugaidi, uharamia na kukabiliana na maafa.
Brigedia Jenerali Kapinga amesema mazoezi  hayo ni ya siku 17.

Kumbusho aachiwa baada ya kuhojiwa polisi


Dar es Salaam. Mbunge wa serikali ya wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Kumbusho Dawson ameachiwa baada ya kuhojiwa na polisi wa kitengo cha makosa ya mtandao.
Kumbusho alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi leo Jumanne Desemba 5,2017 akitokea Oysterbay alikokwenda kuripoti asubuhi baada ya kuachiwa kwa dhamana jana usiku.
Wakili Alex Masaba anayewakilisha Kumbusho amesema polisi wamemuachia baada ya mahojiano na wanaendelea na upelelezi hivyo wakimuhitaji watamwita.
Masaba amesema mteja wake amekamatwa kwa kosa la kusambaza picha zinazoonyesha nyufa kwenye jengo la  mabweni ya chuo hicho. Hata hivyo, amesema anaamini kilichofanyika si jinai.
"Kosa la kusambaza picha zilizopigwa si jinai hata polisi nimewaeleza kwa kitendo kilichofanyika inabidi apongezwe," amesema Masaba.

Mtanzania afa baada ya kuzidiwa akiwa ndani ya ndege.


Dar es Salaam. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Sianga amethibitisha kupokea taarifa ya Mtanzania kufariki dunia akisafirisha dawa za kulevya.
Amesema alikuwa akisafiri kuelekea nchini China kwa ndege ya Shirika la Ethiopia na alizidiwa kutokana na dawa alizokuwa amemeza.
“Ni kweli kuna Mtanzania amekutwa amekufa kwenye ndege ya Shirika la Ethiopia akiwa amemeza dawa za kulevya. Tunaendelea kufuatilia kujua jina lake na amezitoa wapi hizo dawa,” amesema.
Sianga akizungumza na MCL Digital leo Desemba 5,2017 amesema taarifa hizo walizipata jana na kwamba wanaendelea kufuatilia.
Amesema hivi sasa Watanzania wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya wengi wanatumika kupokea mizigo na kuisafirisha kunakohitajika.

Lukuvi amesema kodi inapaswa kulipwa kila mwezi


Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewaonya wamiliki wa nyumba wanaopangisha na kudai kodi ya mwaka mzima.
Akizungumza leo Jumanne Desemba 5,2017 akifungua jengo la makao makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Dar es Salaam na sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere, amesema kodi ya nyumba inatakiwa kutozwa kila mwezi.
"Mpangaji anatakiwa kulipa kodi kila mwezi labda atake mwenyewe kulipa kwa miezi zaidi ya mmoja," amesema.
Lukuvi amesema hata NHC inatoza kodi kwa wateja wake kwa mwezi. "Acheni tamaa wenye nyumba chukueni kodi kila mwezi," amesema.
Amesema kuna vijana wanaoajiriwa wanashindwa kukaa jirani na mjini kutokana na kutozwa kodi ya nyumba kwa mwaka.
Mbali ya kauli hiyo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula Novemba 17,2017 akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Halima Bulembo bungeni alisema Serikali iko katika mchakato wa maandalizi ya muswada wa sheria ambayo itasimamia sekta ya nyumba, hivyo kuondoa changamoto ya wamiliki kudai kodi ya pango ya zaidi ya mwezi mmoja.
Halima katika swali lake alisema vijana ambao ni kati ya asilimia 56 na 60 nchini, wanashindwa kutimiza ndoto zao kutokana na gharama kubwa ya kodi ambayo hutakiwa kulipa kwa kipindi cha mwaka mmoja au miezi sita.
Akijibu swali hilo, Mabula alisema Serikali imeliona tatizo hilo na ipo katika mchakato wa kuandaa muswada wa sheria utakaosimamia sekta hiyo.
Mabula alisema baada ya kukamilika kwa sheria ambayo itaunda chombo cha kusimamia sekta hiyo, wapangaji hawatalipa kodi ya mwaka wala miezi sita tena bali watalipa kwa mwezi na kuweka amana ya miezi mitatu.

HESLB yatoa orodha ya waliopata mikopo


Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha yenye wanafunzi  2,679 waliopata mikopo yenye thamani ya Sh9.6 bilioni baada ya kukamilika uchambuzi wa rufaa walizowasilisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema leo Jumanne Desemba 5,2017 kuwa wanafunzi 1,847 ni wa mwaka wa kwanza ambao mikopo yao ina thamani ya Sh6.84 bilioni na wengine 832 ni wanaoendelea na masomo lakini hawakuwa na mikopo katika miaka iliyopita.
Amesema wanafunzi wanaoendelea na masomo wamepata mikopo yenye thamani ya Sh2.76 bilioni na fedha zimeshatumwa vyuoni.
Badru amesema kutokana na kukamilika kwa rufani hizo, wanafunzi 33,200 wa mwaka wa kwanza wamepangiwa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh108 bilioni kwa mwaka wa masomo 2017/18 hadi sasa.
Amesema bajeti ya jumla kwa wanafunzi wote kwa mwaka 2017/18 ni Sh427.54 bilioni. Badru amesema dirisha la rufaa lilifungwa Novemba 19,2017.
HESLB pia imeanza kuhamisha mikopo iliyokuwa imeelekezwa katika vyuo tofauti.
Badru amesema mikopo ya wanafunzi 590 wa mwaka wa kwanza yenye thamani ya Sh1.78 bilioni ambayo awali ilikuwa imepelekwa katika vyuo tofauti na walipo wanafunzi imehamishwa.

Tani tatu za sangara zanaswa zikisafirishwa kwa magendo


Ngara: Tani tatu za samaki aina ya sangara zenye thamani ya Sh20.8 milioni zimekamatwa zikisafirishwa kwa magendo wilayani Ngara mkoani Kagera.
Samaki hao waliovuliwa katika Ziwa Victoria wilayani Muleba wamekamatwa jana Jumatatu Desemba 4,2017 jioni katika Kijiji cha Murusagamba wilayani Ngara wakisafirishwa kwa gari kwenda nchini Burundi.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Michael Mntenjele amesema leo Jumanne Desemba 5,2017 kuwa samaki hao walivuliwa kinyume cha sheria na walikuwa wakiwasafirisha bila vibali.
Mntenjele amesema samaki hao walikuwa kwenye gari aina ya Mitsubishi likiendeshwa na Ayubu Sanga mkazi wa Dar es Salaam    anayefanya shughuli zake Kata ya Izigo wilayani Muleba.
Amesema dereva huyo akiwa na bosi wake walikatwa wakisafirisha mzigo huo kwa magendo. Alisema bosi huyo alitoroshwa wakati wakihojiwa na polisi kwa msaada wa baadhi ya maofisa uvuvi.
Mkuu wa wilaya amesema dereva na ofisa uvuvi wa kata ya Murusagamba wanashikiliwa na vyombo vya dola kwa mahojiano.
Ofisa Uvuvi Mkoa wa Kagera, Efraz Mkama amesema samaki hao wana uzito wa kuanzia nusu kilo hadi kilo 30 na urefu wa kati ya sentimita 25 na sentimita 90 .
Amesema watuhumiwa wametenda kosa la kusafirisha samaki ambao hawajachakatwa kwa mujibu wa sheria ya uvuvi.
“Mzigo haukuwa na nyaraka, ulisafirishwa usiku na kukiuka utaratibu kuanzia maeneo ya mwaloni katika kata na vijiji mbalimbali wilayani Muleba. Tutafuatilia huko alikotokea,” amesema Mkama.